Deni! Kuingia Humo Kutoka Humo
LOIS na Rick walikuwa wamefunga ndoa kwa karibu mwaka mmoja. Kama waume na wake wengi vijana, walitaka kupata kila kitu mara moja—tena ilikuwa rahisi! Malipo ya TV yalikuwa dola 52 tu kwa mwezi, na kuongezea VCR kuliongezea malipo kuwa dola 78 tu. Fanicha mpya za nyumba zilikuwa ngumu zaidi kidogo—malipo yalikuwa dola 287 kwa mwezi. Bila shaka, hiyo haikuhusisha vitambaa vya madirisha na zulia, ambavyo viliinua malipo hayo kwa dola 46.50. Lakini kampuni ya fedha ilikuwa imeonyesha ushirikiano.
Walivipata vifaa hivyo kwa urahisi zaidi kwa sababu duka lile lilikubali kadi-mkopo yao. Hivyo malipo ya kila mwezi yalipatikana moja kwa moja bila shida, na haikuwa lazima wajaze ombi la mkopo. Ingalikuwa rahisi zaidi kama gari la Rick la mchezo wa mbio lingalikuwa limemaliza kulipiwa kabla ya arusi kama alivyokuwa amepanga, lakini yeye hakuwa amemudu kufanya hivyo.
Rick aliliweka wazo hilo hivi: “Nilifikiri ndoa ingekuwa maridadi, lakini nina wasiwasi sana juu ya madeni yetu hivi kwamba hiyo si raha hata kidogo.” Lois alikubali na kuongezea hivi: “Ilikuwa rahisi sana kuingia katika deni. Je! sisi kweli tutakuja kutoka katika madeni?”
Ulizo hili la kupiga yowe ni kielelezo cha tatizo la kubana ambalo lakabiliwa na mamilioni ya familia katika nchi zilizo nyingi za ulimwengu. Ni watu wachache sana ambao kwa kweli huweza kuishi bila kubeba mzigo mkubwa wa deni, ambao nyakati fulani huwa usiowezeka.
Kuingia Katika Deni
Mtu huingiaje katika deni? Ni sahili! Ni njia ya maisha. Serikali, mashirika yenye kuhusisha mataifa mengi, biashara ndogo-ndogo, familia, na watu mmoja mmoja wote huja kukubali ni jambo la kawaida kuwa na deni.
Mara nyingi kiburi hufanyiza deni. Deni hufanyiza mbaniko. Mbaniko huongoza kwenye magumu mengine. Hivyo basi mtu ataishije katika ulimwengu wenye mwelekeo wa madeni na, wakati ule ule, akae bila deni?
Labda somo la kwanza la kujifunza ni kukinza manunuo sahili. Mtu hawezi kuuingia mlango wa yaliyo mengi ya mashirika ya kifedha bila kukumbwa macho na vibandiko vyenye toleo la mikopo. Kadi-mkopo hupatikana kwa urahisi. Tangu wakopeshaji wenye kula riba hadi mashirika ya benki yenye kustahika, kuna mamilioni ya watu wenye mafanikio na ujasiri wa kukabili magumu katika biashara ya kuuza pesa. Kwao, pesa ni bidhaa—kama vyakula vya kununuliwa madukani—na kazi yao ni kuiuza kwako wewe. Jifunze kusema LA.
Kusimamia Deni
Kuna njia nyingi za kufasili kiasi cha deni ambayo yafaa mtu kuwa nacho kwa kupatana na mapato yake. Lakini zatofautiana sana hivi kwamba nyingi zina umaana mdogo. Mathalani, wanauchumi fulani huhisi kwamba familia yaweza kupangia asilimia 30 ya mapato yao ya jumla ili kulipia makao yao bila shida yoyote. Hii yahusu malipo ya rehani au kodi ya nyumba. Hata hivyo, njia hii huenda isiwafae walio maskini sana. Hivyo basi njia za ujumla huwa mara nyingi hazina maelezo ya wazi. Tatizo kamili la kudhibiti deni hufaa zaidi kufikiriwa na mtu binafsi.
Huenda deni fulani likawa lakubalika, lakini hii hutaka kutumia ufahamu na usimamizi wa uangalifu. Mathalani, watu walio wengi hawawezi kununua nyumba bila kuingia katika deni. Haifai kufikiri kwamba ni lazima familia iishi katika makao ya kukodi mpaka watakapoweka akiba ya pesa za kutosha ndiyo waende wakanunue nyumba kwa pesa taslimu. Labda hilo halitakuja kutukia kamwe. Bali, huenda familia ikahisi kwamba pesa wanazolipia kodi zaweza kuelekezwa upande mwingine ziwe za kumaliza kulipia rehani ya nyumba fulani. Hata ingawa mpango huu utachukua miaka mingi, wao hukata shauri kwamba unafanya kazi vizuri zaidi.
Tung’amuapo kwamba thamani ya nyumba yaelekea itaongezeka kadiri muda upitavyo, yaonekana wazi kwamba ingawa malipo ya rehani huenda yakawa ya juu kuliko kodi ya kila mwezi, huenda hali ya familia ikawa ni afadhali zaidi kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanapata usawaziko wa faida, ambayo ni thamani ya nyumba ile kuondoa kiasi kinachodaiwa dhidi yayo. Kwa hiyo kulipia rehani ya nyumba kwa malipo ya kiasi, yawezayo kulipiwa, huenda kukawa ni deni lenye kukubalika. Jambo hilo hilo laweza kusemwa juu ya manunuo mengine makubwa ya familia, yenye kuhitajiwa.
Huenda namna nyingine za deni zikawa zisizokubalika kabisa. Usimamizi mzuri wa madeni wahusisha uwezo wa kuyakataa. Labda kanuni bora zaidi ni hii: Usinunue usichokihitaji na usichokiweza. Epuka ununuzi wa kushtukia. Hata ikiwa kitu fulani ni cha nusu-bei, kwako wewe bado hakijashuka bei ikiwa hukiwezi. Usikope ili kununua bidhaa za anasa. Usiende safari za malikizo isipokuwa kama waweza kuzilipia kabla ya kwenda. Muda fulani baadaye bado itakuwa ni lazima ulipie chochote ununuacho. Kadi-mkopo ni zenye mafaa ili kuepuka kuchukua pesa taslimu lakini ni ghali sana zitumiwapo kama njia ya kukopa pesa.
Kutoka Katika Deni
Huenda watu fulani wakahisi kwamba ushauri juu ya usimamizi mzuri wa deni umewafikia kwa kuchelewa mno. ‘Tayari niko chini ya mporomoko wa gharama na madeni. Nitatokaje humo?’ Uhakika ni kwamba haijawa kuchelewa mno kuanza.
Hatua ya kwanza yapasa kuwa kuanzisha uhusiano wa kikazi pamoja na benki yenye kusifika. Ikiwa lazima ukope, yaelekea hapa ndipo utatozwa faida ya kiasi kizuri zaidi. Benki yako ikikunyima mkopo, labda inakufanyia hisani kwa kutenda hivyo. Kumbuka, benki imo katika biashara ya kukopesha pesa nayo itakukopesha ikiona inafaa.
Pili, ni lazima uanze kulipa madeni hayo kwa kufuata mpango uliotengenezwa. Katika karatasi, andika jinsi unavyotazamia pesa zako zitumike miezi 24 ijayo. Panga mipango iwezekanayo. Husisha kila pato utarajialo kuwa nalo. Halafu orodhesha kila kitu ambacho ni lazima kilipiwe. Pia weka nafasi wazi ya kununua bidhaa ambazo hata huwezi kuzifikiria kwa sasa. Panga madeni kwa mfuatano unaolingana na umaana wayo. Halafu gawa pesa zako kwa usawa ili kila deni lilipiwe angalau kiasi fulani. Weka lengo la kulipia kila deni ifikapo tarehe fulani.
Pamoja na mpango huu, fikiria ni wapi uwezapo kupunguza gharama. Kujidhabihu kwa kadiri fulani hutakiwa sikuzote ili kupunguza deni. Je! gharama za ununuzi wa kawaida zaweza kupunguzwa kwa kununua bidhaa ambazo hupigiwa bei? Ni vitu gani vya bei nafuu zaidi ziwezavyo kutumiwa wakati wa kupanga mapishi? Je! malikizo yaweza kupunguzwa? Je! kiwango cha maisha yako chaweza kupunguzwa? Je! vitu fulani vya anasa vyaweza kuliwa mara chache zaidi? Nyakati fulani huwa ni lazima tukose kujionyesha huruma. Gharama fulani zaweza kuondolewa katika safu ya “mahitaji ya lazima” na kuingizwa katika safu ya “mambo ya anasa.”
Mara ukiisha kutayarisha mpango wako katika karatasi, uzungumze pamoja na ofisa wako wa mkopo wa benki. Atavutiwa aonapo kwamba hufanyi mchezo. Huenda akaweza kukuonyesha jinsi ya kuufanyia maendeleo mpango huo. Huenda hata akadokeza upate mkopo wa kukuwezesha kulipia jumla ya madeni yote pamoja. Ikiwa ndivyo, hakikisha kufikiria kiasi cha faida itakayotozwa, na urefu wa wakati ambao itachukua kulipa mkopo huo wa ujumla wa madeni. Kwa kawaida itamaanisha zaidi kidogo kwa muda mrefu zaidi. Lakini usishawishwe kutumia mpango huo wa mkopo wa ujumla wa madeni ili kukopa pesa nyingine zaidi.
Wasiliana!
Programu yoyote ya kupunguza madeni hutaka uwasiliano ili iwe na mafanikio. Zuru au upigie simu kila mtu ambaye wewe una deni lake la pesa. Waonyeshe mpango wako, ikiwa wafikiri kufanya hivyo kungesaidia. Angalau ongea nao. Kumbuka, wao wataka kujua unalofanya. Endelea kuwapasha habari. Kitu kimoja ambacho mkopeshaji hawezi kuvumilia ni unyamavu. Unyamavu hufasiriwa upesi kuwa kutojali au hata kukataa kulipa. Wakopeshaji wengi wameanzisha kesi mahakamani ili warudishiwe pesa zao kwa sababu tu hakuna mtu aliyejali kuwaeleza lililokuwa likitendeka.
Je! yakupasa ufikirie kutangaza mfilisiko? Katika mabara fulani, watu wote huwa na haki ya kunufaika na maandalizi hayo ya sheria, lakini hayapasi kuchukuliwa kimchezo. Deni ni kujikabidhi wajibu. Wajibu wa kiadili wahusika. Kutangaza mfilisiko husambaza matatizo kuwafikia wengine. Hilo litabaki likiwa doa baya juu ya rekodi yako.
Hakuna ubaya na lile wazo la kizamani la kwamba “lipa ukiwa mwendoni.” Kwa kweli, ikiwa yawezekana, mwendo wa hekima ni kutokuwa katika deni mwanzoni. Deni laweza kuwa kama mchanga-topea ambao hukufyonza. Rick na Lois walijiruhusu wamezwe kabisa. Ni sharti wafanye mabadiliko, lakini hatua kwa hatua waweza kupanda juu watoke kwenye madeni yao.
Kama ungezikwa chini ya poromoko-ardhi la halisi, ungetumia uwezo wowote ulio nao ili uanze kujichimbua. Huenda likawa jambo la polepole, lakini lafanya kazi! Kumbuka, hata ichukue muda gani au iwe vigumu namna gani, kutoka katika deni kwastahili sana.
[Picha katika ukurasa wa 22]
Kuzama katika deni la kupita kiasi ni kama kufyonzwa na mchanga-topea