Ushirikina Umeenea Kadiri Gani Leo?
UKO kila mahali—kazini, shuleni, katika magari ya abiria, na barabarani. Unapopiga chafya, watu usiowajua, wapita-njia, husema: “Mungu akubariki” au “Ubarikiwe.” Lugha nyingi zina semi sawa na hizo. Katika Kijerumani itikio ni “Gesundheit.” Waarabu husema “Yarhamak Allah,” na Wapolinesia wa Kusini ya Pasifiki husema “Tihei mauri ora.”
Huenda hukufikiri sana sababu inayowafanya watu waseme hivyo, na huenda ulidhani ni hisani tu ya kawaida inayotegemea adabu ya mahusiano. Hata hivyo, chimbuko la usemi huo ni ushirikina. Moira Smith, mkutubi katika Folklore Institute katika Chuo Kikuu cha Indiana huko Bloomington, Indiana, Marekani, asema hivi juu ya usemi huo: “Unatokana na wazo la kwamba unapiga chafya nafsi yako.” Kusema “Mungu akubariki” kwa kweli, ni kumuomba Mungu airejeshe.
Bila shaka, huenda watu wengi wakakubali kwamba si jambo la kiakili kuamini kuwa nafsi hutoka mwilini unapopiga chafya. Kwa hiyo, si ajabu kwamba, Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary hufasili ushirikina kuwa “itikadi au zoea linalotokana na kutojua, hofu ya mambo yasiyojulikana, kutumaini mizungu au nasibu, au maoni bandia juu ya kisababishi.”
Haishangazi kwamba mwanafizikia mmoja wa karne ya 17 aliuita ushirikina uliokuwapo katika siku zake kuwa “makosa ya watu wa kawaida” wasioelimika. Hivyo, wanadamu walipoingia katika karne ya 20 huku wakiwa wametimiza mengi kisayansi, The Encyclopædia Britannica cha 1910 kilitabiri kwa matumaini kwamba wakati ungewadia ambapo “ustaarabu [haungekuwa] na ushirikina wa aina yoyote.”
Umeenea Kuliko Wakati Mwingineo Wote
Matumaini hayo yaliyodumu kwa miongo minane hivi hayakuwa na msingi, kwani yaonekana kwamba ushirikina umeimarika zaidi kuliko wakati mwingineo wote. Ushirikina umedumu kwa muda mrefu. Neno “superstition” [ushirikina] latokana na neno la Kilatini “super,” linalomaanisha “kupita,” na “stare,” “kudumu.” Kwa kweli, mashujaa waliookoka vitani waliitwa, “superstites,” kwa kuwa waliishi muda mrefu zaidi ya askari wengine vitani, kwa njia halisi “walidumu” kuwapita. Kinapozungumzia ufafanuzi huu, kitabu Superstitions chataarifu hivi: “Ushirikina ambao ungali upo leo umedumu licha ya jitihada za enzi nyingi za kuukomesha.” Fikiria mifano michache tu ya ushirikina uliopo.
◻ Baada ya kifo cha ghafula cha gavana wa jiji moja mashuhuri huko Asia, wafanyakazi waliovunjika moyo wa makao yake walimshauri gavana mpya awasiliane na mtaalamu wa maono, mtaalamu huyo alidokeza mabadiliko kadhaa yaliyohitaji kufanywa ndani na nje ya makao hayo. Wafanyakazi hao walifikiri kwamba mabadiliko hayo yangeondoa ndege mbaya.
◻ Msimamizi wa kampuni moja yenye ufanisi huko Marekani hubeba daima jiwe fulani la pekee. Yeye hulibeba popote aendapo, tangu alipofanikiwa katika maonyesho ya kibiashara kwa mara ya kwanza.
◻ Kwa kawaida mameneja wa kibiashara huko Asia hutafuta ushauri wa mtabiri, kabla ya kukamilisha mapatano muhimu ya kibiashara.
◻ Mwanariadha ajapofanya mazoezi ya kutosha, anategemea kwamba nguo fulani itamwezesha kushinda. Kwa hivyo, anaendelea kuivaa—bila kuifua—katika mashindano ya wakati ujao.
◻ Mwanafunzi anatumia kalamu fulani hususa wakati wa mtihani kisha anapata maksi za juu. Tangu hapo, anaiona kalamu hiyo kuwa yenye “bahati.”
◻ Wakati wa arusi yake, bibi-arusi fulani huchagua mavazi yake kwa njia ya kwamba yanatia ndani “kitu fulani cha kale, kitu fulani kipya, kitu fulani kilichoazimwa, na kitu fulani cha buluu.”
◻ Mtu fulani hufungua Biblia bila kufikiri na kusoma andiko analoona kwanza, akiamini kwamba maneno hayo yataandaa mwongozo anaohitaji wakati huo.
◻ Ndege aina ya jumbo jeti iendapo kwa kasi kwenye barabara ya ndege ili iweze kupaa, abiria kadhaa wanafanya ishara ya msalaba. Abiria mwingine anapapasa-papasa sanamu ya “Mtakatifu” Christopher wakati wa safari.
Ni dhahiri kwamba hata leo ushirikina umeenea sana. Kwa kweli, Stuart A. Vyse, profesa mwandamizi wa saikolojia katika Connecticut College, ataarifu hivi katika kitabu chake Believing in Magic—The Psychology of Superstition: “Ingawa tunaishi katika jamii iliyoendelea kitekinolojia, ushirikina umeendelea kuenea.”
Ushirikina umeimarika sana leo hivi kwamba jitihada za kuukomesha hazijafua dafu. Mbona iko hivyo?