Zawadi ya Uhai au Busu la Kifo?
“Ni watu wangapi ambao ni lazima wafe? Ni vifo vingapi ambavyo mwahitaji? Tupeni ukingo wa kifo ambao nyinyi mwauhitaji ili mwamini kwamba jambo hili linatendeka.”
DON FRANCIS, ofisa mmoja wa CDC (Vitovu vya United States vya Kudhibiti Magonjwa), aligongesha ngumi mezani alipokuwa akipaaza maneno yaliyo juu kwenye mkutano pamoja na wawakilishi wakuu wa biashara ya benki ya damu. CDC ilikuwa ikijaribu kusadikisha wanabenki wa damu kwamba UKIMWI ulikuwa ukienea kupitia ugavi wa damu wa taifa.
Wanabenki wa damu hawakusadiki. Waliuita ushuhuda huo kuwa usiotosha—konzi moja tu la visa—nao wakaamua kutokuongeza jitihada ya kuchunguza damu au kuipima kwa uangalifu. Hiyo ilikuwa katika Januari 4, 1983. Miezi sita baadaye, rais wa Shirika la Kiamerika la Benki za Damu alishikilia hivi: “Kuna hatari kidogo tu au hata hakuna yoyote kwa umma kwa ujumla.”
Kwa wastadi wengi, tayari kulikuwa na ushuhuda wa kutosha wa kuhitaji kuchukua hatua fulani. Na tangu wakati huo, hilo “konzi moja tu la visa” limeongezeka ajabu. Kabla ya 1985, labda ni watu 24,000 waliotiwa mishipani damu yenye kiini kibaya cha HIV (Vairasi Ipunguzayo Kinga ya Kibinadamu), ambayo husababisha UKIMWI.
Damu iliyotiwa uchafu ni njia ya kuieneza kwa kadiri kubwa ajabu ile vairasi ya UKIMWI. Kulingana na The New England Journal of Medicine (Desemba 14, 1989), yuniti moja ya damu huenda ikabeba vairasi ambayo yatosha kusababisha kufikia maambukizo milioni 1.75! CDC iliambia Amkeni! kwamba kufikia Juni 1990, katika United States pekee, watu 3,506 walikuwa tayari wamepata UKIMWI kutokana na kutiwa damu mishipani, visehemu vya damu, na mipandikizo ya tishu.
Lakini hizo ni hesabu tu. Haziwezi hata kuanza kuonyesha kina cha misiba ya kibinafsi ihusikayo. Mathalani, ufikirie msiba wa Frances Borchelt, mwenye miaka 71. Mwanamke huyo aliwaambia madaktari hakutaka kamwe kamwe kutiwa damu mishipani. Hata hivyo alitiwa damu mishipani. Alikufa kwa maumivu makali kutokana na UKIMWI huku familia yake ikimtazama kihoi.
Au fikiria msiba wa msichana wa miaka 17 ambaye, kwa kuteseka kutokana na mtoko-damu mwingi wa hedhi, alipewa yuniti mbili za damu ili kurekebisha ukosefu wa damu tu. Alipokuwa na miaka 19 na mwenye mimba, aligundua kwamba huko kutiwa damu mishipani kulikuwa kumempa vairasi ya UKIMWI. Akiwa na miaka 22 alilemewa na UKIMWI. Zaidi ya kujua kwamba karibuni angekufa kutokana na UKIMWI, alibaki akijiuliza kama alikuwa amepitishia mtoto wake ugonjwa huo. Orodha ya misiba yasonga mbele zaidi na zaidi, kuanzia kwa watoto hadi kwa wazee-wazee, kotekote ulimwenguni.
Katika 1987 kitabu Autologous and Directed Blood Programs kiliomboleza hivi: “Karibu muda ule tu uliofuata kutoa maelezo ni vikundi gani vya asili vyenye hatari, jambo lisilowazika lilitukia: wonyesho wa kwamba ugonjwa huu uwezao kuua [UKIMWI] ulikuwa ukiambukizwa na ugavi wa damu ya wenye kuitoa kwa hiari. Hilo ndilo lililokuwa chungu zaidi kati ya matokeo yote ya kitiba yasiyokuwa yametazamiwa; kwamba ile zawadi ya damu iliyo ya thamani kubwa kwa kutoa uhai ingeweza kugeuka kuwa chombo cha kuleta kifo.”
Hata dawa zenye kutolewa katika plasma zilisaidia kueneza tauni hii kuzunguka ulimwengu. Wenye damu isiyogandamana, ambao wengi wao hutumia kisaidiaji chenye plasma cha kugandamanisha damu ili kutibu ugonjwa wao, walikufa kwa wingi. Katika United States, kati ya asilimia 60 na 90 kati yao walipata UKIMWI kabla utaratibu haujawekwa wa kuitibu dawa kwa joto ili kuiondolea kiini kibaya cha HIV.
Na bado, hadi leo hii, damu haiko salama kutokana na UKIMWI. Na UKIMWI siyo hatari pekee itokanayo na kutiwa damu mishipani. Ni mbali na hivyo.
Hatari Ambazo Zafanya UKIMWI Uwe Si Kitu
“Ndicho kitu kilicho hatari zaidi ambacho sisi hutumia katika tiba,” asema Dkt. Charles Huggins juu ya damu. Apaswa kujua; yeye ndiye mkurugenzi wa huduma ya kutia damu mishipani kule hospitali ya Massachusetts. Wengi hufikiri kwamba kutia damu mishipani ni jambo sahili kama kupata mtu mwenye namna ya damu inayolingana na ya mwingine. Lakini zaidi ya zile namna za ABO na aina ya Rh ambazo kwa kawaida hufanya damu zipatanishwe, huenda ikawa kuna tofauti nyingine 400 au zaidi ambazo haipatanishwi. Kama vile mpasuaji Denton Cooley wa mishipa ya moyo asemavyo: “Kutia damu mishipani ni kupandikiza kiungo. . . . Mimi nafikiri kuna hali fulani za kutopatana katika karibu visa vyote vya kutia damu mishipani.”
Haishangazi kwamba kutia mishipani kitu chenye kutatanika jinsi hiyo kungeweza “kuvuruga” mfumo wa kukinga mwili na maradhi, kama wazo hilo lilivyowekwa na mpasuaji mmoja. Kwa uhakika, kutia damu mishipani kwaweza kukandamiza kinga ya mwili kwa muda mrefu hata kufikia mwaka mmoja. Kwa watu fulani, hilo ndilo jambo lenye kutisha zaidi juu ya visa vya kutia damu mishipani.
Halafu pia kuna magonjwa yenye kuambukiza. Yana majina ya kigeni, kama vile ugonjwa wa Chaga na vairasi-vimbisha-chembe. Matokeo yaanzia kuwa na homa na baridi kali hadi kifo. Dkt. Joseph Feldschuh wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Cornell asema kwamba kuna nasibu 1 kati ya 10 ya kupata ambukizo la namna fulani kutokana na kutiwa damu mishipani. Ni kama kutumia bastola yenye vijumba kumi vya risasi ili kucheza ule mchezo-nasibu wa Kirusi wa kuonyesha ubingwa kwa kufanya ni kama kwamba unajifyatua bastola kichwani. Uchunguzi wa hivi majuzi pia umeonyesha kwamba visa vya kutia damu mishipani wakati wa kupasua kansa huenda kwa kweli vikaongezea hatari ya kutukia tena kwa kansa.
Si ajabu programu moja ya habari za televisheni ilidai kwamba kutia damu mishipani kungeweza kuwa ndilo pingamizi kubwa zaidi la kupata nafuu baada ya upasuaji. Ugonjwa wa kufura ini huambukiza mamia ya maelfu na kuua wapokeaji wengi zaidi wa damu watiwayo mishipani kuliko vile UKIMWI huambukiza, lakini hilo halitangazwi sana. Hakuna mtu ajuaye vifo ni vingapi, lakini mwanauchumi Ross Eckert asema kwamba huenda vikawa ni sawa na ndege ya DC-10 iliyojaa watu ikianguka kila mwezi.
Hatari na Benki za Damu
Benki za damu zimeitikiaje ufichuzi wa hatari zote hizi katika bidhaa yao? Si vema, wachambuzi wadai. Katika 1988 ile Report of the Presidential Commission on the Human Immunodeficiency Virus Epidemic ilishtaki shughuli hiyo kuwa “yenye ukawivu usio wa lazima” katika kuchukua hatua juu ya tisho la UKIMWI. Benki za damu zilikuwa zimehimizwa kuwavunja moyo washiriki wa vikundi vyenye hatari kubwa visichange damu. Walikuwa wamehimizwa wachunguze damu yenyewe, kuipima kwa uangalifu kuona ishara za kama inatoka kwa wachangaji wenye hatari kubwa. Benki za damu zilikawia. Zilipuuza hatari hizo kuwa ni woga mwingi mno wa bure. Kwa nini?
Katika kitabu chake And the Band Played On, Randy Shilts adai kwamba wanabenki fulani wa damu walipinga uchunguzi zaidi “sana-sana kwa sababu za kifedha. Ingawa kwa kadiri kubwa shughuli ya damu huendeshwa na mashirika yasiyotafuta faida kama vile Msalaba Mwekundu, ilikuwa ya pesa nyingi, ikiwa na mapato ya kila mwaka ya dola milioni elfu moja. Shughuli yao ya kuandaa damu kwa ajili ya visa milioni 3.5 vya kutia damu mishipani ilitishika.”
Zaidi ya hilo, kwa kuwa benki za damu zisizotafuta faida hutegemea sana sana wachangaji wa hiari, zilisita-sita kuudhi yeyote wa hao kwa kutohusisha vikundi fulani vyenye hatari ya juu, wagoni-jinsia-moja hasa. Watetezi wa haki za watu wa jinsia moja wenye kulalana walionya kichinichini kwamba kuwakataza kuchanga damu kungekuwa ni kuvunja haki za kiraia na kungekuwa kama kipindi kingine cha ile fikira iliyotumika katika kambi za mateso.
Kupoteza wachangaji na kuongeza machunguzi mapya kungegharimu pesa nyingi zaidi pia. Katika masika ya 1983, Benki ya Damu ya Chuo Kikuu cha Stanford ikawa ya kwanza kutumia uchunguzi-badala wa damu, jambo ambalo lingeweza kuonyesha kama damu ilitoka kwa wachangaji wenye hatari kubwa ya kuwa na UKIMWI. Wanabenki wengine wa damu walichambua hatua hiyo kuwa njia ya kibiashara ya kuvuta wagonjwa zaidi. Machunguzi huongeza bei. Lakini kama wazo hilo lilivyowekwa na mume na mke wamoja, ambao mtoto wao alitiwa damu mishipani bila wao kujua: “Hakika sisi tungalilipa dola 5 zaidi kwa painti” ili machunguzi hayo yafanywe. Mtoto wao alikufa kwa UKIMWI.
Lile Jambo la Kujihifadhi
Wastadi fulani husema kwamba benki za damu zina uzembe wa kuchukua hatua juu ya hatari zilizo katika damu kwa sababu hazina jibu kwa matokeo ya kutotimiza wajibu wazo zenyewe. Mathalani, kulingana na ile ripoti katika The Philadelphia Inquirer, shirika la FDA (Usimamizi wa Chakula na Dawa za Kulevya Katika United States) lina daraka la kuhakikisha kwamba benki za damu zatimiza kiwango, lakini hilo hutegemea sana hizo benki za damu ili kuweka viwango hivyo. Na baadhi ya maofisa wa FDA hapo kwanza walikuwa viongozi katika ile biashara ya damu. Hivyo, visa vya kukagua-kagua benki za damu kwa kweli vilipungua wakati hatari ya UKIMWI ilipokuwa ikiendelea kuonekana wazi!
Benki za damu za United States zimetetea pia kuandikishwa kwa sheria yenye kuzilinda na mashtaka mahakamani. Katika karibu kila mkoa, sasa sheria yasema kwamba damu ni huduma, si bidhaa. Hiyo yamaanisha kwamba mtu anayeshtaki benki ya damu ni lazima athibitishe kutojali kwa benki—pingamizi gumu la kisheria. Sheria za jinsi hiyo huenda zikafanya benki za damu ziwe salama zaidi kutokana na mashtaka mahakamani, lakini hazifanyi damu iwe salama zaidi kwa wagonjwa.
Kama awazavyo mwanauchumi Ross Eckert, kama benki za damu zingechukuliwa kuwa na wajibu kwa damu zichuuzayo, zingefanya mengi zaidi kuhakikisha ni bora. Mwanabenki wa damu aliyestaafu Aaron Kellner aafikiana na hilo: “Kwa kuchanganya-changanya sheria, damu ikawa huduma. Kila mtu akawa huru kufanya atakavyo, kila mtu yaani, isipokuwa yule mhanga asiye na hatia, yule mgonjwa.” Aongezea hivi: “Sisi tungaliweza kuonyesha angalau ule udhalimu, lakini hatukufanya hivyo. Tulihangaikia hatari yetu wenyewe; lilikuwa wapi hangaiko letu kwa mgonjwa?”
Shauri lenye kukatwa laonekana kuwa lisiloepukika. Biashara ya benki ya damu yapendezwa zaidi na kujilinda kifedha kuliko kulinda watu na hatari za bidhaa yao. ‘Lakini je! hatari zote hizi ni kitu,’ huenda watu fulani wakasababu, ‘ikiwa damu ndio utibabu pekee uwezekanao ili kuokoa uhai? Je! manufaa si nyingi kuliko hatari zilizopo?’ Haya ni maswali mazuri. Visa vyote hivyo vya kutia damu mishipani vina ulazima gani hasa?
[Blabu katika ukurasa wa 9]
Madaktari huchukua hatua kubwa za kujilinda wenyewe na damu ya wagonjwa wao. Lakini je! wagonjwa wamelindwa vya kutosha kutokana na damu yenye kutiwa mishipani?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Je! Damu Iko Salama Kutokana na UKIMWI Leo?
“NI Habari Njema Kweli Kweli Kuhusu Damu,” kikatangaza kichwa kikuu katika Daily News la New York siku ya Oktoba 5, 1989. Makala hiyo iliripoti kwamba nasibu za kupatwa na UKIMWI kutokana na kutiwa damu mishipani ni 1 katika 28,000. Utaratibu wa kuweka vairasi hiyo nje ya ugavi wa damu, ikasema, sasa una matokeo ya asilimia 99.9.
Tazamio kama hilo hilo ni jingi katika biashara ya benki ya damu. ‘Ugavi wa damu ni salama kuliko wakati mwingine wowote,’ wao hudai. Msimamizi wa Shirika la Kiamerika la Benki za Damu alisema kwamba hatari ya kupata UKIMWI kutokana na damu ilikuwa ‘ni kama imekomeshwa.’ Lakini ikiwa damu ni salama, kwa nini mahakama hata madaktari wameigongelea sana vibandiko kama “yenye sumu” na “haiepuki kutokuwa salama”? Kwa nini madaktari fulani hufanya upasuaji wakiwa wamevaa zile zionekanazo kama suti za kusafiria angani, wamejaza vifunika uso na viatu vya kuvuka mahali penye kina, yote hayo ili waepuke mgusano na damu? Kwa nini hospitali nyingi sana huuliza wagonjwa watie ishara fomu ya idhini kuondolea hospitali lawama kwa madhara ya visa vya kutia damu mishipani? Je! kweli damu ni salama kutokana na magonjwa kama vile UKIMWI?
Usalama huo wategemea hatua mbili zitumiwazo kulinda damu: kuwapima kwa uangalifu wachangaji waitoao na kuichunguza damu yenyewe. Machunguzi ya hivi majuzi yameonyesha kwamba zijapofanywa jitihada zote za kuwapima kwa uangalifu wachangaji damu ambao mtindo wa maisha yao huwaweka katika hatari kubwa ya kuwa na UKIMWI, kungali kuna wengine ambao hupita bila kugunduliwa na kipimaji. Wao hutoa majibu yenye makosa kwenye fomu ya maswali nao huchanga damu. Wengine wao hutaka kujua kibusara tu kama wao wenyewe wameambukizwa.
Katika 1985 benki za damu zilianza kuchunguza damu kuona kama ina viua-vijasumu ambavyo mwili hufanyiza ili kupigana na ile vairasi ya UKIMWI. Tatizo la uchunguzi huo ni kwamba mtu aweza kuambukizwa vairasi ya UKIMWI kwa muda fulani kabla hajasitawisha viua-vijasumu vyovyote ambavyo uchunguzi huo ungegundua. Pengo kubwa hili huitwa kipindi cha kuchungulia.
Wazo la kwamba kuna nafasi 1 katika 28,000 za kupata UKIMWI kwa kutiwa damu mishipani latokana na uchunguzi uliochapishwa katika The New England Journal of Medicine. Gazeti hilo la pindi kwa pindi lilikiweka kielekeacho kuwa kipindi cha kuchungulia kuwa cha wastani wa majuma manane. Ingawa hivyo, miezi tu kabla ya hapo, katika Juni 1989, jarida hilo hilo lilichapisha uchunguzi uliokata shauri kwamba kipindi cha kuchungulia chaweza kuwa kirefu zaidi—miaka mitatu au zaidi. Uchunguzi huo wa mapema kidogo ulidokeza kwamba vipindi virefu hivyo vya kuchungulia huenda vikawa ni virefu kuliko ilivyofikiriwa wakati mmoja, na ulidhania kwamba, kwa ubaya zaidi, watu fulani walioambukizwa huenda wasisitawishe kamwe viuavijasumu kwa vairasi hiyo! Hata hivyo, uchunguzi ulio wa matazamio mazuri zaidi haukutendesha kazi mapato haya, ukiyaita “yasiyoeleweka vema.”
Si ajabu Dkt. Cory Ser Vass wa Tume ya Rais juu ya UKIMWI alisema hivi: “Benki za damu zaweza kuendelea kuambia umma kwamba ugavi wa damu ni salama sana, lakini umma hawainunui tena kwa sababu wao wahisi hiyo si kweli.”
[Hisani]
CDC, Atlanta, Ga.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Damu Itiwayo Mishipani, na Kansa
Wanasayansi wanajifunza kwamba damu yenye kutiwa mishipani yaweza kukandamiza mfumo wa kinga ya mwili na kwamba kinga iliyokandamizwa yaweza kuathiri vibaya muda wa kuishi wa wale waliopasuliwa kwa ajili ya kansa. Katika toleo lalo la Februari 15, 1987, jarida Cancer laripoti juu ya uchunguzi mmoja wenye kuarifu uliofanywa katika Uholanzi. “Katika wagonjwa wenye kansa ya utumbo mpana,” jarida hilo likasema, “ilionekana athari kubwa mbaya ya kutiwa damu mishipani kwa tegemeo la kuishi muda mrefu. Katika kikundi hicho kulikuwako idadi ya wenye kuokoka iliyojumlika kwa muda wa miaka mitano kuwa asilimia 48 kwa waliotiwa damu mishipani na asilimia 74 kwa wagonjwa wasiotiwa damu mishipani.”
Matabibu kwenye Chuo Kikuu cha Kalifornia Kusini pia walipata kwamba kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa kansa wengi zaidi hurudiwa na kansa ikiwa walitiwa damu mishipani. Kichapo Annals of Otology, Rhinology & Laryngology, Machi 1989, kiliripoti juu ya uchunguzi uliofuatishwa na matabibu hawa kuhusu wagonjwa mia moja: “Kiasi cha kurudi kwa kansa zote za koromeo kilikuwa asilimia 14 kwa wale wasiopokea damu na asilimia 65 kwa wale waliopokea. Kwa kansa ya umio wa mdomo, kikoromeo, na pua au mianzi ya juu puani, kiasi cha kutokea tena kilikuwa asilimia 31 bila kutiwa damu mishipani na asilimia 71 kwa kutiwa damu mishipani.”
Katika makala yake “Mitio-Damu-Mishipani na Upasuaji wa Kansa,” Dkt. John S. Spratt alimalizia hivi: “Huenda mpasuaji wa kansa akahitaji kuwa mpasuaji asiyetumia damu.”—The American Journal of Surgery, Septemba 1986.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kuna ubishi kwamba damu ni dawa yenye kuokoa uhai, lakini hakuna ubishi kwamba hiyo huua watu