Kwa Sababu Gani Kuoa Wanawake Wengi Kuliruhusiwa
WAKATI Yesu Kristo alipokuwa duniani alitangaza kanuni ya Mungu kuhusu ndoa. Alipoulizwa kama mwanamume aweza kutaliki mkewe “kwa kila sababu,” Yesu alijibu: “Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”—Mt. 19:3-6.
Kwa hiyo, Mkristo wa kweli hawezi kuoa wake wengi. Mtume Paulo aliandika akifuata uongozi wa Yesu, akasema hivi: “Kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe.” (1 Kor. 7:2) Alishauri pia kwamba “mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.” (1 Kor. 7:10, 11) Paulo pia aliandika juu yake mwenyewe na Wakristo wenzake waliokuwa wakiongoza wakiwa mifano kwa wengine: “Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu [si ‘wake walio ndugu’], kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana na Kefa?”—1 Kor. 9:5.
Kwa hiyo, kwa kuwa kanuni ya Mungu kwa Wakristo ni mke mmoja au mume mmoja, kwa sababu gani Mungu aliruhusu watu wake wa kale wa Israeli wawe na wake zaidi ya mmoja?
HISTORIA FUPI YA KUOA WAKE WENGI
Kuoa wake wengi hakukuanza kati ya wale waliokuwa waabudu wa kweli wa Yehova Mungu. Maandishi ya kwanza ya kuoa wake wengi yahusu Lameki, mzao wa Kaini asiyeaminika. (Mwa. 4:19) Lakini mtumishi wa Mungu Nuhu alikuwa na mke mmoja tu, kama kila mmoja wa wana wake watatu. (Mwa. 7:13; 1 Pet. 3:20) Rafiki ya Mungu Ibrahimu alikuwa na mke mmoja, Sara. Lakini Sara, aliyekuwa tasa kwa muda mrefu, kwa kujua kwamba Ibrahimu alikuwa ameahidiwa “uzao,” alimsihi afanye ngono na kijakazi Mmisri wa Sara, Hagari, ambaye kwa njia hiyo akawa suria wa Ibrahimu. (Mwa. 16:1-4) Isaka mwana wa Ibrahimu, aliyezaliwa na Sara baadaye kwa mwujiza, na ambaye ndiye aliyekuwa “uzao” ulioahidiwa, alikuwa na mke mmoja tu. (Mwa. 21:2, 12; 24:67) Walakini, Yakobo mwana wa Isaka alikuwa na wake wawili kwa sababu ya kufanyiwa hila na baba-mkwewe Labani. Yakobo alikuwa na masuria pia.—Mwa. 29:21-29; 30:1-13.
Kwa hiyo Torati ilipotokea, haikuruhusu kuoa wake wengi wala kuwa na masuria, wala haikutia watu moyo wawe na mazoea hayo. Kwa kweli, kuoa wake wengi hakukuzoewa na watu wengi katika Israeli ya kale; sana sana kulifanywa na walio mashuhuri zaidi na wenye utajiri, ingawa si hao peke yao. (Amu. 8:30; 2 Nya. 11:21) Kati ya mataifa kuwa na wake wengi kulikuwa kama ‘ishara ya cheo’ cha mtu.—2 Sam. 16:20-22.
Mitajo katika Zaburi, Mithali na Mhubiri juu ya ndoa zenye furaha inaelekea kusema hasa juu ya kuoa mke mmoja tu. “Umfurahie mke wa ujana wako,” yasema Mithali 5:18. Na Mhubiri 9:9 yashauri: “Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.” (Linganisha Zaburi 128; Mithali 18:22; 31:10-31.) Tena, hatari ya kuoa wake wengi ilikaziwa katika shauri la Mungu kwa wafalme: “Wala [mfalme] asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke.” (Kum. 17:17) Mfalme Sulemani alipuza onyo hili, akaona majonzi.—1 Fal. 11:4-6.
TORATI YA MUSA ILIVUNJA WATU MOYO WASIOE WAKE WENGI, IKALINDA WANAWAKE
Mipango ya Torati ilipangwa kwa njia ya kuvunja watu moyo wasioe wake wengi. Kila mara mwanamume alipofanya ngono na mkewe alikuwa mchafu kwa siku moja, kwa njia ya kidini. (Law. 15:16, 17) Hivyo, ilikuwa vigumu kwa Mwebrania kufanya ngono na wake wengi mara kwa mara, kwa maana uchafu ulizuia mwanamume asifanye ngono mara nyingi. (Law. 7:20, 21; 1 Sam. 21:3-5; 2 Sam. 11:11) Pia, sheria za urithi zilitaka mwanamume ampe mwana mzaliwa wake wa kwanza urithi maradufu, hata ikiwa huyo alikuwa mwana wa mke asiyependwa sana na mume huyo. (Kum. 21:15-17) Katika pande hizo, kuoa wake wengi hakukuwa jambo la kutamanika.
Hata ingawa kuoa wake wengi kuliachiliwa, Torati ililinda wanawake, ikawapa wanawake wa Kiebrania cheo cha juu zaidi na chenye kuheshimiwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika mataifa mengine. Ikiwa mwanamume alitongoza bikira asiyeposwa, alitakiwa amwoe, na asingeweza kumtaliki kamwe. (Kum. 22:28, 29; Kut. 22:16, 17) Ikiwa mwanamume alishtaki mkewe kwa uongo kwamba hakuwa bikira walipooana, asingeweza kumtaliki kamwe. (Kum. 22:13-21) Pia, mwanamume mwenye wake wengi alitakiwa kumpa mke wake asiyempenda sana riziki kamili na haki yote ya ndoa. (Kut. 21:10, 11) Msichana bikira wa kigeni aliyetekwa vitani akawa mtumwa angeweza kutwaliwa awe mke na askari mwenye kumteka. Lakini ikiwa baadaye alimfukuza kwa sababu hakumpendeza, asingeweza kumwuzia mtu mwingine. Alipaswa kumwacha mke huyo aende zake kama atakavyo. (Kum. 21:10-14) Kuruhusu askari waoe bikira waliowateka kulikuwa baraka kwa wasichana hao, kwa sababu kama wasingaliolewa wasingalikuwa na nyumba wala rafiki.
Tena, mwanamume asingeweza kutaliki mkewe bila sababu yenye kufaa. Alipaswa kumwandikia hati ya kisheria ya talaka. Hiyo ilihitaji mkuu fulani wa watu awe shahidi na jambo hilo laelekea lingefanywa mbele ya wazee wa mji, ili watoe ruhusa rasmi. Mpango huu, pamoja na sheria ya ziada iliyosema mwanamume asingeweza kumwoa tena mke huyu akiisha kuolewa na mwanamume mwingine ambaye alikufa baadaye au akamtaliki, ulizuia talaka za haraka haraka au za ovyo ovyo. (Kum. 24:1-4) Tena, hati ya talaka ilikuwa ushuhuda wa kisheria kuonyesha mwanamke huyo anaweza kuolewa tena. Ilimlinda asishtakiwe umalaya au uzinzi.—Linganisha Kumbukumbu la Torati 22:13-21.
“WAKATI WA MATENGENEZO MAPYA”
Kwa hiyo ingawa Mungu alipunguza kuoa wake wengi, hakuona ilifaa kumaliza kabisa desturi hiyo kati ya watu wake wakati huo, kama vile asivyomaliza kabisa utumwa, bali akaupunguza tu. Haukuwa bado wakati wake wa kurudisha mambo yote kwenye cheo chake kikamilifu. Mwandikaji wa kitabu cha Biblia cha Waebrania amtaja Yesu kama anataja habari ya dhabihu nyingi za wanyama walizotoa Wayahudi, kwa kusema: “Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari.” (Ebr. 10:5) Mpango wa Torati wa kutoa dhabihu za wanyama ulikuwa kivuli tu, si kitu chenyewe. Yesu Kristo ndiye aliyetoa dhabihu yenye kutosha kabisa ili aondoe dhambi. Mwandikaji anasema juu ya dhabihu na sehemu nyingine za Torati na kunena hivi: “Ni sheria za jinsi ya mwili tu, vyakula na vinywaji na kutawadha kwingine kwingine, zilizoamriwa hata wakati wa matengenezo mapya”—Ebr. 9:10.
Kwa hiyo, Yesu Kristo alipotokea duniani wakati ulifika wa kuanza kutengeneza mambo. Yeye alifahamisha watu waziwazi kanuni ya Mungu ya kuoa mke mmoja tu, na ya talaka inayopatana na Maandiko ikitegemea sababu za uzinzi tu. (Mt. 19:9). Alipoulizwa na Mafarisayo sababu gani Mungu hakufikiliza kanuni hii juu ya Israeli, Yesu alijibu: “Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.”—Mt. 19:7, 8.
Kupatana na aliyosema Yesu, Yeremia nabii alikuwa ametabiri zamani sana kwamba kungekuwa na badiliko katika matendo ya Mungu wakati ambapo agano jipya, lenye kutegemea dhabihu ya Kristo, lingekuja. Yeremia alisema. “Angalia, siku zinakuja, asema [Yehova], nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. . . . Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika.”—Yer. 31:31-33; Ebr. 10:16-18.
Agano jipya lingelainisha ugumu wa mioyo ya wenye kuingizwa ndani yalo. Kuamini dhabihu ya Kristo kungeondoa maono ya kujisikia wenye dhambi, jambo ambalo halikuweza kufanywa kamwe na dhabihu za wanyama. Sheria ya agano hili isingeandikwa katika mbao za mawe. Ingeandikwa juu ya mioyo. Ingewapa dhamiri safi, jambo ambalo Torati haikufanya.—Ebr. 9:13, 14.
Zaidi ya hilo, twaona kwamba hata Kristo alipokuja, si mambo yote yaliyotengenezwa mara moja. Baada ya kufundisha wanafunzi wake miaka mitatu na nusu, Yesu aliwaambia hivi usiku uliotangulia kifo chake: “Bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.” (Yohana 16:12) Wanapojaribu sana kufikia kanuni kamilifu ya Mungu, wanadamu hawawezi kufanya mabadiliko yote ya lazima maishani mwao mara moja, hawawezi kufanya yote katika kipindi kifupi. Kwa mfano, Wakristo Waebrania wa zamani walikuwa na mengi ya kujifunza juu ya kujitenga na mengi ya mapokeo ya Kiyahudi. Mtume Paulo alilazimika kuwanyosha kuhusu kuadhimisha kwao siku fulani kama takatifu kuliko nyingine, kuhusu kula, kuhusu kutahiriwa, na kadhalika. Kwa upendo na huruma Mungu hakuona ilifaa kuwalemeza na mabadiliko yote hayo kwa wakati mmoja.—Rum. sura 14; Matendo 15:1-29.
Ndivyo ilivyokuwa kwa habari ya kuoa wake wengi. Kwa sababu ya “ugumu wa mioyo” ya Wayahudi Mungu hakuleta badiliko. Wakati huo halikuwa la maana. Ni kama mtume Paulo aelezavyo: “Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi.” “Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo. . . . Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.” (Gal. 3:19, 23-25) Mungu aliwafanya Wayahudi wawe taifa lililo peke yake kwa kuwapa Torati. Lakini hata katika mpango wake wa kupunguza kuoa wake wengi wao walikuwa tofauti, kwa maana hakuna lo lote la mataifa yale mengine lililokuwa na sheria hizo.
Huruma ya Yehova na uongozi wa hatua hatua kwa watu wake unaonekana wazi katika jambo hili la kuoa wake wengi. (Zab. 103:10, 14) Mungu anao wakati wake wa kutimiza sehemu fulani za kusudi lake anapoondoa wanadamu katika hali ya chini sana ya dhambi. Itachukua miaka elfu ya utawala wa Mwanawe Yesu Kristo kuondoa kabisa matokeo yote ya dhambi na kuleta wanadamu kwenye hali ya ukamilifu, ambapo hawatazuiwa tena na dalili zo zote za “ugumu wa mioyo” na kwa hiyo wanaweza kuishi kulingana na kila upande wa kanuni kamilifu ya Mungu. Yatupasa tushukuruje kwa saburi na fadhili zake zisizostahilika!—Rum. 8:21; 11:33-36.