Kuutazama Ulimwengu
WIVI WA WAFANYA KAZI
Uhalifu hugharimu utengenezaji-bidhaa wa Uingereza dola zaidi ya 9,000,000,000 kila mwaka, adai John Banham, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utengenezaji-Bidhaa la Uingereza. Katika jumla hii, kuanzia dola elfu mbili hadi elfu tatu milioni ni kwa sababu ya wivi wa wafanya kazi. Likiripoti matokeo ya uchunguzi mmoja wa karibuni, Daily Telegraph la London hufunua kwamba asilimia 85 ya waliohojiwa hawangeripoti mfanya kazi mwenzi kwa mkubwa wao kwa sababu ya kuibia kampuni. Kati ya matendo mengine ya kukosa unyofu, hesabu hiyo ya watu ilionyesha kwamba maelekeo yalitofautiana na umri. Huku zaidi ya nusu ya wafanya kazi wa miaka zaidi ya 45 wakikuona kupiga simu za kibinafsi kwa kutumia simu ya kampuni kwamba hakukubaliki, chini ya mmoja kati ya wanne wa miaka 16 kufikia 24 walikataa. Pia, ni asilimia 19 pekee wa kikundi hiki kichanga waliokuona kule kuzungumza mambo yasiyohusu kampuni wakati wa kazi kuwa ni “wivi wa wakati.”
KADIRI YA KIFO CHA WATOTO WACHANGA
Amerika sasa inakaribia kuwa juu zaidi katika orodha ya mataifa yaliyoendelea yaliyo na kadiri ya juu sana ya vifo vya watoto wachanga, asema Dkt. Regina Lederman, mkuu mshirika katika chuo kikuu na profesa kwenye Shule ya Uuguzi ya Tawi la Kitiba la Chuo Kikuu cha Texas. Miaka 20 iliyopita Amerika ilikuwa katika mahali pa 5 kimataifa kwa kuwa na wachanga wenye afya, lakini kufikia 1987 ilikuwa imeshuka kwenye nafasi ya 20. Amerika imesongwa na utumizi mbaya wa dawa za kulevya na ulevi, UKIMWI, ulaji mbaya, ukosefu wa makao, mikazo, tisho la mimba za matineja, na matokeo ya uvutaji sigareti. Yote hayo yanachangia kuzaliwa kwa watoto wakiwa na uzani wa chini, ambao ndilo tisho kubwa sana kwa watoto waliozaliwa karibuni na ni kisababishi cha vizuizi vingi vya muda wote wa maisha. Kulingana na Lederman, katikati mwaka 1950 na 1987, kujikabidhi kwa taifa kwa ajili ya afya ya wanawake na watoto kuliendeleza Japani kutoka mahali pa 17 hadi pa 1, wakifaulu kuwa walio na kadiri ndogo sana ya vifo vya watoto ulimwenguni. “Karibu uchunguzi wote unaonyesha kwamba utunzi wa kabla ya kuzaa unaongeza nafasi ya uzazi mzuri na mtoto mwenye afya,” asema Lederman. Kwa uhalisi, utunzi wa kabla ya uzalishaji unaanza kabla ya mimba kutungwa.”
UPUNGUFU WA NYANI
Tumbili wakubwa wasio na mikia wa Mwamba wa Gibraltar wanaojulikana kama “makaki Barbari” wanapungua idadi, laripoti The Times la London. Nyani hao wamekuwa mpaka sasa wakitafuta chakula kwa uhuru juu ya Mwamba huo chini ya usimamizi wa boma la majeshi ya Uingereza. Lakini wengi wa watalii milioni tatu u nusu ambao huzuru kila mwaka huwapa tumbili hao chokoleti na peremende nyingine. Kama tokeo, unene na uzoevu wa peremende unafanya baadhi ya “makaki Barbari” “kupoteza tamaa ya kuzaa na hupigania chakula.” Hili limesababisha kupungua kwa idadi ya uzalishaji, na hesabu yao kupungua kutoka 130 hadi 70. Ili kukabiliana na hilo, serikali ya Gibraltar sasa imeanzisha hifadhi yenye ulinzi ambapo kundi moja la tumbili litalindwa na kuweka utaratibu wa chakula ulio na sukari kidogo zaidi, asili yake ikiwa ni vidonge vya chakula. Mkurugenzi wa hifadhi hiyo anatumaini kwamba hili litatokeza mwenendo wa kawaida na litasaidia kuhifadhi jamii hii iliyo hatarini.
UPENDEZI WA KITAIFA KATIKA ULAYA
“Wasimamizi wa miaka ya Tisini [90],” laripoti The European, “itawabidi kushinda zaidi tu ya kizuizi cha lugha” ili kupata kazi ng’ambo. Uchunguzi mbalimbali uliofanywa katika Ulaya unaonyesha kwamba “upendezi wa waziwazi wa kitaifa” upo inapokuwa wakati wa kuajiri watu wa nchi za kigeni. Katika uchunguzi wa kampuni 700 za Uingereza, Wajerumani na Waholanzi walionekana kuwa wanachukuana kukiwa na zaidi ya theluthi moja, huku Waitaliano na Wahispania wakiwa hawapendwi sana. Wafaransa na Wabelgiji mara nyingi wanakubalika kama wafanya kazi wa kigeni, lakini Waswisi wanasemekana kuwa ghali sana na wenye kudai. Kwa kampuni za Hispania, chaguo lililo bora zaidi ni Wafaransa. Waingereza na Waholanzi hupenda kugawia wengine sehemu ya kazi yao, lakini Wafaransa na Waitaliano hawapendi hivyo. “Watu ni tofauti,” laeleza gazeti hilo, “na hivyo wanaamua uwezo wa kazi kwa njia tofauti.”
SABABU YA WATOTO KUTOROKA
Gazeti la Australia Canberra Times lilichanganua sababu za watoto kutoroka nyumbani. Kwa baadhi ya wengine, ni uamuzi wa mara hiyo. Wengine wanatoroka ili wapate jambo la kujasiria. Wengi wa wakimbizi hawa hupatwa upesi na njaa na upweke na kurudi baada ya siku chache. Lakini wengine wana sababu za kina zaidi, kama matatizo ya shuleni, wazazi walevi, kutendwa vibaya kimwili na kingono, na mvunjiko wa ndoa ya wazazi. Wale ambao hutoroka nyumbani kwa sababu hizi hukaa mbali kwa muda mrefu, wengine daima. Huenda wakageukia umalaya na wivi mdogo ili wapate fedha za kuendelea kuishi. Ishara za tahadhari ni: mabishano ya kila wakati nyumbani, kuchelewa nje usiku sana kwa ukawaida, na kutoroka-toroka. Ili kupunguza nafasi ya utoro, makala hiyo inaorodhesha madokezo haya kwa wazazi: “Mwandae mazingira ya nyumbani yaliyo na ujoto, na upendo; mwe na usawaziko kati ya kuendekeza na kutumia mamlaka kupita kiasi; wapeni watoto uhuru wa kujitawala na daraka; kuzeni stadi za mawasiliano yenye matokeo mazuri, hasa uwezo wa kusikiliza; andaeni mashauri ya haki na yenye upatani.’
WABUDHA KULINDA MALI
Wauza mawe ya thamani katika Japani wanaripoti kwamba sanamu za dhahabu za Budha kwa ghafula ndizo vifaa vyenye kuuzwa sana. Kwa nini? Vifaa vya kidhahabu vimekuwa bei rahisi tangu mfumo mpya wa kodi ulipoanzishwa. Isitoshe, kuna usadikisho unaokubaliwa na watu wengi kwamba sanamu hizi za kidini hazitozwi kodi ya urithi. Hata hivyo Uwakili wa Kodi (Tax Agency), unatisha kutoza sanamu za Budha ambazo zimenunuliwa ili kukiuka sheria na si kwa ajili ya sababu za kidini. Wauza mawe ya thamani hueleza, pia, kwamba kazi inayohusika katika kurembesha Budha huongeza bei kwa kipimo cha zaidi ya asilimia 75 ya thamani ya dhahabu, ikiifanya iwe isiyofaa kununua.
WAUAJI KWENYE BARABARA KUU
◻ Wengi wa watu wanaouawa kwenye barabara kuu wanatumia kokeni,” asema Dkt. Peter Marzuk, mwandishi-mwenzi wa uchunguzi uliochapishwa katika The Journal of the American Medical Association. Uchunguzi huo, uliofanywa kwa sababu vifo vinavyotokana na aksidenti za barabarani vilikuwa vimeongezeka katika Jiji la New York, ulionyesha kwamba asilimia 56 ya wale waliouawa walikuwa na mabaki ya kokeni au pombe, au zote mbili, katika miili yao wakati wa kifo chao. Marzuk afikiri dereva wengi zaidi wanatumia kokeni kuliko vile uchunguzi ulivyoonyesha. Wengine hawauawi, hali wengine wanaouawa hawakutumia ya kutosha kuweza kugunduliwa.
◻ “Kulala usingizi hali mtu akiendesha gari husababisha vifo vya barabarani kama 6,500 kila mwaka na huenda kukasababisha aksidenti 400,000 kwa mwaka “katika Amerika, lasema gazeti Science, likiripoti juu ya maoni ya Michael Aldrich, mwenye elimu ya mishipa ya fahamu na mchunguzi wa usingizi katika Chuo Kikuu cha Michigan. Kufikia asilimia 25 ya idadi ya watu huugua kutokana na maradhi ya usingizi, asema Aldrich, na ndio wepesi zaidi kulala wanapoendesha gari. Kutoweza kupumua wakati mtu amelala, hasa wakati wa usiku, ndiyo maradhi ya kawaida zaidi, na huacha mgonjwa akihisi uchovu siku inayofuata. Hata hivyo, idadi kubwa zaidi ilitukia kwa wale walio na ugonjwa wa nakolepsia, hali ambayo hutokeza “mashambulizi” ya usingizi wa ghafula.
KUWAWEZA MENDE
“Mende wanaweza kuvumilia kiasi kikubwa cha mwenezo wa joto kuliko wanadamu wawezavyo,” asema Richard Brenner wa Huduma ya Utafiti wa Ukulima United States, “lakini hawawezi kusawazisha joto, hivyo joto ambalo sisi twaweza kuvumilia—kwa sababu sisi hutoa jasho kuweza kupunguza joto la mwili wetu—litawaua.” Sasa kampuni ya kuzuia wadudu wanaosumbua iliyo katika Kalifornia inatumia jambo hilo hakika kuondoa mende na wadudu wengine wenye kusumbua. Nyumba iliyoambukizwa inafunikwa kwa hema zito. Viwasho vyenye kutumia mafuta-propeni, na vipepea-hewa, vinawekwa ndani kuinua hali ya joto hapo kufikia digirii 150° Fahrenheit. “Baada ya masaa manne chini ya joto hilo, kila sehemu ya jengo itakuwa imefikia zaidi ya digirii 50°C (122°F.), ambayo imetosha kuua mende, siafu, inzi, papasi, nondo, na hata mchwa,” yasema New Scientist.
“KWA MEMA ZAIDI AU KWA MABAYA ZAIDI”
“Ndoa, inasemwa, huwa zafanyiziwa mbinguni,” laeleza India Today. “Lakini kwa wenzi wawili hawa katika kijiji cha Patan, ndoa zinaonekana kama hazifanyiziwi duniani.” Ilitukia wakati vikundi viwili vya wanaofanya ndoa vilipofika kufanya ndoa zao katika wakati mmoja. Wote walikuwa na haraka, na sherehe zilifanywa kwa haraka. Mshtuko ulikuja wakati zile shela zenye kufunika nyuso za wale bibi arusi zilipoondolewa, na mvurugo wa mabibi arusi ukagundulikana. “Ingawa waliokuwa wakioana walichukizwa na mbadilishano huo, watu wa ukoo walisisitiza kwamba kilichokwisha kufanywa hakiwezi kurudishwa nyuma,” lasema India Today. Kwa hiyo sasa, kwa mema zaidi au kwa mabaya zaidi, wale wenzi ni lazima wawe pamoja mpaka kifo kiwatenganishe.”
KOMBORA-SANAA LA MISRI LINALODHURU BAADA YA MUDA
“Wachoraji katika Misri ya kale waliunda michoro ya rangi za kuvutia, sanamu zilizoandikwa katika ukuta mbichi, sanamu zenye rangi, majeneza na maziara (makaburi). Walikuwa chama chenye utalaamu wa juu sana na waliona rangi ya kwanza isiyo ya asili, buluu nyangavu ‘ya Misri,’ kuwa nzuri kuliko rangi nyingine zote za buluu ya asili walizokuwa nazo,” laandika The German Tribune. Lakini “hawakung’amua kwamba wakiwa na buluu yao ya Misri walikuwa wanaanzisha msaliti katika kazi zao za sanaa. Ilikuwa na vairasi ya kemikali ambayo ingeweza kuziangamiza.” Tatizo lenyewe huletwa na madini ya atakamaiti, ambayo haikuongezwa kimakusudi bali ambayo, wachunguzi walipata, hutokea baadaye kupitia tendo la kikemikali, polepole ikiibadili buluu kuwa kijani kibichi. Mwendo huo huendelea chini ya hali ya hewa yenye unyevunyevu wenye joto, ikiilegeza rangi na kuifanya ichakae na kutokatoka. Mwingi wa unyevunyevu huo wenye joto hutokezwa na ziara za watalii, ukiacha wenye mamlaka wa Misri wakiwa na tatizo-pande-mbili: wafunge maeneo ya utalii, ambayo nchi huyategemea kiuchumi, au wahatarishe kupoteza rangi zote za buluu na kijani-kibichi mnamo muda wa karne moja.