Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita
Sehemu ya 22: 1900 na kuendelea—Dini Bandia— Yafikiliwa na Wakati Wayo Uliopita!
“Ufunguo wa wakati ujao wa taifa umo kwa wakati wayo uliopita.”—Arthur Bryant, mwanahistoria Mwingereza wa karne ya 20
BABULONI MKUBWA ndilo jina ambalo Biblia huiita milki ya ulimwengu ya dini bandia, ikiifananisha na taifa la kale la Babuloni. (Ufunuo 18:2) Yaliyotendeka kwa milki hiyo ya zamani si dalili nzuri kamwe kwa somo wake wa ki-siku-hizi. Katika usiku mmoja tu katika 539 K.W.K., Babuloni ilianguka mikononi mwa Wamedi na Waajemi chini ya Sairasi Mkubwa. Baada ya kuelekeza kando maji ya Mto Eufrati, yaliyotiririka kupita katika jiji hilo, vikosi vishambulizi viliweza kupita mtoni bila kugunduliwa.
Yehova Mungu na Mwana wake, Yesu Kristo, mfalme mkubwa kuliko Sairasi, atapata ushindi kama huo juu ya Babuloni Mkubwa asiye mwaminifu. Biblia humsimulia kuwa kahaba mkubwa ambaye ameketi juu ya maji mengi, hiyo ikionyesha tegemezo apokealo kutoka kwa “vikundi vya watu na umati wa watu na mataifa na ndimi.” Lakini kabla ya uharibifu, tegemezo hilo, kama “mto mkubwa Eufrati,” ni lazima ‘likauke kabisa, ili njia iweze kutayarishwa kwa ajili ya wafalme kutoka zukio la jua.’—Ufunuo 16:12; 17:1, 15, NW.
Uthibitisho wa kwamba hatua hizo za kukauka kabisa zinatukia leo ungekuwa wenye thamani kubwa sana katika kutambua dini bandia. Je! kuna uthibitisho wowote?
Matazamio Maangavu Yafifia
Karne ya 20 ilipokuwa ikipambazuka, kila mtu wa tatu duniani alidai kufuata Ukristo. Matazamio ya Jumuiya ya Wakristo yalikuwa maangavu. Katika 1900, mwevanjeli na mshindi wa tuzo la Nobeli John R. Mott alionyesha matazamio mazuri, akichapisha kitabu chenye kichwa The Evangelization of the World in This Generation.
Lakini “karne ya 20,” yakiri World Christian Encyclopedia, “imethibitika kuwa tofauti ajabu na matarajio haya.” Ikieleza kwamba “hakuna mtu katika 1900 aliyeitarajia mikengeuko mikubwa ya kuuacha Ukristo ambayo ilitukia baadaye katika Ulaya ya Magharibi kwa sababu ya kufuata uulimwengu, katika Urusi na baadaye Ulaya ya Mashariki kwa sababu ya Ukomunisti, na katika zile Amerika kwa sababu ya ufuatiaji wa vitu vya kimwili,” yasema kwamba hizi na “dini bandia” nyinginezo zilivuvumka “kutoka hali hafifu sana katika 1900, asilimia 0.2 tu ya tufe lote, . . . hadi asilimia 20.8 ya tufe lote kufikia 1980.”
Hii “mikengeuko mikubwa sana” imeacha makanisa ya Ulaya Magharibi yakiwa kama matupu. Tangu 1970 Kanisa la Kilutheri katika Jamhuri ya Mwungano ya Ujeremani limepoteza zaidi ya asilimia 12 ya washiriki wayo. Zaidi ya theluthi moja ya makanisa katika Uholanzi yamefungwa, baadhi yayo yakageuzwa kuwa mabohari, mikahawa, nyumba za kupanga, na hata majumba ya disko. Na katika Uingereza karibu kila kanisa la nane la Kianglikana lililokuwako miaka 30 iliyopita halitumiwi tena. Si ajabu kwamba kasisi mmoja akiongea mwaka juzi kwenye mkutano wa wanatheolojia na makasisi Waprotestanti wa Ulaya alilalamika kwamba “ile ambayo zamani ilikuwa ‘Magharibi ya Kikristo’ haiwezi tena kujiita kuwa ya Kikristo. . . . Ulaya limekuwa shamba la kimisionari.”
Hata hivyo, tatizo hilo lapatikana pia ng’ambo ya Jumuiya ya Wakristo na ng’ambo ya Ulaya. Kwa kielelezo, yakadiriwa kwamba kotekote ulimwenguni, kwa mwaka dini ya Buddha inapoteza watu 900,000 kwa uagnosti (imani ya kwamba ya Mungu hayajulikani).
Ukosefu wa Wafanya Kazi
“Ili uamshe kijiji amsha kwanza mapadri wacho,” yashauri mithali moja ya Kijapani. Lakini mapadri gani? Katika mwongo uliotangulia 1983, hesabu ya mapadri Wakatoliki ulimwenguni pote ilipungua kwa asilimia 7. Na katika muda wa miaka 15, watawa wa kike wakapungua kwa asilimia 33. Kwa sasa, matazamio ya kupata wengine wa kuchukua nafasi hizo ni hafifu. Katika muda unaopungua miaka 20, wenye kuandikishwa kwenye seminari za Kikatoliki katika United States walishuka sana kutoka 48,992 hadi 11,262.
Vyeo vya Kikatoliki vinaathirika pia. Wakati mmoja, Sosaiti ya Yesu, iliyoanzishwa katika Paris katika 1534 na Ignatio wa Loyola, ni kama ndiyo iliyoongoza elimu katika nchi kadhaa. Washiriki wayo, ambayo kwa umaarufu huitwa Wayeswiti, ndio walioongoza katika utendaji wa kimisionari. Lakini tangu 1965, hesabu ya washiriki imepungua kwa zaidi ya robo moja.
Ni ubaya wa kutosha kwamba wafanya kazi wanapungua; lakini ni ubaya hata zaidi kwamba wengi wao hawawezi tena kutumainiwa. Hesabu ya mapadri na watawa wa kike ambao hupinga mwongozo rasmi wa kanisa juu ya useja wa kidini, kudhibiti uzazi, na sehemu ambayo wanawake wapaswa kushiriki katika dini inaongezeka. Hiyo ilionyeshwa katika Januari 1989 wakati wanatheolojia Wakatoliki 163 wa Ulaya walipotoa taarifa ya peupe—kufikia Mei 1 ilikuwa imetiwa sahihi na watu wengine zaidi 500—wakiishtaki Vatikani juu ya kutawala kimamlaka na kutumia vibaya uwezo.
Mamilioni ya watu katika Jumuiya ya Wakristo wamekuwa wafu kiroho, mihanga wa utapiamlo wa kiroho. Mwanakanisa mmoja wa United States alikiri hivyo hivyo alipolalamika hivi: “Kanisa [limekuwa] sokokuu lenye kugawa chakula ovyo cha kiroho kwa wapitaji. Mahubiri ya pasta huwa yakaribia kufanana na bidhaa itangazwayo nyakati zote kuwa ‘bidhaa maalumu ya wiki,’ ambayo hutolewa kwa wahudhuriaji kwa kupunguziwa bei ya wajibu uwapasao kutimiza.”
Tangu 1965, hesabu ya washiriki katika zile madhehebu tano kubwa-kubwa za Kiprotestanti katika United States imeshuka kwa asilimia kama 20 na wenye kujiandikisha katika shule ya Jumapili wamepungua kwa zaidi ya asilimia 50. “Si kwamba madhehebu zile za tangu zamani zinashindwa tu kuwapasha watu ujumbe uwapasao,” laandika gazeti Time, bali pia “zinazidi kutojua vizuri ujumbe huo ni nini hasa.” Kwa sababu ya njaa hiyo ya kiroho, si ajabu sana kwamba majarida mengi ya kanisa yamesimamisha uchapaji. Tayari katika miaka ya katikati ya 1970, mmoja wao aliomboleza hivi: “Ile enzi yenye kawaida ya kuwa na gazeti la kanisa . . . imepita.”
Kundi Lisilojali Mambo na Lisiloitikia
Katika karne ya 18, mwanataifa Edmund Burke aling’amua kwamba “hakuna jambo lenye kuua dini kama kutojali mambo.” Kama angekuwa hai leo, angeona wanadini wasiojali mambo wakiwa tele.
Kwa kielelezo, walipohojiwa miaka kadhaa iliyopita, asilimia 44 ya Walutheri katika United States walisema kwamba kama pasta wao angewaomba waongee na familia zao zisizoenda kanisani juu ya imani yao, wao hawangefanya hivyo. Uchunguzi wa maoni ya watu uliofanywa majuzi ulionyesha kwamba zaidi ya robo tatu za Wakatoliki wa United States huhisi kwamba kutoafikiana na papa, hata juu ya masuala ya kiadili, hakuwakoseshi ustahili wa kuwa Wakatoliki wema.
Katika Japani, asilimia 79 ya idadi ya watu husema kwamba ni jambo la maana kuwa mwanadini. Lakini kwa kuwa, kulingana na Religions of Modern Man, ni theluthi moja tu ambao hudai kuwa na dini, yaonekana kwamba wengi wana kutojali kwingi mno wasiweze kutekeleza mambo.
Watu wazima wasiojali dini huwa kwa kawaida hawana watoto walio na bidii na uitikivu. Uchunguzi ambao mkurugenzi wa Taasisi ya Saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Bonn, Ujeremani, alifanya kwa vijana wa miaka 11 hadi 16 ulifunua kwamba zaidi ya wakati mwingine wowote, vijana wanatafuta nyutu ambazo zitakuwa kigezo chao cha kufuata. Lakini walipoulizwa wao huiga nani kuwa vigezo vyao, vijana walishindwa kutaja viongozi wa kanisa hata mara moja.
Nguvu za Kisiasa Zinamalizika
Dini iliyopangwa kitengenezo haina tena nguvu za kisiasa ilizokuwa nazo wakati mmoja. Kwa kielelezo, hata katika nchi za Kikatoliki zilizo kubwa, Vatikani imeshindwa kuzuia kupitishwa kwa sheria za utoaji mimba, talaka, na uhuru wa kuabudu ambazo kwa wazi haizipendi. Vivyo hivyo, hali zililazimisha Vatikani kuafikiana na mkataba mmoja wa 1984 ulionyang’anya Ukatoliki heshima yao ya kuwa dini kuu ya Italia!
Mambo ambayo dini bandia ilifaulu kuyafanya zamani kwa kutumia werevu wa mkazo wa kisiasa sasa yajaribu kuyafanya kwa harakati za kufanya umma watete kwa kuongozwa na makasisi wayo mashuhuri, kama vile askofu mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini.
Tukiungamana Twasimama, Tukigawanyika Twaanguka
Mkutano mmoja wa 1910 wa sosaiti za kimisionari za Kiprotestanti katika Edinburgh, Scotland, ulizaa harakati ya ki-siku-hizi ya kuleta mwungamano wa makanisa. Harakati hii imeongezewa nguvu hivi majuzi katika jaribio la kuendeleza ushirikiano na uelewano wa kidini, hiyo ikiruhusu “dini ya Kikristo” iseme kwa sauti moja.
Harakati hiyo ya kuleta muungamano wa makanisa huwa ya namna nyingi. Hatua ya maana ilichukuliwa katika 1948 katika Amsterdam wakati Baraza la Makanisa Ulimwenguni lilipoanzishwa. Baraza hilo ambalo hapo kwanza lilikuwa na makanisa karibu 150 ya Kiprotestanti, Kianglikana, na Kiorthodoksi sasa huona fahari ya kuwa na maradufu ya hesabu hiyo.
Ingawa Kanisa Katoliki la Kiroma si mshiriki wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, laonekana ni kama linasonga likawe. Katika 1984 kwenye makao makuu ya baraza hilo huko Uswisi, Papa John Paulo alijiunga na mwandishi mkuu wa baraza hilo mwenye kuondoka cheoni katika kuongoza ibada ya sala ya mwungamano wa makanisa. Na katika Mei 1989, Wakatoliki walikuwa miongoni mwa wanakanisa zaidi ya 700 Wa Ulaya waliokutana katika Basel, Uswisi, kwenye lile ambalo gazeti moja lililiita “tukio lililo kubwa zaidi la kutafuta mwungamano tangu ule Mrekebisho [wa Kidini].”
Tangu miaka ya katikati ya 1930, nia hii ya kutafuta uridhiano imeonekana wazi zaidi kwa sababu ya kuzidi kukubali lile wazo la kwamba dini zote ‘za Kikristo’ zina mwungamano wa kindani ambao zimerithi kwa kupewa na Mungu. Kwa “uthibitisho” wa mwungamano wa kurithi, Baraza la Makanisa Ulimwenguni hukazia kwamba washiriki walo wote hukubali fundisho la Utatu, wakimchukua “Yesu Kristo kuwa Mungu na Mwokozi.”
Pia Jumuiya ya Wakristo imetafuta maongezi na dini zisizo za Kikristo. Kulingana na The Encyclopedia of Religion, kusudi ni kupata uridhiano wenye matokeo “kati ya maoni ya ubeberu wa kitheolojia, ambayo hudokeza kwamba ikiwa imani moja ndiyo ukweli hakuna imani nyingine zozote zenye haki ya kuwako, na maoni ya mchangamano, ambayo hudokeza kwamba tofauti zilizo kati ya imani hizo hazitoshi kuleta mgogoro na kwamba kadiri fulani ya kuzichanganya yaweza kufanyiza imani mpya kwa ajili ya wakati ujao.”
Kwa uhalisi, dini bandia ni kama kamba yenye nyuzi nyingi, zote zikiwa zinavutwa kuelekea pande tofauti. Huu ni utangulizi wa msiba, kwa maana maneno ya Yesu hayajapata kamwe kukanushwa: “Utawala wowote uliogawanyika makundimakundi yanayopingana, hauwezi kudumu, na mji wowote au jamaa yoyote iliyogawanyika makundimakundi yanayopingana, itaanguka.”—Mathayo 12:25, HNWW.
Ikubali Iliyo ya Kweli, Ikatae Iliyo Bandia!
Huenda watu fulani wakachagua kupuuza uthibitisho. Lakini kutazamia mema bila msingi mzuri ni hatari. “Makanisa yameishi kwa zaidi ya kizazi kimoja yakiwa na tumaini la kwamba mambo yatajitengeneza yenyewe tu,” likasema The Times la London katika Oktoba 1988. Liliongezea hivi: “Kujapokuwa na mzoroto wa muda mrefu katika hesabu ya washiriki wa kanisa katika Uingereza, katika makanisa kumekuwa hakuna jitihada nyingi ya kuueleza au kuubadili, au kutunga miongozo ya kulingana na hali.” Halafu likamalizia hivi kwa mawazo yafaayo: “Shirika lolote la kibiashara ambalo hupata mauzo yalo yakipungua kwa uendelevu lingejitayarisha kupatwa na msiba wa kabisa au lingechukua hatua za kufanya maendeleo ya utengenezaji na uuzaji bidhaa.”
Hakuna kionyeshi chochote kwamba dini bandia ‘itachukua hatua za kufanya maendeleo ya utengenezaji na uuzaji bidhaa.’ Msingi pekee wa watu wanaomhofu Mungu kuwa na matazamio mazuri ni kugeukia dini moja tu ya kweli, ambayo vijito vyavyo vinavyotiririsha maji ya kiroho havimo katika hatari ya kukauka. Kwa habari ya dini bandia, “Wakati wa Kufanya Hesabu U Karibu.” Jifunze mengi zaidi wakati makala hiyo itakapotokea katika toleo letu linalokuja.
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Mashahidi wa Yehova: Maji Yao Hayakauki
“Wakati dini za tangu zamani zinapozorota polepole, makanisa na mahekalu yao yakizidi kuwa matupu wakati wote, Mashahidi wa Yehova wanapata ongezeko la hesabu ya washiriki na hata wanajipatia majengo yaliyokuwa makanisa hapo zamani na vifaa vingine vipya ili wakusanye washiriki wao wapya humo.”—Le Petit Journal, gazeti la Kikanada.
“Katika Italia kuna karibu 45 elfu . . . Leo dhehebu hilo lina magazeti halisi, yaliyo mazuri na hata ya kupendeza (yana habari na makala nyingi nzuri kutoka sehemu zote za ulimwengu), huchapa vitabu vidogo-vidogo vya kisasa na pia huwajibu wanachuo Wakatoliki walio wastadi zaidi kuhusiana na Biblia, hugawanya Biblia zilizotafsiriwa moja kwa moja kutoka Kiebrania . . . Wakiwa na njia hizo, Mashahidi hata wamekuwa na mafanikio makubwa sana.”—Famiglia Mese, gazeti la Kikatoliki la Kiitalia (lililoandikwa katika 1975; kufikia Aprili 1989, hesabu ya Mashahidi wa Yehova katika Italia ilikuwa imeongezeka kuwa 169,646.)
“[Mashahidi wa Yehova] wanabatiza mamia hali sisi tunabatiza wawili-wawili na watatu-watatu.”—The Evangelist, kichapo rasmi cha “Evangelical Tract Distributors.” (Mashahidi wa Yehova walibatiza watu 69,649 katika 1962 wakati taarifa hiyo iliposemwa; katika 1988 hesabu ya Mashahidi wapya waliobatizwa ilikuwa 239,268.)
“Katika 1962 mimi nilimaliza uchunguzi wa Mashahidi wa Yehova kwa maoni haya: ‘Jambo la kwamba Sosaiti ya Ulimwengu Mpya itapunguza mwendo ghafula ni lenye mashaka.’ . . . Leo [1979] Mashahidi ni zaidi ya mara mbili kuliko walivyokuwa wakati huo. Ishara zote zaonyesha kwamba Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi labda itakuwa maradufu tena kwa ukubwa muda wa mwongo unaokuja.”—William J. Whalen katika U.S. Catholic. (Wale Mashahidi 989,192 wa 1962 waliongezeka wakawa 3,592,654 kufikia 1988.)
Tangu 1970 hesabu ya Mashahidi wa Yehova katika Jamhuri ya Mwungano ya Ujeremani (na Berlin ya Magharibi) imeongezeka kwa asilimia 38. Katika miaka 30 iliyopita, hesabu ya makundi ya Mashahidi wa Yehova katika Uholanzi imeongezeka kutoka 161 hadi 317, na katika Uingereza kutoka 825 hadi 1,257, ikaleta uhitaji wa kujenga Majumba ya Ufalme mengi mpya katika nchi zote mbili.—Linganisha fungu la 3 chini ya kichwa kidogo “Matazamio Maangavu Yafifia.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Dini hukaa ikipuuzwa katika pirika-pirika za ulimwengu wa leo