Miujiza na Mizuka— Je! Ni Ishara Zitokazo kwa Mungu?
“MIUJIZA leo ingali yachukuliwa kuwa . . . namna fulani ya barua ya pendekezo, uhakikisho kamili wa kwamba ujumbe ni wa kweli na umetoka kwa Mungu, kwamba yeye amethibitisha utume au neno fulani lenye kutoka kwake kwa kuutia muhuri wa uweza wake wote.” Miujiza yenye kurejezewa hapa na Joseph Vandrisse, mchangaji habari kwenye karatasi-habari ya kila siku Le Figaro ya Kifaransa, ni ile ambayo kwa asili yakubaliwa na Kanisa Katoliki. Lakini ni viwango gani ambavyo kanisa hutumia ili kuamua kama muujiza au mzuka watoka kwa Mungu kikweli?
Je! Kanisa Lapaswa Kuamua Kisa Chalo Lenyewe?
Kulingana na wenye mamlaka Wakatoliki, ili mizuka iwe ya kweli ni lazima itimize masharti mawili. Kwanza, ni lazima ipatane na mafundisho ya kanisa. Kielelezo cha kutokeza sana ni ule mzuka uliotokea Lourdes, ambako “Bikira” alijionyesha mwenyewe kuwa ndiye “Mchukuliwa Mimba Asiye na Dhambi ya Asili.” Kwa kupendeza, miaka michache iliyopita kabla ya jambo hilo, Papa Pius 9 alikuwa ameamrisha kwamba Mariamu alipochukua mimba alihifadhiwa awe huru na dhambi ya asili. Katika 1933 Pius 12 wa wakati ujao alieleza maoni yake ya kwamba matukio hayo mawili yalihusianishwa, akitaarifu hivi: “Yule Bikira Asiye na Dhambi ya Asili, Mama ya Mungu na mbarikiwa miongoni mwa wanawake, alitaka kuthibitisha kwa midomo yake mwenyewe jambo lile ambalo lilielezwa wazi katika Roma na Pontifu wake [Papa] Mkuu Zaidi asiyeweza kukosea. Yeye [bikira] alifanya hivyo muda mfupi baadaye katika mzuka maarufu kwenye Kipango cha Massabielle [Lourdes].”
Pili, ni lazima mwenendo wa mtu aliyeona mzuka huo ufikiriwe. Kama vile askofu wa Tours alivyotaarifu: “Kanisa . . . liliamini katika mizuka hiyo [ya kule Lourdes] kwa sababu ya utakatifu wa Bernadette.” Na wenye mamlaka wa kidini huchukua kwamba wote wawili Bernadette na Lucie, ambao mmoja wao alidai kwamba alimwona Mariamu kule Lourdes na yule mwingine akamwona kule Fátima, walitimiza sharti hilo kwa kuwa watawa wa kike baadaye.
Ujumbe walioutoa ulipatana na fundisho la Kikatoliki. Maisha za wananjozi hao zilipatana na kiolezo kilichosimamishwa imara na kanisa. Katika visa hivi, haishangazi kwamba mizuka yenye kutambuliwa na Kanisa Katoliki yathibitisha mapokeo na mafundisho yaliyo katika kanisa hilo peke yalo, hata mizuka ile ya majuzi zaidi, kama ule wa Mchukuliwa Mimba Asiye na Dhambi ya Asili.
Lakini je! kwa kweli miujiza na mizuka ni ishara zitokazo mbinguni kuthibitisha ukweli wa mafundisho ya kanisa? J. Bricout, mhariri wa Dictionnaire pratique des connaissances religieuses (Kamusi ya Maarifa ya Kidini), alinukuu mtungaji mwingine Mkatoliki, P. Buysse, aliyeandika hivi: “Kwa kuwa miujiza ya Lourdes ina ukamatano wa wazi na ‘imani zilizo za Kanisa Katoliki peke yalo’ (Mchukuliwa Mimba Asiye na Dhambi ya Asili, maelezo yenye kutolewa na mamlaka ya kipapa kuhusu fundisho hili lenye kushikiliwa kwa ushupavu, kuheshimiwa sana kwa ile Sakramenti Iliyobarikiwa, kuheshimiwa sana kwa Bikira Mariamu, na kadhalika), mtu aweza, au ingefaa zaidi kusema, ni lazima mtu atambue kwamba ‘mafundisho ya kanisa yana muhuri wa kibali cha Mungu.’”
Hata hivyo, Kanisa Katoliki haliwezi kwa haki kudai kwamba lina idhini hiyo ya kimungu. Kwa kujichukulia lenyewe mamlaka ya kuamua kama mizuka (na miujiza yenye kushirikiana nayo) hutoka au haitoki kwa Mungu, linajisimamisha kuwa hakimu wa kesi yalo lenyewe.
Dini nyingine nyingi hudai eti zina ushuhuda wa miujiza na kudai kuwa zaungwa mkono na Mungu. Je! Mungu aunga mkono miujiza ambayo hufanywa katika harakati za kikarisma (kutia na zile zisizo za Kikatoliki) au hata katika dini zisizo za Kikristo? Ni vigumu kuamini kwamba yeye hufanya hivyo, kwa maana Biblia yatuambia kwamba Mungu “si Mungu wa machafuko, bali wa amani.”—1 Wakorintho 14:33.
Ni nini msingi sahihi wa kuhukumu? Kitabu Les signes de crédibilité de la révélation chrétienne (Ishara za Kuaminika kwa Ufunuo wa Kikristo) kilieleza kwamba viwango vya kuona muujiza kuwa wa kweli huwa hasa vya kiadili na vya kidini.
Je! Ni ya Kweli Kulingana na Ufunuo?
Kulingana na watungaji mbalimbali Wakatoliki, “takwa la Kwanza ni kwamba ujumbe wenye kutolewa uwe wa kweli kulingana na ufunuo wa Gospeli na pokeo la mafundisho ya kanisa.” “Hakuna ufunuo wowote mpya uwezao kutia marekebisho katika ufunuo ule wa kwanza.” Pia, Papa John Paulo 2 alieleza kwamba “ujumbe uliotolewa kule Fátima katika 1917 ni ukweli mtupu wa ile Gospeli.” Yote haya yamaanisha kwamba zaidi ya yote, ujumbe wenye kutolewa na mizuka hiyo ni lazima upatane na ule “ufunuo,” Maandiko Matakatifu. Je! kweli hivyo ndivyo mambo huwa?
Ni maneno gani yaweza kukatwa kutokana na njozi za helo yenye moto ambayo wale wachungaji walipewa katika Fátima? Maandiko yaonyesha wazi kwamba watenda dhambi hawaadhibiwi kwa njia hii wakifa. Yesu mwenyewe alitaarifu kwamba twapaswa kuhofu yule Mmoja awezaye kuharibu vyote viwili nafasi na mwili, hivyo akionyesha kwamba nafsi yaweza kufa. Maandiko mengine ya Biblia yafundisha wazi kwamba hakuna fahamu katika kifo na kwamba tumaini la kuishi tena lategemea msingi wa ahadi ya Biblia ya ufufuo wa wakati ujao.—Mathayo 10:28; Mhubiri 9:5, 10; Yohana 5:28, 29.
Na namna gani “Mchukuliwa Mimba Asiye na Dhambi ya Asili” aliyenenwa na Bernadette? Huo tena ni upinganisho wa fundisho la Biblia. Maandiko yaonyesha kwamba Mariamu, kama wazao wote wa Adamu, ‘alichukuliwa mimba katika dhambi’ na akarithi kifo. (Zaburi 51:5; Warumi 3:23) Ikiwa Mariamu alichukuliwa mimba bila dhambi, mbona yeye akatoa toleo la dhambi baada ya kuzaliwa kwa Yesu? (Walawi 12:6; Luka 2:22-24) Zaidi ya hilo, hakuna andiko hata moja la Biblia la kuunga mkono fundisho la Kikatoliki lisemalo kwamba yeye alihifadhiwa awe bila dhambi ya asili kwa neema ya pekee. Kwa kuwa ibada ya Mariamu haina msingi wa Kimaandiko, yafaa kabisa kutokeza maswali juu ya kama mizuka yake hutoka kwa Mungu.
Je! Ingeweza Kuwa Yatoka Kwenye Chanzo Kingine?
Bila shaka, wanachuo wa Biblia wajua kwamba si ishara zote za kimuujiza ambazo hutoka kwa Mungu. Baada ya kutaja miujiza ambayo wanamizungu Wamisri walifanya mbele ya Farao na Musa, Dictionnaire de la Bible, iliyohaririwa na F. Vigouroux, yataja kwamba “katika siku za mwisho, manabii bandia na Makristo bandia, wote wakiwa mawakili wa Ibilisi, watafanya miujiza mingi kufikia hatua ya kudanganya wanafunzi wenye imani wa Yesu Kristo wenyewe, kama hiyo ingewezekana.”—Mathayo 24:24; Kutoka 7:8-13.
Lakini namna gani ikiwa, kama ilivyokuwa katika kisa cha kule Fátima, mzuka wenyewe hualika aina ya binadamu kutubu na kuwaomba waamini wasali ili watenda dhambi waongolewe? Kwa kupendeza, kitabu kimoja chenye kupendelea mizuka, chenye kichwa Fátima—Merveille du XXe siècle (Fátima—Staajabu la Karne ya 20), chanukuu kwamba yule padri, ambaye wakati huo alikuwa katika Fátima, alionyesha mashaka yake kuhusu asili ya ujumbe huu mbalimbali hata kama una mambo gani. Yeye alitaarifu hivi: “Hata vingeweza kuwa ni viinimacho vya roho waovu.” Kwa kweli, Biblia yaonyesha kwamba Shetani “huenda akisingizia kuwa malaika wa nuru” na kwamba “watumishi wake, pia, husingizia wenyewe kuwa watumishi wa uadilifu.” (2 Wakorintho 11:14, 15, The Jerusalem Bible) Kwa hiyo kuwako kwa ujumbe wenye kusikika kuwa wenye kuaminika si uthibitisho wa kwamba kwa kweli mzuka fulani hutoka kwa Mungu.
Shauri hilo ndilo pia lililokatwa na Dictionnaire historique de la Bible [ya Kikatoliki] ya Calmet, ambayo yataarifu hivi: “Miujiza na ajabu haiwi sikuzote ishara hakika kwamba wale wanaoifanya ni watakatifu wala kwamba fundisho lao ni sahihi, wala si ushuhuda hakika wa kwamba wananjozi hao walipokea utume fulani.”
Tofauti na hivyo, Kristo alifanya miujiza mingi akiwa duniani. Kusudi lake lilikuwa nini, nayo yaangaza nuru gani juu ya miujiza na ajabu za leo? Maswali haya yatajibiwa katika makala inayofuata.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Desemba 9, 1531.
Mhindi Mmeksiko, jina lake Juan Diego, alikuwa akiharakisha kwenda Misa katika Jiji la Meksiko. Njiani alikutana na bibi mmoja aliyemtuma akamwombe askofu wa Jiji la Meksiko kujenga kanisa katika ardhi ile ile ambapo bibi huyo alisimama. Kidogo askofu huyo alitia mashaka kuhusu ujumbe wa Mhindi huyo.
Kwenye mzuka fulani uliofuata, bibi huyo alijijulisha kuwa ndiye mama ya yule Mungu wa kweli na baadaye kidogo kuwa ndiye “Mariamu Mtakatifu wa Guadalupe.” Ili ampe Juan Diego ishara fulani, bibi huyo alimwambia akusanye mawaridi fulani, ingawa hayo hayakuwa majira ya maua hayo wala hayakuwa yakipatikana mahali hapo. Hata hivyo, Juan aliyapata maua na kuyafungilia katika joho lake. Alipokuwa akimpa askofu maua hayo, umbo la mfanano na ukubwa wa yule “Bikira” lilitokea katika joho lake.
Mchoro wa tamasha hiyo waonyeshwa leo katika Basilika ya Guadalupe, karibu na Jiji la Meksiko.
[Picha]
Guadalupe
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Februari 11, 1858.
Msichana Mfaransa wa miaka 14 jina lake Bernadette Soubirous, akiwa na dada yake, na rafiki walikuwa nje wakikusanya kuni karibu na Lourdes, mji mmoja katika Ufaransa ya kusini-magharibi karibu na mpaka wa Kihispania. Bernadette akiwa ndiyo sasa tu anaenda kuvuka kijito, “bibi” mmoja alimtokea katika kipango. Katika pindi nyinginezo, “bibi” uyo huyo aliomba kwamba kikanisa kijengwe mahali hapo hapo na akasihi kwamba aina ya binadamu yote itubu.
Kwa kukutana na mzuka mwingine bado, Bernadette alimsikia “bibi” huyo akisema hivi katika kilugha kile cha huko: “Mimi ndimi Mchukuliwa Mimba Asiye na Dhambi ya Asili.” Akijitetea peke yake dhidi ya wenye mamlaka wa kiserikali na hata wa kidini, Bernadette Soubirous alishikilia kwamba majulisho yake yalikuwa ya kweli. Mwishowe, Kanisa Katoliki liliitambua kirasmi ile mizuka ya “Bikira.” Tokeo la jambo hilo likawa ni kuwapo kwa pale mahali patakatifu pa kule Lourdes.
[Picha]
Lourdes
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Mei 13, 1917.
Mchungaji mchanga na wachungaji wawili wa kike walikuwa wanalinda makundi yao kule Fátima, katika Ureno ya katikati, wakaona huo mzuka wao wa kwanza wa yule “Bikira.” Wakati wa mzuka mmoja wa baadaye, watu waliharakisha kwenda mahali hapo kwa matumaini ya kupokea ishara. Walidai kuwa waliona jua likiyumbayumba katika mbingu halafu likaanguka duniani.
Pia watoto hao walipokea “mambo ya siri.” Waliona njozi ya helo, ambako waliona watenda dhambi wakiteseka vibaya sana katika miali mikali sana ya moto. Pia “Bikira” huyo aliomba kwamba Urusi itengwe kwa utumizi mtakatifu wa “moyo [wake] usio na dhambi ya asili.” Mapapa wa baadaye walitimiza takwa lake. “Siri” moja ya mwisho imelindwa na wale walio na mamlaka ya juu zaidi katika Kanisa Katoliki, na kwa sasa wao hukataa kujulisha watu siri hiyo.
[Picha]
Fátima