Je! Uikamate Chafya?
NYAKATI fulani sisi sote hutaka sana kukandamiza chafya. Labda ni wakati wa sherehe yetu ya arusi, tusimamapo tukiwa tayari kutwaa nadhiri zetu. Au huenda ikawa ni wakati wa mkutano au pindi nyingine ya umaana mzito, hata maziko.
Bila shaka, kuna nyakati nyingi ambapo kupiga chafya kubwa huonekana jambo la kuonewa shangwe sana, na hisia ya ustarehe wenye hali njema hufuata. Lakini mara nyingi tatizo ni jinsi ya kushughulikia chafya isiyotakwa.
Si chafya zote zilizo sawasawa. Watu fulani wana ile ambayo ingeweza kuitwa chafya yenye mvumo mkubwa wa kufurahisha, iwezayo kusikiwa umbali wa kutosha. Wengine wana chafya pole zaidi. Halafu kuna ile chafya yenye kujirudia-rudia: chafya tatu, nne, tano, au hata zaidi kwa mfululizo. Katika visa vichache sana, watu mmoja mmoja wamesitawisha kupiga chafya ya daima kila sekunde chache au dakika wakiwa macho, kwa muda wa saa nyingi, siku, majuma, au hata miezi.
Ni nini hutufanya tupige chafya? Je! kuna njia yoyote hakika ya kukandamiza chafya? Je! kuna hatari za kuzuia chafya kwa lazima mara kawaida hiyo ikiisha kuanza? Na je! hatua zozote zaweza kuchukuliwa ili kuondolea mbali kupiga chafya?
Kisababishi cha Kupiga Chafya
Yaonekana kwamba kila mtu hupiga chafya nyakati fulani—wazee na vijana, watu wazima na watoto wachanga. Hata wanyama wajulikana kuwa hupiga chafya. Katika visa vilivyo vingi kisababishi ni kitu kigeni (kama vumbi au chavuo) ambacho huwasha mianzi ya pua. Lakini hisia-moyo zetu pia zaweza kuleta pigo la chafya. Baadhi yetu huenda hata wakapata kwamba nuru nyangavu ya jua yatosha kusababisha kupiga chafya. Hii ni kwa sababu mishipa ya fahamu za macho yashikamana kwa ukaribu na ncha za mishipa ya fahamu katika pua.
Ncha zenye hisia nyepesi za mishipa ya fahamu huitikia kuwapo kwa kitu chenye kuwasha kwa kupeleka ujumbe fulani ubongoni. Huo nao huagiza pua iandae umajimaji wa kusaidia kuondoa kitu hicho kisichotakwa. Pia ubongo hupeleka jumbe kwenye mapafu hivi pumuo la hewa lavutwa kuingizwa mapafuni, halafu kwenye kanda za sauti ili kufunga mrija wa hewa na kuzuia hewa isiponyoke. Misuli ya ukuta wa kifua na tumbo huambiwa ikazane, hivyo kufinya hewa iliyo katika mapafu. Mwishowe, kanda za sauti huagizwa zilegee, na ile hewa iliyofinywa huondoshwa haraka sana, kwa kawaida ikiondosha nje kile kiwasho kisichotakwa pamoja na umajimaji ule. Yote haya hutukia bila jitihada yenye kufahamiwa, tena kwa haraka kuliko muda ambao imechukua kuzisoma habari za jambo hilo.
Katika visa vilivyo vingi, kupiga chafya daima ni dalili ya mwathiriko wa kawaida mwilini ambao huitwa mafua-nyasi-kavu. Chavuo (unga-unga) ya mimea ndiyo huandaa kiwasho hicho, na ingawa huenda jina hilo mafua-nyasi-kavu likadokeza kwamba nyasi zilizokauka au zilizokatwa karibuni ndizo kisababishi, huenda isiwe hivyo sikuzote. Huenda ikawa wenye kuteseka huathiriwa na chavuo kadhaa tofauti-tofauti, au labda moja tu. Hivyo basi ni rahisi kuelewa ni kwa nini wenye kuteswa na mafua ya kunusa manyasi huogopa sana misimu ambapo pepo kali kavu huvuma kwa siku nyingi. Mianzi ya pua ikiisha kuwashwa kisha chafya yenye kuendelea ianze, hata kavumbi ambako kwa kawaida hakingesababisha mwasho huelekea kumwanzishia mtesekaji duru nyingine ya kupiga chafya.
Kuwafikiria Wengine
Wakati mianzi ya pua ijazanapo kwa sababu ya mafua mazito ya kichwani, kupiga chafya kwaweza kumpa mtesekaji kadiri fulani ya kitulizo. Kupumua huwa rahisi zaidi wakati kamasi iondolewapo puani kwa njia hii. Lakini chafya isipofunikwa, watu walio karibu huathiriwaje?
Madaktari bado hawajadai kuwa na uelewevu kamili wa njia zote ambazo mafua yaweza kuenezwa. Hata hivyo, dokezo moja thabiti ni kwamba mtu aweza kupata mafua kwa kupumua viini vibaya ambavyo vimenyunyizwa hewani na chafya. Hasa jambo hili lawezekana katika msongamano wa chumba chenye ujoto, au gari-moshi au basi lililosongamana ambamo hewa safi huwa kidogo. Magonjwa mengine, kutia na influenza, surua, machubwichubwi, mchochota wa pafu (kichomi), kifua kifuu, na kifaduro huaminiwa kuwa huenezwa na kupiga chafya.
Utafiti fulani juu ya mwendo wa kurusha chafya nje wafunua kwamba vijitone vya umajimaji ulio na viini vibaya huondoshwa puani na kinywani kwa mwendo wa zaidi ya kilometa 160 kwa saa na waweza kushikana na nyuso za vitu vilivyo umbali wa karibu futi 12. Vijitone vingine huelea hewani kwa muda ili vivutwe na wapitaji wasio na hatia.
Je! Chafya Yaweza Kukandamizwa?
Njia nyingi zimejaribiwa kwa mafanikio ya kadiri mbalimbali. Watu fulani hudai kuwa walikwisha kuzuia au kupunguza “mlipuko” wa chafya kwa kufinya kidole sana kwenye mdomo wa juu chini kidogo tu ya pua. Kufinya sana hapo husemwa kuwa hufunga baadhi ya mishipa ya fahamu ihusikayo katika ile kawaida au taratibu ya kupiga chafya. Njia nyingine yaweza kuwa kupenga pua yako kwenye kitambaa wakati ule ule uhisipo chafya ikija.
Kwa chafya ya muda mrefu au ya kudumu, nyakati fulani dawa za kuvuta puani hutoa kitulizo, hata ikiwa ni mvuke wa maji moto tu wenye kuvutwa hivyo. Hii ingeweza kueleza ni kwa nini wauguaji wengi wa mafua-nyasi-kavu hupata kitulizo cha muda wanapokuwa wakioga kwa maji moto ya mnyunyizo au ndani ya hodhi katika chumba chenye kujaa mvuke.
Mbinu na njia mbalimbali zimedokezwa muda wa miaka iliyopita, baadhi yazo zikiwa za kueleweka, nyingine zikiwa za kiupuuzi. Krimu za kuingizwa kwa mrija ndani ya pua zimejaribiwa zikawa na mafanikio fulani. Nyingine ni pamoja na vitulizo, kudungwa sindano, kutia matone, vibonge, majimaji ya kunywa, utibabu wa kutuliza fikira, kuchoma tando za pua, na kunusa kitunguu saumu au mmea aina ya mronge. Madokezo yaliyo ya kiupuuzi zaidi ni kuanzia kuweka pini ya nguo puani hadi mtu kusimama kwa kichwa chake, kukariri herufi za alfabeti kinyumenyume, au kusugua uso kwa mafuta ya nguruwe.
Tahadhari: Si wazo zuri sikuzote kukandamiza au kufungia chafya. Kuizuilia kwa lazima chafya yenye kutoka kwa nguvu kumejulikana kuwa husababisha mitoko ya damu puani na huenda kukapandisha viini vibaya vyenye kuwasha viingie ndani ya mapango ya pua, na hiyo ingeweza kusababisha ambukizo lienee. Katika pindi chache, mifupa ndani na kuzunguka pua imevunjika, na mfupa mmoja katika sikio la kati ukateguka.
“Ubarikiwe!”
Katika mabara mengi ni desturi ya wenye kusimama karibu kumwambia “ubarikiwe” mtu mwenye kupiga chafya. Desturi hiyo ilianzia wapi?
Kulingana na kitabu How Did It Begin? na R. Brasch, wakale fulani waliamini kwamba binadamu alipopiga chafya, alikuwa karibu na kifo. Brasch aongezea hivi: “Hofu hiyo ilikuwa na msingi wa wazo lenye makosa lakini lenye kushikiliwa mahali pengi. Nafsi ya binadamu ilionwa kuwa ndiyo kiini cha uhai. Uhakika wa kwamba wanadamu wafu hawakupumua kamwe ulifanya shauri likatwe kimakosa kwamba ni lazima nafsi yake iwe ni pumzi. . . . Hivyo haishangazi kwamba kuanzia siku za mapema kabisa watu walijifunza kuwa na wasiwasi juu ya chafya na kumtakia sana mpiga chafya kwamba Mungu amsaidie na kumbariki na kuhifadhi uhai wake. Kwa njia fulani katika nyakati za katikati asili hii ya mapema ya desturi hiyo ni lazima iwe ilisahauliwa kwa sababu Papa Gregori Mkubwa ndiye aliyesifiwa kuwa mwanzishi wa usemi ‘Ubarikiwe na Mungu,’ kwa mtu yeyote aliyepiga chafya.”
Tafadhali Kumbuka Kitambaa Chako
Huenda ikakushangaza kujua kwamba kupiga chafya kumetumiwa kwa uhalifu. Ndiyo, wavunja sheria wametunga njia za kutumia, au kutumia vibaya, upigaji chafya kwa makusudi maovu. Karibu miaka mia moja iliyopita, wezi fulani katika Uingereza walikuja kuitwa waoteaji-wa-chafya. Walikuwa wakitupa ugoro (tumbako) katika uso wa mtu wasiyemjua. Halafu, alipokuwa amegekengeushwa fikira na mshiko wa kupiga-piga chafya kwa nguvu, wezi hao walikuwa wakimnyang’anya vithaminiwa vyake.
Walio wengi kati yetu hawatapiga chafya kamwe kwa kujazwa ugoro usoni. Lakini awe amepatwa na chafya ya ghafula au mtokeo wa chafya ya mfululizo, mtu mwenye kufikiri atatumia kitambaa sikuzote au karatasi nzito ili kufunika pua na kinywa chake. Si kwamba tu huu ni wonyesho wa adabu bali pia ni tahadhari ya kutumia akili. Husaidia kulinda dhidi ya kunyunyizia hewa vijitone vilivyojaa viini vibaya vikingoja tu kuvutwa na mtu yule mwingine mwenye kuja hapo bila kuwa na habari. Kupenda jirani pia kungetulazimisha tujaribu kulinda wengine na magonjwa kwa kufanya kila tuwezalo tupunguze mweneo wa viini vibaya.
Huenda lisiwe jambo la hekima au isiwezekane kukandamiza chafya. Lakini wengine watathamini kama nini ufikirio wako—na utumizi wako wa kitambaa—ili uikamate chafya!