Wakati Ujao wa Dini kwa Kutegemea Wakati Wayo Uliopita
Sehemu ya 21: 1900 na kuendelea— Marinda Yaliyopakwa-pakwa Damu
“Hakuna msingi imara uwekwao juu ya damu.”— Shakespeare, mshairi na mwanatamthilia Mwingereza (1564-1616)
JE! WEWE waikumbuka tanzia iliyotokea Novemba katika Jonestown, Guyana, miaka 11 iliyopita? Washirika zaidi ya 900 wa kikundi cha kidini kijulikanacho kuwa “People’s Temple” (Hekalu la Watu) kilijiua kihalaiki, walio wengi wakifanya hivyo kwa kujipendea, kwa kunywa kinywaji cha matunda kilichoongezewa asidi sayanaidi.
Kwa kushtuka, watu waliuliza hivi: ‘Ni dini ya aina gani ambayo hudhabihu uhai wa washiriki wayo yenyewe?’ Hata hivyo, damu isiyo na hatia imemwagwa kwa jina la dini kwa karibu miaka 6,000. Na bado, katika karne ya 20 damu imemwagwa mara nyingi na kwa njia nyingi zaidi kuliko katika wakati wowote mwingine katika historia. Fikiria kisehemu tu cha uthibitisho wa jambo hilo.
Dhabihu za Kibinadamu kwa Mungu Bandia
Tangu 1914, vita vya ulimwengu viwili na mapigano madogo-madogo zaidi ya mia moja yamemwaga damu mfano wa bahari kuu. Karne moja iliyopita, Guy de Maupassant mwandikaji Mfaransa alisema kwamba “yai ambalo kutokana nalo vita huanguliwa” ni uzalendo, ambao aliuita “aina fulani ya dini.” Kwa uhakika, The Encyclopedia of Religion husema kwamba binamu ya uzalendo, utukuzo wa taifa, “umekuwa namna kuu ya dini katika ulimwengu wa ki-siku-hizi, ikiuacha wazi tena utupu ulioachwa na mzoroto wa thamani za kidini za tangu zamani.” (Italiki ni zetu.) Kwa kushindwa kuendeleza ibada ya kweli, dini bandia ilifanyiza uwazi wa kiroho ambamo utukuzo wa taifa uliweza kumiminika.
Hakuna mahali popote ambamo kielezi cha jambo hilo kilionyeshwa vizuri kuliko katika Ujeremani ya Nazi, ambayo raia zao mwanzoni mwa Vita ya Ulimwengu 2 walidai kuwa ni asilimia 94.4 ya Wakristo. Kati ya mahali pote, Ujeremani—mahali pa kuzaliwa kwa Uprotestanti paliposifiwa na Papa Pius 10 katika 1914 kuwa makao ya “Wakatoliki bora kabisa ulimwenguni”—pangalipaswa kuwa kiwakilishi bora kabisa cha Jumuiya ya Wakristo.
Jambo la maana kuangaliwa ni kwamba Adolf Hitler Mkatoliki aliungwa mkono kwa utayari zaidi miongoni mwa Waprotestanti kuliko miongoni mwa Wakatoliki. Wilaya za Kiprotestanti hasa zilimpa asilimia 20 ya kura zao katika uchaguzi wa 1930, huku wilaya za Wakatoliki zikimpa asilimia 14 tu. Tena wingi kamili wa kwanza kuunga mkono Chama cha Nazi katika uchaguzi wa taifa ulikuwa katika 1932 katika Oldenburg, wilaya iliyo ya Kiprotestanti kwa asilimia 75.
Kwa wazi, “uwazi utupu ulioachwa na mzoroto wa thamani za kidini za tangu zamani” ulikuwa mkubwa zaidi katika Uprotestanti kuliko katika Ukatoliki. Na yaeleweka ingekuwa hivyo. Theolojia yenye uhuru mwingi na uchambuzi wa juu zaidi wa Biblia ilikuwa hasa zao la wanatheolojia Waprotestanti wenye kusema Kijeremani.
Jambo jingine pia lililo la maana kuangaliwa ni lile lililotia uthabiti katika hali nyonge ya Wakatoliki kutomwunga Hitler mkono. Mwanahistoria Mjeremani Klaus Scholder aeleza kwamba “kwa mapokeo Ukatoliki wa Ujeremani ulikuwa na mahusiano ya karibu sana na Roma.” Kwa kuona kwamba Unazi ulikuwa ngome thabiti dhidi ya Ukomunisti, Vatikani haikukataa kutumia uvutano wayo ili kuimarisha mkono wa Hitler. “Maamuzi ya msingi yalihamishwa zaidi na zaidi yakawa ya Curia [baraza la kusaidia katika usimamizi wa kanisa],” asema Scholder, “na kwa kweli msimamo na wakati ujao wa Ukatoliki katika Milki ya Tatu ulikuja hatimaye kuwa ukiamuliwa katika Roma tu karibu wakati wote.”
Sehemu ambayo Jumuiya ya Wakristo ilishiriki katika vita vya ulimwengu vyote viwili iliongoza kwenye kupoteza heshima. Kama vile Concise Dictionary of the Christian World Mission ielezavyo: “Wasio Wakristo waliona mbele ya macho yao . . . uhakika wazi kwamba mataifa yaliyokuwa yamekuwa na fundisho la Kikristo kwa miaka elfu moja yalikuwa yameshindwa kudhibiti tamaa zao na kuuwasha moto ulimwengu mzima ili kuridhisha tamaa za makuu zisizo za kupendeza hata kidogo.”
Bila shaka, vita vyenye kuchochewa na dini si jambo jipya. Lakini tofauti na wakati uliopita ambapo mataifa ya dini tofauti-tofauti yalipigana vita, karne ya 20 imezidi kuwa na mataifa ya dini ile ile yakifungamana katika pigano kali. Kwa wazi mungu wa utukuzo wa taifa ameweza kuitumia miungu ya dini kama apendavyo. Hivyo, wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 2, Wakatoliki na Waprotestanti katika Uingereza na United States walipokuwa wakiua Wakatoliki na Waprotestanti katika Italia na Ujeremani, Wabuddha katika Japani walikuwa wakiwatenda hivyo hivyo ndugu zao Wabuddha katika Esia ya kusini-mashariki.
Hata hivyo, kwa sababu ya nguo zayo zenye madoa ya damu, Jumuiya ya Wakristo haiwezi kutikisia wengine kidole cha lawama kwa kujihesabia uadilifu. Kwa kutetea, kuunga mkono, na nyakati fulani kuchagua serikali za kibinadamu zisizokamilika, wenye kudai kuwa Wakristo na wasio Wakristo pia ni lazima washiriki daraka kwa damu ambayo serikali hizo zimemwaga.
Lakini ni dini ya aina gani ambayo ingeweka serikali juu ya Mungu na kutoa washirika wayo wenyewe wawe dhabihu za kisiasa juu ya madhabahu ya mungu wa vita?
“Waliendelea Kumwaga Damu Isiyo na Hatia”
Maneno hayo, yaliyosemwa karne nyingi zilizopita juu ya Israeli mwasi-imani, yatumika kwa dini zote bandia na kwa zile za Jumuiya ya Wakristo hasa. (Zaburi 106:38) Usisahau mamilioni ya maisha zilizofutiliwa mbali katika lile Teketezo la Umati, tanzia ambamo makanisa ya Jumuiya ya Wakristo hayakukosa kuwa na hatia.—Ona Amkeni! la Novemba 8, 1989.
Makasisi Wajeremani pia walibaki kimya juu ya suala jingine, lisilojulikana sana kama hilo, lakini lenye msiba wa kadiri ile ile. Katika 1927, miaka miwili baada ya Hitler kupangilia mawazo yake juu ya ubaguzi wa rangi katika Mein Kampf, mhariri na mwanatheolojia Mkatoliki Joseph Mayer alichapisha kitabu chenye idhini ya usomaji ya kiepiskopali ambayo ilisema hivi: “Wagonjwa wa akili, wakichaa wa kiadili, na watu wengine wa hali duni hawana haki ya kuyaeneza fikira kama vile wasivyo na haki ya kuwasha mioto.” Pasta Mlutheri Friedrich von Bodelschwingh aliona kwamba ilipatana na mapenzi ya Yesu kuondoa nguvu za uzazi katika wale wasiojiweza.
Mtazamo huo wenye kuungwa mkono kidini ulisaidia kutayarisha njia ya kuingia kwa ile “amri ya euthanasia” ya Hitler ya 1939, iliyoongoza kwenye kifo cha raia zaidi ya 100,000 wenye kasoro za akili na kushurutisha kuondoa nguvu za uzazi za watu waliokadiriwa kuwa 400,000.a
Katika 1985, miaka 40 baada ya mwisho wa vita, ndipo maofisa wa Kanisa la Kilutheri katika Rhineland walipokuja kukiri hivi peupe: “Kanisa letu halikupinga kwa uthabiti wa kutosha uondoaji wa nguvu za uzazi kwa lazima, uuaji wa watu wagonjwa na wasiojiweza, na kufanywa kwa majaribio ya tiba yenye ukatili juu ya wanadamu. Sisi twaomba msamaha wa mihanga ambao wangali hai na wa watu wa ukoo wao waliobaki hai.”
Ni kweli kwamba kampeni ya euthanasia ya serikali ilipungua sana baada ya askofu Mkatoliki wa Münster kutoa ushambulizi wa maneno makali siku ya Agosti 3, 1941, akiita sera hiyo uuaji. Lakini kwa nini ikachukua miezi 19 na vifo 60,000 kabla ya laana kali la peupe kusikika?
Hatia ya Damu kwa Dini
Dini zilizo nyingi hudai kustahi uhai na kupendezwa kulinda watu na madhara. Lakini je! makasisi huonya makundi yao kwa upatani juu ya hatari za kimwili zinazohusika katika kuvuta sigareti; katika utumizi mbaya wa dawa za kulevya, kutia na kileo; katika kutwaa damu ndani ya mwili; na katika ngono za ovyo-ovyo? La maana zaidi, je! wao hulaani vikali hizo kazi za mnofu kama vile Biblia ifanyavyo, wakieleza kwamba zaweza kutunyang’anya kibali cha Mungu?—Matendo 15:28, 29; Wagalatia 5:19-21.
Bila shaka, baadhi yao hufanya hivyo. Na Kanisa Katoliki na pia makanisa mengi ya Kifandamentali (yenye kuyapa maandiko umaana halisi wa mambo yote) huonyesha staha kwa uhai kwa kadiri ya kushutumu vikali utoaji mimba kuwa ni kumwaga damu isiyo na hatia. Hata hivyo, sheria ya utoaji mimba ya Italia ya Kikatoliki ni moja ya zilizo na ulegevu kabisa.
Pia Ubuddha hulaani vikali vitendo vya kutoa mimba. Lakini kwa mwaka mmoja tu katika Japani, visa 618,000 vya utoaji mimba vyaripotiwa kuwa vilifanyishwa, hata ingawa asilimia 70 ya wakaaji hushikilia Ubuddha. Hiyo yatokeza swali: Ni kwa msingi gani twapaswa kuhukumu dini, kulingana na yale ambayo mashirika yazo rasmi na baadhi ya makasisi wayo husema au kulingana na yale ambayo hesabu kubwa ya washiriki wayo walio katika msimamo mwema hufanya?
Kielelezo kingine cha kushindwa kumwonya mwovu chahusu orodha ya matukio ya Biblia na utimizo wa unabii wa Biblia. Hayo yote mawili huonyesha kwamba katika 1914 Ufalme wa kimbingu wa Mungu ulisimamishwa ukiwa mikononi mwa Yesu Kristo.b Ingawa Jumuiya ya Wakristo huadhimisha ile ambayo hudhaniwa kuwa ndiyo siku ya kuzaliwa kwa Kristo kila Desemba, makasisi hawapigi mbiu kwamba yeye ni Mfalme mwenye kutawala kama vile tu viongozi wa Dini ya Kiyahudi hawakumkubali kuwa Mfalme-Mkusudiwa karne 19 zilizopita.
Hata kama ni wa imani gani, makasisi ambao hushindwa kuonya juu ya matokeo ya kutotii sheria za Mungu juu ya maadili na juu ya kukataa kujitiisha kwenye Ufalme wa Mungu unaotawala, kulingana na Ezekieli 33:8 wanarundika hatia ya damu juu yao wenyewe. Kimya chao ni sawasawa na kusimama kilegevu tu huku mamilioni ya kundi lao wakiwa na hatia ya damu.
Hivyo, kwa kurushia-rushia marinda yayo damu ya wasio na hatia, dini bandia inaiondolea thamani damu ya Kristo Yesu iliyomwagwa yenye kupa uhai. (Ona Mathayo 20:28 na Waefeso 1:7.) Kwa sababu hiyo, hivi karibuni—tena karibuni sana—ile damu iliyopakwa-pakwa juu ya marinda ya dini bandia itakuwa yayo yenyewe!—Ufunuo 18:8.
“Dini Bandia—Ifikiliwapo na Wakati Wayo Uliopita!” haitaponyoka. Acheni toleo letu linalokuja lieleze.
[Maelezo ya Chini]
a Hii hukumbusha juu ya “wachawi wa kike” wakadiriwao kuwa 300,000 hadi 3,000,000 ambao, mwanzoni mwa karne ya 15, waliuawa kwa baraka ya papa.
b Ona Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani, sura 16-18, kilichochapishwa katika 1982 na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
“Katika sehemu nyingi za ulimwengu leo, dini imekuwa kijakazi wa mapinduzi . . . Hiyo huendelea kutia moyo mauaji katika Ailandi Kaskazini sawasawa na katika Bara Hindi na katika Ufilipino.”—The Encyclopedia of Religion.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Hatia ya damu ya wakati uliopita ya dini bandia, kama ilivyoonyeshwa katika mchoro huu uliochorwa katika mti wa kuteketeza halaiki ya wazushi, huwa si jambo kubwa ikilinganishwa na kumbukumbu la matendo yayo katika karne ya 20
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kengele za makanisa ya Ujeremani ziliyeyushwa ziwe za makusudi ya vita katika Vita ya Ulimwengu 1
[Hisani]
Bundesarchiv Koblenz