Kile Ambacho Mazoezi Yaweza Kukufanyia
UCHUNGUZI wa wazi uliofanywa kwa wahitimu 17,000 ambao walisomea Harvard, ulioelezwa katika The New England Journal of Medicine miaka minne iliyopita, ulionyesha kwamba mazoezi ya kimwili yanaweza kuzuia mwelekeo wa urithi wa kufa mapema. “Una afya nzuri kwa sababu unafanya mazoezi,” akamalizia Dkt. Ralph S. Paffenbarger, Jr., kiongozi wa uchunguzi huo.
Katika Juni 1989 The Journal of the American Medical Association ilisema hivi: “Mazoezi ya kimwili yameonwa kuwa yanazuia na kudhibiti matatizo mengi ya kitiba, kama ugonjwa wa mishipa ya damu moyoni, ugonjwa wa msukumo wa damu, . . . matatizo ya afya ya akili.” Iliongezea hivi: “Ugonjwa wa mishipa ya damu moyoni unaweza kutokea mara 1.9 zaidi kwa mtu asiyefanya mazoezi kumshinda anayefanya mazoezi. Uhusianisho huo ni wa ajabu.”
Jarida hilo hilo lilichapisha katika Novemba 1989 uchunguzi uliofanywa kwa watu 13,344, na ukazidi kuonyesha umaana wa mazoezi. Uchunguzi huo wenye kuhusisha wengi ulionyesha kwamba hata zoezi dogo tu—kama kutembea upesi kwa nusu-saa kila siku—linatokeza ulinzi kwa kifo kitokezwacho na mambo mengi.
Dkt. Norman M. Kaplan, wa Shule ya Kitiba ya Kusini-magharibi ya Chuo Kikuu cha Texas iliyoko Dallas, ambaye ni mwenye mamlaka kuhusu ugonjwa wa msukumo mkubwa wa damu, sasa anatambua umaana wa mazoezi katika kutibu msukumo mkubwa wa damu. “Kwa vile nimeona uthibitisho ukiongezeka katika miaka mitatu au minne iliyopita, nimekuwa mwenye kutia watu moyo wafanye mazoezi.”
Dkt. Kaplan sasa anaagiza wagonjwa wa msukumo mkubwa wa damu wafanye mazoezi yenye kufanya mtu apumue sana. “Nawaambia wagonjwa wangu waongeze mpigo wao wa damu,” anaeleza. “Naambia watu waanze polepole. Usirukie jambo hilo. Anza kwa kutembea na kukimbia polepole na kuongezea-ongezea. Ukipata matatizo yoyote, acha.” Ili yawe msaada wa kweli kwa afya, mazoezi yanapaswa kufanywa kila mara, afadhali zaidi mara tatu au nne kila juma yakichukua muda wa dakika 20 hadi 30 au zaidi kila wakati.