Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita
Sehemu 13: 476 W.K. na Kuendelea—Kutoka Gizani, Kikaja Kitu “Kitakatifu”
“Dhambi zitendazwo gizani huonekana Mbinguni zikiwa kama miali miangavu ya moto.”—Mithali ya Kichina
KATIKA Aprili 1988 Kanisa katika Urusi lilishangilia kumsikia Katibu Mkuu Mikhail Gorbachev akitaarifu peupe kwamba makosa yaliyofanywa na Serikali katika uhusiano walo na Kanisa na washiriki walo yangepasa kusahihishwa.
Ufa wa aina nyingine pia ulionekana ukikaribia kuzibwa wakati papa wa Katoliki ya Kiroma, John Paul 2, alipolipelekea salamu lile “kanisa ambalo limekuwa dada yao kwa miaka elfu moja ili ziwe wonyesho wa tamaa yenye kuhisiwa moyoni ya kuufikia ule muungano mkamilifu alioutaka Kristo ambao ni wa msingi katika asili ya Kanisa.” Lakini mtengano ulikuja-kujaje hapo kwanza kati ya ‘makanisa yaliyo dada na dada’?
Kupoteza Muungamano Ambao Haukuwa Kamwe Muungamano
Mapema katika karne ya nne, Konstantino Mkuu alipokwisha kuwa mmaliki wa Milki ya Kiroma, yeye alihamisha mji wake mkuu ukaacha kuwa Roma na kuwa jiji la Kigiriki la Byzantium, lililo katika fuo za Bosporus. Liliitwa upya Konstantinopo, nasi leo twalijua kuwa Istanbul, Uturuki. Mhamo huo ulifanyizwa ili uungamanishe milki iliyoelekea kugawanyikana. Kwa uhakika, mapema sana kwenye nusu ya mwisho ya karne ya pili, “dalili za kuwa na milki iliyogawanyika zilikuwa tayari zimetokea, hata kama ni kwa njia isiyoonekana wazi sana,” yataarifu The New Encyclopædia Britannica.
Ukristo ulikuwa umeenea sehemu yote ya mashariki ya milki hiyo kwa haraka na utayari mwingi kuliko ulivyofika katika sehemu ya magharibi. Kwa hiyo Konstantino aliona kwamba angeweza kupata kani ya kuleta muungamano kwa kutumia dini yenye kuwapo kila mahali (hiyo ikiwa ndiyo maana ya katoliki). Lakini kama vile milki ilivyogawanyika kwa sehemu kubwa, ndivyo na dini yayo. Kanisa la Mashariki likawa zaidi lisilotaka mabadiliko makubwa kuliko lile lenye kitovu katika Roma, nalo likakinza mabadiliko mapya ya kitheolojia ambayo Roma ililitolea. “Kuendelea moja kwa moja mpaka karne ya kumi na mbili kungekuwa na mabishano mengi ya kisiasa na kitheolojia kati ya makanisa hayo mawili,” yasema The Collins Atlas of World History.
Moja la mabishano haya ya kitheolojia yalihusisha ndani Kanuni ya Imani ya Nisene, ambayo iliongezea usitawi wa lile fundisho la Utatu lisilo la Kimaandiko. Kama ilivyositawishwa na mabaraza matatu makuu ya kwanza yaliyofanywa na kanisa (Nisea [Nikaya] katika 325 W.K, Konstantinopo katika 381 W.K., Efeso katika 431 W.K.), imani hiyo ilinena juu ya “Roho Mtakatifu . . . ambaye hutoka kwa Baba.” Lakini kwenye baraza moja katika karne ya sita, kanisa la Magharibi lilibadili kifungu cha maneno hayo kikasomeka “ambaye hutoka kwa Baba na yule Mwana.” Suala hili la filioque (neno la Kilatini la kusema “na yule mwana”) lilikuwa na lingali ni jambo la kubishaniwa kati ya makanisa haya “ya Kikristo” yaliyo dada na dada.
Ukosefu wa muungamano ulionekana wazi zaidi wakati milki ile ya magharibi ilipoisha katika 476 W.K., hiyo ikiwa ndiyo alama ya mwanzo wa zile Enzi Zenye Giza. Kwa habari ya Ukristo, kwa kweli zile Enzi Zenye Giza zilikuwa kipindi cha giza la kukosa uelewevu na maarifa. Kwa wakati huo, nuru ya gospeli ya Ukristo ilikuwa imelemewa na giza la Jumuiya ya Wakristo.
Giza la kidini halisaidii kuleta muungamano. “Sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kikristo zilikuwa zikitafuta daima muungamano ambao haukupatikana kamwe,” asema aliyekuwa Kanoni wa Canterbury Herbert Waddams. “Hakikuwa kisa cha muungamano kamili ambao ulivunjwa baadaye,” yeye asema, akiongezea kwamba “wazo la kwamba wakati mmoja Jumuiya ya Wakristo ilikuwa Kanisa moja kubwa lenye muungamano ni jambo la kuwazia tu.”
“Mtoto” Azaliwa
“Mtoto” aliyezaliwa katika 800 W.K. Siku ya Krismasi alikua akaja kuitwa mtakatifu. Huyo alikuwa milki ya magharibi iliyorudishwa baada ya Papa Leo 3 kuvunja uhusiano na kanisa la Mashariki na kumvika taji Charlemagne, mfalme wa Wafranki, ili awe mmaliki. Baada ya mkatizo mfupi, milki ya magharibi ilirudishwa upya katika 962 W.K. na baadaye ikaja kujulikana kwa mtajo wenye kisingizio kikubwa zaidi, eti Milki Takatifu ya Kiroma.
Kwa kweli, jina Milki ya Kiroma lilikuwa jina lisilofaa. Sehemu kubwa ya eneo layo, ambalo sasa ni Ujeremani, Austria, Chekoslovakia ya magharibi, Switzerland, Ufaransa ya mashariki, na zile Nchi za Chini, lilikuwa nje ya Italia. Mabara ya Ujeremani na watawala wa Ujeremani walikuwa ndio wenye mamlaka nyingi zaidi, kwa hiyo jina layo rasmi lilibadilishwa baadaye likawa Milki Takatifu ya Kiroma ya Taifa la Kijeremani.
Milki hiyo ilichanganya dini na siasa. Collier’s Encyclopedia yaeleza kwamba wazo lilikuwa “kwamba kwapasa kuwa na kichwa mmoja tu wa kisiasa ulimwenguni, mwenye kufanya kazi kwa upatano na lile Kanisa la kila mahali, kila moja likiwa na eneo na mamlaka yalo yenyewe yenye kutoka kwa Mungu.” Lakini mipaka yenye kugawa maeneo haikuwa wazi sikuzote, na hivyo jambo hilo lilileta magomvi. Hasa kati ya kipindi cha katikati ya karne ya 11 na katikati ya karne ya 13, Kanisa na Serikali zilishindania kuongoza Ulaya. Watu fulani huhisi kwamba mhusiko wa dini katika siasa ulikuwa wa ubinafsi na wenye haki, lakini kama vile ambavyo mtungaji Waddams akubali wazi, “hakuna shaka kwamba makuu ya papa ya kujitakia mamlaka yalishiriki sana katika tukio hilo.”
Wakati wa karne moja na nusu ya mwishoni mwa kuwako kwayo, milki hiyo ilizorota ikawa mkusanyo wa mataifa legelege ikiwa chini ya udhibiti mlegevu wa mmaliki mmoja wa ujumla. Ni yenye kufaa sana maneno yaliyosemwa na Voltaire mwandikaji Mfaransa wa kipindi hiki cha historia, aliyesema kwamba haikuwa “yenye utakatifu, wala haikuwa ya Kiroma, wala haikuwa milki.” Mwisho, katika 1806, huyo “mtoto mtakatifu” alikufa akiwa na mvi za uzee na bila kitu chochote cha kumpendekeza kuwa mtakatifu. Katika 1871 ilirudishwa upya ikiwa Raiki (neno la Kijeremani kwa “milki”) ya Pili lakini ikaanguka katika 1918, chini ya miaka 50 baadaye. Na katika 1933, Raiki ya Tatu ya Adolf Hitler ilianza kupiga hatua zenye uhakika katika Ulaya, kumbe ikafikia mwisho wenye aibu katika 1945 kwa kubaki ikiwa magofu ya Berlin.
Mavutano ya Kijeremani Katika Magharibi
Kitabu chenye marejezo ya Kijeremani Meyers Illustrierte Weltgeschichte (Historia ya Ulimwengu Iliyofanyiwa Vielezi na Meyere) chasema kwamba “zile nguzo tatu zilizotegemewa ili kutokeza zile Enzi za Katikati Katika Ulaya . . . [zilikuwa ni] desturi kubwa za kale zilizorithiwa zikiwa kwa namna iliyofanyizwa upya na Waroma, [halafu] Ukristo, na mwisho mapokeo yaliyo ya Kiroma yaliyochukuliwa na jamii za Kijeremani kutoka kwa wazazi wao wa kale.” Kwa kuthibitisha hivyo, Emil Nack aliye mtungaji Mjeremani asema hivi: “Mara nyingi zile sikukuu za Kijeremani zenye kusherehekewa kila mwaka ziliendelezwa zikiwa kwa namna ya holidei za Kikristo, kwa kuwa kanisa, kama lilivyoundwa na Papa Gregori Mkuu, liligeuza sikukuu nyingi za kipagani zikawa za Kikristo.”
Kuadhimisha sikukuu hizi za kidini hakukumaanisha kwamba jamii za Kijeremani zilifuata dini kwa kina kirefu. Andreas Heusler, mtungaji mfu sasa ambaye aliandika kuhusu dini ya Kijeremani, aieleza kuwa dini ambayo “ilikataza mambo machache sana na ikawa haina matakwa yoyote magumu, ikihusisha ndani desturi zozote zilizotokana na hadithi zisizo za kweli. Mtu alionwa kuwa mchaji ikiwa alitoa dhabihu zake, akalipa kodi yake ya hekaluni, akawa hapavunjii heshima patakatifu, na akawa hakuandika vifungu vyovyote vya kuidhihaki miungu.” Yeye akata shauri hivi: “Juhudi ya kidini haikuwako sana. . . . Mawazo yenye kumwongoza Mjeremani hayakuitegemea dini yake.”
Ingawa jamii za kale za Kijeremani ziliamini katika miungu, zilihisi kwamba kwa kweli kulikuwa kungali kuna mamlaka ya juu zaidi, iliyokuwa imeiumba miungu. Hii ilikuwa “mamlaka ya ajali [nasibu],” aeleza mtungaji Nack, ambayo, yeye asema, ‘haikukubali kubadili maoni kwa kupelekewa dhabihu wala sala.’ Hata hivyo, ajali haikuonwa kuwa “yenye kushikilia mambo kwa upofu,” kwa kuwa ilifanya kazi kulingana na sheria za kiasili. Kwa hiyo mtu alionwa kuwa “kitu chenye hiari ya kuchagua, si cha kushurutishwa na hali.”
Dini ya Kijeremani ilipata chanzo kwenye vitu vya kiasili. Mara nyingi dhabihu zilitolewa mbali na makao, katika vichaka na misitu. Hadithi moja ya ubuni wa Kijeremani yanena juu ya mti wa kilimwengu uitwao Yggdrasill, ambapo miungu ilifanya baraza kila siku. The Encyclopedia of Religion yaeleza jambo hili hivi: “[Uliinuka juu] kufika kwenye anga, na matawi yao yalienea juu ya ulimwengu mzima. . . . Ufanano wa mti huo . . . huonyeshwa katika mapokeo mengine. Kwa kielelezo, katika Babulonia ya kale mti mmoja wa kilimwengu, Kiskanu, ulikua katika mahali fulani patakatifu. . . . Katika India ya kale, ulimwengu wote mzima wafananishwa na mti uliosimama juu-chini. . . . [Lakini] hakuna uthibitisho wa kwamba kuna kiasili chochote kwamba Yggdrasill ulitokana na Wayudea Wakristo.”
Kwa sababu ya habari hizi za matukio ya kule nyuma, haishangazi kwamba katika nchi ambazo zimekuwa na uvutano thabiti wa dini ya Kijeremani, mara nyingi watu hutegemea ajali iongoze mambo, wala hawawi wafuata dini sana nao huelekea kusema: ‘Mungu wangu ni maumbile!’ Pia yaeleweka kwamba nyingi za desturi za kipagani ambazo dini ya Kijeremani iliingiza katika Jumuiya ya Wakristo zimetokana na vitu vya kiasili. Desturi za Krismasi, kama vile kutumia mianga na mizotou (mti mnyonyaji), kuchoma gogo la Yule [jioni yenye kutangulia Krismasi], au kuweka wonyesho wa mti wa Krismasi, ni vielelezo vichache tu.
Ilivyokuwa Wakati Huo Katika Mashariki
Kwa sababu ya kuhitilafiana sikuzote na kanisa la Magharibi, kanisa la Mashariki halikuwa na amani hata ndani yalo lenyewe, kielezi cha jambo hilo kikiwa ni ule ubishi wa kwamba aikoni hazikupasa kutumiwa. Aikoni, ambazo ni tofauti na mifano yenye pande tatu, kama zile sanamu zilizomo kwa wingi katika kanisa la Magharibi, ni mifano au picha za kidini zilizo katika uso wa kitu kilicho tambarare, kutia na maumbo yaliyoinuka kutoka kwenye uso huo. Kwa ujumla aikoni hizo huonyesha Kristo, Mariamu, au “mtakatifu” fulani. Zilikuja kuwa maarufu sana katika Mashariki hivi kwamba, kulingana na John S. Strong wa Koleji ya Bates, zilikuja “kuonwa kuwa vifananishi au vionyeshi vya moja kwa moja vya maumbo ambayo viliyawakilisha, [na] . . . hivyo zilifikiriwa kuwa zenye kujaa nguvu takatifu ambazo zingeweza kufanya miujiza.” Hata hivyo, mapema katika karne ya nane, Leo wa 3 mmaliki wa Byzantium aliharamisha utumizi wazo. Ubishi huo uliendelea bila kutatuliwa mpaka ilipofika 843 K.W.K., na tangu wakati huo idhini imetolewa ya kutumia aikoni katika kanisa la Mashariki.
Kielelezo kingine cha ukosefu wa muungamano katika Mashariki chatoka Misri. Ingawa Wakatoliki fulani Wamisri walinena Kikopti, wengine walinena Kigiriki, huku vikundi vya lugha mbili hizo vikiwa bila makubaliano kuhusu jinsi Kristo alivyo. Hiyo ilifanyiza mtokeo halisi wa makanisa mawili yaliyotengana, hata ingawa wenye mamlaka wa Byzantium walikataa kukiri hivyo. Muda wote huu, kila upande wenye mzozo ulijaribu kutumia werevu ili mmoja wa maaskofu wao aingie cheo cha kuwa mkale wa kanisa katika Alexandria.
Leo, kanisa la Mashariki lingali limegawanyika. Kwa kielelezo, makanisa fulani ya muundo wa Mashariki, yajulikanayo kuwa Waungamani, hukubali kuwa chini ya usimamizi wa mamlaka ya papa wa Roma. Kwa upande ule mwingine, makanisa ya Orthodoksi ya Mashariki na yale yaitwayo makanisa madogo ya Mashariki hayaukubali.
Kama Miali Miangavu ya Moto
Muda mrefu kabla ya kumalizika kwa Milki-pungufu ya Roma isiyo takatifu, “kawaida ya Wakristo kuchukia Wakristo wengine ilikuwa imekazwa kwa kina kirefu katika mioyo ya Wakristo wa Mashariki,” asema Waddams mwanakanisa Mwanglikana. Kwa uhakika, ile dhambi ya “Mkristo” kuchukia “Mkristo,” hata kama ilifanywa gizani, haikukosa kuonekana mbinguni bali ilikuwa wazi kama miali miangavu ya moto.
Zaidi ya hilo, dhambi ya Jumuiya ya Wakristo ya kuwa na nyumba iliyogawanyika haikukosa kuonekana duniani. Kwa kielelezo, Mwarabu fulani mashuhuri wa karne ya saba W.K., ambaye “alijua mengi kuhusu Ukristo kutokana na safari zake na kutokana na watu wenye uhusiano wa karibu naye,” asema kwamba kasisi Waddams hakuvutiwa na “magomvi aliyoona miongoni mwa Wakristo.” Mtu huyo alitafuta njia bora kuliko ile ya Jumuiya ya Wakristo yenye mgawanyiko. Je! aliipata? Leo katika 1989, asilimia 17 kamili za watu wa ulimwengu huunga mkono njia aliyoifuata. Makala ifuatayo itajibu mtu huyo alikuwa nani na alihisije kuhusu “Kunyenyekea Penzi la Mungu.”
[Ramani katika ukurasa wa 27]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kwenye anguko la Milki ya Kiroma (476 W.K.), Jumuiya ya Wakristo iligawanyika chini ya maaskofu sita wenye kushindana—Roma, Konstantinopo, Antiokia, Aleksandria, Yerusalemu, na Salamisi (Saiprasi)
Roma
Konstantinopo
Antiokia
Salamisi
Yerusalemu
Aleksandria
[Picha katika ukurasa wa 26]
Aikoni (mfano wa kidini) wa Yesu na Mariamu
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.