Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 5/8 kur. 6-11
  • Manufaa za Misitu ya Mvua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Manufaa za Misitu ya Mvua
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msitu wa Kipekee
  • Chakula, Hewa Safi, na Dawa
  • “Tutahifadhi Kile Tu Tukipendacho”
  • Misitu ya Mvua Je, Inaweza Kuokolewa?
    Amkeni!—2003
  • Kutumiwa Vibaya kwa Misitu ya Mvua
    Amkeni!—1998
  • Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
    Amkeni!—1997
  • Je, Misitu Yetu ya Mvua Itaokoka?
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 5/8 kur. 6-11

Manufaa za Misitu ya Mvua

KATIKA mwaka wa 1844, msomi Mgiriki Konstantin von Tischendorf aliona makaratasi 129 ya hati za zamani katika pipa ndani ya nyumba ya watawa. Tischendorf alienda na makaratasi hayo yenye thamani, na sasa ni sehemu ya ile Kodeksi ya Sinai—mojawapo ya hati za Biblia zijulikanazo sana ulimwenguni.

Hazina hiyo iliokolewa kwa wakati ufaao. Misitu ya mvua—ambayo thamani yake kwa kawaida hupuuzwa—kwa nadra huweza kufanikiwa hivyo. Kila mwaka katika msimu wa kiangazi, maelfu ya mioto iliyoanzishwa na wafugaji na wakulima wa kuhamahama humulika anga la kitropiki. Al Gore, ambaye sasa ni makamu wa rais wa Marekani, aliyeshuhudia moto mkubwa kama huo katika eneo la Amazon, alisema: “Angamizo hilo ni lisiloaminika. Ni mojawapo ya misiba mikubwa katika historia yote.”

Ni mara chache ambapo watu huchoma kile wajuacho thamani yake. Msiba wa msitu wa mvua ni kwamba unaharibiwa kabla hatujafahamu thamani yake, kabla hatujaelewa jinsi hiyo hutenda kazi, na hata kabla hatujajua ni nini kilicho ndani yake. Kuwasha moto msitu wa mvua ni kama kuchoma maktaba ili kupasha nyumba joto—bila kuchunguza yaliyomo katika vitabu.

Katika miaka ya karibuni wanasayansi wameanza kuchunguza “vitabu” hivi, lile ghala kubwa la habari lililofungiwa katika misitu ya mvua. Hufanyiza “usomaji” wenye kuvutia sana.

Msitu wa Kipekee

“Miti ya [West] Indies ni kitu ambacho hakiwezi kuelezeka, kwa sababu ya wingi wake,” Gonzalo Fernández de Oviedo mwandika-matukio Mhispania akasema kwa mshangao katika mwaka wa 1526. Karne tano baadaye kadirio lake la thamani lingali sahihi. “Msitu wa mvua,” aandika mwandikaji Cynthia Russ Ramsay, ni “wenye unamna mwingi, wenye utata, na mfumikolojia usioeleweka sana katika dunia.”

Mwanabiolojia wa kitropiki Seymour Sohmer ataarifu: “Hatupaswi kamwe kusahau uhakika wa kwamba twajua machache sana au hatujui lolote kuhusu jinsi ambavyo misitu mingi yenye unyevu ya kitropiki imeundwa na jinsi ifanyavyo kazi, bila kutaja spishi zilizo ndani yake.” Idadi kubwa sana ya spishi na utata wa uhusiano wake hufanya kazi ya mtafiti kuwa yenye kukatisha tamaa.

Msitu ulio katika maeneo yenye joto la wastani huenda ukawa tu na spishi chache za miti katika kila eka. Kwa upande ule mwingine, eka moja ya msitu wa mvua, yaweza kuwa na spishi tofauti-tofauti 80, hata ingawa jumla ya idadi ya miti kwa kila eka kwa wastani ni karibu 300 tu. Kwa kuwa uainishaji wa hali kama hiyo ya kuwa na unamna-namna ni kazi ya kuchosha na yenye kuhitaji uangalifu wenye bidii, ni visehemu vichache tu vya msitu wa mvua ambavyo vimeweza kuchanganuliwa. Hata hivyo, vile ambavyo vimechanganuliwa, hutoa matokeo yenye kushangaza.

Miti ya namna nyingi huandaa makao yasiyohesabika yanayotoa mambo yahitajikayo kwa ajili ya kuendelea kuwako kwa spishi kwa ajili ya idadi kubwa ya wakazi wa msituni—nyingi sana kuliko ilivyoweza kuwaziwa. Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha Marekani chasema kwamba eneo lifananalo na hilo la kilometa kumi za mraba za eneo la msitu wa mvua wa zamani laweza kuwa na spishi tofauti-tofauti 125 za mamalia, spishi 100 za wanyama-watambazi, spishi 400 za ndege, na spishi 150 za vipepeo. Kwa kulinganisha, twaona ya kwamba Amerika Kaskazini yote imetembelewa na spishi zipunguazo 1,000 tu za ndege.

Ingawa baadhi ya mamiriadi ya spishi za mimea na wanyama zaweza kupatikana katika sehemu kubwa ya msitu wa mvua, nyingine ziko tu katika safu moja ya milima. Hilo ndilo huzifanya ziwe rahisi kudhuriwa. Kufikia wakati wakataji-miti walipomaliza kufyeka safu moja ya misitu katika Ekuado miaka michache iliyopita, spishi 90 za kienyeji zilikuwa tayari zimetoweka.

Kwa kukabili misiba kama hiyo, shirika la United States Interagency Task Force on Tropical Forests laonya hivi: “Jumuiya ya mataifa yapaswa kuanzisha upesi shambulio lililoharakishwa na lenye umoja kuhusu tatizo hilo ikiwa mali hizi zilizoshushiwa thamani na ambazo huenda zisiweze kurudishwa tena zapasa kulindwa dhidi ya kuharibiwa kikweli kufikia mapema mwa karne ijayo.”

Lakini maswali yaweza kuzuka: Je, mali hizi za asili ni zenye thamani jinsi hiyo? Je, kufa kwa msitu wa mvua kwaweza kuathiri sana maisha zetu?

Chakula, Hewa Safi, na Dawa

Je, wewe huanza siku kwa kunywa bakuli ya uji, labda yai lililochemshwa, na kikombe cha kahawa moto? Ikiwa wewe hufanya hivyo, unafaidika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na misitu ya kitropiki. Mahindi, mbegu za kahawa, kuku aliyetaga yai, na hata ng’ombe aliyetoa maziwa—zote zilikuwa na mwanzo katika mimea na wanyama wa msitu wa kitropiki. Mahindi yalitoka Amerika Kusini, mbegu za kahawa zamani zilikua katika misitu ya Ethiopia, kuku wa kufugwa walizalishwa kutoka kwa kuku wa msituni wa Asia, na ng’ombe wa maziwa walitokana na banteng walio hatarini wa Kusini-Mashariki mwa Asia. “Kikamili asilimia 80 ya chakula tunachokula kilitoka katika tropiki,” chaeleza kitabu Tropical Rainforest.

Mwanadamu hawezi kuthubutu kupuuza chanzo cha ugavi wake wa chakula. Mimea na wanyama wa kufugwa waweza kudhoofishwa kwa uzalishaji unaopita kiasi baina ya spishi za nasaba moja. Msitu wa mvua, ukiwa na wingi wa spishi, waweza kuandaa unamna-namna wa kijeni unaohitajiwa ili kuimarisha mimea hii au wanyama. Kwa kielelezo, mwanabotania Mmexico Rafael Guzmán aligundua spishi mpya za nyasi zinazohusiana na mahindi ya kisasa. Ugunduzi wake uliwasisimua wakulima kwa sababu nyasi hii (Zea diploperennis) hukinza magonjwa makubwa tano kati ya yale saba ambayo hushambulia mahindi. Wanasayansi wanatumainia kutumia spishi hiyo mpya ili kutokeza namna nyingi za mahindi zenye kukinza ugonjwa.

Katika mwaka wa 1987 serikali ya Mexico ilihami safu ya milima ambako mahindi hayo ya msituni yalipatikana. Lakini kukiwa na msitu mkubwa sana unaoangamizwa, hakuna shaka kwamba spishi zenye thamani kama hii zinapotezwa, hata kabla hazijajulikana. Katika msitu wa Kusini-Mashariki mwa Asia, kuna spishi kadhaa za ng’ombe wa msituni ambazo zingeweza kuimarisha uzao wa ng’ombe wa kufugwa. Lakini spishi hizi zote ziko ukingoni mwa kuangamizwa kwa sababu ya kuharibiwa kwa makao yao.

Hewa safi ni ya muhimu kama vile tu chakula tunachokula. Kama vile mtu yeyote afurahiaye kutembea katika msitu awezavyo kuona, miti hufanya kazi nyingi ya kuijaza tena angahewa kwa oksijeni. Lakini inapochomwa, kaboni katika namna ya kaboni dioksidi na kaboni monoksidi hutokezwa. Gesi hizi mbili husababisha matatizo.

Wengine hukadiria kuwa kazi za mwanadamu tayari zimeongezea maradufu idadi ya kaboni dioksidi katika angahewa ya dunia. Ingawa uchafuzi wa kiviwanda hudhaniwa kuwa mshukiwa mkuu, uchomaji wa misitu wahesabiwa kutokeza zaidi ya asilimia 35 ya utokezaji wote wa kaboni dioksidi. Mara iwapo katika angahewa, kaboni dioksidi hutokeza kile kiitwacho ongezeko la joto duniani, ambalo wanasayansi wengi wanatabiri kuwa laweza kusababisha utiaji-joto mbaya sana wa tufeni.

Kaboni monoksidi ni mbaya hata zaidi. Ni kiungo cha msingi chenye kufisha kipatikanacho katika ukungu ambao ni sumu ya vitongoji vya jiji. Lakini mtafiti James Greenberg alishangaa kupata “kiasi kilekile cha kaboni monoksidi katika misitu ya Amazon kama ilivyo katika vitongoji vya Marekani.” Kuchomwa bila kufikiria kwa misitu ya Amazon kulikuwa kumechafua angahewa ambalo miti hiyo ilipaswa kusafisha!

Mbali na kuwa chanzo cha chakula na hewa safi, msitu wa mvua waweza kuwa kabati la dawa kwa kweli. Robo ya dawa zote ambazo madaktari huwaandikia wagonjwa hutolewa katika mimea ambayo hukua katika misitu ya kitropiki. Kutoka katika misitu ya milima ya Andes hutoka kwinini, kwa ajili ya kupigana na malaria; curare hutoka katika eneo la Amazon, dawa ambayo hutumiwa kutuliza misuli wakati wa upasuaji; na kutoka Madagaska ile rosy periwinkle, ambayo alkaloidi zake kwa kutazamisha huongezea kiwango cha kuendelea kuishi kwa wengi wa wagonjwa wa leukemia. Licha ya matokeo kama hayo yenye kuvutia, ni karibu asilimia 7 tu ya mimea yote ya kitropiki ambayo imechunguzwa kwa uwezekano wake wa kuwa na tabia za dawa. Na wakati wapunguka. Taasisi ya Kansa ya Marekani yaonya kwamba “kuenea sana kwa uangamizo wa misitu ya mvua yenye unyevu kwaweza kutokeza hitilafu katika kampeni ya kupigana na kansa.”

Kuna mambo mengine ya muhimu ambayo misitu ya mvua hufanya—hata ingawa umaana wao kwa nadra huthaminiwa hadi misitu inapotoweka. Kati ya hizi ni utaratibu wa mvua na halijoto vilevile kulinda dhidi ya mmomonyoko wa udongo. “Mazao mengi ya misitu ya kitropiki ya ulimwengu hupita sana uelewevu wetu wa sasa kuuhusu,” charipoti kitabu The Emerald Realm: Earth’s Precious Rain Forests. “Lakini twajua hata sasa kwamba thamani yake haihesabiki.”

“Tutahifadhi Kile Tu Tukipendacho”

Kuharibu mali ambayo hutuandalia kwa wingi sana hivyo kwa kweli ndio mwanzo wa upumbavu. Zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, Mungu aliwaagiza Waisraeli wahifadhi miti ya matunda walipokuwa wakipigana na jiji la maadui. Sababu aliyowapa ilikuwa sahili: “Hiyo huwaandalia chakula.” Zaidi ya hilo, “miti hiyo ya shambani si watu kwamba uizingire.” (Kumbukumbu la Torati 20:19, 20, The New English Bible) Hili pia laweza kusemwa kuhusu msitu wa mvua unaoshambuliwa kutoka pande zote.

Kwa wazi, misitu ya mvua ina faida nyingi inapoachwa imesimama kuliko wakati imekatwa kama vile tu miti ya matunda ilivyo. Lakini katika ulimwengu huu wa kisasa, manufaa za muda mfupi kwa kawaida hupuuza thamani ya muda mrefu. Hata hivyo, elimu yaweza kubadili mitazamo. Mwanaikolojia wa Senegal Baba Dioum atoa hoja hivi: “Mwishowe tutahifadhi kile tu tukipendacho; tutapenda tu kile tunachoelewa; na tutaelewa tu kile tufunzwacho.”

Tischendorf aliiba yale makaratasi ya zamani katika Jangwa la Sinai kwa sababu alipenda hati za zamani na alitaka kuzihifadhi. Je, idadi kubwa ya watu itaweza kujifunza kupenda misitu ya mvua kwa wakati ufaao ili kuiokoa?

[Blabu katika ukurasa wa 11]

Kuwasha moto msitu wa mvua ni kama kuchoma maktaba ili kupasha nyumba joto—bila kuchunguza yaliyomo katika vitabu

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Kuwahifadhi Viumbe wa Msituni

KWA karibu muda wa miaka 15 Jesús Elá aliwawinda sokwe pamoja na wanyama wengine wa msitu wa mvua wa Afrika. Lakini sasa hawindi tena. Sasa amekuwa kiongozi katika hifadhi ya asili iliyowekwa kando ili kuwalinda sokwe 750 katika Guinea ya Ikweta.

“Mimi hufurahia msitu wa mvua zaidi wakati ambapo siwindi,” aeleza Jesús. “Kwangu msitu ni kama kijiji changu kwa sababu mimi huhisi kustarehe nikiwa huku na huniandalia kila kitu ninachohitaji. Lazima tufanye yote tuwezayo ili tuwahifadhie watoto wetu misitu hii.”

Jesús, ambaye hushiriki kwa utayari upendo wake kuelekea msitu pamoja na wengine, ana pendeleo. Sasa anachuma fedha nyingi kwa kuwalinda sokwe kuliko wakati alipokuwa akiwawinda. Kwa kuwa watalii wanafurahi kulipa kwa ajili ya pendeleo la kuwaona wanyama kama hao msituni, mbuga za wanyama zaweza kuandaa mapato kwa ajili ya wenyeji na kuwapa wageni mwono wa mara moja wa kukumbukwa wa utele wa viumbe. Lakini uhifadhi wa “sehemu hii tata ya maisha” yenye kuvutia sana, chaeleza kitabu Tropical Rainforest, huhitaji “maeneo makubwa yaliyotengwa kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi wanyama na miti, ambayo hutia ndani eneo la mwinuko linalogawa maji.”a

Kwa nini mbuga zinahitaji kuwa kubwa hivyo ili kutoa utunzaji wa kutosha? Katika kitabu chake Diversity and the Tropical Rain Forest, John Terborgh, apiga hesabu kwamba idadi ya chui wa Amerika ya Kusini na Kati kuweza kuwapo (karibu wanyama 300 waliokomaa) huhitaji angalau kilometa za mraba 7,500. Amalizia hivi, “Kwa kanuni hii kuna mbuga chache tu duniani ambazo zaweza kuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya chui wa Amerika ya Kusini na Kati.” Simbamarara huenda wakahitaji hata nafasi kubwa zaidi. Kikundi kinachozalisha cha simbamarara (wanyama 400) huenda kikahitaji eneo kubwa kama kilometa za mraba 40,000.

Kwa kuweka kando hifadhi kubwa kama hizi kwa ajili ya wanyama-wawindaji kama hawa, maeneo mazima ya msitu wa mvua yaweza kulindwa. Likiwa kama manufaa ya ziada, wanyama hawa huwa na sehemu ya muhimu katika kudumisha afya ya jumla ya jumuiya ya wanyama.

[Maelezo ya Chini]

a *Eneo la mwinuko linalogawa maji ni sehemu ambayo humwaga maji katika mto, mfumo wa mto au namna nyingine ya maji.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Viumbe Wakubwa na Wadogo

1. Panzi wengi wa msitu wa mvua hupakwa rangi zenye urembo mno. Wadudu wengine wanaweza kujificha kwa matokeo sana hivi kwamba inakuwa vigumu kuwafahamu

2. Vipepeo huonekana kwa urahisi sana na ni viumbe vinavyotaka uangalifu mkubwa vya msitu wa mvua

3. Kikundi cha tumbili wakicheza-cheza kutoka kwa utanzu mmoja hadi mwingine ni mojawapo ya maono ya kuburudisha sana ya msituni

4. Ijapokuwa chui wa Amerika ya Kusini na Kati ni mfalme wa misitu ya Amerika asiyebishwa, ni wanaviumbe wachache ambao wamewahi kumwona mmoja katika msitu

5. Kuchanua kwa okidi zenye kuhitaji utunzaji mzuri hupamba mawingu yenye unyevu ambayo hufunika milima ya kitropiki

6. Kuna simbamarara wanaopungua 5,000 waliobakia msituni

7. Mdudu anayeitwa kwa kufaa kifarujoho wa Amerika ya kitropiki ana pembe za kutisha sana lakini hadhuru

8. Ingawa sokwe ni spishi zinazolindwa, bado nyama yao yaweza kupatikana katika masoko ya Afrika. Jitu hili lenye uanana ni mla-mboga na hutembea-tembea katika msitu wakiwa vikundi vya kifamilia

9. Ocelots walikuwa karibu kumalizwa kwa kuwindwa kwa sababu ya ngozi yao yenye fahari

10. Kasuku ni kati ya ndege wenye kelele zaidi na wenye urafiki zaidi msituni

11. Kama vile macho yake makubwa yadokezavyo galago hutafuta chakula usiku

[Hisani]

Foto: Zoo de Baños

Foto: Zoo de la Casa de Campo, Madrid

[Hisani]

Foto: Zoo de Baños

[Picha katika ukurasa wa 7]

Misitu ya mvua hutoa: (1) kakao, (2) rosy periwinkle, ya muhimu sana katika kutibu leukemia, na (3) mawese. (4) Kukata misitu huongoza kwenye maporomoko ya ardhi yenye kuangamiza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki