Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 7/8 kur. 3-7
  • Kuuza Damu ni Biashara Kubwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuuza Damu ni Biashara Kubwa
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi Damu Ilivyobaki Ikiwa Yenye Faida
  • Faida Katika Eneo Lisilo la Faida
  • Soko la Tufe Lote
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Kutia Damu Mishipani—Je, Kutaendelea?
    Amkeni!—2006
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Damu
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 7/8 kur. 3-7

Kuuza Damu ni Biashara Kubwa

DHAHABU NYEKUNDU! Kama vile jina hilo la kubandika lidokezavyo, hiki ni kitu kimoja chenye kuthaminiwa sana. Ni umajimaji wenye bei, mali asili iliyo ya maana sana ambayo imelinganishwa si na dhahabu tu bali pia na mafuta na makaa-mawe. Hata hivyo, dhahabu nyekundu haichimbwi katika mishipa iliyo katika miamba kwa keekee na baruti. Huchimbwa katika mishipa ya watu kwa njia ya werevu zaidi.

“Tafadhali, msichana wangu mdogo ahitaji damu,” lasihi tangazo kubwa sana juu ya barabara kuu yenye pirikapirika katika Jiji la New York. Matangazo mengine yahimiza hivi: “Ikiwa wewe ni mchangaji, wewe ndiwe namna ya mtu ambaye ulimwengu huu hauwezi kuishi bila yeye.” “Damu yako ni ya maana. Saidia.”

Watu watakao kusaidia wengine kwa wazi huuelewa ujumbe huo. Wao hujipanga makundi makundi, ulimwenguni pote. Bila shaka walio wengi kati yao, na pia watu wanaokusanya damu na watu wenye kutia damu hiyo mishipani, wataka kwa moyo mweupe kuwasaidia wenye masumbufu na huamini kwamba wanafanya hivyo.

Lakini baada ya damu kuchangwa na kabla haijatiwa mishipani, hupita katika mikono zaidi na kufanyiwa taratibu zaidi kuliko vile walio wengi kati yetu wang’amua. Kama dhahabu, damu huchochea pupa. Huenda ikauzwa kwa faida halafu iuzwe upya kwa faida kubwa zaidi. Watu fulani hupigania haki za kukusanya damu, huiuza kwa bei za juu sana, hupata pesa nyingi kutokana nayo, na hata huifanyia ulanguzi haramu kutoka nchi moja hadi nyingine. Kotekote ulimwenguni, kuuza damu ni biashara kubwa.

Katika United States, wakati mmoja wachangaji walilipwa papo hapo kwa damu yao. Lakini katika 1971 mtungaji Mwingereza Richard Titmuss alidai kwamba kwa kushawishi maskini na wagonjwa jinsi hiyo ili wachange damu kwa ajili ya dola chache, mfumo wa Kiamerika ulikuwa bila usalama. Pia alitoa hoja ya kwamba lilikuwa jambo la ukosefu wa adili kwa watu kufaidika kutokana na kutoa damu yao ili kusaidia wengine. Shambulio lake liliharakisha kukomeshwa kwa malipo ya wachangaji wa damu nzima-nzima katika United States (ingawa bado mfumo huo wasitawi katika mabara fulani). Hata hivyo, hiyo haikufanya soko la damu lipungukiwe na faida. Kwa nini?

Jinsi Damu Ilivyobaki Ikiwa Yenye Faida

Katika miaka ya 1940, wanasayansi walianza kutenganisha damu kuwa katika vile visehemu mbalimbali viifanyizavyo. Utaratibu huo, ambao sasa waitwa ugawegawe, hufanya damu iwe biashara yenye kuleta pesa nyingi hata zaidi. Jinsi gani? Basi, fikiria: Gari la muundo wa karibuni likitengwa vipande vipande huenda likapanda bei mara tano kuliko likiwa lote pamoja. Vivyo hivyo, damu ina bei kubwa zaidi igawanywapo kisha visehemu vyayo kuuzwa vikiwa kandokando.

Plasma, ambayo ni karibu nusu ya mweneo jumla wa damu, ni kisehemu cha damu chenye faida sana kifedha. Kwa kuwa plasma haina yoyote ya zile sehemu zenye chembe za damu—chembe nyekundu, chembe nyeupe, na visahani—yaweza kukaushwa na kuwekwa akibani. Zaidi ya hilo, mchangaji huruhusiwa kutoa damu nzima-nzima mara tano tu kwa mwaka, lakini aweza kutoa plasma kufikia mara mbili kwa juma kwa kufanyiwa utenganisho-plasma. Katika utaratibu huu, damu nzima-nzima hutolewa, plasma ikatengwa, halafu vile visehemu vyenye chembe hutiwa tena katika mishipa ya mchangaji.

United States bado huruhusu wachangaji walipwe kwa ajili ya plasma yao. Tena, nchi hiyo huruhusu wachangaji watoe kiasi cha karibu mara nne zaidi cha plasma kila mwaka kuliko vile Shirika la Afya Ulimwenguni lipendekezavyo! Basi, si ajabu kwamba United States hukusanya zaidi ya asilimia 60 ya ugavi wa plasma ya ulimwengu. Plasma yote hiyo yenyewe ina thamani ya karibu dola milioni 450, lakini huleta nyingi zaidi sokoni kwa sababu plasma yaweza kutenganishwa pia iwe visehemu mbalimbali. Ulimwenguni pote, plasma hutumiwa kuwa msingi wa biashara ya dola 2,000,000,000 kwa mwaka!

Japani, kulingana na gazeti Mainichi Shimbun, hula karibu theluthi moja ya plasma ya ulimwengu. Nchi hiyo huingiza asilimia 96 ya kifanyizo hiki cha damu kutoka nchi za nje, sehemu kubwa zaidi ikiwa ni kutoka United States. Wachambuzi walio ndani ya Japani wameiita nchi hiyo “popo mfyonza damu ulimwenguni,” na Wizara ya Afya na Masilahi ya Wajapani imejaribu kuibana biashara hiyo, ikisema kwamba si jambo la akili kufaidika kutokana na damu. Kwa uhakika, Wizara hiyo yadai kwamba mashirika ya kitiba katika Japani hupata faida za dola 200,000,000 kila mwaka kutokana na kifanyizo kimoja tu cha plasma, albumini.

Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani hutumia vitu vingi zaidi vyenye kufanyizwa na damu kuliko sehemu nyingine yote ya Ulaya ikiwekwa pamoja, kiasi kingi zaidi kwa mtu mmoja kuliko nchi yoyote ulimwenguni. Kitabu Zum Beispiel Blut (Mathalani, Damu) chasema hivi juu ya vitu vyenye kufanyizwa kwa damu: “Zaidi ya nusu huingizwa kutoka nchi za nje, sana-sana kutoka U.S.A., lakini pia kutoka Ulimwengu wa Tatu. Vyovyote vile hiyo hutoka kwa maskini, ambao wataka kuleta nafuu ya mapato yao kwa kuchanga plasma.” Baadhi ya maskini hawa huuza kiasi kingi sana cha damu yao hata wakafa kutokana na upotevu wa damu.

Vitovu vingi vya biashara ya plasma vimewekwa kwa maarifa katika maeneo yenye mapato ya chini au kando ya mipaka ya nchi zilizo maskini zaidi. Wao huwavuta maskini na mahohehahe, ambao huwa kabisa na nia ya kubadilishana plasma kwa pesa na huwa na sababu ya kutosha kutoa kiasi kingi kuliko iwapasavyo au kuficha magonjwa yoyote ambayo yangeweza kuwa ndani yao. Uchuuzi huo wa plasma umetokea katika nchi 25 kuzunguka ulimwengu. Mara tu ukikomeshwa katika nchi moja, hutokea katika nyingine. Kuhonga maofisa na ulanguzi haramu si jambo lisilo la kawaida.

Faida Katika Eneo Lisilo la Faida

Lakini benki za damu zisizotafuta faida pia zimekuja chini ya uchambuzi mkali hivi majuzi. Katika 1986 mwandishi wa habari Andrea Rock alidai katika gazeti Money kwamba yuniti moja ya damu hugharimu benki za ulimwengu dola 57.50 kuikusanya kutoka kwa wachangaji, kwamba huzigharimu hospitali dola 88.00 kuinunua kutoka benki za ulimwengu, na kwamba hugharimu wagonjwa kuanzia dola 375 hadi dola 600 kuipokea katika utiaji wa mishipani.

Je! hali imebadilika tangu wakati huo? Katika Septemba 1989 mwandishi wa habari Gilbert M. Gaul wa The Philadelphia Inquirer aliandika mfululizo wa makala za gazeti juu ya mfumo wa kuweka damu benki katika United States.a Baada ya uchunguzi wa mwaka mmoja, alitoa habari kwamba benki fulani za damu huomba watu wachange damu halafu hugeuka na kuuza hata kufikia nusu ya damu hiyo kwa vitovu vingine vya damu, kwa faida kubwa. Gaul alikadiria kwamba benki za ulimwengu hufanya biashara ya karibu painti milioni moja za damu kila mwaka kwa njia hiyo, katika soko la kichinichini lenye kuleta dola 50,000,000 kwa mwaka ambalo kwa njia fulani hufanya kazi kama shughuli ya kuuziana umiliki wa mali na hisa.

Ingawa hivyo, pana tofauti kubwa: Badilishano hili la damu halielekezwi na serikali. Hakuna mtu awezaye kupima ni la kadiri gani hasa, achia mbali kurekebi bei zalo. Na wachangaji wengi wa damu hawajui lolote juu yalo. “Watu wanapumbazwa,” mwanabenki mmoja aliyestaafu aliambia The Philadelphia Inquirer. “Hakuna mtu anayewaambia kwamba damu yao inatuendea sisi. Wangewaka kasirani kama wangejua juu ya hilo.” Ofisa mmoja wa Msalaba Mwekundu alieleza hilo kwa uwazi mfupi hivi: “Wanabenki wa damu wamepumbaza umma wa Waamerika kwa muda wa miaka.”

Katika United States pekee, benki za damu hukusanya lita kama milioni 6.5 za damu kila mwaka, nazo huuza zaidi ya yuniti milioni 30 za vitu vifanyizwavyo kutokana na damu kwa dola karibu milioni elfu moja. Hiki ni kiasi kikubwa ajabu cha pesa. Benki za damu hazitumii neno “faida.” Hizo hupendelea kifungu cha kwamba ni “mazidio juu ya gharama.” Mathalani, shirika la Msalaba Mwekundu lilipata dola milioni 300 katika “mazidio juu ya gharama” kuanzia 1980 hadi 1987.

Benki za damu zateta kwamba hizo ni mashirika yasiyotafuta faida. Zadai kwamba tofauti na mashirika makubwa katika Wall Street, pesa zao haziendei wawekaji wa pesa za mtaji. Lakini kama shirika la Msalaba Mwekundu lingekuwa na watu wenye hisa humo, lingehesabiwa miongoni mwa mashirika yenye kufaidika zaidi katika United States, kama vile General Motors. Na maofisa wa benki za damu wana mishahara mizuri. Kati ya maofisa katika benki 62 za damu ambazo zilichunguzwa na The Philadelphia Inquirer, asilimia 25 walipata faida ya dola zaidi ya 100,000 kwa mwaka. Wengine walipata faida ya zaidi ya mara mbili za kiasi hicho.

Wanabenki wa damu pia hudai kwamba wao ‘hawauzi’ damu wakusanyayo—wao hutoza pesa za hatua za kuitayarisha tu. Mwanabenki mmoja wa damu ajibu dai hilo kwa ukali hivi: “Mimi hujisikia vibaya sana shirika la Msalaba Mwekundu lisemapo kwamba haliuzi damu. Hiyo ni kama vile supa-duka kusema wanakutoza pesa za katoni tu, si za maziwa.”

Soko la Tufe Lote

Kama biashara ya plasma, biashara ya damu nzima-nzima yazunguka tufe lote. Ndivyo na uchambuzi wayo. Mathalani, shirika la Kijapani la Msalaba Mwekundu liliamsha fujo katika Oktoba 1989 lilipojaribu kutumia kifua kuingia katika soko la Kijapani kwa kutolea mapunguzio makubwa juu ya vitu vilivyotolewa kutokana na damu iliyochangwa. Hospitali zilivuna faida kubwa sana kwa kudai katika fomu zazo za bima kwamba zilikuwa zimenunua damu kwa bei za kikanuni.

Kulingana na gazeti la Thailand The Nation, nchi fulani za Kiesia zimelazimika kulibana soko la kuuza hiyo dhahabu nyekundu kwa kukomesha michango ya kulipwa. Katika India watu kufikia 500,000 huuza damu yao wenyewe wajipatie riziki. Watu fulani, wakiwa maskini fakiri walio hoi, husingizia sura zao ili waweze kuchanga kiasi kingi kuliko kile kiruhusiwacho. Wengine hukamwa kimakusudi damu nyingi kupita kiasi na benki za damu.

Katika kitabu chake Blood: Gift or Merchandise, Piet J. Hagen adai kwamba vitendo vya kichinichini vya benki za damu ni vibaya zaidi katika Brazili. Mamia ya benki za ubiashara wa damu katika Brazili huendesha soko la dola milioni 70 ambalo huwavuta wasiotia shaka. Kulingana na kitabu Bluternte (Mavuno ya Damu), maskini na wasioajiriwa humiminikia zile benki nyingi sana katika Bogotá, Colombia. Wao huuza nusu-lita ya damu yao kwa peso chache sana za kuanzia 350 hadi 500. Huenda wagonjwa wakalipa kuanzia peso 4,000 hadi 6,000 kwa ajili ya nusu-lita hiyo hiyo ya damu!

Kwa wazi, angalau jambo moja halisi linalohusu tufe lote laonekana wazi kutokana na yaliyotangulia: Kuuza damu ni biashara kubwa. ‘Halafu? Kwa nini damu isiwe biashara kubwa?’ huenda watu fulani wakauliza.

Basi, ni nini hufanya watu wengi wawe na wasiwasi juu ya biashara kubwa kwa ujumla? Ni pupa. Kwa kielelezo, pupa hiyo huonekana wakati biashara kubwa ivutapo watu kuwasadikisha wanunue vitu wasivyovihitaji kikweli; au kwa ubaya zaidi, wakati iendeleapo kudanganya umma wakubali bidhaa fulani zijulikanazo kuwa hatari, au ikataapo kutumia pesa kufanya bidhaa zayo ziwe salama zaidi.

Ikiwa biashara ya damu ina madoa ya aina hiyo ya pupa, uhai wa mamilioni ya watu kotekote ulimwenguni umo hatarini. Je! pupa imefisidi biashara ya damu?

[Maelezo ya Chini]

a Katika Aprili 1990, habari zilizofichuliwa na Gaul ziliishindia Huduma ya Umma Zawadi ya Pulitzer. Pia zilifyatusha uchunguzi mkubwa wa kongresi katika biashara ya damu mwishoni mwa 1989.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]

Uchuuzi wa Plasenta (Kondo la Nyuma)

Labda ni wanawake wachache sana ambao wamezaa sasa hivi hujiuliza ni jambo gani hutendeka kwa plasenta, lile tungamo la tishu ambalo hulisha mtoto angali katika tumbo la uzazi. Kulingana na The Philadelphia Inquirer, hospitali nyingi hulihifadhi, huligandisha kwa barafu, na kuliuza. Katika 1987 tu, United States ilisafirisha kama kilo milioni 0.8 za plasenta kuzipeleka ng’ambo. Shirika moja karibu na Paris, Ufaransa, hununua tani 15 za plasenta kila siku! Plasenta hizo huwa ni chanzo tayari cha plasma ya damu ya umama, ambayo shirika hilo hufanyiza kuwa dawa mbalimbali na kuziuza katika nchi zapata mia moja.

[Grafu/Picha katika ukurasa wa 4]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Viasili Vikuu vya Damu

Plasma: karibu asilimia 55 ya damu. Ni maji kwa asilimia 92; sehemu ile nyingine ni mjumliko wa protini tata, kama vile globulini, faibrinojeni, na albumini

Visahani: karibu asilimia 0.17 ya damu

Chembe Nyeupe: karibu asilimia 0.1

Chembe Nyekundu: karibu asilimia 45

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki