Wakati Ukimwi Si Tisho
Katika jioni ya Oktoba 3, 1984, Kyle Bork mchanga alizaliwa majuma saba kabla ya wakati wake. Mapafu yake madogo sana yalikuwa yamebaki mno kukomaa hivi kwamba hayakuweza kufanya kazi ifaavyo, hivyo basi akahamishwa kilometa 56 kupelekwa Hospitali ya Watoto ya Jimbo la Orange, kulikokuwa na vifaa vya kutunza watoto walio mahututi.
Daktari alieleza kwamba damu ya Kyle ingehitaji kujazwa upya kwa kutiwa mishipani; au sivyo kwa uyamkini wote angekufa. Ingawa hilo lilitatiza sana wazazi, walisimama imara kwenye uamuzi wao wenye msingi wa Biblia kutoruhusu mtoto wao atiwe damu mishipani. (Mwanzo 9:4, 5; Walawi 17:10-14; Matendo 15:28, 29) Daktari alielewa na kushirikiana. Hata hivyo, yeye alisema, kama hali ingekuwa ya hatari kabisa, angeenda kupata agizo la mahakama ili amtie damu mishipani.
Kwa kushangaza, Kyle alionyesha maendeleo yenye kuongezeka kwa uthibitifu, na kufikia siku ya tisa, aliondolewa kwenye chombo cha kusaidia upumuaji. Siku mbili baadaye wazazi walimpeleka nyumbani, naye akakua akawa mtoto mwenye furaha na afya, kama uwezavyo kuona kutokana na picha hii. Lakini haikushia hapo.
Mwaka uliopita (1989) habari moja ya televisheni Los Angeles iliripoti kwamba watoto kadhaa waliokuwa wamekuwa katika Hospitali ya Watoto ya Jimbo la Orange karibu na wakati ule Kyle alipokuwa huko waliambukizwa UKIMWI kutokana na damu iliyochafuka. Hospitali ilikuwa ikijaribu kupashana habari na familia za watoto karibu 3,000 ili waweze kutahiniwa kama wana vairasi ya UKIMWI.
Mara ile ile, wazazi wa Kyle walipigia simu kwenye hospitali kuhakikisha kwamba hakuwa ametiwa damu mishipani bila wao kujua. Upesi, hospitali nayo ikawapigia simu kuwahakikishia kwamba hakuwa amepokea damu yoyote na hivyo basi hakuwa katika hatari ya kuambukizwa UKIMWI. “Tulipiga magoti kihalisi tukamshukuru Yehova,” wazazi hao wakaeleza, “kwa kutupa sheria zake adilifu na imara ya kudumisha uaminifu wa maadili kwa kukabiliana na mtihani wa jinsi hiyo.”