Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 9/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • MWONGO WENYE JEURI
  • MCHOCHOTA-INI “B” (“HEPATITIS B”) HAUGUNDULIWI KATIKA DAMU
  • WANADINI WALIO WASANII WA KUHADAA
  • KUFANYIA UTOFAUTI
  • MAPENZI YA KUTILIANA SHAKA
  • MAONI YENYE KUUA
  • HASARA YA PUPA
  • JE! KUNA DAWA YA KUPONYA?
  • MISIBA YA BUSTANINI
  • WANAWAKE NA UHALIFU KATIKA JAPANI
  • TAKATAKA ZA MAGARI-MOSHI
  • MAZIKO YASIYO YA KIDINI
  • Utiaji-damu Mishipani—Ni Salama Kadiri Gani?
    Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?
  • Mashahidi wa Yehova Wana Maoni Gani Kuhusu Mazishi?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 9/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

MWONGO WENYE JEURI

Kadiri ya uuaji katika United States inaongezeka tena. The New York Times yasema kwamba ingawa kadiri yenyewe ilipungua kidogo katika miaka ya mapema ya 1980, baada ya 1985 ilianza kuongezeka tena. Hesabu ya waliouawa katika 1989 ilikuwa karibu asilimia 5 juu kuliko wale 20,680 waliouawa katika 1988, hiyo tayari ikiwa ni wastani wa mtu 1 mwenye kuuawa kila dakika 25. Bunduki zilihusika katika asilimia 60 hivi ya visa vya mauaji na hivyo zikawa ndicho kisababishi cha nane chenye kuongoza katika vifo taifani. Katika shule pekee, kulingana na uchunguzi mmoja, siku ya wastani huona angalau wanafunzi mia moja elfu wakiwa na bunduki. Hivyo shule za Jiji la New York hulazimika kudumisha “jeshi la usalama ambalo ni la kumi na moja kwa ukubwa katika United States,” lasema gazeti Time. Kwa Jiji la New York, miaka ya 80 ndiyo iliyokuwa mwongo wenye jeuri kabisa katika historia ya jiji hilo, kukiwa na mauaji 17,000 hivi. Kuja kwa ile dawa ya kulevya iitwayo “crack” kulichangia ongezeko hilo.

MCHOCHOTA-INI “B” (“HEPATITIS B”) HAUGUNDULIWI KATIKA DAMU

Miaka mitano iliyopita mwanamume mmoja wa Afrika Kusini alipata ugonjwa wa mchochota-ini “B” kutokana na damu aliyotiwa mishipani wakati wa kupasuliwa moyo. Leo kutembea kwake ni shida sana, ana maumivu, na amelazimika kustaafu. Miezi mitatu kabla ya upasuaji huo, mchangaji wa damu hiyo alikuwa amechunguzwa na kupatikana kuwa bila viini vichafu. Zaidi ya hilo, mwanamke huyo alikuwa na historia ndefu ya kuchanga damu—yuniti 67 kwa ujumla. Wachangaji ambao wametoa-toa damu bila kusababisha maambukizo huchukuliwa kotekote kuwa ndio wachangaji salama kabisa. Basi jambo hilo lilikuwa limetokeaje? Muda wa kuja kudhihirika kwa mchochota-ini “B” hutofautiana kuanzia majuma 4 hadi 26. Hivyo, vairasi ya mchangaji, laeleza gazeti la Afrika Kusini Rapport, “ilikuwa ingali katika hatua ya kuja kudhihirika na haikuweza kugunduliwa wakati wa michunguzo ya kwanza.”

WANADINI WALIO WASANII WA KUHADAA

“‘Manabii bandia wa ulimwengu wenye kujiwekea akiba’ wamehadaa Waamerika wanadini karibu dola 500,000,000 katika miaka mitano iliyopita,” yataarifu The Dallas Morning News. Hao “wasanii wenye kunukuu Biblia” wamehadaa Waamerika zaidi ya 15,000 katika njama zao za kidini, kulingana na ripoti moja iliyotayarishwa na Baraza la Biashara na Ofisi Bora taifani na Shirika la Wasimamizi wa Dhamana Amerika Kaskazini. Kwa kuchochewa na kiasi cha pesa kilichokusanywa na waeneza-evanjeli wa televisheni, hao wasanii wenye kuhadaa wamejifaidi kutokana na ongezeko la programu za kidini ili kuwanyemelea wahadaliwa wao. “Njama hizo ni kuanzia michango ambayo wenye kujidai wamezaliwa tena wanaahidi kwa ubandia kuwa ni ya kuwekwa akibani hadi kwa wenye kutoa ushauri ‘wenye uvuvio wa kimungu’ kuhusu sarafu, metali zenye thamani, programu zenye kuhusiana na umiliki wa viwanja na majengo yaliyomo na uchimbuzi wa mafuta,” likasema gazeti hilo.

KUFANYIA UTOFAUTI

Vatikani ina sera thabiti ya kuruhusu mapadri mmoja mmoja wanywe divai isiyo na kileo wakati wa kuadhimisha Misa ikiwa wao wanafanya ombi hilo. Lakini hivi majuzi mapadri wa jimbo lote la Friuli la Italia wamepewa ruhusa kunywa kwenye Misa umajimaji wa zabibu isiyochachishwa badala ya divai. Kwa nini? Kulingana na Catholic Herald, mapadri hao walifanya ombi hilo kwa sababu walihofu kwamba wale ambao miongoni mwao ni wazoelevu wa kunywa vileo wangeweza ‘kurudia unywaji wa kupindukia’ kwa kunywa ile divai kidogo tu kwenye Misa. Pia gazeti hilo la Kikatoliki lilisema hivi: “Michunguzo iliyofanywa katika jimbo la Friuli huonyesha kwamba asilimia 15 ya idadi ya watu ina tatizo la kunywa na kwamba wengi wa wale mapadri 400 wa eneo hilo wamo katika kile kikundi cha walio katika hatari kubwa.”

MAPENZI YA KUTILIANA SHAKA

“Mapenzi” katika kipindi hiki cha UKIMWI na ukosefu wa adili wenye kuenea sana yamekuwa yakiongezeka kuwa yenye hatari. Katika jitihada ya kupunguza hatari hizo, wanawake zaidi waseja wanakodi wapelelezi wa faragha kuwachunguza wanaume wanaofanya matembezi ya kirafiki nao, laripoti The New York Times. Ingawa mashirika ya upelelezi yanasema ongezeko la sasa katika biashara yao limesababishwa na mweneo wa UKIMWI, yanasema kwamba wanawake pia huwauliza kwa ukawaida wachunguze cheo cha wachumba wao, mshahara, na elimu, na pia mazoea ya kingono. Shirika moja la upelelezi hata huwa na tangazo katika gazeti moja la Chicago. Huuliza hivi: “Je! wewe wamjua unayefanya matembezi ya kirafiki naye?” na kuongeza hivi: “Sasa zaidi ya wakati mwingine wowote, ni jambo la maana kujua.”

MAONI YENYE KUUA

Ufaransa ndiyo yenye matukio mabaya zaidi ya vifo vya barabarani miongoni mwa mataifa yenye usitawi wa viwanda—vifo 330 kwa kila magari milioni moja barabarani, kwa kulinganishwa na 185 katika United States, 182 katika Italia, 163 katika Japani, 162 katika Ujeremani Magharibi, na 127 katika Uingereza. International Herald Tribune ya Paris laripoti kwamba wanasaikolojia kwenye kikao kimoja cha hivi majuzi kuhusiana na mwenendo wa kuendesha magari waliweka kadiri kubwa ya lawama juu ya kukosa subira, kuvurugika fikira, na ujeuri. Walisema kwamba wengi hutumia magari yao kama njia ya kuonyesha majivuno yao wenyewe na madharau waliyo nayo kwa wengine.

HASARA YA PUPA

Ingawa wanasayansi fulani hukana kwamba uchafu wa kibinadamu unasababisha halianga yetu iongezeke joto kwa tokeo la kupita kiasi, mwanagronomia Mfaransa Rene Dumont ashikilia kwamba tayari tokeo hilo linaua watu—milioni moja katika mwaka mmoja tu uliopita. Yeye asema kwamba tokeo hilo husababisha hali za ukavu, ambazo nazo husababisha njaa. Dumont, ambaye ajulikana kwa muda mrefu juu ya kutabiri njaa kwa mafanikio, aonya kwamba “sisi tuko kwenye ukingo wa njaa iliyo kubwa kabisa katika historia ya wanadamu.” Yeye huweka lawama la hali mbaya hiyo juu ya kutumia nishati kwa pupa katika mataifa yaliyositawi: “Kuna watu bilioni mbili wanaoishi katika umaskini ulimwenguni nao ni watekwa-nyara wa pupa yetu, wa utapanyaji wetu wa nishati.”—The Globe and Mail, Toronto, Kanada.

JE! KUNA DAWA YA KUPONYA?

Kuuawa kwa wavulana wachanga watatu, wawili kati yao wakiwa wametumiwa vibaya kingono, katika United States ya Magharibi kumetia kuni katika ubishi wenye kuongezeka juu ya kama wenye mazoea ya kutumia watoto vibaya waweza kuponywa au sivyo. Mwanamume aliyeshtakiwa katika mauaji hayo alikuwa amehukumiwa-hukumiwa kupewa mashauri ya habari za ngono kwa sababu ya kutenda visa vya uhalifu dhidi ya watoto. Kabla ya kukamatwa kwa mauaji matatu hayo, alikuwa amemaliza miezi minane ya kushauriwa na mwanasaikolojia ambaye yeye mwenyewe alikuwa amekaa miaka 13 gerezani akiwa mlanguzi wa dawa za kulevya na mnyang’anyi mwenye kutumia silaha. “Mtu yeyote aweza kubandika kibao cha kutangaza [ofisi ya] udaktari kisha ajiite mwenyewe kuwa ni tabibu,” alalamika mkuu wa Shirika la Kutibu Mwenendo wa Watumia Ngono Vibaya katika The New York Times. Gazeti hilo Times lasema kwamba watabibu wengi zaidi na zaidi wanakata shauri kwamba “watu fulani wenye tabia ya kutumia watoto vibaya huwa kwa msingi hawaponyeki na wapaswa kufungiwa muda wa maisha yote.”

MISIBA YA BUSTANINI

Shirika la kuzuia misiba, “Royal Society for the Prevention of Accidents,” lilitoa tarakimu za karibuni zaidi juu ya majeraha yenye kutukia bustanini katika Uingereza. Wakati wa kipindi cha mwaka mmoja, “watu 21 waliuawa katika bustani yao—14 waliuawa na vyombo vya kazi hali ‘mimea na miti’ ilisababisha vifo vile vingine saba,” laripoti The Medical Post. Takwimu za Uingereza zaonyesha kwamba wanabustani 151,000 walitibiwa katika hospitali mbalimbali. Majeraha yalikuwa ni pamoja na 6,400 kutokana na mashine za kukata nyasi, 4,200 kutokana na vikata-ua, 4,000 kutokana na nyuma za kuchimba bustani, 3,000 kwa kolego za bustanini, 2,000 kutokana na miundu ya kupogoa, 1,000 kutokana na miundu ya nyasi kubwa, na 1,600 kutokana na mianzi ya kuchomekwa chini. Fanicha (vifaa) za uwanjani zilisababisha aksidenti 3,200, wilibaro ilitia majeraha 1,200, na “kijungu cha maua kikajeruhi wanabustani 59.”

WANAWAKE NA UHALIFU KATIKA JAPANI

Hesabu ya uhalifu inaongezeka katika Japani, na wanawake wanasababisha asilimia fulani yenye kuongezeka. Katika 1988 baadhi ya visa kama 1,641,310 vya uhalifu vilifanywa katika Japani, hilo likiwa ni ongezeko juu ya mwaka uliotangulia la visa kama 63,000. Wajapani ambao kwa ujumla huwa ni wafuata sheria walisononeka kuona uhalifu katika 1989 ukifikia kiwango cha juu kuliko wakati wote tangu baada ya vita. Lakini labda jambo la kushangaza zaidi ni kwamba sasa wanawake hufanya asilimia 25 hivi ya visa vya uhalifu wa Japani, laripoti Sankei Shimbun la Tokyo.

TAKATAKA ZA MAGARI-MOSHI

Amtrak, huduma ya magari-moshi ya Kiamerika, imechambuliwa vikali hivi majuzi kwa zoea layo la kutupa takataka ya kinyesi kibichi cha kibinadamu juu ya njia za magari-moshi. Sikuzote vyoo vimepigwa maji katika magari-moshi moja kwa moja kwenye reli zilizo chini, na Amtrak yaita zoea hilo kuwa “lisilo na madhara ya kimazingira.” Lakini wenye mamlaka katika Florida walianza kuchunguza reli hiyo baada ya wavuvi wa samaki kulalamika juu ya kunyunyiziwa kinyesi wakati magari-moshi yalipopita katika madaraja yaliyo juu yao. Mahakama moja ya Florida imeipata Amtrak kuwa yenye hatia ya uchafuzi wa kibiashara. Amtrak yapanga kuomba rufani ya kesi hiyo na yadai kwamba ingegharimu dola milioni 147 kufuata njia za hali ya juu zaidi za kutibu kinyesi. Kwa sasa, makondakta wa magari-moshi watawaomba abiria wajiepushe na kupiga maji chooni wakati magari-moshi yapitapo juu ya madaraja fulani.

MAZIKO YASIYO YA KIDINI

Kukiwa na ongezeko la mzinduko wa kuona jinsi dini ilivyo hasa, Waingereza zaidi wanapendezwa na maziko ya kilimwengu yasiyohusisha jambo lolote la kidini. Shirika British Humanist limechapisha kitabu maarufu chenye kichwa Funerals Without God: A Practical Guide to Nonreligious Funerals nalo hutuma wenye kujitolea wakaendeshe maziko ya kilimwengu. Mratibu wa sosaiti hiyo adai kwamba familia zimechoshwa na makasisi ambao husema maneno yale yale kwenye maziko yote; kwa hiyo sosaiti hiyo hujaribu kufanya maziko hayo yaguse watu kibinafsi zaidi. Kwenye maziko mamoja ya mwanamume aliyependa kucheza dansi, waombolezi walicheza muziki wa tango. Kwenye maziko mamoja ya mwigiza sarakasi, wana wa mfu huyo walifanya kawaida ya viini-macho vyenye kuvutia mbele ya jeneza lile.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki