Liberia
“KUPENDA uhuru ndiko kulikotuleta hapa.” Maneno hayo yalisemwa na walowezi waliovuka bahari kuu Atlantic wakafikia katika kisiwa kidogo sana kiitwacho Providence Island katika pwani ya magharibi ya Afrika, Aprili 25, 1822. Wakuu wa mji na wakurugenzi wajasiri walisaidiwa na American Colonization Society wakaanza Jamhuri ya kwanza ya weusi katika Afrika, Liberia, mwaka 1847. Nchi hiyo ina ukubwa unaokaribia kulingana na wa Louisiana, nayo imepakana na Sierra Leone, Jamhuri ya Guinea na Ivory Coast.
Liberia hasa iko pwani, mimea yake inakuwa mibichi-bichi nyakati zote na ina misitu ambamo tembo, chui na viboko wafupi sana wanatembea-tembea. Hii ni nchi yenye miti ya mipira, nayo ina mashamba makubwa yanayotunzwa vizuri. Katika milima mifupi kazi nyingi zinafanywa kuchimbua madini yaliyo bora zaidi duniani pote, ya kutengeneza chuma.
KWELI YENYE KUKOMBOA WATU YAFIKA LIBERIA
Kufika mwaka 1867, miaka 20 baada ya jamhuri hiyo kuanzwa, jumla ya walowezi 13,136 walikuwa wamekwisha hamia Liberia hasa kutoka Amerika. Kukawa na makao pwani, nje ya Monrovia, ambao ndio mji mkuu, kutoka Mto Mano mpaka Mto Cavalla—Robertsport, Marshall, Buchanan, Greenville, na Harper. Karibu na mwaka 1895, katika makao hayo ya Harper yaliyo katika Cape Palmas, ndipo gazeti Zion’s Watch Tower and Herald of Christ’s Presence lilipochunguzwa na darasa la wanafunzi wa Biblia, na hiyo ndiyo iliyokuwa mikutano ya kwanza ya namna hiyo Liberia, au katika Afrika Magharibi yote, kwa kadiri ijulikanavyo. Kwa mara ya kwanza Waliberia walikuwa wakipokea kweli ya Biblia inayokomboa watu.—Yohana 8:32.
Haijulikani kabisa jinsi na wakati wale ndugu wawili wazee, Henry na Joseph Gibson, walivyopata gazeti Zion’s Watch Tower. Lakini masomo ya nyumbani ya Biblia yalifanywa kwa kawaida, kama ambavyo watu wengi wa zamani wamethibitisha, kutia na aliyekuwa rais wa Jamhuri hiyo, William V. S. Tubman Alikumbuka kwamba mikutano ilifanywa alipokuwa kivulana tu. Wenye dhihaka ya kusema, “Mashahidi wa Yehova wamekuwa Liberia muda gani?” walikuwa wakinyamazishwa kwa kuambiwa: “Rais asema mikutano yetu ilifanywa hapa karibu miaka 75 iliyopita.” Kikundi fulani kiliadhimisha Ukumbusho wa kifo cha Bwana wetu kila mwaka katika usiku wenye kulingana na tarehe ya kalenda ya Kiyahudi ya Nisani 14. Ndugu hao wa damu, akina Gibson, walikufa karibu na mwanzo wa karne, na yaelekea madarasa yalikwisha wakati huo.
Lakini, karibu robo karne ilipita kabla ujumbe wa ufalme wa Yehova haujatangazwa hadharani katika Liberia. Mwaka 1926, Claude Brown, Mwanafunzi wa Biblia kutoka Freetown, Sierra Leone, alitembelea Monrovia kwa juma kadha. Alifungua njia ya ziara ya W. R. (“Bible”) Brown, wa tawi la Afrika Magharibi la Watch Tower Society. Kwa juma tatu, W. R. Brown, mjumbe hodari sana wa ufalme wa Yehova, alihutubu kila usiku katika jumba la Bunge la Monrovia, akaeneza vitabu vingi. Makundi makubwa ya watu, kutia na watu mashuhuri, walimiminika wamsikie akifunua kweli kwa njia yenye kushangaza.
Washiriki wa makanisa mbalimbali walishangazwa sana na hotuba za “Bible” Brown, ambazo zilifunua uongo wa dini zao na kuzitikisa barabara. Hotuba zake zilizungumzwa sana, nao wazee wangali wakizinena, baada ya miaka 50! Kabla Ndugu Brown hajaondoka, alifanya mipango kukawa na darasa la Biblia lenye kusimamiwa na Bw. Faulkner, mwanamume ambaye alikuwa amegombea cheo cha urais mara mbili. Mmojawapo washiriki thabiti wa darasa hilo alikuwa J. G. Hansford, Mliberia aliyekuja na “Bible” Brown kutoka Freetown. Hata mapadre walihudhuria masomo hayo mara kwa mara.
WAPINGWA
Wakati “Bible” Brown aliporudi Monrovia mwaka 1929, wanadini walikuwa wamezidisha upinzani. Miaka ya mwanzoni ya 1920, wanawake mashuhuri wa Liberia walikubali mafundisho yenye chuki ya Bi. January, mhubiri Mpentekoste. Wanawake hao hasa walichochea wakuu wa serikali. Shime ilikuwa kwamba ‘mahubiri ya Brown yangebomoa makanisa yao.’ Baada ya kutoa hotuba moja tu katika ziara hiyo, “Bible” Brown alikatazwa ruhusa ya kukaa nchini, akalazimishwa kuondoka baada ya juma moja tu. Lakini alikwenda kwingineko Afrika, kwenye matunda mengi hata zaidi.
Hata hivyo, masomo ya Biblia yaliendelea, na baadaye yalisimamiwa na Shahidi wa kutoka Sierra Leone. Miaka ya mwanzoni ya 1930 hali za uchumi zilikuwa mbaya, na watu wengine walidhani mahubiri ya ndugu huyu yalishambulia serikali. Ikawaje? Alipelekwa mpakani kwa nguvu, akafukuzwa. Matisho yalipoza juhudi ya wengine, nalo darasa la kujifunza Biblia likatawanyika.
USITAWI WA KIROHO WAANZA
Usitawi wenye kuhitajiwa sana Liberia katika hali ya uchumi ulitokana na Firestone Company, shirika ambalo lilikuwa limeanza kupanda miti ya mipira katika Harbel, mwaka 1926, na miaka saba baadaye walikuwa wakilima eka 55,000. Lakini miaka ya 1940 ndiyo iliyokuwa na usitawi mwingi kimwili na kiroho, Liberia. Vita ya Ulimwengu ya Pili iliinua hali ya kimwili ya Liberia, kwa maana Marafiki wa nchi hiyo walitaka mahali pa kutua ndege katika Afrika Magharibi, wakachagua Roberts Field, karibu na Firestone, Harbel. Karibuni wanajeshi Waamerika walimiminika Liberia, wakaleta pesa na desturi za Uzungu. Hata Roosevelt, Rais wa Amerika, alitembelea huko kifupi. Ndipo nchi hiyo ilipopata mkopo wa pesa zilizowezesha Monrovia ipate uwanja wa ndege wa kisasa, ipate barabara iliyofyekwa vizuri na madaraja, na vilevile reli yao ya kwanza.
Sasa wanauchumi wa mataifa yote walifahamu kwamba Liberia ingeweza kuwa na madini bora ya kutengenezea chuma. Mashirika mengine ya mpira waliona faida za kuwa na mashamba katika nchi yenye urafiki na nchi za Uzunguni na yenye kuingilika kupitia Atlantic Ocean (bahari kuu), badala ya kutegemea mashamba ya Mashariki ya Mbali. Ndivyo ulivyoanza usitawi wa hali ya uchumi usiopata kuonekana tena katika historia yote ya Liberia, baada ya vita. Hali za maisha zikawa na maendeleo kwa ujumla, na hata serikali sasa ikawa na pesa za kuendeleza elimu iliyohitajiwa sana, na kujenga barabara.
Mwaka 1946, usitawi wa kiroho ulianza pia alipofika Harry C. Behannan, mmisionari aliyehitimu katika darasa la tatu la Watchtower Bible School of Gilead. Ndugu Behannan alikuwa na kipawa cha muziki, na alikuwa amefanya maonyesho ya kucheza piano katika Ulaya yote, hata mbele ya wafalme. Alimtumikia Mungu kwa juhudi nyingi, juhudi iliyofaa sana kutiwa mafuta kwake kama mmoja wa “kundi dogo” la Bwana. (Luka 12:32) Alifika Monrovia akiwa painia halisi, akiwa peke yake. Moja kwa moja Ndugu Behannan alianza kuhubiri nyumba kwa nyumba. Muda mfupi wa miezi sita alikuwa amefanya urafiki na watu wengi, akaangusha zaidi ya vitabu 500. Ili apeleke kweli katika sehemu nyingine za nchi, alisafiri kwenda Greenville, Sinoe County, kwa mashua iliyo wazi inayofaa hali za mawimbi, maili 150 (kilomita 240) kutoka Monrovia.
Looo, ndugu huyu mwenye upendo hakuweza kukuza mwenyewe mbegu nyingi alizopanda na kupalilia! Alipotoka Greenville, Ndugu Behannan aliuawa hospitalini na homa kali. Wakuu wa makao ya ubalozi ya Amerika, pamoja na watu wengine, walihudhuria maziko yake. Mtu mmoja wa Liberia alisema yafuatayo juu ya Ndugu Behannan: “Alienenda kama mtu mwenye kusudi kuu.” Kusudi hilo halikupaswa kushindwa.
KOLAHUN, HO!
Juni mwaka 1956, Bayo Gbondo aliwekwa kuwa painia wa pekee wa kwanza Mliberia. Kwanza aliendelea kukuza kazi katika Harbel. Lakini Februari mwaka 1957, yeye na mkewe, Teetee, aliondoka kwenda kwenye mgawo wao mpya katika Kolahun, karibu maili 300 (kilomita 483) kutoka Monrovia, katika pembe ya nchi ambako Sierra Leone na Guinea zimepakana. Borbor Tamba Seysey, ndugu mwingine kutoka Kundi la Harbel aliyewekwa wakati huo awe painia wa pekee, alijiunga nao.
Kolahun ulikuwa mji mkubwa kati ya Wagbandi. Lakini walikuwako pia watu wa kabila la Kisi, na wengi wao walipendezwa na kweli ya Biblia. Kabla ya mwaka kwisha, painia wa pekee mwingine aliyewekwa karibuni, Fallah Neal, Mkisi vile-vile, alijiunga na ndugu wale wengine waliokuwa sasa wakitembelea zaidi vijiji vya Wakisi. Desemba mwaka 1957 kundi dogo lilianzwa Kolahun. Lakini Wakisi wa kijiji cha Tarma walipendezwa sana hata painia akapewa mgawo huko.
Watu wa vijiji vingi vya eneo hilo walishika sheria za ushirikina na miiko ya kutofanya mambo, kama vile kutotaja neno “chui” katika kijiji, na kutochukulia maji penginepo, isipokuwa juu ya kichwa. Hata hivyo, kadiri wanavijiji wengi zaidi na zaidi walivyoanza kujifunza kweli, hawakutaka tena kutii sheria za imani za ujinga.
Kwa mfano: Katika Tamar mtu asingeweza kutoa kinu shambani kikiwa juu ya kichwa; ilikuwa lazima kibingirishwe chini. Kama wangevunja sheria hiyo, wana-vijiji waliamini kwamba hakuna mwanamke wa mji huo angeweza kuzaa watoto. Kama mchele ungepikwa kwa kuni zilizotolewa katika vichaka vya siri (ambako wanawake tu walikaa wakizoeza mabinti hali za kike), mtu angefura tumbo na kufa.
Lakini, Mkristo huleta kinu kijijini kwa kukichukua kichwani. Hata hivyo, siku ile ile inayofuata mwanamke akizaa, sheria hiyo inaonekana kuwa bure. Ndugu hukata kuni karibu na eneo lililokatazwa na kuzitumia kupika mchele, lakini hakuna anayekufa. Ndipo sheria nyingine inapoonekana kuwa bure!
Baada ya hapo, majirani wakawa wakijia painia wa pekee nyumbani kwake kuomba makaa ya mawe kuwasha mioto. Painia huyo aliuliza mwanamke mmoja: “Wewe huogopi kutumia makaa haya yaliyotolewa katika vichaka wanakokaa wanawake?” Akajibu: “Usijali. . . . Ya kale tumekwisha yaacha nyuma!”
Ingawa majumbe wengine walijitahidi sana kufanyia watumishi wa Mungu matata, watu walimiminika ndani ya tengenezo la Yehova. Kwa hiyo, Agosti 1958 kundi lilianzwa katika Tarma.
Kupenda kweli kwa ndugu hawa wapya kulijaribiwa mara nyingi walipokosa faida za kimwili kwa sababu ya kushikamana na kanuni. Wakati mwangalizi wa mzunguko alipotembelea kijiji cha Lilionee, watu walikuwa wakiongea kihuzuni. Je! mtu alikuwa amekufa? Hapana. Kulingana na wanavijiji, jambo baya zaidi lilikuwa limetokea. Mtu aliyekuwa na wake watatu alifukuza wawili, akawapa uhuru kamili. Tena, hakutaka kudai dola 300 alizokuwa amewalipia mahari. Lilikuwa jambo lisilopata kusikika! Mwanakijiji huyo alikuwa David Saa, aliyekuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
David Saa alihudhuria mikutano ya Kikristo kwa kawaida bila kuacha jamaa yake, hata kitoto kile kidogo zaidi kilikwenda kikiwa mgongoni pa mama. Ndugu huyo alikuwa jumbe wa kijiji lakini akajiuzulu. Alisema: “Nataka nitumikie ufalme wa Mungu unaosimamiwa na Kristo Yesu. Najua mtu hawezi kutumikia mambo mawili. Nikiwa jumbe huenda ikanipasa kufanya jambo ambalo halitapatana na ufalme wa Mungu. Hivyo huenda nikapoteza upendeleo wa Mungu. Afadhali nipate kibali ya Mungu, hata ikiwa nitakuwa kibarua wa kawaida tu.”
Ndugu huyo aliyekuwa peke yake alikataa kujiunga na wanavijiji wenzake kutoa dhabihu mbele ya mlima, kusihi sana na kuheshimu mababu waliokufa. Ndipo majira ya kulima yalipofika. Watu wote walianza kuweka nyungu zao katika mashamba ya mpunga ziwe hirizi, wakidhani zingelinda mashamba na kuleta mazao mengi. Ndugu yetu akakataa tena. Watu wote walisema alikuwa na wazimu. Angelindwa na nani? Asingepata mchele wo wote. Lakini yeye aliwajibu: “Yehova akitaka kunibariki na mchele mwingi, atafanya hivyo, lakini isipokuwa hivyo, siwezi kutolea mungu mgeni dhabihu wala kumtegemea.”
Miezi ilipita kisha mashamba ya mpunga yakawa tayari kuvunwa. Ni shamba la nani lililozaa mazao bora zaidi katika wilaya? Ala, ni shamba la ndugu yetu, David Saa! Yehova asifiwe! Wanavijiji waliduwaa. Watu walikuja kutoka mitaa mingine wajionee wenyewe. “Kweli Yehova aweza kukubariki,” walisema. “Wasema hukutoa dhabihu yo yote, hukuweka nyungu shambani iwe hirizi, na kwamba hukupatwa na madhara? Lo! mpunga wako! Sisi tulifanya yote hayo tusifanikiwe?”
Watu walibadili nia. Hawakuwa na uadui tena. Hata ndugu mdogo wa Saa aliyekuwa akimpinga alitafuta Shahidi katika kijiji jirani, akaomba afundishwe habari za Yehova. Wanavijiji wote waliheshimu sana mafundisho ya Neno la Mungu.
AENDELEO KATIKA NCHI YA WAKISI
Julai 1958 ulikuwa wakati wenye kumfurahisha Bayo Gbondo na Fallah Neal. Waliacha kwa muda migawo yao ya upainia wa pekee wakahudhurie Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Mataifa yote katika mji New York. Baada ya hapo, walihudhuria darasa la 32 la Shule ya Gileadi.
Walipotoka Gileadi mwaka 1959, Gbondo na Neal walipewa mgawo waende katika nchi ya Wakisi, walikohitajiwa. Ndugu Neal alitumwa kwenye eneo jipya, Limbaba. Kufika miaka ya katikati ya 1960 kundi lilianzwa huko pia.
Oktoba 1960 kusanyiko la mzunguko lilifanywa la makundi yale matatu katika eneo la Wakisi na Wagbandi. Baada ya miaka mitatu na miezi kadha tu ya kuhubiri, walikuwako wahubiri 55 na mapainia 10. Lakini ilionekana kwamba watu wengi sana walipendezwa, kwa sababu 291 walihudhuria hotuba ya watu wote. Watu 22 walibatizwa katika kusanyiko hilo.
Wakati huo ndugu katika Tarma walikuwa wakipanga kujenga Jumba la Ufalme lao wenyewe. Wakuu wa kabila walijaribu kuzuia lisijengwe, lakini wapi. Kwa mwaka mmoja ndugu mmoja alikata miti na magogo, huku wale wengine wakimpandia mpunga, kumtunzia na kumvunia. Ndipo yale magogo yalipopelekwa kwenye barabara ya mbali yakauzwe. Pesa zilitumiwa kununua saruji na mabati, navyo vilichukuliwa vichwani saa nyingi vikipelekwa mahali pa ujenzi. Watu walijitolea kuweka msingi, kisha kikundi chote cha karibu watu 50 kikaanza kujenga kwa juhudi moto-moto. Baada ya karibu siku nne tu jengo lilikuwa limekwisha. Watazamaji walistaajabu wakapaza sauti: “Neno la Mashahidi wa Yehova lina nguvu!”
KUONDOA HALI YA KUTOJUA KUSOMA WALA KUANDIKA
Kutojua kusoma wala kuandika kulitatiza sana Wakisi na Wagbandi. Vijiji vizima havikuwa na wasomaji. Hata hivyo kila mahali watu walipendezwa sana na habari njema. Wakati mmoja, kijiji cha watu 50 kiliomba mtu wa kwenda kuwafundisha, lakini hakupatikana mtu mwenye kustahili kutumwa. Ndugu wachache waliojua kusoma walikuwa tayari wana kazi nyingi. Ilifaa sana ndugu Wakisi na Wagbandi wajifunze kusoma lugha yao wenyewe. Injili ya Yohana ilikuwako katika Kigbandi. Lakini katika Liberia, ilielekea kwamba hakukuwa na sehemu za Maandiko katika lugha ya Wakisi. Baadaye, ilijulikana kwamba sehemu kubwa ya Biblia ilichapwa katika lugha ya Wakisi katika Guinea, lakini ilitofautiana kidogo na lugha iliyotumiwa Liberia.
Rene leRoux, aliyetumikia kama mwangalizi wa mzunguko, alisaidia ndugu wakatayarisha vitabu vyao wenyewe vya masomo ya msingi katika lugha za Wakisi na Wagbandi. Kitabu cha Wakisi kilikuwa na picha nzuri, nasi tulichapiwa na Idara ya Habari na Mambo ya Utamaduni, katika Monrovia. Kitabu cha Kigbandi kilinakiliwa katika afisi ya tawi ya Watch Tower Society. Baada ya kupokea misaada hiyo, akina ndugu walitia juhudi wajifunze kusoma. Kufika Agosti 1962, ndugu 47 Wakisi na Wagbandi walikuwa wamejua kusoma na kuandika katika lugha zao! Wakisi walikuwa wakitazamia kupokea trakti na kijitabu “Habari Njema Hizi za Ufalme” vitumiwe katika utumishi wa shambani. Makao ya Brooklyn ya Sosaiti yalikuwa yamepelekewa hati za vijitabu hivyo ili kuvichapa.
KUSANYIKO “HEKIMA YENYE KUTOA UZIMA”
Kusanyiko hilo la taifa la 1957 lilifanywa Harper, Cape Palmas, kutoka Desemba 18 mpaka 22. Ilikuwa ndiyo mara ya kwanza kuwa na kusanyiko la namna hiyo katika Cape, na karibu ndugu 90 kati ya 291 wa nchi hiyo waliweza kuhudhuria. Kama ilivyokuwa katika kusanyiko la mwaka uliotangulia katika Greenville, meli ilihitajiwa kusafirisha wajumbe kutoka Monrovia. Lakini, wakati huu meli kubwa ya Kijeremani ya kuchukua shehena iliwasafirisha haraka kwa usiku mmoja. Wajumbe waliimba nyimbo, wakajifunza Mnara wa Mlinzi melini na kufika katika mji wa kusanyiko mapema.
Jengo jipya kabisa la Usimamizi lilikuwa mahali ambapo ufuo wa bahari wa Cape ungeweza kuonekana vizuri pamoja na mitende iliyokuwa kandokando, na lilifaa sana kuwa mahali pa kusikilia “hekima yenye kutoa uzima” ya Yehova Mungu, Watu wanane walizamishwa. Watu 166 walihudhuria hotuba ya watu wote na baada ya hapo wengine zaidi wakaja kuona sinema mpya ya Sosaiti, hudhurio likaongezeka kuwa 228.
Lakini wajumbe wangerudije Monrovia? Ilitegemea kama kungekuwa na meli yenye kuja pwani wakati unaofaa, na kama ingekubali kuchukua abiria iwalaze peupe katika sakafu ya meli. Ndugu hawakuwa na wasiwasi wa jambo hilo wakati wa kusanyiko, kwa maana walitosheka kumwachia Yehova. Imani ilitakiwa, kwa sababu ilikuwa kawaida watu kukaa Cape Palmas juma nyingi wakingojea meli.
Muda mfupi kabla ya hotuba ya watu wote, meli ilionekana kipande ikija pwani. Vipindi vilipokwisha, mipango ilikuwa imekwisha fanywa pamoja na wajumbe wa usafirishaji. Jumatatu wajumbe walipandishwa melini kwa kiti cha mwunzi wa meli na kamba. Kufika Jumanne jioni wote walikuwa wamekwisha rudi Monrovia. Huo ulionekana kama mwujiza! Hasa raia za Cape walishangaa kwa vile Yehova alivyosaidia watu wake.
“MTAZIKWA NA NANI?”
Watu wengi walikuwa wa makanisa mbalimbali kwa sababu tu walitaka kuhakikishiwa watazikwa vizuri na kanisa. Ikiwa hawakulipa haki zao, wasingepigiwa-pigwa kengele ya kanisa wala wasingezikwa kikanisa. Mara nyingi jamaa zilikazwa sana zilipe pesa ambazo marehemu wa ukoo wao hakuwa amelipa. Makanisa yalitumia desturi hiyo kuvunja wanakanisa moyo wasishirikiane nasi, wakisema: “Ukiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova hakuna atakayekuzika!”
Miaka mingi vifo havikutokea kati ya ndugu zetu wala wenye kushirikiana nasi. Hali hiyo, pamoja na kuhubiri kwetu kwamba watu wasingekufa kamwe katika taratibu mpya ya mambo, ilifanya watu waulize: “Ni kweli kwamba Mashahidi wa Yehova hawafi?” Watu hawakutaka kushirikiana nasi, maana walidhani tengenezo halikuwa na mipango ya kuzika wafu. Ndugu wengine walipokufa, watu wengi wa nje walishangaa kuona jeneza likiingizwa ndani ya Jumba la Ufalme ili kuwe na hotuba ya kawaida ya maziko. Badala ya kufuata desturi ya watu wote ya kukodi jamii ya wanamuziki wapige nyimbo za maombolezo wakiwa mbele ya maandamano ya maziko, ndugu wote walifuata jeneza kwa utaratibu, wakiimba nyimbo za Ufalme walipokuwa wakipita katika barabara kubwa kuelekea makaburini. Hilo lilihakikishia watu wengi kwamba tulizika watu wetu, na kwamba tulifanya hivyo bila kutaka malipo ya kanisa.
Watu wengi wameudhika kwa vile ambavyo Mashahidi wa Yehova hawakeshi wakilinda maiti, wakiimba nyimbo za kidini na kunywa usiku kucha. Kwa kawaida mapadre ndio hufungua vipindi hivyo, nazo jamaa hutazamiwa kuleta vinywaji na viburudisho, hata ziwe ni maskini wa mwisho. Kukiwa na mvinyo nyingi, watu wengi watahudhuria, lakini kusipokuwa na vinywaji vingi watu hunung’unika sana: “Kesha hilo halikuwa na vitu!” Ulevi ni wa kawaida sana katika mambo hayo, nao unaleta uasherati, mabishano makali, mapigano na hata mauaji.
Shahidi afapo, kwa kawaida kunakuwa na ubishi mkali juu ya kufanya kesha ikiwa washiriki wale wengine wa jamaa hawamo katika kweli, hata ikiwa marehemu alisema asikeshewe. Wakati mke kijana wa ndugu mwenye juhudi alipokufa miaka kadha iliyopita, ndugu huyo alipinga sana, sana, jitihada za jamaa kufanya kesha. Msimamo wake uliwashangaza sana, hata yeye mwenyewe alipokufa, walikubali kwa hiari wasikeshe wakilinda maiti yake. Jambo hilo liliwafanya wamheshimu sana.
KUFUATA NDOA YA KIMUNGU
Kazi ilipoanza kupanuka, ilionekana lazima hati za ndoa zidaiwe. Kulikuwa na uzembe mwingi wa kuungana katika ndoa kulingana na mila. Kwa kuwa wazazi walikuwa wakiomba mahari nyingi sana kwa ajili ya binti zao, serikali iliweka sheria mahari isipite dola 40. Vilevile, sheria ilisema mtu apewe hati na mkuu mwenyeji anayefaa wakati wa kuandikisha ndoa.
Lakini, kwa kawaida wakuu wengi wenyeji hawakuandikisha ndoa wala kutoa hati. Mume na jamaa ya msichana ndio walioachiwa kuamua kiasi cha mahari na kuona kama wenye kutaka kuoana watapewa ruhusa. Wengi walikuwa na “ndoa ya kuonja,” ambapo mwanamume alitolea wazazi kiasi kidogo, pengine dola 5, apate pendeleo la kuishi na binti mpaka atakapomaliza kulipa mahari na kupewa rasmi binti. Nyakati nyingine, jamaa hazikutaka kulipwa mahari kamili wakati ule ule, maana zilidhani kama kungetokea tukio lisilotazamiwa hata wahitaji pesa, wangeweza kudai mahari wakati huo. Nyakati nyingine, wanaume maskini walikuwa wakilipa mahari kidogo kidogo muda wa miaka mingi.
Ndugu walishauriwa wamalize kulipa mahari mara moja na kupata hati za ndoa. Wakati mkuu mwenyeji hakutoa hati, karatasi inayoitwa Tangazo la Ndoa ilijazwa na ndugu na mkewe na kukubaliwa mpaka wakati ambao wangeweza kupata hati. Miaka iliyofuata, Idara ya Mambo ya Ndani iliona ingefaa waharakishe utoaji wa hati za ndoa zote za mahari. Hizo ziliitwa hati za “mke wa kwanza.” Ikiwa mwanamume alidai kwamba mwanamume mwingine alimchafua mke wake wa kwanza, au akamnyang’anya, adhabu ya kupatikana na hatia ilikuwa kutoa dola 100. Lakini, ilikuwa lazima mshtaki atoe hati ya “mke wa kwanza” kuhakikisha kweli alikuwa ndiye mke wake wa kwanza, si mke wa pili.
Watu wa Yehova walijifanyia jina kwa kutetea hati za ndoa hivi kwamba, katika Idara ya Mambo ya Ndani ya Monrovia, kitabu cha pekee cha uandikishaji kimewekwa kando kwa ajili ya Mashahidi wa Yehova peke yao. Ikiwa ndugu katika mahali pengine po pote nchini hawezi kupata hati, jambo analotakiwa kufanya ni kutoa ushuhuda wa kukubali kulipa mahari, naye atapewa hati.
Mara nyingi watu wenye kupendezwa waliotaka kuhubiri habari njema hawakuwa wameandikisha ndoa. Kwa hiyo, ndoa nyingi zilianza kufanywa. Mwaka 1957 maoni yetu juu ya ndoa yalizungumzwa sana katika Harbel, kwa maana alasiri moja mwangalizi wa wilaya alioza wanaume saba na wake zao kwa kuwaagiza watoe nadhiri, nalo gazeti moja la Monrovia likaeleza habari hizo. Watu wengi walikuja kujionea. Watu 242 walishuhudia sherehe hizo!
KUSONGA MBELE, KUWA NA NGUVU ZAIDI!
Januari 1958, kwa mara ya kwanza katika Liberia yote, walikuwako wahubiri 300 wenye kuripoti. Katika Kolahun, baada ya Bayo Gbondo kutembelea-tembelea mji wa mbali, wenye kupendezwa huko waliamua kwamba ili kuwa Mashahidi wa Yehova halisi, iliwapasa kuzihubiri habari njema pia. Kwa hiyo walikwenda peke yao wakatolea watu wa eneo lote ushuhuda. Baadaye halmashauri moja ilikwenda Jumba la Ufalme maili kadha kutoka hapo, ikashangaza ndugu kwa kuwapa majina ya watu 20 waliokuwa wametumia saa 186 wakieleza watu habari za taratibu mpya ya Mungu.
MAKUSANYIKO MAPENZI YA KIMUNGU
Jambo kuu lililotokea mwaka 1958 ni nafasi ambayo ndugu wa Liberia walipata kuhudhuria Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko la Mataifa yote katika mji New York. Huko nyuma mwaka 1953 jumla ya wajumbe watano walikwenda huko kuhudhuria Kusanyiko Sosaiti ya Ulimwengu Mpya. Ni wangapi ambao wangeweza kwenda huko wakati huu? 22! Picha kubwa ya wajumbe wenye kuhudhuria kusanyiko hilo ilionyeshwa katika gazeti kuu zaidi la Monrovia. Baadaye, makala tisa mbalimbali zilichapwa katika magazeti ya huko kuhusu kusanyiko kubwa hilo, nao watu wakawa wakisimamisha barabarani wajumbe wa kusanyiko waliorudi, wakitaka kupashwa habari za tukio la ajabu.
Kulikuwa na shauku nyingi pia juu ya Mapenzi ya Kimungu Kusanyiko katika Liberia yenyewe, lililofanywa kuanzia Februari 28 mpaka Machi 3, 1959. Juma ya mwisho ya Februari, kikundi baada ya kikundi kilianza kufika Monrovia. Wajumbe wengine wa nchini ndani walishangaa sana kuona mji wa kisasa kwa mara ya kwanza, zaidi ya kukutana na ndugu na dada wengi wenye urafiki. Kikundi kimoja cha wahubiri kumi na watatu walitembea miguu kutoka Cape Palmas, karibu maili 200 (kilomita 322) kwa muda wa siku tisa, na wakati huo waliangusha vitabu vyote vya kueleza watu Biblia, wakatolea watu 450 hotuba kumi na tano.
Mara baada ya kusanyiko kuanza alasiri ya Jumamosi, afisa wa Idara ya Serikali alikuja akasema kwamba wakili wa United Nations alikuwa amepewa ruhusa na rais atumie jengo hilo mpaka Jumanne, ambayo ndiyo iliyokuwa siku ya mwisho ya kusanyiko letu. Asubuhi yake Rais Tubman alithibitisha uamuzi huo. Kwa hiyo ikawa lazima kusanyiko letu lifanywe katika uwanja wa mpira.
Kipindi chetu cha asubuhi ya Jumapili kilifanywa katika Jumba la Ufalme dogo mno mpaka tulipoweza kukamilisha mipango ya kutumia uwanja Antoinette Tubman Stadium. Mwishowe, uwanja ulifunguliwa adhuhuri, nalo kusanyiko likaharakishwa huko kwa furaha kuu, mara tu idara ya kusafisha ya kusanyiko ilipokuwa ikimaliza kusafisha sehemu za kukalia kwa burashi na vifagio. Ndugu hawakuhangaikia upungufu wa viti, maana walitandaza vitambaa vyao vya mfukoni, mikeka na nguo za kujitanda mapajani, katika vipandio vya saruji. Ilionekana walishukuru kuwa na mahali pa kukusanyikia, kwa vile walivyosikiliza kwa njia isiyo ya kawaida wakati wa programu yote ya saa tano.
Jioni ilipokuwa ikiingia Jumatatu hiyo, umeme wote katika uwanja ulikatika isipokuwa ule wa vipaza-sauti. Mwangalizi wa tawi ndiye aliyekuwa akitoa hotuba wakati huo, halafu kwa ghafula akajikuta amezungukwa na wadudu wenye kunuka wa karibu namna zote. Walivutwa na taa ya pekee iliyokuwa juu ya kinara cha msemaji. Alitoa ishara nyingi katika hotuba yake, nyingine za mkazo na nyingine za kujizuia na wadudu hao wenye kumtaabisha. Ndugu Knorr, aliyetembea huko kutoka Betheli ya Brooklyn, ndiye aliyekuwa msemaji atakayefuata, naye alipoona mambo yalivyokuwa alijimwagia-mwagia dawa ya kufukuza wadudu kisha akatumia hekima kupeleka kinara na kikuza-sauti gizani, mahali palipokuwa na nuru ndogo tu kiasi cha kuangaza karatasi zake. Kwa njia hiyo hakusumbuliwa sana na wadudu. Hotuba yake ilipokwisha taa zilikuwa zimekwisha washwa, nao wasikilizaji waliweza kuona njia ya kwenda zao.
Ilipofika jioni ya Jumanne tulirudia mahali petu pa kwanza, Centennial Memorial pavilion. Huko Ndugu Knorr alitolea watu 518 hotuba “Dunia ya Paradiso Kuletwa na Ufalme wa Mungu.” Alikazia uhitaji wa ndugu wengi zaidi kujua kusoma na kuandika. Kitabu kipya Kutoka Paradiso iliyopotea Mpaka Paradiso Iiyopatikana kilisaidia wengine kusoma maneno yote, si kujua tu maana ya picha zote zilizomo.
Katika kusanyiko hilo, ilikuwa ndiyo mara ya kwanza hesabu ya wenye kubatizwa kuwa 69. Tena, lilichangamsha sana Mashahidi Waliberia hivi kwamba, mwishoni mwa mwaka 1959 wa utumishi, kulikuwa na wahubiri 415 wenye kuripoti—na hicho kilikuwa kilele cha sita cha mfululizo, na vilevile ongezeko la 42 kwa mia kupita wastani ya mwaka uliotangulia!
KUJIFUNZA KUSOMA
Baada ya kusanyiko, mkazo zaidi ulitiwa juu ya kujua kusoma na kuandika. Madarasa yalitayarishwa katika makundi, na vitabu vikapatikana kwa kuomba msaada wa afisi ya serikali ya masomo ya ngumbaru. Ingawa ilikuwa vigumu wazee fulani kujifunza, hesabu karibu zote zilionyesha kwamba, kipindi cha miaka mitano iliyoisha mwaka 1962, jumla ya watu 109 walikuwa wamefundishwa kusoma na kuandika katika madarasa ya makundi. Bila shaka hiyo ilisaidia sana kufanya kazi ya kuuhubiri Ufalme iwe na matokeo mazuri sana.
Ndugu na dada walizidi kupendezwa na kusoma, kama inavyoonyesha ripoti ya mwaka 1959 ya mwangalizi wa mzunguko mmoja. Aandika, “Nilipokuwa hapa miezi minne iliyopita nilimkuta Maria mdogo, na wakati huo alikuwa na miaka karibu saba. Sikuweza kuongea naye wakati huo maana hakujua Kiingereza. Lakini sasa ni mhubiri, hutoa mahubiri mazuri ya kutumia Maandiko na huangusha vitabu pia. Lakini juu ya yote, yeye husoma. Nilifurahi nikashangaa alipoinua kikaratasi cha kukaribisha watu mkutanoni akasoma, si kichwa tu, bali pia yaliyoandikwa nyuma ya kikaratasi!”
HESABU YA WAHUBIRI YAWA MARADUFU BAADA YA MIAKA MITATU
Kufika Agosti 1961 hesabu ya wahubiri katika Liberia ilikuwa imekwisha fika 620, na hiyo ilikuwa ajabu! Miaka mitatu barabara kabla ya hapo, mwaka 1958, wahubiri 301 walikuwa wameripoti utumishi wa shambani. Ijapokuwa hudhurio la Ukumbusho wa mwaka 1958 lilikuwa 510, liliongezeka likawa 1,396 miaka miwili baadaye, na mwaka 1961 hesabu ya kushangaza ilihudhuria, watu 1,710.
Kufika mwaka 1960 nchi ilikuwa imegawanywa kukawa na mizunguko mitatu, nayo makusanyiko yalifanywa mahali pengi ili wahubiri waweze kuhudhuria bila kusafiri mbali. Watu waliona kwamba makusanyiko haya hayakuwa ya kikabila bali yalikuwa na mchanganyiko wa mataifa mengi. Mwangalizi wa mzunguko mmoja aliyekuwa mweupe, aliandika hivi: “Usiku mmoja mwanamume Mpentekoste alinijia akaniambia, ‘Ninaloona hapa sijapata kuliona—mzungu akaa ndani ya nyumba ya mweusi, kushirikiana na kula naye. Sisi tuna wamisionari wetu. Wao huja kutuhubiri, lakini hawaji kamwe nyumbani kwetu kula, kushirikiana wala kulala. Mara nyingi sisi huwalaumu ninyi, lakini hatuwezi kukana jambo moja—mwapendana, na hakika hiyo ndiyo njia ya kweli!’”
Wakati wa kipindi cha miaka mitatu, kutoka 1958 mpaka 1961, hesabu ya wahubiri ikawa maradufu. Ndivyo na hesabu ya makundi, maana yaliongezeka kutoka tisa yakawa kumi na manane. Tena, vikundi vilivyokuwa peke yake vilikuwa korija moja (20) au zaidi. Kufika mwishoni mwa 1962 wanafunzi kumi na wawili waliohitimu katika Shule ya Gileadi walikuwa wakitumikia Liberia, na wanne kati yao walikuwa wenyeji.
UPINZANI WAONGEZEKA
Hasa katika maeneo ya Wakisi karibu na Kolahun, majumbe wa makabila waliiona kazi yenye kufanywa na Mashahidi wa Yehova kwa juhudi kama tisho kwa mamlaka yao. Ndugu na watu wenye kupendezwa hawakufuata tena sheria za kabila za kutumia hirizi wala hawakulipa pesa za kutolea mababu waliokufa dhabihu (kuwatambikia). Wasiofuata sheria hizo kwa sababu ya dhamiri walikamatwa na kuadhibiwa isivyo haki, tena majumbe wakuu na wasimamizi wakuu katika wilaya walielezwa kisha wakapasha Katibu wa Ndani katika Monrovia baadhi ya habari hizo.
Ni wazi kwamba, kwa kadiri fulani ndugu wenyewe walijiongezea matata kwa kukaidi mno desturi za kwao isivyokuwa lazima. Wapya wengine walikataa kufanya kazi zilizofanywa na mtaa mzima. Vilevile, wengine hawakujibu wakuu sikuzote kwa heshima na upole waliostahili.—Tito 3:1, 2.
Katika eneo la Limbamba, ndugu walianza kujenga nyumba zao karibu karibu, kama kwamba wawe na mtaa wao wenyewe ulio kando. Pengine hilo lingewaondolea matata ya sheria fulani za kijiji, lakini pia lingeweza kuonwa na wengine kama njia ya kujisimamia wenyewe. Kwa hiyo, ikawa lazima mwangalizi wa mzunguko Rene leRoux aongee kirefu na wakuu wa eneo hilo ili kuwapunguzia wasiwasi na kuwaeleza vizuri makusudi yetu.
KUSANYIKO “WATU WENYE NIA NJEMA”
Kusanyiko la ajabu zaidi ambalo watu wa Yehova wamepata kuwa nalo Liberia lilifanywa mwaka 1970. Kusanyiko kuu la Kiingereza lilianza Desemba 3 na kumalizika tarehe 6 katika jumba Centennial Memorial Pavilion lililopambwa upya na kuwekewa vitu vya kuingiza hewa. Katika Jumba la Ufalme, vipindi viliongozwa katika lugha mbalimbali za kienyeji.
Siku kadha kabla kusanyiko halijaanza, kulikuwa na taraja kutokana na kichwa cha habari ya gazeti “Mashahidi wa Yehova wa U.S. Watazamiwa Kusanyikoni.” Hakika hili ndilo lingekuwa kusanyiko la kwanza la mataifa yote katika Liberia. Siku mbili baada ya makala ya gazeti kutokea, wajumbe wawili wa kwanza kufika kutoka ng’ambo walihojiwa katika televisheni.
Kulikuwa na furaha Jumatano asubuhi wakati wasafiri 55 walipolakiwa kwa uchangamfu na ndugu wengi katika uwanja wa ndege wakiwa wa Jamii ya 4 ya utalii iliyopangwa na Watch Tower. Bas lililo bora zaidi nchini lilikuwa likingoja wageni wetu liwapeleke Monrovia. Lakini kwanza wangekwenda kuona shamba Firestone Plantation. Wageni wengi walishangaa kuona vitu vya kisasa Monrovia, motokaa za kisasa, nyumba zenye gharama nyingi na majengo yenye orofa nyingi.
Wageni walitayarishiwa kipindi cha pekee alasiri hiyo, katika Pavilion. Kilihusu hotuba za historia ya kazi yetu Liberia, kuhoji wamisionari, na maelezo juu ya makabila makubwa manne ya Liberia, na ndugu wenye kuyawakilisha wakaonyesha mavazi yanayovaliwa na wenyeji na kueleza mambo ya kustaajabisha juu ya makabila hayo. Ndipo wahubiri wa Bassa na Kpelle walipoonyesha maonyesho ya kupendeza sana, “Maisha Katika Shamba,” wakaenenda-enenda na kuimba wanavyofanya wakitayarisha shamba la mpunga, wanavyopanda mbegu, wanavyokwaruza udongo, wanavyotawanya ndege, wanavyovuna, na mwishowe jinsi wanavyotwanga mchele katika kinu na kuutayarisha waupike. Kila dada mgeni alipewa kipepeahewa kilichofumiwa Liberia kwa ufundi, kutokana na nyuzi za majani ya mitende, na kupambwa kandokando kwa manyoya ya kuku. Akina ndugu walipewa pete zilizotengenezwa kwa kokwa za tende.
Ndipo kukawa na karamu nzuri sana ya nyama za Kiafrika na Kilebanoni. Wasafiri walikula vitamu-vitamu kama wali uitwao jallaf, majani ya viazi, ndizi za kukaanga na pombe ya tangawizi. Chakula halisi cha muhogo uliochachwa, kiitwacho fufu, kilionjwa. Msafiri mmoja alisema yafuatayo siku ya kwanza ya kuwa Afrika ilipokwisha: “Hata tusipoendelea kusafiri, tumepata thawabu!”
Ndugu Waliberia walifurahia kutolea watu ushuhuda pamoja na wageni asubuhi iliyofuata, katika utumishi wa shambani. Ndugu hao walikuwa wa nchi mbalimbali, lakini walikuwa na roho moja ya upendo, ya udugu.
Wakati wa kusanyiko, watu 62 walibatizwa katika bahari Atlantic Ocean. Wenye kubatizwa walikuwa watu walioishi maisha ya namna nyingi. Mmoja alikuwa wakili mashuhuri, mwingine alikuwa mwanamke Mwamerika aliyekuja Liberia na askari waitwao Peace Corps. Alikuwako kisichana mrembo Neini mwenye umri wa miaka kumi na saba, aliyetoka Ganta, naye alikuwa amefukuzwa shuleni majuzi kwa sababu ya imani, na vilevile Angeline, mke kijana aliyepigwa vikali na kufukuzwa mwishowe na mumewe mwenye hasira, kwa sababu ya kweli. Halafu alikuwako “Baba” Beckles, aliyekuwa mhubiri Mprotestante.
Jamii ya 4 iliyotayarishwa utalii na Watch Tower ilipoondoka asubuhi hiyo ya Ijumaa, jamii ya pili ilifika. Ilikuwa na Mashahidi 40, kutia na M. G. Henschel, aliyekuwa amevumilia mateso kwa uaminifu akiwa na ndugu zake Waliberia uwanjani katika Gbarnga, miaka saba kabla ya hapo. Alikuwa amepona mapigo makali ya kichwa na shingo aliyopata kutokana na matako ya bunduki, na alasiri hiyo ya Ijumaa alihuhubu habari yenye kufaa “Twaabudu Tukijuacho.” Kipindi cha alasiri kilipokwisha, wengi waliokuwa katika uwanja huko Gbarnga walikuja kupeana mikono na salamu za kushikana vidole na ndugu yao mwaminifu. Walikumbushana mateso yaliyowapata, wakacheka majina fulani ambayo ndugu mbalimbali walipewa na askari. Walikuwako pia baadhi ya watoto wenye adabu waliokuwa wamevumilia mateso hayo wakawa wahubiri wazuri wa Ufalme. Ulikuwa wakati bora wenye furaha, wakati wa kutiana sana moyo na kukaza nia kuendelea kuwa thabiti.
Asubuhi yake, ndege iliyochukua Ndugu Henschel na kikundi hiki cha pili ilipotoweka hewani, ndege nyingine ilitua. Mwanamume na mwanamke walishuka pamoja na abiria wengine, wakaonekana wakitembea haraka uwanjani. Walijulikana—Ndugu na Dada Knorr! Ndege yao ilikuwa imetoka Freetown kuelekea Accra, kukawa na ushirika wenye kufurahisha kwa muda mfupi waliotua hapo Liberia.
UKUZI WAENDELEA
Kufika 1975, kazi ya kuuhubiri Ufalme ilipanuka sana katika maeneo yaliyo peke yake hata ikawa lazima makundi mapya yaanzwe. Kufika mwishoni mwa mwaka huo yalikuwako makundi 22 nchini. Wafanya kazi wengi zaidi walihitajiwa kwa sababu ya ukuzi huo mkubwa.
Kusanyiko letu la wilaya “Ushindi wa Kimungu” lililofanywa Desemba 5-9, 1973, lilikuwa la pekee kwa njia nyingi. Tulifurahi kwa vile ambavyo ndugu na dada 88 wa ng’ambo walilihudhuria wakiwa katika safari yao ya kutalii Afrika Magharibi. Ndugu wenyeji walionyesha vionyesho vya kupendeza kuhusu kazi inayofanywa katika shamba la mpunga. Akina dada walionyesha hatua zinazochukuliwa kutayarisha mchele upikwe—kuukausha, kuutwanga katika kinu, kuupepeta ili kuondoa vitakataka (makapi) kisha kuuchagua-chagua. Wakati wote huo walikuwa wakiimba nyimbo za kienyeji zinazoimbwa na mkulima Mliberia anapofanya kazi yake. Mwishoni, matunda na mboga zinazolimwa hapa zilionyeshwa zikatia watu hamu.
Ingawa tulikodi uwanja Tubman mapema sana, tulijulishwa Ijumaa kwamba mchezo wa mpira ulikuwa umepangwa Jumapili saa 10 alasiri, wakati ule ule wa mkutano wetu wa watu wote. Hotuba ilipangwa upya itolewe saa 5 asubuhi ya Jumapili. Ni watu wangapi wangeweza kuja wakati huo? Ndugu William Jackson wa Betheli ya Brooklyn alipomaliza hotuba yake, walikuwako watu 2,225 na hilo ndilo lililokuwa hudhurio kubwa zaidi katika hotuba yo yote ya watu wote. Ushuhuda mkubwa uliotolewa na kusanyiko hili, na furaha ya kuwa na wageni Wakristo wa nchi nyingine waliokuja wawe pamoja nasi wakati huo, ulichangamsha sana kila mmoja wetu hapa ili tushiriki zaidi katika utumishi wa Yehova.
Jumapili, Aprili 7, 1974, ilikuwa siku yenye kufurahisha sana Mashahidi wa Yehova katika Liberia. Wahubiri wale 939 walijitahidi sana kukaribisha watu wengi walivyoweza wahudhurie Chakula cha Bwana cha Jioni siku hiyo. Je! watu wangekuja kwa wingi? Yehova alishukuriwa sana watu 3,310 walipokusanyika katika Majumba ya Ufalme yetu nchini pote. Mwishoni mwa mwaka huo wa utumishi, wapya 160 walikuwa wamebatizwa. Lo! jinsi ulivyokuwa mwaka mzuri wa kujitahidi sana, kwa msaada wa Yehova!
TWATAZAMA MBELE TUKIWA NA MATUMAINI MAZURI
Mei 1947 ndipo Ndugu na Dada Watkins walipofika hapa wakiwa wamisionari. Ndugu Watkins alikuwa ametazamia muda mrefu kuona tukiwa wahubiri wa Ufalme 1,000 katika Liberia. Mwishowe, iliwezekana—baada ya miaka 20. Tuliona furaha inayohusiana na maneno, “Mudogo atakuwa elfu,” nasi tulimshukuru sana Yehova!—Isa. 60:22. ZSB.
Januari 1976 tukawa wahubiri 1,060. Sasa twatafuta njia za kuanza kazi katika maeneo yaliyo peke yake, ambayo hayajapewa ushuhuda. Twatumaini kwamba watangazaji zaidi wa Ufalme wataweza kuwa mapainia wa pekee. Hivyo wafanya kazi watapatikana watumwe mahali hapo penye uhitaji.
Twaendelea kujitahidi kushinda vipingamizi viwili vinavyozuia maendeleo—kutojua kusoma na kuandika na maelekeo ya uasherati. Karibu 24 kwa mia kati ya wahubiri wetu bado hawawezi kusoma na wengine 15 kwa mia wanasoma kwa shida. Miaka mitano iliyopita, watu 130 wametengwa na ushirika kwa sababu ya uasherati. Lakini waaminifu wanaendelea na kazi, nao wana nyingi.
Kati ya idadi ya watu 1,670,000 wa Liberia, wako Wakristo wa jina tu, Waislamu na hesabu kubwa yenye kuamini kwamba vitu vyote (miti, mawe, upepo, n.k.) vina nafsi. Miaka 29 iliyopita, sehemu ziitwazo ‘za Wakristo’ zimemalizwa vizuri. Lakini, ni kazi ndogo sana ambayo imefanywa katika maeneo ya Waislamu thabiti. Vilevile, wengi wanaoamini vitu vyote vina nafsi hawajafikiwa, na wengi wao wametawanyika katika vijiji vidogo vidogo na nusu-miji huko kando-kando ya nchi.
Kazi yetu ya kuhubiri na kufundisha yaendelea, hasa katika maeneo yenye watu wengi. Lakini, mapainia wa pekee wakipatikana, twatumaini kwamba sehemu nyingine zenye watu zitasikia habari njema mwishowe. Twaendelea kumwomba Yehova Mungu wakazi wengi wa hii inayojulikana sana kuwa “nchi ya uhuru” wakubali kweli inayoleta uhuru halisi na uzima wa milele.
—1977 Yearbook