Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb88 kur. 136-197
  • Korea

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Korea
  • 1988 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • NCHI ILIYOGAWANYIKA
  • KUPENDEZWA KATIKA MASHARIKI
  • MKOREA WA KWANZA ALIYE WAKFU
  • MSAADA ZAIDI KUTOKA NG’AMBO
  • MATBAA YA KWANZA
  • CHINI YA USIMAMIZI MPYA
  • UTENDAJI WA KOLPOTA
  • MAVAMIZI YA POLISI
  • ILE KAZI YAENDELEA
  • JAMAA YENYE UVUTANO MKUBWA YAKIMBIA “BABULONI”
  • ONYO LA WAKATI UFAAO
  • WASHIKA UKAMILIFU WA MAPEMA
  • MWAMINIFU MPAKA KIFO
  • BAADA YA VITA YA ULIMWENGU YA PILI, MZINDUKO
  • “MASHAHIDI WA YEHOVA WAMEKUWA HAI TENA”
  • “KARIBU, MJUMBE WA TUMAINI WA MNARA WA MLINZI”
  • HUDUMA ILIYOPANGWA KITENGENEZO YAANZA
  • MIKUTANO ILIYOPANGWA KITENGENEZO YACHOCHEA NDUGU
  • WAMISIONARI WENGINE WAWASILI
  • VITA YA KOREA
  • WAMISIONARI WAHAMISHWA
  • WAAMINIFU YAJAPOKUWA MAGUMU
  • WAKIMBIZI TENA
  • KAZI YASONGA MBELE ZIJAPOKUWA HALI ZA UKIMBIZI
  • MSAADA WA MISIONARI WARUDI
  • HATIMAYE! MNARA WA MLINZI WENYE KUPIGWA CHAPA
  • TAWI LAANZISHWA
  • MSAADA KUTOKA CHANZO KISICHOTAZAMIWA
  • MKUSANYIKO MKUBWA WA KWANZA
  • GILEADI YATUMA MSAADA ZAIDI
  • KAO LA WAMISIONARI LA PUSAN
  • ZIARA YENYE KUONYESHA MAENDELEO MAKUBWA
  • MSAADA KWA ELIMU YA BIBLIA
  • JAMAA YA WAFANYA KAZI WENYE BIDII
  • MAPENZI YA KIMUNGU KUSANYIKO LA KIMATAIFA LA 1958
  • MPANUKO KATIKA KAZI YA MZUNGUKO
  • KUPONEA CHUPUCHUPU WAKATI WA GHASIA
  • VIZUIZI VYA MUDA
  • “HABARI NJEMA ZA MILELE” MAKUSANYIKO
  • MPANUO WA TAWI WA KWANZA
  • VITABU VYENYE JALADA LAINI VYA KUTUMIWA SHAMBANI
  • NI SHAURI LA DHAMIRI
  • ULIOPATA KUWA MKUBWA ZAIDI
  • SABABU YA HANGAIKO
  • NJIA YA KURUDI, NDEFU LAKINI HAKIKA
  • JUMBA LA KUSANYIKO LA KWANZA KATIKA MASHARIKI
  • MAREKEBISHO YA UTANGAZAJI WA MAGAZETI
  • WAMISIONARI WAZUIWA KUINGIA
  • MRADI MKUBWA MNO
  • MATBAA-VIKUTO YENYE MWENDO WA KASI INAVUMA
  • KUTAZAMA MBELE
1988 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb88 kur. 136-197

Korea

KAMA inavyoonekana kutoka satelaiti kilometa nyingi juu, Korea ni peninsula yenye mandhari nzuri sana katika kaskazini-mashariki mwa Esia. Iko kidogo tu magharibi mwa visiwa vya Japani, na China na Urusi zimepakana nayo upande wa kaskazini. Visiwa zaidi ya 3,000 vinatapakaa katika ile bahari pande za pwani za kusini na magharibi ingawa 2,600 havikaliwi. Na ukubwa wa Korea? Ina ukubwa unaokaribia ule wa Uingereza.

Inapoonwa tokea karibu, Korea inabadilika kuwa mojapo mandhari za ulimwengu zenye vilima-vilima, ikiacha asilimia ipatayo 20 ya ardhi inayofaa kwa ukulima, mpunga ukiwa ndio zao kubwa nchini. Nyanda hutandaa kuelekea pwani za magharibi, kaskazini-mashariki, na kusini. Pepo za misimu huvuma zikipita kati ya nchi, kwanza upande mmoja, kisha upande mwingine, na kuiletea vipupwe vikavu vyenye baridi, na viangazi vyenye joto na mvua.

Mtazamo wa uso kwa uso unafunua kwamba Wakorea walio wengi wana tabia za mwilini zinazofanana na za Waesia wengine—uso mpana, nywele nyeusi zilizonyooka, ngozi ya zeituni-hudhurungi, na macho meusi. Hata hivyo, wao ni tofauti katika utamaduni wao, lugha, mavazi, na upishi nao wanadai kuwa na historia ya kibinadamu ya zaidi ya miaka 4,000. Lugha yao, ambayo ni ya jamaa ya lugha ya Kialtai, inasemwa leo na watu zaidi ya milioni 60.

NCHI ILIYOGAWANYIKA

Kwa sababu ya Korea kuwa mahali panapofaa kuongozea mambo ya kivita, mataifa yenye nguvu zaidi, kama vile China na Japani, kwa muda mrefu yametumia uvutano wenye nguvu juu ya watu wayo. Kama njia ya kujikinga, watu wa Korea walijitenga wenyewe wakawa ule ambao umepata kuitwa ufalme mpweke. Katika 1910 Japani ililazimisha juu ya Korea utawala wa kikoloni ulioendelea mpaka mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili, wakati ambapo peninsula hiyo iligawanywa kwenye latitudo ya 38 kati ya majeshi ya United States upande wa kusini na majeshi ya Urusi upande wa kaskazini. Katika 1948, kwa azimio la Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) iliundwa upande wa kusini. Katika mwaka uo huo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Korea (Korea Kaskazini) iliundwa upande wa kaskazini. Serikali zote mbili zinadai kuwakilisha Korea yote.

Katika Juni 25, 1950, kwa sababu ya kusini kuvamiwa na kaskazini, ile vita ya Korea ya miaka mitatu ikaanza. Hiyo ilifanya nchi igawanywe kwa kadiri ya kudumu zaidi na eneo lililoondolewa majeshi, lenye kutoka mashariki kwenda magharibi kilometa 56 tu kaskazini mwa mji wa Seoul. Ile serikali ya kaskazini hairuhusu nafasi kwa ajili ya dini, na hivyo inakataza utendaji wa Mashahidi wa Yehova.

KUPENDEZWA KATIKA MASHARIKI

Msimamizi wa kwanza wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, Charles Taze Russell, akiwa mwenyekiti wa IBSA (International Bible Students Association) halmashauri ya watu saba, alitembelea Mashariki kwa mara ya kwanza mapema katika 1912 “kuona hali za wapagani,” likaripoti Mnara wa Mlinzi la Desemba 15, 1912. “Kama matokeo ya uchunguzi huo iliamuliwa kwamba hali katika upagani zilitoa haki ya kutumiwa kwa baadhi ya fedha za Sosaiti katika kutangaza ile Gospeli ya Ufalme kule,” lile simulizi likaendelea. “Kwa hiyo, vitabu vya bure vilichapishwa katika lugha sita kubwa,” kutia na Kikorea.

Akikubaliana na yaliyopata kuonwa na ile halmashauri, Ndugu Robert R. Hollister aliliwakilisha Shirika hilo katika Mashariki, kutia na Korea. Yeye alipangia tafsiri na uchapishaji wa kile kitabu The Divine Plan of the Ages katika lugha ya Korea. Kilichapwa katika Yokohama, Japani, kikionyesha tarehe yayo ya kutangazwa kuwa Machi 18, 1914, mtangazaji akiwa International Bible Students Association na R. R. Hollister akiwa mwakilishi. Ndugu na Dada W. J. Hollister pia walitumia wakati mwingi sana wakipanda mbegu za ukweli wa Ufalme katika Korea.

MKOREA WA KWANZA ALIYE WAKFU

Mnara wa Mlinzi wa Agosti 15, 1914 (katika Kiingereza), ulichapisha barua yenye kuvutia aliyoandikiwa Ndugu Russell, ikitaarifu: “Mimi ni mgeni kwako katika maana moja; lakini mimi nilikuja kwenye maarifa ya Ukweli wa Sasa kupitia maandishi yako miezi ishirini na miwili tu iliyopita. Kwa wakati fulani mimi nimekuwa na hamu ya kuandika nikuambie juu ya uthamini wangu wa pekee wa ule Ukweli, lakini hali hazikuniruhusu mpaka sasa.

“Wewe utapendezwa kujua kwamba mimi ni Mkorea. Wakati wamisionari wa kwanza walipofika hapa (katika 1885) Korea ilikuwa ufalme mpweke. Tangu wakati huo Wakorea fulani wakaja kutambulishwa na Ukristo.

Kwa miaka ipatayo minane mimi nilipeperushwa kupitia ile mikondo hatari ya kile ambacho sasa ninakijua kuwa ni Mawasiliano na Ulimwengu wa Roho—mafundisho ya Kishetani. Sasa mimi nashukuru Mungu kwamba Yeye alituma Ndugu yetu mpendwa R. R. Hollister hapa pamoja na zile Habari Njema na kuniokoa na mikondo hii iliyokuwa ikiniongoza mahali pasipojulikana.

“Hisia zangu zilikuwa karibu zimepotea; ilichukua karibu miezi sita kufungua macho na masikio ya ufahamu wangu. Tangu hapo mimi nimejitoa mwenyewe kwa Bwana na ninaendelea kumsifu Yeye.”—Imesainiwa, P. S. Kang.

P. S. Kang alikuwa nani, naye alijifunzaje ukweli?

Ndugu R. R. Hollister alieleza hadhirina ya mkusanyiko mmoja wa shirika IBSA katika San Francisco jinsi yeye alivyokutana na Bw. Kang. “Katika Korea, Bwana alinielekeza mimi kwa Kang Pom-shika ambaye hapo mwanzoni aliajiriwa afanye kazi ya tafsiri kwa msingi wa kibiashara kabisa,” akasema Hollister. “Upesi yeye alianza kupendezwa sana kibinafsi na makala alizokuwa akifanyia kazi, na baada ya kutumia miezi fulani katika afisi yetu, yeye alidai kujitoa kabisa [kujiweka wakfu] kwa Bwana. Tangu hapo yeye ametumiwa sana katika kutafsiri, kukalimani, kuongoza darasa, na kusimamia tawi la Korea. Mimi ninatazamia kwa uhakika ile raha ya kujulisha yeye kwa ninyi mlio kwenye Kusanyiko Kuu akiwa mjumbe kutoka lile ‘Taifa Pweke.’”

MSAADA ZAIDI KUTOKA NG’AMBO

Katika 1915 Dada Fanny L. Mackenzie, kolpota (mhubiri wa wakati wote) mmoja kutoka Uingereza, alianza kufanya ziara za pindi kwa pindi katika Korea, akilipia gharama zake mwenyewe za kusafiria. Yeye alitumia karatasi yenye anwani ya IBSA kutoa ushuhuda. Jinsi gani? Ni kwa kuchapa ujumbe fulani wa Ufalme upande wa mbele wa karatasi hiyo katika Kiingereza na kuchapa upande wa nyuma tafsiri ya Kichina, lugha ambayo ingeweza kueleweka na walio wengi katika nchi za Mashariki.

Ile barua ilitolea watu nafasi ya kuachiwa kile kitabu The Divine Plan of the Ages kwa msingi wa jaribio. Maandishi ya tawi yanaonyesha yeye aliangusha vitabu 281. Licha ya bidii-endelevu yake katika kazi hii ya kugawa vitabu, yeye pia alimlipa Ndugu Kang kiasi kinacholingana na dola 15 kwa ajili ya gharama zake za kibinafsi. Katika 1949, akiwa na umri wa miaka 91, yeye alimpa maandishi haya mratibu wa sasa wa tawi, Don Steele, kabla ya yeye kuja Korea.

MATBAA YA KWANZA

Ndugu Kang, mwandishi aliyesimamia kazi katika Korea, na washiriki wenzake waliendelea kueneza ujumbe, lakini itikio lilikuwa la polepole. Hata hivyo, katika 1921 wao walifanya mikutano ya watu wote kwa “kusafiri-safiri” kote kote nchini, na kile kijitabu Millions Now Living Will Never Die kilitangazwa katika lugha ya mahali hapo na kugawanywa. Korea sasa ikajiunga na ile orodha ya matawi 18 ya Sosaiti nje ya United States.

Kuchapisha ule ujumbe katika lugha ya Korea nje ya nchi kulifanyiza magumu mengi. Kwa hiyo, katika 1922 Ndugu Rutherford alimtumia Ndugu Kang dola 2,000 za Kiamerika asimamishe matbaa ndogo yenye kufikia mashine saba. Hizo mashine za chapa zilitokeza vitabu katika lugha za Kikorea, Kichina na Kijapani. Na bado, hakuna ongezeko kubwa lililoonekana wakati wa miaka hiyo.

CHINI YA USIMAMIZI MPYA

Sosaiti ilianzisha tawi moja katika Japani katika vuli ya 1926 na ikamweka rasmi Junzo Akashi, Mjapani-Mwamerika, awe mwakilishi wa Japani, China, na Korea. Katika wakati ule ule, Ndugu Kang, ambaye alikuwa amekuwa akisimamia kazi katika Korea, alikuwa akitumia matbaa ya Sosaiti kwa matumizi yake mwenyewe, akichapisha vitabu vya kilimwengu. Hata alikuwa na usafihi wa kuiuza ile matbaa bila ruhusa. Ndugu Park Min-joon alichukua mahali pake katika 1927.

Ndugu Park, kolpota, alikuwa ndugu mwaminifu ambaye alikuwa amefanya safari ndefu kwa miguu juu na chini ya ile peninsula akifanya mikutano ya watu wote na kuangusha vitabu. Yeye alikutana na upinzani wa pekee kutoka kwa wamisionari Waprotestanti, lakini polisi wa mahali pale, ambao wakati huo walikuwa Wajapani kwa sababu Korea ilikuwa chini ya utawala wa Kijapani, mara nyingi walimsaidia.

Kwa kuwa kufikia 1931 makao makubwa zaidi yalihitajiwa kwa ajili ya afisi, ilihamishwa kupelekwa kwenye kao la Ndugu Park kwenye 147 Key Dong katika Seoul.

Ndugu Park alijua lugha ya Kiingereza vizuri naye alitafsiri vitabu Reconciliation na Government, na vingine pia, kutoka Kiingereza kuingiza katika Kikorea. Ufasaha wake katika lugha ya Kiingereza ulimwezesha yeye kuandikiana moja kwa moja na Sosaiti katika New York. Kwa wazi, hata hivyo, Ndugu Park hakuwa stadi katika Kijapani kwa kadiri ambayo Akashi alitamani, na hivyo mwingine alichukua mahali pake katika 1935. Ndugu Moon Tae-soon, mwalimu wa shule, aliwekwa asimamie ile kazi. Bidii-endelevu ya Ndugu Moon akiwa mfanya kazi wa shambani wakati wote ingejaribiwa katika wakati ujao.

UTENDAJI WA KOLPOTA

Ndugu Lee Shi-chong, akiwa na umri wa miaka 22, aliweka maisha yake wakfu kwa Yehova katika 1930 na akajitoa mwenyewe kwa utumishi wa kolpota. “Mimi sikuwa shujaa vya kutosha kuhubiri katika mji, kwa hiyo mimi nilijipatia baiskeli moja na kuamua kuhubiri katika mikoa,” Ndugu Lee anatuambia. “Mimi nilirundika mizigo na vitabu vyangu juu ya baiskeli yangu, na mahali pa kwanza nilipokwenda palikuwa ile afisi ya jimbo katika Mkoa wa Kyŏnggi. Mimi nilisita-sita kuingia ndani, lakini nikafikiria utume wangu nikiwa balozi wa Ufalme, usemi niliokuwa nimeusikia mara nyingi kutoka kwa meneja wa tawi. Tokeo likawa kwamba niliangusha vitabu kadhaa kwa wale wakuu, nami nikatiwa moyo sana na nikawa na uhakika tokea hapo na kuendelea.”

Ndugu Lee, ambaye sasa anatumikia akiwa mzee katika kundi moja la Seoul, alisafiri urefu na upana wa ile nchi, akifikia ile ambayo sasa ni Korea Kaskazini na hata akaingia Manchuria. Yeye alikuwa akiagiza vitabu kutoka afisi ya Seoul na kuomba vitumwe mbele kwenye kijiji au mji uliofuata. Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha yake kwa miaka mitatu mpaka 1933 wakati kazi ya kutoa ushuhuda ilipokuja chini ya magumu.

Maandishi ya mwaka 1931 yanaonyesha kwamba watangazaji wa Ufalme walikuwa wenye shughuli. Wao walifikia makao 30,920, wakatumia saa 11,853 katika shamba, na wakagawa vitabu 2,753, vijitabu 13,136, na nakala 3,940 za gazeti Golden Age. Katika 1932 Korea ikawa na mkusanyiko wayo wa kwanza, kuanzia Juni 11 mpaka 13 katika Seoul, kukiwa na 45 waliohudhuria. Katika mwaka uo huo nakala 50,000 za kile kijitabu The Kingdom, the Hope of the World zilitolewa katika Kikorea ili zigawanywe bure. Hivyo, kazi katika Korea ilikuwa inapanuka.

MAVAMIZI YA POLISI

Ile serikali ya kijeshi ya Japani ilitenda kwa ukali kwa ajili ya utendaji huu ulioongezeka wa watu wa Yehova. Mwangalizi wa tawi katika Japani alitoa ripoti ifuatayo, iliyohusu Japani na Korea pia:

‘Mimi niliondoka Tokyo kwenda safarini katika Mei 10, 1933, na nikapokea barua iliyokuja kwa ndege kwenye Mukden ya Manchuria, katika Mei 15, ambayo kutokana nayo nilijifunza kwamba ndugu wote watano walio wafanya kazi kwenye tawi letu [katika Tokyo] walikamatwa na kutiwa gerezani nayo kazi katika tawi ikaendelezwa na akina dada. Nyusipepa za Mei 16 na 17 zilitumia karibu kurasa nzima-nzima kutoa ripoti za kukamatwa kwa Mashahidi wa Yehova.

‘Polisi walivamia afisi za Sosaiti katika Tokyo na Seoul. Wao walipokonya akiba nzima ya vichapo vyetu. Ninyi hakika mtafurahi kujua kwamba akina ndugu Wajapani na Wakorea walishikilia uaminifu na ukamilifu wao kwa Yehova na Mfalme wake mpakwa-mafuta hata wakati wa mitihani hii mikali.’

Kiasi cha vitabu vilivyonyakuliwa na polisi kutoka afisi ya Sosaiti ya Seoul katika Juni 17, 1933, kilikadiriwa kuwa vipande 50,000. Vilipelekwa penye Mto Han katika Seoul kwa mikokoteni 18 na kuchomwa hadharani, ikaripoti nyusipepa ya Seoul Tong A Ilbo. Hiyo makala ilisema pia kwamba katika Agosti 15, 1933, karibu vipande 3,000 vya vitabu vilipokonywa na kuharibiwa kwenye makao ya akina ndugu karibu Pyongyang, sasa katika Korea Kaskazini. Lakini je! mavamizi hayo ya polisi yalinyamazisha kazi ya kutoa ushuhuda?

ILE KAZI YAENDELEA

Kolpota Lee Shi-chong, aliyeitwa arudi Seoul kwa sababu ya kule kukamatwa kwa akina ndugu, anakumbuka: “Upesi akina ndugu walipata tena uhodari wao na wakaanza tena kuhubiri kwa kutumia The Golden Age, kichapo pekee ambacho hakikupigwa marufuku, na, bila shaka, sisi tuliendelea kufanya mikutano yetu.”

The Golden Age lilitumiwa katika shamba la Korea kuanzia 1933 kufika 1939 na liliandikishwa kuwa nyusipepa. Bei yalo ilikuwa jeon mbili, kiasi kinacholingana na senti moja (ya Kiamerika). Ijapokuwa ile akiba kuu ya vitabu ilikuwa imeharibiwa, wengi wa akina ndugu wangali walikuwa na vitabu na vijitabu kadhaa vyao wenyewe, na hivi vilikopeshwa na kubadilishanwa miongoni mwa akina ndugu ili kwamba watu ambao walipendezwa kweli kweli waweze kupokea ule ujumbe.

Mikutano ilifanywa Jumapili kila juma. Ndugu aliyekuwa akiongoza alikuwa akisema kwa saa moja, na ikiwa walikuwapo wapya, yeye alikuwa akizungumzia yale mafundisho ya msingi kwa ajili yao. Kiongozi alikuwa akieleza pia makala ya Mnara wa Mlinzi, kwa kuwa wale wengine hawakuwa na nakala ambayo katika hiyo wangefuata. Mnara wa Mlinzi ulichapishwa kwa namna ya kijitabu na katika Kijapani. Wakati nchi ilipotwaliwa na jeshi la Wajapani, Wakorea walilazimika kutumia lugha ya Kijapani na kwa hiyo wangeweza kuisoma, kuiandika, na kuiongea.

Hata hivyo, walikuwako ndugu wachache waliostahili katika Seoul kuongoza mikutano hii. Ni kwa sababu gani ilikuwa hivyo? Kwa sababu mwangalizi wa tawi aliandikisha wale wote ambao angeweza kuandikisha katika kazi ya kolpota kisha kuwatuma kwenye maeneo ya mbali. Kama tokeo, wale ndugu wenye ujuzi walitapakaa kwenye ile peninsula nao hawakuweza kushirikiana pamoja. Maendeleo yo yote katika njia za kuongoza mikutano yalikuwa sasa sharti yangoje kuwasili kwa wamisionari wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, katika wakati fulani uliokuwa ungali unakuja.

JAMAA YENYE UVUTANO MKUBWA YAKIMBIA “BABULONI”

Vitabu vyote vya Mnara wa Mlinzi vikiwa sasa vimepigwa marufuku isipokuwa The Golden Age, ile kazi ilikuwa haina budi kufanywa kwa tahadhari. Akina ndugu walikuwa hawana budi kuwa waangalifu, wenye akili katika kuja na kuondoka kwao. Ingawa hakukuwa na mikutano ya kawaida iliyopangwa kitengenezo, wale waliochukua ukweli walikuwa watu wenye ushujaa na wenye kupiga moyo konde.

Ile jamaa ya Ok ni kielelezo kimoja chenye kutokeza. Wote walikuwa Waadventisti wa Siku ya Sabato, walioelimishwa vizuri, na walio katika hali nzuri kiuchumi nao walikuwa na sifa yenye kutokeza katika ujamii. Baba ya Ok Ji-joon alikuwa mzee katika kanisa na mkuu wa shule ya Waadventisti, na mke wake Kim Bong-nyob alikuwa mkaguzi wa hesabu ya shule hiyo ya mahali hapo.

“Siku moja katika 1937, Ok Ji-joon anatuambia, “ilitukia kwamba mimi nilipata gazeti, The Golden Age, katika pipa la takataka. Kwa kuwa mimi nilikuwa mfuasi wa dini sana, mimi nilipendezwa na zile makala za kidini zilizokuwamo nami nikazisoma kikamili. Siku kadhaa baadaye wanaume wawili walinitembelea na kunitolea vitabu zaidi kutoka ule ‘Mnara Wenye Taa.’ [Huu ndio usemi uliotumiwa kwa “Mnara wa Mlinzi” uliotafsiriwa kimakosa na kutumiwa na mwangalizi wa tawi la Japani na hivyo pia ukatumiwa katika Korea.] Wao walinifanya nisome kile ambacho baadaye nilijifunza kilikuwa kadi ya ushuhuda. Kwa furaha mimi nilikubali vitabu vyote walivyokuwa navyo. Baadaye, nilipovisoma nilipata kuona mambo mengi ambayo yalipingana na imani yangu ya Kiadventisti. Mimi niliandika kwa kutumia anwani ya Tokyo iliyoonekana kwenye kurasa za nyuma za kile kitabu na kwa miezi kadhaa nikaendeleza mazungumzo hayo ya kimafundisho kwa barua. Lile tawi la Tokyo lingejibu maswali yangu, likitia ndani magazeti fulani ya Mnara wa Mlinzi yakiwa yamepigwa mistari chini kwa rangi nyekundu kwenye sehemu zenye maana.

“Lile Kanisa la Kiadventisti la Sariwon katika Mkoa wa Hwanghae, sasa katika Korea Kaskazini, lilinifanyia matata kwa sababu niliendelea kuuliza maswali juu ya ukweli huu mpya uliopatikana. Yule mhudumu alijaribu kuepa kujibu na kwa kutakabari akasema kwamba kumuuliza mhudumu maswali kama hayo, hasa mmoja ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa baba yangu, kulikuwa ni kukosa heshima. Lakini mimi nilifikiri mahusiano ya kibinafsi hayapasi kuingilia mazungumzo ya Biblia na kwamba yeye aliniwia jibu. Ndugu yangu mdogo pia aliutambua ukweli na akaja katika ukweli pamoja nami, kama alivyofanya ndugu yangu mkubwa. Mwishowe sisi tukaacha kuhudhuria kanisa.

“Baba yangu alitupinga sisi. Wakati ndugu yangu mkubwa nami tulipofunga kiwanda chetu chenye kusitawi cha vyombo vya ukulima ili tuwe na wakati kwa ajili ya kazi ya kuhubiri, yeye alighadhibika na akatufukuza tutoke nyumbani. Hata hivyo, sisi hatukuacha lakini tuliendelea kujaribu kumshawishi yeye kwa habari kutoka katika Mnara wa Mlinzi.”

Ok Ryei-joon, ndugu mkubwa wa Ok, anafuatia kutuambia jinsi macho ya baba yao yalivyofunguliwa kwenye ukweli.

“Siku moja mhudumu wetu Mwadventisti alitutembelea na kutuambia kwamba sehemu ya upelelezi ya Idara ya Polisi ilikuwa imeamuru kanisa letu lihudhurie patakatifu pa Shinto ya Kijapani ili kuabudu miungu ya Kijapani na kuinua bendera ya Kijapani kwenye kanisa, kusalimu bendera, na kuimba wimbo wa taifa kabla ya kila ibada. Oni la pasta mwenyewe lilikuwa kwamba Waadventisti wangekuwa hawana budi kujipatanisha au sivyo kanisa lingepigwa marufuku na Waadventisti wangetoweka. Yule mhudumu aliuliza jambo hilo kwenye makao makuu ya kanisa, na kisha yeye akatutembelea sisi ili atupe jibu. Makao makuu yao yalisema kwamba wanapaswa kutii amri ya polisi, ingawa lingekuwa jaribu kubwa. Baba yetu alitamaushwa sana katika uamuzi huo.”

Baba yao alitaka kujua oni la Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi juu ya jambo hili. Ili ajue, yeye alianza kujifunza Biblia pamoja na wanaye. Kama tokeo, yeye alitambua jinsi Mashahidi wa Yehova walivyokuwa sahihi. Ile jamaa nzima—baba, mama, wana wanne, na binti-wakwe wawili—wakaacha kwenda kanisani.

“Baadaye, katika 1938, Kanisa la Kiadventisti lilituma mmisionari Mwamerika kwenye kao letu, naye akatuambia sisi kwamba wamisionari wao walikuwa wameamua kuondoka Korea kwa sababu ya uonevu wa serikali ya Japani,” anaendelea Ok Ryei-joon. “Yeye pia alisema kwamba kujiondoa kwa jamaa yetu kutoka kanisa kwa sababu ya tatizo la kusalimu bendera na ibada ya patakatifu pa Shinto kulikuwa kwenye kusifika sana naye akatutia moyo sisi tuendeleze imani yenye nguvu katika Yehova Mungu, hata kama walivyofanya Mashahidi wote wa Yehova katika Korea.”

Wakati mwangalizi wa tawi kutoka Japani alipozuru, jamaa yote hii ilibatizwa katika Novemba 19, 1937. Leo, watatu wa ndugu hawa wanatumikia wakiwa wazee. Kwa sababu ya msimamo wake juu ya suala la kutokuwamo, ndugu yao mchanga zaidi, Ok Ung-nyun, alikufa akiwa mwaminifu katika gereza la Kijapani katika 1939.

ONYO LA WAKATI UFAAO

Katika Desemba 1938, wakati wa ziara ya mwisho ya Junzo Akashi katika Korea, yeye alikutana na ndugu 30 kwenye nyumba ya Moon Tae-soon katika Seoul na akaonya kwamba wangekamatwa upesi. Hilo lifanyikapo, yeye akawatahadharisha, msionyeshe utovu wa heshima kwa bendera ya taifa au kwa mfalme. Wala msiache msimamo wenu, yeye akasema pia. Yeye alihimiza wote kuhubiri kadiri iwezekanavyo kwa kutumia vile vijitabu vitatu vilivyopatikana, Protection, Warning, na Face the Facts.

Katika kile kijitabu kipya Face the Facts, Akashi alikazia sana jambo moja ambalo lingekuwa na uvutano mbaya kwa ndugu Wakorea. Kile kijitabu kiliwatia moyo wavulana waliochumbiana wangoje “miaka michache,” mpaka baada ya Har–Magedoni, kabla ya kufunga ndoa. Yeye alifafanua hilo kumaanisha miaka miwili tu au mitatu, badala ya kipindi cha wakati kisichokuwa dhahiri. Hivyo, wale ndugu Wakorea waliitikadi kwamba wao walikuwa na miezi michache tu iliyobaki ya kuhubiri, kisha wangekamatwa, na wakiwa gerezani, Har–Magedoni ingetokea.

Majuma machache baadaye nyusipepa zilianza kushambulia tengenezo na kumwita Ndugu Rutherford kuwa “msuluhishi mwenye kichaa.” Wakati mwana wa Junzo Akashi na ndugu mwingine Mjapani walipokataa mazoezi ya kijeshi katika Januari 1939, Akashi mwenyewe aliitwa kwenye makao makuu ya jeshi la Kijapani katika Tokyo aeleze sababu. Kukamatwa kwa akina ndugu kulifuata—katika Japani Juni 21, katika Taiwan Juni 22, na katika Korea Juni 29. Mashahidi wengi kwa kufululiza walitumia wakati katika magereza mpaka mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Pili katika 1945.

WASHIKA UKAMILIFU WA MAPEMA

Dada Chang Soon-ok, aliyekuwa Mkatoliki hapo kwanza ambaye alijifunza ukweli kwa kusoma The Golden Age, anatuambia yaliyotokea baada ya mkutano huo wa mwisho katika Seoul pamoja na Junzo Akashi. “Wale waliosikia hotuba yake walitoka nje kwenye eneo lao walilogawiwa wakiwa na vitabu vingi,” yeye anaanza. “Mimi nilienda Pusan nikahubiri. Kwenye mapambazuko ya Julai 29, 1939, polisi mmoja alinikamata. Tisa wa sisi akina dada tulifungiwa ndani ya seli moja pamoja na wahalifu wa kawaida. Ilikuwa yenye joto na chafu, nayo ilinuka vibaya. Sisi tulifungwa gerezani kwa mwaka mmoja hata kabla ya kuletwa kwenye jaribio.

Katika gereza wao walilazimisha wale wafungwa kumwabudu mfalme kila asubuhi. Kwa sababu sisi tulikataa, walitia pingu kwenye mkono mmoja nyuma ya mgongo wetu, ule mkono mwingine ukiwa umezungushwa kwenye bega letu. Nyakati nyingine walitia pingu maradufu juu yetu, na nyakati nyingine watu wawili walifungwa pamoja kwa mnyororo, mgongo kwa mgongo. Katika wakati huo ilikuwa sharti wabadili pingu zetu kwenye upande wa mbele kila wakati tulipokula mlo. Mwishowe, baada ya miezi saba, walishindwa nao wakaondolea mbali zile pingu.

“Baada ya vifungo vyetu vya kawaida kumalizika, wanne wa sisi akina dada tuliwekwa katika kambi ya kifungo ya kutoa himaya katika Ch’ungju kuwa wasioweza kutengenezwa tabia. Mlinzi mmoja aliambia akina dada kwamba kila mmoja katika kambi ile alitazamiwa kuuawa katika muda wa siku chache. Halafu kwa ghafula ile vita ikaisha, nasi mwishowe tukaachiliwa katika Agosti 16, 1945. Mpaka leo hii mimi hujawa na hisi za moyoni ninapofikiria miaka yote hiyo katika gereza.”

Ile jamaa ya Ok ilikuwa pia miongoni mwa wale waliokamatwa. Lee Jung-sang, mke wa yule ndugu mkubwa zaidi, Ok Ryei-joon, anasimulia yaliyowapata.

“Nilipokuwa ningali kitoto cha kiroho, nikiwa nimebatizwa kwa muda ulio punde kuliko miaka miwili, polisi kutoka Seoul walichukua mume wangu na nduguye mdogo, Ok Ji-joon, huko gerezani,” yeye anakumbuka. “Kwenye wakati huo walio wengi wa akina ndugu na dada Wakorea walikamatwa na hatimaye wakawekwa katika gereza la Sodaemun katika Seoul. Polisi kwa mara nyingine tena walitwaa vichapo vyote vya Sosaiti—au ndivyo wao walivyofikiri!

“Sisi tulipokuwa tungali huru, dada-mkwe wangu, Kim Bong-nyo, na dada mwingine Kim Kyung-hui nami, tulienda kwenye ghala ya Sosaiti na kuchukua vitabu vyote ambavyo tungeweza kubeba, kwa kuwa ilikuwa akilini mwetu kuangusha vingi vyavyo kadiri iwezekanavyo kabla sisi wenyewe hatujakamatwa. Sisi tulienda Pyongyang, upande wa kaskazini, na tulipokuwa tukifanya kazi huko, sisi pia tulikamatwa katika Novemba 1939 kwa sababu ya kuvuruga amani na kueneza vitabu vilivyokuwa vimepigwa marufuku. Sisi tulifungwa katika stesheni ya polisi ya Tongdaemun na baadaye tukahamishwa kwenda kwenye gereza la Sodaemun walikokuwa wale akina dada wengine. Wote pamoja, akina ndugu na dada 38 walikuwa gerezani wakati huo.”

MWAMINIFU MPAKA KIFO

Dada Park Ock-hi, ambaye wakati huu ni painia wa pekee akiwa na umri wa miaka 86 na mwingine wa hao waaminifu waliokuwa wametiwa gerezani, anakumbuka hizo siku zenye magumu.

“Baada ya kutumia majira yote ya baridi katika Mkoa wa Kyŏngsang katika Kusini mwa Korea tukihubiri habari njema, sisi tulikuja nyumbani Seoul katika Februari 1939,” anasema. “Na mume wangu, Choi Sungu-kyu, alikamatwa mara hiyo na polisi kutoka stesheni ya polisi ya Tongdaemun katika Seoul. Polisi walimshitakia kukataa kuabudu penye patakatifu pa Shinto. Wakati wa siku zake 20 kifungoni, yeye alishikwa na homa ya matumboni, nao wakamhamisha kumpeleka hospitalini. Baada ya siku 40 katika hospitali, yeye aliachiliwa, na mara tu akajikuta miongoni mwa akina ndugu waliokamatwa katika Juni 1939.

“Ndugu-mkwe wa mume wangu alikuwa na cheo chini ya ile serikali ya Japani, naye alituma mwanasheria atekeleze uachiliwa wake kutoka gerezani. Yule mwanasheria alimwambia mume wangu kwamba njia pekee ambayo yeye angeweza kupanga aachiliwe ilikuwa ya kwamba yeye aabudu penye patakatifu pa Shinto. Mume wangu alikataa toleo lake pale pale na akamwambia asije kamwe kumwona tena. Kisha mume wangu akaniandikia akiniuliza, ‘Ni nani aliyetuma yule mwanasheria? Kaa macho! Soma Warumi 8:35-39.’ Barua hii ilitutia moyo sana sisi sote tuliokuwa nje, na wale wapya walikuwa wameazimia kuendelea kumsifu Yehova.

“Baadaye, katika Septemba 1941, mimi nilikamatwa tena lakini nikafungwa kwa siku 15 tu. Mimi niliambiwa kwamba kwa kuwa mume wangu alikuwa akiachiliwa kutoka gerezani, inanipasa kuleta won 500 (dola 250 za Kiamerika). Nilikopa zile fedha nikaenda gerezani. Ulikuwa usiku mweusi ti, wenye baridi. Nilimkuta mume wangu akiwa amelala chini, amefunikwa shuka nyeupe, akiwa mahututi kabisa. Wao walikuwa wamemfunga gerezani kwa miaka miwili na nusu na sasa walidai won 500 ili wamwachilie akiwa katika hali hii! Mume wangu, akiwa na umri wa miaka 42, alikufa muda wa saa nane baadaye.

“Mimi nilikamatwa kwa mara ya nne katika Septemba 1942 na wakati huu nilipelekwa katika gereza la Sodaemun katika Seoul pamoja na wale akina dada wengine waliotiwa gerezani. Huko tulikuwa hatuna budi kuvumilia mateso yasiyoelezeka.”

Yule mlinzi wa kike alikuwa akikasirikia akina dada hawa kwa kukataa kumwabudu mfalme wa Japani. Hilo lilitokeza kazi ya ziada kwake. Kwa kila mlo yeye alikuwa sharti abadili pingu na minyororo yao. Lakini kwa wazi yeye aliona uaminifu wa dada hawa wapendwa. Kwa kushangaza, zaidi ya miaka 20 baadaye yeye alianza kujifunza Biblia, akaunganishwa tena na akina dada hawa kwenye mkusanyiko wa wilaya, na akabatizwa katika 1970.

Akina ndugu walihojiwa mara nyingi kwa kuwa wenye mamlaka walitafuta njia za kuwashtaki. Wao waliulizwa: “Je! ni kweli kwamba mataifa yote yako chini ya uvutano wa Ibilisi? Je! Milki kuu yetu ya Japani inatiwa ndani? Je! wewe ni jasusi wa Amerika? Har–Magedoni itakuja wakati gani?” Akina ndugu walijibu lile swali la mwisho wakisema: “Baada ya kazi ya kuhubiri kufanywa.” Kisha wenye mamlaka wangeshtaki: “Kwa kuhubiri kwenu kwa kweli ninyi mnahimiza kuja kwa Har–Magedoni, maana yake ninyi mnahimiza kuangamizwa kwa milki yetu ya Japani. Kwa hiyo ninyi mnahalifu sheria ya utengamano wa raia.” Ndipo wengi wa wale akina ndugu walipokamatwa na kutupwa ndani ya gereza kwa miaka miwili kufika minne.

Watano wa wale 38 waliotiwa gerezani walikufa wakiwa waaminifu walipokuwa gerezani, kutia Moon Tae-soon, aliyekuwa amekuwa akiangalia kazi chini ya mwangalizi wa tawi la Japani.

BAADA YA VITA YA ULIMWENGU YA PILI, MZINDUKO

Junzo Akashi ndiye aliyekuwa mwenye daraka la kazi katika nchi ya Korea tokea wakati ilipowekwa chini ya tawi la Japani katika 1926. Baada ya kuachiliwa kwao katika 1945, akina ndugu walimtegemea kwa kupata mwelekezo. Hata hivyo, Akashi, ambaye alikuwa amekuwa akiishi maisha ya ukosefu wa adili na alikuwa ameacha msimamo wake juu ya ukweli chini ya mkazo, alikuwa ameacha tengenezo la Mungu.

Ingawa hivyo, wale akina ndugu Wakorea walisumbuka, kwa sababu wao walikuwa wameitikadi elezo lake lisilo sahihi juu ya ile “miaka michache” iliyobaki kabla ya Har–Magedoni. Hilo kundi dogo la akina ndugu likagawanyika. Wengine, waliokuwa wenye nguvu katika imani, waliitikadi iliwapasa waendelee kuhubiri; wengine walipoteza bidii yao.

Kwa miaka kadhaa baada ya 1939, hakukuwa na uwasiliano na tengenezo la Yehova. Wale akina ndugu walihisi wameachwa. Wengi wao waliitikadi kwamba yale yaliyokuwa yakiwapata katika Korea yalikuwa yakitukia kwa tengenezo lote zima kuzunguka ulimwengu. Wao hawakuwa na habari kwamba Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi ilikuwa ingali inatenda, achia mbali kwamba ndugu zao katika nchi nyinginezo walikuwa wameshikilia sana ukamilifu wao wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili au kwamba maongezeko yalikuwa yameanza kutukia. Bila ye yote wa kuchukua uongozi na bila uwasiliano pamoja na tengenezo, ibada ya kweli katika Korea ilipunguza mwendo ikawa karibu kukoma kabisa.

“MASHAHIDI WA YEHOVA WAMEKUWA HAI TENA”

Mlango wa kuingia kwenye ibada ya kweli ulifunguliwaje tena? Dada Park Ock-hi anaeleza:

“Baada ya kukombolewa kutoka chini ya Wajapani katika 1945, ijapokuwa akina dada kadhaa walisisitiza ulikuwa wakati wa kungojea Har–Magedoni katika ‘mahali pa siri,’ sisi tuliendelea kufanya mikutano fulani katika nyumba yangu. Hii haikuwa mikutano iliyopangwa kitengenezo; badala yake, yule ndugu mwenye kuongoza alikuwa akituhubiria kutoka kwa vichapo vya zamani vilivyopatikana. Hii ndiyo iliyokuwa kadiri ya utendaji wetu kwa miaka michache iliyofuata. Mmoja wa wale waliokuwa wakihudhuria alikuwa mpwa wangu wa kiume, Park Chong-il, mvulana mchanga wa miaka 15 ambaye baadaye angekuja kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi katika Korea.

“Ndipo, kwa mshangao wetu, siku moja katika Agosti 1948, Ndugu Choi Young-won akatuonyesha makala moja katika nyusipepa ya Jeshi la Kiamerika Stars and Stripes. Lilitaarifu kwamba Mashahidi wa Yehova walikuwa watendaji wenye bidii katika United States na kwingineko. Sisi tulifurahi sana. Sisi sote tulimtia moyo ndugu Choi aiandikie Sosaiti katika United States. Alifanya hivyo, nayo Sosaiti ikajibu mara hiyo, ikitutumia furushi la vitabu. Kwa furaha sisi tulijaza mikoba yetu ya vitabu kwa vijitabu hivi, tukaenda moja kwa moja kwenye kazi ya nyumba kwa nyumba katika Seoul. Sisi tukawa na wakati mzuri ajabu! Mwanamke mmoja hata alitamka, ‘Mashahidi wa Yehova wamekuwa hai tena.’”

Watu mmoja mmoja kumi na wawili walifanyiza lile kundi la kwanza la Mashahidi wa Yehova katika Juni 24, 1949.

“KARIBU, MJUMBE WA TUMAINI WA MNARA WA MLINZI”

Haikuwa mpaka yule wa kwanza wa mstari mrefu wa wamisionari waaminifu alipowasili, mwishowe wakifikia hesabu ya jumla ya 52, kwamba kukawa kweli kweli na kiunganishi chenye nguvu na makao makuu ya Sosaiti.

Baada ya kundi la Seoul kuandikishwa na Sosaiti, mipango ilifanywa kutuma nchini wamisionari waliozoezwa kutoka Shule ya Biblia ya Gileadi ya Mnara wa Mlinzi. Ijapokuwa mwanzoni walikuwa wamepewa mgawo wa kwenda Japani, wahitimu wanane wa lile darasa la 11 la Gileadi walibadilishiwa migawo kwenda Korea. Don na Earlene Steelec walichaguliwa kwenda kwanza. Baada ya kazi nyingi sana ya karatasi, viza zikatolewa na Jamhuri ya Korea na katika Agosti 9, 1949, wao wakawasili katika Korea.

Kwa sababu ya hatua za kulinda usalama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimpo, ni ndugu wawili tu waliongojea kuwasalimu akina Steele. Juu ya ua uliokuwa karibu na barabara ya kurukia ndege, wao waliangika ishara moja iliyosomwa, “Karibu, Mjumbe wa Tumaini wa Mnara wa Mlinzi.” Hakuna ye yote wa ndugu hawa aliyejua Kiingereza cho chote, lakini tabasamu zao changamfu na salamu za kupeana mkono za kirafiki ndiyo yote waliyohitaji akina Steele.

Baada ya akina Steele kuwekwa katika hoteli ndogo, akina ndugu wapatao kumi walikusanyika pamoja na mtumishi wa kundi, Choi Young-won, aliyesema Kiingereza. Hili ndilo lililokuwa kutano la kwanza katika miaka kumi na ye yote anayewakilisha tengenezo. Sasa akina ndugu wangeweza kupata majibu kwa maswali yao yenye kuchoma-choma juu ya kazi iliyobaki. Kwa hiyo mkutano mmoja ulipangiwa jioni iliyofuata. Katika barua yake ya kwanza kwa Sosaiti, yenye tarehe ya Agosti 12, 1949, Ndugu Steele aliripoti:

“Kwa mshangao wetu, akina ndugu 40 na watu wenye nia njema walihudhuria. Tuliwapelekea salamu za akina ndugu katika United States, tukaongea juu ya tengenezo la Mungu katika wakati huu kisha tukajibu mengi ya maswali yao. Akina ndugu katika njia nyingi wana ufahamu wenye kina na bila shaka wanatamani kufanya linalotakwa kufanywa. Ni wawili au watatu tu walio na mawazo yenye kosa, wakiwa na uchungu kwa sababu ile ‘miaka michache’ mpaka Har–Magedoni iliyotajwa katika kile kijitabu Face the Facts imerefuka kufikia sasa.”

Idadi ya watu wa Seoul wakati huo ikiwa 1,500,000, kubwa mara mbili zaidi ya kabla ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, kupata nyumba kwa ajili ya wamisionari kulikuwa kama ile Mithali ya kutafuta sindano katika chungu kubwa la nyasi. Lakini kufikia mwisho wa Agosti jengo zuri lilipatikana karibu na kitovu cha mji. Lilikuwa jengo la matufali lililojengwa vizuri, la mtindo wa Kimagharibi ambalo hapo kwanza lilikuwa limekaliwa na serikali ya Japani lakini sasa lilikuwa limeaminishwa kwa serikali ya Korea. Ile nyumba ilikuwa na vyumba vya kulala vinne, sebule kubwa, chumba cha kulia, na jikoni. Sasa Sosaiti ingeweza kutuma wale wamisionari wengine sita. Mali hii si kwamba tu ilitumikia kama kao la wamisionari na mahali pa kukutania kundi la Korea bali katika wakati ujao lingetumika pia kuwa afisi ya tawi.

HUDUMA ILIYOPANGWA KITENGENEZO YAANZA

Kukiwa na ile akiba ndogo ya vitabu iliyopatikana na kukiwa na vifurushi vichache tu vilivyokuwa vikija kwa posta, kwa miezi michache iliyofuata wale wamisionari 2 na akina ndugu wenyeji 28 walikuwa wakiwaazima watu wenye kupendezwa vile vijitabu waliopatikana katika kazi ya nyumba kwa nyumba na kisha warudi kuchukua vijitabu hivyo ili wavitumie tena pamoja na wengine.

Katika Januari 1, 1950, wahubiri wanne waliotamani kuchukua utumishi wa wakati wote waliwekwa rasmi kuwa mapainia. Kufikia Februari robo moja ya kundi walikuwa mapainia, saba kwa jumla, na wahubiri waliobaki walikuwa na wastani wa saa 33 kila mwezi. Ile kazi ya kufanya ziara za kurudia na kazi ya funzo la Biblia la nyumbani, jambo ambalo hawakujua hapo mbele, liliwafurahisha sana.

Ule mwezi wa kwanza kamili wa utendaji wa wamisionari ulimalizika wakiwa na hesabu ya mafunzo ya Biblia 16. Wale wanafunzi walikuwa wakija kwenye kao la wamisionari badala ya kujifunzia katika makao yao wenyewe yaliyo dhalili. Tatizo halikuwa kupata mafunzo bali, ni kupata watu waliopendezwa kikweli na ujumbe wa Ufalme wala si kujifunza tu Kiingereza au kushirikiana na wageni wa kutoka ng’ambo.

Kwa kuwa wamisionari walikuwa na hamu nyingi ya kuwa na vitabu katika lugha ya Korea kwa matumizi katika shamba, Sosaiti ilitoa agizo kwamba kile kitabu “Let God Be True” kitafsiriwe na kutangazwa upesi iwezekanavyo. Ndugu Choi ndiye pekee aliyekuwa na uwezo wa kutafsiri. Hata hivyo, kazi yake ya kimwili ilimshughulisha sana hivi kwamba ilikuwa vigumu hata kuendeleza tafsiri ya Mnara wa Mlinzi kwa funzo la kila juma. Ili kurahisisha mzigo wake, watu wawili waliokuwa wakijifunza na wamisionari, mmoja profesa wa Kiingereza na yule mwingine mkuu wa benki, waliombwa wasaidie kazi hii. Kwa kushangaza, kwa kufikiria maarifa yao machache ya ukweli na ya tengenezo, ile tafsiri ilitokea vizuri sana.

MIKUTANO ILIYOPANGWA KITENGENEZO YACHOCHEA NDUGU

Ilikuwa ni baada tu ya wamisionari kuwasili kwamba funzo la Mnara wa Mlinzi lililopangwa kitengenezo likaanza. Baada ya Ndugu Choi kutafsiri somo, ndipo Ndugu Park Chong-il angenakili kwa mkono somo lote kupitia karatasi tisa nyepesi na kaboni. Kukiwa na 47 waliohudhuria kwenye funzo hilo la kwanza la Mnara wa Mlinzi katika Agosti 14, 1949, ilikuwa sharti wengi wakusanyike pamoja kuzunguka kila nakala ya karatasi nyepesi ili kushiriki katika mkutano. Kisha ukafuata Mkutano wa Utumishi wa kwanza uliopata kufanywa katika Korea.

Ndugu Shin Wan, ambaye sasa alianza kushirikiana tena na kundi, aliendesha duka dogo la mashine ya kurudufisha ambalo lilitumiwa vizuri kwa ajili ya Ufalme. Baada ya tafsiri ya somo la Mnara wa Mlinzi kufanywa, ile nakala ilitiwa kwenye stensili ya nta nazo nakala za habari hiyo zikatolewa kwa njia ya kuzungusha wenzo kwa mkono, ikiandaa nakala moja moja kwa wote waliohudhuria kwenye mikutano. Hapana tena nakala zilizofanywa kwa mkono!

WAMISIONARI WENGINE WAWASILI

Wote katika kundi walingojea kwa hamu nyingi kuwasili kwa wamisionari waliobaki. Katika Machi 12, 1950, Winfield (Scott) na Alice Counts, Grace na Gladys Gregory, Norrine Miller (sasa ni Thompson), na Florence Manso (sasa ni Janczyn) walikaribishwa kwenye mgawo wao mpya kwa karamu ya Kikorea na ukaribishaji-wageni mchangamfu wa kidesturi.

Wale wamisionari wapya hawakuwa wametangulia kuzoezwa katika lugha kabla ya kuwasili katika Korea, lakini kufikia Mei 1950 wale wamisionari wanne walikuwa na wastani wa mafunzo ya Biblia 20 kila mmoja. Kwa ajili ya hotuba zao kwa kundi, wakalimani walitumiwa, lakini wale wakalimani, kwa kukosa ustadi katika Kiingereza, nyakati nyingine walikosa usahihi. Mathalani, wakati misionari mmoja alipokuwa akiwatia ndugu moyo katika utumishi, mkalimani alitumia usemi “utumishi wa kivita.”

Baada ya Shule ya Huduma ya Kitheokrasi kupangwa kitengenezo, mikutano ya watu wote ilianzishwa pia katika masika ya 1950. Wengi sana walikuwa wakihudhuria, kufikia 162 sasa, hivi kwamba mipango ilifanywa mfululizo wa hotuba za watu wote zitolewe katika Jumba la Shule ya Msingi ya Chae Dong. Kwa kushangaza, ile hotuba ya kwanza, “Yatakayoipata Dunia Yetu,” ilitolewa kwa amani katika Juni 25, 1950—ile siku yenye msiba ilipoanza Vita ya Korea.

Ndugu Steele aliripoti hivi baadaye: “Nilipokuwa nikimaliza mhadhara wangu katika jumba moja la shule katika Seoul, Juni 25, polisi walitujulisha kwamba Korea Kusini ilikuwa imeshambuliwa, na kafyu ilikuwa imetangazwa. Wakati huo, kupendezwa katika Theokrasi kulikuwa kumeongezeka sana hivi kwamba kulikuwako watu 336 waliohudhuria mhadhara huu wa mwisho! Usiku uliofuata njia za ulinzi za Korea Kusini zilibomoka na Seoul ukaja chini ya mazingiwa.”

VITA YA KOREA

Kufikia Julai 1949 majeshi yote ya United States na Urusi pia yenye kutwaa nchi yalikuwa yameondelewa, na kila nchi ikaacha wanaume kadhaa katika vyeo vya kushauri. Ile peninsula ilikuwa karibu kutaabishwa na mojapo vita vyenye kuharibu zaidi vya ki-siku-hizi. Katika Juni 1950 wakati pigano lilipoanza, jeshi la Korea Kusini lilikuwa na wanaume wachache kuliko elfu mia moja, wakiwa na silaha ndogo-ndogo tu. Yale majeshi ya Korea Kaskazini, hata hivyo, yalikuwa na idadi yapata 135,000, kutia na kikosi kimoja cha vifaru vyenye mizinga. Kwa sababu hiyo, Kaskazini ilikuwa katika hali nzuri ya kuzoezwa na kutayarishwa kwa vifaa, hali Kusini haikuwa imetayarishwa kukinga uvamizi.

Katika Juni 28 ule mji mkuu wa Seoul ukaanguka kwa majeshi ya Korea Kaskazini ambayo yalishinda nguvu jeshi la Korea Kusini. Ile vita ilikuwa ikipembea-pembea kwenye latitudo ya 38 mpaka mapatano ya kuacha vita yalipotiwa sahihi katika Julai 27, 1953.

WAMISIONARI WAHAMISHWA

Siku ya pili baada ya vita kuanza, Redio Korea ya Amerika ilitangaza kwamba Waamerika wote waliamriwa kuhama ile nchi. Wale wamisionari sasa walikabili uamuzi mgumu wa kuchagua kati ya mambo mawili. Je! iliwapasa wakae na kufanya kazi pamoja na wale akina ndugu waaminifu Wakorea au waondoke? Wale wamisionari wanane walikutana, wakaomba mwelekezo wa Yehova, na kuzungumza ile hali yenye wasiwasi. Kubaki kungemaanisha kukamatwa na kutiwa gerezani pasipo shaka. Wote wakakubali—inawapasa waondoke. Matukio yaliyofuata yalionyesha kwamba walifanya uamuzi uliofaa.

Ripoti moja kutoka kwa wale wamisionari baadaye ilitaarifu: ‘Sisi tulikuwa na dakika 30 tu ili kuwahi ule msafara wa mwisho wa ulinzi uliokuwa ukiondoka mjini. Mali za kibinafsi na za kijamaa zilipelekwa kwa mtumishi wa kundi wa huko. Wakati ule ule mji ulikuwa chini ya shambulio la mizinga, na katika ule mwendo wa kasi sana wa kwenda kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimpo mabasi yetu yalishambuliwa kwa makombora yenye kuangushwa na eropleni. Tulisafirishwa kwa ndege mpaka Japani, sisi sote wanane kwa sasa tunafanya kazi katika Kobe.’

Yule mtumishi wa kundi katika Seoul, Ndugu Lee Shi-chong, aliandika pia kwamba wale wageni wachache wa kutoka ng’ambo waliobaki nyuma walikuwa wamepelekwa wote kwenye “msafara wa kifo.”

Hivyo, upesi mno, wale wamisionari wanane wakamaliza kwa ghafula mgawo wao katika Korea, akina Steele wakiwa wamekuwa huko kwa muda uliozidi kidogo tu miezi kumi na wale wengine sita wakiwa wamekuwa kule kwa muda uliozidi kidogo tu miezi mitatu. Lakini wakati wa muda huo mfupi, walikuwa wamekuja kuwapenda sana ndugu zao Wakorea wenye bidii. Kwa mara nyingine tena tengenezo la Korea lingekuwa bila uwasiliano wo wote wa moja kwa moja na Sosaiti. Kuendeleza ile huduma na kudumisha kutokuwamo kwa Kikristo katika hali hizi mpya sasa kukakabili kila Shahidi Mkorea mmoja mmoja.

WAAMINIFU YAJAPOKUWA MAGUMU

Asilimia 43 ya vifaa vya viwanda vya Korea vikiwa vimebomolewa, na asilimia 33 ya makao yayo yakiwa yameharibiwa, sehemu kubwa ya idadi ya watu, kutia na akina ndugu, sasa waliishi kama wakimbizi. Makao yaliharibiwa, mali ya kibinafsi ikatoweka. Kuwa chonjo daima kulimaanisha uhai. Akina ndugu kadha walikuwa, wakinaswa na makombora yenye kuangushwa na ndege za lo lote la majeshi yale. Wachache, kutia na wale waliopata kimbilio katika mali ya Sosaiti, walipigwa risasi na kuuawa kikatili na askari. Hata hivyo, wale waliookoka hawakuacha kamwe utume wao wa kuhubiri Ufalme kuwa tumaini la ulimwengu. Wao hawakuacha kamwe kupanda mbegu za ukweli.

Katika zile siku chache za kwanza za vita, sehemu kubwa ya idadi ya watu wa Seoul walinaswa ndani ya mji. Akina ndugu walijua wangeshurutishwa kuingia katika Jeshi la Kujitolea la Watu ikiwa wao hawakutorokea kusini. Ndugu Park Chong-il na Ok Ung-suk walijificha katika mji mpaka Julai 5 na kisha wakaponyoka wakavuka Mto Han katika jitihada ya kufikia eneo “salama” kusini mwa Seoul. Walipita korija kadhaa za maiti, vifaru vilivyolemazwa, na majengo yaliyoharibiwa kwenye njia yao ya kutorokea, lakini kadiri walivyokaribia maeneo ya vita, ndivyo ilivyokuwa vigumu zaidi kujificha wasionwe na askari wa Korea Kaskazini.

Likiwa tokeo la Jenerali MacArthur Inchon wa U.S. kutua nchini katika Septemba 15, 1950, mji wa Seoul uliwekwa huru na utawala wa Korea kaskazini, mpaka penduli la vita lingepembea kwa mara nyingine tena kuelekea njia nyingine. Ndugu Park alirudi Seoul katika Oktoba 1, 1950, na akaamua kwenda nyumba kwa nyumba, akipendezwa katika kuona itikio la watu lingekuwaje. Yeye aliwapata wakiwa wenye wasiwasi na woga.

Ijapokuwa alikuwa hajabatizwa bado, Roh Pyung-il alikabili pia matatizo kabla tu ya vita. Yeye alikuwa mwana-mkwe wa dada Kim Chu-ok, aliyekuwa amethibitisha uaminifu wake katika gereza wakati wa nchi kutwaliwa na Wajapani. Wakati wa Seoul kutwaliwa mara ya kwanza na Korea Kaskazini, yeye alitorokea milimani ili aepuke kushurutishwa kuingia katika jeshi lao. Hata hivyo, wale askari waliona moshi uliotoka kwenye moto wake wa kupikia, na hivyo akakamatwa. Akipelekwa kwenye ukingo wa mji, yeye aliwekwa pamoja na hesabu fulani ya wanaume vijana wengine waliokuwa wamekusanywa. Waliulizwa maswali, mmoja mmoja. Wale vijana ambao hawakuweza kutosheleza wahoji wao walichukuliwa kando na kupigwa risasi. Roh alifikiri angeuawa hata aseme nini na kwa hiyo akaazimia kutoa ushuhuda kabla jambo hilo halijatukia.

Yeye aliulizwa ni kwa sababu gani alikuwa akiepuka Jeshi la Kujitolea la Watu. “Mimi ninaweza kutumikia Ufalme wa Mungu tu,” yeye akajibu. “Kwenye Har–Magedoni pande zote mbili katika shindano hili la kisiasa zitaharibiwa na Mungu, na mimi sitaki kuwa upande wo wote. Mimi siwezi kuhalifu sheria ya Mungu kwa ajili ya sheria yo yote iliyofanywa na mwanadamu kinyume cha ile yake. Mimi siogopi kufa kwa sababu mimi naitikadi katika ufufuo.”

Wahoji wake walisema kwamba yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kusema ukweli, lakini apaswa kusimama kando hata hivyo. Wale askari waliinua bunduki zao, wakalenga, na kufyatua, wakimkosa makusudi. Roh alizimia, na kuamka muda mfupi baadaye, akishangaa kwa kuwa hai. Maneno yake ya kwanza yalikuwa: “Ukweli kwa hakika ni wenye nguvu nyingi!”

WAKIMBIZI TENA

Baada ya miezi miwili na nusu chini ya utawala wa Korea Kusini, katika Desemba 24, 1950, serikali ya Korea Kusini iliamuru wakazi wote wa Seoul, isipokuwa wale waliokuwa na umri wa kuandikishwa jeshi, wahame mjini kwa mara nyingine tena.

Siku 11 tu baadaye, Januari 4, 1951, askari wa Korea Kaskazini na wa China waliutwaa mji tena. Kabla ya hapo, ingawaje, akina ndugu walinyakua mali yo yote ambayo wangeweza kubeba wakienda kwa miguu au katika mikokoteni, wakaanza maisha wakiwa wakimbizi tena. Pia walichukua vibweta kadha vya kile kijitabu Furaha ya Watu Wote ambavyo walikuta vimeachwa katika kao la wamisionari. Hivyo vilitumiwa kupanda mbegu za ukweli wakati wa kipindi hiki cha ukimbizi wa pili.

Bila shaka, wale akina ndugu wachanga, hawangeweza kutoroka mjini. Ijapokuwa msimamo wao wa Kikristo wa kutokuwamo ulitokeza matatizo, mara nyingi ulithibitika kuwa wenye kuokoa uhai, kama Ndugu Park Chong-il alivyopata kujua upesi. Baada ya jeshi la Korea Kaskazini kuingia mjini tena, yeye na Cho Young-ha, mwalimu wa shule ya sekondari na Mmethodisti aliyependezwa katika ukweli, waliishi kwa amani katika nyumba ya dada mmoja kwa miezi mitatu na nusu.

Ndugu Park na mwenzake walikuwa wamekaa katika ficho lao kwa muda wa siku chache tu wakati polisi wa siri wa Korea Kaskazini alipokuja akibisha mlango wao. Yule polisi alishuku kwamba walikuwa ama majasusi ama askari wa jeshi la Korea Kusini. Polisi-mpelelezi mmoja alichunguza mikono yao kuona kama walikuwa wamekuwa wakishika bunduki.

“Sisi ni Wakristo wasioweza kushiriki katika vita na kwa hiyo hatukuweza kuuhama mji, kwa kuwa tungalikamatwa na ule upande mwingine,” wakamwambia yule mpelelezi. Polisi akaamuru wasiondoke nyumbani na akatisha kurudi siku ifuatayo. Mara polisi alipoondoka, Ndugu Park na Cho Young-ha waliharibu kwa haraka majina yote, anwani, na picha za Mashahidi walizokuwa nazo na kisha wakaazimia kumtolea ushuhuda polisi siku iliyofuata ingawa walijua kwamba huenda wakatiwa gerezani.

Kesho yake asubuhi yule polisi alikuja tena akiwa na mpelelezi tofauti. Ndugu Park alitoa ushuhuda kwa muda upatao saa moja na nusu, kana kwamba alikuwa akitoa hotuba ya watu wote. Wale wanaume walisikiliza bila kukatiza na wakaonekana kupendezwa na ujumbe wake. Ndipo, baada ya maswali machache, wakaondoka ghafula. Siku mbili baadaye mmoja wao akarudi akiwa bado na mpelelezi tofauti, na Ndugu Park na rafiki yake wakawa na nafasi nyingine ya kutoa ushuhuda. Hakuna polisi aliyerudi tena kamwe. Ingawa hivyo, wao walikuwa waangalifu, wasiondoke nyumbani. Imani ya Cho ilitiwa nguvu sana, naye akaja katika ukweli moja kwa moja.

Sasa vita ikapembea kuelekea upande mwingine, na kufikia Machi 31, 1951, majeshi ya UM yakawa yamefika tena kaskazini kwenye latitudo ya 38. Kwa mara nyingine tena Seoul ukawa chini ya amri ya UM. Park Chong-il alikuwa huru sasa kuondoka nyumbani. Yeye alianza kuvuka mji ili kukagua kao la wamisionari lakini akasimamishwa na majeshi ya UM. Wale askari wa Korea Kusini, waliokuwa pamoja na majeshi ya UM, walimshuku. Na si ajabu! Baada ya kukaa ndani ya nyumba kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu, uso wake ulikuwa kijivu-jivu na nywele zake zilikuwa ndefu. Kwa kuwa alijua Kiingereza kiasi fulani, Ndugu Park aliwaambia wale askari Waamerika kwamba yeye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova na alikuwa akishirikiana na wamisionari Waamerika wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, naye alikuwa akienda kukagua mali ya wamisionari. Wale askari walimwitikadi na kumwacha aende.

KAZI YASONGA MBELE ZIJAPOKUWA HALI ZA UKIMBIZI

Akina ndugu, sasa wakiwa wakimbizi, walilowea sana sana katika majiji makubwa matano—Taejon, Taegu, Pusan, Chonju, na Kunsan. Idadi za watu katika majiji haya ziliongezeka zikauzidi kwa mara kadhaa ukubwa wazo wa kawaida kwa kadiri watu walivyotegemea sana kinga yo yote ambayo wangeweza kupata—vibanda, pande za vilima, mapango.

Dada Kim Chi-duk, sasa akiwa na umri wa miaka 87 na akiwa angali painia, alikuwa miongoni mwa Mashahidi wa kwanza kuwasili katika Taegu. Wawili wa wanaye walikuwa wameuawa wakati wa vita. Sasa, akiwa na wale watoto wengine wawili, yeye akaanza mara hiyo kutoa ushuhuda. Katika wakati mfupi yeye akaangusha vitabu vyote alivyokuwa amekuja navyo na kisha akatumia juma la pili kufanya ziara za kurudia.

Mkimbizi mwingine katika Taegu, Ndugu Lee In-won, pamoja na dada Kim, walifanya mikutano pamoja na dazeni dazeni za wengine wengi. Sura zilizorudufiwa za vitabu “Let God Be True” na “This Means Everlasting Life” zilitumiwa kwa mikutano yao na katika utumishi wa shambani. Kundi la kwanza lililopangwa kitengenezo chini ya hali za ukimbizi lilikuwa katika jiji hili la Taegu.

Ndugu Ok Ryei-joon na mke wake, Lee Jung-sang, wakimbizi kutoka Korea Kaskazini, walikalishwa tena katika Chonju. Dada Lee anatuambia yaliyotukia kufuatia hapo:

“Mimi nilianza funzo la Biblia na wanawake wanne mashemasi kutoka Kanisa la Kati la Kipresbiteri. Wao hawakutaka kutumia vichapo vya Sosaiti, ila Biblia tu. Viongozi wa kanisa wa huko waliona sisi kuwa wakimbizi wenye kudharauliwa na walijaribu kutuzuia kuhubiri, hata wakatuma watu wenye ghasia kunifuata mimi. Wanawake wanne hao walinisaidia niwatoroke watu hao wenye ghasia. Ijapokuwa viongozi wa kanisa walifanya jitihada hizo dhidi yangu, wanawake hao waliendelea na funzo lao la Biblia. Kama tokeo, hatimaye watu 20 walitoka katika kanisa hilo wakaingia katika ukweli.”

MSAADA WA MISIONARI WARUDI

Chini ya hali za wakati wa vita zilizokuwa zikiendelea, kuingia ndani ya Korea kulikuwa jambo lisilowezekana. Hata hivyo, baada ya kutimiza mambo mengi sana yaliyotakwa na serikali, Don Steele aliweza kurudi, peke yake, na aliwasili kwenye bandari ya Pusan katika Novemba 11, 1951. Makao Makuu ya McArthur wakati ule yalikubalia kila misheni kupata mtu mmoja tu, na hakuna wanawake walioruhusiwa kuingia. Ungekuwa mwaka mwingine kabla ya Earlene, mke wa Don, kujiunga naye.

Katika Novemba 17, 1951, Ndugu Steele alipewa ruhusa na Jeshi la United States azuru Seoul. Yeye anatuambia yale ambayo yeye na wengine walipata kuona:

“Alasiri hiyo tulitembea kupitia jiji la Seoul kwenda kwenye kao la wamisionari. Karibu majengo yote makubwa yalikuwa magofu tu. Jiji lilikuwa kimya kama vile nchi. Magari pekee yalikuwa ya kivita. Tokea mbali mimi ningeweza kuona kao la wamisionari. Majengo yaliyolizunguka yalikuwa yamebomolewa kabisa, lakini kao la wamisionari lilikuwa lingali likisimama. Ingawa hivyo, lilikuwa limepigwa na kombora moja kwenye pembe moja, likiacha tundu la meta 0.6 katika ule ukuta wa matufali. Madirisha yote yalikuwa yamevunjwa-vunjwa, lipu ya dari ilikuwa imeanguka chini, milango iliyo mingi ilikuwa imeangushwa, na waya zilikuwa zimeondolewa.”

Jioni iyo hiyo Mashahidi wapatao 35, sana sana akina dada, walikutana kusikiliza hotuba ya utumishi ya Ndugu Steele, na mipango ikafanywa kwa ajili ya utumishi wa shambani kwa siku zilizofuata. Kesho yake watu 18 walijitokeza kwa ajili ya kazi ya kutoa ushuhuda wa kikundi. Kabla ya wiki ya ziara yake kwisha, wahubiri 24 walitoa ripoti ya wakati wa utumishi wa shambani. Wale akina dada mashujaa waliobaki katika Seoul muda wote wa vita sasa walikuwa wakivuna matunda ya kazi yao ngumu.

Wale wahubiri wapya walitamani kubatizwa—lakini wapi? Vifaa pekee vilivyopatikana vilikuwa nyumba za kuogea ambazo sasa zilitumiwa na askari wa UM pekee. Mipango ilifanywa kuwabatiza hao wapya kwenye nyumba za kuogea kabla ya wafanya kazi wa UM kuwasili kwa ajili ya kazi ya siku. Kwa hiyo, Jumamosi, Desemba 29, 1951, kabla ya saa 2 asubuhi, wapya 27 walibatizwa, kutia na dada ya aliyekuwa hapo kwanza malkia wa Korea.

Pusan ulikuwa ndio mji mkuu wa muda wa nchi, nao ndio uliokuwa mahali panapofaa ambapo kutoka hapo ndugu wangetumikiwa kote kote nchini. Mashine mpya ya kurudufia iliagizwa na kupokewa kupitia Afisi ya Posta ya kivita ya Amerika. Kwa kushangaza, akina ndugu waliweza kupata, pia, mojapo taipureta za kwanza zenye chapa za Kikorea. Hatua nyingine kubwa ya kusonga mbele kwa Mashahidi katika Korea!

Katika Desemba 1951 na Januari 1952, Ndugu Steele aliweza kuzuru mahali kote ambako makundi na vikundi yalikuwa yameanzishwa. Ebu wazia, kabla ya vita kulikuwako jumla ya wahubiri 61 tu katika kundi moja katika Seoul. Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1952, kukawa na kilele cha wahubiri 192 katika makundi matano, tena katika hali za wakati wa vita, na hesabu kubwa zaidi ya akina ndugu wakiwa wanaishi katika hali ya ukimbizi.

Wakati wa pindi hii Sosaiti pia ilidhamini mchango wa mavazi. Tani mbili za mavazi na viatu ziliwasili kutoka United States.

HATIMAYE! MNARA WA MLINZI WENYE KUPIGWA CHAPA

Septemba 1952 ulikuwa mwezi wa maana kwa Mashahidi—lile gazeti Mnara wa Mlinzi liliandikishwa kwa serikali, na ruhusa ya kulitangaza ikatolewa. Mwanzoni, nakala zilizorudufiwa ziliandikwa kwa mkono, lakini baada ya Februari 1953 zikaandikwa kwa taipureta. Zile chapa za kwanza za kurasa 16 zilikuwa nakala kama 700 tu kila chapa.

Lile toleo la Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 1954, ndilo lililokuwa mwanzo wa magazeti yaliyopigwa chapa. Chapa ya kwanza ilikuwa nakala 2,000, kuanza na toleo la Januari 1955 kurasa zikaongezwa kuwa 20 na nakala 5,000. Lilikuwa gazeti la kila mwezi lililochapwa na kampuni ya kibiashara katika Seoul. Hata hivyo, lilikuja kuwa gazeti la mara mbili kwa mwezi katika 1961 na likawa lenye kurasa 24 kwa toleo la Januari 1967.

Ili iwe dini iliyotambuliwa kisheria nchini, ikawa lazima Mashahidi waunde shirika. Hivyo shirika The Watch Tower Songso Chaekja Hyuphoi of Korea likaundwa na kuandikishwa kwa Wizara ya Elimu katika Oktoba 30, 1952, likiwa na wakurugenzi sita na washiriki tisa. Katika Februari 25, 1969, kwa amri ya serikali, uandikisho huu ulihamishwa kwenye Wizara ya Utamaduni na Habari, na ndicho chombo cha kisheria kinachotumiwa mpaka leo hii. Sasa, likiwa shirika lililoandikishwa kisheria, iliwezekana kununua mali ambayo wamisionari walikuwa wametumia kabla ya vita.

TAWI LAANZISHWA

“Mambo yamekuwa yakienda vizuri sana katika Korea, hivi kwamba ni kama hayasadikiki,” ikataarifu barua ya Sosaiti ya Oktoba 18, 1952, waliyoandikiwa ndugu Wakorea. Halafu katika Julai 27, 1953, mapatano yenye wasiwasi ya kuacha vita yakatiwa sahihi, na ukanda wenye kuondolewa majeshi ulitiwa alama kati ya Korea Kaskazini na Kusini. Mpaka leo hii hakuna mawasiliano kati ya zile Korea mbili au kati ya washiriki wa jamaa wenye kutenganishwa na ule ukanda ulioondolewa majeshi.

Kufikia mwisho wa mwezi uliofuata, Don na Earlene Steele walikuwa wamerudi Pusan baada ya kuhudhuria mkusanyiko wa New York. Walifurahi sana kuona mwaka wa utumishi wa 1953 katika Korea ukifungwa kukiwa na wahubiri 417 katika makundi 7. Hivyo Sosaiti ikaelekeza kwamba kuanzia Septemba 1, 1953, tengenezo katika Korea lingeacha kuwa chini ya tawi la United States, liwe tawi la Korea. Don Steele angekuwa mtumishi wa tawi; leo yeye ndiye mratibu wa Halmashauri ya Tawi.

Tawi la Korea lilihamia kao lile lile katika Seoul lililotumiwa na wamisionari kabla ya vita. Sehemu za jengo zilizotengenezwa ni zile tu zilizokuwa na uhitaji mkubwa. Bado maji yalipasa kuletwa ndani, na kulikuwako umeme kidogo tu wa kutumia. Wamisionari walichagua sakafu ya pili, nalo kundi la pale likatumia sakafu ya kwanza kwa mikutano yao.

MSAADA KUTOKA CHANZO KISICHOTAZAMIWA

Muda wote wa miaka iliyopita baadhi ya yale maelfu ya wanaume wa jeshi la United States ambao wametumikia katika Korea si kwamba tu wameonyesha kupendezwa katika ukweli bali wameendelea kiroho. Baada ya kurudi United States na kufanya mabadiliko yaliyohitajiwa kabisa katika maisha zao, wamekuja kuwa Mashahidi watendaji.

Norbert Matz Sajini wa Daraja la Kwanza wa Jeshi la United States alikuwa kielelezo chenye kutokeza. Yeye alitamani uhusiano unaofaa pamoja na Mungu. Kwa hiyo yeye akaanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi alipokuwa katika United States. Yeye alisonga mbele kwa haraka, sana sana hivi kwamba wakati jeshi lilipomhamishia Korea, yeye aliweza kwa kweli kuongoza mafunzo na Wakorea. Pia alisaidia akina ndugu kupitia Shule ya Huduma ya Kitheokrasi. Jinsi gani? Hakukuwa na kitabu cha mafunzo cha Shule ya Huduma ya Kitheokrasi katika Kikorea, kwa hiyo yeye alikuwa akiwasaidia wafahamu ile habari ya shule kupitia mkalimani. Pia yeye alisaidia kupangia ubatizo wa kikundi katika Juni 30, 1953, na akatumia magari ya kivita kwa usafirishaji kwenye mahali pa ubatizo—52 wakazamishwa. Yeye alithibitika kuwa msaada mkubwa wakati wa pindi ile ambayo wamisionari hawakuweza kuwa katika Seoul. Leo, akiwa Ndugu Matz, yeye anatumikia akiwa mzee katika kundi moja katika United States.

Mwanafunzi wa Biblia mmoja wa Norbert Matz alikuwa kijana Mkorea daktari wa jeshi, Chun Young-soon. Yeye alibatizwa katika 1953 na upesi baada ya hapo akaanza kazi yake ya maisha katika utumishi wa wakati wote. Akiwa mhitimu wa Gileadi, akawa mwangalizi asafiriye na mwangalizi wa Kao la Betheli na kwa sasa anatumikia katika Halmashauri ya Tawi. Katika mwaka uo huo wa 1953, Park Chong-il alikabili suala la utumishi wa kivita kwa mara ya pili. Kwa mara nyingine tena yeye aliweka kielelezo kizuri cha kutokuwamo kwa Kikristo kwa ndugu hawa, pamoja na wengine, ambao wangefuata.

MKUSANYIKO MKUBWA WA KWANZA

Sheria ya kivita ikiwa mwishowe imeondolewa wakati wa vuli ya 1953, iliwezekana sasa kwa Korea kuwa na mkusanyiko wa wilaya—Agosti 6-8, 1954. Mahali pao palikuwa Shule ya Msingi ya Chae Dong. Kwa mara ya kwanza, akina ndugu kutoka kote kote nchini walikusanyika. Hadhirina iliyokadiriwa ilikuwa imewekwa kuwa 700, lakini 1,043 walikuwapo siku ya kwanza, ikikua kufikia 1,245 kwa Mkutano wa Watu wote Jumapili. Wengi, wakikumbuka zile siku za huzuni za Vita ya Ulimwengu ya Pili ikifuatwa na hofu za vita ya Korea, walikuwa na macho yaliyojaa machozi ya shangwe. Wao walidhani hawangeweza kamwe kuona siku ambayo watu wengi sana hivyo wangekusanywa upande wa Yehova.

Jambo la kutokeza kwenye mkusanyiko huu lilikuwa ule ubatizo wa kwanza wa watu wengi. Mume wa dada mmoja ambaye alikuwa mkuu katika idara ya moto alipanga kile kidimbwi kwenye shule kijazwe maji baada ya akina ndugu kusafisha na kuondoa takataka iliyoachwa ndani yacho kutokana na ile vita. Siku hiyo, kwa mshangao wenye furaha wa wote, 284, au asilimia 23 ya wote waliohudhuria, walizamishwa. Sasa ikawa wazi kwamba tawi lingekuwa na kazi kubwa mbele yalo kusaidia wote hawa wapya wafanye maendeleo kiroho.

GILEADI YATUMA MSAADA ZAIDI

Katika Machi 1955 lile wimbi la pili la wamisionari liliwasili katika Korea—Milton na Liz Hamilton, Keith na Evelyn Kennedy, Karl Emerson, Norris Peters, Elaine Scheidt (sasa ni Ness), na Druzilla (Dru) Craig (sasa ni Youngberg). Kikundi kikubwa cha akina ndugu kiliwalaki kwenye Uwanja wa Ndege wa Yoido. Wakati ule uwanja wa ndege ulikuwa katika kisiwa cha mchanga katika Mto Han ambacho leo ni jiji ndani ya jiji. Ijapokuwa hapana ye yote wa wale wamisionari wapya aliyejua ile lugha, tabasamu, machozi ya shangwe, na ishara zilieleza hisi zao. Sasa ile afisi ya tawi kwa mara nyingine tena ingekuwa ikivuma wafanya kazi, kwa kuwa ilikuwa muungano wa afisi ya tawi na kao la wamisionari.

Mwezi mmoja baada ya wamisionari kuwasili, kusanyiko la mzunguko lililo la kwanza katika Korea lilifanywa katika Aprili 1955. Lo! hilo lilikuwa jambo lenye kusisimua kama nini kwa akina rafiki! Wale wamisionari hata walikuwa na sehemu katika programu lakini wakasema kupitia wakalimani.

KAO LA WAMISIONARI LA PUSAN

Katika vuli ya 1955 kao la wamisionari lilifunguliwa katika jiji bandari la Pusan mwendo wa meta za angani zipatazo 320 kusini mwa Seoul. Wakati ule jiji la Pusan lilikuwa na idadi ya watu wapatao 1,100,000 na lilikuwa na kundi moja tu la Mashahidi. Akina Hamilton, Evalyn Myung Hae Park (sasa ni Emerson), na dada mmoja Mkorea wakaanzisha kao hilo.

Kwa sababu ya idadi kubwa ya wakimbizi, makao katika jiji yalikuwa yenye gharama sana, lakini mahali padogo palipatikana. Palikuwa katika sakafu ya pili na palikuwa na vyumba viwili vya kulala na chumba kidogo kimoja cha kulia, na veranda ikatumika kuwa jikoni. Hakukuwa na majimtiririko na umeme kidogo ulipatikana, jambo ambalo lilifanya kupika, kusafisha, na kuosha kuwa kazi zenye kuchosha. Ili kufanya maji yanyweke, ilikuwa sharti kuyachemsha au kuyatia klorini.

“Akina ndugu hawakuwa na vitu vingi katika siku hizo, lakini walikuwa wachangamfu na wenye urafiki na walikuwa na bidii kwa utumishi wa shambani,” asema Ndugu Hamilton.

Jumla ya wamisionari 17 wametumikia katika jiji la Pusan, na leo kuna makundi 51 katikati ya idadi ya watu 3,500,000. Sikuzote akina ndugu wameliona kuwa pendeleo kuwa walikuwa na kao la wamisionari katika jiji lao.

ZIARA YENYE KUONYESHA MAENDELEO MAKUBWA

Ule wakati wenye maana kubwa ukafika—mzuruji rasmi wa kwanza kutoka makao makuu ya ulimwengu tangu siku ya Ndugu Hollister. Ndugu Nathan H. Knorr, wakati huo akiwa msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, alikanyaga kwa mguu udongo wa Korea Aprili 27, 1956, kwenye Uwanja wa Ndege wa Yoido, ambapo 500 wa wale wahubiri 1,500 walimkaribisha. Walioandamana na Ndugu Knorr ni Don Adams kutoka Afisi ya Brooklyn na Lloyd Barry (sasa wa Baraza Linaloongoza), ambaye alikuwa akizoezwa kazi ya eneo la dunia katika Mashariki.

Ziara ya Ndugu Knorr ya siku sita ilikuwa tukio la maana katika historia ya kitheokrasi ya Korea. Hotuba yake ya kwanza kwa waliokusanyika 1,330 kwa mkusanyiko wa kitaifa iliwahakikishia tena kwamba wao walikuwa kweli kweli sehemu ya tengenezo la Yehova la ulimwenguni pote. Kwenye mkusanyiko huu 303 walibatizwa katika yale maji zizima ya masika ya Mto Han. Kuonyesha matazamio kwa wakati ujao, umati wa watu 3,473 ulikusanyika katika Uwanja wa Mchezo wa Seoul kwa ajili ya hotuba ya watu wote “Kufanya Wanadamu Wote Kuwa Mmoja Chini ya Muumba Wao.”

Ndugu Knorr aliona kwamba sasa kazi ya maana katika Korea ilikuwa kusaidia hawa wapya wasonge mbele kiroho. Yeye aliweka daraka kuu la kazi hii mabegani mwa washiriki wa tawi na wamisionari. Pia yeye alitambua kwamba wengine walikuwa wakibatizwa upesi mno, bila maarifa ya kutosha ya Maandiko. Kama tokeo, wengine walikuwa wamekengeuka. Kwa hiyo aliagiza washiriki wa tawi kwamba ubatizo ungefanywa tu kwenye makusanyiko ya mzunguko au mikusanyiko mikubwa zaidi. Hilo lilisaidia. Watu wenye kupendezwa sasa walijifunza na wakashirikiana na kundi muda mrefu zaidi kabla ya ubatizo, jambo ambalo liliwatayarisha kutimiza madaraka yao ya wakati ujao wakiwa Mashahidi.

MSAADA KWA ELIMU YA BIBLIA

Kazi ya funzo la Biblia ikawa ya kadiri mpya katika 1956 ilipotolewa chapa kamili ya Kikorea ya kitabu “Let God Be True.” Kwa Wakorea, elimu ni mojapo ya mambo ya maana zaidi katika maisha, jambo linaloshuhudiwa na uhakika wa kwamba kadiri ya kutojua kusoma na kuandika leo ni asilimia 8 tu. Tawi halijawa kamwe na lazima ya kudhamini madarasa ya kusoma na kuandika. Huo, bila shaka, ni msaada katika kuelimisha watu katika Biblia, nao wahubiri wana zawadi ya kutolea kazi hiyo.

La kupendeza pia ni ule mfanyizo wa kidini wa watu katika nchi. Asilimia ipatayo 22 ya wakazi wa Korea 42,000,000 ni Wabudha, asilimia 20 nyingine hudai kuwa Wakristo, na wanaobaki hawafuati itikadi yo yote maalum. Hata hivyo, Ushamani ungalipo kwa wingi sana kote kote nchini, na Ukonfusho unatawala mielekeo na kanuni za walio wengi. Wahubiri wamekuwa chonjo kuwatolea elimu ya Biblia wote hao waliovurugika kidini. Matokeo yamekuwa nini? Yenye kutokeza!

Mwaka 1956 uliona 12 wakiwekwa rasmi kwenye kazi ya painia wa pekee kuongezea wale wamisionari 11 waliokuwa tayari katika shamba. Mpaka leo hii jeshi hili la mapainia wa pekee, lililo na hesabu ipatayo 100 sasa, huendelea kuzaa tunda zuri sana. Katika nyakati zilizopita maongezeko yaliyo makubwa zaidi yalikuja kutoka idadi za watu wa majiji. Lakini sasa kukiwa na njia za ki-siku-hizi, za mawasiliano na usafirishaji, vile vijiji vidogo zaidi na miji ambako mapainia wa pekee wanapelekwa huonyesha matokeo mazuri sana.

JAMAA YA WAFANYA KAZI WENYE BIDII

Ndugu Park Young-shin, mwangalizi wa mzunguko, anasimulia jinsi jamaa yake ilivyochukua ibada ya kweli kwa sababu ya jitihada za mapainia wa pekee na kile kitabu “Let God Be True.” Ilianza katika jiji la Sunch’ŏn, katika mkoa wa Chŏlla kusini mwa Korea.

“Wakati ule walikuwako mapainia wa pekee watatu katika jiji, na wakati mama yangu alipokuwa akitembelea majirani, yeye alikubali gazeti la Mnara wa Mlinzi kutoka kwa mmoja wao,” yeye anaanza. “Dada yangu mkubwa nami tulimwambia mama asikubali hayo, kwa kuwa Mashahidi walikuwa wazushi wasio na maarifa. Hata hivyo, mama yangu alisisitiza kwamba wao walionekana kuwa watu wazuri waliotumia Biblia. Muda uo huo, Mashahidi wawili wanawake wakatutembelea. Mimi niliuliza tofauti ilikuwa nini kati yao na Waprotestanti. Nilifikiri elezo lao lilikuwa la akili, nami nikakubali kile kitabu “Let God Be True” na nikakubali kujifunza Biblia pamoja nao, si ili niwe mmoja wao, bali kuongeza maarifa yangu ya Biblia.

“Haikuchukua muda mrefu kuona kwamba mimi nilikuwa nimefundishwa fundisho la bandia. Hilo lililemea dhamiri yangu, nami mwishowe nikaamua kujiuzulu kanisa. Nilipomwambia pasta, yeye alisema: ‘Sababu gani Mashahidi wa Yehova? Ikiwa lazima ufanye badiliko, ungeweza kwenda Methodisti au lile Kanisa la Utakatifu. Wewe umechagua dini mbaya.’

“Katika Oktoba 1957 mama yangu, dada yangu mkubwa, nami tulibatizwa, tukifuatwa baadaye na baba yangu na watoto saba, kwa ujumla. Mama yangu akiwa katika umri wa miaka 73 ni painia wa kawaida, hali dada yangu mkubwa amekuwa katika kazi ya painia wa pekee tangu 1967 na amesaidia watu wapatao 60 kufikia wakfu na ubatizo. Ndugu zangu wawili wakubwa ni waangalizi wasafirio.”

Mkusanyiko mwingine wa taifa ulipangiwa Januari 1957 kwa sababu ya ile ya kwanza ya ziara kadhaa za Ndugu Frederick W. Franz, ambaye sasa ndiye msimamizi wa Sosaiti. Mara tu alipotoka katika ndege, akina ndugu walimpeleka mbiombio moja kwa moja kwenye jumba la mkusanyiko, ambako yeye alishangaza hadhirina kwa kusema anasikitika kwamba ilimchukua miaka 63 kufika kule. Kisha akawapendelea kwa nyimbo za Ufalme kwa kupiga kinanda chake cha mdomo.

Katika zile siku chache baada ya mkusanyiko, ko kote Ndugu Franz alikoenda, akina ndugu wangefuata, wakijawa na maswali ya Biblia ambayo walihisi wakitaka sana kuuliza. Katika moja ya siku hizo, chakula kikubwa kilipangwa kiliwe saa saba alasiri. Baada ya kila mmoja kujifurahisha mlo mtamu wa Kikorea, akina ndugu walianza maswali yao ya Biblia na kumweka Ndugu Franz akiwa na shughuli nyingi akijibu maswali haya mpaka saa kumi na mbili jioni hiyo. Ndugu Franz hakuchoka, lakini mmoja wa watafsiri wake alichoka na ikawa lazima kutumia wa pili.

MAPENZI YA KIMUNGU KUSANYIKO LA KIMATAIFA LA 1958

Wakati wamisionari 2 zaidi, Bradley Ness na Bill Phillips, walipowasili na wakawa wanaweza kuangalia mali katika Seoul, wale wamisionari wengine 11 waliweza kuhudhuria ule mkusanyiko wa kimataifa katika Jiji la New York. Kuongezea, wajumbe Wakorea 14 walihudhuria huko. Kufuata mkusanyiko huo, ndugu wawili, Park Chong-il, ambaye alikuwa amekuwa mtafsiri mkazi wa kwanza kwenye tawi katika 1956, na Kim Jang-soo na dada wawili, Kim Kyung-hi na Lee Hae-young, walichaguliwa wahudhurie Gileadi.

Mkusanyiko wa Mapenzi ya Kimungu wa Korea ulikuwa katika Oktoba. Ulifanywa nje kwenye uwanja wa michezo, ambako wajumbe 2,800 walivumilia hali ya hewa yenye baridi kidogo ya vuli ili wahudhurie Jumapili, na 153 wakabatizwa.

MPANUKO KATIKA KAZI YA MZUNGUKO

Kwa sehemu, tawi limetimiza ule uhitaji wenye kuendelea wa waangalizi wasafirio wanaostahili kwa kuwapa ndugu waliozoezwa Gileadi migawo ya kazi ya mzunguko au wilaya. Hao walikuwa ni kutia ndani Norris Peters na Karl Emerson, waliokuja Korea katika 1955. Mwanzoni, walipotembelea makundi, wakalimani walihitajiwa mpaka wao wakawa wenye ufasaha katika lugha. Ndugu Chae Soo-wan, mwangalizi katika Idara ya Utumishi na mshiriki wa Halmashauri ya Tawi, alikuwa afisa katika jeshi la Korea wakati alipoanza kujifunza. Katika 1957 yeye aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa mzunguko na alihudhuria Gileadi katika 1962.

Kufikia mwisho wa mwaka wa utumishi wa 1958, kulikuwa na kilele cha wahubiri 2,724 katika makundi 54 na vikundi vingi vilivyo peke yavyo vyenye kufanyiza mizunguko mitano. Kukiwa na ongezeko hili katika shamba, ilikuwa sharti akina ndugu zaidi waliostahili wapatikane na kuongezwa kwenye wale waliokuwa katika kazi ya kusafiri. Ok Ryei-joon na mke wake waligawiwa kazi ya mzunguko, na ndivyo na Milton na Liz Hamilton, wamisionari mume na mke wa kwanza kuingia kazi ya kusafiri katika Korea.

Kwa akina Hamilton hili lilimaanisha kuishi pamoja na wenyeji na kujihusisha sana katika njia zao za maisha zilizo tofauti na maisha katika kao la wamisionari. Kwa sababu walikuwa wageni wa kutoka ng’ambo, ilikuwa sharti wao wajifunze ile kawaida ya kila siku ya kula na kulala sakafuni kuongezea kuketi sakafuni wanapokuwa kwenye mikutano katika Jumba la Ufalme. Wakati ule majimtiririko yalikuwa haba, na mabomba ya kuleta maji ndani ya nyumba hayakuwako. Hata hivyo, yote haya yalikuwa sehemu ya kazi ya misionari. Leo, Ndugu Hamilton anatumikia katika Halmashauri ya Tawi na ndiye mwangalizi wa kiwanda.

Ndugu Park Ii-kyun alianza utumishi wa wakati wote katika 1956 na akaandamana na mmoja wa wamisionari katika kazi ya mzunguko akiwa mkalimani. Baada ya mazoezi ya Gileadi, yeye alipewa tena mgawo kwenye afisi ya tawi na sasa anatumikia akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.

Baada ya Jerry na Barbara Tylich kuwasili Korea katika 1966, wao walipewa mgawo kwenye kundi moja la Seoul na baadaye wakatumikia katika mzunguko. Jim Tylich, Merlin Stoin, na Durand na Rachel Norbom walijiunga nao katika kazi ya mzunguko katika 1967. Akina Norbom sasa ni washiriki wa jamaa ya Betheli ya Kongdo. Rachel anakumbuka baadhi ya maswali aliyoulizwa walipokuwa wakizuru makundi.

“Hata juzijuzi tu mapema mwa muda wa tangu 1970 ilikuwa ajabu mwanamke wa kutoka nchi za Magharibi kuonekana katika sehemu za mashambani, na ilikuwa sharti mmoja azoee maswali ya kibinafsi sana,” yeye anaeleza. “‘Wewe una umri gani?’ ‘Je! umeolewa?’ ‘Una watoto wangapi?’ na kisha, ‘Sababu gani huna wo wote?’ Katika mahali pamoja uvumi ulienezwa kwamba mume na mke Waamerika walikuja kuchukua baadhi ya watoto kuwapeleka [United] States wakalelewe huko, na kwa hiyo wanawake kadhaa wakaja ili watoe watoto wao wakapelekwe kwa yale ambayo wao walidhani yangekuwa maisha yenye ufanisi zaidi.”

Wengine pia wanaotumikia leo katika kazi ya kusafiri kati ya mizunguko 43 ya Korea ni Josef Breitfuss (kutoka Austria), Perry na Geline Jumuad (kutoka Ufilipino), na John na Susan Wentworth (kutoka United States), wote wakiwa wamisionari kwa miaka 14 kufika 17 iliyopita.

KUPONEA CHUPUCHUPU WAKATI WA GHASIA

Ile ndege iliyokuwa inabeba Ndugu Milton Henschel ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kimpo siku ya Aprili 13, 1960. Ziara yake ya eneo la dunia kwenye tawi ilisadifu na mkusanyiko wa siku nne uliofunguliwa kwa hadhirina ya 2,385.

Kusanyiko la Kufuatia Amani lilipokuwa likifanywa, serikali ya Korea ilikuwa ikijaribu kuzuia ghasia zenye umwagaji wa damu za maelfu ya wanafunzi. Mapigano yenye ghasia nyingi yalitokea kwenye barabara ya mji karibu tu na uwanja wa mkusanyiko. Kwa furaha, hadhirina ya mkusanyiko, ilikua kufikia zaidi ya 4,000—hicho kikiwa ndicho kilele kilichopata kuwako kwa mkutano wa Watu Wote—kikijaza kila pembe ya uwanja wa michezo wa Samil Dang.

Jumatatu Jioni, ile siku iliyofuata mkusanyiko, Ndugu Henschel alifanya usimamizi wa arusi ya wamisionari Bradley Ness na Elaine Scheidt. Hata hivyo, kutoka kwenye mahali pa arusi kwenda hotelini kulithibitika kuwa hatari. Ndugu Henschel na wamisionari kadhaa walitoka mahali pa arusi wakaingia kibarabara chembamba. Ghafula, wakanaswa kati ya maelfu ya wanafunzi wenye kuja mbio kwa ghasia kutoka upande mmoja wa barabara na malori yaliyojaa mapolisi wenye silaha yakiharakisha toka upande ule mwingine. Ndugu Henschel na washiriki wake waliruka kama mshale kuvuka barabara ya mji na kuingia ndani ya mkahawa muda mchache tu kabla ya zile pande mbili kupambana. Ilishangaza jinsi walivyopona! Ingawa hivyo, mara walipokuwa ndani ya hoteli, kukawa amani na utulivu.

Wakati wahitimu wa Gileadi watano zaidi walipopewa mgawo kwenda Korea, maombi yao ya viza yalikataliwa na serikali ya Korea, kwa kuwa wapinzani walikuwa wamewashtaki Mashahidi kuwa wanamapinduzi. Don Steele aliweza kupangiwa mahoji pamoja na Walter McConaughy balozi wa United States, siku ya Aprili 6, 1960.

Balozi huyo aliambia Ndugu Steele kwamba ilikuwa kinyume cha mambo kilicho kibaya kabisa kuwashtaki Mashahidi wa Yehova kuwa wanamapinduzi. Yeye alikuwa ametumikia katika nchi moja ya Ulaya Mashariki na alijua jinsi Mashahidi walikuwa wameteswa katika Ujeremani Mashariki. Lakini yeye pia alitaja kwamba kwa kuwa Korea ni nchi iliyo na enzi yayo yenyewe, ina haki ya kumpa viza mtu ye yote inayotaka. Hata hivyo, yeye angejaribu kupangia Ndugu Steele mahoji pamoja na waziri wa mambo ya nje. Hili lilipangiwa Jumanne, Aprili 19, 1960. Kwa kuwa ndugu Henschel, ambaye ni Mkurugenzi wa Sosaiti katika United States, alikuwa angali katika Korea, yeye pia angeweza kusema na yule waziri.

Hali katika nchi zilikuwa zikizorota; serikali haikuweza kukomesha ghasia zilizokuwa zikifanywa. Jumanne ikawasili. Wale akina ndugu walikuwa wakutane na waziri wa mambo ya nchi za nje mjini, ambapo ndipo palipokuwa mahali pa ghasia kali zaidi. Bila kutishika na kwa kutotaka kuvunja mwadi, wale akina ndugu wakashika njia yao kwenda kwenye Wizara.

Walikuta lile jengo limefungwa kikiki, madirisha ya chuma yakiwa yameteremshwa na mifuko ya mchanga pande zote kwa kuwa wakazi wa lile jengo walijikinga kwa boma dhidi ya shambulio la wanafunzi. Kwa wazi hakungekuwa na mahoji siku hiyo, na ndugu Henschel na Steele walikimbia kurudi nyumbani kupitia vibarabara vya kando-kando kwa haraka walivyoweza, wakikanyaga kando-kando ya majeruhi waliokuta njiani.

Siku kadhaa baadaye, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ikajulisha Tawi kwamba kila “kisababishi” cha yale makatao “kilikuwa kimeondolewa” na wangeweza kupewa viza. Katika Juni wa mwaka huo, Russell na Dottie MacPhee, Delauris Webb (sasa ni Peters), Audrey Wendell (sasa ni Holmes), na Lois Dyke (sasa ni Renter) waliwasili kuchukua utumishi wao wa misionari. Kao jingine la wamisionari likaanzishwa katika Kwangju.

VIZUIZI VYA MUDA

Serikali ya Syngman Rhee ilianguka katika masika ya 1960. Miezi kadhaa baadaye, serikali iliyochaguliwa rasmi ikachukua uongozi, ikaja kuangushwa tu na mapinduzi ya kivita katika Mei 1961. Kwa mara nyingine tena sheria ya kijeshi ikakandamiza nchi kwa ujumla. Hivyo, hata mikutano mikubwa ya kidini ilipigwa marufuku mpaka wale wenye mamlaka wapya walipokuwa wameiweza hali. Hata hivyo, hadhirina kwa mikutano ya kundi haikupatwa na upungufu chini ya hali hizi.

Wakati vizuizi vilipoondolewa, matengenezo yote ya kidini yalikuwa hayana budi kujiandikisha upya kwa wale wenye mamlaka wapya. Hili lilikuwa jambo gumu likitokeza kazi kubwa ya kuandika-andika karatasi nyingi. Kulingana na utaratibu shirika The Watch Tower Songso Chaekja Hyuphoi of Korea liliandikishwa tena na Wizara ya Elimu katika Novemba 25, 1961.

“HABARI NJEMA ZA MILELE” MAKUSANYIKO

Furaha ilijaa tele wakati ilipotangazwa kwamba Korea ingekaribisha mojapo “Habari Njema za Milele” Makusanyiko katika 1963. Wakati huo Korea ilikuwa nchi changa. Ijapokuwa leo watalii milioni moja hivi huja Korea kila mwaka, wakati ule hiki kilikuwa ndicho kimojapo vikundi vikubwa zaidi vya watalii vilivyopata kuzuru Korea—watu zaidi ya 400 kutoka nchi 19. Hivyo, kila Shahidi Mkorea alipendezwa na kuwasili kwa hawa akina ndugu kutoka ng’ambo.

Ile ndege ya kwanza, ikiwa na wajumbe 94 wenye kuja mkusanyikoni kutoka nchi za kigeni, iliwasili asubuhi ya Agosti 24, 1963, Ndugu na Dada Knorr wakiwamo. Afisa mkuu wa itifaki (protokali) wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje alikuwapo kumkaribisha Ndugu Knorr na mkeye, ambao walitangulia kuchukuliwa kwa gari la kibinafsi. Lakini upesi msafara wa mabasi yaliyojaa wale wajumbe wengine, ukisindikizwa na polisi kwa kutoa heshima ya pekee, ulipita lile gari la kibinafsi na kuliacha nyuma mbali sana.

Ubatizo wa watu 612 ulikuwa ndio mkubwa zaidi kabisa kufikia hapo. Tangazo la kwamba sasa Amkeni! la Kikorea lingekuwa la mara mbili kwa mwezi lilileta shangwe kwa wote katika hadhirina kwa sababu tangu toleo lalo la kwanza la Kikorea la Septemba 8, 1959, Amkeni! lilikuwa limekuwa gazeti la mara moja kwa mwezi. Hadhirina ya mhadhara ilikua kufikia 8,975, elfu tatu kati yao walikuwa watu wenye kupendezwa! Lisilo la kusahauliwa, hata hivyo, lilikuwa lile ongezeko la asilimia 12 katika wahubiri kwa mwaka huo na hadhirina ya 9,893 kwenye Ukumbusho.

MPANUO WA TAWI WA KWANZA

Kulikuwako uhitaji wenye kukua wa kupanua vifaa vya tawi ili kwenda sambamba na ongezeko kubwa katika wahubiri. Ingawaje, katika muda ulio chini ya miaka 15 ukuzi ulipanda kutoka konzi moja tu la wahubiri waliokuwako kabla ya ile Vita ya Korea hadi zaidi ya 5,000 kufikia mwanzo wa mwaka wa utumishi wa 1964. Katika Agosti 1964 mwanzo ulifanywa wa kujenga mpanuo wa tawi wa orofa tatu ambao ungeongeza mara tatu nafasi ya sakafu iliyokuwapo.

Jamaa ya Betheli ilihamia jengo jipya Mei 1, 1965. Lile Jumba la Ufalme jipya lilikuwa jambo la kwanza katika Korea—lilikuwa na viti!

VITABU VYENYE JALADA LAINI VYA KUTUMIWA SHAMBANI

Julai 19, 1966, ilikuwa siku nyingine yenye kufanyiza historia. Kuanzia wakati huo na kuendelea vitabu vyote vya Sosaiti katika lugha ya Korea vingechapwa katika Korea. Tawi la United States halingehitaji tena kuandaa shehena ya zawadi za vitabu vyenye jalada gumu.

Vitabu vilichapwa katika rangi moja kwa kutumia karatasi ya habari na kufungwa kwa jalada laini kwa sababu vitabu vyenye jalada gumu vingekuwa ghali kwa watu wa kawaida. Kwa vyo vyote, ule ujumbe kwa kweli ndio uliokuwa jambo la maana na huo ungekuwa ule ule. Licha ya hilo, vitabu vilivyo vingi vilivyofanyizwa Korea wakati ule vilikuwa pia vyenye jalada laini. Ni kichapo kipi kilichokuwa cha kwanza? “Mambo Mawili Yasiyobadilika Asiyoweza Mungu Kusema Uongo.”

Zile nakala za kwanza 50,000 za kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele, kilichotolewa katika Kikorea Januari 1969, zilidumu miezi michache tu na ikawa sharti kichapwe tena mara hiyo. Akina ndugu sasa wakatumia vizuri shambani kifaa hiki kisicho ghali cha funzo la Biblia la nyumbani. Hesabu ya mafunzo ya Biblia ikapanda upesi sana! Karibu wote waliokuja katika ukweli wakati wa pindi hiyo walijifunza mafundisho ya msingi ya Biblia kupitia kichapo hiki. Mpaka leo hii, zaidi ya nakala milioni 2.2 za kitabu hiki zimechapwa na kuenezwa katika Korea pekee! Idadi ya wahubiri ilipanda kutoka zaidi kidogo tu ya 8,000 mwishoni mwa 1968 kufika zaidi ya 30,000 katika 1982, wakati kile kitabu Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani kilipotolewa.

Kilele cha 22 mfululizo cha wahubiri, jumla ya 10,610, kilifuatwa upesi na “Amani Duniani” mkusanyiko wa kimataifa katika Seoul uliofanywa kwenye uwanja wa Chang Choong Gymnasium katika Oktoba 1969. Kwa wasikilizaji 14,529, Ndugu Franz alitoa kile kitabu Is the Bible Really the Word of God? Kwa mara ya kwanza, kichapo katika Kikorea kilitolewa wakati ule ule na Kiingereza.

NI SHAURI LA DHAMIRI

Jamhuri ya Korea ina mojapo vikosi vyenye silaha vilivyo vikubwa zaidi ulimwenguni. Lazima ya kuandikisha raia wote katika jeshi la kivita imekuwa ikiendelea bila kuwaacha viongozi wa kidini au wenye kukataa kwa sababu ya dhamiri.

Katika Februari 22, 1971, barua ya rejesta kutoka kwa serikali iliwasili kwenye tawi. Ile barua iliwashtaki Mashahidi kuwa wanafundisha watu wasiimbe nyimbo za kizalendo au wasipige kura katika machaguzi ya kisiasa na kuwatia moyo makusudi waepuke lazima ya kuandikishwa jeshini. Katika kujibu mashtaka haya, tawi lilieleza ni kwa sababu gani Mashahidi wa Yehova si wachochezi wa uasi juu ya serikali na msingi wa Biblia wa kujitiisha chini ya mamlaka zilizo kuu. Tawi lilisema kwamba Mashahidi hawaingilii tendo lo lote la serikali, kutia na kupiga kura au kuandikisha watu jeshini kwa lazima.

Mambo yalizidi kuwa mabaya. Baada ya kupata habari za matukio zaidi, Ndugu Knorr alidokeza kwamba akina ndugu wafanye ziara kwenye afisi ya balozi wa United States. Kwa hiyo katika Machi 24, 1971, Ndugu Steele na Hamilton wakakutana kwa saa moja na Naibu Mkuu wa Ujumbe wa United States, Francis T. Underhill. Baada ya mazungumzo machangamfu juu ya kazi ya Mashahidi wa Yehova na msimamo wao juu ya mambo haya, Bw. Underhill alisema kwamba yeye angeripoti jambo hilo kwa Idara ya Serikali katika Washington. Hata hivyo, hakuna lo lote zaidi juu ya jambo hilo lililotukia wakati ule.

Hivyo muda wote wa miaka iliyopita, malejioni ya akina ndugu—wazee na vijana—wamekuwa hawana budi kuvumilia masuala haya. Wengine hawakuweza kumaliza masomo yao au hawangeweza kupata kazi. Bado wengine ambao wamemaliza maisha yao kwa kushika ukamilifu wanangojea ufufuo.

ULIOPATA KUWA MKUBWA ZAIDI

Wakati ulikuwa unakaribia kwa mkusanyiko wa kimataifa wa tatu kufanyiwa Seoul, katika kiangazi cha 1973. Ule mkusanyiko wa “Ushindi wa Kimungu” ulikuwa ndio mkusanyiko mmoja mkubwa zaidi uliopata kufanywa Korea—zaidi ya 29,000 walihudhuria na 2,002 wakabatizwa.

Ndugu Park Ii-kyun, ambaye kwa mkusanyiko huu alikuwa ndiye mwangalizi wa mkusanyiko, anatoa ripoti hii: “Kwa sababu ya msukosuko nchini, bado kulikuwa na wasiwasi upande wa wenye mamlaka. Kama matokeo, idara ya polisi ilituma makachero 130, na 2 kati yao waliwekwa katika kila idara ya mkusanyiko kuongezea wale waliowekwa kote kote katika uwanja. Polisi hao walitaja kwamba sisi tulitii vizuri zaidi ya watu wenye elimu ya koleji.

“Inapoanza kunya wakati wa michezo na mikutano mingine inayofanywa nje, machafuko hutukia. Kila mmoja akienda mbio kuelekea sehemu za kutokea. Wakati wa pindi moja ya mkusanyiko, mvua ilianza kunya, nao polisi wakaenda mbio kufungua sehemu zote za kutokea, lakini kwa mshangao wao, hakuna mtu aliyeondoka. Badala yake, wote walifungua miavuli yao na wakakaa kwa utulivu tu na kusikiliza programu.

“Katika kuongezea, meneja wa uwanja ule wa michezo aliniambia kwamba ule uwanja wa michezo haujapata kamwe kuwa safi kama ulivyokuwa, na ikiwa angeweza kuukodisha kwa Mashahidi wa Yehova mara moja kwa mwezi, sikuzote ungekuwa safi.”

SABABU YA HANGAIKO

Yote yalionekana kuwa sawa katika masika ya 1975. Jamaa ya Betheli ilihamia vifaa vyao vipya vyenye nafasi kubwa, na ndugu Lloyd Barry alizuru kutoka Japani kuja kutoa hotuba ya wakfu. Mwaka wa utumishi wa 1975 ulimalizika ukiwa na ripoti ya shambani yenye kutokeza—kutia na 8,120 waliobatizwa mwaka huo. Hivyo, katika wakati wa miaka mitatu tu 19,600 walibatizwa. Zaidi ya nusu ya Mashahidi Wakorea walikuwa wamekuja katika ukweli kwa muda wa punde kuliko miaka mitatu.

Hata hivyo, ile miezi michache ya kwanza ya mwaka wa utumishi wa 1976 ilianza na mpunguo ulio wazi katika wahubiri na mafunzo ya Biblia ya nyumbani. Mwendo huu wa kushuka ungeendelea kwa zaidi ya miaka mitatu, mpaka kwenye kiwango cha chini cha asilimia 26 katika wahubiri, toka 32,693 katika Agosti 1975 kufika 24,285 katika Novemba 1978. Hadhirina ya Ukumbusho ilishuka pia, toka zaidi ya 68,000 katika 1975 kufika 49,545 katika 1978. Akina ndugu kwenye tawi walitatizika. Je! mwendo huo ungebadilika?

Bila shaka, wala wao wala Sosaiti hawakuwa wanaachilia hivyo tu. Barua ya Sosaiti ya Aprili 4, 1977, ilitaarifu:

“Sisi tunatumaini akina ndugu ni waangalifu katika kufundisha kwao. Kwa wazi wengine walitilia mkazo sana tarehe ya 1975, na kwa hiyo msingi mzuri haukuwekwa. Msingi, bila shaka, unapaswa uwe imani katika Kristo Yesu na dhabihu ya ukombozi, na wakfu wapaswa ufanywe kwa kuelewa.”

Hilo ni oneleo la unyofu kweli kweli! Walimu fulani wa Biblia waliweka mkazo mwingi mno juu ya tarehe. Wapya wengi waliobatizwa waliuchukua ukweli kwa kupigwa na wimbi la hisi za moyoni. Hata wazee fulani walikuwa wamekaza kikiki matumaini yao kwenye 1975. Kwa kuongezea, upendo wa vitu vya kimwili ulipenya ndani ya nchi kama tokeo la ukuzi wa haraka wa kiuchumi katika Korea, nao utukuzo wa taifa ulikuwa unapanda. Tokeo likawa: ubaridi miongoni mwa akina ndugu.

NJIA YA KURUDI, NDEFU LAKINI HAKIKA

Mashahidi zaidi ya 24,000, thabiti katika imani, hawakutikiswa na tarehe yo yote. Na bado, ile njia ya kurudi kwenye kilele kipya cha wahubiri ingechukua miaka minane mirefu nacho hakikufikiwa mpaka Agosti 1983.

Sasa hakukuwa kuruka-ruka kuingia ndani ya ukweli kwa hisi za moyoni tu, na wale waliokuwa wakibatizwa walikuwa wakifanya wakfu wakiwa wanaelewa. Wengi waliokuwa wamekuwa wasiotenda walianza kurudi, wakitambua kwamba kwa kweli hapakuwa na mahali pengine pa kwenda. Wengi walijifunza kwa njia ngumu kwamba ukweli unapatikana mahali pamoja tu.

JUMBA LA KUSANYIKO LA KWANZA KATIKA MASHARIKI

Kufikia katikati ya muda wa miaka ya tangu 1970, magumu yalizuka katika kupata mahali penye kufaa kufanyia makusanyiko ya mzunguko na matukio ya pekee. Ukiwa ufumbuzi, akina ndugu waliamua kujenga Jumba la Kusanyiko kwa mikono yao wenyewe. Muundo na ujenzi walo ulikuwa mwepesi lakini wenye kutosha kufanya kusanyiko liwe lenye kustarehesha kwa wote katika hadhirina. Kwa hiyo, Jumba la Kusanyiko la kwanza la Mashahidi wa Yehova katika Mashariki liliwekwa wakfu katika Aprili 1976 katika Pusan, Korea. Kufikia leo hii, Korea ina Majumba ya Kusanyiko saba yakitumikia asilimia ipatayo 75 ya wahubiri wote.

MAREKEBISHO YA UTANGAZAJI WA MAGAZETI

Masharti mapya ya serikali katika 1980 yalilazimisha tawi lifanye marekebisho katika utangazaji wa magazeti Mnara wa Mlinzi na Amkeni! Kwa hiyo ikiwa tengenezo fulani lingetangaza magazeti mawili, ni moja tu lingeweza kuruhusiwa kuendelea. Katika Novemba 1980 gazeti Amkeni! lilikuwa moja la magazeti 67 ya mara kwa mara yaliyofutwa na serikali. Kila jitihada ilifanywa na tawi la Korea kubadili uamuzi huo lakini bila kufaulu.

Kisha, baada ya miezi miwili, ujumbe ukaja bila kutazamiwa kutoka kwa wenye mamlaka kwamba wangeruhusu nyongeza kwa Mnara wa Mlinzi itangazwe. Roho takatifu ilikuwa ikifanya kazi! Ile nyongeza ingekuwa na tarehe ile ile kama Mnara wa Mlinzi, ya kwanza na ya kumi na tano. Utaratibu huu ungali unafuatwa.

WAMISIONARI WAZUIWA KUINGIA

Wamisionari wa nchi za kigeni hawahitajiwi tena kufanya kazi katika shamba la Korea, kwa kuwa mapainia wenyeji wa Korea wanaweza kuangalia vya kutosha kazi hii. Lakini wamisionari wangali wanahitajiwa kwa kuzoeza na kujenga akina ndugu kiroho. Ikiwa na jambo hili akilini, Sosaiti iliwagawia wamisionari watano zaidi kwenda Korea katika vuli ya 1977. Kwa mshangao wa tawi, hawangeweza kupata viza. Wale wamisionari 17 waliokuwa tayari wanatumikia katika nchi wangeweza kubaki, lakini hakuna wamisionari wapya wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi wangeruhusiwa. Zaidi ya hilo, wale wamisionari waliopo, hawangepewa ruhusa ya kuingia nchini tena ikiwa wangeondoka nchini.

Hata hivyo, tangu mwishoni-mwishoni mwa 1987, wamisionari wamethamini sana vile ambavyo wenye mamlaka wamewafikiria kwa kuwapa ruhusa ya kuingia tena nchini kwa njia ile ya kawaida.

MRADI MKUBWA MNO

Katika kiangazi cha 1979, Baraza Linaloongoza lililipa tawi ruhusa ya kuanza kutafuta mahali pa tawi jipya. Baada ya utafutaji wa mwaka mmoja, kisehemu cha hekta 3.6 cha shamba na ardhi yenye msitu kilipatikana kilometa zapata 67 kusini mwa Seoul, katika Kyonggi Do, Ansung Kun, Kongdo Myun. Hiyo ingeliweka tawi katika mazingira yasiyo na uchafuzi.

Mradi huo wa upanuzi ulikuwa wa kadiri kubwa mno unapolinganishwa na miradi ya wakati uliopita. Sasa tawi lingekuwa likichukua kazi ya kuchapa magazeti na pia kujitayarishia uchapaji wa vitabu wakati ujao. Mwako wa msisimuko ulienea katika Mei 8, 1982, wakati yale majengo yaliyomalizwa yalipowekwa wakfu, na Ndugu Franz na Barry kutoka makao makuu ya ulimwengu wakawa hapo ili kutoa hotuba za pekee.

Kwa sababu ya msaada kutoka kwa akina ndugu katika United States na Japani, pamoja na ushirikiano kutoka kwa kampuni ya kibiashara ya uchapaji ya mahali pale, sasa tawi lina matbaa yalo lenyewe. Kwa wakati mfupi sana uchapaji wa kila toleo la yale magazeti uliongezeka kufikia karibu 200,000, ukizipa mashine zote shughuli nyingi siku yote nzima.

Miaka mitatu baada ya tawi kuhamishiwa Kongdo, Ndugu Albert Schroeder wa Baraza Linaloongoza, akitumikia kama mwangalizi wa eneo la dunia, aliiweka wakfu nyongeza ya mali hiyo katika Mei 1985. Nyongeza hiyo iliongeza maradufu nafasi ya sakafu kufikia chini tu ya meta za mraba 9,290. Wahubiri waliongezeka kutoka 30,000 katika 1982 kufika zaidi ya 39,600 katika 1985. Ukuzi ulioje!

Kwa kuwa Seoul si mji mkuu tu wa Korea Kusini bali pia kitovu cha biashara, lilionekana kuwa jambo lenye kuhitajiwa kabisa kwamba ile afisi ya shirika iliyoandikishwa ibaki kule. Jengo jipya zuri sana lenye afisi kwa ajili ya tawi, Jumba la Ufalme, na chumba chenye nafasi kubwa vya kutosha kwa ajili ya depo ya vitabu lilijengwa katika Seoul na kuwekwa wakfu Desemba 20, 1986. Washiriki wanne wa jamaa ya Betheli wanaishi na kufanya kazi humo.

MATBAA-VIKUTO YENYE MWENDO WA KASI INAVUMA

Karibu miaka 600 iliyopita Wakorea waliendeleza tekinolojia ya upigaji chapa walipobuni kwa mara ya kwanza herufi za metali zinazoweza kuondolewa na kutumiwa upya. Leo, Mashahidi Wakorea wanatumia tekinolojia ya upigaji chapa wa kisasa kusogeza mbele masilahi ya Ufalme. Wao hawana tatizo la kutokeza magazeti na vitabu vya kutosha, kwa kuwa kazi yao inayotangulia upigaji chapa inatiririka kutoka kwa vifaa ambavyo vinasaidiwa na kompyuta na mashine mpya ya upigaji chapa, vikuto-ofseti ya Mitsubishi, ambayo kwa dakika moja inatoa magazeti 500 ya kurasa 32 yakiwa na rangi kamili. Wazo la kwanza la kupata mashine kubwa hivyo ya upigaji chapa lilianza katika kiangazi cha 1983 wakati Ndugu Lloyd Barry, akitumikia akiwa mwangalizi wa eneo la dunia, alipoona hali ya kulemewa na kazi ya kiwanda cha kupigia chapa.

Wakati huo kiwanda kilikuwa kimejaa pomoni. Haikuwako nafasi yo yote ya kuweka sakafuni mashine ya upigaji chapa ya tani 132.1, yenye urefu wa meta 25.9. Hilo lilimaanisha jengo jingine, mpanuo wa pili katika Kongdo katika muda wa miaka minne tu. Kufikia wakati huu magazeti ya Kikorea yalikuwa yamekuwa miezi mitatu nyuma ya chapa za Kiingereza, kwa hiyo tazamio la kuchapa magazeti sawia na Kiingereza lilifanya kazi ile yote istahili.

Ingawa hivyo, kuingiza nchini mashine ya upigaji chapa kama hiyo kulizungukwa na matatizo mengi. Ongozi la serikali liliweka sharti kwamba pendekezo lilipasa lipokewe kutoka kwa serikali kabla ruhusa haijatolewa kuiingiza nchini. Hiyo ilikuwa ni kama haiwezekani. Hata hivyo, katika kiangazi cha 1985 kizuizi hicho kiliondolewa, na akina ndugu kwenye tawi wakapata mara hiyo leseni ya kuingiza nchini. Katika muda wa majuma sita baada ya kupata ruhusa hiyo, sheria ilibadilika ikarudia tena hali ya zamani, ikitaka pendekezo. Roho takatifu ilikuwa imefungua njia; akina ndugu walitenda kwa haraka. Hivyo, leo katika tawi ile mashine ya upigaji chapa inavuma ili mikono ya wahubiri iendelee kujazwa vitabu vya kutumiwa katika kutoa ushuhuda.

KUTAZAMA MBELE

Kwa watu wa nchi hiyo, Korea inajulikana kuwa Chosŏn, “nchi ya utulivu wa asubuhi.” Miaka mingi iliyopita ndugu wa Korea walitaka kujua wangekuja kuwezaje kufikia watu wote katika nchi yao wakiwa na ujumbe wa Ufalme na ni wangapi wa watu hao ambao Yehova angechagua wawe “kondoo” zake.—Mt. 25:32.

Leo kuna asilimia 7 tu ya eneo asilogawiwa mtu, na karibu lote hilo linashughulikiwa na wahubiri katika ile miezi ya kiangazi. Maeneo katika miji mara nyingi yanaenezwa zaidi ya mara moja kwa mwezi. Kwa kuwa zaidi ya robo moja ya wale wahubiri zaidi ya 48,000 wamo katika kazi ya painia wa kawaida kuongezea wale waliomo katika kazi ya painia msaidizi kila mwezi, watu wa Korea wanajua Mashahidi wa Yehova ni akina nani. Kweli kweli, Yehova amechagua “kondoo” wake pia miongoni mwa Wakorea.

Kama mwandikaji mmoja wa Biblia alivyolieleza jambo hilo: “Asubuhi panda mbegu zako, wala jioni usiuzuie mkono wako. Kwa maana wewe hujui ni zipi zitakazofanikiwa, kama ni hii au hii, au kama zote zitafaa sawasawa.” Mbegu zimepandwa na mavuno yamekuwa mazuri. Wakati ujao ni mwangavu. Ni roho ya Yehova tu ingeweza kufanya hilo litukie hapa katika Korea.—Mhu. 11:6.

[Maelezo ya Chini]

a Katika Korea jina la jamaa sikuzote linatangulizwa katika kusema na kuandika.

b Wanawake walioolewa huendelea kutumia jina la jamaa yao.

c Baada ya miaka 36 ya kufanya utumishi wa misionari kwa uaminifu katika Korea, Earlene Steele alikufa katika 1985, kufuatia ugonjwa ulioendelea kwa muda mrefu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 193]

Katika Mei 23, 1987, nyongeza ya orofa tatu kwenye vifaa vya tawi katika Kongdo iliwekwa wakfu na Milton G. Henschel wa Baraza Linaloongoza. Lile jengo jipya la kiwanda linaipa makao matbaa-vikuto-ofseti mpya ya tani 132.1, yenye kutokeza picha zenye rangi nne. Ndugu Henschel alihutubia watu 2,060 waliokusanyika mahali penye tawi. Hii ni nyongeza kubwa ya pili ya tawi tangu 1982

[Picha]

Jengo la kwanza kabisa la makao liliwekwa wakfu 1982

[Picha]

Jengo la afisi; kiwanda (sehemu yenye rangi ya krimu ikiwa kati); na, upande wa kulia, jengo jipya la makao lililowekwa wakfu 1985

[Picha]

Nyongeza ya kiwanda, upande wa kulia, iliwekwa wakfu 1987

[Picha]

Mchoro wa mrasimu ramani za ujenzi kuonyesha jinsi jengo la tawi la Korea lilivyo

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 136]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KOREA

CHINA

URUSI

Bahari Manjano

Pyongyang

Sariwon

UKANDA ULIOONDOLEWA MAJESHI

SEOUL

Inchon

Mto Han

Ansung–Kongdo

Pyungtaek

Taejon

Kunsan

Taegu

Chonju

Pusan

Kwangju

Cheju

Bahari ya Japani

JAPANI

[Picha katika ukurasa wa 143]

Lee Shi-chong, kolpota ambaye alisafiri kwa baiskeli kupitia maeneo ya mashambani katika muda wa mapema wa kuanzia 1930 kueneza ujumbe wa Ufalme

[Picha katika ukurasa wa 146]

Ok Ung-doo, Ok Ryei-joon, na Ok Ji-joon (kushoto kwenda kulia) walielekeana na majaribu makali wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili

[Picha katika ukurasa wa 153]

Choi Sung-kyu alitaabika vikali mpaka kifo katika 1941 kwa sababu ya itikadi zake, lakini imani yake ilikuwa kitia-moyo kikubwa kwa ndugu zake

[Picha katika ukurasa wa 157]

Wamisionari na jamaa ya tawi mbele ya tawi lililopanuliwa katika Seoul. Nyongeza upande wa kulia iliwekwa wakfu katika 1975

[Picha katika ukurasa wa 159]

Earlene na Don Steele, wamisionari wa kwanza wa Mnara wa Mlinzi katika Korea, Agosti 1949

[Picha katika ukurasa wa 175]

Akina ndugu na dada wakaribisha Nathan H. Knorr, ambaye wakati huo alikuwa ndiye msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, baada ya ndege yake kutua Aprili 27, 1956, kwenye Uwanja wa ndege wa Yoido, Korea. Walioanda-mana naye ni Don Adams na Lloyd Barry

[Picha katika ukurasa wa 178]

Katika Januari 1957 wakati wa mkusanyiko uliofanywa katika Seoul, Frederick W. Franz, akiwa sasa ndiye msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, aitikia ukaribishaji wa wajumbe kwa mchanganyiko wa nyimbo za Ufalme kwa kutumia kinanda chake cha mdomo

[Picha katika ukurasa wa 180]

Durand na Rachel Norbom na Liz na Milton Hamilton wamisionari wanne ambao wamekuwa katika Korea (kushoto) kwa zaidi ya miaka 20 na (kulia) kwa zaidi ya miaka 33

[Picha katika ukurasa wa 181]

Wamisionari wanaotumikia katika kazi ya mwangalizi asafiriye. Kushoto kwenda kulia: Susan na John Wentworth, Geline Jumuad, Josef Breitfuss, na Perry Jumuad

[Picha katika ukurasa wa 183]

Kim (Phillips) Kyung-hi, Evalyn Park (Emerson), na Liz na Milton Hamilton walianzisha kao la wamisionari katika Pusan, 1955

Keith na Evelyn Kennedy, Karl Emerson, Druzilla Craig (Youngberg), Elaine Scheidt (Ness), Norris Peters, na Earlene na Don Steele kwenye ngazi za tawi na kao la wamisionari lililotiwa makovu na marisawa katika Seoul, 1957

[Picha katika ukurasa wa 191]

Akina ndugu hawa wa Halmashauri ya Tawi wametumikia wastani wa miaka 37 katika utumishi wa wakati wote. Safu ya mbele, kushoto kwenda kulia: Chae Soo-wan, Don Steele (mratibu wa Halmashauri ya Tawi), na Chun Young-soon. Safu ya nyuma, kushoto kwenda kulia: Park Ii-kyun, Milton Hamilton, na Park Chong-il

[Picha katika ukurasa wa 194]

Wafanya kazi wa tawi la Japani na Korea walifanya kazi na kupata mazoezi pamoja baada ya ile mashine ya upigaji chapa wa rangi nne, yenye urefu wa meta 28, kuwekwa katika nyongeza ya tawi katika Kongdo mwaka 1986

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki