Kung’ang’ania Eneo “Takatifu”
KATIKA Julai 15, 1099, Krusedi ya Kwanza iliyoidhinishwa na papa wa Roma, ilitimiza mradi wake wa kuteka Yerusalemu. Uchinjaji uliofanywa ulikuwa wenye kuogofya! Wakazi pekee walionusurika walikuwa gavana na mlinzi wake wa kibinafsi, baada ya rushwa kubwa kutolewa. Katika kitabu chake The Crusades, kasisi Antony Bridge aripoti kuhusu yaliyowapata wakazi wale wengine ambao walikuwa Waislamu na Wayahudi: “Mara wale waliopigana katika Krusedi waliporuhusiwa kufanya waliyotaka jijini humo, walishindwa na uchu mkubwa wenye kutisha wa kutaka kumwaga damu. . . . Waliua kila mwanamume, mwanamke na mtoto walioweza kupata jijini humo . . . Walipomaliza kuua watu wote, washindi hao walifanya mwandamano kupitia barabara za jiji hilo . . . kwenda kwenye Kanisa la Kaburi Takatifu ili kumshukuru Mungu.”
Tangu wapiganaji hao wa krusedi washinde, kuwapo kwa Jumuiya ya Wakristo huko Yerusalemu kumebainishwa na mabishano kati ya Katoliki, Othodoksi ya Mashariki, na dini nyingine zinazodaiwa kuwa za Kikristo. Katika mwaka wa 1850 mabishano kati ya viongozi mbalimbali wa makanisa juu ya maeneo matakatifu ya Yerusalemu pamoja na mazingira yake yalichangia sana kuzuka kwa Vita ya Crimea. Ufaransa, Uingereza, na Serikali ya Uturuki zilipigana dhidi ya Urusi, vita iliyosababisha vifo vya watu nusu milioni.
Vita hiyo haikukomesha mabishano kati ya Jumuiya ya Wakristo kuhusu Yerusalemu na maeneo yake matakatifu. Waturuki, ambao wakati huo walitawala nchi hiyo, walijaribu kuleta amani kwa kugawanya maeneo hayo matakatifu miongoni mwa dini mbalimbali. “Kanuni hiyo,” aeleza Dakt. Menashe Har-el katika kitabu chake This Is Jerusalem, “ilikubaliwa . . . na Umoja wa Mataifa wakati Azimio la Kugawanya la Novemba 1947 lilipotolewa. Hivyo, azimio hilo ni sehemu ya sheria ya kimataifa.” Tokeo limekuwa kwamba Kanisa la Kaburi Takatifu limemilikiwa kwa pamoja na Wakatoliki, Othodoksi la Kigiriki, Waarmenia, Wasiria, na Wakoptiki. Hatimaye, Waethiopia (yaani, watawa wa kiume wa Kanisa la Wahabeshi) nao hutetea haki yao ya kuwa na sehemu katika kanisa hilo kwa kuwafanya washiriki fulani waishi katika vibanda kwenye paa lake. Wengi huliona Kanisa la Kaburi Takatifu kuwa eneo lililo takatifu zaidi la Jumuiya ya Wakristo. Limejazwa vihekalu, sanamu, na picha za watakatifu. Eneo jingine liitwalo Gordon’s Calvary, ambalo hudaiwa kuwa takatifu, hupewa staha ya kiibada na baadhi ya Waprotestanti kama mahali padhaniwapo kuwa Yesu aliuawa na kuzikwa.
Wakati mrefu uliopita, Yesu alimwambia mwanamke aliyeamini katika maeneo matakatifu hivi: “Saa inakuja wakati ambapo wala si katika mlima huu wala katika Yerusalemu nyinyi watu mtamwabudu Baba. . . . Waabudu wa kweli watakapomwabudu Baba kwa roho na kweli.” (Yohana 4:21-24) Hivyo, Wakristo wa kweli hawayatolei staha ya kiibada maeneo matakatifu. Kuharibiwa kwa Yerusalemu lisilo jaminifu na jeshi la Waroma katika mwaka wa 70 W.K. kwabaki kuwa onyo kwa Jumuiya ya Wakristo. Ibada yake ya sanamu, migawanyiko, na hatia yake ya damu yathibitisha kuwa la uwongo lile dai lake kuwa ni ya Kikristo. Kwa hiyo, yeye atapatwa na mwisho ambao Mungu ametabiri kupata dini zote zinazofanyiza Babiloni Mkubwa.—Ufunuo 18:2-8.