Kuutazama Ulimwengu
WARUKAO KWA NDEGE MARA NYINGI HUPATWA NA MNURURISHO
Wasafiri wa hewani huwa katika hali ya kupatwa na kadiri kubwa zaidi ya mnururisho kutoka kwenye nyota na jua kuliko watu walio hapa chini, ndivyo uonyeshavyo uchunguzi wa kutoka Idara ya Usafiri ya United States. Wafanya kazi wenye kusafiri hewani, warukaji wa ndege wasafirio safari ndefu mara nyingi sana, na wanawake wenye mimba wako katika hatari kubwa zaidi, yasema ripoti hiyo. Kadiri ndege inavyoruka juu zaidi na kadiri ikaribiavyo zaidi zile ncha za dunia, hasa wakati wa dhoruba za jua, kiasi cha mnururisho huzidi. Hata hivyo, Dakt. A. B. Wolbarst wa Shirika la Ulinzi wa Mazingira United States aliambia The New York Times kwamba hatari za kupatwa na kansa kutokana mnururisho wakati wa kuruka kati ya New York na Athens “ni ndogo zikilinganishwa na hatari za aina ambayo mtu hukabili katika ulimwengu.”
NI NINI CHA MAANA KWA VIJANA?
Uchunguzi mmoja uliuliza vijana zaidi ya 2,000 wa Australia Magharibi wa kuanzia miaka 12 hadi 24 wakadirie habari zilizo za maana zaidi kwao. Matokeo yalionyesha kwamba maisha ya familia yalikuwa ndilo suala la maana zaidi kwa vijana, kupita kwa mbali habari nyinginezo. Pia vijana hao walionyesha hangaiko juu ya wakati ujao wao wa kibinafsi na wakati ujao wa jamii ya watu kwa ujumla, kulingana na gazeti The West Australian. Masuala yale mengine ya maana zaidi yalikuwa elimu na mazoezi, amani, mapato, na afya. Lakini masuala ya kisiasa na ya kidini yalipangwa chini sana katika orodha.
“TALAKA YA NDANI YA NYUMBA”
Katika Japani talaka miongoni mwa waume na wake wa makamo imekuwa zaidi ya maradufu katika miaka 20 iliyopita. Mshauri wa mambo ya talaka Yoriko Madoka aeleza kwamba, kwa kawaida mke hutafuta talaka kwa ghafula baada ya miaka 30 ya ndoa, na mume huhisi “mkono wake umeumwa na mbwa kipenzi wake mwenyewe.” Ingawa hivyo, kulingana na The Daily Yomiuri wanawake wengi huona ni afadhali kuchagua “talaka ya ndani ya nyumba” badala ya kukabili magumu ya kuwa watalikiwa. Ndiyo kusema, mume huishi kwenye ghorofa ya nyumba na mke sehemu ya chini pamoja na watoto. Mke hamfanyii mume lolote na hujaribu kuepuka kukutana naye. Hivyo, hadhi yao katika jamii ya watu, uthabiti wa kiuchumi, na heshima ya kuonekana kwao hudumishwa. Lakini kwa muda gani? Talaka zilizoruhusiwa na mamlaka kwa watu wa miaka zaidi ya 60 ziliruka asilimia 42.3 kati ya 1983 na 1988, kukiwa na hesabu zinazolingana za waume na wake wenye kutafuta talaka.
BIASHARA HATARI YA NYUNI
Biashara ya nyuni-mwitu yalaumiwa kwa mamilioni ya vifo vya nyuni kila mwaka—makadirio yakiinuka juu kufikia vifo mia moja milioni. “Kati ya nyuni washikwao mwituni mmoja ndiye huuzwa akiwa hai na angalau watano hufa,” ladai jarida Personality la Afrika Kusini. Ili kushika nyuni wa kigeni, wafanya biashara fulani huiangusha miti yenye viota na kukamata wachanga ambao hufaulu kuokoka anguko hilo. Njia nyingine ni kufyatua kundi la nyuni kwa vitonge fulani na kushika wale waangukao ardhini wakiwa na majeraha madogo mabawani. Halafu hufuata ile kazi ya kuwatunza nyuni wakiwa hai na kuwasafirisha kwa eropleni hadi mabara ya mbali, ambako mara nyingi wao huwasili wakiwa wamekufa. Kungeweza kuwa na faida gani katika jambo hilo? Personality laeleza hivi: “Hesabu ya nyuni wafanyiwao biashara hukadiriwa hesabu ya kiasi kuwa karibu milioni 5 kwa mwaka. Lakini hiyo haitii ndani ile hesabu kubwa sana ya nyuni wafanyiwao ulanguzi . . . Watu wapendao nyuni na kuwakusanya wako tayari kulipa kufikia dola 250,000 ili wapate namna-namna zitamaniwazo sana lakini zenye kulindwa.”
MKATABA WA HALIHEWA YA TUFE LOTE
Baada ya masikilizano magumu, mataifa yote 159 yaliyo washiriki wa UM yaliafikiana kuandika mswada wa mapatano ya kuimarisha halihewa ya dunia. Watakutana Brazili katika 1992 kuzungumza njia za kuzuia kupata joto kwa halianga na kupunguza matokeo mazito ya usitawi wa uchumi juu ya mazingira. Lakini mwafaka waishia hapo, na masuala mengi yaliyo ya umuhimu mkubwa bado yahitaji kutatuliwa. Kulingana na Paul Lewis mwandishi wa habari, nchi zinazositawi zaona kwamba hangaiko ambalo ulimwengu uliositawi kiviwanda unalo juu ya mazingira laweza kutumiwa kuwa nafasi ya kukazania ili haki fulani za kiuchumi ziruhusiwe. Kwa malipo ya ushirikiano wao, zataka ziruhusiwe kutumia mbinu mpya za kiufundi zilizo salama kwa mazingira, na pia kuondolewa madeni na kupewa bei za juu zaidi kwa bidhaa wanazopeleka nje. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba watu milioni elfu moja—karibu sehemu moja kwa tano ya idadi ya watu wa ulimwengu—wangeweza kuwa watoro ikiwa hali ya dunia itakuwa yenye joto kali mno kufanya usawa wa bahari uinuke sana.
REKODI ZINAZOOZA
Karibu asilimia 70 ya Hifadhi za Rekodi za Kiserikali za North Rhine-Westphalia, Jamhuri ya Muungano ya Ujeremani, zaelekea kuoza. Uozi huo, kulingana na waziri mmoja wa serikali, wasababishwa hasa na karatasi yenyewe. Tangu karne ya 19, karatasi yenye kutengenezwa viwandani imekuwa na vitu vyenye kutoa asidi ambavyo hutokeza uozi. Frankfurter Allgemeine Zeitung laripoti kwamba asilimia 26 ya bidhaa zilizopo tayari zimegeuka kuwa manjano kwa kadiri zenye kutofautiana. Njia za tangu zamani za kuzihifadhi na kuzirudishia hali ya kwanza zasaidia kutatua jambo hilo kwa sehemu tu.
MAANDISHI JUU YA AFYA
◻ Kula mara nyingi kwaweza kuwa na manufaa, wasema watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Toronto. Kwa kulishwa kiasi kile kile na namna ile ile ya chakula lakini kwa visehemu 17 vya baada ya kila saa moja badala ya kulishwa mara tatu kwa siku, kikundi cha wanaume kilichofanyiwa uchunguzi kilionekana kuwa na mpunguo wa asilimia 13.5 kwa wastani katika kolesteroli LDL (“mbaya”), jumla ya asilimia 8.5 ya kolesteroli ya damu, na insulini ya damu ya asimilia 29. Kula mlo mmoja mkubwa kwa siku kulisemwa kuwa ndicho kigezo kibaya zaidi cha kula. Kipingamizi kimoja ni kwamba kubwakia vyakula vidogo-vidogo kwa kawaida huongoza kwenye ulaji mkubwa zaidi wa kalori.
◻ Uchunguzi mmoja uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association waonyesha kwamba wanawake wanaotumia vibonge vinavyoruhusiwa kununuliwa bila agizo la daktari vya vitamini za namna nyingi vyenye asidi-foliki wakiwa wanajaribu kutunga mimba na kwa angalau majuma sita baada ya kuwa na mimba hupunguza sana uwezekano wa kuzaa watoto wenye kasoro katika mrijaneva. Kasoro za mrijaneva zaweza kusababisha kupooza, uzuizi wa ukuzi wa akili, na kifo.
◻ “Sasa kuna uthibitisho mwingi sana kwamba ulaji wenye matunda na mboga nyingi waweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata kansa,” lasema gazeti New Scientist. Vitamini ambazo hupatikana kwa njia hiyo “hutia matokeo yazo yenye ulinzi kwa kupambana na utendaji wenye madhara katika chembe za mwili.” Watafiti wasema kwamba kadiri mboga ziliwavyo zaidi, ndivyo ielekeavyo zaidi kwamba mtu hatapatwa na kansa ya mapafu. Na bila vitamini C ya kutosha, matokeo ya kuchanganyikana kwa oksijeni katika mkondo wa damu yangeweza kuleta maradhi kama mipoozo, ugonjwa wa moyo, na mitoto ya macho.
JE! MBWA WAWEZA KUONA RANGI?
Mbwa wana uwezo haba wa kuona rangi, ndivyo wakatavyo shauri watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Kalifornia kule Santa Barbara. Baada ya uchunguzi wa mwaka mmoja, wanasayansi walipata kwamba mbwa waweza kutofautisha rangi ya mwisho huu na ya mwisho ule mwingine katika lile fungu la rangi mbalimbali, nyekundu na buluu, lakini hawawezi kutofautisha kati ya manjano, kijani, na rangi ya chungwa.
KUFIKIRI SANA
JUU YA MITIO-MISHIPANI
Kumekuwa na ongezeko la mitio-damu mishipani katika nchi zinazositawi ili kutibu wagonjwa wachanga wa maleria walio na upungufu wa damu mwilini kwa kadiri ya kutisha uhai. Kwa kielelezo, katika 1986 mitio-mishipani hiyo 16,352 ilitolewa kwenye Hospitali ya Mama Yemo, Kinshasa, Zaire. Hata hivyo, wakati wa 1987 hesabu ya mitio-mishipani ilipungua. Kwa nini? Gazeti Panoscope lenye makao London laripoti kwamba baada ya madaktari huko Mama Yemo kugundua kwamba asilimia 13 ya kikundi cha watoto waliotiwa damu mishipani kwa sababu ya maleria waliambukizwa HIV, ile vairasi yenye kubeba UKIMWI, wafanya kazi wa tiba kwenye hospitali hiyo walibadili mwongozo wao wa “damu moja kwa moja kwa watoto wenye upungufu wa damu mwilini.” Badala ya hivyo, wagonjwa fulani wachanga kwenye hospitali hiyo ya Kinshasa walipewa viongeza-chuma-mwilini ili kusaidia kuongezea damu yao. Kwa njia hiyo, yasema Panoscope, “hesabu ya mitio-damu mishipani ilipunguzwa kwa asilimia 73 ikawa 4,531—na hakuna uhai wa hata mtoto mmoja uliopotea.”
MATOKEO MACHUNGU
Katika miaka ya 1970 wanaume wengi Wajeremani walichagua kuondolewa nguvu za uzazi. Gazeti Main Post laripoti kwamba walinaswa katika “lile wimbi la uhuru wa ngono.” Profesa W. Schulze, wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hamburg-Eppendorf, afikiri kwamba wengi walichagua upasuaji huo kwa utayari mwingi kupita kiasi. Sasa hesabu inayoongezeka ya wanaume walioondolewa nguvu za uzazi wangependa wapasuliwe upya ili kurudisha nguvu za uzazi. Hata hivyo, katika asilimia 10 ya visa hivyo, haiwezekani tena kurudisha nguvu za uzazi. Zaidi ya hilo, mawezekano ya kufanikiwa kurekebisha kuondolewa kwa nguvu za uzazi yazidi kuwa machache zaidi kadiri wakati upitavyo.
SANDWICHI YENYE KULISHA MWILI
Wazazi hawahitaji kuhangaika sana ikiwa watoto wao hula siagi-karanga na mkate tu wakati wa chakula cha mchana shuleni. Eleanor Brownridge, mchunguzi wa mambo ya lishe wa London, Ontario, Kanada, adai kwamba hakuna kasoro “kuhusiana na sandwichi ya siagi-karanga kwa sababu kipakwa hicho na mkate huwa ni viambato bora vya protini.” Mwanamke huyo aongezea kwamba ni jambo sahili “kuongezea ubora wa ladha na lishe ya siagi-karanga kwa vichanganyio vingine . . . kama tofaa lililokatwa-katwa, zabibu kavu, aprikoti, tende, ndizi iliyokatwa-katwa, hata kolislo.” Wanafunzi wachanga zaidi huelekea kuhisi wakiwa salama kwa kula namna moja za vyakula vya mchana walivyozoelea. Lakini, laripoti The Vancouver Sun, “ni vizuri pia kuhusisha mambo machache yasiyotazamiwa kama vile kuukata mkate kwa kisu cha kukatia au kuufunga taarifa fupi katika kisanduku cha kuchukulia chakula cha mchana.”