Kuutazama Ulimwengu
UKIMWI KATIKA MIAKA YA 1990
Kwenye mkutano mmoja katika Marseilles, Ufaransa, Dakt. Jonathan Mann, mkurugenzi wa Programu ya Shirika la Afya Ulimwenguni Kuhusiana na Ukimwi Katika Tufe Lote, alionya juu ya mweneo mkubwa sana wa UKIMWI katika tufe lote katika miaka ya 1990. Watu wengi kufikia milioni kumi huenda sasa wakaambukizwa vairasi hiyo katika nchi 152 kuzunguka ulimwengu. Kufikia mwaka 2000, huenda UKIMWI ukaua watu milioni sita. Ripoti katika The Times la London yasema kwamba Afrika ndiyo imepigwa zaidi. Katika Dar es Salaam, Tanzania, asilimia 42 ya wanawake wanaofanya kazi katika nyumba za pombe na mikahawa waripotiwa kuwa na vairasi hiyo. Katika Côte d’Ivoire, watatu kati ya watu wazima kumi walisemwa kuwa wameambukizwa. Juu ya hali hatari iliyo katika United States, Taasisi Hudson yaonya kwamba “msiba mkuu unaipiga kikumbo Amerika.” Yatabiri kwamba vairasi ya UKIMWI itaambukiza Waamerika wapatao milioni 14.5 kufikia mwaka 2002 na kuua Waamerika wengi zaidi katika miaka ya 1990 kuliko vita vyote katika historia ya taifa hilo vikiunganishwa pamoja.
“VICHUJO VYA KIBAYOLOJIA”
Maofisa Waholanzi wanachukua hatua mpya za kujianzia wenyewe ili kusafisha uchafuzi wa ziwa Zoommeer la hektari 1,210 katika Uholanzi. Wao wapanga kutumia makome (jamii ya chaza) kama walaji wa uchafuzi. Kama ilivyoripotiwa katika International Herald Tribune, lililochapishwa katika Ufaransa, makome hawa waweza kutenda kama “vichujo vya kibayolojia.” Majaribio ya uchunguzi yameonyesha kwamba makome hula na kumaliza kemikali zenye sumu na metali. Takataka chafu za vitu hivyo hutulia chini ambako huvutwa juu. Wanasayansi wadai kwamba makome hao waweza kumaliza asilimia 50 ya PCB (baifenili zenye klorini) na asilimia 30 au zaidi ya kadmiamu kutoka kwenye maji.
KARAMU ZENYE KUHITAJISHA POLISI
Karamu yenye fujo katika Bracebridge, Ontario, Kanada, imeongoza kuwe na programu mpya ya polisi katika eneo hilo. Wazazi waliacha mwana wao wa miaka 15 atunze nyumba na ndugu yake wa miaka 10 walipokuwa wameenda zao. Mwana huyo aliandaa karamu kwa ajili ya vijana karibu mia moja, na muda si muda ikawa na fujo. Majirani waliita polisi, lakini mvulana huyo akakataa kuwaacha waingie nyumbani. Baadaye, yule mvulana wa miaka kumi aliwaita polisi. Vijana hao walikuwa wamemlazimisha kunywa pombe mpaka akalewa halafu wakamkaanga na kumla kipenzi samaki wake wa kitropiki mbele yake. Kufikia wakati ambapo polisi walirudi wakiwa na hati ya ruhusa ya upekuzi, vijana hao walikuwa wamefanya hasara ya dola 13,000 kwenye nyumba hiyo. Tangu hapo, programu mpya yawezesha wazazi wanaoacha matineja wakitunza nyumba yao kuwajulisha polisi mapema, wakiwapa mamlaka ya kuingia ndani ya nyumba wakishuku kuna mivunjo yoyote ya sheria za dawa za kulevya, pombe, au uhalifu.
UTOAJI MIMBA WA KUJISAIDIA BINAFSI
Baada ya utungaji wa sheria ya hivi majuzi ulioipa mikoa katika United States mamlaka zaidi ya kuzuia visa vya kutoa mimba, vikundi vingi vya wanawake kujisaidia binafsi vinatokea upya na kutangaza njia ambazo wanawake waweza kujitoa mimba. The New York Times laripoti kwamba mamia ya wanawake hivi majuzi wametoana mimba kwa njia hiyo, na kwamba makala, vitabu, na kanda za vidio zenye kupangilia njia hizo zagawanywa kotekote. Mteteaji mmoja wa haki za wanawake aliliambia Times kwamba hiari hizo huwapa wanawake mamlaka zaidi. Lakini hata vikundi fulani ambavyo hupendelea kutoa mimba vyapinga utoaji mimba wa kujisaidia binafsi, wakishutumu hatari ya kufanya hivyo.
MAOMBI YA KANISA YASIYO NA PADRI
Upungufu wa mapadri Wakatoliki katika United States umeongezeka vikali sana hivi kwamba kusanyiko la hivi majuzi la maaskofu wa nchi hiyo lilikubali maombi ya Jumapili kwa mitaa isiyo na mapadri. Shemasi au mtu wa kikawaida, wa kiume au wa kike, aweza kuongoza maombi mapya hayo. Yatahusisha tenzi za kuimbwa, zaburi, usomaji wa Maandiko, Sala ya Bwana, na Komunio Takatifu ikiwa kwapatikana mkate ambao umetakaswa na padri au ukaletwa kutoka kwenye Misa halisi. Maaskofu hao wakazia kwamba maombi mapya hayo si Misa. Lakini kadiri ambavyo mitaa mingi yalazimika kuwa bila mapadri, huenda maombi hayo yakahitajiwa sana.