Dunia Safi Twaihitaji
Na mleta habari za Amkeni! katika Uingereza
JE! ulijua kwamba madereva wa teksi wa London hupasishwa na sheria kuweka teksi zao zikiwa safi? Tokeo la kutofanya hivyo laweza kuwa marufuku kwao wasiwe katika barabara za jiji kwa kipindi fulani. Hata wakati hali za barabarani ziwapo mbaya na motakaa zilizo nyingi zibakipo zikiwa chafu kwa siku nyingi, teksi ya London huwa safi kabisa. Nyuso zenye kumeta-meta za gari hilo hutia katika dereva na abiria zake hisia za fahari na raha.
Vivyo hivyo, wakati nyumba yetu, nguo zetu, na vitu vyetu viwapo safi, hiyo huendeleza ndani yetu hisia ya hali njema. Ole wake mvulana wa shule ambaye mamaye amwona akiingia ndani ya nyumba ali akiacha zulia likiwa na alama za matope kutoka kwenye viatu vyake vichafu!
Kwa uhakika, afya nzuri hutegemea sana usafi wa kibinafsi. Mwili wetu hutaka utunzaji wa ukawaida na usafi wa kuondoa uchafu ambao huandaa msingi imara wa kutokeza magonjwa. Mashirika ya kibiashara hupata faida kubwa sana kwa kuuza dawa za kutakasa, vizuia-viini, ving’arisho, sabuni, shampuu (viosha nywele), na dawa za kuua-viini ambazo sisi hutumia kutunza usafi wetu wenyewe na wa mazingira yetu. Kwa uhakika, watu walio wengi hujali uhitaji wa kuwa safi. Lakini ikiwa wewe waishi katika jiji, wajua kwamba mambo yote hayawi hivyo.
Hatari—Uchafuzi
Wakaaji wa majiji wajua vema juu ya uchafuzi na mazingira yenye kuchafuzwa. Wao huuona katika takataka zisizokusanywa, katika vifusi vilivyoachwa kizembe kwenye barabara, na katika michoro ya kukwaruza ovyo majengo ya umma. Wao huunusa katika mioshi yenye kusonga pumzi kutoka kwenye magari yaliyosongamana na katika ukungu wa moshi mkali ambao hukumba majiji fulani.
Labda hiyo ndiyo sababu pindi kwa pindi watu wengi waishio majijini hujaribu kutumia wakati mashambani. Wao huona shangwe kujaza mapafu yao kwa hewa safi, labda hata kunywa maji maangavu kabisa kutokana na kijito fulani cha mlimani. Wengine hupenda kwenda ufuoni na kustarehe juu ya mchanga au kupoa kwa kujichovya kwa njia yenye upendezi katika bahari kuu.
Ingawa hivyo, ebu ngoja kidogo! Hata huko kuna taka na uchafuzi wenye kujificha. ‘Yawezaje kuwa hivyo?’ wewe wauliza. ‘Paonekana kuwa safi.’ Basi, acheni tuyatazame kwa ukaribu zaidi hewa hiyo “safi” na maji hayo “maangavu.”