Walipataje Manyoya ya Kupendeza Jinsi Hiyo?
KAMBU KIFUA-BULUU-NYEKUNDU-NYEUPE wanapatikana sana katika Afrika ya kati na ya kusini. Wao hupenda kutua juu ya miti na waya za simu kandokando za njia. Hiyo huwapa mahali pafaapo pa kuchunguza mazingira yao ili wapate wadudu na chakula kingine.
Ukisafiri kupitia Botswana au Zimbabwe, waweza kuona mstari wa manyoya buluu nyangavu wakati mmoja wa ndege hao anapovuka barabara. Wao nyakati nyingine huonyesha manyoya yao yenye rangi maridadi kwa wonyesho wa kupinduka-pinduka hewani. Picha iliyopo hapa kando ya ndege huyo pamoja na picha ndogo inayoshikana nayo ya ubawa wake zaonyesha manyoya ya rangi nyangavu ya Kambu kifua-buluu-nyekundu-nyeupe. Manyoya ya ubawa yana mchanganyiko wa namna nne za rangi ya buluu pamoja na nyeusi na hudhurungi. Lo, hiyo yatofautianaje na kile kifua chekundu, mashavu ya rangi-machungwa, kipaji cheupe cha uso, na utosi wa rangi nyepesi ya kijani kibichi! Hii yatokeza swali la maana: Walipataje manyoya mazuri kama hayo?
Ukitazama miguu ya kambu, utaona kwamba imefunikwa na magamba, si manyoya. Je! manyoya yao yalitokea yenyewe tu kwa nasibu kutoka kwenye magamba ya mnyama mwenye kutambaa, kama vile wanamageuzi hufundisha?
Basi, fikiria kwamba nyoya ni kazi ya ufundi wa kustaajabisha. Safu za mishale hutawanyika kutoka kwenye uti wa nyoya. “Iwapo mishale miwili inayoshikana itaachana—na nguvu nyingi zahitajiwa ili kuutenganisha ubapa wa manyoya—inaunganishwa mara moja tena kama kwamba kwa zipu kwa kulipitisha nyoya katika ncha za vidole,” chaeleza kitabu cha masomo ya sayansi Integrated Principles of Zoology. “Bila shaka, ndege huyo hufanya hivyo kwa mdomo wake.”
Je! mamia ya “zipu” hizo zenye kufanya kazi vizuri sana zinazojumlika kuwa nyoya moja yangeweza kuwa yalitokea kwa nasibu? Je! wanasayansi wana uthibitisho hata mmoja kwamba kwa kweli gamba moja ndilo lililogeuka kuwa nyoya? “Kwa kushangaza,” kinakiri kitabu kilichonukuliwa hapo juu, “ingawa ndege wa kisasa wana magamba (hasa katika miguu yao) na manyoya pia, hakuna hatua yoyote ya katikati ambayo imegunduliwa katika visukuku [masalio ya zamani] au namna zenye uhai.”
Kwa hakika, manyoya humtolea ushuhuda Fundi Stadi ambaye pia ni mstadi wa kuchangamanisha rangi zenye uzuri. Viumbe kama kambu kifua-buluu-nyekundu-nyeupe wanatiwa kati ya “ndege wenye mbawa” ambao “wa[na]lisifu jina la BWANA [Yehova, NW],” Mungu wa kweli.—Zaburi 148:7, 10-13.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
National Parks Board of South Africa