Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 2/8 kur. 18-20
  • Meroë— Ushuhuda kwa Fahari Iliyosahauliwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Meroë— Ushuhuda kwa Fahari Iliyosahauliwa
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Watu na Historia Yao
  • Pambazuko la Milki
  • Ethiopia Yenye Kupendeza
    Amkeni!—1996
  • Filipo Ambatiza Ofisa Mwethiopia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Misri ya Kale ya Kwanza ya Zile Serikali Kubwa za Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Piramidi za Mexico
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 2/8 kur. 18-20

Meroë— Ushuhuda kwa Fahari Iliyosahauliwa

Na Mleta Habari za Amkeni! katika Kenya

ULIMWENGU umekuwa karibu kusahau lile jiji la kale la Meroë. Likiwa katika ukingo wa mashariki wa Mto Naili zapata kilometa 208 kaskazini-mashariki mwa Khartoum, Sudan, wakati mmoja Meroë lilikuwa ndilo jiji kuu lenye fahari la Milki ya Ethiopia. Lakini sasa linachakaa tu likiwa mahali pa utalii. Mahekalu yanayomumunyika, majumba ya kifalme matupu, na usanii uliovunjika vipande wa jiji hilo ni wonyesho hafifu wa zama zenye utukufu. Acheni tuangalie mengine ya magofu ya kale.

Hapa ndipo ulipo uwanja wa hekalu la Amoni. Wakati mmoja ulikuwa na urefu wa karibu meta 137. Hata leo mabaki yalo yanatokeza nje kidogo juu ya mchanga wa jangwa. Sanamu za jiwe graniti za kondoo waume, ambazo nyingine zazo zinaweza bado kuonekana, wakati mmoja zilipangwa kwa mfuatano katika njia pana ya msafara kufika kwenye mwingilio wa hekalu.

Katika eneo la pale pale hekaluni, bado unaweza kuona nyingine za sanamu, michongo, na michoro-rangi iliyoyapamba vizuri majumba ya kifalme. Au huenda ukataka kuona upendezi wa nguzo zile zilizotiwa nakshi kwa uzuri zikiwa zimezunguka kidimbwi cha kuogelea cha hapo karibu. Mfumo wa mabomba ya maji ambao hapo kwanza uliingiza maji ndani ya kidimbwi hicho kupitia vinywa wazi vya sanamu ndogo zenye vichwa vya simba ni wa akili nyingi hata kwa viwango vya karne ya 20. Maumbuko ambayo yametokea kutokana na kupita kwa wakati, jua, na mchanga wa jangwa hayakufifisha kabisa zile rangi za kuvutia ajabu zinazopamba nguzo zinazozunguka kidimbwi hicho.

Kwenye ukingo wa mashariki wa Meroë lipo Hekalu la Jua, ambalo wakati mmoja lilikuwa maarufu sana katika ibada ya wakaaji wa jiji hili. Ingawa halina ukubwa wa kuvutia kama hekalu la Amoni, hata hivyo limepambwa kwa uzuri mwingi ukutani na sakafuni kwa vigae vya buluu na manjano, na pia tamasha za michongeleo inayoonyesha visa vya ushindi wa kijeshi.

Ushuhuda mkubwa kwa fahari ya Meroë ni ile ardhi ya kuzikia. Upande huu hadi upande mwingine wa uwanda mkubwa ulio jangwa, lakini kwa kukaribiana kadiri fulani na mjini, kuna hesabu fulani ya piramidi tofauti-tofauti. Ingawa hayana ukubwa na utukufu wa piramidi zile kubwa za Misri, hata hivyo maziara haya ya kuzikia yana uvutio mwingi. Hapa pana ushuhuda wa kutosha wa mtindo-maisha wa kifalme uliosahauliwa. Katika enzi zalo zenye kuvuma, Meroë lilikuwa jiji maarufu sana—mfano wa kale wa Paris, Washington, au Moscow.

Lakini nani aliishi na kufanya kazi huko? Na ni nini kilichoongoza kwenye kukoma kwa jiji hili?

Watu na Historia Yao

Waanzishi wa Meroë walikuwa Wakushi, au Waethiopia. Michoro ya ukutani inaonyesha wazi maumbo ya sura zao za Kiafrika. Utamaduni wa Kimisri uliishika Meroë, lakini kuelekea mwisho wa mileani ya pili K.W.K., Ethiopia ilijiweka huru kutoka udhibiti wa Misri.

Katika sehemu ya mwisho ya karne ya nane K.W.K., kwa kweli Ethiopia ilishinda Misri na kuitawala kwa karibu miaka 60. Hivyo basi ingawa wengi wanawazia kwamba Misri ndiyo iliyokuwa milki ya pekee kutokea katika Afrika, hii si kweli. Mmoja wa watawala wa Ethiopia wakati wa karne ya nane K.W.K., Mfalme Tirhakah, hata anatajwa katika Biblia.

Kulingana na usimulizi wa Biblia, mfalme Senakeribu alikuwa akipigana na Libnah akiwa wakati uo huo anajitayarisha kushambulia Yerusalemu. Kwa ghafula, habari ikaja kwamba Mfalme Tirhakah alikuwa njiani kupigana na Waashuri. (2 Wafalme 19:8, 9; Isaya 37:8, 9) Hata hivyo, miandiko ya Kiashuri inasema kwamba Tirhakah alishindwa huko Eltekeh. Nusu karne baadaye, umiliki wa Ethiopia wa Bonde la Naili ulimalizika wakati Ashuru ilipotiisha Misri kabisa.—Nahumu 3:8-10; Isaya 20:3-6.

Katika kipindi hicho jiji la Napata lilikuwa limetumika kuwa jiji kuu la Ethiopia. Lakini katika 540 K.W.K., Meroë lilianza utawala walo wa miaka 800 likiwa jiji kuu la milki. Na ingawa milki ilizorota katika nguvu na uvutano, Meroë bado iliweza kutokeza nguvu fulani.

Katika kipindi cha umiliki wa Kiroma, towashi mmoja Mwethiopia alisaidiwa na Filipo mwevanjeli kuwa Mkristo. (Matendo 8:26-29, 38) Biblia inasema kwamba mwanamume huyu alikuwa mweka-hazina chini ya Kandake, malkia wa Waethiopia. Jina Kandake linaonekana lilikuwa cheo kilichomaanisha malkia waliotawala wakiwa Meroë. Hivyo basi huenda Meroë likawa lilikuwa na uzito fulani juu ya hata kundi la Kikristo.

Pambazuko la Milki

Kwa nini, basi, Meroë likatokomea? Habari zilizopo ni kidogo sana. Mambo yanafanywa magumu zaidi na uhakika wa kwamba lugha ya kale ya Kikushi bado haijafahamika waziwazi. Hati ya mwandiko-mviringo wa Kimeroe inayoonekana kwenye miingilio ya mahekalu, majumba ya kifalme, na majengo mengine ya mawe yaliyotapakaa sehemu zote za magofu hayo hayana kifani, ingawa namna ya Kimisri iliyorekebishwa ya mwandiko wa herufi-picha ilitumiwa katika kipindi cha mapema kidogo. Maneno ya Kimeroe yanaweza kusomwa na kutamkwa lakini, pole, hayawezi kueleweka. Hivyo basi ni lazima kwa kadiri fulani tujaribu kutegemea kudhania ili kuamua ni jambo gani hasa lililotukia.

Labda ule ufalme wenye kuinuka wa Axum ulinyang’anya Meroë nguvu zalo za kufanya biashara, halafu hilo nalo likaongoza kwenye mzoroto wa milki. Vyovyote ilivyokuwa, mwishowe Axum ilishambulia na kuharibu Meroë karibu 350 W.K. Hivyo ndivyo Meroë, majiji yaliyo dada zake, mwerevuko walo, na utamaduni walo vilififia kutoka historia mpaka machimbuo ya kiakiolojia hivi majuzi yakaufukua utukufu walo uliopita.

Marundo makubwa sana ya mavi ya chuma yaliyotapakaa kwenye mandhari karibu na Meroë la kale yanaonyesha kwamba watu wa huko waliijua siri ya kuyeyusha mawe yenye chuma, tena kwa kadiri kubwa sana. Katikati ya magofu ya Meroë, mtu anakuta vifaa vya ukulima na vita vilivyofanyizwa kwa chuma. Mahali ilipokuwa Meroë katika njia kuu ya kibiashara kati ya Mashariki na Magharibi palileta wafanya biashara wengi na misafara kwenye eneo la milki yalo. Kukiwa na uwezekano wa kuingia Bahari Kuu ya Hindi kupitia miinuko ya Ethiopia na kufika Afrika kwa kuelekea magharibi kusini mwa Sahara, Meroë lingeweza kwa urahisi kueneza maarifa na uongozi walo kwenye sehemu nyinginezo za Afrika.

Hata hivyo, sasa Meroë imo miongoni mwa falme nyingine zisizohesabika zilizoonja umashuhuri na mamlaka kwa ufupi halafu zikatoweka. Ingawa hapo kwanza lilikuwa na usanii na utajiri mwingi, jiji hilo leo ni kama rundo la magofu tu. Hata hivyo, bila shaka jiji hili la Kiethiopia la fahari iliyosahauliwa lilitia alama isiyofutika juu ya ukuzi na mweneo wa mwerevuko katika sehemu zote za Afrika.

[Picha katika ukurasa wa 18 ]

Mchoro wa kuchongwa juu ya ziara (kaburi) la piramidi

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 19]

Juu: Magofu ya hekalu huko Meroë

Chini: Maziara ya piramidi huko Meroë

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

SUDAN

Meroë

Bahari Nyekundu

MISRI

SAUDI ARABIA

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki