Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 10/22 kur. 14-15
  • Korongo Wenye Taji—Wachezaji-Dansi Wenye Kishungi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Korongo Wenye Taji—Wachezaji-Dansi Wenye Kishungi
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Utunzaji wa Wazazi
  • Baleti ya Ndege
  • Pigano Ili Kuokoka
  • Kucheza Dansi Pamoja na Korongo
    Amkeni!—2003
  • Manyoya—Ubuni wa Ajabu
    Amkeni!—2007
  • Walipataje Manyoya ya Kupendeza Jinsi Hiyo?
    Amkeni!—1991
  • Je, Wanataka Tu Kujirembesha?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 10/22 kur. 14-15

Korongo Wenye Taji—Wachezaji-Dansi Wenye Kishungi

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA

KORONGO mwenye taji ni mmoja kati ya ndege warembo zaidi ulimwenguni. Ni ndege mwenye madaha aliye na rangi zenye kupendeza na umbo zuri sana. Akiwa na kimo cha zaidi ya meta moja, ana mabawa mapana na shingo refu nyepesi, ambayo ni kawaida kwa aina nyinginezo za korongo.

Korongo wenye taji wa kiume na wa kike wafanana. Manyoya yake ya nyuma yenye utusitusi hufunika kwa kupendeza manyoya ya mabawa yaliyo meupe pepepe ambayo yameteremka katika pande zote mbili za ndege huyu na hubadilika kuwa rangi ya dhahabu karibu na mkia. Manyoya mengine ya mabawa yana rangi ya kahawia.

Uso wa korongo mwenye taji wapendeza sana. Mashavu yake yana rangi ya pembe ya tembo na yamezungukwa na manyoya ya kichwani yaliyo mororo kabisa kwenye taji na koo. Macho yake ni buluu maridadi. Kutoka kwenye manyoya meusi ya shingo kwaning’inia ndevu nyekundu nyangavu, ambayo huning’inia kama ushanga mwekundu-mwangavu korongo anyooshapo shingo lake mbele. Yenye kuvutia zaidi ya yote ni manyoya ya kichwani yaliyo membamba na yenye rangi ya dhahabu yafanyizayo taji linalolingana lenye fahari. Manyoya haya mangavu, membamba huonekana kama dhahabu yanapomulikwa na miali ya jua. Rangi hizi zote zenye kuvutia na zilizo tofauti-tofauti zasawazika juu ya miguu miwili mirefu, myembamba iliyo myeusi.

Mlio wa korongo mwenye taji ulio kama tarumbeta ni mmoja wa sauti zisizosahaulika za Afrika: O-wahng! O-wahng! O-wahng! Mlio huu mkubwa waweza kusikika kwa mbali sana. Kwa kawaida korongo wenye taji wawili hulia pamoja warukapo kutoka au kuelekea kwenye miti yenye kiota chao. Nyakati fulani mwakani, korongo wenye taji hukusanyika nao waweza kufika ndege 30, wakitoa mchanganyiko wa sauti wenye kupendeza kusikiza.

Utunzaji wa Wazazi

Yaonekana kwamba korongo wenye taji huwa waaminifu kwa wenzi wao. Wanapatikana katika sehemu nyingi za Afrika Mashariki, hasa katika kinamasi na mabwawa, ambapo wao hutengeneza viota na kulea watoto wao. Kiota ni rundo la nyasi na tete zilizowekwa katika muundo wa pia ambazo hutokeza jukwaa ambalo juu yake yule wa kike hutaga mayai makubwa mawili au matatu yenye rangi ya buluu ya kijani. Wote wawili wa kiume na wa kike huchukua zamu ya kuatamia mayai, na kwa muda wa mwezi mmoja vifaranga huanguliwa. Wazazi wote wawili hufanya kazi pamoja kuwatunza wachanga wao wororo, na watawakinga watoto wao bila woga.

Mlo mkuu wa korongo mwenye taji wahusisha wadudu, vyura, nyoka wadogo, na mbegu. Wakitumia miguu yao mirefu ionekanayo kuwa dhaifu na nyayo zao kubwa, wao hugonga ardhi kwa nguvu, wakila upesi viumbe wadogo-wadogo wowote ambao wanatoa katika nyasi.

Baleti ya Ndege

Korongo wenye taji ni wachezaji-dansi wenye shauku na wenye kutumbuiza. Wakipigapiga mabawa yao makubwa yenye rangi nzuri, wao hujiinua angani wakiwa wima na kisha wanaelea kwa wanana kurudi kwenye ardhi kana kwamba wameunganishwa na mwavuli. Wakiruka huku na huku kwa madaha, wao hukimbia na kuruka hewani, wakiwazunguka wenzi wao na kuinua na kuinamisha vichwa vyao kwa haraka kama mcheshi. Wakiwa wamefungua mabawa yao makubwa, wao husimama wima na kuonyesha rangi maridadi ya manyoya ya mabawa yao.

Wakati mwingine korongo wawili watapinda shingo zao kwa namna yenye madaha na kuangaliana ana kwa ana. Midomo ikiwa imeangaliana, wao hutamka mfululizo wa sauti za chini, wakitoa sauti nzito kana kwamba wanaimbiana. Wakisimama wima tena, wanarudia tena baleti yao ya ndege yenye kupangwa kwa uangalifu sana.

Pigano Ili Kuokoka

Korongo wenye taji ni wenye kuwastahimili wanadamu na waweza kufugwa kwa urahisi. Kwa sababu ya rangi yao yenye kupendeza na umbo lao na maonyesho yao ya dansi yenye kutumbuiza, wako mashuhuri kwenye bustani za wanyama na wanapendwa sana ili kupamba nyumba na bustani za kibinafsi. Kukiwa na uhitaji mkubwa kadiri hiyo, haishangazi kwamba idadi yao yapungua. Msongo zaidi kwa korongo mwenye taji watokana na kuharibiwa kwa mabwawa ili yatumiwe na utumizi wa sumu na dawa za kuulia wadudu, ambazo huchafuza maziwa na vijito.

Ingekuwa huzuni ikiwa siku moja hatungewaona wala kuwasikia korongo wenye taji. Hata hivyo, Biblia yaahidi kwamba karibuni dunia yote itafanywa kuwa mpya. (Linganisha 2 Petro 3:13.) Kisha, wakazi wote wa dunia watafurahia usanifu wa uumbaji wa Mfanyi Mtukufu, Yehova Mungu, na wachezaji-dansi wake wenye rangi nzuri walio na kishungi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki