Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 3/8 kur. 21-23
  • Napaswa Kufanya Nini Watu Wakipiga Porojo Kuhusu Mimi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Napaswa Kufanya Nini Watu Wakipiga Porojo Kuhusu Mimi?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Lile Umivu la Porojo
  • Epuka Kitendo cha Kupita Kiasi!
  • Mbinu za Kushughulika na Porojo
  • Hayo Uliyojionea Ni Somo
  • Porojo Jinsi ya Kuepuka Kujiumiza Mwenyewe na Wengine
    Amkeni!—1992
  • Nifanye Nini Ikiwa Watu Wanaeneza Porojo Kunihusu?
    Vijana Huuliza
  • Ninaweza kuzuiaje porojo?
    Amkeni!—2007
  • Porojo Ina Ubaya Gani?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 3/8 kur. 21-23

Vijana Wauliza . . .

Napaswa Kufanya Nini Watu Wakipiga Porojo Kuhusu Mimi?

“ASILIMIA tisini na tano ya watu walio katika shule yetu ya sekondari hupiga porojo,” asema mwanafunzi mmoja wa kidato cha pili katika shule moja ya sekondari ya New York. Wao hupiga porojo kuhusu nini hasa? “Wanafunzi wengine: nyutu zao, jinsi sura zao zilivyo, nani apenda nani, na mambo ambayo wao husema kuhusu mmoja na mwenzake.”—Gazeti Seventeen, Julai 1983.

Ingawa hivyo, mara nyingi porojo huelekezwa kwenye mambo yasiyofaa na hutokeza hasara nzito kwa sifa ya wengine.a Na kwa kuwa porojo huzoewa kila mahali ulimwenguni miongoni mwa vijana na pia watu wazima, kuna elekeo kubwa la kwamba wewe mwenyewe ni jeruhi wa kupigiwa porojo zenye kuumiza (au siku fulani itakuwa hivyo kwako). Ikiwa ndivyo, waweza kufanya nini? Je! kuna njia yoyote ya kukomesha ubwabwaji huo wenye kuumiza?

Lile Umivu la Porojo

Hakuna shaka kwamba: Wewe huumia kweli kweli habari za kibinafsi zikitobolewa kwa wengine au ukiwa jeruhi wa uvumi wa bandia. Huenda hisia za kasirani na za kulipa kisasi zikaandamana na vipindi vya umizo na mshuko wa moyo. “Hiyo hufanya uhisi ukitaka kuumiza mtu yule,” akasema jeruhi mmoja wa kupigiwa porojo. Mwingine alisema: “Wahisi umepondeka [roho]; ni kama kudungwa mgongoni. Yaweza kukufanya uhisi hutaki kamwe kunena na watu hao tena. Huwa umeacha kabisa kuwaamini, nawe washindwa kabisa kuacha kufikiria tatizo lile.”

Kweli kweli, porojo zimesababisha vijana wengi walemewe kabisa na aibu. Hivyo msichana mmoja mchanga alihamia shule nyingine kuliko kuonana uso kwa uso na vijana walioshiriki kueneza uvumi mbaya usiopendeza kamwe kumhusu. Hata hivyo, kulipa kisasi, kasirani, wala kuona aibu yenye kukumaliza nguvu hakuleti hata chembe moja ya maendeleo katika hali ile. Kuna njia zenye matokeo mazuri zaidi za kushughulika na maongeo yaliyo kinyume.

Epuka Kitendo cha Kupita Kiasi!

Kabla hujafanya lolote, kumbuka hivi: “Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga.” (Mithali 14:17) Ujumbe hapo ni nini? Kwamba usifanye kitendo cha kupita kiasi! Mara nyingi vitendo vya haraka-haraka hufanyiza matatizo mengi kuliko yale ambayo huyatatua. Biblia yatahadharisha hivi: “Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.” Kwa nini? Kwanza, huwezi kamwe kukomesha watu wasiongee kuhusu watu wengine. Kunenewa ni sehemu tu ya maisha. Sulemani alizidi kushauri hivi: “Usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa . . . Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana [umewalaani viovu, NW] watu wengine.”—Mhubiri 7:9, 21, 22.

Sulemani hakuwa akitetea kwamba ni haki kupiga porojo zisizofaa. Alikuwa akitambua tu kwamba huu ni uhakika wa maisha. Hata uchukizwe namna gani kwa sababu ya kunenewa, je! si kweli kwamba labda wewe umenenea wengine mambo ambayo ingalikuwa afadhali zaidi kama yasingalinenwa?

Katika kitabu chake Gossip, Patricia Meyer Spacks alionelea hivi: “Zilizo za kawaida zaidi ni porojo ambazo hazitokani na nia mbaya ya kuumiza kwa makusudi bali . . . zenye kutokana na kutofikiri . . . Hutokana na tamaa isiyofikiriwa vizuri ya kusema jambo fulani bila kufikiri kwa kina kirefu. Bila kukusudia, wapiga-porojo huelezana-elezana vijineno na habari za kusisimua kuhusu watu wengine.” Kung’amua hivi huenda kukasaidia kusawazisha ghadhabu yako.

Mbinu za Kushughulika na Porojo

Mithali 14:15 yasema kwamba “mwenye busara huangalia sana aendavyo.” Hii ingedokeza kupanga ramani ya uangalifu kuhusu mbinu fulani ya kushughulika na porojo kwa matokeo mazuri.

Ungeweza kuanza kwa kufikiria porojo hizo zina uzito gani. Labda hadithi inayoenea kukuhusu, ijapokuwa ni yenye kuaibisha au hata isiyo ya kweli, ni ya kuchekesha sana na kwa kweli haiharibu sifa yako. Ndiyo kusema, ingalikuwa ni afadhali zaidi kama ulimwengu usingalijua kwamba ulisahau ufunguo wa nyumba yako na ukanyeshewa na mvua kali ukiwa umesimama hapo nje au kwamba kaptura yako ilipasuka miguuni katikati ulipokuwa ukijiinua-inua juu-chini kwa mazoezi ya mwili, lakini kwa sababu sasa habari hizo zimefikia watu, je! hilo kweli ni jambo ku-u-u-bwa mno? Labda njia bora zaidi ya kuacha uvumi ule ufifie na kumalizika ni kwamba wewe uonyeshe hali ya ucheshi kuhusiana na jambo hilo.

Ingawa hivyo, iweje kama uvumi ule kwa kweli hauleti sifa nzuri au ni wa kuvunja heshima? Je! kweli huo utaelekea kusababisha hasara ya daima kwa sifa yako—au yaelekea utafifia na kumalizika karibuni? Ikiwa hali hii ya pili ndiyo itaelekea kutukia, huenda jambo bora zaidi likawa ni kuvumilia tu mpaka imalizike. Hali ya ‘kujikaza kiofisaa kama kawaida’—badala ya kutembea-tembea ukiwa umenuna mashavu au ukionyesha sura yenye hatia—angalau kutazuia usiongezee kuni katika uvumi ule. Mithali 26:20 yasema hivi: “Moto hufa kwa kukosa kuni; na bila mchongezi fitina hukoma.”

Ingawa hivyo, nyakati fulani jambo lile huwa ni zito mno lisiweze kupuuzwa. Yesu Kristo alishauri wafuasi wake la kufanya iwapo mtu fulani alisababisha udhia wa kibinafsi kama ule wa kuchongea: “Nenda ukafunue kosa lake kati yako wewe na yeye peke yenu.” (Mathayo 18:15, NW) Hapo huenda ikawezekana kufuatilia mambo mpaka ujue chanzo cha maongeo yale yenye kudhuru na kuzungumzia mambo kwa utulivu pamoja na mtu yule mwenye daraka la kuanzisha uvumi ule.

Ni kweli kwamba, huenda mtu huyo akawa si Mkristo. Lakini ikiwa wajua kwamba ni mtu mwenye kusababu mambo kiakili, labda yeye ataitikia ifaavyo. Huenda ukapata kujua kwamba jambo lote lile limetokana na hali nzito ya kutoelewana vizuri. Ikiwa uchukivu ndilo shina la kufanya vile, labda mwaweza kulainisha jambo hilo kati yenu.

Ingawa hivyo, mara nyingi huwa ni vigumu sana kufuatilia jambo mpaka ujue chanzo cha uvumi. Na hata ukiweza, huenda yule mwenye daraka la kuutokeza asiwe na nia ya kujitwalia jukumu la kusababisha ukosefu huo wa busara. Hapo iweje? Kumbuka kwamba Yesu Kristo alikuwa jeruhi wa “maongeo yaliyo kinyume.” (Waebrania 12:3, NW) Hata hivyo, Yesu hakuudhika sana hata akaacha kazi yake ya kuhubiri na kujiondokea akamtafute mtu yule aliyeanzisha maongeo haya yenye kusumbua. Bali, alisema hivi: “Hekima huthibitishwa na kazi zayo kuwa yenye uadilifu.”—Mathayo 11:19, NW.

Yesu alijua kwamba wale wenye kuamua mambo kihaki wangeona kazi zake nzuri na kukata shauri kwamba maongeo hayo yenye kuumiza hayakuwa na msingi. Vivyo hivyo, acha mwenendo wako uwe ndiyo kinga yako iliyo bora zaidi dhidi ya porojo. Kwa kuwa rafiki zako halisi wajua ukweli ni nini kuhusu wewe, wao hawataamini hadithi za kiajabu-ajabu. Hata hivyo, wewe waweza kuwajulisha kwamba uwongo fulani unaenezwa kuhusu wewe. Mara nyingi wao waweza kusaidia sana kuukandamiza uvumi huo kwa kuusahihisha wakutanapo na watu wowote waliopashwa habari zisizofaa.

Lakini namna gani ikiwa tayari hadithi hiyo imekwisha kuenezwa kwa mapana? Kwa kawaida huwa si mbaya sana kama vile wewe wawazia. Zaidi ya hilo, watu hawaongei kuhusu hali yoyote kwa wakati usio na kikomo. Sikuzote huwa kuna matukio tele ambayo huwa yakiendelea kusitawi wakati ule ule na muda si muda hutokea yakaondoa fikira zote juu yako. Ingawa hivyo, kwa sasa usiteseke ukiwa umejinyamazia. Kwa nini usishiriki hisia zako pamoja na mzazi au mtu mzima mwingine aliyekomaa? Mara nyingi, kuongea mambo wazi husaidia kufanya tatizo lichukuliwe kwa maoni yaliyo sawasawa.

Hayo Uliyojionea Ni Somo

Kuwa jeruhi wa kupigiwa porojo kwakutokezea pia fursa za kujifunza masomo fulani yenye thamani. Kwa kielelezo, ukiisha kujionea binafsi jinsi maongeo ovyoovyo yaweza kuleta hasara, kwa nini usiazimie usiwe kamwe mhusika katika kueneza habari za uvumi?

Usumbufu mkubwa huo wa kupigiwa porojo huenda ukawa umefunua dosari zilizo katika utu wako, kama elekeo la kutafuta kulipa kisasi. Au huenda ikawa kwamba kiburi cha kujivunia heshima yako kimethibitika kuwa tatizo kubwa kuliko hata uvumi wenyewe. Kuhangaikia sifa yako kwa kadiri isiyofaa huenda kukawa kumesababisha ‘ujifikirie zaidi wewe mwenyewe kuliko vile yahitajiwa kufikiri.’ (Warumi 12:3, NW) Sasa huu ungekuwa ndio wakati wa kuanza kujitahidi kupunguza hali yako ya kujichukua kuwa mtu wa maana sana.

Utazamapo nyuma, huenda pia ukang’amua kwamba uamuzi mbaya kwa upande wako ulichangia kuenea kwa uvumi ule. Kwa kielelezo, je! wewe ulisema siri ya mawazo yako ya ndani kabisa kwa kijana aliye na sifa ya ‘kupanua wazi midomo yake’? (Mithali 13:3, NW) Basi labda utachagua msiri wako kwa uangalifu zaidi wakati ule mwingine. Pia utakuwa mwangalifu kujiendesha bila dosari ili usiwape wengine marisau yoyote ya kufyatulia porojo.—Linganisha 1 Petro 2:15.

Ndiyo, shughulikia mambo kwa utulivu na fadhili, nawe waweza kuinuka ukashinda habari za uvumi wa kipumbavu—na labda hata uzikomeshe.

[Maelezo ya Chini]

a Ona makala “Porojo—Zina Madhara Gani?” iliyo katika toleo hili la Amkeni!

[Picha katika ukurasa wa 21]

Nyakati fulani yawezekana kufuatilia mambo mpaka ujue chanzo cha uvumi ule na kufanya zungumzo la ana kwa ana pamoja na mpiga-porojo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki