Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 2/8 kur. 14-17
  • Korongo—Ndege “Mwaminifu-Mshikamanifu”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Korongo—Ndege “Mwaminifu-Mshikamanifu”
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Miingio na Miondoko
  • Kile Kiota Kisicho cha Kawaida
  • Shida ya Sasa ya Korongo
  • Mambo Tunayojifunza Kutokana na Ndege wa Mbinguni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2016
  • Kuchungua Mafumbo ya Uhamaji
    Amkeni!—1995
  • “Waangalieni kwa Makini Ndege”
    Amkeni!—2014
  • Maajabu ya Hekima ya Kisilika
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 2/8 kur. 14-17

Korongo—Ndege “Mwaminifu-Mshikamanifu”

Na mleta habari za “Amkeni!” katika Hispania

KORONGO—dalili yenye kutumiwa kimapokeo kwa kutabiri masika, watoto wachanga, na nasibu njema—amekuwa na umaana wa pekee katika hadithi na shauku za binadamu. Mruko wake wenye madaha, kupenda kwake makao ya kibinadamu, na sehemu yake yenye manufaa katika kudhibiti wadudu wenye kuharibu ukulima, yote hayo yamechangia sifa yake ya kupendwa sana.

Lakini labda jambo lake linalomfanya kipenzi sana ni uaminifu wake—uaminifu kwa kiota chake, ambacho yeye anakirudia kila mwaka, na uaminifu-mshikamanifu kwa mwenzi wake, ambaye anashikamana naye katika kifungo cha maisha yote. Kwa uhakika, jina lake katika Kiebrania linamaanisha “mwaminifu-mshikamanifu” au “mmoja aliye wa fadhili-upendo” kwa sababu, kama vile Talmud inavyoeleza, yeye ni kiumbe tofauti sana kwa kutendea mwenzi wake kwa shauku.

Shukrani kwa sifa hii ya kupendwa sana, karibu miaka mia mbili iliyopita korongo alikuwa jamii yenye kulindwa katika Holland na, inaripotiwa kwamba, korongo waliofugwa wangeweza kuonekana wakizunguka kimaringo kwenye soko la samaki la Uholanzi. Baadaye alifanywa kuwa ndege wa kitaifa wa Ujeremani. Na siku hizi, katika miji mingi ya Ulaya, majukwaa yanasimamishwa juu ya paa za nyumba ili kumtia moyo ndege huyu mwenye urafiki aweke kiota juu yazo. Korongo ni majirani wenye kukaribishwa!

Miingio na Miondoko

Korongo fulani wa Ulaya wanaenda kukaa Afrika Magharibi kusini mwa Sahara wakati wa kipupwe, hali wengine wanasafiri mbali kufika Afrika Kusini. Wanaanza safari yao ndefu katika Agosti. Kwa kuwa wao si warukaji imara, safari hiyo inafanywa hatua kwa hatua. Wanapendelea zaidi kuhama wakiwa vikundi vyenye ukubwa unaotofautiana, na mara nyingi korongo wote katika eneo fulani watajiunga pamoja kabla ya kuondoka katika mhamo wao. Wakiwa miongoni mwa ndege wahamaji walio wa mapema zaidi kurudi kaskazini, wanawasili kurudia viota vyao katika Februari au Machi.

Kwa sababu ya kadiri ya ukubwa wao—mweneo wa mabawa yao ni karibu meta 1.8—na utegemeko wao, korongo wenye kuhama wamevuta uangalifu sikuzote. Makundi makubwa ya korongo yanapita kwa kuwahi katika Palestina katika vuli na masika. Zaidi ya miaka 2,500 iliyopita, nabii Yeremia alivuta uangalifu kwenye uhakika huu, akimsimulia korongo kwa usahihi kuwa ndege “anayejua wakati wa kuhama.”—Yeremia 8:7, The New English Bible.

Umbali ambao wao wanasafiri kila mwaka—safari ya kwenda na kurudi ya kilometa zaidi ya 16,000 katika visa fulani—ni ya kustaajabisha, zaidi sana inapofikiriwa kwamba wao husafiri bila kupigisha mabawa sehemu kubwa ya mwendo huo. Kama wale ndege wakubwa wenye kula wengine, wao wanategemea mikondo yenye joto, mafungu ya hewa yenye joto, ili kupata mwinuko, na baada ya hapo wanafaidika kutokana na mabawa yao mapana kwa mwendo laini usio na jitihada kwa umbali mrefu, wakipiga-piga mabawa mara chache tu.

Sehemu isiyo na kifani ya mhamo wa korongo ni kuvuka kwao Bahari ya Mediterania. Wao wanapendelea zaidi kutosafiri juu ya maji, mahali ambako hakuna mikondo yenye joto. Hivyo, kila Agosti maelfu ya korongo wanakusanyika ili kufanya mvuko kwenye sehemu mbili ambapo umbali wa kuruka juu ya maji ni mfupi zaidi (Mlangobahari wa Gibraltar na Bosporus). Kwa kushangaza, ile safari ndefu ya kuvuka Jangwa la Sahara haiwavunji moyo kama ule mtandao wa kilometa kumi na nne wa maji yanayotenganisha Hispania na Afrika, unaoweza kuwachukua muda wa kufikia saa tano.

Kile Kiota Kisicho cha Kawaida

Korongo wanapendelea zaidi kufanya kiota katika mahali penye kutokeza sana, kama kilele cha mti mrefu, ingawa nyakati fulani wanatosheka na kifanano cha ki-siku-hizi, kama kiguzo cha nguvu za umeme. Nyakati za Biblia, mara nyingi walijenga “nyumba” yao katika mreteni.—Zaburi 104:17.

Lakini kwa karne nyingi, vilele vya paa, makanisa, na mabomba ya kutoa moshi nyumbani katika sehemu zote za Ulaya yamekuwa mahali panapopendwa sana kwa viota. Ndege wa kiume na wa kike pia wanajenga kiota chao kwa subira, nacho ni mjengo usio wa kawaida unaoweza kuonekana kama kwamba utaporomoka chini wakati wowote utoke kwenye kituo chao. Lakini sura zinaweza kudanganya, na ni mara chache ambapo vile viota vikubwa vinaangushwa kutoka vilipo hata kukiwa na dhoruba zilizo kali sana. Viota ni vya kudumu sana hivi kwamba kwa kawaida korongo wanaporudi kila mwaka wanatumia juma moja hivi wakifanya marekebisho kidogo kwenye makao yao.

Kazi hii ya marekebisho, inayohusisha kuongeza vitawi na vifaa vingine, kwa kawaida inafanywa na korongo wote wawili mara tu wakiisha kufika kutoka makao yao ya wakati wa kipupwe. Na mwishowe, kazi hii ya marekebisho ndiyo inayoangamiza kiota—kinaanguka kabisa kwa uzito wacho chenyewe. Kufikia wakati huo huenda kiota kikawa na kimo cha kufikia meta saba na kipenyo cha karibu meta mbili au zaidi.

Wakati ule ule wazazi wanaporudi kwenda kwenye kiota chao kila masika, watoto wao wanajaribu kupata mahali ambapo kwa kadiri inavyowezekana ni karibu na mahali pao pa kuangulia mayai. Hivyo, majengo fulani ya zamani yanakuwa makao ya viota vikubwa sana dazani moja au zaidi, vyote vikikaliwa na wazao wa mume na mke wamoja wa pale mwanzoni.

Shida ya Sasa ya Korongo

Kujapokuwa na majaribio ya kufanya korongo ajisikie anakaribishwa katika miji mingi ya Ulaya, wakati ujao wake unaonekana kutokuwa na matumaini. Karne iliyopita kulikuwako viota kama 500 katika Uswisi, lakini sasa ni vichache tu ambavyo vimebaki. Matazamio kama hayo yasiyo maangavu yanatokea Uswedi, Uholanzi, Udeni, na Ujeremani, ambako idadi zao zinapungua ajabu. Katika Hispania, ambako wao wangali wakionekana kwa kawaida, viota vyenye kukaliwa vimepunguzwa kwa nusu katika muda wa miaka kumi tu. Idadi nzima ya Ulaya sasa inakadiriwa kuwa wawili-wawili wa kuanzia 10,000 kufika 20,000 tu. Ni jambo gani linalopata mmoja wa ndege wanaopendwa zaidi na binadamu?

Inaonekana mambo mengi yanahusika, lakini mengi yayo yanahusiana na uharibifu wa binadamu wa mazingira. Katika maeneo wanakokaa katika Afrika wakati wa kipupwe, mara nyingi korongo wanawindwa na kuuawa kwa chakula: msiba wa kimazingira, kwa kuwa korongo wanatumia miezi ya kipupwe wakimeza-meza makundi ya nzige wanaoharibu sana mazao ya Kiafrika yaliyo muhimu kwa uhai. Kwa sasa, mayai yasiyoweza kutokeza ndege katika Ulaya, yanayosababishwa na utumizi ulioenea sana wa dawa za kuua wadudu, na kupotezwa kwa maeneo yenye malisho yamekuwa na tokeo la kulea watoto wachache zaidi kila mwaka. Zaidi ya hilo, kamba za nguvu za umeme ni hatari yenye kuua ndege wengi wakubwa, na wawindaji wenye kufurahia kuwafyatua wanasababisha kifo cha wengine wengi.

Wahifadhi mazingira wanafanya jitihada za kumlinda korongo, lakini programu yenye mafanikio itategemea ushirikiano wa mataifa mengi, jambo ambalo si rahisi kutimiza. Wapenzi wa uumbaji wa Mungu wanatumaini kwamba wakati hautafika kamwe ambapo yale mabawa yenye fahari ya korongo yatatoweka kutoka anga zetu, wakati ambapo masika hayatatangazwa tena na ndege mwenye kuonyesha hali ya ujirani mzuri na uaminifu-mshikamanifu.

[Sanduku katika ukurasa wa 16]

Korongo na Vitoto

Kwa karne nyingi, watoto wameambiwa kwamba korongo ndio wanaoleta watoto wachanga, na korongo wangali wanaonekana sana katika kadi zinazopongeza wazazi wakati mtoto anapozaliwa. Hadithi hiyo ilianza wapi?

Inaonekana kwamba, wazo hilo linategemea hekaya mbili. Miaka iliyopita, watu waliona kwamba korongo walitokea kwa njia iliyoonekana kama ya kimwujiza kila mwaka wakati ule ule. Wengine wao walifikiri kwamba walienda Misri katika miezi ya kipupwe na kuwa wanaume, halafu kugeuka kuwa ndege wakati wa masika (jambo hilo likaeleza ni kwa nini walipenda sana makao ya kibinadamu).

Pia ilionwa kwamba korongo walitumia sehemu kubwa ya mchana wakijilisha katika maeneo yenye mabwawa ya maji, yaliyosemwa kuwa ndiyo makao ya nafsi za watoto wachanga waliozaliwa karibuni. Kwa kuwa korongo walikuwa ndege walio wazazi wenye ufikirio sana, hakukutakiwa uwazio mwingi mno ili watu waunganishe uhakika na ubuni na kutokeza wazo la kwamba watoto wachanga waliletwa na korongo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Godo-Foto

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

Godo-Foto

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki