Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/8 kur. 12-15
  • Zile Krusedi—“Uwongo Wenye Msiba”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Zile Krusedi—“Uwongo Wenye Msiba”
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Visababishi
  • Mwito Katika Clermont
  • Kuondoka Mara Mbili
  • Ushindi na Machinjo-Chinjo Mengine
  • Mwisho wa Uwongo
  • Somo Lapuuzwa
  • Sehemu ya 15: 1095-1453 W.K.— Kugeukia Upanga
    Amkeni!—1990
  • Bado Mataifa Hayajajifunza Somo
    Amkeni!—2002
  • Kung’ang’ania Eneo “Takatifu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Uasi-Imani—Njia ya Kwenda Kwa Mungu Yazibwa
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/8 kur. 12-15

Zile Krusedi—“Uwongo Wenye Msiba”

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ITALIA

MIAKA ipatayo mia tisa iliyopita, katika mwaka wa 1096, Krusedi ya Kwanza ilikuwa karibu kuanza. Kama ungaliishi katika Ulaya ya Magharibi wakati huo, huenda ungalishuhudia misafara mikubwa ya watu, magari ya kukokotwa, farasi, na meli. Misafara hiyo ilikuwa ikienda Yerusalemu, lile jiji takatifu, ambalo lilikuwa limekuwa chini ya udhibiti wa Waislamu tangu karne ya saba W.K.

Hiyo ilikuwa ya kwanza kati ya zile Krusedi. Wanahistoria wengi huorodhesha Krusedi nane kubwa. Misafara hiyo iliharibu historia ya mahusiano kati ya Mashariki na Magharibi. Ziliandamana na machinjo makubwa na ukatili uliofanywa kwa jina la Mungu na la Kristo. Krusedi kubwa ya mwisho ilianza miaka 174 baadaye, katika mwaka wa 1270.

Neno “krusedi” latokana na neno la Kilatini crux, limaanishalo “msalaba.” Washiriki wa misafara mingi walishonelea ishara ya msalaba katika mavazi yao.

Visababishi

Kusudi lililotangazwa la zile Krusedi lilikuwa kutwaa Yerusalemu na lile lililoitwa eti kaburi takatifu kutoka kwa Waislamu. Lakini kulikuwa na visababishi zaidi. Mbali na visa vichache, mahusiano kati ya wale waliodai kuwa Wakristo walioishi katika Mashariki ya Kati na Waislamu yalikuwa yamekuwa matulivu kwa kulinganisha. Jambo kubwa lililotokeza zile Krusedi lilikuwa hali mbaya ya kisiasa, ya kiuchumi, na ya kidini ambayo ilienea katika Ulaya.

Katika karne ya 11, maeneo mapya ya mashambani yalikuwa yakifyekwa ili yatumike kwa kilimo, katika jitihada za kuongeza mazao ya chakula. Maeneo ya jiji yalikuwa yamevuvumka. Idadi ya watu ilikuwa ikiongezeka. Hata hivyo, njaa kuu iliposababisha wakulima wengi wadogo-wadogo wawe maskini, wengi walimiminikia majiji, ambako ukosefu wa kazi za kuajiriwa na taabu iliwangoja. Mara nyingi mateto yalifyatuka.

Kileleni mwa matabaka ya jamii mlikuwa na wakuu wenye kutawala. Wakuu hao walio wataalamu wa vita walitaka kutumia kwa faida yao fursa iliyoachwa na kuvunjika kwa milki ya Charlemagne na kutwaa mashamba mapya.

Kanisa la Roma lilikuwa pia katika kipindi cha mvurugo. Katika mwaka wa 1054 lilishindwa kudhibiti Kanisa la Mashariki. Kwa kuongezea, wengi wa makasisi walikuwa wakishtakiwa kwa ukosefu wa maadili na kwa kujiingiza katika siasa.

Mwito Katika Clermont

Katika hali hii Krusedi ya Kwanza iliitishwa na Papa Urban wa Pili. Kwa maoni yake kuchukua hatua za kijeshi za kutwaa tena Yerusalemu na Palestina kungetimiza makusudi kadhaa. Kungeimarisha muungano wa Jumuiya ya Wakristo ya Magharibi na kuthibitisha tena ukuu wa Kanisa Katoliki. Kungeandaa njia ya kupoza mizozo ya daima miongoni mwa matabaka ya juu. Kwa kupata manufaa za kidini na zaidi ya yote ya kiuchumi, hao wangetumia ustadi wao wa kijeshi kwa makusudi “mazuri,” wakiwa jeshi la kanisa.

Novemba 27, 1095, kabla ya baraza lililofanywa huko Clermont, Ufaransa, Urban alianzisha mwito wake. Kanisa lilifafanua vibaya maadui wao, likisisitiza kwamba walistahili adhabu ya Mungu. Foucher de Chartres, kasisi aliyeshiriki katika Krusedi ya Kwanza, alisema kwamba hiyo vita ilihitajiwa ili kulinda “Wakristo” wa Mashariki dhidi ya Waislamu. Wale ambao wangekufa wakiwa njiani au vitani waliahidiwa kuondolewa dhambi papo hapo. Badala ya kuzozana wao kwa wao, wakuu hao wenye kutawala sasa wangeweza kupiga vita “takatifu” dhidi ya “makafiri.” Katika baraza hilo, mwito uliotolewa kwa nguvu ukawa shime ya Krusedi ya Kwanza: “Ni mapenzi ya Mungu!”

Kuondoka Mara Mbili

Tarehe ya kuondoka, Agosti 15, 1096, ilipowekwa tu, papa alihakikisha kwamba amepata tegemezo la wakuu wenye kutawala, ambao walikabidhiwa mipango ya kijeshi. Kanisa lilihakikisha litalinda mashamba ya wakuu hao katika kipindi ambacho wangekuwa vitani. Wale wasio matajiri walihimizwa wadhamini kifedha utume huo kwa upaji.

Hata hivyo, wengine waliondoka kabla ya tarehe iliyowekwa. Huu ulikuwa umati usiozoezwa na usio na nidhamu ambao ulitia ndani wanawake na watoto. Waliitwa pauperes Christi (Maskini wa Kristo). Mradi wao: Yerusalemu. Wao waliongozwa na wachocheaji wa umma, labda aliye mashuhuri zaidi akiwa Peter the Hermit, mtawa ambaye alikuwa ameanza kuhubiri miongoni mwa umma kuelekea mwisho wa mwaka wa 1095.

Kulingana na mrekodi-matukio wa enzi za kati Albert wa Aix, awali Peter alikuwa amesafiri hadi Yerusalemu. Ilisemwa kwamba usiku mmoja alipata ono ambamo Kristo alimhimiza amwendee askofu-mkuu wa Yerusalemu, ambaye angempa barua ya kumstahilisha arudishe Magharibi. Albert alisema kwamba ndoto hiyo ilitimia na kwamba baada ya kupokea hiyo barua, Peter alifunga safari ya kwenda Roma, ambapo alikutana na papa. Masimulizi ya Albert huchanganya mambo halisi pamoja na fantasia, lakini zile zisemwazo eti ni ndoto, maono, na barua zilikuwa njia zenye nguvu za kuongoza umma.

Kikundi ambacho kilimkusanyikia Peter the Hermit kilitoka Cologne Aprili 20, 1096. Bila kuwa na namna ya kusafiri kupitia bahari, pauperes walilazimika kukabili safari ndefu ya kwenda Bara Takatifu kwa miguu au katika magari ya kukokotwa yaliyochakaa. Punde si punde wakijikuta kwamba kumbe hawana chakula wala silaha, njiani wakaanza kuwapora watu wa sehemu hizo waliopigwa butaa kwa kuwasili kwa kikosi hiki cha “askari-jeshi wa Kristo” wasio na nidhamu.

Waliopambana nao kwanza walikuwa Wayahudi wa Ulaya, ambao walishtakiwa kwa kuwakopesha pesa maaskofu wafisadi. Ukatili mbalimbali ulifanywa na wafuasi wa Peter the Hermit dhidi ya Wayahudi, katika sehemu kama vile Rouen na Cologne, jiji waliloanzia safari. Albert wa Aix ataarifu kwamba Wayahudi katika Mainz “walipoona kwamba Wakristo hata hawakuwaacha watoto wao wala kumwonea huruma mtu yeyote, hao Wayahudi walishambulia ndugu zao, wake zao, mama zao, na dada zao nao walichinjana. Jambo lenye kusikitisha mno ni kwamba akina mama wenyewe walikata shingo za watoto wao waliokuwa wakinyonya au kuwadunga hadi kifo, wakiona ni bora watoto wao wafe mikononi mwao kuliko kuuawa kwa mikono ya wasiotahiriwa.”

Visa kama hivyo vilirudiwa njiani kuelekea Balkani, wakienda Asia Ndogo. Umati huo ulipofika tu Konstantinopo, Maliki Alexius wa Kwanza alifanya mpango wa pauperes kupitia wakienda ufuo wa Asia ili kisa kama kile kisirudiwe. Huko, wanawake na watoto wengi na vilevile wagonjwa na wazee-wazee walichinjwa-chinjwa na majeshi ya Waislamu. Ni waokokaji wachache tu waliofaulu kurudi Konstantinopo.

Kwa wakati uo huo, katika kiangazi cha mwaka wa 1096, majeshi yaliyozoezwa yalianza safari. Hayo yaliongozwa na viongozi mashuhuri wa wakati huo. Kuondoka mapema kwa wale pauperes wasiotawalika kulikuwa kumemhangaisha Papa Urban, ambaye alifanya mipango ya kudhibiti misafara ya kwenda Mashariki. Wale waliokuwa wakiondoka sasa walipaswa kuthibitisha kwamba walikuwa na ugavi wa kutosha wa chakula. Kusudi lilikuwa kupunguza ushiriki wa wanawake, watoto, wazee-wazee, na maskini.

Ushindi na Machinjo-Chinjo Mengine

Baada ya kukutana pamoja katika Konstantinopo, majeshi, wakuu, na wale pauperes waliookoka waliendelea mbele kuelekea mradi wao. Tena, visa vya ujeuri vilifanywa katika jina la Mungu. Mrekodi-matukio Petrus Tudebodus asimulia kwamba wakati wa kuzingirwa kwa Antiokia, baada ya kuwachinja-chinja maadui, hao wafanya-krusedi “waliitupa miili yao yote katika kaburi moja na kuleta vichwa vyao vilivyokatwa katika kambi [yao] ili kujua idadi yao, bila kutia ndani vichwa vilivyobebwa na farasi wanne, ambavyo vilipelekwa pwani, kwa mabalozi wa kadhi wa Babiloni.”

Julai 15, 1099, Yerusalemu lilianguka mikononi mwa wale wafanya-krusedi. Raymond wa Aguilers asimulia: “Tamasha ya kuogofya sana ingeweza kuonekana. Baadhi ya [maadui], wale waliosalimika, walikuwa wamekatwa-katwa viungo, wengine walianguka kutoka ukutani wakiwa wamejaa mishale; wengine wengi walichomeka katika miale. Marundo ya vichwa, mikono, na miguu zilizokatwa zingeweza kuonekana barabarani na katika mabaraza ya jiji.” Lakini tena, hao wafanya-krusedi walijaribu kutetea ujeuri huo katika jina la dini.

Mwisho wa Uwongo

Ushindi huo ulitokeza Ufalme wa Kilatini wa Yerusalemu. Kuwako kwa ufalme huo kulikuwa hatarini kwa sababu ya upinzani ambao punde si punde ulifyatuka kati ya wakuu wenye kutawala ambao walikuwa wamejisitawisha katika Mashariki. Kwa wakati uo huo, Waislamu walijipanga tena vizuri kijeshi. Hakika, wao hawakutaka kupoteza eneo katika Palestina.

Baadaye, Krusedi nyinginezo zilipangwa, ya mwisho ikifanywa katika mwaka wa 1270. Lakini, kwa sababu ya kushindwa-shindwa, wengi walianza kutilia shaka uhalali wa kufanya krusedi katika jina la dini. Ikiwa kweli Mungu alikubali vita hivi “vitakatifu,” wao walifikiri, kwa hakika angependelea wale waliodai kutenda kwa baraka yake. Na bado, tokea karne ya 13 na kuendelea, wazee wa kanisa walijaribu kutetea vita kama hivyo vya kidini na fungu la makasisi katika vita hivyo.

Ile juhudi iliyochochea wafanya-krusedi wa kwanza ikapoa. Zaidi ya jambo jinginelo lote, kuendelea kwa vita hivyo kungeharibu hatimaye masilahi ya kiuchumi ya Magharibi. Basi wakaanza kupiga vita dhidi ya maadui waliokuwa katika Jumuiya ya Wakristo ya Ulaya: wale Waarabu waliokuwa Hispania, “wazushi,” na wapagani wa Kaskazini.

Katika mwaka wa 1291 jiji la Acre, lililokuwa ngome ya mwisho ya wafanya-krusedi, liliangushwa na Waislamu. Yerusalemu na ‘Kaburi Takatifu’ lilibaki mikononi mwa Waislamu. Katika karne mbili za mapambano, masilahi ya kiuchumi na kisiasa yalikuwa yamedhibiti masuala ya kidini. Mwanahistoria Mwitalia Franco Cardini aonelea: “Kufikia wakati huu zile Krusedi zilikuwa zimebadilika polepole kuwa utendaji wenye uangalifu sana wa kisiasa na kiuchumi, mchezo tata wa mamlaka uliohusu maaskofu, wakuu wa watawa, wafalme, wakusanya-upaji, wakuu wa mabenki. Katika mchezo huu . . . ni kaburi la Yesu lililopoteza umaana wote.” Pia Cardini asema: “Historia ya zile Krusedi ni historia ya kosa kubwa zaidi, udanganyifu tata zaidi, uwongo wenye msiba zaidi, na katika njia nyinginezo wenye upuuzi zaidi katika Jumuiya ya Wakristo yote.”

Somo Lapuuzwa

Zile Krusedi na kushindwa kwake zingalipaswa kufundisha kwamba pupa ya kiuchumi na tamaa ya kupata umashuhuri wa kisiasa kwaweza kutokeza ushupavu na machinjo. Lakini somo hilo limepuuzwa. Uthibitisho umeonekana katika jambo la kwamba mapambano mengi yameendelea kuchafua sehemu nyingi za sayari yetu kwa damu. Katika mapambano haya, mara nyingi dini imetumika ikiwa sababu ya kufanya mambo yenye kuchukiza.

Hata hivyo, hali hii haitaendelea kwa muda mrefu. Karibuni sana roho iliyochochea zile Krusedi na ambayo inaendelea kuchochea vita vya siku ya kisasa vilivyo “takatifu” itapotelea mbali pamoja na dini yote isiyo ya kweli na mfumo wote unaodhibitiwa na Shetani.—Zaburi 46:8, 9; 1 Yohana 5:19; Ufunuo 18:4, 5, 24.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]

The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck

[Picha katika ukurasa wa 15]

Juu: Kaburi la Kiyahudi katika Worms, Ujerumani—kikumbusha cha machinjo ya Krusedi ya Kwanza

Kushoto: Mchongo wa kichwa cha mfanya-krusedi

Kushoto zaidi: Nembo ya familia moja mashuhuri katika kufanya krusedi

[Hisani]

Nembo na kichwa: Israel Antiquities Authority; picha: Israel Museum, Jerusalem

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki