Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 4/8 kur. 11-13
  • Je! Mapenzi Ni Kama Yalivyo Katika Nyimbo za Mapenzi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Mapenzi Ni Kama Yalivyo Katika Nyimbo za Mapenzi?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Masomo Yaliyo Katika Nyimbo za Mapenzi
  • Maneno ya Nyimbo Zenye Kutoboa Mambo Wazi
  • “Wakati wa Kupenda”
  • Dokezo la Kujifunza
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2023
  • Nyimbo Zinazotusaidia Kumkaribia Mungu Zaidi
    Jinsi Michango Yako Inavyotumiwa
  • Msifu Yehova kwa Shangwe Kupitia Nyimbo
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2018
  • Mwimbieni Yehova!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 4/8 kur. 11-13

Vijana Wauliza . . .

Je! Mapenzi Ni Kama Yalivyo Katika Nyimbo za Mapenzi?

NYIMBO za mapenzi—nyimbo ambazo zatukuza mapenzi ya kweli, nyimbo ambazo zaomboleza mapenzi yaliyopotezwa—ndilo jambo kuu katika mawimbi ya redio. Na hata kama zitakuja kwa kisingizio cha midundo gani, ya polepole na yenye kutia majonzi, ya kuchochea hisia kama soli na popu, au ya makelele kama roki, zina umaarufu mwingi miongoni mwa vijana-matineja. Sababu ni nini?

Ni kwamba tu nyingi za nyimbo hizo zina uvutio imara wa kimuziki—melodia zenye sauti tamu, maneno yenye kupasua moyo kwa utamu, midundo iwezayo kuchezewa dansi. Hugusa hisia za moyoni na zaweza kufanyiza tabia ya moyoni ambayo hukaribia kupumbaza fikira za mtu kuhusiana na mahaba. “Ikiwa mimi naongea na msichana wangu kwenye simu kuhusu hali yenye ugumu fulani na maneno yangu yakose kutiririka,” asema kijana mmoja aitwaye Rusty, “wimbo mzuri wa mapenzi wenye kusikika mbali nyuma yangu hunitia hali ya raha, na maneno hunijia kwa urahisi zaidi.”

Hata hivyo, kitu ambacho hufanya nyimbo za mapenzi ziwe maarufu si ustahili wowote wa kimuziki tu ambao waweza kuwa katika tyuni (mahadhi) zile. Uwapo kijana-tineja, hapo huwa unajifunza jinsi ya kushughulika na hisia zako za ngono. Kwa kutaka kujua mafumbo ya mapenzi na mahaba, huenda kwa urahisi ukajihusisha na nyimbo zenye kueleza raha na maumivu ambayo hutokana na kufanya matembezi ya kirafiki na kuvunja uhusiano. Kama vile mwandikaji mmoja awekavyo wazo hilo, kupitia nyimbo za mapenzi, vijana-matineja “waweza kuonja kidogo jinsi mapenzi yalivyo, na hivyo wapate kadiri fulani ya raha na mitamauko ya mapenzi.”

Kwa kukosa ujuzi katika njia za mahaba na labda kwa kukosa uhakika juu ya kama wana uwezo wa kuonyesha hisia zao, watu fulani hata hutegemea nyimbo za mapenzi ndiyo wapate maneno yafaayo ya kumwambia fulani huyo wa pekee. Vijana fulani hukiri kwamba wamepata kujaribu kunasa watu wa jinsia tofauti kwa kuwaambia vijineno walivyovitoa moja kwa moja katika nyimbo zilizo maarufu. Lakini ni kwa kadiri gani hasa nyimbo za mapenzi hufundisha vijana kuhusu mapenzi?

Masomo Yaliyo Katika Nyimbo za Mapenzi

Kwanza, fikiria mmoja wa nyimbo nzuri zaidi za mapenzi ambazo zimepata kuandikwa. Huo ni ule Wimbo Ulio Bora (Wimbo wa Sulemani), na ndio usimulizi wa Biblia wa msichana mzuri Mshulami mwenye mapenzi kwa mvulana mchungaji. Mapenzi yao yatishwa kuharibiwa na Mfalme Sulemani, ambaye, akiwa na utukufu wake wenye kumetameta, hekima, na utajiri, ajaribu kuiba moyo wa msichana huyo—lakini wapi. Kumbe mapenzi yake yakathibitika kuwa ya namna isiyo na ugeugeu. Msichana mchanga huyo alitangaza hivi: “Usisitizo wa kufuata ujitoaji usiohusisha ndani wengine uko kama Sheoli kwa kutokubali kuacha nafasi ya wazi. Miwakowako yao ni kama miwakowako ya moto, ule mwali wa Yah.”—Wimbo wa Sulemani 8:6, NW.

Je! nyimbo za mapenzi leo zaendeleza vivyo hivyo maoni yaliyotukuka, lakini yenye kulingana na hali halisi, kuhusu mapenzi ya kimahaba? Ni kinyume kabisa. Mwandikaji Sally Helgesen aonelea kwamba nyimbo za mapenzi “huadhimisha ulimwengu wa hali zenye kufurahisha sana na nyege zenye kuumizwa sana, ambamo mapenzi” mara nyingi ndiyo hutafuta “azimio [lililo] kamilifu.” Jambo la kusikitisha ni kwamba, ‘maazimio makamilifu’ ni machache sana, na kuyatafuta ni kualika mvurugiko wa akili. Naam, hata mashairi bora ya Sulemani yalishindwa kumfanikisha kuyapata mapenzi ya yule msichana Mshulami! Helgesen aongezea hivi: “Nyimbo hizo huamsha mawazio kombokombo kuhusu maisha ya utu mzima ambamo nyege za kimahaba huwaka zikamaliza kila hisia-moyo nyingineyo na daraka lenye kuhusika huonekana kuwa lisilolemea mtu yeyote.” Hapa tena, hayo ni mawazio yaliyo kinyume kabisa na maisha halisi.

Sheila Davis, profesa wa kuandika maneno ya nyimbo kwenye Chuo Kikuu cha New York, asema kwamba nyimbo tena hupumbaza watu wawaze kwamba kuwa na wajibu wa kutimiza ni “jambo la kizamani.” Hata hivyo wazo jingine kubwa lililo maarufu katika nyimbo za mapenzi ni kwamba mapenzi hutokea papo kwa hapo. Wimbo mmoja ulio maarufu ulijulisha kwamba mapenzi yalitokea “ghafula” baada ya “salamu ya kwanza” na “tabasamu ya kwanza.” Hivyo nyimbo za mapenzi hufundisha kwamba mapenzi ni yenye upofu, yakitambua sifa za uthabiti wa mtu lakini yakikataa kuona hata sifa za unyonge ulio wazi kabisa.

Masomo hayo yana uhalali gani? Basi, fikiria hivi: Je! maoni ambayo huingia akilini mara ya kwanza kuhusu mtu yaweza kweli kuwa msingi wa uhusiano wenye kudumu? Ni vigumu. Angalia jinsi Biblia yaeleza mapenzi (upendo) ya kweli: “Upendo ni wenye saburi na fadhili . . . Upendo hauna tabia mbaya wala si wenye ubinafsi wala si wenye kuudhika-udhika . . . Upendo hauchoki kamwe kwa kushindwa; na imani, tumaini na saburi yao haishindwi kamwe. Upendo ni wa milele.”—1 Wakorintho 13:4-8, Today’s English Version.

Hivyo mapenzi halisi hayatukii papo hapo, wala hayahusishi hisia na nyege tu. Mapenzi yenye ukomavu yana macho; huona sifa za uthabiti wa mtu lakini hayapuuzi sifa za unyonge wake. Mapenzi halisi husitawishwa kwa kipindi fulani kwa kadiri ambavyo mtu ajipatia maarifa kuhusu utu na sifa za mwingine—“yule mtu wa siri wa moyoni.” (1 Petro 3:4, NW) Mapenzi halisi hayaepi kujifunga katika wajibu; hudumu katika uhusiano na kujitahidi kufanya maendeleo hata mambo yakiwa magumu. Lo, mapenzi halisi yatofautiana kama nini na mapenzi ambayo huelezwa mara nyingi katika nyimbo!

Maneno ya Nyimbo Zenye Kutoboa Mambo Wazi

Pia nyimbo za mapenzi huelekea kufanya mapenzi (upendo) na ngono yaonekane kuwa jambo moja—somo ambalo hufunzwa siku hizi kwa kusema mambo wazi kabisa kwa njia yenye kugutusha. Ni kweli kwamba nyimbo za mapenzi ambazo wazazi wako au hata wazaa-wazazi walichezea dansi wakati mmoja huenda zikawa zilikuwa na mstari mmoja au miwili yenye kudokezea kijambo fulani. Lakini nyimbo nyingi za leo zimezidi kiasi cha kusema mambo kwa ujanja tu. Sheila Davis, aliyenukuliwa mapema kidogo, asema hivi: “Si kwamba tu hali ya kutoboa mambo wazi imekuwako badala ya ile ya kuyasema kwa ujanja tu, na kwamba mahaba yamepanuka yakaja kuhusisha ndani kupiga punyeto na ngono [zilizopotoshwa], bali pia maneno ya nyimbo hata yameingilia kutaja ngono haramu za watu wa ujamaa mmoja ambazo hapo kwanza zilikuwa mwiko.” Sasa mashirika kadhaa ya sahani-santuri za United States yamekubali kuweka vibandiko vya onyo juu ya sahani-santuri zilizo na maneno yahusuyo ngono au jeuri.

Leslie wa miaka kumi na sita abisha hivi: “Maneno si ya maana sana ikiwa waweza kuyachezea dansi. Mimi sifikiri yatafisidi mtu yeyote. Huo ni muziki tu.” Wastadi hawakubaliani na hilo. “Kurudiwa-rudiwa kwa muziki ule ule maarufu mara nyingi kila siku huwezesha kukumbuka kwa urahisi ujumbe wa ngono,” ndivyo aonelea mtafiti mmoja. Je! wewe, kama vile watu fulani, umepata kujikuta ukitokwa mdomoni na maneno ya kuudhi au ya ukosefu wa adili kwa sababu tu uliyasikia tena na tena? (Waefeso 4:29) Dakt. Joseph Stuessy, profesa wa muziki kwenye Chuo Kikuu cha Texas kule San Antonio, aonya hivi: “Muziki wa aina yoyote huathiri tabia ya moyo wetu, hisia za moyoni, mitazamo yetu na mwenendo wenye kutokana nao.”—Italiki ni zetu.

Je! lingewezekana kuwa jambo lenye afya kusikiliza au kuimba maneno yenye kueleza wazi au kuendeleza ukosefu wa adili katika ngono? Je! kufanya hivyo kusingeweza kufisidi maoni yako juu ya fungu lifaalo kutimizwa na ngono katika ndoa?—1 Wakorintho 7:3-5.

“Wakati wa Kupenda”

Wazo jingine lenye makosa ambalo hufundishwa katika muziki maarufu ni kwamba vijana-matineja wako tayari kufanya uhusiano wa kindani pamoja na watu wa jinsia tofauti. Ni kweli kwamba kuna “wakati wa kupenda”—lakini hapa Biblia hairejezei mapenzi ya kimahaba. Kuhusu mapenzi katika ndoa, je! kweli huu sasa ndio wakati wako wa kufanya hivyo? Je! haielekei zaidi kwamba itakuwa hivyo miaka kadhaa kutoka sasa, wakati ambapo wewe utakuwa na umri wa kutosha? (Mhubiri 3:8) Ikiwa jambo hili la pili ndilo lakuhusu wewe, je! ni jambo la akili kuamsha tamaa kali kwa kitu ambacho huwezi bado kukipata?

Kwa kukosa mahali pa kufungulia hisia za mahaba walizoziamsha, vijana fulani hunaswa katika ulimwengu wa kuwazia-wazia jinsi mahaba yalivyo. Baadhi yao huwazia kuwa wana “mapenzi” pamoja na waimbaji wawapendeleao zaidi, huku wakiwaza-waza kwamba kila neno jororo lenye kuimbwa huwa linanong’onezwa ndani ya masikio yao wenyewe. Wao hukusanya kila albamu (sahani), foto, na kibandiko wawezacho kukipata cha msanii huyo na kuwaza-waza juu ya kufunga ndoa na mtu huyo. Lakini tokeo la pekee liwezalo kuwa katika uhusiano huo wa kuwaziwa ni mtamauko na umivu.

Hivyo Wimbo Ulio Bora wafundisha somo jingine zaidi lililo la maana. Akiwa na tamaa ya kubaki mshikamanifu kwa mvulana wake mchungaji, yule msichana Mshulami alihimiza waandamani wake wasichana ‘wasiamshe au wasichochee upendo ulio ndani yake’ ili uwe kwa Mfalme Sulemani, ambaye alitafuta shauku za msichana huyo. (Wimbo Ulio Bora 2:7, NW) Kwa kujua nguvu ziwezazo kuwa katika upendo, msichana huyo alikataa katakata kusikiliza maongeo ambayo yangeweza kuathiri vibaya hisia za moyo wake. Mwendo kama huo ungethibitika kuwa wenye hekima kwako katika kuchagua muziki. Kwa nini usiepuke kabisa muziki ambao huchochea hisia kali za mahaba ndani yako au ambazo hukufanya uhisi ukiwa na huzuni na upweke?

Kumbuka: Muziki ni zawadi kutoka kwa Mungu. Nawe waweza kuwa na uhakika kwamba yeye hafurahishwi na muziki ambao hushusha tabia na maadili, ambao hupotosha thamani za maadili ya Kikristo au kutia moyo maadili malegevu. Kwa hiyo ni lazima vijana Wakristo wawe wateuzi katika chaguo lao la muziki. Scott wa miaka kumi na tisa asema hivi: “Kabla sijanunua rekodi [sahani] au kaseti, mimi huchunguza jalada na kupata wazo fulani juu ya maneno yaliyomo. Ikiwa ni yenye kudokeza mambo yasiyofaa, siinunui.”

Mapenzi (upendo) hayako hata kidogo kama yalivyo katika nyimbo za mapenzi. Wewe utajifunza uhakika huu kupitia majionea ya maisha ambayo nyakati fulani huwa yenye maumivu. Kumbuka, pia, kwamba nyimbo nzuri-nzuri haziwezi kuchukua mahali pa marafiki wa kweli. Badala ya kujitenga mwenyewe katika ulimwengu wa kimuziki ulio wa kuwazia-wazia mambo tu, tumia wakati pamoja na watu—wazazi wako, vijana wenye kuhofu Mungu, na Wakristo wakomavu. (Mithali 18:1) Kutokana na ushirika huo utahisi unapendwa kwa njia ya kimungu—hisia ambayo yapita kwa mbali ile misisimuko ya kuwaziwa tu iliyo katika nyimbo za mapenzi.

[Blabu katika ukurasa wa 13]

“Muziki wa aina yoyote huathiri tabia ya moyo wetu, hisia za moyoni, mitazamo yetu na mwenendo wenye kutokana nao”

[Picha katika ukurasa wa 11]

Je! nyimbo zote za mapenzi huonyesha jinsi maisha halisi yalivyo?

[Picha katika ukurasa wa 12]

Uwe mteuzi kuhusu kile ambacho wewe husikiliza!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki