Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 5/8 kur. 3-5
  • Kutumiwa Vibaya kwa Misitu ya Mvua

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutumiwa Vibaya kwa Misitu ya Mvua
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Miti Ikuayo Jangwani”
  • Shamba, Mbao, na Nyama Zilizosagwa
  • Ni Nini Kinachofanywa ili Kulinda Msitu?
  • Huzuni kwa Msitu Huo wa Mvua
    Amkeni!—1997
  • Manufaa za Misitu ya Mvua
    Amkeni!—1998
  • Misitu ya Mvua Je, Tunaweza Kuitumia Bila Kuiharibu?
    Amkeni!—2003
  • Kutafuta Masuluhisho
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 5/8 kur. 3-5

Kutumiwa Vibaya kwa Misitu ya Mvua

HAPO zamani za kale, mshipi mkubwa wa emeraldi ulishikilia sayari yetu. Miti ya kila namna ilifanyiza muundo wake, na mito mikubwa ilipamba uso wake kana kwamba kwa gidamu.

Kama kibanda kikubwa cha kukuza mimea cha asili, ilikuwa milki ya uzuri na unamna-namna. Nusu ya spishi zote za ulimwengu za wanyama, ndege, na wadudu ziliishi huko. Lakini ijapokuwa ilikuwa sehemu yenye wingi zaidi duniani, lilikuwa pia rahisi kuharibika—rahisi sana kuharibika kuliko vile yeyote angeweza kuwazia.

Msitu wa mvua wa kitropiki, kama tuuitavyo leo, ulionekana mkubwa sana—karibu kuwa usioweza kuangamizwa. Haukuwa hivyo. Msitu wa mvua ulianza kutoweka katika visiwa vya Karibea. Mapema sana katika mwaka wa 1671—miaka kumi kabla ya ndege aliyeitwa dodo kutoweka kabisa—mashamba ya miwa yalimeza msitu katika Barbados.a Visiwa vingine katika eneo hilo vilipatwa na jambo kama hilo, mwonjo wa mwelekeo wa tufeni pote ambao umeongezeka sana katika karne ya 20.

Leo misitu ya mvua ya kitropiki hufunika asilimia 5 tu ya uso wa dunia, ikilinganishwa na asilimia 12 karne moja iliyopita. Na kila mwaka eneo la msitu lililo kubwa kuliko ukubwa wa Uingereza, au kilometa za mraba 130,000, hukatwa au huchomwa. Kiasi hiki kikubwa chenye kufadhaisha cha uharibifu chatisha kuuhukumu msitu wa mvua—pamoja na wakazi wake—kwa msiba uleule kama dodo. “Ni hatari kusema kuwa msitu utatoweka kufikia mwaka fulani kihususa, lakini isipokuwa mambo yabadilike, msitu utatoweka,” aonya Philip Fearnside, mtafiti wa msitu wa mvua katika Brazili. Diana Jean Schemo aliripoti hivi katika Oktoba ya mwaka jana: “Data katika majuma ya karibuni zadokeza kwamba kukata na kuchoma msitu kunakoendelea katika Brazili mwaka huu ni kwingi zaidi ya lililotukia huko Indonesia, ambako miji mikuu imesongwa sana chini ya blanketi za moshi ambazo zasambaa kuingia katika nchi nyingine. . . . Kuchoma msitu katika eneo la Amazon kumeongezeka kwa asilimia 28 zaidi ya mwaka jana, kulingana na data ya satelaiti, na tarakimu za kukata misitu za mwaka wa 1994, za karibuni zaidi ziwezazo kupatikana, zaonyesha ongezeko la asilimia 34 tangu mwaka wa 1991.”

“Miti Ikuayo Jangwani”

Kwa nini misitu ya mvua ambayo karibu ilikuwa haijaguswa kwa njia yenye kudhuru karne moja iliyopita, inamalizwa haraka hivyo? Misitu iliyo katika maeneo yenye halijoto la wastani, ambayo hufunika asilimia 20 ya uso wa dunia, haijapunguzwa sana katika miaka 50 iliyopita. Ni nini hufanya misitu ya mvua iwe rahisi kudhuriwa? Jibu liko katika umbo lake la kipekee.

Katika kitabu chake Tropical Rainforest, Arnold Newman, asema kwamba misitu ya mvua imefafanuliwa kwa kufaa kuwa “miti ikuayo jangwani.” Aeleza kwamba katika sehemu fulani za bonde la Amazon na katika Borneo, “kwa kushangaza misitu mikubwa, hata inashikiliwa na mchanga ambao karibu ni mweupe kabisa.” Ingawa misitu mingi ya mvua haiwezi kukua kwenye mchanga, karibu yote huwa kwenye mchanga kame, na mchanga kidogo sana, wa juu. Ingawa mchanga wa juu katika msitu ulio katika eneo lenye joto la wastani huenda ukawa na kina cha meta mbili, katika msitu wa mvua hupita sentimeta tano kwa nadra sana. Mimea yenye kuzaa sana ya dunia yawezaje kusitawi katika mazingira yenye ukame kama hayo?

Wanasayansi waligundua kitatuzi kwa fumbo hili katika miaka ya 1960 na 1970. Walipata kuwa kwa uhalisi msitu huo hujilisha kutokana nao wenyewe. Vingi vya virutubishi ambavyo mimea huhitaji hutoka kwa takataka za matawi na majani ambayo hufunika sakafu ya msitu na kwamba—kwa sababu ya joto na unyevu wa daima—kwa haraka huozeshwa na mchwa, kuvu, na viumbe vingine. Hakuna chochote kinachopotezwa; kila kitu kinafanywa upya. Kupitia mvuke na mvukizo kutoka katika kanopi ya msitu, msitu wa mvua hata hufanya upya kufikia asilimia 75 ya mvua inayopokea. Baadaye, maji yaliyofanyizwa kwa njia hii huunywesha msitu tena.

Lakini mfumo huu wa ajabu sana uko katika hali ya kuweza kudhuriwa. Ikiwa itaharibiwa kupita kiasi, haitaweza kujirekebisha. Kata sehemu ndogo ya msitu wa mvua, na katika muda wa miaka michache, itajirudisha yenyewe; lakini kata sehemu kubwa, nayo huenda haitajirekebisha kamwe. Mvua kubwa huondosha virutubishi, na jua kali huunguza sehemu ya juu iliyo nyembamba ya mchanga hadi inakuwa kwamba ni nyasi hafifu tu iwezayo kukua.

Shamba, Mbao, na Nyama Zilizosagwa

Kwa nchi zinazoendelea zisizo na mashamba ya kilimo, maeneo yake ambayo hayajaharibiwa ya msitu wa mvua yalionekana kuwa tayari na yenye kufaa kwa kutumiwa. Kitatuzi “rahisi” kilikuwa kuwatia moyo wakulima wadogo walio maskini kukata sehemu ya msitu na kuichukua—hali ifananayo na jinsi wahamaji Wazungu walivyofanya makao katika Amerika Magharibi. Hata hivyo, matokeo yalikuwa yenye kufadhaisha kwa msitu na kwa wakulima pia.

Msitu wa mvua wenye rutuba waweza kutoa wazo la kwamba chochote chaweza kukua huko. Lakini mara tu miti inapokatwa, ule udanganyifu wa rutuba isiyoisha watoweka upesi. Victoria, mwanamke Mwafrika anayelima shamba dogo ambalo familia yake ilichukua kutoka kwa msitu karibuni, aeleza tatizo.

“Baba-mkwe wangu ametoka tu kukata na kuchoma sehemu yake ya msitu ili niweze kupanda njugu, mhogo, na ndizi kadhaa. Mwaka huu napaswa kupata vuno zuri sana, lakini kwa muda wa miaka miwili au mitatu, mchanga utachoka, na itatubidi tufyeke sehemu nyingine. Ni kazi ngumu, lakini ndiyo njia tu ya kutuendeleza.”

Kuna angalau wakulima milioni 200 wanaokata na kuchoma misitu kama Victoria na familia yake! Nao wana hatia ya kuharibu asilimia 60 ya msitu wa mvua kila mwaka. Hata ingawa walimaji hawa wa kuhama wangependelea njia rahisi zaidi ya kulima, hawana uchaguzi wowote. Wakikabiliwa na pigano la kila siku ili kuendelea kuishi, wanaona uhifadhi wa msitu wa mvua kuwa starehe ambayo hawawezi kugharimia.

Huku wakulima wengi wakikata misitu kwa ajili ya kupanda, wengine huikata kwa ajili ya kulisha mifugo. Katika msitu wa mvua wa Amerika ya Kati na Kaskazini, ufugaji wa ng’ombe ni sababu nyingine kuu ya ukataji wa misitu. Nyama ya ng’ombe hawa kwa kawaida huishia Amerika Kaskazini, ambako mikahawa hudai kupata nyama ya kusagwa isiyo ghali.

Hata hivyo, wafugaji pia hupatwa na matatizo yaleyale kama wakulima wadogo. Malisho yanayomea kati ya majivu ya msitu wa mvua hayawezi kulisha ng’ombe kwa zaidi ya miaka mitano. Kugeuza misitu ya mvua kuwa nyama ya kusagwa kwaweza kuwa na faida kwa watu wachache, lakini kwa kweli iko kati ya njia za kutokeza chakula zilizo na hasara zaidi ambazo mwanadamu amewahi kutokeza.b

Tisho jingine kubwa kwa misitu ya mvua ni ukataji-miti. Si kwamba ukataji-miti huharibu msitu wa mvua kwa ukawaida. Kampuni fulani huvuna spishi za kuuza kwa njia ambayo baada ya muda mfupi msitu husitawi tena. Lakini thuluthi mbili za zile kilometa za mraba 45,000 za msitu ambazo kampuni za mbao hutumia kila mwaka zimekatwa miti sana hivi kwamba ni mti 1 tu kati ya 5 ya msitu hubaki bila kuumizwa.

“Mimi hufadhaika sana nionapo msitu maridadi ukiwa umeharibiwa kwa ukataji-miti usiodhibitiwa,” atweta mwanabotania Manuel Fidalgo. “Ijapokuwa ni kweli kuwa mimea na miti mingine yaweza kumea katika eneo lililokatwa miti, ukuzi huo mpya ni msitu wa hali ya chini—ambao ni hafifu zaidi kwa idadi ya spishi. Itachukua karne au hata mileani kabla msitu wa zamani haujajithibitisha tena.”

Kampuni za ukataji-miti pia huharakisha uharibifu wa msitu kwa njia nyingine. Walishaji wa ng’ombe na wakulima wa kuhamahama huingilia msitu hasa kwa kupitia barabara zilizotengenezwa na wakataji-miti. Nyakati nyingine mabaki ya vipande vya miti ambayo wakataji-miti huacha huanzisha mioto ya msitu, ambayo huharibu msitu mkubwa zaidi kuliko ule wakataji-miti walikata. Katika Borneo, moto mmoja kama huo ulimaliza hektari milioni moja katika mwaka wa 1983.

Ni Nini Kinachofanywa ili Kulinda Msitu?

Tutishwapo hivyo, jitihada fulani zafanywa ili kuokoa misitu iliyobakia. Lakini kazi hiyo ni kubwa sana. Mbuga za taifa zaweza kulinda sehemu ndogo tu zilizotengwa za msitu wa mvua, lakini kuwinda, kukata miti, na ukulima wa kukata na kuchoma misitu waendelea ndani ya mipaka ya hifadhi nyingi. Nchi zinazoendelea zina kiasi kidogo sana cha pesa za kutumia katika usimamizi wa hifadhi hizo.

Serikali zilizo na uhaba mkubwa wa pesa hushawishiwa kwa urahisi na makampuni ya kimataifa ili ziuze haki zao za ukataji-miti—katika visa fulani ndiyo tu raslimali ipatikanayo ili kulipia madeni ya kigeni. Na mamilioni ya wakulima wa kuhamahama wanakuwa hawana popote pa kwenda ila kuingia ndani zaidi katika msitu wa mvua.

Katika ulimwengu unaoteseka kutokana na matatizo mengi hivyo, je, uhifadhi wa misitu ya mvua ni jambo muhimu hivyo? Tuna nini cha kupoteza ikiwa misitu hiyo itatoweka?

[Maelezo ya Chini]

a Dodo alikuwa ndege mkubwa, mzito, asiyeweza kuruka aliyetoweka katika mwaka wa 1681.

b Kwa sababu ya kuteta dhidi ya hilo, mikahawa fulani imeacha kununua nyama ya ng’ombe isiyo ghali kutoka katika nchi za kitropiki.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki