Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb88 kur. 198-252
  • Kosta Rika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kosta Rika
  • 1988 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • UKWELI WA BIBLIA WAVUMBULIWA
  • UJUMBE WAENEA
  • MIKUSANYIKO YA MAPEMA
  • MAMBO YA PEKEE
  • MBEGU ZA FARAKA ZAPANDWA
  • UVUTANO MBAYA SANA
  • ZIARA YA KWANZA KUTOKA MAKAO MAKUU
  • WENGINE WALIKENGEUSHWA
  • KIJIA CHA KURUDIA UMOJA
  • KAZI YAWAKA MOTO TENA
  • ENEO JIPYA LAFUNGUKA
  • PAINIA WA KWANZA WA KIHISPANIA
  • KUNDI LA SAN JOSÉ
  • WAHITIMU WA GILEADI WAONGEZA UTHABITI
  • TAWI LAANZISHWA
  • UMOJA KATIKA SAN JOSÉ
  • MTUMISHI KWA AKINA NDUGU
  • MWANGALIZI WA MZUNGUKO WA KWANZA MWENYEJI
  • KAZI YA PAINIA YAENEZA UJUMBE
  • AKINA DADA WAFANYA UPAINIA
  • FARASI NA YULE KINYOZI
  • NDOA NA MICHEZO YA BAHATI NASIBU
  • “MAVUMBI KWA MAVUMBI”
  • MAKUSANYIKO MASHAMBANI
  • KUTOKA KUWA WAVUVI WA SAMAKI KUWA WAVUVI WA WATU
  • JUMBA LA KUSANYIKO LA KWANZA
  • JUMBA LA UFALME LATEKETEZWA
  • TENDO LA WATU WENYE GHASIA LAZUIWA
  • VITA YA WENYEWE KWA WENYEWE
  • USAFIRI KWA KUTUMIA GARI-NYUMBU
  • MABADILIKO KATIKA TAWI
  • KIAMSHI CHA KUPANUA
  • MATATIZO JUU YA KUSALIMU BENDERA
  • VOLKANO IRAZÚ NA ARENALI ZAAMKA
  • KUPUNGUZA MWENDO KATIKA ILE MIAKA YA 1960
  • WAMISIONARI ZAIDI WACHOCHEA ILE KAZI
  • TETEMEKO LA DUNIA KATIKA MANAGUA
  • UMOJA WA JAMAA WALETA FANIKIO
  • ROHO YA UMISIONARI HUAMBUKIA
  • KOSTA RIKA YASHIRIKI WAMISIONARI WAYO NA NCHI NYINGINEZO
  • KUTOKA KONDAKTA WA GARI-MOSHI KUWA MWANGALIZI WA MZUNGUKO
  • UKAMILIFU WATAHINIWA NA LILE SUALA LA DAMU
  • “MWANAMUME ATAKWA”
  • JITIHADA ZAIDI ZA KUFIKIA
  • “WENYE UMOJA KATIKA IBADA”
  • WAMISIONARI WASIOTARAJIWA
  • USHUHUDA KUPITIA IDHAA YA HABARI
  • JAMAA YA BETHELI YAONGEZEKA
  • SABABU GANI BADILIKO?
  • VIFAA VIPYA VYA TAWI
  • TAREHE IKAWEKWA
  • LILILOTUKIA KWA WALE WASICHANA WA MIAKA YA 1940 NA KITU
  • PWANI YENYE UTAJIRI KWELI KWELI!
1988 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb88 kur. 198-252

Kosta Rika

KARIBU karne tano zilizopita, mwanamume mrefu, mwenye maungo aliyekuwa na pua iliyopindika alisimama kwenye sitaha ya meli yake, akitazama sana pwani ya Amerika ya Kati katika kutafuta kipito cha kwenda Bahari Kuu ya Hindi. Yeye hakuipata. Hata hivyo, alichogundua katika 1502 ni ile nchi iliyopewa jina la Kosta Rika, kumaanisha “Pwani Yenye Utajiri.”

Huyo mwanamume alikuwa Christopher Columbus, Mwitalia aliyekuwa akisafiri kwa meli chini ya bendera ya Hispania akiwa katika safari yake ya nne na ya mwisho ya kwenda kwenye ule Ulimwengu Mpya. Yeye pamoja na wale wavumbua-nchi wengine pia walitumaini kupata dhahabu katika Kosta Rika. Badala yake, lile eneo lilitoa madini yenye thamani ndogo sana. Hata hivyo, bila Columbus kujua, utajiri ulio mkubwa zaidi sana ungekuwa watu wa nchi hiyo, hasa wale waliokuwa na sifa ambazo huwafanya wawe wenye thamani kubwa kwa Yehova.

Nchi ambayo Columbus alivumbua ilikuwa tayari inakaliwa na Wahindi, ambao walikuwa wamelowea kwenye shingo hii ya nchi inayounganisha Amerika Kaskazini na Kusini, angalau kufikia mwaka 1,000. Nchi hiyo ikoje leo?

Bahari Kuu ya Atlantiki (Bahari ya Karibea) ikiwa upande wayo wa mashariki na ile ya Pasifiki upande wayo wa magharibi, Kosta Rika ina mstari wa safu-safu za milima mirefu yenye mawe-mawe unaotandaa kutoka mpaka wa Nikaragua upande wa kaskazini hadi kwenye mpaka wa Panama upande wa kusini-mashariki. Baadhi ya vile vilele virefu zaidi sana ni volkano zenye kutenda. Kwenye miiniko ya chini zaidi kando-kando ya mpaka wa pwani, ambako hali ya hewa ni yenye joto, misitu ya kitropiki husitawi. Wengi wa idadi ya watu wamelowea kwenye sehemu tambarare zilizo juu, ambazo hali ya hewa ni baridi kidogo kuuzunguka mji mkuu na ulio mkubwa zaidi, San José, ambako miti ya kahawa hufunika pande za vilima vinavyouzunguka mji.

Leo, idadi ya watu wa nchi hiyo inayokadiriwa kuwa 2,600,000, asilimia 97 ni machotara na weupe, hasa wa asili ya Kihispania, kukiwa na idadi ya Wahindi wapatao 5,000. Hispania ndiyo lugha rasmi, nayo dini ya kiserikali ni Ukatoliki wa Roma, ingawa dini zisizo za Kikatoliki zipo pia bila kizuizi.

Miaka ya mwisho-mwisho ya muda wa tangu 1800 iliona wahamiaji wengi wakiwasili katika Kosta Rika, kutoka Jamaika, Trinidad, na Barbados. Watu hawa wazoevu wa kazi walikuja kufanya kazi katika mashamba ya migomba ya ndizi yenye kusitawi ya United Fruit Company kando-kando ya Pwani ya Atlantiki. Bila shaka, pamoja nao, zikaja desturi na dini zao za Kiprotestanti na Kikatoliki. Watu hawa wenye nia thabiti na ambao ni wafanya kazi wenye bidii, kwa sehemu kubwa walikuwa wapenda Biblia.

UKWELI WA BIBLIA WAVUMBULIWA

Hivyo, kabla ya mwanzo wa karne ya ishirini, uvumbuzi mwingine wa maana sana zaidi ya ule wa Columbus ulifanywa katika Kosta Rika—uvumbuzi wa Biblia. Jinsi ujumbe wa Ufalme ulivyoletwa kwa mara ya kwanza katika Kosta Rika ni fumbo. Lakini Mashahidi wa Yehova katika Jamaika wanaripoti kwamba Wajamaika wawili waliokuwa wamehamia Kosta Rika, H. P. Clarke na Louis Facey, waliukuta ukweli kule na waliporudi, wakapeleka zile habari njema kwenye nchi ya kwao Jamaika.

Anna Reynolds, mwanafunzi wa Biblia mwenye hamu nyingi kutoka Jamaika, alitua kwenye bara la Kosta Rika katika 1904. Muda mfupi baada ya kuwasili kwake, Sosaiti ilituma msafiri mmoja, Ndugu Condell, ajiunge naye katika kazi ya kolpota, au kazi ya kuhubiri wakati wote. Mara tu Ndugu Condell aliporudi Jamaika na kuripoti juu ya kupendezwa kulikopatikana, iliamuliwa kwamba kolpota mwingine, Frank Hudson, yapasa atumwe Kosta Rika. Yeye aliwasili katika 1906 na akaamsha kupendezwa kwingi miongoni mwa idadi ya watu weusi wenye kusema Kiingereza. Toleo la Mnara wa Mlinzi la Januari 1, 1907 liliripoti kwamba, katika pindi ya 1906, Kosta Rika ilikuwa udongo wenye rutuba kwa maangusho ya vitabu vya Biblia.

UJUMBE WAENEA

Kufikia mwaka 1914, ukweli ulikuwa umepenya ndani ya sehemu zote za eneo la pwani ya Atlantiki. Huo ulikuwa ndio mwaka ambao Henry Adamson alipanga kitengenezo eklezia, au kundi la kwanza, katika Guácimo, umbali upatao kilometa 80 kutoka Puerto Limón, kile kitovu cha kibiashara cha sehemu hii yenye usitawi wa kilimo. Kufikia wakati huo ule ujumbe hata ulikuwa umefika kwenye mji mkuu wa San José, uliokuwa zaidi ya kilometa 160 kutoka Puerto Limón. Angalau ndugu wawili wenye kusema Kiingereza waliishi kule, lakini kwa kuwa San José ulikuwa na idadi ya watu wenye kusema Kihispania na vichapo vilikuwa katika Kiingereza, maendeleo madogo sana yalifanywa kwa idadi fulani ya miaka. Ingawa mikutano ilifanyiwa katika nyumba za faragha, haikutangazwa.

Hata hivyo, kazi ilikua katika sehemu nyingine za nchi kwa kadiri ya kwamba ikawa lazima kuweka rasmi ndugu mwenyeji awe msafiri (mwangalizi wa mzunguko) ili atembelee akina ndugu katika sehemu zote za Kosta Rika, kutia na San José. Victor Samuels akachaguliwa.

MIKUSANYIKO YA MAPEMA

Katika mwaka 1914 mkusanyiko mmoja ulifanywa katika mji wa Puerto Limón, ambao katika huo 11 walibatizwa. Karibu na wakati huo William na Claudia Goodin, Henry na Matilde Steele, akina Wilson, na akina Williams wote walibatizwa. Watoto, wajukuu, na vitukuu vya wafanyi kazi hao wa mapema wana sehemu katika kazi ya kutoa ushuhuda leo katika Kosta Rika. Lakini zaidi ya hayo ni baadaye.

Kwenye hii mikusanyiko ya mapema, Sosaiti haikuandaa mihtasari ya habari. Kwa hiyo wahutubu waliogawiwa walichagua habari zao wenyewe na kutayarisha mihtasari yao wenyewe baadhi yao hata wakisema bila habari zilizoandikwa. Fedha na vyakula vilichangwa kwa ukarimu kwa ajili ya milo, ambayo ilitolewa bure kwenye kao la mmoja wa akina ndugu. Mchuzi wa kuku uliokolezwa sana, kuambatana na wali na njegere zilizopikwa kwa maziwa ya nazi, na ndizi zilizoiva zikiwa zimekaangwa zilikuwa za lazima katika kila pindi!

Kwenye mwisho wa mikusanyiko, ilikuwa desturi kusherehekea kilichojulikana kuwa karamu za upendo, ambazo katika hizo akina ndugu wangeimba nyimbo za kidini na kupitisha biskuti za soda kuzunguka wote waliohudhuria. Zile nyimbo ziliimbwa katika sehemu nne zenye upatani kwa sauti aali za melodia.

MAMBO YA PEKEE

Wakijivika mavazi meupe, wale akina ndugu walisherehekea, kimakini Ukumbusho wa kila mwaka wa kifo cha Kristo. Aghalabu watoto hawakualikwa, wasije wakakatiza na kuondosha fikira kwenye uzito wa chakula kile. Wote waliishiriki mifano ya mkate na divai, na baaaye wangeondoka kwenda kila mmoja kwenye kao lake bila kusemezana hata neno moja.

Ubatizo ulipangwa hasa kabla tu ya wakati wa Ukumbusho. Akina ndugu na dada walitiwa moyo wavalie suti na mavazi meupe kwa ajili ya pindi hiyo. Ili kuepuka watazamaji wenye udadisi, wao wangeamka mapema, kabla ya mapambazuko na kufika kwenye ufuo wa bahari na kumaliza sherehe za ubatizo kabla ya majirani kung’amua lililokuwa limetukia. Huku wenye kubatizwa wakizamishwa ndani ya bahari, wale wengine wangepatanisha kwa nyimbo.

Hotuba za watu wote zilikuwa kama hotuba za bustanini. Mashahidi wote walikuwa wakikusanyika mahali palipotangulia kupangwa huko nje, naye mhutubu alikuwa akitoa hotuba yake ya Biblia kwa wale waliokuwa wakisimama au kuketi kumzunguka katika kikao cha nusu-duara. Watu wa nje pia walihudhuria na wakajiunga nao wakati kuimba kulipoanza.

Jina moja lililotumiwa kuhusu akina ndugu lilikuwa Kanisa la Watu Wazee kwa sababu hakuna jitihada au ni jitihada ndogo tu zilizofanywa kusaidia watoto wao kiroho, na walio wengi wa wale waliokuwa wa tengenezo walikuwa wenye umri mkubwa. Baadaye, akina ndugu walipanga shule ya Jumapili yao wenyewe kwa ajili ya watoto wao, na hatimaye wakang’amua kwamba kuzoeza watoto lilikuwa daraka la wazazi wenyewe. Lakini Matilde Steele tayari alithamini uhitaji huo. Josephine, mtoto wa saba wa Matilde, alizaliwa 1918. Wakati Josephine alipokuwa na umri wa siku 40 tu, mama yake alimpeleka kwenye kusanyiko katika Kahuita, mji uliokuwa kwenye ufuo wa bahari kusini mwa Puerto Limón. Halikuwa jambo lenye hatari ndogo kusafiri siku nzima kwa gari-moshi, merikebu, na nyumbu katika hali ya hewa yenye joto na jasho. Safari hiyo ngumu haikumdhuru Josephine mdogo. Akiwa mwenye umri wa miaka 17 yeye alibatizwa, na anaendelea kwa uaminifu kumtumikia Yehova pamoja na jamaa yake.

MBEGU ZA FARAKA ZAPANDWA

Tengenezo lilipokuwa lingali changa, Shetani alianza kupanda fitina miongoni mwa akina ndugu kwa mbegu za husuda, kiburi, wivu, na ubinafsi wa kujitakia makuu. Ile roho ya ushindani ilidhihirika wakati watu mbalimbali waliposhindania vyeo vya ukubwa katika makundi. Kwa kuwa yaliongozwa kidemokrasi, uchaguzi ulifanywa pindi kwa pindi, na wazee waliingizwa katika vyeo vyao kwa kura, kwa kuinuliwa mikono na walio wengi. Akina ndugu wenye kujitakia makuu waliodhani walikuwa na ufahamu mzuri wa ukweli kuliko wale waliotiwa katika vyeo kwa kura walijaribu kudhoofisha uhakika wa kundi katika wale ndugu waliokuwa katika uangalizi. Walifanyaje hilo? Kwa kuzusha maswali na maswali ya kupinga wakati wa mikutano. Akina ndugu waligawanyika, na yakiwa matokeo, vikundi viwili mbalimbali vya washiriki wa kundi vilianza kukutana mahali tofauti-tofauti katika Puerto Limón.

UVUTANO MBAYA SANA

Matata zaidi yalikaribia kuangukia kikundi hiki kidogo kilichogawanyika cha Wakristo wakati msimamizi wa kwanza wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, Charles T. Russell, alipokufa katika 1916. Kwenye makao makuu ya ulimwengu katika Brooklyn, New York, kulikuwako hila ya kiibilisi iliyofanywa na akina ndugu wenye ubinafsi ya kupokonya usimamizi wa Sosaiti kutoka kwa yule msimamizi aliyefuata, Joseph F. Rutherford, na wengine waliowekwa rasmi. Lakini Yehova hakuruhusu tengenezo lake liangukie mikononi mwa hao wasio waaminifu.

Kiongozi mmoja wa huo upinzani alikuwa Paul Johnson aliyeitikadi, kinyume na elezo la Sosaiti, kwamba ukombozi wa Yesu ungetumiwa pia kwa ajili ya Adamu na Hawa. Yeye aliandika barua na kupelekea akina ndugu katika Kosta Rika mambo yake aliyoyaandika, akiwaambia wasimuunge mkono Ndugu Rutherford. Watu wachache mmoja mmoja walipendelea mafundisho ya Johnson kuliko mafundisho ya Biblia na wakajiondoa wenyewe kutoka kwenye tengenezo.

ZIARA YA KWANZA KUTOKA MAKAO MAKUU

Katika 1917 Kosta Rika ilipendelewa kuwa na ziara yayo ya kwanza iliyofanywa na mjumbe Walter Bundy, akiambatana na mkeye kutoka makao makuu ya Sosaiti katika Brooklyn. Lakini ni kwa sababu gani Sosaiti ingegharimiwa hata itume mjumbe mbali huko Kosta Rika? Basi, idadi ya wanafunzi wa Biblia ilikuwa inakua. Kufikia 1918 walikuwako 73, jambo lililomaanisha kwamba Kosta Rika ilikuwa na idadi ya nne iliyo kubwa zaidi sana ya Mashahidi kati ya nchi zote katika ulimwengu. Ni Visiwa vya Uingereza, United States, na Australia tu zilizoizidi. Idadi ya watu wa Kosta Rika wakati huo ilikuwa chini ya nusu milioni.

WENGINE WALIKENGEUSHWA

Shetani alijishughulisha tena katika jitihada zake za kukomesha ukweli akajaribu kuvuta kando fikira za akina ndugu kutoka kusudi lao kuu la kutegemeza jina la Yehova. Tengenezo jipya lenye kujulikana kuwa Universal Negro Improvement Association (UNIA) lilitokea miongoni mwa watu weusi katika ukanda wa Atlantiki.

Kusudi lalo lilikuwa nini? Kama vile jina linavyodokeza, lililenga kuleta maendeleo katika hali ya watu weusi. Mojapo kampeni zalo iliitwa harakati ya Kurudi Afrika na ilionwa na idadi ya watu weusi kuwa kitu kinachofanana na kurudi kwa Kiyahudi katika Palestina.

Akina ndugu hawakuonyesha kupendezwa tu na tengenezo hili bali walifikia hatua ya kutumia vibaya maandiko fulani ya Biblia kuunga mkono malengo yalo. Tokeo likawa nini? Baadhi ya akina ndugu walikengeushwa kutoka kazi yao ya kuhubiri habari njema za Ufalme wa Mungu kuwa utatuzi wa matatizo ya mwanadamu. Hata yule msafiri Victor Samuels alifanywa ayumbe-yumbe. Yeye aliwekwa rasmi awe kasisi wa UNIA naye alikuwa akihubiri kwenye mikutano yao badala ya kwenye kundi. Hakuna shaka lo lote juu ya matokeo yenye kudhuru ambayo jambo hili lililetea akina ndugu.

Wapata mwaka 1924, Victor Samuels alisafiri kwenda Afrika kusaidia watu wa Afrika. Katika barua moja ambayo alimpelekea mmoja wa akina ndugu katika Kosta Rika kutoka Lagos, Naijeria, yeye alisimulia kwamba alikuwa ameangusha nakala 2,500 za kitabu Harp of God. Utangazaji ulio mkubwa zaidi ulipewa kwa ujumbe wa Ufalme katika Naijeria likiwa tokeo.

KIJIA CHA KURUDIA UMOJA

Baada ya Victor Samuels kuondoka Kosta Rika, Henry Adamson, kutoka lile kundi la kwanza kabisa katika Guácimo, aliwekwa rasmi na Sosaiti katika 1924 kuwa msafiri na kusimamia kazi. Baadhi ya akina ndugu katika Puerto Limón hawakupenda njia ambayo Ndugu Adamson alishughulikia mambo, kwa hiyo waliasi. Yapata miaka miwili baadaye, Sosaiti ilituma George Young mjumbe mwingine kutoka Brooklyn. Mgawo wake: Kuunganisha akina ndugu katika Puerto Limón na kuanzisha tena kazi ya kuhubiri katika njia inayofaa. Kwanza, chini ya mwangaza wa taa, yeye alitoa mhadhara wa Biblia akitumia slaidi katika Jumba la Mawonyesho la Arrasty katika Puerto Limón. Baadaye, yeye alitembelea akina ndugu katika San José ili kuifanya kazi iendelee miongoni mwa watu wenye kusema Kihispania katika mji mkuu.

Jitihada ya Ndugu Young kuunganisha vile vikundi viwili katika Puerto Limón haikufanikiwa, kwa hiyo yeye akarudi United States. Ndugu Adamson alihamishwa kutoka Kosta Rika kwenda Panama katika ile sehemu ya mapema ya 1927. Baada ya kuondoka kwao, Sosaiti haikuweka rasmi msafiri mwingine kuangalia kazi mpaka miaka kumi baadaye, katika 1937. Lakini wale ndugu wa pale walibaki bila kuogopa. Wao waliendelea kuhubiri katika zile sehemu nne au tano ambako vikundi vilikutana, na walipeleka ripoti zao za utumishi wa shambani moja kwa moja kwa Sosaiti katika Brooklyn.

Katika 1931 sala za wale waaminifu kwa ajili ya umoja zilijibiwa wakati Sosaiti ilipopeleka barua kwenye makundi yote wakiwahimiza wale waliokuwa na upatani na Sosaiti wakubali lile jina jipya—Mashahidi wa Yehova. Azimio hilo lilitoa onyo la kifo cha kikundi chenye kuasi, kisicho na jina. Wakafa fo, fo, fo na ile migawanyiko ikakoma katika kundi la Puerto Limón. Kuwekwa rasmi kitheokrasi kwa watumishi katika 1938 kuliunganisha zaidi akina ndugu.

KAZI YAWAKA MOTO TENA

Kabla ya Ndugu Adamson kuondoka kwenda Panama, yeye alianzisha kikundi kimoja katika Ri̇́o Hondo, kijiji kidogo katika ukanda wa Atlantiki. Mmoja wa wale waliobatizwa katika Novemba 17, 1926, alikuwa Albert Ezra Pile. Yeye alikuwa amesikia juu ya ukweli kwa mara ya kwanza katika ile siku aliyowasili kutoka Barbados katika 1918 akiwa na umri wa miaka 29, lakini hakung’amua hata kidogo wakati huo kwamba yeye angetimiza sehemu kubwa katika historia ya Mashahidi wa Yehova katika miaka ijayo. Alipokuwa akienda kulala, Ezra alimwomba mkaribishaji wake kitu fulani cha kusoma naye akapewa lile buku la kwanza la Studies in the Scriptures. Usiku huo ile cheche ya ukweli wa Biblia iliwasha upendo wake kwa Yehova. Upesi yeye akawa painia na sasa akiwa na umri wa miaka 99 anashirikiana na Kundi la Siquirres. Lakini yeye alikuwaje na uvutano juu ya kazi ya kutoa ushuhuda?

Katika 1927 Ndugu Pile alihamia ule mji mdogo wa Siquirres, ambako alikutana na Frank Hudson, yule kolpota aliyekuwa amekuja katika nchi hii katika 1906 kuanzisha kazi. Lakini kufikia wakati huu bidii ya Ndugu Hudson katika utumishi ilikuwa imepoa kwa kuvunjika moyo. Kwa hiyo Ndugu Pile na Hudson waliamua kuungana pamoja na kuianza kazi tena katika njia iliyopangwa zaidi kitengenezo.

Mawingu ya vita yalipokuwa yakining’inia juu ya Ulaya katika 1937, Ndugu Pile aliogopa kwamba lile tisho la vita lingekatiza ugavi wa vitabu vya Kosta Rika vinavyokuja kutoka makao makuu. Kwa hiyo yeye aliandikia Brooklyn akajitolea kutunza akiba ya vitabu vya Sosaiti katika kao lake. Sosaiti ilikubali, navyo vitabu vikahamishwa kutoka Puerto Limón kupelekwa Siquirres. Ndugu Pile akawa mtumishi wa depo naye akawa akipeleka vitabu kwenye sehemu zote za mji ambako Mashahidi waliishi.

ENEO JIPYA LAFUNGUKA

Kufikia sasa sisi tumezungumzia tu yale matokeo yaliyotukia kwenye pwani ya Atlantiki miongoni mwa idadi ya watu wenye kusema Kiingereza. Lakini jitihada halisi ilikuwa haijafanywa ili kuwafikia kwa ujumbe wa Ufalme watu wasemao Kihispania katika sehemu hii ya nchi.

Siquirres ndiko shamba kubwa mno la lugha ya Kihispania lilifunguka katika ukanda wa Atlantiki wakati Florencio Pérez, Mnikaragua, aliposikia ukweli katika njia isiyo ya kawaida kutoka kwa Frank Hudson. Huo ulikuwa mwaka 1932. Sanamu moja iliyokuwa ya Ndugu Hudson ndiyo iliyoamsha hamu ya Florencio kwa ajili ya ukweli. Ndugu Hudson alikuwa amefanyiza kiolezo thabiti cha mfano wa ndoto ya Nebukadreza chenye kichwa cha dhahabu, kifua cha fedha, na miguu ya chuma. Yeye alizoea kuweka kiolezo hiki kwenye veranda ya nyumba yake, na wakati mpitaji ye yote aliposimama, yeye alikuwa akieleza maana yacho. Nyakati nyingine yeye alikuwa akiweka ubao wa kuandikia sokoni ili kueleza unabii wa Biblia kwa watu waliokusanyika.

Frank Hudson alisema Kihispania kidogo, na Florencio alisema Kiingereza kidogo sana. Ijapokuwa kizuizi hiki cha lugha, yeye alipendezwa na elezo la Hudson juu ya Biblia, hata akajifunza mwenyewe jinsi ya kusoma na kuandika.

Wakati Florencio aliposoma kijitabu Home and Happiness, yeye alisadikishwa kwamba huu ulikuwa ndio ukweli na akaandikia Sosaiti katika Brooklyn, akisema kwamba yeye alitaka kufanya kazi pamoja na Mashahidi wa Yehova. Sosaiti ilijibu kwa barua ya kitia-moyo na kupeleka Biblia ya Kihispania. Tangu wakati huo, yeye alianza kutumia wakati wake wote kueneza ujumbe wa Ufalme, akitumia vitabu vya Biblia kutoka kwa Ndugu Hudson. Mwishowe, katika 1938 Florencio alibatizwa kwenye kusanyiko moja katika Siquirres.

PAINIA WA KWANZA WA KIHISPANIA

Mwaka mmoja kabla Florencio Pérez hajabatizwa (ijapokuwa tayari yeye alikuwa amejiweka wakfu), alipelekea Sosaiti ombi la kuingia utumishi wa painia. Yeye aliwekwa rasmi katika Juni 1, 1937, hivyo akawa painia wa kwanza kuwekwa rasmi mwenye kusema Kihispania katika Kosta Rika. Mgawo wake wa kwanza ulikuwa idadi ya watu wasemao Kihispania wa ukanda wa Atlantiki. Pia yeye alipewa mgawo wa kufanya kazi pamoja na lile kundi dogo lenye kusema Kihispania la San José.

Ndugu Pérez alitumia njia nyingi kueneza ujumbe wa Ufalme. Nyakati nyingine yeye alikuwa akifunga vijitabu kwenye matawi ya miti kando ya vijia ambako wapitaji wangeweza kuvipata. Au yeye angeenda kwenye uwanja wa ndege katika San José na kuangusha vitabu kwa abiria waendao nchi za ng’ambo na kuwafanya waahidi watapitishia mtu mwingine vile vitabu. Akisafiri kwa miguu kupitia misitu mizito, yeye alikuwa akilala po pote usiku ulipomkuta, nyakati nyingine blanketi yake ikiwa ni nyota tu na kuliwa na umbu. Mara nyingi yeye alivunja kimya cha usiku kwa kucharaza gitaa yake aliyokuwa nayo daima. Roho yake ya kutembea huku na huku, ya kueneza evanjeli ilisafiri pamoja naye kwenda Nikaragua, ambako yeye aliendelea kufanya upainia kwa miaka mingi.

KUNDI LA SAN JOSÉ

Kundi lisemalo Kihispania katika San José lilikuwa limeundwaje? Tangu zile siku za vita ya kwanza ya ulimwengu, mikutano yenye kusema lugha ya Kiingereza ilikuwa imefanywa nyumbani mwa Ndugu Williams, ambaye alijifunza ukweli katika 1912 na baadaye akawa mwangalizi msimamizi. Hapo kwanza alikuwa amekuwa mhubiri wa kawaida katika kanisa la Kievanjeli ambako mke wake alicheza kinanda. Kwa kuwa kulikuwa watu wachache wasemao Kiingereza waliokuwa wakiishi katika mji mkuu katika wakati ule, ukuzi ulikuwa wa polepole.

Hata hivyo, wakati vitabu vya Kihispania vilipopatikana, kuhubiri kukawa rahisi zaidi. Kufikia 1931 kikundi cha watu 10 au 12 wasemao Kihispania kilikutana pamoja katika nyumba za faragha. Felipe Salmerón alikuwa mmoja wao. Yeye alitoa ushuhuda pia katika bandari Puntarenas ya Pwani ya Pasifiki. Mwishowe, baada ya miaka zaidi ya 30, ukweli ukawa umeenea toka pwani kwenda pwani.

Kuelekea mwisho wa 1941, Ndugu Pile alipelekwa San José kutoka Siquirres akachukue mahali pa Ndugu Williams kuwa mwangalizi. Lile kundi sasa lilikutania nyumbani mwa Flavio Romero, na Sosaiti ilikuwa ikiandikiana nao kupitia painia Florencio Pérez.

WAHITIMU WA GILEADI WAONGEZA UTHABITI

Alipokuwa akitoa ripoti yake kwa Sosaiti juu ya hali ya kundi katika San José, Ndugu Pile alipendekeza kwamba ndugu mmoja aliye imara katika njia ya Kitheokrasi apelekwe Kosta Rika kusimamia kazi. Akina ndugu hawakuwa na muda mrefu wa kungojea kwa sababu katika Desemba 23, 1943, Theodore Siebenlist na mkeye Hermena, kutoka darasa la kwanza la Gileadi, waliwasili. Kosta Rika ilikuwa mojapo nchi nne za kwanza katika ulimwengu kupokea wahitimu wa Gileadi.

Ndugu Siebenlist alikuwa na msingi imara wa tengenezo. Baba yake alibatizwa 1913, siku mbili baada ya Theodore kuzaliwa. Kao la wazazi wake lilitumiwa kwa ajili ya mikutano, naye alishiriki pamoja nao katika ugawaji wa trakti. Yeye alibatizwa kwenye ule mkusanyiko wa Washington, D.C., katika 1935. Kwenye mkusanyiko mmoja katika 1937, yeye alikutana na Hermena Deines nao wakafunga ndoa mwaka uliofuata.

Matokeo ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, ambayo ilikuwa ingali inapiganwa vikali katika Ulaya, yalihisiwa katika Kosta Rika. Kwa hiyo wakati akina Siebenlist walipowasili katika San José, ishara za ugumu wa kupata vitu zilionekana kila mahali. Wao walitafuta kwa mwezi mzima kabla ya kupata kao linalofaa katika ghorofa ya pili yenye chumba ambacho kingetumika kuwa Jumba la Ufalme. Lilikuwa mahali panapofaa hatua chache kutoka barabara kuu ya mji na hivyo pakawa mahali penye kujulikana. Kile chumba kiliendelea kutumiwa kikiwa Jumba la Ufalme mpaka 1956, wakati afisi ya tawi ilipojengwa ikiwa na Jumba la Ufalme karibu nayo.

TAWI LAANZISHWA

Yapata miezi mitatu baada ya wamisionari kuwasili, Nathan H. Knorr, msimamizi wa tatu wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, na mpambe wake, Milton Henschel wakazuru. Ulikuwa ndio wakati wa kwanza msimamizi wa Sosaiti kukanyaga Kosta Rika. Depo ya vitabu tayari ilikuwa imehamishwa kutoka Siquirres katika Januari 1944 kupelekwa San José, na sasa katika Machi, Ndugu Knorr akaanzisha afisi ya tawi. Hii ilikuwa hatua ya maana ya kutoa mwelekezo wa kusimamia kazi ya kutoa ushuhuda. Wakati wa ziara yake, Ndugu Knorr aliagiza kwamba kao kubwa zaidi la wamisionari litafutwe, kwa kuwa msaada zaidi ungewasili. Kao moja lilipatikana katika sehemu ya kaskazini-magharibi mwa San José.

Katika pindi ya miaka miwili iliyofuata, Charles na Lora Lea Palmer, Woodrow (“Woody”) Blackburn, Donald H. Burt, William Eugene Call, na Franklin na Emily Hardin, wote wahitimu wa Shule ya Gileadi, walijiunga na jamaa ya wamisionari. Lo! ni rundo la msaada mzuri kama nini! Donald Burt alikaa kwa muda mfupi tu, kwa kuwa alipewa mgawo mwingine kwenda Honduras na baadaye Peru, ambako yeye anatumikia sasa akiwa mratibu wa Halmashauri ya Tawi.

UMOJA KATIKA SAN JOSÉ

Mbali na kile kikundi kilichokuwa kimegawanyika hapo kwanza katika Puerto Limón, kingine kilikuwako katika San José. Ilitukiaje kwa kikundi kile katika San José? Ndugu Siebenlist alitia moyo kuwe na umoja. Shime yake ilikuwa, “Fanya inavyofaa, au usifanye kabisa.”

Ripoti ya Ndugu Siebenlist ya kila mwaka ya 1944 kwa Sosaiti iling’aa kwa maendeleo. Yeye aliandika: “Wale akina ndugu wa Kihispania katika Kosta Rika, wapatao 75 sasa, walikuwa wamegawanyika wakati sisi tuliwasili hapa katika Desemba na mpaka mwezi uliopita walikuwa wamedumisha Majumba ya Ufalme mawili katika San José. Mara tulipowasili, vile vikundi viwili vilialikwa viungane na kukutana kwa ukawaida katika Jumba lile lile. Kwenye mkutano wa kwanza vikundi vyote viwili vilikuwapo, wakiwa wapatao 30 jumla yao. Sasa, kwa neema ya Bwana, tengenezo la hapa linafanya kazi barabara, nacho kile kikundi kimekua kufika watu wapatao 60.”

Kufikia Aprili iliyofuata, kulikuwako kilele kipya katika wahubiri—223! Ni ukuzi kama nini, tukifikiria kwamba wakati akina Siebenlist walipowasili, punde kuliko miaka miwili mapema, wahubiri wapatao 120 walishirikiana na yale makundi manne yasemayo Kiingereza na yale mawili yasemayo Kihispania!

MTUMISHI KWA AKINA NDUGU

Katika pindi ya mwaka wake wa kwanza katika Kosta Rika, Ndugu Siebenlist alitumikia akiwa mtumishi kwa akina ndugu, (mwangalizi wa mzunguko). Yeye alizuru yale makundi sita na wale watu wenye kupendezwa waliokuwa peke yao, hata ingawa miendo ilikuwa mbali na usafiri ulikuwa mgumu. Wamisionari zaidi walipowasili, ziara zaidi kwenye makundi zingeweza kufanywa.

Misionari mmoja, Ndugu Blackburn, baada ya ziara ya majuma matatu kwa yale makundi yasemayo Kiingereza akiwa mtumishi kwa akina ndugu, aliripoti hivi: “Bidii na upendo ambao ndugu hawa wanaonyesha kwa ajili ya Theokrasi ni wa kusifiwa. Akina ndugu ni maskini kifedha, hata hivyo wao ni wakarimu sana katika kukaribisha watumishi wa Sosaiti katika makao yao na kuwapa kilicho bora zaidi walicho nacho kutoa. Wao ni wasikivu na wanatamani maagizo. Wao si wanung’unikaji kwa sababu ya kulazimika kutembea kilometa nyingi kupitia joto na matope ili kufanya marudio [ziara za kurudia] na mafunzo ya Biblia.”

Ndugu Blackburn angali anaendelea katika utumishi wa wakati wote—karibu miaka 40 baada ya yeye kutoa ripoti hiyo. Ametumikia katika Nikaragua, Honduras, na Meksiko pamoja na jamaa yake.

Zile ziara za mtumishi kwa akina ndugu zilithaminiwa si na makundi tu bali pia na idadi ya watu wa mahali. Franklin Hardin (anayejulikana vizuri zaidi kuwa “Dak” kwa sababu yeye alikuwa daktari wa maungo ya mwili) na Emily, mke wake, walizuru Puerto Limón katika 1946. Nyusipepa ya mahali hapo ilitoa elezo hili: “Yule mgeni mashuhuri aliandamana na mke wake mwenye kupendeza sana. Wao ni wawili ambao hatujapata kamwe kuona, lakini ule muda mfupi tuliokuwa pamoja nao unatoa kwa urahisi maono yenye kupendeza na kukumbukwa, nayo maana ya usemi wao inatutajirisha na kutupendeza sana kana kwamba tumekuwa tumejuana nao kwa miaka mingi. Sisi tulifuata kwa upenyezi yale maandiko mengi aliyonukuu katika kuthibitisha ujumbe wake.”

MWANGALIZI WA MZUNGUKO WA KWANZA MWENYEJI

Ripoti juu ya kazi ya mzunguko katika zile siku za mapema haiwezi kuwa kamili bila kutaja Arnold Williams kutoka Puerto Limón. Yeye alisimamia duka la United Fruit Company, lakini upesi alivyoweza, yeye alifanya mipango afanye upainia kikawaida. Katika hili yeye aliweka kielelezo bora kwa walio wachanga zaidi katika kuweka masilahi za Ufalme kwanza. Kwa sababu ya bidii na kupiga moyo konde kwake, alizoezwa kuwa mwangalizi wa mzunguko katika San José na katika 1948 akaanza kazi ya mzunguko. Alioa Mildred Gumbs (sasa ni Ortega), nao waliendelea pamoja katika kazi ya mzunguko mpaka 1959. Kwa sababu yeye alielimishwa katika Kiingereza na Kihispania pia, yeye alitafsiria Ndugu Knorr katika pindi ya ziara hiyo ya kwanza. Ilikuwa hasara yenye kuhuzunisha kwa wote wakati yeye alipokufa akiwa mchanga, akiacha nyuma “barua za pendekezo” zilizo nyingi.—2 Kor. 3:1, NW.

KAZI YA PAINIA YAENEZA UJUMBE

Mbali na msaada wenye thamani kubwa wa wamisionari na waangalizi wa mzunguko, mapainia walitimiza sehemu yenye maana kubwa katika kueneza ujumbe nje kwenye maeneo mapya. Mwanzoni mwa 1944, kulikuwa na mapainia wawili, lakini kufikia Agosti kikundi kilipanda kufikia tisa.

Kulikuwa na wahubiri 13 wakikutana katika Grecia, ambako akina Dada Evelyn Ferguson (sasa ni Taylor) na Mildred Gumbs walipewa mgawo wakiwa mapainia wa pekee wa kwanza katika nchi. Katika pindi ya mwaka uliofuata, 1945, Eugenia Dillon pia alijiunga na hesabu za mapainia wa pekee.

Berta Solera, mjane mwenye umri mkubwa aliyekuwa akifanya upainia katika San José, alikuwa na tamaa ya kurudi kwenye mkoa wa kwao, Guanacaste, lakini hakuwa na fedha zo zote mpaka alipouza njia yake pekee ya kujiruzuku, cherahani yake ndogo ili alipie safari hiyo. Yeye na Anita Taylor walifanya safari ya kuhubiri huko katika 1947 na wakapata katika Liberia na Filadelfia pia, watu ambao kupendezwa kwao katika mambo ya kiroho kuliwasukuma wakaribishe mapainia kwenye makao yao. Kufikia 1949, Berta, akiandamana na bintiye, alipewa mgawo kwenda Liberia akiwa painia wa pekee, ambako wale wasichana wawili wa Swaby walijiunga naye. Ni nani hao wasichana wa Swaby?

AKINA DADA WAFANYA UPAINIA

Claudia Goodin, mwanamke mrefu, mwenye rangi ya ngozi nzuri wa asili ya Jamaika, alikuwa na binti wawili, Joy na Fe. Wakati huo, Claudia alikuwa akiishi na dada yake wa kimwili Arelminta Swaby katika Puerto Limón. Arelminta alikuwa na binti wanne—Dorell, Calvie, Lila, na Casel. Dorell alikuwa wa kwanza wa wale wasichana wa Swaby kujasiria kwenda nje akiwa painia. Yeye na Corina Osorio (sasa ni Novoa) walipewa mgawo wa kwenda Point Quepos, ambao uko pwani ya magharibi. Baadaye, dada watatu wa Dorell walijiunga na hesabu za mapainia pia.

Binti wawili wa Claudia Goodin, Fe na Joy, walianza upainia wa pekee 1948 katika Alajuela, ambako kundi jingine lilikuwa limeanzishwa. Dora Argentina Vargas (sasa ni Call) aliongezwa pia kwenye kikosi cha mapainia. Katika 1950 Dorell Swaby na Fe na Joy Goodin walihudhuria Shule ya Gileadi na wakapewa mgawo kwenda Panama. Lila Swaby na Evelyn Ferguson walienda Gileadi katika masika ya 1953 na Argentina alijiunga na darasa lililofuata. Tangu muda wa kuanzia 1940 mbegu nyingi za Ufalme zimepandwa na akina dada hawa wenye bidii.

FARASI NA YULE KINYOZI

Karibu 1944 wakati afisi ya tawi ilikuwa ikianzishwa katika San José, mfuasi mmoja wa imani ya Roma Katoliki katika San Carlos alipokea kupitia barua kile kijitabu Armageddon na akakipitisha kwa Naftalí Salazar, Mwevanjeli. Naftalí alishangazwa sana na mambo ambayo yeye alisoma katika kile kijitabu hivi kwamba alikionyesha kwa pasta wa kanisa lake. Yule pasta alikasirika na kumwonya dhidi ya hii “sumu ya Kiruseli.”

Hata hivyo, Naftalí alitamani kukutana na mtu kutoka tengenezo la Mnara wa Mlinzi, lenye kutangaza kitabu kile. Yeye alikuwa amesikia juu ya kinyozi Mwitalia ambaye pia alikuwa akipokea vile vitabu. Yule kinyozi aliishi katika Grecia, umbali upatao kilometa mia moja. Naftalí aliazimia kumtembelea kinyozi huyo. Yeye aliwaza kwamba ili asafiri kwenda Grecia, yeye angeweza kujiandikisha kuwa msafirishaji ng’ombe kwa mwendo wa siku tatu na katika safari ya kurudi angetua katika Grecia.

Alipowasili katika Grecia, mwelekezo mmoja uliongoza Naftalí kwenye kao la watu wawili wazee-wazee waliooana ambao hawakuweza kusema Kihispania. Yeye alikitoa kile kijitabu alichothamini sana na kuwaonyesha. Wao waliweza kusema tu “Biblia, Biblia” na upesi wakaelekeza kwenye barabara inayoelekea kwenye kilima. Akiwa ametamaushwa, yeye alipanda farasi wake kuelekea upande huo. Juu ya kilima kile, Naftalí aliondoka kwenye njia kuu, akaingia kwenye kijia chembamba na kusimama kwenye lango. Naftalí alifungua lile lango, na farasi akageuka kuelekea nyuma kumsaidia alifunge. Kumbe walikuwa kwenye shamba la mtu fulani. Naftalí na farasi wake walienda kupitia lile shamba wakafika kwenye lango jingine. Mbele ya lile lango palikuwa kibanda kidogo kikiwa na mwanamume mmoja, mke wake, na watoto wawili wadogo wameketi chini nje.

“Wataka nini?” akauliza yule mwanamume.

“Kunradhi, lakini farasi wangu amenileta hapa. Mimi natafuta kinyozi Mwitalia.”

“Ndiye mimi, nawe ni nani?”

“Mimi ni Naftalí Salazar kutoka San Carlos.”

Kwa wazi akiwa tayari amekwisha kusikia juu ya mtu huyu, yule kinyozi aliinua mikono yake na kusema, “Yehova na asifiwe. Yeye amekutuma hapa.” Hiyo ilikuwa siku yenye furaha kama nini kwa Naftalí!

NDOA NA MICHEZO YA BAHATI NASIBU

Kazi ya Ufalme ilipokuwa ikienea, kulikuwako pia uhitaji wa usafi wa kiadili. Ndugu Knorr katika ziara yake ya pili, katika 1946 aliandamana na Ndugu F. W. Franz, aliyethibitika kuwa msaada mkubwa sana. Ndugu wenyeji walipashwa habari ya kuandikisha ndoa kisheria. Leonard Hurst, ambaye wakati ule hakuwa amefunga ndoa kisheria na yule mwanamke aliyekuwa akiishi naye, anakumbuka jambo alilosema Ndugu Knorr. “Ninyi nyote mlio hapa jioni hii mnaoishi na mwanamke lakini hamjapanga ndoa yenu kisheria, mimi nawatolea shauri. Nenda kwenye Kanisa Katoliki na kuandikisha jina lako kuwa mshiriki kwa sababu huko unaweza kuzoea mambo haya. Lakini hili ni tengenezo la Mungu, na huwezi kuzoea mambo haya hapa.”

Leonard alidhani kwamba ndiye Ndugu Knorr alikuwa ameandama, hivyo punde kuliko mwezi mmoja yeye alikuwa amepata talaka ya kuachana na mke wake wa kwanza na akafunga ndoa kisheria na yule mwanamke ambaye alikuwa amekuwa akiishi naye.

Kununua tikiti za bahati nasibu lilikuwa jambo jingine lililohitaji rekebisho. Evelyn Ferguson sikuzote alichukua namba fulani yenye bahati na hata akasali ili namba yake iweze kushinda. Kwa sababu gani? Ili aweze kufanya upainia. Wakati alipong’amua kwamba hilo halikuwa sahihi Kimaandiko, yeye alipiga moyo konde aache kununua tikiti za bahati nasibu.

Yule mwanamume ambaye kutoka kwake Evelyn alinunua tikiti za bahati nasibu alimtembelea kama kawaida na kusisitiza kwamba yeye acheze tena namba yake yenye bahati. Hata hivyo, Evelyn, alibaki akiwa imara katika uamuzi wake na hakutamaushwa hata kidogo wakati namba yake iliposhinda siku iyo hiyo. Upesi baada ya tukio hilo, yeye akawa painia—na alifanya hivyo bila msaada wa yule ‘mungu wa bahati.’—Isa. 65:11.

“MAVUMBI KWA MAVUMBI”

Mashahidi pia waliacha kufuata mazoea ya kidini ya kimapokeo yaliyotilika mashaka. Mathalani, kwenye maziko ya Shahidi mmoja, ndugu aliyekuwa anasimamia ibada ya maziko alimalizia kwa sala fupi kaburini. Kwa sababu yeye hakufuata pokeo la kidini kwa kutamka “majivu kwa majivu na mavumbi kwa mavumbi” na kurusha kidesturi konzi la mchanga juu ya jeneza, wanadini waliokuwapo walikasirika sana na wakafanya hivyo wenyewe.

Wakati fulani baadaye dada mmoja mzee-mzee alikufa. Penye kaburi lake, kabla tu ya kuteremsha jeneza, ndugu aliyekuwa akitoa hotuba ya maziko alifungua Biblia yake na kusoma maneno haya, “Kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” (Mwa. 3:19) Akigeukia ule umati uliokuwa ni pamoja na wanadini wale wale, yule ndugu akasema: “Hakuna lo lote lililosemwa hapa juu ya majivu. Teremsheni sanduku, akina ndugu.” Wakiwa wameduwazwa, wale wapinzani hawakutupa kimapokeo konzi lao la udongo.

Ni nini yaliyokuwa matokeo ya ziara za mwangalizi wa mzunguko, kumiminika kwa wamisionari, na kushikamana na sheria za Kimaandiko? Ni umoja na ukuzi. Alama ya elfu moja ya hesabu ya wahubiri ilipitwa hata kabla ya kuanza muda wa miaka ya 1950, mafunzo ya Biblia zaidi ya 850 yalikuwa yakiripotiwa kila mwezi, na makundi 32 yalikuwa yameanzishwa.

MAKUSANYIKO MASHAMBANI

Mpaka kufikia 1950 yaliyo mengi ya makusanyiko yalikuwa yamefanywa Puerto Limón na San José. Lakini sasa kupendezwa kwingi vya kutosha kulikuwa kumeamshwa kuwezesha kusanyiko moja lifanywe katika kijiji kimoja kidogo kiitwacho Argentina de Tilarán.

Haikuwa rahisi kwa Ndugu na Dada Siebenlist kufika Argentina de Tilarán. Walisafiri kwanza kwa ndege na kisha wakapanda basi moja kuukuu, lililowapeleka kupitia barabara yenye mashimo-mashimo. Kwenye panda ambapo ile barabara iliishia, akina ndugu walikuwa wanawangojea wakiwa na farasi. Ile sehemu iliyobaki ya safari waliifanya wakiwa wamepanda farasi. Mashamba yaliyotapakaa tu ndiyo yaliyozunguka mahali pa kusanyiko. Hata hivyo, akina ndugu, walikuwa wamesisimuka sana—hili lilikuwa ndilo kusanyiko lao la kwanza. Baadhi yao walikuwa wamesafiri kwa miguu kupitia vijia vya milima-milima kwa muda upatao saa tisa. Hesabu ilipochukuliwa Jumapili, karibu watu 300 walikuwa katika hadhirina, wengine walisimama na wengine waliketi juu ya bechi zilizotengenezwa apo hapo kwa mbao ambazo ziliwekwa juu ya magunia ya mchele.

Wakati wa kusanyiko, mwangalizi wa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi aliyekuwa amewekwa rasmi karibuni aliongoza shule. Kabla ya kuanza, mwangalizi wa mzunguko alimpa maagizo yenye mambo mengi juu ya jinsi ya kushauri wahutubu wanafunzi. Mathalani, yeye aliambiwa kwamba inampasa kushauri kila mwanafunzi juu ya mambo mawili mazuri na mambo mawili yenye udhaifu. Mwangalizi wa mzunguko alihisi ana uhakika kwamba yule ndugu alifahamu na kwamba shule ingeendelea barabara. Kwa udhiko la mwangalizi wa mzunguko, baada ya mwanafunzi wa kwanza kumaliza hotuba yake, yule mwangalizi wa shule alisimama na kwa wasiwasi, lakini kwa unyofu, akasema, “Ndugu, wewe ulikuwa na mambo mawili mazuri na mambo mawili mabaya. Jaribu kufanya vizuri zaidi wakati ujao.” Halafu, bila neno jingine la shauri, yeye akakaribisha mwanafunzi aliyefuata.

KUTOKA KUWA WAVUVI WA SAMAKI KUWA WAVUVI WA WATU

Katika 1940 Josephine Steele alisafiri kwenda Moín, kaskazini tu mwa Puerto Limón. Ili kuanza utoaji wake wa ushuhuda, yeye alitweka kinanda chake kwenye stesheni ya gari-moshi katika Moín. Akakaza mota ya kinanda kwa kuzungusha mpini wayo mara kadhaa, na kwa uangalifu mwingi akaweka sindano kwenye mfuo wa kwanza wa sahani ya santuri iliyorekodiwa sauti ya Jaji Rutherford, akatia swichi ya kuanzisha. “Dini ni Mtego na Hila,” ikavuma ile sauti kutoka kwa kile kinanda. Kikundi kikubwa cha watu kilikusanyika. Mmoja wa hicho kikundi, Vincente Sanguinetty, akapeleka habari ili Silbert Spence, mwanamume mvuvi wa samaki rafiki yake, akaitwe. Silbert, suruali yake ikiwa imekunjwa, akakaribia kile kikundi cha wasikilizaji, akaweka mikono yake viunoni mwake, akatazama rafiki yake Vincente, na kuuliza: “Ni nani huyo anayesema?”

“Ni Jaji!” akajibu Vincente, akimaanisha Joseph F. Rutherford, msimamizi wa pili wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi.

Kwa kuwa tayari Vincente alikuwa amesoma baadhi ya vitabu vya Ndugu Rutherford, wale wanaume wawili walimshughulisha Josephine siku nzima kwa maswali yao ya Biblia. Vincente alimwambia Dada Steele kwamba siku moja akiwa baharini katikati ya dhoruba mbaya sana, yeye alisali kwa Bwana kuomba msaada na akaahidi kumtumikia ikiwa angeokoka. Alikuwa angali akitaka kutimiza ahadi yake kwa Mungu, lakini mambo mawili yalikuwa yakimsumbua—wasichana na dawa za kulevya. Funzo la Biblia lilianzishwa na hawa wanaume wawili, na upesi baada ya hapo, katika Septemba 21, 1940, wote wawili walibatizwa, pamoja na mke wa Silbert, Valmina.

“Shangwe yangu ilianza kuongezeka nilipokuja kung’amua kwamba maneno ambayo Yesu aliambia Petro na Andrea yalikuwa yakitimizwa katika mimi,” akasema Silbert. “Mimi sasa nilikuwa nikivua watu.” Joshua Steelman, aliyekuwa akizuru akiwa mjumbe wa pekee wa Sosaiti, alimuuliza Silbert: “Wewe unapanga kufanya upainia wakati gani, wakati Har–Magedoni itakapokuwa ikibisha penye mlango?” Silbert aliona uharaka wa nyakati. Yeye na Valmina wakaanza upainia Novemba 1948.

Hata ingawa Silbert alikuwa na wakati mgumu akisema lugha ya Kihispania, yeye alipewa mgawo kuwa mwangalizi wa mzunguko wa Kihispania. Mwanzoni, hotuba zake zote zilikuwa katika Kiingereza, na mtu fulani alikuwa akitafsiri. Siku moja ndugu mmoja mwenye kusema Kihispania alimpa Silbert uhakikisho kwa maneno haya: “Ndugu Silbert, usiwe na wasiwasi juu ya Kihispania chako. Sisi tunang’amua kwamba wewe una tatizo, lakini wakati ule ule sisi tunajifunza ukweli kwa urahisi zaidi kutoka kwako.” Hivyo, upendo hauna vizuizi vya lugha.

Mke wa Silbert alifanya kazi kwa uaminifu pamoja naye katika kazi ya mzunguko mpaka kifo chake katika 1974. Silbert alitumikia kwa uaminifu akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi mpaka kifo chake katika Mei 1985.

JUMBA LA KUSANYIKO LA KWANZA

Ongezeko katika idadi ya Mashahidi lilianza kuhisiwa na viongozi wa kidini kote kote nchini. Wao walitia mkazo juu ya matengenezo ya mambo ya kijamii, hivyo kufanya liwe jambo gumu zaidi na zaidi kukodi mahali kwa ajili ya makusanyiko ya mzunguko katika Puerto Limón. Kwa hiyo Mashahidi wa mahali hapo wakaamua kujenga Jumba la Ufalme moja ambalo lingeweza kutumika pia kama Jumba la Kusanyiko. Kwenye uwanja mmoja uliokuwa mwendo wa majengo matatu tu kutoka soko kuu, jengo moja lenye sakafu mbili liliinuliwa. Jumba la Ufalme lilikuwa penye sakafu ya juu, sakafu ya chini ikawa makao ya kuishi mwangalizi wa mzunguko, pamoja na jikoni na nafasi ya kupakulia vyakula kwa ajili ya kafeteria ya kusanyiko. Alhamisi, Agosti 19, 1954, liliwekwa wakfu. Katika 1972, jengo hili lilijengwa upya na kwa sasa linatumiwa na makundi matatu na kwa ajili ya makusanyiko madogo zaidi ya Kiingereza.

JUMBA LA UFALME LATEKETEZWA

Kwenye pwani iliyokuwa upande mwingine, wa Pasifiki, akina ndugu hawakupata shangwe ile ile na Jumba la Ufalme lao. Kundi moja la wahubiri wapatao 45 walikutana katika mtaa mdogo wa mashambani wa Manzanillo de Ario. Upinzani ulipanda dhidi yao mpaka matisho ya jeuri yakazaa tunda baya.

Usiku mmoja, wapata usiku wa manane, Jumba la Ufalme la mahali hapo kwa ghafula liliteketea kwa miale ya moto. Liliteketea upesi sana hivi kwamba hakuna cho chote ambacho kingeweza kuokolewa—hasara kubwa ya mali za kimwili na za kiroho kwa watu ambao tayari walikuwa maskini. Je! pigo hili la ufidhuli wa kutekeza mali kwa makusudi lililemaza kazi ya Ufalme? Hapana! Wahubiri wasiotenda waliinuka ghafula kwenye uhai wa kiroho; wapya wakaanza kushirikiana na Mashahidi. Walihamisha mikutano yao ikapelekwa kwenye kao la ndugu mmoja na wakaendelea na mipango yao kwa ajili ya mwadhimisho wa Ukumbusho.

Je! tendo hili la jeuri liliathiri hadhirina ya Ukumbusho? Ndiyo, lakini kwa matokeo mema. Kulikuwako na ongezeko la karibu asilimia 300 kuliko miaka iliyopita. Imani ya kweli haiwezi kutikiswa na wapinzani, jambo ambalo lilionyeshwa vizuri ajabu na Kristo Yesu na wale mitume, na ambalo linaigwa katika karne hii na maelfu ya Mashahidi ambao wanathibitisha ubora wa imani yao chini ya mtihani.—1 Pet. 1:6, 7.

TENDO LA WATU WENYE GHASIA LAZUIWA

Mwingi wa upinzani huo ulichochewa na viongozi wa kidini. Mathalani, ili waonye kundi lao wakati wo wote Mashahidi walipokuwa katika ujirani, makasisi waliweka vipaaza-sauti katika minara ya kengele za makanisa yao. Walichapisha ishara zenye kutaarifu: “Sisi ni Wakatoliki. Sisi hatukubali propaganda za Kiprotestanti.” Kisha wale viongozi wa kidini waliuzia waparokia ishara hizo, ambao wangeziweka kwenye madirisha ya nyumba zao. Bila shaka, Mashahidi walipuuza ishara hizo.

Eugenia Dillon alipata kuona kwamba si watu wote walishawishwa na wale viongozi wa kidini. Siku moja akiwa katika utumishi wa shambani, watu wenye ghasia walikusanyika na kumfuata, wakipaaza sauti hivi, “Bikira wa malaika atawala hapa. Papa mwenye enzi na aishi muda mrefu. Sisi ni Wakatoliki na hatukubali propaganda za Kiprotestanti.” Kwa haraka yeye alisali kwa Yehova apate msaada. Kwenye mlango aliofuata kutembelea, mwanamume mmoja, akiwaona wale watu wenye ghasia, akauliza, “Je! watu hawa wanafuata wewe? Njoo ndani, nami nitakukinga na kundi hili la wakatili.”

Mara dada Dillon alipoingia ndani, akiitikadi kwamba sala yake ilikuwa imejibiwa, yule mwanamume alitimua mbio kuingia ndani ya chumba kingine, akanyakua bastola yake, akaishindilia risasi, na kukimbia nje ya nyumba kwenye lango. Hapo, akipunga-punga bastola yake, alipaazia sauti wale watu wenye ghasia akiwaambia, “Msichana huyu si wa dini yangu, lakini mimi namkinga nami naamuru watu hawa wenye ghasia watawanyike ikiwa ninyi hamtaki kufa.”

Mara hiyo watu hao wenye ghasia wakatawanyika. Yule mwanamume akarudi nyumbani akitabasamu, akisema kwamba kwa kweli yeye hakuwa anataka awaue lakini kwamba mtutu wa bunduki ndio lugha pekee ambayo genge katili hilo la kishetani lingeelewa.

Pindi nyingine, Ndugu Pile, akibeba kinanda chake, alichukua kikundi kikubwa cha wahubiri pamoja naye wakafanye kazi Juan Viñas, magharibi mwa Siquirres. Padri wa mahali hapo alianza kupiga kengele za kanisa, akiita watu wake. Yeye aliagiza baadhi ya waungaji mkono wake waende nyumba kwa nyumba wawaambie wale wengine wasisikilize wakati Mashahidi wangetembelea.

Lazima yule padri awe alitumbua macho kwa kupendezwa akifikiri alikuwa anafanikiwa, mpaka yule jefe político, mtu aliye kama meya-liwali, alipowaita akina ndugu na mapolisi wengine waje katika afisi yake. Kisha jefe político aliomba kwamba Ndugu Pile apige santuri asikilize ujumbe. Baada ya kusikiliza zile rekodi za Ufalme, wale mapolisi walikubali vitabu. Yule liwali hakuweza kuona jambo lo lote lililokuwa mbaya katika kazi ya kutoa ushuhuda na akawaambia akina ndugu waendelee kuhubiri.

Ushindi wenye shangwe ulitokea wakati John Craddock alitoa hotuba ya watu wote katika San Ramón kwenye jukwaa la wanabendi katika bustani ya starehe. Watu wachache wa mahali hapo, wale mapainia kutoka San Ramón, na akina ndugu wapatao sita waliokuwa wameandamana na Ndugu Craddock kutoka San José walikuwa katika hadhirina. (John na mke wake Emma Marie, wahitimu wa darasa la kumi la Gileadi, walikuwa wamejiunga na ile jamaa ya wamisionari katika 1949. Sasa, mwaka mmoja na nusu tu baadaye, walikuwa karibu kupata mwonjo wa ule upinzani.) Padri mmoja akiwa na kikundi cha watoto walipanda jukwaa la wanabendi nyuma ya Ndugu Craddock wakaanza kumsumbua kwa maswali. Wakati ule ule, kutoka upande mwingine wa mbali wa uwanja wa watu wote, kundi lenye ghasia la watu wazima lililotangulia kupangwa lilitokea ghafula likipaaza sauti, “Mwue, Mwue!”

Kwa wazi, wale watu wenye ghasia walitaka tu kumwogopesha Ndugu Craddock kwa sababu walipita karibu tu bila kumgusa. Akishindwa kumaliza hotuba yake, John, akiandamana na Marie na wale wengine kutoka San José walienda kwenye kituo cha basi, ambako meya wa mji aliwaendea na kusema jinsi alivyosikitika kwa vile hotuba ilikuwa imekatizwa. Yule meya alisihi kwamba John arudi akatoe hotuba nyingine na akaahidi kwamba himaya ya polisi ingeandaliwa.

Basi ikawa kwamba, majuma matatu baadaye, kikundi cha wahubiri kilirudi San Ramón na hata kilitangaza ile hotuba kote kote mjini kwa vikaratasi. Wakati ulipofika kwa ile hotuba, Polisi walikuwa wamejipanga mstari kwenye uwanja wa watu wote. Wakati huu hakukuwa na usumbuo.

VITA YA WENYEWE KWA WENYEWE

Uchaguzi wa 1948 ulitokeza mapinduzi. Jambo hilo lilifanya iwe vigumu kwenda huku na huku katika utumishi wa shambani. Eugenia Dillon, alipokuwa akifanya kazi katika eneo la mashambani pamoja na mhubiri mwenzake, alisimamishwa na askari-jeshi. “Simama, nani anatembea huko?” wakabweka wale askari-jeshi, bunduki zao zikiwa zinalenga hao akina dada. “Ninyi ni wa chama gani cha kisiasa?”

“Sisi ni Mashahidi wa Yehova,” akina dada wakajibu. “Sisi tunatangaza Ufalme wa Mungu kupitia Kristo Yesu, serikali pekee inayoweza kuleta amani halisi kwa wanadamu.”

Wale askari-jeshi walipokuwa wakipekua-pekua mikoba yao, wale mapainia wakawatolea ushuhuda. Dada hao waliachiliwa na wakaendelea kuhubiri katika ujirani huo kwa watu ambao, walikuwa katika huzuni kuu kwa sababu ya ile vita.

Wakati wa vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, wengi wa wale wachungaji-bandia, wale viongozi wa kidini, waliacha makundi yao, wakakimbia. Hilo liliwapa Mashahidi nafasi ya kuhubiria wenye mfano wa kondoo walioachwa nyuma. Sasa wale watu wa nchi waliweza kuona kwamba wachungaji wao viongozi wa kidini hawakuwa wakiwalisha bali walikuwa tu wakiwanyang’anya mali yao. Wakati wale wachungaji-bandia waliporudi, walipata, kwa fadhaa yao, wengi wa kundi lao wakijifunza pamoja na Mashahidi.

USAFIRI KWA KUTUMIA GARI-NYUMBU

Usafiri unafungamanishwa karibu karibu na kazi ya kuhubiri, na njia mbalimbali zimetumiwa katika Kosta Rika. Magari-moshi yametumiwa. Lakini si magari-moshi yote yanakokotwa na mashine yenye injini. Lile gari-nyumbu ni gari la aina ya pekee ambalo hupita juu ya reli na kukokotwa na nyumbu mmoja. Linaweza kukupa misisimuko mingi zaidi ya kile kigari cha kujifurahisha kinachopita juu ya reli.

Gari hilo linafanyizwa kwa jukwaa linalowekwa juu ya gurudumu. Lile jukwaa lina mabenchi yanayoweza kukaliwa na watu 20. Gari-nyumbu hilo linapoenda mbio juu ya reli, breki pekee ni boriti ya mti iliyowekwa kupitia shimo sakafuni. Linazunguka kama leva na kubana gurudumu. Hivyo, mteremko humaanisha hatari kwa nyumbu ikiwa dereva hazuii lile jukwaa lenye kusogea-sogea lisigonge mnyama huyo kwa kishindo. Pia, wale maabiria wananyunyiziwa matope yanayorushwa na makwato ya yule nyumbu, lakini hilo ndilo tatizo lililo dogo zaidi. Magurudumu yakiacha reli wale maabiria wanaweza kurushwa hewani, hilo likisababisha miguu na mikono iliyovunjika inapopiga chini.

Safari za mito zinafanywa katika mashua ndogo zenye mota iliyo upande wa nje inayoweza kuondolewa, au kwa mitumbwi yenye makafi ya miti. Mathalani, ili kufika Guanacaste katika safari ya kuhubiri, Dada Solera alichukua gari moshi mpaka Puntarenas, kisha akavuka Ghuba ya Nicoya kwa mashua kubwa, na baadaye akapanda mkototeni wenye kukokotwa na ng’ombe-dume kwa saa 15. Halikuwa jambo dogo kwa mwanamke mwenye umri wa miaka zaidi ya 60!

MABADILIKO KATIKA TAWI

Theodore Siebenlist alitumikia akiwa mwangalizi wa tawi tangu kufanyizwa kwa lile tawi katika Machi 1944 mpaka June 1952, wakati yeye na mkeye walipoondoka wajitayarishie uzawa wa binti yao Janet.

William Call, mhitimu wa darasa la tatu la Gileadi ambaye alikuwa ametumwa Nikaragua kutoka Kosta Rika katika 1946 kuangalia tawi huko, alirudi Kosta Rika akiwa mwangalizi wa tawi. Yeye aliendelea akiwa hivyo mpaka 1954, wakati alipooa Dora Argentina Vargas, mhitimu wa Gileadi, ambaye mwanzoni alikuja kutoka Guatemala. Mwana wao Robert sasa anatumikia kwenye Betheli ya Brooklyn. William Aubrey Bivens kutoka Guatemala ndiye aliyefuata kupewa mgawo wa kuwa mwangalizi wa tawi. Yeye na mke wake, Bertha, walikuwa wamekuwa katika nchi hiyo tangu kuhitimu kutoka darasa la tano la Gileadi. Baadaye walipewa tena mgawo wa kwenda Brazili, ambako yeye alitumikia akiwa mwangalizi wa tawi mpaka kifo chake katika 1969.

Kwa kuwa Ndugu Bivens aligawiwa tena kwenda Brazili, Charles Sheldon alitenda akiwa badala ya mwangalizi wa tawi mpaka Machi 1964, wakati George Jenkins na mke wake walipowasili. Sababu za afya ziliwalazimisha akina Jenkins kuondoka Kosta Rika katika 1966. Lorence A. Shepp, mwangalizi wa tawi aliyefuata, alikuwa angali Nikaragua. Yeye alifikaje Kosta Rika?

Lorence alikuwa amekuwa katika utumishi wa wakati wote tangu 1958 na alikuwa ametumikia katika kazi ya mzunguko katika Kanada na Alaska. Wakati waangalizi wa mzunguko walipoalikwa kwenda makao makuu Brooklyn kwa Shule ya Huduma ya Ufalme ya pekee, Ndugu Knorr aliuliza kama wo wote walikuwa na nia ya kukubali mgawo wa kuwa wamisionari katika nchi ya kigeni bila ya kuhudhuria Shule ya Gileadi. Ndugu Shepp alikubali mwaliko huo. Yeye alipewa mgawo kwenda Nikaragua katika 1961, ambako alimwoa Juana Olimpia Guinart, Mkyuba, na mhitimu wa darasa la 22 la Gileadi. Huu ulikuwa ndio mgawo wake wa tatu, akiwa tayari ametumikia kama misionari katika Honduras na Meksiko.

Baadaye Ndugu Shepp alipokwisha kuhudhuria Shule ya Gileadi ya miezi kumi, yeye na Olimpia walipakia mifuko yao waende mgawo mpya, El Salvador. Kwanza wao waliamua kuchukua likizo katika Kosta Rika na mara moja wakapapenda sana mahali hapo. Hawakujua hata kidogo kwamba barua ilikuwa tayari katika posta ikibadili mgawo wao waende Kosta Rika.

Akina Shepp waliwasili katika Septemba 1966, na kwenye kusanyiko la kimataifa katika Desemba mwaka huo, Ndugu Knorr alitangaza kwamba Ndugu Shepp alikuwa amewekwa rasmi kuwa mwangalizi wa tawi. Sasa yeye ndiye mratibu wa Halmashauri ya Tawi hilo.

KIAMSHI CHA KUPANUA

Katika Desemba 1954 Ndugu Knorr alizuru Kosta Rika tena na akatangaza kujengwa kwa kao jipya la tawi na Jumba la Ufalme. Idili ilipanda juu. Mipango ilifanywa kununua uwanja mmoja katikati ya San José. Kisha, mapema katika Januari, wakati ule tu ambapo akina ndugu walikuwa tayari kuanza ujenzi, uvamizi wa kikosi chenye silaha ukaingia kutoka kaskazini. Ijapokuwa miji na vijiji ilikuwa ikimiminiwa risasi kwa kutumia ndege, akina ndugu waliendelea kutoa ushuhuda nyumba kwa nyumba wakifariji watu kwa ujumbe wa Ufalme wa Mungu. Ripoti za shambani za Januari zilionyesha kwamba kilele cha mwaka uliotangulia kilikuwa kimepitwa. Lakini kilele cha Aprili kilithibitika kuwa kikubwa hata zaidi! Kulikuwako ongezeko la asilimia 30, kukiwa na wahubiri 2,078.

Namna gani juu ya vile vifaa vipya vya tawi? Je! vilicheleweshwa? Ujenzi wa tawi ulimalizwa Januari 25, 1956, siku mbili tu kabla ya ziara isiyotazamiwa ya Ndugu Knorr na mke wake Audrey. Liliwekwa wakfu Januari 27, 1956.

MATATIZO JUU YA KUSALIMU BENDERA

Katika Septemba 1959 lile suala la kusalimu bendera lililetwa mbele katika shule za Puerto Limón. Wanafunzi kumi na watatu, wote Mashahidi wa Yehova, walikataa kushiriki sherehe hizi kwa sababu hilo lingehalifu dhamiri zao za Kikristo. Ijapokuwa wao hawakuwa wameshiriki tendo lo lote la kutoonyesha heshima, na mwenendo wao ulikuwa umekuwa bila lawama, wale watoto Mashahidi walishtakiwa uasi na kutotii na wakafukuzwa shuleni.

Mahakama ya mahali hapo ilikataa ruhusa ya hao watoto kurudishwa shuleni maadamu walikataa kusalimu bendera. Rufani ya kesi hiyo iliombwa kwenye Mahakama Kuu Zaidi ya Kosta Rika. Huko Mahakama ilielezwa kwamba Katiba ya Kosta Rika inahakikisha uhuru wa ibada na haki ya kuelimishwa katika shule za serikali. Hata hivyo, Mahakama Kuu Zaidi ilitegemeza ule uamuzi wa ile mahakama ya chini zaidi, ikisema kwamba ile sheria kuhusu uhuru wa ibada haikuwa imehalifiwa.

Kwenye mwanzo wa muhula uliofuata, walio wengi wa wale wanafunzi waliruhusiwa tena shuleni lakini wakafukuzwa tena wakati walipokataa kujiunga katika sherehe nyingine za kusalimu bendera. Ndipo ombi lilipofanywa kwa Baraza Kuu la Elimu, lakini katika Julai 5, 1960, ombi hili lilikataliwa.

Suala hilo la kusalimu bendera lilitokeza utangazaji mwingi sana kwa magazeti na redio pia. Suala hilo lingali lipo shuleni mpaka leo hii, lakini wengi wa walimu wanatambua ule mwenendo bora wa Mashahidi wachanga na, badala ya kutokeza matata kuhusu msimamo ambao watoto hao wanachukua kulingana na dhamiri, wao wanajifanya hawaoni jambo hilo. Wanang’amua kwamba katika visa vingi kufukuza shuleni wanafunzi hawa kungemaanisha kupoteza sehemu iliyo bora zaidi ya darasa.

Katika shule moja ya mashambani, kati ya wanafunzi 50 walioandikishwa ni 6 tu ambao hawakuwa Mashahidi wa Yehova. Kwa hiyo ikiwa hawa Mashahidi wangefukuzwa, ile shule ingekuwa haina budi kufungwa, naye mwalimu angepoteza kazi yake.

Walimu wengi walifikiri kwamba wale waliofukuzwa shuleni hawangefaulu kupata riziki maishani bila elimu rasmi. Milton Hylton, mjukuu wa Francela Williams, aliwathibitisha kuwa wenye kosa. Ingawa yeye alifukuzwa shuleni, “hili lilitokeza baraka,” yeye anasema. “Kwanza mimi nilikuwa na nafasi ya kuthibitisha ukamilifu wangu kwa Yehova na kisha kufurahia zile manufaa za miaka zaidi ya 13 katika utumishi wa wakati wote.” Wakati ilipohitajiwa kabisa Ndugu Hyton afanye kazi wakati wote, yeye alipata kazi kama karani afisini na baadaye akapata cheo akiwa mhasibu wa faragha wa kampuni ile ile, bila kuachilia utendaji wake wa kitheokrasi.

VOLKANO IRAZÚ NA ARENALI ZAAMKA

Katika Machi 13, 1963, Irazú, mojapo volkano nyingi za Kosta Rika, iliamka kutoka usingizi wayo mfupi wa miaka 20 ikawa na utendaji wa kipindi cha miaka 2. Volkano hiyo iliyo kilometa zapata 32 kutoka mji mkuu, ilitupa majivu katika zile pepo za kawaida, ambazo zilichukua majivu hayo ya kivolkano kutoka kasoko (shimo) na kuyaangusha juu ya San José, ambako wapatao robo moja ya Wakosta Rika wote huishi. Jiji la Cartago, linalotulia chini ya ile volkano, halikuathiriwa na anguko hili, kwa kuwa zile pepo zilichukua yale majivu juujuu ya hilo jiji. Lakini Cartago lilipigwa upesi na msiba mkuu wa aina nyingine tofauti.

Katika usiku wa Desemba 9, 1963, mvua kubwa zililowesha zile chunguchungu za majivu zenye kina kirefu kando za ile volkano. Kwa kulemewa sana, yale majivu yaliyolowana yaliporomoka chini ya mlima na kuingia kwenye mito iliyozibwa na majivu, yakiifanya ifurike kingo zayo. Mto mmoja uliofurika ulipita kasi kwenye jiji la Cartago, ukifagilia mbali makao pamoja na wenyeji waliokuwa wakilala, pamoja na mifugo na wanyama. Watu walipoteza uhai wao katika furiko hili hata ingawa magari ya polisi yakiwa na vipaaza-sauti yalifanya doria katika barabara za jiji kabla ya wakati, yakionya juu ya msiba uliokuwa unakaribia. Wale waliopatwa na maafa ama hawakuchukua lile onyo kwa uzito, ama hawakuwa na nia ya kuacha mali zao za kimwili. Wao walilipa kwa uhai wao kwa kukosa kusikiliza.

Kwa miaka mingi watu wa Cartago walikuwa wamechukua mwelekeo unaofanana na huo juu ya onyo kuhusu vita ya Har–Magedoni inayokaribia. Hapana shaka wao walihisi kuwa salama kutokana na dhara kwa sababu jiji lao ndilo kao la ile basilika yenye sifa kubwa ambamo unakaa ule mfano wa “mtakatifu” aliye msaidizi wa kike wa Kosta Rika. Lakini baada ya msiba ule na baada ya zaidi ya miaka 30 ya kuhubiri katika jiji hili, mwishowe kundi moja lilianzishwa kuelekea mwisho wa 1964.

Baada ya Mlima Irazú kuchoka kutapika kifo na uharibifu, volkano nyingine, Arenali, ilianza kipindi cha utendaji baada ya kukaa bila kutenda kwa muda wapata miaka 600. Wakati Arenali, iliyoko katika sehemu ya kaskazini ya Kosta Rika, ilipoanza kulipuka, kulikuwa makundi matano katika ukanda ulioathiriwa. Wengi wa akina ndugu katika eneo hilo hawakuwa na jingine la kufanya ila kukimbia. Hakuna wo wote wao waliopoteza uhai wao, lakini walipoteza mali zao za kimwili. Upesi, akina ndugu katika sehemu zote za Kosta Rika wakaja kusaidia kwa michango ya chakula, mavazi, na pesa.

KUPUNGUZA MWENDO KATIKA ILE MIAKA YA 1960

Ile miaka ya 1964 na 1965 haikuleta ongezeko. Ripoti ya kila mwaka ya Kosta Rika ililaumu hali za kiuchumi. Wahubiri wengi walikuwa hawana budi kuondoka Kosta Rika wakapate kazi ya kimwili kwingineko. Sababu nyingine ilitajwa pia katika ile ripoti ya mwaka: “Kwa kusikitisha, idadi kubwa ya watu ilikuwa sharti itengwe na ushirika kwa kuishi maisha machafu, lakini wote wanatamani sana kuendeleza tengenezo likiwa safi kwa ajili ya ibada safi.”

Ile kazi ilichechemea kwa miaka mitatu zaidi bila ongezeko. Wakati huo uliruhusu kuweko kutahiniwa na kukomaa kwa wanaume wa kiroho ambao wangehitajiwa kwa ajili ya ukuzi wa ghafula ambao ungekuja. Mmojapo wanaume hao alikuwa Andrés Garita. Yeye alitumikia katika kazi ya mzunguko na ya wilaya kwa miaka 20. Yeye aliona sababu ya uvumilivu wake ilikuwa nini? “Wazazi wangu walianza kujifunza katika 1946, na sisi sikuzote tulihudhuria mikutano kwa uaminifu,” akasema. “Mimi nilibatizwa katika 1953 nikiwa na umri wa miaka 14. Mikutano na utumishi wa shambani ilinileta katika ushirika wa karibu na waangalizi wa mzunguko, ambao sikuzote walinipa uangalizi wa pekee na kitia-moyo nichukue utumishi wa wakati wote.” Katika masika ya 1979, yeye aliwekwa rasmi kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi. Alitumikia kwa uaminifu akiwa hivyo katika kazi ya mzunguko na ya wilaya pia pamoja na mke wake Mayra na binti yao Andrea mwenye umri wa miaka sita, mpaka alipopatwa na ugonjwa wa ghafula na kifo kisichotazamiwa akiwa na umri wa miaka 48 katika Julai 7, 1987. Yeye alipendwa sana na kujulikana karibu na kila Shahidi katika Kosta Rika, jambo ambalo lilikaziwa na uhakika wa kwamba karibu watu 4,000 walihudhuria maziko yake.

WAMISIONARI ZAIDI WACHOCHEA ILE KAZI

Ule muda wa tangu 1960 ulitokeza mbele “zawadi katika wanaume” walio vijana zaidi. (Efe. 4:8, NW) Gileadi hakika imeongezea ukuzi wa kiroho na ukomavu wa Kosta Rika. Alvaro Muñoz na Milton Hylton walikuwa Wakosta Rika walioalikwa kuja Gileadi na kisha wakapewa migawo kurudi nyumbani kwao. Miaka waliyotumia katika kazi ya mzunguko ilithaminiwa sana, nao wanaendelea kuwa chanzo chenye kuburudisha wakiwa wazee katika makundi ya nyumbani kwao.

Douglas Little na Frederick Hiltbrand kutoka United States, wahitimu wa darasa la 45 la Gileadi, walipewa migawo kwenda Kosta Rika katika 1968. Wote wawili walitumikia katika kazi ya mzunguko. Katika 1972 Douglas Little alioa Saray Campos, ambaye tayari alikuwa akifanya upainia kwa miaka saba. Jamaa ya wamisionari ilikua wakati ndugu wawili zaidi waliwasili, John Griffin na Lothar Mihank.

Katika 1976 Frederick Hiltbrand alioa Mirtha Chapa, misionari kutoka darasa la 55 la Gileadi. Kwa sasa Frederick anatumikia akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.

TETEMEKO LA DUNIA KATIKA MANAGUA

Maufungamano ya karibu yamedumishwa kati ya akina ndugu katika Kosta Rika na wale walio katika Nikaragua kwa muda wa miaka iliyopita, si kwa sababu tu ya kuwa majirani bali kwa sababu ukuzi wao wa kitheokrasi umehusiana. Akina ndugu katika Nikaragua waliangukia uhitaji ghafula wakati tetemeko la dunia lenye nguvu lilipotikisa mji mkuu Managua, katika Desemba 1972.

Mara moja, mipango ilifanywa katika Kosta Rika kupeleka msaada kwa akina ndugu katika Managua. Ijapokuwa kupashana habari kwa njia ya redio na Managua hakukuwa kumefanywa, lori moja lilipelekwa likiwa na karibu tani moja ya vyakula. Vyote hivyo vilikuwa vimekusanywa katika muda wa dakika 60 tu tokea wakati akina ndugu walijulishwa kwanza juu ya kukusanywa kwa msaada. Afisi ya balozi wa Nikaragua iliwapa viza akina ndugu wenye kusafiri waliposikia ilikuwa ni kwa ajili ya msaada kutoka kwa Mashahidi wa Yehova. Milango yote ya urasimu ilifunguliwa wazi, hivi kwamba msaada ungeweza kupelekwa moja kwa moja kwa akina ndugu.

UMOJA WA JAMAA WALETA FANIKIO

Trino Rojas na ndugu zake wawili ndio waliokuwa watu wenye ugomvi wa makelele katika mji wa Guápiles. Wakati Mark Taylor, painia wa pekee, alipoanza kutembelea wazazi wa Trino, yeye hakupenda jambo hilo na pindi moja kwa ufidhuli hata alialisha mjeledi wake wa farasi nyuma ya Mark. Lakini Mark alistahimili katika ziara zake, na polepole Trino alipata habari chache za ukweli. Baadaye, Trino alipokwisha kumwoa Carmen, mwanamke jirani aliwapa kitabu cha hadithi za Biblia za Kikatoliki. Trino aling’amua kwamba hadithi hizi za Biblia zilipatana na mambo aliyokuwa amesikia kutoka kwa Mark. Alipomwambia mwanamke Mkatoliki hilo, yeye aliudhika akakichukua tena kitabu kile, hivyo akiamsha hamu ya Trino ya kutaka maarifa zaidi ya Biblia. Kwa hiyo Trino na Carmen walianza kujifunza pamoja na Mashahidi na wakabatizwa katika 1950.

Walikuwa na watoto 11. Mmoja wao, David, hukumbuka kielelezo ambacho baba na mama yake waliwekea jamaa. “Udumifu wao katika ukweli ndio uliotuvutia sote. Sisi hatukukosa kamwe mkutano hata ingawa sisi tulikuwa watoto 11 na nyakati zilikuwa ngumu. Baba alinunua shamba katika Roxana, nasi tukahama ili kusaidia kikundi cha watu wenye kupendezwa huko.”

David amekuwa akifanya upainia kwa miaka zaidi ya kumi. “Ule utegemezo aliotupa baba ndio uliofanya iwezekane kufanya upainia,” yeye anasema. Noé, mmoja wa ndugu wachanga zaidi wa David, anakumbuka: “David akawa kielelezo changu. Nilipokuwa na umri wa miaka 13, nilikuwa nikifanya saa 100 katika utumishi. Mimi nilitamani sana siku moja ambayo ningepanda shamba la nafaka, niuze nafaka, nimpe baba fedha, niende kufanya upainia.” Yeye alifanya hivyo.

Ijapokuwa wazazi wao, Trino na Carmen, wamekufa, wale watoto wanadumu wakiwa imara katika imani.

ROHO YA UMISIONARI HUAMBUKIA

Kosta Rika ina kikundi mashuhuri cha watumishi wa wakati wote ambao ni watoto wa waliokuwa wamisionari. Robert Conroy, ambaye aliwasili pamoja na mwenziye John Alexander katika 1959, baadaye alioa na akaendelea katika kazi ya mzunguko katika Kosta Rika. Wakati mke wake, Dina, alipokuwa mja mzito, Robert alisema, “Mke wangu nami tulisali kwa Yehova tupate mwongozo katika kuwalea watoto wetu, tuking’amua kwamba hii ilikuwa pia baraka kutoka kwa Yehova.” Wale wazazi wakiwa sasa wanashiriki tena katika kazi ya mzunguko baada ya kituo cha miaka 20, watoto wao wawili, Judy na Rodney, wanatumikia sasa katika Betheli ya Kosta Rika.

Donald Fry, kutoka darasa la 22 la Gileadi, aliona mwanaye, David, akifuata hatua zake madarasa 50 baadaye. David alihudhuria lile darasa la 72 la Gileadi naye akapewa mgawo kwenda nchi ile ile kama baba yake—Kosta Rika. Ni kwa sababu gani David aliamua kuwa misionari kama baba yake? “Ushirika wangu wa wakati uliopita na wamisionari wenye furaha katika Kosta Rika, pamoja na mwongozo wa kitheokrasi kutoka kwa wazazi wangu, ulinichochea mimi nitake kuwa kama wao,” yeye asema.

Iwe imewezekana kuendelea kuishi katika nchi ya kigeni au sivyo, roho hii yenye kuambukia imeenea katika jamaa ya wengi waliokuwa hapo kwanza wamisionari. Akina Call, akina Sheldon, na akina Blackburn wote wamelea jamaa zao wakiwa na roho hii nzuri.

KOSTA RIKA YASHIRIKI WAMISIONARI WAYO NA NCHI NYINGINEZO

Katika wakati uliopita, baadhi ya wamisionari katika Kosta Rika walipewa migawo kwenda katika nchi nyinginezo. Katika miaka ya majuzi zaidi, John Alexander, aliyekuja Kosta Rika katika 1959 kutoka Gileadi, na mkeye, Corina, walipewa mgawo mwingine kwenda Panama katika 1979. Baadaye, katika masika ya 1982, Lothar Mihank na mkeye Carmen waliombwa watumikie katika Panama.

Je! jambo hili lilidhoofisha utendaji wa kuhubiri katika Kosta Rika? “Ingawa bila shaka ni kweli kwamba sisi tunaikosa ile kazi nzuri ambayo akina ndugu hao waaminifu wamefanya,” ajibu Ndugu Shepp, mratibu wa Halmashauri ya Tawi, “lile pengo ambalo wao waliacha linajazwa upesi na ndugu wa hapa waliokomaa. Mathalani, ile kazi ya wilaya. Ingawa miaka michache iliyopita sisi tulitegemea wamisionari ambao walitumikia wilaya kutoka kwenye afisi ya tawi, sasa ndugu wa hapa wanafanya kazi nzuri katika kujaza pengo hili. Ndivyo ilivyo pia na kazi ya mwangalizi wa mzunguko. Sasa wingu kubwa ambao hutumikia katika cheo hiki cha madaraka ni ndugu wa hapa Kosta Rika. Kwa hiyo sikuzote Yehova anahakikisha kwamba ile kazi haitegemei mtu ye yote mmoja.”

KUTOKA KONDAKTA WA GARI-MOSHI KUWA MWANGALIZI WA MZUNGUKO

Guillermo Badilla alikuwa amekuwa kondakta wa gari-moshi kwenye njia itokayo San José kufika Puntarenas kwa zaidi ya miaka 20. Wakati yeye alipostaafu akiwa na umri wa miaka 50, mara moja yeye aliingia katika utumishi wa wakati wote. Mojapo makundi matano aliyosaidia kuanzisha lilikuwa katika Cartago. Alipowasili kule, alipata mhubiri mmoja tu, ambaye “alikuwa kama kipande cha barafu,” akumbuka Ndugu Badilla. Hata hivyo, baada ya miezi kumi, kundi liliundwa likiwa na wahubiri tisa. Akiongoza maisha za watu kwenye njia tofauti, yeye amesaidia watu zaidi ya 90 wafikie ubatizo. Na akiwa mwenye umri wa miaka 70, aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa mzunguko.

UKAMILIFU WATAHINIWA NA LILE SUALA LA DAMU

Mashahidi wa Yehova wanakataa utiwaji damu mishipani kwa sababu za Kimaandiko, hata kama maisha zao zinahatarishwa. (Matendo 15:29) Lakini wao wana nia ya kukubali matibabu tofauti ya kitiba. Baadhi ya madaktari hushirikiana na Mashahidi juu ya jambo hili la maana la kitiba, hali wengine wanawapinga.

Mathalani, Wilson Rojas alipigwa na mlipuko wenye nguvu nyingi sana hivi kwamba ulimrusha kupitia ukuta wa ghala, na kumwangusha umbali upatao meta nane hata akapoteza fahamu. Mwenzake aliuawa pale pale. Wilson hakupata tena fahamu zake mpaka siku nane baadaye, akapata tu kujua kwamba yeye alikuwa amepoteza utumizi wa jicho moja, sikio moja, mkono mmoja, na mguu mmoja. Wilson alikataa katakata utiwaji damu mishipani. Mke wake, Clarissa, alimtegemeza katika uamuzi wake. Daktari, kwa kuchukizwa, alisema, “Mwache afe. Yeye anabaki na siku tano za kuishi, si zaidi.”

Ingawa Ndugu Rojas alitia sahihi fomu ya kitiba akiiondolea hospitali daraka lote kwa matibabu ya bila damu, hospitali iliacha kumpa utibabu wote isipokuwa kubadilisha vitambaa vilivyofunga majeraha. Hata hivyo, kama muujiza, katika kipindi cha majuma mawili yaliyofuata, polepole hali yake ilipata nafuu. Ndipo ikaja hatari nyingine. Mgandamo wa damu katika mguu wake wa kushoto ulitisha kupasuka dakika yo yote. Daktari-stadi wa ugonjwa huo alipendezwa sana na kisa chake na aliweza kuyeyusha ule mgandamo kwa madawa. Upesi baada ya hapo, alipotembelea Wilson kitandani mwake, daktari-stadi huyo alimuuliza ni kwa sababu gani alikataa kutiwa damu mishipani. Baada ya Wilson kueleza, daktari-stadi alisema: “Sababu iliyofanya mgandamo huo wa damu usipasuke na kukuua kilikuwa kile kipimo cha kiasi cha chini cha damu na wembamba wa damu. Kama ungalikubali utiwaji damu mishipani, yaelekea sana ungekuwa umekufa. Hongera!”

“MWANAMUME ATAKWA”

Njia nyingine ya kufikia mioyo na akili za watu wenye mfano wa kondoo ni kupitia mwenendo wa Kikristo. Katika kiwanda kimoja ambako mzee mmoja hufanya kazi, waajiriwa-kazi walikuwa wakiteta dhidi ya hali za kazi na kudai mishahara ya juu zaidi. Katika pindi ya mkutano kati ya wasimamizi na hawa wafanya kazi, simu ilikuja kutoka kwa meneja wa kampuni nyingine. Alipoambiwa juu ya kutoridhika miongoni mwa waajiriwa-kazi, yeye alijisifu hivi: “Sisi hatuna tatizo la aina hiyo na wafanya kazi wetu, maana walio wengi wao ni Mashahidi wa Yehova.”

Haukupita muda mrefu kabla ya tangazo hili kutokea katika mojapo nyusipepa za taifa zinazosomwa zaidi sana: “MWANAMUME ATAKWA KUFANYA KAZI KATIKA KAMPUNI YETU. LAZIMA AWE MMOJA WA MASHAHIDI WA YEHOVA, ALIYE WAKFU, ALIYEBATIZWA. KWA KUFAA ZAIDI [AWE] MZEE AU MTUMISHI WA HUDUMA.” Kwa wazi hakuna sifa za kufaa nyinginezo zilizokuwa za lazima zaidi.

JITIHADA ZAIDI ZA KUFIKIA

Wakati wa muda wa kuanzia mwaka wa 1970, jitihada zilifanywa kufikia miji midogo zaidi kwa habari njema. Basi ikawa kwamba katika 1972 Ndugu na Dada Siebenlist walirudi kutoka United States na kulowea katika mji wa Tres Ríos, kilometa 10 kutoka San José.

Katika mji huu, mvulana tineja alikuwa ameongoza farakano dogo liitwalo Waabudu wa Yehova. Farakano hilo lilitumia vitabu vya Sosaiti. Kwa sababu ya migawanyiko miongoni mwa kikundi hiki, ile jamaa ya Gutiérrez, ilivunja ushirika na kikundi hiki ikawasiliana na afisi ya tawi ikiomba funzo la Biblia. Douglas Little alipewa mgawo wa kuwasaidia. Yeye anatoa simulizi linalofuata la yaliyotukia:

“Funzo lilianzishwa mara moja na jamaa ya Gutiérrez Miguel, Inés, na wavulana wao wachanga watatu. Wale wazazi walikuwa na maarifa ya ukweli ya kufanya kazi, kwa kuwa walikuwa wamekuwa wakisoma vichapo vya Sosaiti kwa bidii kwa miezi kadhaa. Kwa kuwa walikuwa wamekuwa miongoni mwa ‘mitume 12’ wa kile kikundi na wakiongoza katika ‘utumishi wa shambani,’ wao walikuwa wamekuja kutambua kwamba ni kikundi kimoja tu cha watu kinachofurahia baraka ya Yehova, ukweli ambao, mwanzoni, haukuthaminiwa na washiriki wengine.

“Wakati fulani baada ya akina Gutiérrez kujitenga na lile farakano, washiriki waliobaki waliwasiliana na tawi. Wao pia walitaka funzo, nami niligawiwa kuangalia mahitaji yao. Mipango ilifanywa mimi nizuru kile kikundi chote na kuongoza wonyesho wa funzo la Biblia. Kwa mshangao wangu, mimi nilikuta watu kumi na tano wameketi chini katika nusu duara, mistari ikiwa imepigwa chini ya majibu katika kile kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele na Biblia za New World Translation zikiwa zimefunguliwa na tayari. Wale watu wazima 15 wote waliokuwapo usiku huo, licha ya wengi wa watu wao wa ukoo na marafiki, wameweka maisha zao wakfu kwa Yehova na sasa wanatumikia katika tengenezo lake moja la kidunia.” Leo, kuna makundi mawili katika Tres Ríos.

“WENYE UMOJA KATIKA IBADA”

Mateso katika Kyuba yameunganisha akina ndugu katika Kosta Rika na ndugu zao za kiroho kutoka Kyuba. Baada ya kufungwa kwa njia ya kuhama kutoka Kyuba kwenda United States katika 1980, Kosta Rika ikawa mojapo nchi zilizotumiwa na Wakyuba kuwa njia ya vituo vya kwenda kwenye nchi nyinginezo. Wakyuba waliwasili katika Kosta Rika kwa hiari yao au kwa sababu ya mkazo wa kiserikali au kwa sababu vifungo vyao vya gereza vingefutwa ikiwa wao wangeondoka Kyuba.

Mashahidi wa Kyuba zaidi ya mia moja wameingia Kosta Rika. Mmoja wao, Ubaldo Fernández, ndugu Mkyuba, aliyetumikia akiwa mzee katika kundi la Santo Domingo, alisema kwa niaba ya akina ndugu Wakyuba. “Ndugu wote ambao wamewasili hapa ni wenye shukrani kwa Yehova kwa kuwa huru na wanashukuru sana akina ndugu wa Kosta Rika kwa ukaribishaji-wageni wao na ule upendo wa Kikristo ambao wameonyesha katika kila njia. Kwa hiyo sisi tunaendelea tukiwa jamii moja ya watu wenye umoja katika ibada kwa Mungu mmoja tu wa kweli, Yehova.”

WAMISIONARI WASIOTARAJIWA

Msaada unathaminiwa sikuzote, na kama alivyosema Yesu: “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”—Mathayo 9:37, 38.

Msaada ulikuja kwa namna ya wamisionari kutoka Mwendelezo wa Shule ya Gileadi katika Meksiko. Juan na Rebecca Reyes na Arnoldo Chaves walihitimu kutoka darasa la kwanza na wakapewa migawo kwenda Nikaragua. Mgawo huu katika Nikaragua ulikuwa wa muda mfupi, kwa kuwa hawakuweza kupata ruhusa ya kukaa, nao wakaambiwa waende Kosta Rika wakajaribu kuomba ukazi kutoka huko, jambo ambalo limethibitika kuwa lisilofanikiwa. Wao wamebaki katika Kosta Rika katika kazi ya mzunguko.

Jumamosi, Machi 20, 1982, ndiyo siku wale wamisionari 19 walipofukuzwa kutoka Nikaragua—wageni zaidi wasiotarajiwa. Tisa kati yao walihamishwa nchini wakavuka mpaka wa Kosta Rika kwa njia ya barabara. Wale wengine kumi walipelekwa Panama kwa ndege. Kevin na Ruby Block walivuka mpaka wa Kosta Rika kufikia adhuhuri. Kufikia saa kumi na mbili jioni hiyo wale wengine saba, wakiwa na mali zao zote ambazo wangeweza kupakia katika sutikesi moja, walijikuta wenyewe wakiketi chini ya nyota katika barabara moja isiyopita watu ndani ya eneo la Kosta Rika. Upesi akina ndugu wakiwa na magari waliwasili na kuwapeleka kwa motokaa mpaka Liberia, ambako jamaa ya Jorge Meléndez ilikuwa imewatayarishia chakula chenye moto na mahali pa kulala. Siku iliyofuata wakapelekwa kwenye tawi katika San José. (Jumanne wale wamisionari kumi waliokuwa wamehamishwa kupelekwa Panama pia waliwasili katika Kosta Rika).

USHUHUDA KUPITIA IDHAA YA HABARI

Kufikia usiku wa Jumamosi zungumzo kuu la habari za ulimwengu lilikuwa wamisionari waliofukuzwa. Nyusipepa zaidi ya 41 na vituo vya redio na TV vilipigia afisi ya tawi simu kutoka kote kote ulimwenguni, vikitafuta kuwahoji wamisionari. Jumatano asubuhi, Rodrigo Fournier, mwelezaji mashuhuri wa habari Mkosta Rika, aliomba kuwe na mazungumzo ya kuzunguka meza asubuhi na mapema pamoja na wamisionari waliohamishwa. Reiner na Jeanne Thompson na Ian Hunter walihojiwa kwenye programu ya TV ya taifa zima iliyoendelea kwa dakika 40. Yaliyokaziwa katika pindi ya programu hiyo yalikuwa msimamo wetu wa kutokuwamo kuelekea serikali zote za kidunia, kupendezwa kwetu na serikali ya Mungu, na jinsi fundisho letu linavyotegemeza umoja wa jamaa. Programu hiyo ikaja kuwa zungumzo la nchi na kufungua nafasi nyingi za kutoa ushuhuda.

Mipango ilifanywa ili kikundi hiki cha wamisionari kilichofumwa karibu karibu kikae kwenye kao la Betheli. Katika muda wa majuma machache, migawo mipya iliwasili kutoka Brooklyn, na wale wamisionari walitawanywa kwenda Belize, Ekwedori, El Salvador, Guatemala, na Honduras, isipokuwa Ndugu na Dada Thompson na Ndugu Edward Errichetti. Wao walipewa migawo ya kukaa katika Kosta Rika, na Ndugu Thompson akawekwa rasmi kuwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.

Bill na Mavis Rogers hawakufukuzwa pamoja na wale wamisionari wengine 19, kwa hiyo wao walibaki miezi mingine mitano katika Nikaragua. Baada ya kuwekwa katika ‘kizuizi cha nyumbani’ kwa majuma mawili katika hoteli moja, walihamishwa nchini wakaenda Kosta Rika katika Agosti. Wao pia walihojiwa kwenye TV. Walipoulizwa walikuwa wakifanya nini katika Nikaragua kilichofanya wahamishwe, Bill aliwaambia wale watazamaji wa TV, “Kuhubiri tu habari njema za Ufalme wa Mungu.” Halafu, kwenye programu iyo hiyo, askofu mkuu wa Kosta Rika alihojiwa. Yeye aliulizwa alichofikiri Wakristo wapaswa kuwa wakifanya leo. Yeye alikuwa hana budi kujibu, “Kuhubiri gospeli ya Ufalme.” Mwishowe, ndugu na dada Rogers waliondoka kwenda kwenye mgawo wao mpya katika El Salvador.

JAMAA YA BETHELI YAONGEZEKA

Jamaa ya Betheli ilikuwa ya washiriki wanne katika 1977. Lakini kwa sababu ya ongezeko la idadi ya wahubiri, kufikia 1982 walikuwako sita wakifanya kazi kwenye Betheli ili kutosheleza mahitaji ya makundi katika Kosta Rika na pia eneo jingine ambalo tawi liligawiwa. Katika 1980 ile alama ya 5,000 katika wastani ya wahubiri ilipitwa, na 1981 iliona kilele chenye kutokeza cha wahubiri 6,183. Kufikia 1981 makundi 118 yakiwa na mizunguko sita yaliripoti na katika 1982 hesabu hii iliruka kufikia makundi 138 katika mizunguko saba.

Mojapo kazi za kila mwezi za afisi ya tawi ni kuandalia kila mhubiri Huduma ya Ufalme Yetu. Ijapokuwa ilichapiwa Brooklyn, New York, katika 1965 Kosta Rika ilianza kujihariria Huduma ya Ufalme Yetu, hilo likiruhusu matangazo zaidi ya kwao yatiwe ndani. Ndipo hatua nyingine ya kusonga mbele ilipokuja katika Januari 1982, wakati Kosta Rika ilipoanza kujichapia Huduma ya Ufalme Yetu kwenye matbaa-ofseti yayo yenyewe. Katika kiangazi cha 1983, IBM Composer ilinunuliwa ili kuwezesha matbaa ndogo ifanye kazi za namna nyingi zaidi, na kufikia 1984 wafanya kazi zaidi ya kumi walihitajiwa katika Betheli ili kuangalia mahitaji ya makundi.

SABABU GANI BADILIKO?

Kwa miaka mingi, mwelekeo wa kinaya, na kuridhika ulikuwako miongoni mwa idadi ya watu wa nchi. Wengi walikuwa na kiburi cha kidini nao walikataa kuzungumza Biblia. Lakini kadiri hali za ulimwengu zilivyozidi kuwa mbaya, katika utimizo wa unabii wa Biblia, zikagusa zaidi maisha za watu, mioyo yao ilianza kutaka kujua maana yayo yote. Hatari za kiuchumi, harakati za wavamizi-haramu, na wakimbizi—hali zote hizi zilifungua njia kwa ajili ya huduma ya nyumba kwa nyumba yenye kuitikiwa zaidi, ikitokeza mafunzo ya Biblia zaidi. Hivyo, miaka ya 1982-87 imeleta nini? Sababu ya kushangilia! Kilele cha wahubiri kiliongezeka kutoka 6,611 kufika 10,374.

Sababu nyingine ya ongezeko ni kwamba jumla ya hesabu ya mapainia ilirudufika zaidi ya mara mbili ikafika 792. Tangu 1984, hesabu ya mafunzo ya Biblia ya nyumbani imepita hesabu ya wahubiri.

VIFAA VIPYA VYA TAWI

Katika Januari 1984 jitihada yote kuelekea ujenzi wa vifaa vipya vya tawi zilianzishwa. Katika 1955 tawi lilikuwa limejengwa katika kitovu cha San José. Halafu katika 1977 lilitengenezwa upya. Katika muda wa miaka michache tu, jengo la tawi lilikuwa limejaa pomoni. Maktaba ilikuwa na madawati manne, na nyakati nyingine wafanya kazi wa afisi walitumia vyumba vyao wenyewe kwa sababu ya kukosa nafasi katika afisi. Kumbi zilitumika kuwa ghala, nayo meza ya chumba cha mapakizi ikarudufika kuwa kitanda cha kuongezea. Chumba cha mazungumzo kiligeuzwa kuwa kiwanda cha kuchapia. Je! ulikuwa ni wakati wa kupanua?

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, washiriki wa Halmashauri ya Tawi walitafuta ardhi inayofaa. Mwishowe, kwa msaada wa Ndugu John Craddock, aliyejuana na watu katika sehemu ya biashara, mahali penye kufaa palipatikana: hekta 6.47 za ardhi yenye rutuba katika mandhari ya mashambani, kando tu ya Pan-American Highway kati ya kituo cha ndege cha Juan Santamaría na San José. Ardhi hiyo inazungukwa na majiji makubwa matatu na hata hivyo ni kubwa vya kutosha kuruhusu mpanuko wa wakati ujao. Ni mandhari yenye amani, yenye mazingira mazuri ya pinde-mvua nzuri zenye kuvutia kila siku na mawingu yenye kubadilika yakiteremka juu ya milima ya volkano.

Kufikia Mei 1984 ile ardhi ilikuwa imenunuliwa. Nafasi ya sakafu ilipangwa kuwa meta za mraba zaidi ya 4,200 ikilinganishwa na meta za mraba 550 za lile tawi la hapo kwanza. Msaada ulikuja kutoka kwa Wanabetheli, waangalizi wote wa mzunguko wa nchi, na wengi wa mapainia wa pekee, mapainia, na wahubiri wa kundi. Kuongezea hawa walikuwa wale wafanya kazi wa ujenzi wenye ujuzi kutoka United States, Kanada, Uholanzi, Ujeremani, Finland, Guatemala, na Panama. Wale wafanya kazi wa kutoka nchi za nje walijumuika kuwa zaidi ya 300, na kukaa kwao kulianzia siku chache kufika miaka kadhaa.

Kufikia wakati ule ujenzi ulimalizika, wahubiri karibu 5,000 kutoka makundi yaliyo mengi walikuwa wameshiriki ujenzi wenyewe. Waliobaki walikuwa na ushiriki kwa njia ya saa zao za bidii, kitia-moyo, na michango. Jitihada yote hii ilitolewa kwa sababu watu wa Yehova wanaitibari ahadi yake ya ‘kufanya kitu kikue.’—1 Kor. 3:7.

TAREHE IKAWEKWA

Kuwekwa wakfu, Januari 4, 1987! Nchi nzima ilialikwa. Ndugu Swingle na Underwood kutoka Betheli ya Brooklyn walitoa hotuba zenye kutia moyo za Kimaandiko, na kisha Milton Henschel, pia kutoka Betheli ya Brooklyn, akaeleza kusudi la ile pindi: kuweka wakfu vile vifaa kwa Yehova na masilahi Yake. Jua lilipokuwa likitua upande wa magharibi, wote 13,311 katika hadhirina walishukuru Yehova kwa roho yake na mwongozo wakati wa kile kipindi cha miaka miwili cha mradi wa ujenzi.

Hata katika wakati wa kipindi cha ujenzi, ilikuwa wazi ongezeko lilikuwa likiendelea. Vilele vipya 24 katika wahubiri vilifikiwa tangu ujenzi uanze. Kukiwa na vilele vipya vya wahubiri 10,374 na mafunzo ya Biblia ya nyumbani 13,425, ni wazi kwamba vile vifaa vipya upesi vitatumiwa kwa ukamili. Lile tawi jipya litatumikia mahitaji ya wale Mashahidi wa Yehova wa wakati ujao waliomo miongoni mwa wale 30,534 waliohudhuria Ukumbusho katika 1987.

LILILOTUKIA KWA WALE WASICHANA WA MIAKA YA 1940 NA KITU

Wawakumbuka wale wasichana mapainia wa miaka ya 1940 na kitu? Wako wapi sasa. Je! akina dada hawa walichoka? Sivyo hata kidogo! Wote wangali watendaji. Akina dada sita walihudhuria Gileadi, na wanne wangali wamisionari. Watano ni mapainia wa pekee, na watatu wanafanya upainia baada ya kulea jamaa zao au kufanya marekebisho katika ratiba zao.

Ni kwa sababu gani wao wameendelea wakiwa na shughuli nyingi katika kuhubiri Ufalme? Lila Swaby anajibu: “Kufanya kazi pamoja na wale akina dada watiwa-mafuta wa umri mkubwa zaidi tulipokuwa wachanga kulitujenga sisi. Sisi si wachanga tena, lakini kielelezo chao kinaendelea kuwa kichochezi kwetu sisi.”

PWANI YENYE UTAJIRI KWELI KWELI!

Ilifaa sana wakati Christopher Columbus alipoliita bara lile Pwani Yenye Utajiri, lakini kwa sababu zilizopita kuwaza kwake. Sasa, miaka zaidi ya 80 tangu ukweli ufike pwani hizi, zile hazina za Kosta Rika zimethibitika kuwa watu wayo ambao Mungu wao ni Yehova. Kusafishwa kwa utajiri huu kulikuja na ziara za Ndugu Knorr na wajumbe wengine wa pekee kutoka makao makuu ya Sosaiti. Kuwapo kwa wamisionari kulisogeza mbele kazi ya kuhubiri, na kukaimarisha makundi ambayo nayo yametokeza utajiri zaidi—wasifaji wa Yehova. Kweli kweli, Kosta Rika ni pwani yenye mali nyingi za kiroho!

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 199]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

COSTA RICA

NIKARAGUA

Bahari Karibea

WILAYA YA SAN CARLOS

Liberia

Guápiles

Grecia

Guácimo

Puntarenas

Alajuela

Siquirres

Puerto Limón

SAN JOSÉ

Cartago

Cahuita

Point Quepos

San Isidro

Golfito

BAHARI KUU PASIFIKI

PANAMA

[Picha katika ukurasa wa 202]

Wahubiri wa mapema wenye bidii, waliobatizwa karibu 1914: (juu, kushoto kwenda kulia) Claudia Goodin, Lea Wilson; (chini) Ina Williams

[Picha katika ukurasa wa 204]

Henry Steele na mke wake, Matilde, walibatizwa karibu 1914, wanaonyeshwa pamoja na jamaa. Wengi wa watoto wao, wajukuu, na vitukuu ni Mashahidi watendaji leo

[Picha katika ukurasa wa 209]

Albert Ezra Pile, aliyebatizwa katika 1926, alisaidia kuchochea moto wa kazi

[Picha katika ukurasa wa 213]

Kikundi cha kwanza cha wamisionari. Safu ya kwanza, kushoto kwenda kulia: Charles Palmer; Lora Lea Palmer; Hermena Siebenlist, Theodore Siebenlist, mtumishi wa tawi tangu 1944 kufika 1952. Safu ya nyuma, kushoto kwenda kulia: William Eugene Call, Donald Burt, na “Woody” Blackburn

[Picha katika ukurasa wa 217]

“Dak” na Emily Hardin walitumikia katika kazi ya mzunguko na walisafiri sana kwa gari-moshi

Arnold Williams, mwangalizi wa mzunguko wa kwanza mwenyeji aliacha kazi yenye matazamio mazuri ili kuhubiri habari njema

[Picha katika ukurasa wa 218]

Evelyn Ferguson (sasa ni Taylor), painia wa pekee tangu 1944, anaonyeshwa akiwa na kinanda chake

[Picha katika ukurasa wa 225]

Silbert Spence, akichochewa na hotuba iliyorekodiwa ya Ndugu Rutherford “Dini Ni Mtego Na Hila,” alianza kufanya upainia pamoja na mke wake Valmina, katika 1948. Mshiriki wa Halmashauri ya Tawi mpaka kifo chake Mei 1985

[Picha katika ukurasa wa 233]

Lorence Shepp ambaye ametumikia akiwa mratibu wa Halmashauri ya Tawi tangu 1966, akiwa na mkeye, Olimpia

[Picha katika ukurasa wa 239]

Frederick Hiltbrand, anaonyeshwa hapa akiwa na Mirtha, mke wake, alisaidia kuanzisha utendaji wa chapa

[Picha katika ukurasa wa 250]

Tawi jipya linavyoonekana ukiwa angani, likiwa na duara afisi-mapokezi mbele, matbaa, mapakizi, na afisi zikiwa kushoto, na makazi kulia

[Picha katika ukurasa wa 252]

Wasichana mapainia wa miaka ya 1940 na kitu wangali wana roho ya painia. Kushoto kwenda kulia: Jenny Taylor; Evelyn Taylor; Mireya Ortega; Jenny Dillon; Corina Novoa; Lila Swaby

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki