Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w80 12/15 uku. 19
  • Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova (Ufaransa)

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova (Ufaransa)
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
  • Vichwa vidogo
  • MKATA-KUNI MSWISI ASIYEJULIKANA
  • “KULIMA” ARDHI YA WAFARANSA
  • RUSSELL AFANYA ZIARA MBILI ZAIDI UFARANSA
  • RUTHERFORD AZURU​—⁠TENGENEZO JIPYA
  • KUSANYIKO LA MATAIFA YOTE KATIKA PARIS
  • MWITO KWA MAKOLPOTA
  • KUFANYA UKOLPOTA KATIKA UFARANSA
  • BIDII NA UVUMILIVU ULIO MFANO BORA
  • UTENDAJI WAHARAKISHWA KWA KADIRI VITA ILIVYOKARIBIA
  • TENGENEZO LAPIGWA MARUFUKU
  • UFARANSA YAGAWANYWA SEHEMU MBILI
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1980
w80 12/15 uku. 19

Historia ya Kisasa ya Mashahidi wa Yehova (Ufaransa)

KWA ujumla, Ufaransa ni nchi ya Kikatoliki, jamii ya Waprotestanti wa Ufaransa ikiwa ilipunguzwa sana na mateso ya karne ya 16 na ya 17. Hata hivyo, kikieleza juu ya hali ya kidini katika Ufaransa, kitabu Encyclopcedia Britannica kinasema hivi:

“Tukio ambalo limekuwa kawaida ya nchi zote za magharibi (Ulaya) walakini jambo lenye kuonekana sana katika Ufaransa ni watu wengi kuachana na vikundi vya kidini. Linashirikishwa na ukuzi wa viwanda na watu kuhamia mijini. Ingawa jamii za watu mashambani kwa sehemu kubwa zinaendelea kushikamana na imani ya kimila, watu wa mjini, sana sana katika mitaa iliyo mijini, wanaendelea kuachana na Ukristo.”

MKATA-KUNI MSWISI ASIYEJULIKANA

Wakati fulani katika mwaka 1890 na kitu, mkata-kuni Mswisi asiyejulikana mwenye jina Adolphe Weber alisafiri mpaka United States. Huko, katika Pittsburgh, alimfanyia kazi Ndugu Russell akiwa kama mtunza bustani naye akapata maarifa mengi sana ya Kimaandiko kutoka kwake. Baada ya muda fulani, Weber alijitolea kurudi Ulaya akafanye kazi ya kiinjilisti katika nchi zenye kuzungumza lugha ya Kifaransa. Mwishowe Ndugu Russell alikubali pendekezo lake naye akakubali kutoa fedha za kuendesha kazi ya kuhubiri katika sehemu zenye kuzungumza Kifaransa za Ulaya.

Adolphe Weber alikuwa mmoja wa akina yahe mwenye kuonekana kama mmashamba. Walakini, wakati uo huo, alikuwa Mkristo mtawa aliyekomaa aliyejua vizuri lugha za Kiingereza, Kifaransa na Kijeremani. Aliporudi Switzerland, alitia matangazo katika magazeti ya kidini ya lugha ya Kifaransa juu ya Kitabu cha Kwanza cha Studies in the Scriptures na vijitabu vilivyoandikwa na Ndugu Russell.

“KULIMA” ARDHI YA WAFARANSA

Kama matokeo ya kampeni ya kutangaza magazetini ya Ndugu Weber, watu wengi zaidi na zaidi walikuwa wakiagiza kujifunza vitabu vya Biblia vya Sosaiti.

RUSSELL AFANYA ZIARA MBILI ZAIDI UFARANSA

Katika mwaka 1911, tukio kubwa lilikuwa ziara ya msimamizi wa Sosaiti, Charles T. Russell. Katika Aprili 14, alizungumza na kikundi cha zaidi ya watu 100 katika kusanyiko moja lililofanyiwa Denain, na siku iliyofuata akazungumza na watu 70 katika Lens. Wanafunzi wa Biblia kutoka Belgium walikuwapo pia katika makusanyiko hayo.

RUTHERFORD AZURU​—⁠TENGENEZO JIPYA

Kama alivyokuwa ametazamia, Ndugu Rutherford alizuru Paris katika Septemba 1920. Katika Septemba 19, alikutana na karibu ndugu 120, ambao kati yao karibu 40 walikuwa wametoka Ubelgiji na kutoka Alsace.

KUSANYIKO LA MATAIFA YOTE KATIKA PARIS

Kusanyiko kubwa la kwanza katika Paris lilifanywa katika Pleyel Hall, Mei 23-26, 1931; lilianzisha sehemu ya maana katika historia ya Mashahidi wa Yehova katika Ufaransa.

MWITO KWA MAKOLPOTA

Mwito wa kutaka makolpota (mapainia) wengi zaidi ulitolewa katika kusanyiko la Paris. Jambo hilo, pamoja na wonyesho ulio wazi wa roho ya Mungu, lilihimiza wengi waingie katika kazi ya wakati wote. John Cooke, akiwa tineja tu wakati huo lakini ambaye baadaye alitumika kama misionari katika Spania na ambaye kwa sasa anatumika katika Afrika ya Kusini, aandika hivi:

“Lo! hilo lilikuwa kusanyiko kama nini! Sitalisahau kamwe. Lilikuwa jambo lenye kusisimua kwa ndugu kijana aliyezoea kundi dogo kusafiri pamoja na mamia ya ndugu toka London mpaka Paris. Na bado lilikuwa jambo lenye kusisimua kukutana na kundi kubwa zaidi kutoka Ujeremani na ndugu kutoka nchi nyinginezo kadha wa kadha. Ndugu hawa wa kutoka bara walionekana wenye kuchangamka na wenye shauku sana kwetu sisi Wanigereza wapole! . . . Kila kitu kilionekana kimetayarishwa vizuri sana, chenye nguvu nyingi, naye kila mtu alionekana kuwa mwenye furaha sana.

“Ndipo nilipofanya uamuzi ule mkubwa ambao ulibadili maisha yangu. Tayari nilikuwa nimekwisha kufikiria sana juu ya kuwa painia nami nilikuwa na tamaa ya kuwa mmoja, walakini upinzani wa baba yangu ulinizuia. Walakini, mara tu baada ya kipindi cha kwanza, dada mmoja ambaye nilikuwa nikizungumza naye alisema hivi: ‘Ndugu kijana kama wewe apaswa kuwa kolpota (painia), sababu gani wewe si mmoja wao?’ Mara kadha watu mbalimbali walisema mambo kama hayo. Ndugu Rutherford alisema hivi katika njia yake ya kukazia: ‘Cho chote chini ya jua kisiwazuie ninyi vijana msifanye kazi ya ukolpota (upainia).’ “

Ndugu mwingine Mwingereza, Eric Wilkinson, aandika kwamba ‘mtu ye yote kutoka nchi yo yote alialikwa aje Ufaransa ashiriki katika kazi hiyo.’

KUFANYA UKOLPOTA KATIKA UFARANSA

Ndugu Wilkinson anasema hivi juu ya kazi ya ukolpota katika Ufaransa:

“Tulipewa mgawo wa kufanya kazi katika mtaa wenye nyumba mbovu wa Paris. Mabawabu [walinda-milango] walikuwa wameazimia kwamba sisi hatutafanya kazi katika majengo yao kama vile sisi tulivyokuwa tumeazimia tutafanya kazi katika majengo yao. Mara nyingi polisi waliletwa nasi tulipelekwa kwa Mkuu wa Polisi, ambaye mara nyingi alituhurumia na kutuachilia twende zetu. Mwishowe, tulishona nguo ya namna fulani ya kujifunga nyuma yenye mifuko mitano na mishipi iliyopita juu ya mabega yetu. Tuliivaa chini ya koti zetu, nayo ilikuwa ikibeba vitabu vya kutosha jengo moja. Tukiwa nayo tuliweza kuwapita mabawabu (katika vyumba vyao vyenye kuta za kioo), tukiacha vitabu vyetu vilivyosalia juu ya baiskeli zetu. Tulikuwa, bila shaka, tukifanya kazi kwa kadi za kutolea ushuhuda, walakini rafiki yangu (ambaye alizungumza Kifaransa) alishangaa sana kuona kwamba, tofauti na matazamio yake, nilikuwa nikiangusha vitabu zaidi kumpita. Yeye aliwaambia mambo mengi mno, alipomaliza hakukuwa udadisi (kutaka kujua) uliobaki.

BIDII NA UVUMILIVU ULIO MFANO BORA

Mona Brzoska, dada Mwingereza, aliandika kama hivi juu ya mambo aliyoona kama painia katika Ufaransa katika mwaka 1931 na miaka iliyofuata:

“Mahali petu pa kulala wakati wote palikuwa pa kikale sana mojalapo la matatizo makubwa lilikuwa kupasha joto wakati wa majira ya baridi. Mara nyingi tulilazimika kutosheka na chumba chenye baridi nyingi sana mahali ambapo tulilazimika kuivunja barafu iliyokuwa ndani ya bilauri asubuhi yake kabla ya kuweza kunawa. Jiko dogo la mafuta lilitumika kupika chakula chetu rahisi. Vyombo vya kupiga hema vilivyoko leo havikuwako wakati huo. Kwa hiyo vyombo vyetu vilikuwa vya kikale nayo njia yetu ya kuishi haikuwa na mambo mengi.

“Hatukupata kuwaona Wanafunzi wa Biblia wengine; tulikuwa peke yetu kabisa. Hilo ndilo lililokuwa badiliko kubwa zaidi kwa kulinganisha na nchi yetu wenyewe ambapo sikuzote tulikutana na ndugu. Tulilazimika kupigana na hali hiyo ya kuwa pekee kwa kujifunza vitabu vya Sosaiti kwa ukawaida. Kwa kuwa huko nyuma katika siku hizo hatukufanya marudio wala mafunzo ya nyumbani ya Biblia, jioni tulipata wakati wa kuandikia jamaa yetu barua na sana sana mapainia wengine, kushiriki mambo tuliyoyaona na kutiana moyo. Miaka fulani tulilazimika kuufanya Ukumbusho pamoja, sisi wawili tu.

“Tulifanya kazi kwa sehemu kubwa sana ya siku. Tulisafiri kilometres 50 au 60 [maili 31-37] kwa baiskeli zetu kila siku. Ilitupasa kutoka asubuhi mapema, sana sana wakati wa majira ya baridi, ili tutumie vema saa za mchana.”

Ijapokuwa wengi wa mapainia wa kwanza walikuwa Waingereza, kulikuwako wengine wa mataifa mengine, kutia Wajeremani, Waswisi, Wapoland na Wafaransa.

UTENDAJI WAHARAKISHWA KWA KADIRI VITA ILIVYOKARIBIA

Hali ya vita ilikuwa imeanza kuongezeka katika Ulaya, naye Ndugu Knecht alitangulia kuona kwamba yale yaliyokuwa yakiwapata ndugu zetu katika Ujeremani yangeweza kuwapata karibuni Mashahidi wa Yehova katika sehemu nyingine za Ulaya, kutia na Ufaransa. Kwa hiyo alitembelea makusanyiko ya eneo la dunia na makundi katika Ufaransa na kuwaonya ndugu waanze kujitayarisha kwa ajili ya magumu yaliyokuwa mbele.

Katika mwaka 1938 Ndugu Franz Zurcher kutoka Betheli ya Berne alichapa kitabu chenye kichwa “Vita ya Kidini Dhidi (Juu) ya Ukristo,” kilichotoa habari ndefu juu ya mateso ya Mashahidi wa Yehova katika Ujeremani ya Nazi.

Miaka hiyo iliyotangulia vita ilimalizika kukiwapo makundi 84 katika Ufaransa. Kati yake, 13 yalikuwa yenye kusema Kijeremani katika Alsace-Lorrarine, 32 yalikuwa yakisema Kipoland, sana sana yakiwa katika kaskazini mwa Ufaransa, na 39 yalikuwa yakisema Kifaransa. Jumla ya wahubiri ilikuwa 1,004, ambayo ilikuwa ongezeko la asilimia 19 zaidi ya mwaka uliotangulia.

TENGENEZO LAPIGWA MARUFUKU

Katikati ya Oktoba 1939, juma zipatazo sita baada ya kuanza kwa vita hiyo, tengenezo la Mashahidi wa Yehova lilipigwa marufuku katika Ufaransa. Walakini Ndugu Knecht alikuwa ameuona uwezekano huo naye alikuwa amewaonya akina ndugu. Kwa hiyo makundi mengi yalipata nafasi ya kutawanya akiba zao za vitabu kwenye sehemu mbalimbali zilizokuwa salama zaidi, kama ilivyokuwa imefanywa muda mfupi tu kabla ya kutwaliwa kwa afisi ya Sosaiti katika Paris. Betheli katika Enghien-les-Bains ilipekuliwa pia, walakini Ndugu Knecht alikuwa amekwisha kuondoa stenseli zilizokuwa na anwani za watu wote walioandikisha Mnara wa Mlinzi na Consolation, pamoja na faili nyingine za muhimu.

Siku chache baadaye, katika Novemba 2, 1939, Ndugu Knecht akafa, akiwa na umri wa miaka 41. Kwa miaka mingi alikuwa amemtumikia Yehova kwa uaminifu katika utumishi wa wakati wote. Alipendwa sana na akina ndugu katika Ufaransa, zaidi sana kwa sababu wote waliokuwa wamesimamia kazi katika Ufaransa hadi wakati huo (Lanz, Freytag, Binkele, Zaugg na Zopfer) walikuwa wameasi. Iwapo kuna somo fulani liwezalo kutolewa na historia ya kazi katika Ufaransa, ni kwamba bila shaka kazi ya Yehova haimtegemei mtu ye yote mmoja.

UFARANSA YAGAWANYWA SEHEMU MBILI

Majeshi ya Vifaru ya Ujeremani yalivyosonga mbele katika Ufaransa, ndivyo barabara zilizoelekea kusini zilivyokuwa na mfuatano wa wakimbizi waliokuwa wakikimbia majeshi yenye kuteka. Baadhi ya akina ndugu walibaki walipokuwa, hali wengine walikimbia kusini. Ndugu Geiger aliondoka Paris na kurudia mkewe na mwanawe katika Dordogne Department, kusini-magharibi mwa sehemu ya kati. Katika Juni 22, 1940, Jemadari Mkatoliki Petain alitia sahihi mapatano ya kuacha vita kwa muda pamoja na Ujeremani ya Nazi.

Ufaransa iligawanywa sehemu mbili: sehemu ya kaskazini na kisehemu cha nchi katika pwani ya magharibi zilikaliwa na majeshi ya Ujeremani na kusimamiwa nao, hali sehemu nyingine ya Ufaransa haikutwaliwa bali ilisimamiwa na serikali ya Vichy yenye kuunga mkono Ujeremani, ikiwa na Jemadari Petain kama kiongozi wa serikali.

Ikieleza juu ya hali hiyo, ripoti moja iliyotumwa Brooklyn kutoka Afisi ya Ulaya ya Kati katika Berne, Switzerland, ilisema hivi:

“Tangu wakati Ufaransa ilipotwaliwa na Wajeremani kupashana habari na ndugu katika Paris na sehemu zinazokaliwa na majeshi yenye kuteka kumekoma kabisa. Wala hata barua au kadi moja, wala ishara yo yote haijatufikia.

“Kwa habari ya eneo la Ufaransa lisilokaliwa na majeshi yenye kuteka, twapokezana barua kwa ukawaida pamoja na ndugu [Henri Geiger] ambaye hapo kwanza aliwakilisha Sosaiti katika Alsace. Yeye pia anaripoti kwamba hana habari zo zote juu ya ndugu ambao hapo kwanza walifanya kazi katika Paris na kuishi katika nyumba iliyokuwa Enghien.

“Vilevile haiwezekani kabisa kwa ndugu Waswisi kupata cheti ama eneo linalokaliwa na majeshi yenye kuteka ama eneo la Ufaransa lisilokaliwa na majeshi yenye kuteka.”‏​—⁠Kutoka Kitabu cha Mwaka cha 1980.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki