Misitu Inayopunguka, Hali-Joto Zinazopanda
KUHARIBIWA kwa misitu ya kitropiki. Ongezeko la hali-joto la anga la dunia. Mara nyingi matatizo hayo mawili hutajwa pamoja. Na ni kwa sababu nzuri: Lile la kwanza husababisha la pili. Ainabinadamu inapochoma, kufagilia mbali na kugharikisha sehemu kubwa za msitu ili apate nafasi ya malisho, barabara, na maboma ya maji ya kufanya umeme, misitu inatoa akiba yayo kubwa ya kaboni angani. Kaboni dayoksaidi inayofanyizwa ni mojawapo tu ya gesi nyingi zinazofanya anga ihifadhi joto, ikipasha tufe joto polepole.
Ripoti za hivi karibuni kutoka Umoja wa Mataifa zinafunua kwamba matatizo hayo mawili yaweza kuwa makubwa kuliko vile ilivyodhaniwa mbeleni. Kwa mfano, wataalamu wa hali ya anga zaidi ya 300 kutoka ulimwenguni pote walitoa onyo katika Mei 1990 kwamba wastani wa hali-joto ya ulimwenguni pote itapanda kwa digrii 2 katika miaka 35 ijayo na digrii 6 kufikia mwisho wa karne ijayo ikiwa mwanadamu hatarekebisha mwendo wa sasa.
Wanasayansi hao wanadai kuwa hilo lingekuwa badiliko kubwa zaidi katika wastani wa hali-joto ambalo dunia imepata katika miaka elfu kumi. Ingawa ongezeko la hali-joto la anga la dunia limekuwa jambo la kubishaniwa miongoni mwa wanasayansi, The Washington Post inasema: “Wanasayansi walioandika ripoti hiyo . . . walisema kwamba iliwakilisha makubaliano ya kutokeza miongoni mwa mamia ya wanasayansi ambao kwa kawaida huwa washindani.”
Wakati huo huo, ripoti yenye kichwa World Resources 1990-91, ilikadiria kwamba ulimwengu unapoteza misitu yake ya kitropiki kwa asilimia 50 kupita vile makadirio ya mbeleni yalivyoonyesha. Kiwango cha pamoja cha misitu iliyoharibiwa katika nchi tisa—katika Esia, Afrika, na Amerika Kusini—kiliongezeka zaidi ya mara tatu wakati wa miaka ya 1980! Kulingana na ripoti hiyo, jumla ya ulimwenguni pote ni kati ya hektari milioni 16 na 20 ya misitu ya kitropiki inayoharibiwa kila mwaka.
Kuharibiwa kwa misitu tayari kunaleta hasara. Kwa mfano, International Wildlife lasema kwamba misitu ya mvua ya ulimwengu ndiyo makao ya aina za mimea na wanyama angalau milioni 5 na labda milioni 30 hivi—“wengi kuliko wale wanaoishi katika mazingira yale mengine yote ya dunia yakiwa pamoja.” Aina hizo za mimea na wanyama kwa kweli zinaelekea kwisha kabisa. Tayari baadhi ya watazama-ndege katika sehemu za kaskazini wameanza kuona kwamba ndege wanaohama kulingana na majira kutoka misitu ya kitropiki wanazidi kupungua.
Katika Madagaska asilimia 80 hivi ya aina ya mimea yenye kutoa maua hayapatikani mahali penginepo pote juu ya sayari; moja yake, konokonokwekwe (periwinkle), ndio msingi wa dawa ya kansa iliyo maarufu sana ulimwenguni. Walakini, zaidi ya nusu ya misitu ya Madagaska tayari imeharibiwa au kufutiliwa mbali.
Kwa kweli, kama vile Biblia ilivyokuwa imeonyesha zamani, mwanadamu ‘anaiharibu nchi’ katika siku hizi za mwisho.—Ufunuo 11:18.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]
Abril Imagens/João Ramid