Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 5/8 kur. 13-17
  • Sehemu ya 15: 1095-1453 W.K.— Kugeukia Upanga

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sehemu ya 15: 1095-1453 W.K.— Kugeukia Upanga
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Ncha za Panga
  • Upanga Waleta Matokeo Yasiyotarajiwa
  • Panga za Siasa na Mnyanyaso
  • Katenganishwa na Upanga wa Kutoungamana
  • Je! Walikuwa Wakiishi Kulingana na Dini Yao?
  • Zile Krusedi—“Uwongo Wenye Msiba”
    Amkeni!—1997
  • Fahari Iliyosahaulika ya Milki ya Byzantium
    Amkeni!—2001
  • Sehemu 13: 476 W.K. na Kuendelea—Kutoka Gizani, Kikaja Kitu “Kitakatifu”
    Amkeni!—1990
  • Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 5/8 kur. 13-17

Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita

Sehemu ya 15: 1095-1453 W.K.— Kugeukia Upanga

“Wanadamu watazozania dini, waandike habari zayo, waipiganie, waifie; watafanya lolote waishi kwa ajili yayo.”—Charles Caleb Colton, kasisi Mwingereza wa karne ya 19

UKRISTO katika miaka yao ya mapema ulibarikiwa kwa waamini walioishi kulingana na dini yao. Kwa kutetea imani yao, walitumia kwa bidii “upanga wa roho, yaani, neno la Mungu.” (Waefeso 6:17, NW) Lakini baadaye, kama matukio kati ya 1095 na 1453 yalivyotoa kielezi, Wakristo wa jina tu, wasioishi kulingana na Ukristo wa kweli, waligeukia kutumia aina nyingine za panga.

Kufikia karne ya sita, Milki ya Magharibi ya Kiroma ikawa imetokomea. Mahali payo pakawa pamechukuliwa na mlingano wayo wa Mashariki, ile Milki ya Baizantino yenye mji mkuu wa Konstantinopo. Lakini makanisa mbalimbali ya milki hizo, yakipatwa na mahusiano yenye kutikisika zaidi sana, yakajikuta upesi yakitishwa na adui yao wote pamoja, utawala wa Kiislamu wenye kuenea.

Wakati wa baadaye sana ambapo kanisa la Mashariki lilipata kung’amua jambo hili ni katika karne ya saba ambapo Waislamu waliteka Misri na sehemu nyingine za Milki ya Baizantino yenye kuwako Afrika Kaskazini.

Muda unaopungua karne moja baadaye, kanisa la Magharibi lilishtuka kuona Uislamu ukipitia Hispania kuingia Ufaransa, ukafika mwendo wa kama kilometa mia moja na sitini kukaribia Paris. Wakatoliki Wahispania wengi waligeuka kufuata Uislamu, huku wengine wakichagua kufuata adabu za Kiislamu na kupokea kwa moyo utamaduni wa Kiislamu. “Kwa kutiwa uchungu na hasara zalo,” chasema kitabu Early Islam, “Kanisa lilijitahidi bila kikomo miongoni mwa wana walo Wahispania ili kupepea miali ya kisasi.”

Karne kadhaa baadaye, Wakatoliki Wahispania walipokwisha kupata tena sehemu kubwa ya bara lao, ‘waligeukia raia zao Waislamu wakawanyanyasa bila rehema. Waliwalazimisha kukana imani yao, wakawaondosha nchini, na kuchukua hatua kubwa za kung’oa kila salio la utamaduni wa kuchanganya Uhispania na Uislamu.”

Kwa Ncha za Panga

Katika 1095 Papa Urban 2 aliwaitisha Wakatoliki Wanaulaya wachukue upanga halisi. Uislamu ungeondolewa cheoni utoke katika mabara matakatifu ya Mashariki ya Kati ambayo Jumuiya ya Wakristo ilidai kuwa haki zayo kamili.

Wazo la vita “ya haki” halikuwa jipya. Kwa kielelezo, lilikuwa limetokezwa katika pigano dhidi ya Waislamu katika Hispania na Sisili. Na angalau mwongo mmoja kabla ya usihi wa Urban, asema Karlfried Froehlich wa Seminari ya Princetown ya Theolojia, Papa Gregori 7 “aliona njozi ya militia Christi [jeshi-mgambo la Kristo] la kupigana dhidi ya adui wote wa Mungu na tayari akafikiria kupeleka jeshi Mashariki.”

Kwa sehemu kitendo cha Urban kilikuwa itikio la ombi la msaada kutoka kwa mmaliki Alexius wa Baizantino. Lakini kwa kuwa mahusiano kati ya sehemu za Mashariki na Magharibi za Jumuiya ya Wakristo yalionekana yakiwa na maendeleo, huenda papa pia akawa alihamasishwa na uwezekano ambao jambo hili lilitoa wa kuungamanisha upya hayo makanisa dada yenye kuzozana. Kwa vyovyote, aliitisha mkutano wa Baraza la Clermont, ukajulisha wazi kwamba wale wenye nia ya kujitia katika shughuli hii “takatifu” wangepewa ondoleo la adhabu yote ya dhambi. Itikio likawa chanya kwa kutotarajiwa. “Deus volt” (“Mungu apenda hivyo”) ikawa shime ya kuchukua kitendo katika Mashariki na Magharibi.

Mfululizo wa safari za kijeshi ulianza ukahusisha sehemu kubwa ya karne mbili. (Ona sanduku katika ukurasa 16.) Kwanza Waislamu walifikiri wavamizi walikuwa Wabaizantino. Lakini baada ya kung’amua asili yao ya kweli, waliwaita Wafranki, watu wa Kijeremani ambao kutokana nao Ufaransa (France) ilipata jina layo baadaye. Ili kukabili wito wa ushindani wa “washenzi” hawa wa Ulaya, msisimuko uliongezeka miongoni mwa Waislamu ili kuwe na jihadi, vita au pambano takatifu.

Profesa Mwingereza Desmond Stewart aonyesha wazi hivi: “Kwa kila mwanachuo au mwuza-bidhaa aliyepanda mbegu za utamaduni wa Kiislamu kwa mwongozo na kielelezo, kulikuwako askari mmoja ambaye aliona Uislamu ukiwa wito wa kupigana.” Kufikia nusu ya pili ya karne ya 12, kiongozi Mwislamu Nureddin alikuwa amejenga jeshi hodari la kivita kwa kuungamanisha Waislamu katika Siria ya kaskazini na Mesopotamia ya juu. Kwa hiyo “kama vile Wakristo wa Enzi za Katikati walivyochukua silaha kusogeza mbele dini ya Kristo, Waislamu walichukua silaha ili kusogeza mbele dini ya Nabii,” Stewart aendelea kusema.

Bila shaka, kani yenye kuhamasisha haikuwa ni kusukuma mbele makusudi ya dini sikuzote. Kitabu The Birth of Europe chaarifu kwamba kwa Wanaulaya walio wengi, Krusedi “zilitoa fursa zisizokinzika za kupata umaarufu, au kukusanya nyara, au kumiliki viwanja vipya, au kutawala nchi nzima-nzima—au ili tu kuepuka uchoshi katika shughuli tukufu ya kujasiria.” Wauza-bidhaa Waitalia pia waliona fursa ya kuanzisha vituo vya biashara katika mabara ya Mediterania ya Mashariki. Lakini hata kama matilaba ilikuwa nini, yaonekana wazi wote walikuwa na nia ya kufia dini yao—iwe ni katika vita “ya haki” ya Jumuiya ya Wakristo au katika jihadi ya Kiislamu.

Upanga Waleta Matokeo Yasiyotarajiwa

“Ingawa Krusedi zilielekezwa dhidi ya Waislamu katika Mashariki,” yasema The Encyclopedia of Religion, “bidii ya Wanakrusedi ilitumiwa juu ya Wayahudi walioishi katika mabara ambako Wanakrusedi walichaguliwa, yaani, katika Ulaya. Mbinu maarufu miongoni mwa Wakrusedi ilikuwa kisasi kwa kifo cha Yesu, na Wayahudi wakawa ndio mihanga wa kwanza. Mnyanyaso wa Wayahudi ulitukia katika Rouen katika 1096, ukifuatwa haraka na machinjo makuu katika Worms, Mainz, na Cologne.” Huu ulikuwa utangulizi tu wa roho ya upinzani kwa watu wenye asili ya Shemu iliyotokea siku za lile Teketezo la Umati la Ujeremani ya Nazi.

Krusedi ziliongezea pia mkazo wa Mashariki na Magharibi ambao ulikuwa umekuwa ukiendelea tangu 1054, wakati Patriaki Michael Cerularius wa Mashariki na Kadinali Humbert wa Magharibi walipoondoana katika ushirika. Wakrusedi walipoweka maaskofu Walatini ili wachukue mahali pa makasisi Wagiriki katika majiji waliyoteka, fumukano la Mashariki na Magharibi likaja kugusa watu wa kawaida.

Mvunjiko kati ya yale makanisa mawili ukawa kamili wakati wa Krusedi ya Nne wakati ambapo, kulingana na aliyekuwa Kanoni Mwanglikani wa Canterbury, Hebert Waddams, Papa Innocent 3 alitumia “hila mbili.” Kwa upande mmoja, papa alighadhibika juu ya kuporwa kwa Konstantinopo. (Ona sanduku katika ukurasa wa 16.) Aliandika hivi: “Kanisa la Wagiriki laweza kutarajiwaje lirudie ujitoaji kwenye Jimbo la Kimitume hali limeona Walatini wakiweka kielelezo cha uovu na kutenda kazi ya ibilisi hivi kwamba tayari Wagiriki wawachukia vibaya kuliko mbwa, tena kwa sababu njema.” Kwa upande mwingine, kwa utayari aliitumia hali hiyo kwa kuanzisha ufalme wa Kilatini huko chini ya patriaki wa magharibi.

Baada ya karne mbili za pigano ambalo lilikuwa karibu kuwa la uendelevu, Milki ya Baizantino ilidhoofishwa sana hivi kwamba haikuweza kuhimili mashambulizi ya Waturuki Waottoman, ambao, siku ya Mei 29, 1453, waliteka Konstantinopo mwishowe. Milki hiyo ikawa imekatwakatwa si na upanga wa Kiislamu tu bali na upanga uliotumiwa na kanisa dada la milki katika Roma pia. Jumuiya ya Wakristo yenye migawanyiko ikawa imeupa Uislamu msingi ufaao wa kuingia Ulaya.

Panga za Siasa na Mnyanyaso

Krusedi ziliimarisha cheo cha papa cha uongozi wa kidini na wa kisiasa. ‘Ziliwapa mapapa mamlaka ya kudhibiti ubalozi wa Ulaya,” aandika mwanahistoria John H. Mundy. Muda si muda “kanisa likawa ndilo serikali kubwa zaidi ya Ulaya . . . , [likiweza] kutumia mamlaka nyingi ya kisiasa kuliko serikali nyingine yoyote ya Magharibi.”

Kukwea kwenye mamlaka hivyo kulikuwa kumewezekana wakati Milki ya Magharibi ya Kiroma ilipoanguka. Kanisa liliachwa likiwa mamlaka ya pekee ya muungamanisho katika Magharibi na kwa hiyo lilianza kushiriki sehemu ya utendaji mwingi zaidi wa kisiasa katika jamii ya watu kuliko kanisa la Mashariki, ambalo wakati huo lilikuwa lingali chini ya mtawala imara wa kilimwengu, maliki wa Baizantino. Umashuhuri huu wa kisiasa wenye kushikiliwa na kanisa la Magharibi ulitoa sababu ya kuamini dai lalo la kuwa na umashuhuri wa kipapa, wazo ambalo kanisa la Mashariki lilikataa. Ingawa liliruhusu jambo la kwamba papa alistahiki heshima, kanisa la Magharibi halikuwa na mwafaka kwamba yeye alikuwa na mamlaka ya mwisho juu ya fundisho au eneo la utawala.

Kwa kusukumwa na mamlaka ya kisiasa na usadikisho wa kidini wenye kuongozwa vibaya, Kanisa Katoliki la Kiroma lilinyoosha mkono likashika upanga ili kufagilia mbali upinzani. Shughuli yalo ikawa ni kuwinda wazushi. Maprofesa wa historia Miroslav Hroch na Anna Skýbová wa Chuo Kikuu cha Karls katika Prague, Chekoslovakia, waeleza jinsi Baraza la Kuhukumu Wazushi lilivyoendesha mambo: “Tofauti na zoea la ujumla, majina ya wapashaji-habari za watu . . . haikuwa lazima yafunuliwe.” Papa Innocent 4 alitoa tangazo rasmi “Ad extirpanda” katika 1252, ambalo liliruhusu kutesatesa. “Kuteketezwa mtini, ambayo ndiyo njia ya kawaida iliyotumiwa kuua wazushi kufikia karne ya 13, . . . kulifananisha jambo, kudokeza kwamba kwa kufikiliza aina hii ya adhabu, kanisa halikuwa na hatia ya kudondosha damu.”

Wanabaraza la kuhukumu wazushi waliadhibu makumi ya maelfu ya watu. Maelfu wengine waliteketezwa mtini, hiyo ikiongoza mwanahistoria Will Durant kueleza hivi: “Kwa kufikiria kila mwanya unaotakwa kwa mwanahistoria na kuruhusiwa kwa Mkristo, ni lazima tulipange Baraza la Kuhukumu Wazushi . . . kuwa miongoni mwa madoa yaliyo meusi zaidi katika rekodi ya ainabinadamu, yenye kufunua ukatili katika hayawani yeyote.”

Matukio ya Baraza la Kuhukumu Wazushi yarudisha akilini maneno ya Blaise Pascal, mwanafalsafa na mwanasayansi Mfaransa wa karne ya 17, aliyeandika hivi: “Hakuna kamwe wakati ambapo wanadamu hufanya uovu kwa ukamili sana na kwa uchangamfu kama wakati waufanyapo kutokana na usadikisho wa kidini.” Kwa ukweli, kupungapunga upanga wa mnyanyaso dhidi ya watu wa imani tofauti za kidini kumekuwa tabia ya dini bandia muda wote tangu Kaini alipoua Abeli kwa kumpiga dharuba.—Mwanzo 4:8.

Katenganishwa na Upanga wa Kutoungamana

Mgawanyiko wa kutukuza taifa na kuelekeza mambo kwa werevu wa kisiasa kuliongoza katika uhamisho wa makao ya papa katika 1309 kutoka Roma kupelekwa Avignon. Ingawa yalirudishwa Roma katika 1377, ugomvi zaidi ulisababishwa muda mfupi baada ya hapo kwa kuchagua papa mpya, Urban 6. Lakini kikundi kile kile cha makadinali waliomchagua kilichagua pia papa mshindani, Clement 7, aliyelowea katika Avignon. Mambo yakavurugika hata zaidi mwanzoni mwa karne ya 15, wakati ambapo kwa muda mfupi mapapa watatu walikuwa wanatawala kwa wakati ule ule mmoja!

Hali hii, ambayo yajulikana kuwa fumukano la Magharibi au Fumukano Kubwa, ilimalizwa na Baraza la Constance. Lilitokeza kanuni ya upatanisho, nadharia ya kwamba mamlaka ya mwisho ya uanadini imo katika mabaraza makuu wala si katika upapa. Hivyo, katika 1417 baraza liliweza kuchagua Martin 5 kuwa papa mpya. Ingawa kwa mara nyingine tena liliungamana, kanisa lilikuwa limetiwa udhaifu mzito. Hata hivyo, yajapokuwako makovu hayo upapa ulikataa kutambua uhitaji wowote wa kufanya marekebisho makubwa. Kulingana na John L. Boojamra, wa Seminari ya Theolojia ya Kiorthodoksi ya Mtakatifu Vladimir, kushindwa huku “kuliweka msingi wa yale Marekebisho ya karne ya kumi na sita.”

Je! Walikuwa Wakiishi Kulingana na Dini Yao?

Mwanzishi wa Ukristo aliagiza wafuasi wake wafanye wanafunzi lakini hakuwaambia watumie ulazimisho wa kimwili kufanya hivyo. Kwa uhakika, yeye alionya kihususa kwamba “wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.” Vivyo hivyo, yeye hakuagiza wafuasi wake wamtese kimwili mtu yeyote asiye na uelekeo wenye kupendeleka. Hii ndiyo kanuni ya Kikristo iliyopasa kushikwa: “Haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye.”—Mathayo 26:52; 2 Timotheo 2:24, 25.

Kwa kugeukia upanga halisi wa vita, na pia panga za ufananisho za siasa na mnyanyaso, kwa wazi Jumuiya ya Wakristo haikuwa ikifuata uongozi wa Mmoja ambaye ilidai kuwa ndiye Mwanzishi wayo. Ikiwa tayari imeharibiwa kabisa na ukosefu wa muungamano, ilitishika kuangamia kabisa. Ukatoliki wa Kiroma ulikuwa “Dini Yenye Kuhitaji Sana Marekebisho.” Lakini je! marekebisho yangekuja? Ikiwa ndivyo, wakati gani? Kutoka kwa nani? Toleo letu la Juni 8, 1990 litatuambia mengi zaidi.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]

Je! Ni Vita Vizuri vya Kikristo?

Je! Krusedi zilikuwa vita vizuri vya Kikristo ambavyo Wakristo waliagizwa kufanya?—2 Wakorintho 10:3, 4; 1 Timotheo 1:18.

Krusedi ya Kwanza (1096-99) ilikuwa na tokeo la kuteka upya Yerusalemu na kuanzishwa upya kwa dola nne za Kilatini katika Mashariki: Ufalme wa Yerusalemu, Tarafa ya Edessa, Dola ya Mwana-Mfalme ya Antiokia na Tarafa ya Tripoli. Mwenye mamlaka mmoja aliyenukuliwa na mwanahistoria H. G. Wells asema hivi juu ya kutekwa kwa Yerusalemu: “Machinjo yalikuwa mabaya sana; damu ya washinde ilitiririka barabarani, mpaka watu wakawa wanarashiwa damu walipopanda. Usiku ulipoingia, wakrusedi walikuja kwenye mahali pa kuzikia kutoka kwenye mkanyago wao wa shinikizo-divai, na wakaweka mikono yao pamoja kwa sala.”

Krusedi ya Pili (1147-49) ilianzishwa kwa sababu ya Tarafa ya Edessa kushindwa na Waislamu Wasiria katika 1144; ilimalizika wakati Waislamu walipofanikiwa kuwazuia “makafiri” wa Jumuiya ya Wakristo.

Krusedi ya Tatu (1189-92), iliyofanywa baada ya Waislamu kuteka Yerusalemu, ilikuwa na Richard 1 akiwa mmoja wa viongozi wayo, “yule Mwenye Moyo wa Simba,” wa Uingereza. Baada ya muda mfupi “ilizorota,” yasema The Encyclopedia of Religion, “kupitia kuzozana, kugombana, na kukosa ushirikiano.”

Krusedi ya Nne (1202-4) iligeuzwa upande wakati pesa zilipokosekana kutoka Misri kuja Konstantinopo; usaidizi wa kimwili uliahidiwa kwa kusaidia kumtawaza Alexius, mhamishwa Mbaizantino mwenye kusingizia kuwa ndiye mfalme. “Utekaji nyara [uliotokea] wa Konstantinopo kwa kufanywa na Wakrusedi ni jambo ambalo Mashariki ya Kiorthodoksi haijasahau kamwe wala kusamehe,” yasema The Encyclopedia of Religion, ikiongezea hivi: “Ikiwa tarehe yoyote moja yapasa kutajwa kuwa mwanzo thabiti wa fumukano, yenye kufaa zaidi—kulingana na maoni ya kiakili—hiyo ni mwaka 1204.”

Krusedi ya Watoto (1212) ilileta kifo kwa maelfu ya watoto Wajeremani na Wafaransa kabla hata hawajafika walikokuwa wakielekea.

Krusedi ya Tano (1217-21), ya mwisho chini ya udhibiti wa papa, ilikosa mafanikio kwa sababu ya uongozi wenye dosari na kuingilia kwa makasisi.

Krusedi ya Sita (1228-29) iliongozwa na Maliki Frederick 2 wa Hohenstaufen, ambaye Papa Gregori 9 alikuwa amemwondosha katika ushirika hapo kwanza.

Krusedi za Saba na Nane (1248-54 na 1270-72) ziliongozwa na Louis 9 wa Ufaransa lakini zikakosa kufanikiwa baada ya kufa kwake katika Afrika Kaskazini.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Eneo la makaburi ya Kiyahudi katika Worms, Ujeremani—kikumbusha cha Krusedi ya Kwanza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki