Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 8/8 kur. 12-13
  • Dhambi ya Asili Ilikuwa Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Dhambi ya Asili Ilikuwa Nini?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je! Ngono Ilikuwa Ndiyo Dhambi ya Asili?
  • Je! Lilikuwa Ni Maarifa?
  • Je! Kulikuwa Ni Kutotii?
  • Dhambi ya Kwanza Ilikuwa Nini?
    Amkeni!—2006
  • Dhambi ya Kwanza Ilikuwa Nini?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Sababu Kwanini Tunazeeka na Tunakufa
    Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele
  • Twaweza Kujifunza Kutokana na Wenzi Wawili wa Kwanza wa Kibinadamu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 8/8 kur. 12-13

Maoni ya Biblia

Dhambi ya Asili Ilikuwa Nini?

DHAMBI ya asili ilikuwa nini? “Ilikuwa ngono,” watu wengi watajibu. Wao huamini kwamba tunda lililokatazwa katika bustani ya Edeni lilikuwa kifananisho cha mahusiano ya kingono na kwamba Adamu na Hawa walitenda dhambi kwa kufanya kitendo cha ngono.

Wazo hilo si jipya. Kulingana na mwanahistoria Elaine Pagels, “dai la kwamba dhambi ya Adamu na Hawa ilikuwa kujitia katika mwingiliano wa ngono” lilikuwa “kawaida miongoni mwa walimu Wakristo [wa karne ya pili] kama vile Tatian Msiria, aliyefundisha kwamba tunda la mti wa maarifa lilikuwa na maarifa ya kujuana kimwili.” Pia, kwa maoni ya Augustino Baba wa Kanisa wa Jumuiya ya Wakristo wa karne ya tano W.K., dhambi ilipata mianzo yayo katika tamaa ya kingono kwa upande wa Adamu. Kwa uhakika, Psychology Today lilisema “dhambi ya Adamu ilikuwa kujuana kimwili.”

Wengine wamechukua msimamo wa kwamba mti wa maarifa ya mema na mabaya uliwakilisha maarifa yenyewe. Encyclopædia Britannica hushikilia kwamba “maarifa ya mema na mabaya” ulikuwa “wonyesho wa kiwango bora mno cha maarifa yote.” Hiyo ingemaanisha kwamba Mungu alitaka Adamu na Hawa wawe wajinga wasiojua mambo na kwamba wao waliasi dhidi yake kwa kutafuta kupanua maarifa yao.

Kwa uhakika fasiri zote mbili huonyesha juu ya Muumba asiyefuata haki na mwenye kigeugeu. Mbona aumbe binadamu mwenye mahitaji ya kingono na pia mwenye akili ya kuelewa mambo halafu asimruhusu awe na njia ya kutimiza tamaa hizo bila kupata adhabu ya kifo? Ni nani angehisi akivutwa kumpenda na kumtumikia Mungu wa jinsi hiyo?

Je! Ngono Ilikuwa Ndiyo Dhambi ya Asili?

Wengi hawajui kwamba fasiri hizi zote mbili hupingana kabisa kabisa na habari zenye kuzunguka usimulizi huo wa Mwanzo. Acheni tulifikirie kwanza wazo la kwamba kwa kweli katazo la Mungu katika Edeni lilikuwa dhidi ya mahusiano ya kingono. Sheria yenye kuhusika imeandikwa kwenye Mwanzo 2:16, 17: “Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa [maarifa ya, NW] mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.”

Je! kweli hilo lilikuwa rejezeo lenye kuhusu ngono likiwa limefichwa? Basi, kama ilivyoandikwa kwenye Mwanzo 1:27, 28, Mungu aliamuru mwanamume na mwanamke ‘wazae na kuongezeka na kujaza dunia.’ Adamu na Hawa wangetiije amri hiyo bila kufanya mahusiano ya kingono? Je! kweli tudhanie kwamba Mungu aliwapa amri halafu akawahukumia kifo kwa kujaribu kuitii?

Zaidi ya hilo, usimulizi wa Mwanzo huonyesha kwamba Adamu na Hawa walitenda dhambi huku kila mmoja akiwa amejitenga, si kwa wakati ule mmoja. Sura ya 3, mstari wa 6, NW, huelewesha wazi kwamba Hawa alikuwa ndiye wa kwanza kutongozwa ale kutokana na lile tunda na kwamba “baada ya hapo akampa mume wake baadhi yalo na yeye akaanza kulila.” Kwa hiyo lingekuwa jambo la kiupuuzi na lisilo la kiasili kamwe kuonyesha kwamba lile tunda lililokatazwa lilikuwa kifananisho cha mwingiliano wa kingono.

Je! Lilikuwa Ni Maarifa?

Namna gani dai la kwamba tunda lililokatazwa lilikuwa kifananisho cha maarifa yote? Kwa kweli, wote wawili Adamu na Hawa walikuwa tayari wametwaa maarifa tele kabla hawakosa kuitii sheria kwenye Mwanzo 2:16, 17. Muumba wao, Yehova mwenyewe, alihusika moja kwa moja katika kuwaelimisha. Mathalani, yeye alimletea mwanadamu huyo wanyama na ndege wote ili awape majina. (Mwanzo 2:19, 20) Bila shaka ingekuwa lazima Adamu achunguze kila mmoja kwa uangalifu ili ampe jina lifaalo. Lo, elimu-wanyama iliyoje! Ingawa Hawa aliumbwa baadaye, yeye pia hakuwa mjinga asiye na maarifa. Alipoulizwa swali na nyoka, alionyesha kwamba alikuwa ameelimishwa katika sheria ya Mungu. Alijua tofauti kati ya yafaayo na yasiyofaa, na hata alijua matokeo ya vitendo visivyofaa.—Mwanzo 3:2, 3.

Fasiri ya dhambi ya asili kuwa ilikuwa ama ngono ama maarifa iko kama neno lenyewe lilivyo—fasiri ya kibinadamu, na basi. Udhaifu wayo huonyeshwa wazi na swali la Yusufu yule mwanamume mwaminifu: “Kutafsiri si kazi ya Mungu?” (Mwanzo 40:8) Biblia huwa rahisi zaidi kueleweka tusipoiwekelea mawazo ya kibinadamu na, badala ya hivyo, tuache ijifasiri yenyewe. Basi, je! dhambi ya asili ilikuwa nini? Usimulizi wa Mwanzo watupa kila sababu ya kuamini kwamba mti wa maarifa ya mema na mabaya ulikuwa mti halisi. Sisi huambiwa ulikuwa wapi katika bustani hiyo, nao hutajwa kwa kuhusiana na miti mingine. Tunda lao lilikuwa halisi, na Adamu na Hawa walikula tunda hilo kihalisi.

Je! Kulikuwa Ni Kutotii?

Kwa kula kutokana na tunda hilo, walikuwa wakifanya nini? New Catholic Encyclopedia hudokeza hivi bila kuwa na hakika: “Ingeweza kuwa kulikuwa ni kumkaidi Mungu waziwazi, katao la kifidhuli kumtii Yeye.” Je! hivyo sivyo Mwanzo husema waziwazi? Warumi 5:19 huhakikisha jambo hilo: “Kwa kutotii kwa mtu mmoja wengi walifanywa kuwa watenda dhambi.” (The New Jerusalem Bible) Dhambi ya asili ilikuwa kitendo cha kutotii.

Ingawa huenda dhambi ya kutotii ikaonekana kuwa sahili juu-juu, fikiria yale ambayo inayamaanisha kwa kina kirefu. Kielezi cha chini katika The New Jerusalem Bible huweka wazo hilo hivi: “Hayo [maarifa ya mema na mabaya] ni nguvu ya kujiamulia mwenyewe lililo jema na lililo ovu na ya kutenda hivyo, dai la kuwa na ujitegemeo kamili wa kiadili . . . Dhambi ya kwanza ilikuwa shambulio juu ya enzi kuu ya Mungu.” Ndiyo, “mti wa maarifa ya mema na mabaya” ulifananisha haki ya Mungu kuwekea mwanadamu viwango juu ya jambo lenye kukubaliwa au lenye kulaaniwa vikali. Kwa kukataa kutii sheria ya Mungu, mwanadamu alikuwa akitia shaka juu ya haki yenyewe hasa ya Mungu kutawala juu yake. Yehova alilijibu kwa haki dai hilo la ushindani kwa kuruhusu mwanadamu ajitawale mwenyewe. Je! wewe hungeafiki kwamba matokeo yamekuwa yenye msiba?—Kumbukumbu 32:5; Mhubiri 8:9.

Hiyo ndiyo sababu kichwa cha Biblia, Ufalme wa Mungu, huleta tumaini jingi sana. Kwa njia ya Ufalme huo, Yehova huahidi kumaliza utawala wa binadamu ulio na uonevu na mahali pao alete utawala Wake—serikali ambayo itarudisha paradiso ya kidunia—kitu ambacho Adamu na Hawa walipoteza.—Zaburi 37:29; Danieli 2:44.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Je! Adamu na Hawa walitenda dhambi ya asili kwa kufanya mahusiano ya kingono?

[Hisani]

Gustave Doré

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki