Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 3/8 kur. 26-29
  • Sehemu 12: 100-476 W.K.—Kuizima Kabisa Nuru ya Gospeli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sehemu 12: 100-476 W.K.—Kuizima Kabisa Nuru ya Gospeli
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Watakatifu” na Miungu ya Kigiriki
  • “Yaitwayo ‘Maarifa’ kwa Ubandia”
  • Kupotosha Ukweli Kuhusu Kristo
  • Ukatoliki Katika Shida Kubwa
  • Jinsi Jumuiya ya Wakristo Ilivyokuja Kuwa Sehemu ya Ulimwengu Huu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Konstantino Mkubwa Je, Alikuwa Mtetezi wa Ukristo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Konstantino
    Amkeni!—2014
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 3/8 kur. 26-29

Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita

Sehemu 12: 100-476 W.K.—Kuizima Kabisa Nuru ya Gospeli

“Wanadamu wamegundua kwamba ni rahisi zaidi kwao kutohoa nguvu za ukweli kuliko kujitakasa wao wenyewe.” Charles Caleb Colton, kasisi Mwingereza wa karne ya 19

KUANZIA 33 W.K., wakati Roma ilipoua Mwanzishi wa Ukristo, hiyo serikali kubwa ya sita ya ulimwengu katika historia ya Biblia ilihitilafiana daima na Wakristo. Iliwatia gerezani na kutupa baadhi yao kwenye simba. Lakini hata walipotishwa kuuawa kwa sababu ya imani kwa kuwashwa moto miili yao ili iwe tochi za nuru ya bustani za Nero, Wakristo Waroma wa karne ya kwanza waliendelea kuacha nuru yao ya kiroho iangaze. (Mathayo 5:14) Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya muda.

“Katika sehemu ya mapema ya karne ya tatu,” chasema kitabu From Christ to Constantine, “kanisa lilikuwa likianza kuwa lenye kustahika.” Lakini kustahika kulikuwa na gharama fulani, “mshuko wa viwango.” Kwa hiyo, “maisha ya Kikristo hayakuonwa tena kuwa takwa la imani ya Kikristo.”

Nuru ya gospeli (habari njema) ilikuwa imefifia ikawa kianga tu. Na “kufikia karne ya nne,” chasema kitabu Imperial Rome, “si kwamba tu waandikaji Wakristo walikuwa wakidai yawezekana kuwa mambo yote mawili, Mkristo na Mroma pia, bali pia walikuwa wakidai kwamba kwa uhakika historia ndefu ya Roma ilikuwa ndiyo mwanzo wa mapokeo ya Ukristo. . . . Lililomaanishwa lilikuwa kwamba Roma ilikuwa imechaguliwa rasmi kwa njia ya kimungu.”

Mwenye kushiriki maoni haya alikuwa mmaliki Mroma Konstantino Mkubwa. Katika 313 W.K., Konstantino aliufanya Ukristo uwe dini halali kisheria. Kwa kuunganisha Kanisa na Serikali, kuingiza viongozi wa kidini katika utumishi wa Serikali, na kuruhusu Serikali idhibiti mambo ya kidini, Konstantino aliharibu mambo kweli kweli.

Mapema katika karne ya pili, tayari Ignatius, askofu wa Antiokia, alikuwa ameanzisha mbinu mpya ya serikali ya kundi. Badala ya kikundi cha wazee, baraza la wazee watawala liliandaa mpango ili mwanamume mmoja tu wa kanisa asimamie kila kundi. Karibu karne moja baadaye, askofu wa Carthage aliye Msaiprasi, alipanua mfumo huu wa utawala wa kikasisi ukawa na madaraja saba ya kikasisi, huku kile cheo kikubwa zaidi kikikaliwa na aliye askofu. Chini yake walikuwako mapadri, mashemasi, mashemasi-wadogo, na madaraja mengine. Kanisa la Magharibi lilifuatisha kuongezea daraja la nane, huku kanisa la Mashariki likiamua kuwa na utawala wenye madaraja matano ya kikasisi.

Namna hii ya uongozi wa kanisa, wenye kibali cha Serikali, iliongoza kwenye nini? Kitabu Imperial Rome chaeleza hivi: “Miaka 80 tu baada ya lile wimbi kubwa la mwisho la mnyanyaso wa Wakristo, Kanisa lenyewe lilikuwa likianza kuua wazushi wa kidini, na makasisi walo walikuwa wakitumia mamlaka iliyokaribia kulingana na ile ya wamaliki.” Hakika hili silo wazo lililokuwa katika akili ya Kristo aliposema kwamba wanafunzi wake wangepaswa kuwa “si sehemu ya ulimwengu” na kwamba yawapasa waushinde, si kwa kutumia nguvu, bali kwa imani yao.—Yohana 16:33; 17:14, NW; linganisha 1 Yohana 5:4.

“Watakatifu” na Miungu ya Kigiriki

Muda mrefu kabla ya wakati wa Konstantino, mawazo ya kipagani yalikuwa tayari yametohoa nguvu za dini ya Kikristo. Miungu ya Ugiriki ya hadithi za kubuni ambayo hapo kwanza ilikuwa imetia uvutano imara katika dini ya Roma ilikuwa tayari imetia uvutano katika dini ya Kikristo pia. “Kufikia wakati ambapo Roma ilikuwa imekuwa serikali yenye makoloni,” chasema kitabu Roman Mythology, “mambo ya Jupiter yakawa yamerekebishwa yafanane na Zeus wa Kigiriki . . . Baadaye Jupiter aliabudiwa akiwa Optimus Maximus, aliye Bora Zaidi na Mkubwa Zaidi, mtajo ambao ungekuja kuendelezwa ukaingie katika Ukristo nao huonekana katika maandishi yaliyoandikwa katika majengo mengi ya ukumbusho.” The New Encyclopædia Britannica yaongezea hivi: “Chini ya Ukristo, mashujaa Wagiriki na hata miungu walibakia hai wakiwa watakatifu.”

Mtungaji M. A. Smith aeleza kuwa hii ilimaanisha kwamba “yale mafungu mengi ya miungu yalikuwa yakichangamana, na zile tofauti za kijimbo zikawa zikififia. . . . Kulikuwako elekeo la watu kufikiri kwamba kwa kweli ile miungu mbalimbali ilikuwa majina tofauti tu ya kutaja mamlaka moja tu iliyo kubwa. . . . Isisi wa Misri, Artemi wa Waefeso na Astarte wa Siria wangeweza kulinganishwa wawe kitu sawa. Zeus wa Ugiriki, Jupiter wa Roma, Amon-Re wa Misri na hata Yahweh wa Uyahudi wangeweza kuombwa msaada wakiwa ni majina ya yule Mwenye Mamlaka mmoja aliye mkubwa.”

Ujapochanganywa na fikira za Kigiriki na za Kiroma katika Roma, Ukristo ulikuwa pia ukipatwa na mabadiliko katika mahali pengine. Alexandria, Antiokia, Carthage, na Edessa, vyote hivi vikiwa ni vitovu vya utendaji wa kitheolojia, vilisitawisha shule zenye fikira za kidini zenye kutofautiana sana. Kwa kielelezo, Herbert Waddams, aliyekuwa Kanoni Mwanglikana wa Canterbury, asema kwamba ile shule ya Alexandria “hasa ilitiwa uvutano na mawazo ya Kiplatoni,” ikisema kwamba nyingi za taarifa zilizo katika “Agano la Kale” ni mafumbo. Shule ya Antiokia ilichagua kueleza maana za maneno ya Biblia kwa njia ya uhalisi zaidi, kwa mtazamo wenye uchambuzi zaidi.

Umbali, ukosefu wa uwasiliano, na hali za kutoelewana lugha ni mambo yaliyozidisha tofauti zile. Hata hivyo, yenye daraka la kuleta hali ile ni roho ya kujitegemea na makuu yenye ubinafsi wa viongozi wa kidini waliotaka kutohoa nguvu za ukweli ili wapate faida ya kibinafsi, kwa njia hiyo wakiizima nuru ya gospeli.

“Yaitwayo ‘Maarifa’ kwa Ubandia”

Mapema sana katika karne ya kwanza, Ukristo ulitiwa uvutano wa mafundisho bandia ya kidini, hiyo ikisababisha Paulo aonye Timotheo ageukie mbali “kutoka kwenye mapingano ya yale yaitwayo ‘maarifa’ kwa ubandia.” (1 Timotheo 6:20, 21, NW) Huenda hili likawa lilikuwa rejezo kwa harakati fulani yenye kuitwa Ugnosti ambayo ilipata umashuhuri mapema katika karne ya pili lakini ambayo kwa uwazi ilianzishwa katika karne ya kwanza, yawezekana ikiwa na mtu fulani mwenye kuitwa Simon Magus. Watungaji fulani wadai kwamba huenda huyu akawa ndiye yule Simoni mwenye kutajwa katika Biblia kwenye Matendo 8:9.

Ugnosti ulipata jina lao kutokana na neno la Kigiriki gnoʹsis, linalomaanisha “maarifa.” Vikundi vya Kignosti vilikazania kwamba wokovu hutegemea maarifa ya pekee yenye mafumbo kuhusu mambo ya kina kirefu yasiyojulikana na Wakristo wa kikawaida. Kama vile isemavyo The Encyclopedia of Religion, wao walihisi kwamba kuwa na maarifa haya kuliwawezesha kufundisha “ukweli wa kindani uliofunuliwa na Yesu.”

Vyanzo vya fikira ya Kignosti vilikuwa vingi. Kutoka Babuloni, Wagnosti walichukua lile zoea la kuzihesabu namba za Biblia kuwa zina maana zilizofichika, zikisemwa kuwa zilifunua kweli fulani za kifumbo. Wagnosti walifundisha pia kwamba ijapokuwa roho ni njema, chochote kilicho na mata (asili ya kitu) kina asili ya uovu. “Huu ndio mlolongo ule ule wa kusababu mambo,” asema mtungaji Mjeremani Karl Frick, “uliokuwa tayari wapatikana katika muungano wa kanuni mbili za Kiajemi na katika Mashariki ya Mbali katika ‘yin’ na ‘yang’ ya China.” Ni wazi kabisa kwamba “Ukristo” uliotokezwa na maandishi ya Kignosti wategemea vyanzo visivyo vya Kikristo. Kwa hiyo ungewezaje kuwa ndio “ukweli wa kindani uliofunuliwa na Yesu”?

Mwanachuo R. E. O. White auita Ugnosti kuwa ni mchanganyiko wa “makisio ya kifalsafa, hofu ya kishirikina, desturi ambazo ni nusu-ajabu-za-kichawi, na nyakati fulani ni kidhehebu kishupavu na hata chenye machafu.” Andrew M. Greeley wa Chuo Kikuu cha Arizona asema hivi: “Nyakati fulani Yesu wa Wagnosti ni kigeugeu, nyakati fulani hana akili, na nyakati fulani ana hali za kuchukiza sana.”

Kupotosha Ukweli Kuhusu Kristo

Si Wagnosti peke yao waliopotosha ukweli kuhusu Kristo. Nestorius, mwanzishi wa kiaskofu wa mapema karne ya 5 katika Constantinople, yaonekana alifundisha kwamba kwa kweli Kristo alikuwa watu wawili katika mmoja, Yesu aliye wa kibinadamu na Mwana wa Mungu aliye wa kimungu. Katika kuzaa Kristo, Mariamu alizaa mwanadamu lakini si yule Mwana wa kimungu. Maoni haya hayakukubaliana na lile wazo la Asilimoja, lililoshikilia kwamba muungano kati ya Mungu na Mwana ulikuwa usiotenganika, na kwamba ingawa ni mwenye asili mbili, kwa uhalisi Yesu alikuwa mmoja tu, akiwa Mungu kikamili na wakati ule ule mwanadamu kikamili. Kwa hiyo, Mariamu angalikuwa kikweli amezaa Mungu, wala si binadamu Yesu tu.

Nadharia zote mbili zilikuwa machipuko yaliyotokana na kibishanio kilichokuwa kimetokea katika karne iliyotangulia. Arius, padri Mwalexandria, alitoa ubishi kwamba Kristo ni mdogo kwa Baba. Kwa hiyo akakataa kutumia ule mtajo homoousios (kuwa wenye asili moja) katika kueleza uhusiano wa Kristo kwa Mungu. Baraza la Nikaya lilikataa maoni yake katika 325 W.K., likaamrisha kwamba Yesu kwa kweli ni ‘wa asili ile ile kama Baba.’ Katika 451 W.K. Baraza la Chalcedon lilitaarifu kwamba Kristo ni Mungu akiwa katika umbo la kibinadamu. Sasa lile wazo la ujumliko wa asili ya Kibabuloni, ya Kimisri na ya Kigiriki kuhusu Mungu-utatu likawa limelisonga na kuliondoa fundisho la Kristo kwamba yeye na Baba yake ni watu wawili mbalimbali, wasio na usawa kamwe.—Marko 13:32; Yohana 14:28.

Kwa kweli, Tertullian (c. 160–c. 230 W.K.), mshirika wa kanisa la Afrika Kaskazini, ndiye aliyeanzisha neno “trinitas,” likaingia katika utumizi wa Kikristo muda fulani kabla Arius hajazaliwa. Tertullian, aliyekuwa mwanatheolojia wa kwanza kuandika mengi katika Kilatini badala ya Kigiriki, alisaidia kuweka msingi wa theolojia ya Magharibi. Ndivyo alivyofanya “Mtakatifu” Augustine, mwanatheolojia mwingine wa Afrika Kaskazini wa karne mbili hivi baadaye. “[Augustine] hutambuliwa kwa ujumla kuwa ndiye aliyekuwa mtumia-akili mkubwa zaidi aliyepata kuwako zamani zile za Ukristo,” yasema The New Encyclopædia Britannica. Lakini maneno iyasemayo baada ya hapo yapasa kuhangaisha kila Mkatoliki au Mprotestanti mwenye moyo mweupe: “Akili yake ndiyo nyungu iliyotumika kuichanganya kabisa kabisa dini ya Agano Jipya na pokeo la falsafa ya Kigiriki; na pia ndiyo iliyotumika kusafirisha mchanganyo huu kwenye Jumuiya za Wakristo wa Ukatoliki-Roma wa zile enzi za katikati na Uprotestanti wa ile enzi ya Kuvumbua Vitu.

Ukatoliki Katika Shida Kubwa

Kuelekea mwisho wa karne ya nne, Mmaliki Theodosius 1 alikamilisha kilichoanzishwa na Konstantino kwa kufanya Ukatoliki uwe ndiyo dini ya Serikali. Muda mfupi baada ya hapo Milki ya Kiroma iligawanyika, kama vile Konstantino alivyokuwa amehofu ingekuwa. Roma ilitekwa katika 410 W.K. na Wavisigothi, jamii ya watu Wajeremani ambao kwa muda mrefu walikuwa wameisumbua milki, na katika 476 W.K., Odoacer jemadari Mjeremani alimwondoa cheoni mmaliki wa Magharibi na kupiga mbiu kwamba yeye mwenyewe ni mfalme, hivyo akikomesha Milki ya Magharibi ya Roma.

Chini ya hali mpya hizi, Ukatoliki ungeendeleaje? Kufikia 500 W.K., huo ulidai kwamba asilimia 22 hivi ya wakaaji wa ulimwengu walikuwa washirika wao. Lakini kati ya watu hawa wenye kukadiriwa kuwa milioni 43, walio wengi walikuwa wamedhulumiwa na viongozi wa kidini waliokuwa wameona ikiwa rahisi zaidi kwao kutohoa nguvu za ukweli kuliko kujitakasa wao wenyewe. Nuru ya gospeli ya Ukristo wa kweli ikawa imezimwa. Lakini muda si muda, “Kutoka Gizani, Kitu Fulani ‘Kitakatifu’” kingezaliwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 28]

Violezo vya Imani ya Kignosti

Marcion (wa karne ya pili) alitofautisha kati ya Mungu asiyekamilika “wa Agano la Kale,” aliye mdogo kwa Yesu, na Baba ya Yesu, yule Mungu wa upendo “wa Agano Jipya” ambaye hajulikani. Wazo la “mungu asiyejulikana ni kichwa cha habari ya msingi ya ugnosti,” yaeleza The Encyclopedia of Religion. Mungu huyu asiyejulikana hutambulishwa kuwa “ndiye Mwenye Akili aliye mkuu zaidi, asiyefahamika na akili ya kibinadamu.” Kwa upande ule mwingine, muumba wa ulimwengu wa vitu vyenye kuonekana ni mdogo na si mwenye akili kabisa kabisa naye ajulikana kuwa Mungu-mdogo.

Montanus (wa karne ya pili) alihubiri kurudi kwenye kukaribia kwa Kristo na kuanzishwa kwa Yerusalemu Jipya katika ile ambayo leo ni Uturuki. Kwa kuhangaikia zaidi mwenendo kuliko fundisho, ni wazi kwamba yeye alijaribu kurudisha zile thamani asilia za Ukristo, lakini kwa kuchukua hatua za kupita kiasi, mwishowe harakati hiyo ikapatwa na hali ile ile ya uzembe ambao iliulaani vikali.

Valentinus (wa karne ya pili), mshairi Mgiriki na Mgnosti aliye mashuhuri kuliko wote wa nyakati zote, alidai kwamba ingawa mwili usiogusika wa Yesu ulipita katika Mariamu, kwa kweli haukuzaliwa kutokana naye. Hii ni kwa sababu Wagnosti waliona mata yote (asili ya vitu) kuwa yenye uovu. Hivyo, isingaliweza kuwa kwamba Yesu alikuwa na mwili wenye kuonekana au sivyo huo pia ungalikuwa na uovu. Wagnosti wajulikanao kuwa Wadosetisti walifundisha kwamba kila kitu kilichohusu ubinadamu wa Yesu kilionekana kuwa hivyo na kumbe hakikuwa bali kilikuwa mauzauza tu. Hiyo ilitia ndani pia kifo na ufufuo wake.

Manes (wa karne ya tatu) alibandikwa jina la kuwa alBābilīyu, neno la Kiarabu kwa “yule Mbabuloni,” kwa kuwa yeye alijiita “mjumbe wa Mungu aliyekuja Babuloni.” Yeye alijitahidi kufanyiza dini ya ulimwenguni pote yenye kuchangamana na visehemu vya Ukristo, Dini ya Buddha, na Dini ya Zoroasta.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Konstantino alisaidia kuizima nuru ya gospeli kwa kuchanganya Ukristo na ibada ya kipagani

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki