Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
UKIONEKANA kutoka kwenye ndege, msitu wa mvua wa Amazon hukukumbusha zulia lenye vishungi linalotoshana na kontinenti nzima, ukiwa wa kijani kibichi na wa asili kama ulivyokuwa wakati Orellana alipougundua. Unapokuwa ukitembea kwa shida kupitia ardhi ya msitu yenye joto na unyevu, ukijaribu kuepuka wadudu wenye ukubwa wa wanyama wadogo, wapata likiwa jambo gumu kutofautisha mahali ambapo uhalisi huishia na fantasia kuanza. Yale yaonekanayo kuwa majani kumbe kwa kweli ni vipepeo, ionekanayo kuwa mimea yenye kutambaa kumbe kwa kweli ni nyoka, na vionekanavyo kuwa vipande vya miti iliyokauka kumbe kwa kweli ni wanyama wenye kuguguna walioshtuliwa ambao wakimbia kwa kasi sana. Katika msitu wa Amazon ni vigumu kutofautisha mambo hakika na yasiyo hakika.
“Jambo lenye kutatanisha sana,” asema mtoa-maoni mmoja, “ni kwamba uhalisi wa Amazon ni usioaminika kiasi cha kwamba ni kama hekaya zao.” Na kweli ni usioaminika! Ebu wazia msitu mkubwa kama Ulaya Magharibi. Ujaze kwa zaidi ya spishi tofauti-tofauti 4,000 za miti. Upambe kwa urembo wa zaidi ya spishi 60,000 za mimea yenye kuchanua maua. Utie rangi kwa aina za rangi nyangavu za spishi 1,000 za ndege. Uboreshe kwa spishi 300 za wanyama. Ukoleze kwa mvumo wa labda spishi milioni mbili za wadudu. Sasa wafahamu kwa nini yeyote afafanuaye msitu wa mvua wa Amazon hujikuta akitumia maneno bora zaidi ya ufafanuzi. Ni maneno bora zaidi pekee yawezayo kufafanua ifaavyo unamna-namna mwingi wa viumbe-uhai wenye kutokeza wa msitu huu wa mvua wa kitropiki ulio mkubwa kupita yote duniani.
“Wafu Wanaoishi” Waliojitenga
Miaka 90 iliyopita mwandishi na mcheshi Mmarekani Mark Twain alifafanua msitu huu wenye kuvutia kuwa “bara lenye kuvutia mno, bara lenye maajabu mengi sana ya kitropiki, bara lenye uvutio wa kimawazo ambapo ndege wote na maua na wanyama walikuwa wa kipekee sana hivi kwamba walistahili kuonyeshwa kwenye majumba ya hifadhi ya vitu vya asili, na ambapo aligeta na mamba na tumbili walionekana wakiwa starehe kana kwamba walikuwa katika Hifadhi ya Wanyama.” Leo, maelezo ya kiakili ya Twain yamepata badiliko baya sana. Hifadhi za vitu vya asili na hifadhi za wanyama huenda karibuni ndizo zitakuwa makao pekee yaliyobaki kwa idadi zenye kuongezeka za maajabu hayo ya kitropiki ya Amazon. Kwa nini?
Kisababishi kikuu kwa wazi ni mwanadamu kukata msitu wa mvua wa Amazon, akiharibu makao ya asili ya maua na wanyama wa eneo hilo. Hata hivyo, japo uharibifu wa kiwango kikubwa wa makao, kuna visababishi vinginevyo—vyenye hila zaidi—ambavyo vinageuza spishi za mimea na wanyama kuwa “wafu wanaoishi,” hata ingawa bado ziko hai. Yaani, wataalamu waamini kwamba hakuna chochote kiwezacho kuzuia spishi zisiendelee kufa.
Kisababishi kimojawapo ni utengaji. Maofisa wa serikali wanaopendezwa na uhifadhi huenda wakapiga marufuku ukataji wa miti kutoka sehemu fulani ya msitu ili kuhakikisha kusalimika kwa spishi zenye kuishi huko. Hata hivyo, kisehemu kidogo cha msitu huandalia spishi hizi taraja la kifo cha hatimaye. Protecting the Tropical Forests—A High-Priority International Task hutoa kielelezo ili kuonyesha kwa nini visehemu vidogo vya msitu hushindwa kutegemeza uhai kwa muda mrefu.
Spishi za miti ya kitropiki huwa na miti ya kike na ya kiume. Ili kuzaana, hiyo husaidiwa na popo ambao hubeba chavuo wanapopuruka kutoka maua ya kiume hadi ya kike. Bila shaka, utumishi huu wa uchavushaji hufaulu tu ikiwa miti hiyo hukua mnamo eneo la kupuruka la popo. Ikiwa umbali kati ya mti wa kike na wa kiume ni mkubwa sana—kama itokeavyo mara nyingi wakati kisehemu cha msitu kizungukwapo na ardhi iliyochomwa iliyoenea sana—popo huyo hawezi kuvuka umbali mkubwa kama huo. Kisha miti hiyo, yataja ripoti hiyo, hugeuka kuwa “‘wafu wanaoishi’ kwa kuwa uzaanaji wayo wa muda mrefu hauwezekani tena.”
Mlingano huu kati ya miti na popo ni mojawapo mahusiano yafanyizayo jumuiya ya kiasili ya Amazon. Kwa kueleza kisahili, msitu wa Amazon ni kama nyumba kubwa iandaayo chumba na chakula kwa mchanganyiko wa watu tofauti lakini wenye kuhusiana kwa ukaribu. Ili kuepuka kusongamana, wakazi hao wa msitu huo wa mvua huishi kwenye viwango tofauti-tofauti, wengine karibu sana na sakafu ya msitu, wengine juu sana kwenye matawi ya juu kabisa ya miti. Wakazi wote wana kazi, nao hufanya kazi saa 24 kwa siku—wengine mchana, wengine usiku. Spishi zote zikiruhusiwa kufanya sehemu zilizogawiwa kufanya, jumuiya hii kubwa mno ya mimea na wanyama wa Amazon hufanya kazi kwa njia ya kutiririka bila matatizo yoyote.
Hata hivyo, mfumikolojia (“iko” hutokana na neno la Kigiriki oiʹkos, limaanishalo “nyumba”) wa Amazon, ni rahisi sana kupata madhara. Hata ikiwa mwingilio wa mwanadamu katika jumuiya hii ya msitu unahusisha spishi chache tu, uingiliaji wake huendelea kupitia viwango vyote vya msitu huo. Mtaalamu wa uhifadhi Norman Myers akadiria kwamba kutoweka kwa spishi moja tu ya mmea kwaweza hatimaye kuchangia kifo cha spishi zipatazo 30 za wanyama. Na kwa kuwa miti mingi ya kitropiki hutegemea wanyama kwa utawanyaji wa mbegu, tendo la mwanadamu kuharibu spishi za wanyama huongoza kwenye kutoweka kwa miti ambayo wanyama hao wanaihudumia. (Ona sanduku “Uhusiano wa Mti na Samaki.”) Kama utengaji, kutatiza mahusiano kwa hakika huleta spishi nyingi zaidi na zaidi kwa kiwango cha “wafu wanaoishi.”
Je, Ni Kweli Kwamba Kukata Miti Sehemu Ndogo Hutokeza Hasara Chache?
Wengine hutetea ukataji wa miti wa sehemu ndogo kwa kusababu kwamba msitu huo utarudia hali nzuri na kuotesha tabaka mpya ya mimea ya kijani kibichi katika bara kubwa lililokatwa kama vile tu miili yetu ikuzavyo tena ngozi mpya juu ya sehemu iliyokatwa ya kidole. Ni kweli? Sivyo hasa.
Bila shaka, ni kweli kwamba msitu utakua tena mwanadamu akiacha sehemu iliyokatwa miti kwa muda mrefu ifaavyo. Lakini ni kweli pia kwamba tabaka mpya ya mimea haitafanana sana na msitu wa awali kama tu vile fotokopi mbaya haifanani kikamili na hati ya awali. Ima Vieira, mwanabotania mmoja wa Brazili, alichunguza eneo la muda wa karne moja la msitu uliokua tena katika Amazon na kupata kwamba kati ya spishi 268 za miti zilizokuwa zikisitawi katika msitu wa kale, ni 65 tu hufanyiza sehemu ya msitu uliokua tena leo. Tofauti hiihii, asema huyo mwanabotania, ipo pia kwa spishi za wanyama wa eneo hilo. Kwa hiyo ingawa ukataji wa miti haugeuzi, kama wengine wanavyodai, misitu ya kijani kibichi kuwa majangwa mekundu, huo unageuza sehemu za msitu wa mvua wa Amazon kuwa mwigizo hafifu wa msitu wa hapo awali.
Kwa kuongezea, kukata hata eneo dogo la msitu mara nyingi huharibu mimea na wanyama ambao hukua, kutambaa, na kupanda katika eneo hilo tu la msitu si kwingineko. Kwa mfano, watafiti katika Ekuado, walipata spishi 1,025 za mimea katika eneo fulani la kilometa 1.7 za mraba za msitu wa kitropiki. Zaidi ya 250 za spishi hizo hazikukua kwingineko kote duniani. “Kielelezo cha hapa kwetu,” asema mwanaikolojia wa Brazili Rogério Gribel, “ni sauim-de-coleira,” tumbili mdogo mwenye kuvutia, afananaye kana kwamba amevalia tishati nyeupe. “Wachache wanaobaki huishi katika eneo dogo tu la msitu karibu na Manaus katika Amazon ya kati, lakini kuharibiwa kwa makao hayo madogo,” asema Dakt. Gribel, “kutatowesha spishi hii milele.” Kukata miti sehemu ndogo lakini hasara ni kubwa.
Kuharibu Misitu
Hata hivyo, ukataji miti wa waziwazi, ndio unaoleta huzuni yenye kuhangaisha sana kwa msitu wa mvua wa Amazon. Watengenezaji wa barabara, wakataji wa miti, wachimbaji wa madini, na wengine wengi wanaharibu mimea inayofunika misitu, wakiharibu kabisa mifumikolojia yote kwa kipindi kifupi sana cha wakati.
Ingawa kuna kutoafikiana kwa kina kuhusu tarakimu hususa za kiwango cha uharibifu wa misitu Brazili kila mwaka—makadirio ya kiasi huonyesha kuwa ni kilometa za mraba 36,000 kwa mwaka—kiasi cha jumla cha msitu wa mvua wa Amazon ambao tayari umeharibiwa chaweza kuwa zaidi ya asilimia 10, eneo ambalo ni kubwa kuliko Ujerumani. Veja, gazeti kuu la habari la kila juma la Brazili, liliripoti kwamba mioto ya msitu ipatayo 40,000 iliyowashwa na wakulima wenye kukata miti na kuichoma ili kupata ardhi ya kulima ilienea sana nchini kote katika 1995—mara tano zaidi ya mwaka uliotangulia. Mwanadamu anachoma msitu kwa bidii nyingi mno, likaonya Veja, hivi kwamba sehemu za Amazon zafanana na “moto mwingi sana katika mpaka wa kijani kibichi.”
Spishi Zinatoweka—Kwa Hiyo?
‘Lakini,’ wengine huuliza, ‘je, twahitaji mamilioni hayo yote ya spishi?’ Ndiyo, twahitaji, ateta mtaalamu wa uhifadhi Edward O. Wilson, wa Chuo Kikuu cha Harvard. “Kwa kuwa twategemea mifumikolojia ifanyayo kazi ili kusafisha maji yetu, kuboresha mchanga na kutokeza hewa tunayopumua,” asema Wilson, “unamna-namna wa viumbe hai si kitu cha kutupa tu ovyoovyo.” Kitabu People, Plants, and Patents chasema: “Kufikia unamna-namna wa viumbe hai ndiko kutakuwa ufunguo wa kusalimika kwa wanadamu. Unamna-namna huo ukitoweka, muda si muda sisi tutatoweka pia.”
Kwa kweli, athari ya kuharibu spishi huenda kupita ukataji wa miti, kuhatarishwa kwa wanyama, na kusumbuliwa kwa wakazi wenyeji. (Ona sanduku “Athari kwa Binadamu.”) Kutokomea kwa misitu huenda kukakuathiri. Fikiria hili: Mkulima katika Msumbiji akata mashina ya mhogo, mama katika Uzbekistan ameza kibonge cha kuthibiti uzazi, mvulana aliyejeruhiwa katika Sarajevo akipewa mofini, au mteja katika duka la New York akifurahia harufu ya manukato ya kipekee—watu wote hawa, yataja Taasisi ya Panos, wanatumia bidhaa zilizotoka kwenye msitu wa kitropiki. Kwa hiyo msitu ambao haujakatwa bado husaidia watu ulimwenguni pote—kutia ndani wewe.
Hakuna Karamu, Hakuna Njaa Kuu
Ni kweli kwamba msitu wa mvua wa Amazon hauwezi kuandaa karamu ya ulimwenguni pote, lakini waweza kusaidia kuzuia njaa ya ulimwenguni pote. (Ona sanduku “Hekaya ya Rutuba.”) Kwa njia gani? Katika miaka ya 1970, kwa kiwango kikubwa mwanadamu alianza kupanda aina chache tofauti za mimea ambayo ilitokeza mazao makubwa sana isivyo kawaida. Ingawa aina hizi mpya zenye kutokeza sana zimesaidia kulisha watu wengine zaidi ya milioni 500, kuna tatizo lililofichika. Kwa kuwa hazina utofauti wa kijeni, hizo ni dhaifu na ziwezazo kupatwa kwa urahisi na maradhi. Kirusi chaweza kuharibu sehemu kubwa sana ya zao kuu la taifa, matokeo yakiwa njaa kuu.
Kwa hiyo ili kutokeza mazao yawezayo kustahimili hali mbaya na kuepusha njaa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) sasa lasihi “utumizi wa unamna-namna mwingi wa vifanyizi vya kijeni.” Na hapo ndipo msitu wa mvua pamoja na wakazi wao wa awali wanapochangia.
Kwa kuwa misitu ya kitropiki huwa na zaidi ya nusu ya spishi za mimea za ulimwenguni pote (kutia ndani spishi 1,650 ambazo zaweza kuwa mazao ya chakula), bustani ya Amazon ndipo mahali pafaapo kwa mtafiti yeyote anayetafuta spishi za mimea ya porini. Kwa kuongezea, wakazi wa msitu huo wajua jinsi ya kutumia mimea hii. Kwa mfano, Wahindi wa Kayapo wa Brazili, hawakuzi tu namna mpya za mazao bali pia huhifadhi sampuli katika mahali pa kuhifadhi kando ya milima. Uzalishaji-mtambuko wa namna hizo za mazao ya porini na namna za mazao za kukuzwa na wakulima ziwezazo kupatwa na maradhi kwa urahisi utaimarisha nguvu na uwezo wa kustahimili hali mbaya wa mazao ya chakula cha mwanadamu. Na kichocheo hicho chahitajiwa sana, lasema FAO, kwa kuwa “ongezeko la asilimia 60 katika chakula lahitajiwa katika miaka 25 ijayo.” Japo uhitaji huo, matrekta mazito ya kusawazishia ardhi yenye kufyeka msitu yanaendelea kupenya ndani zaidi ya msitu wa mvua wa Amazon.
Matokeo ni nini? Kuharibu kwa mwanadamu msitu wa mvua kwafanana sana na mkulima kula mahindi yake ya mbegu—anatosheleza njaa yake ya papohapo lakini anahatarisha ugavi wa chakula wa wakati ujao. Kikundi cha wataalamu wa unamna-namna wa viumbe hai hivi majuzi walionya kwamba “uhifadhi na usitawi wa unamna-namna wa mazao yanayobaki ni jambo la hangaiko kuu la tufeni pote.”
Mimea Yenye Matarajio
Sasa ingia katika “duka la dawa” la kitamathali la msitu huo, nawe utaona kwamba wakati ujao wa mwanadamu unahusiana sana na mimea yenye kutambaa ya kitropiki na mimea mingineyo. Kwa mfano, alkaloidi zinazoziduliwa kutoka mimea yenye kutambaa ya Amazon hutumiwa zikiwa dawa za kutuliza misuli kabla ya upasuaji; watoto 4 kati ya 5 wenye lukemia husaidiwa kuishi muda mrefu zaidi kwa sababu ya kemikali zipatikanazo katika ua la kiwaridi aina ya konokonokwekwe lipatikanalo msituni. Msitu huo pia huandaa kwinini, itumiwayo kupambana na malaria; digitalis, itumiwayo kutibu kushindwa kwa moyo kufanya kazi; na diosgenin, itumiwayo katika vibonge vya kudhibiti uzazi. Mimea mingineyo imetoa mataraja katika kupambana na UKIMWI na kansa. “Katika Amazon pekee,” yasema ripoti moja ya UM, “kumerekodiwa spishi 2,000 za mimea ambazo hutumiwa kuwa dawa na wenyeji wa huko na zilizo na uwezekano wa kutengeneza dawa.” Ulimwenguni pote, wasema uchunguzi mwingine, watu 8 kati ya 10 hugeukia mimea ya dawa ili kutibu magonjwa yao.
Kwa hiyo ni jambo la kiakili kuhifadhi mimea inayotuokoa, asema Dakt. Philip M. Fearnside. “Kupotea kwa msitu wa Amazon kunaonwa kuwa jambo liwezalo kuwa kizuizi kikubwa sana kwa jitihada za kupata tiba ya kansa ya binadamu. . . . Wazo la kwamba matimizo yaliyo wazi sana ya tiba ya kisasa huturuhusu kuondosha kwa sehemu kubwa ugavi huu wa mimea ya porini,” aongezea, “hutokeza jambo liwezalo kuwa kiburi kibaya sana kiwezacho kufisha.”
Hata hivyo, mwanadamu anaendelea kuharibu wanyama na mimea kwa haraka sana kuliko vile iwezavyo kupatikana na kupewa majina. Inakufanya ujiulize: ‘Kwa nini ukataji miti unaendelea? Je, mwelekeo huo waweza kugeuzwa? Je, kuna wakati ujao kwa msitu wa mvua wa Amazon?’
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Hekaya ya Rutuba
Wazo la kwamba udongo wa Amazon una rutuba, lataja gazeti Counterpart, ni “hekaya ambayo ni vigumu kuiondosha.” Katika karne ya 19, mvumbuzi Alexander von Humboldt alifafanua Amazon kuwa “ghala ya ulimwengu.” Karne moja baadaye, Rais wa Marekani Theodore Roosevelt vivyo hivyo alihisi kwamba Amazon ulikuwa na taraja la ukulima wenye utokezaji. “Bara hilo bora na lenye rutuba,” yeye akaandika, “haliwezi kuachwa libaki bila kulimwa.”
Kwa kweli, mkulima ambaye huamini kama walivyoamini apata kwamba kwa mwaka mmoja au miwili, bara hilo hutokeza mazao mazuri kiasi kwa sababu jivu la miti na mimea iliyochomwa hutumika likiwa mbolea. Hata hivyo, baada ya hapo, udongo huo hugeuka kuwa usio na rutuba. Ingawa mimea ya kijani kibichi ya msitu huo hudokeza kwamba chini kuna udongo wenye rutuba, kwa uhakika, udongo huo ndiyo sehemu dhaifu ya msitu huo. Kwa nini?
Mleta-habari wa Amkeni! alizungumza na Dakt. Flávio J. Luizão, mtafiti kwenye Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti katika Amazon aliye pia mtaalamu wa udongo wa msitu wa mvua. Yafuatayo ni baadhi ya maelezo yake:
‘Tofauti na udongo mwingine mwingi wa misitu, udongo mwingi wa majaruba ya Amazon haupati virutubisho kutoka chini kuja juu, kutoka kwa mwamba wenye kuvunjika-vunjika, kwa sababu mwamba-asilia hauna virutubisho na huwa kina cha chini sana. Badala ya hivyo, udongo uliochujuliwa hupata virutubisho kutoka juu kwenda chini, kutoka mvua na taka yenye kuoza kwenye sakafu ya msitu. Hata hivyo, matone ya mvua na vilevile majani yaliyoanguka huhitaji msaada ili yawe yenye virutubisho. Kwa nini?
‘Maji ya mvua yanayoanguka kwenye msitu wa mvua hayana virutubisho vingi yenyewe. Hata hivyo, yanapogonga majani na kutiririka kwenye mashina ya miti, hayo hukusanya virutubisho kutoka kwenye majani, matawi, moss, mwani, viota vya chungu, vumbi. Kufikia wakati maji hayo yanapenya udongoni, yamegeuka kuwa chakula kizuri kwa mimea. Ili kuzuia chakula hiki cha kiowevu kutiririka tu kuingia katika vijito, udongo hutumia mtego ambao hufanyizwa na mfumo wa mizizi laini iliyoenea kotekote kwenye sentimeta chache za udongo wa juu. Uthibitisho kwa ufanyaji kazi wenye matokeo wa mtego huo ni kwamba vijito vinavyopokea maji haya ya mvua huwa na virutubisho vya hali ya chini zaidi ya udongo wa msitu. Kwa hiyo virutubisho hivyo huingia mizizini kabla ya maji hayo kuingia katika vijito au mitoni.
‘Chanzo kingine cha chakula ni taka—majani yaliyoanguka, matawi, na matunda. Tani nane hivi za taka laini huishia katika ekari mbili na nusu za sakafu ya msitu kila mwaka. Lakini taka hiyo huingiaje ndani ya udongo na katika mfumo wa mizizi ya mimea? Mchwa husaidia. Hao hukata vipande vyenye umbo la kisahani kutoka kwenye majani hayo na kuvibeba vipande hivyo kuviingiza ndani ya viota vyao vya chini ya ardhi. Hasa wakati wa msimu wa mvua, wao ni kikundi chenye utendaji mwingi, wakiingiza asilimia 40 ya taka iliyo kwenye sakafu ya msitu chini ya ardhi. Huko, wao hutumia majani hayo kutengeneza bustani kwa ajili ya kukuza kuvu. Kuvu hizi nazo huvunja-vunja mimea hiyo na kutoa nitrojeni, fosforasi, kalsiamu, na elementi nyinginezo—virutubisho vyenye thamani sana kwa mimea.
‘Ni manufaa gani ambayo mchwa hupata? Chakula. Wao hula kuvu na wanaweza kumeza vijipande fulani vya majani pia. Kisha, vijiumbe katika matumbo ya mchwa hao huwa na shughuli nyingi kugeuza chakula cha mchwa kikemikali, ili kwamba kinyesi cha wadudu hao kiwe chakula cha mimea chenye virutubisho vingi. Kwa hiyo mvua na urejeshaji wa mata ya kikaboni ni mambo mawili ambayo hufanya msitu wa mvua uendelee kuwapo na kukua.
‘Ni rahisi kuona kitakachotukia ukikata kabisa na kuchoma msitu huo. Hakutakuwa tena na matawi ya juu zaidi yatakayozuia mvua au tabaka ya taka ya kurejeshwa. Badala ya hivyo, mvua kuu zitagonga udongo ulio wazi moja kwa moja kwa kani nyingi, na mshindo wayo utafanya uso wa ardhi kuwa mgumu. Kwa wakati huohuo, nuru ya jua inayopiga udongo moja kwa moja huongeza halijoto ya uso wa ardhi na kusongamanisha udongo. Tokeo ni kwamba maji ya mvua sasa yatapita ardhini kwa kasi, yakielekea kuingia mitoni badala ya udongoni. Kupotea kwa virutubisho kutoka bara lililokatwa miti na lililochomwa kwaweza kuwa kukubwa sana hivi kwamba vijito vilivyo karibu na maeneo yaliyokatwa miti vyaweza hata kupata virutubisho vingi kupita kiasi, hilo likihatarisha uhai wa spishi za ndani ya maji. Kwa wazi, ukiachwa bila kusumbuliwa, msitu hujitegemeza, lakini ujiingilizi wa mwanadamu hutokeza msiba.’
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Athari kwa Binadamu
Utatizaji wa mifumikolojia na ukataji wa miti unadhuru si tu mimea na wanyama bali pia wanadamu vilevile. Wahindi wapatao 300,000 ni mabaki ya Wahindi 5,000,000 waliokuwa wakati mmoja wakazi wa eneo la Amazon la Brazili, bado wanaishi pamoja na mazingira yao ya msituni. Wahindi hao wanaendelea kusumbuliwa sana na wakataji wa miti, watafutaji wa dhahabu, na wengineo, wengi wao wakiwaona Wahindi hao kuwa “vizuizi vya maendeleo.”
Kisha kuna wacaboclo, watu wenye nguvu wenye uzawa mchanganyiko wa Wazungu na ukoo wa Wahindi, ambao mababu wao walikaa katika Amazon miaka ipatayo 100 iliyopita. Wakikaa katika vibanda vya milonjo kandokando ya mito, huenda hawajapata kusikia neno “ikolojia,” lakini wanategemezwa na msitu huo bila kuuharibu. Hata hivyo, maisha yao ya kila siku yanaathiriwa na wingi wa wahamiaji wapya ambao sasa wanaingia katika makao yao ya msituni.
Kwa hakika, kotekote katika msitu wa mvua wa Amazon, hakuna mataraja mazuri kwa wakati ujao wa wakusanyaji wa kokwa, wagemaji wa mpira, wavuvi, na wenyeji wengine wapatao 2,000,000, wanaoishi kwa upatano na kawaida za msitu huo na kufurika na kukauka kwa mito. Wengi huamini kwamba jitihada za kuhifadhi msitu huo zapaswa kuzidi zile za kuhifadhi miti ya mkangazi na nguva. Wanapaswa kulinda wakazi wa kibinadamu wa msitu huo vilevile.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Uhusiano wa Mti na Samaki
Wakati wa kipindi cha mvua, Mto Amazon hujaa sana na kufunika miti inayokua katika misitu ya maeneo yaliyo chini. Katika kilele cha mafuriko hayo, miti mingi katika misitu hii hutokeza matunda na kuangusha mbegu zayo—lakini, bila shaka hakuna wanyama wenye kuguguna walio chini ya maji watakaozisambaza. Hapo ndipo samaki aina ya tambaqui (Colonnonea macropomum), mvunja-kokwa mwenye hisi nzuri sana ya kunusa huchangia sehemu. Huku akiogelea katikati ya matawi ya miti iliyo ndani ya maji, samaki huyo hutambua harufu ya miti ambayo iko karibu kuangusha mbegu. Mbegu ziangukapo majini, samaki huyo huvunja magamba kwa taya zake zenye nguvu, kisha humeza mbegu hizo, kumeng’enya tunda hilo lenye nyama nyingi, na kunya mbegu kwenye sakafu ya msitu ambapo hizo huchipuka maji ya mafuriko yaishapo. Samaki na mti vyanufaika. Tambaqui huhifadhi mafuta, na mti hutokeza wazao. Kukata miti hiyo huhatarisha kusalimika kwa tambaqui na spishi nyinginezo zipatazo 200 za samaki walao matunda.
[Picha katika ukurasa wa 5]
Popo hubeba chavuo kutoka maua ya kiume hadi ya kike
[Hisani]
Rogério Gribel
[Picha katika ukurasa wa 7]
Bustani yako na duka lako la dawa
[Picha katika ukurasa wa 7]
Moto hutisha mpaka wa kijani kibichi
[Hisani]
Philip M. Fearnside