Kutafuta Masuluhisho
“KATIKA kujadiliana juu ya athari zenye kuhuzunisha,” akaandika mtungaji Mwingereza John Lyly, “twaweza kukosa kuona visababishi vya msingi.” Ili kuepuka mtego huo, twapaswa kwa hakika kukumbuka kwamba athari zenye kuhuzunisha za leo kwa msitu wa mvua ni wonyesho wa uvutano wa matatizo makubwa zaidi na kwamba uharibifu wa msitu utaendelea isipokuwa visababishi vya msingi vyashughulikiwa. Visababishi hivyo ni nini? “Kani za kimsingi zinazoshambulia uhifadhi wa Amazon,” wasema uchunguzi uliodhaminiwa na UM, ni “umaskini na ukosefu wa haki wa kibinadamu.”
Ukulima Bora Usio Bora Sana
Watafiti fulani hubisha kwamba uharibifu wa msitu, kwa sehemu ni matokeo ya baadaye ya ule ulioitwa eti ukulima bora ambao ulianza miongo kadhaa kusini mwa Brazili na Brazili ya kati. Kabla ya hilo, maelfu ya familia za mashamba madogo-madogo huko yalikuwa yakijiruzuku kwa kupanda mchele, maharagwe, na viazi na kufuga wanyama vilevile. Kisha, utendaji wa kiwango kikubwa wa kutumia mashine wa kukuza maharagwe aina ya soya na miradi ya utokezaji wa umeme kwa kutumia nguvu za maji ukachukua bara lao na kubadili ng’ombe na mazao ya huko kwa bidhaa za kilimo zilizonuiwa kulisha nchi zilizoendelea. Kati ya 1966 na 1979 pekee, bara la kilimo lililotengwa kwa ajili ya mazao ya kuuzwa nje liliongezeka kwa asilimia 182. Likiwa tokeo, wakulima 11 kati ya 12 wenyeji walipoteza mashamba na riziki zao. Kwao, ukulima huo bora badala ya kuboresha maisha zao, ukatokeza huzuni.
Wakulima hawa wasio na mashamba ya kulima wangeenda wapi? Wanasiasa, wakiwa hawako tayari kushughulikia ugawaji usio wa haki wa mashamba katika eneo lao, waliwaandalia suluhisho kwa kufanya eneo la Amazon kuwa “bara lisilo na watu kwa ajili ya kutumiwa na watu wasio na bara.” Kwa kipindi cha mwongo mmoja baada ya kuzinduliwa kwa barabara kuu ya Amazon, zaidi ya wakulima maskini milioni mbili kutoka kusini mwa Brazili na kaskazini-mashariki mwa Brazili penye ukame na umaskini walihamia na kukaa katika vibanda hafifu kando-kando ya barabara hiyo kuu. Barabara nyinginezo zaidi zilipojengwa, waliotarajia kuwa wakulima walisafiri kuja Amazon, wakiwa tayari kufanya msitu kuwa bara la kilimo. Wanapotazama nyuma kwa programu hizi za uhamiaji, watafiti husema kwamba “kufikiria manufaa na hasara kwa karibu miaka 50 ya uhamiaji hakuna matokeo.” Umaskini na ukosefu wa haki “vilikuja na wahamiaji hadi Amazon,” na “matatizo mapya yakatokezwa katika eneo la Amazon” vilevile.
Hatua Tatu za Kusonga Mbele
Ili kusaidia kushughulikia visababishi vya ukataji wa miti na kuboresha hali za kuishi za mwanadamu katika msitu wa mvua wa Amazon, Tume ya Maendeleo na Mazingira ya Amazonia ilichapisha hati iliyopendekeza kwamba, miongoni mwa mambo, serikali katika majaruba ya Amazon zichukue hatua tatu za msingi. (1) Kukazia uangalifu matatizo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yaliyokumbwa na umaskini nje ya msitu wa mvua wa Amazon. (2) Kutumia misitu ambayo haijakatwa na kutumia tena maeneo ambayo tayari yamekatwa miti. (3) Kushughulikia ukosefu wa haki mbaya sana wa jamii—visababishi halisi vya huzuni ya mwanadamu na uharibifu wa msitu. Acheni tuchunguze vizuri mfikio huu wa hatua tatu.
Kuweka Rasilimali
Kukazia uangalifu matatizo ya kijamii na kiuchumi. “Moja la machaguo yenye matokeo zaidi ya kupunguza ukataji wa miti,” yaonelea tume hiyo, “ni kuweka rasilimali katika maeneo maskini sana katika nchi zilizo katika eneo la Amazon, zile ambazo hulazimisha watu kuhamia Amazon ili kutafuta wakati ujao bora zaidi.” Hata hivyo, waongeza wanatume kwamba “ni mara chache sana chaguo hili hufikiriwa katika mipango ya maendeleo ya kitaifa au ya kimkoa au na wale walio katika nchi zilizoendelea ambao huchochea mapunguzo makali katika viwango vya ukataji wa miti katika Amazon.” Hata hivyo, waeleza wataalamu hao, ikiwa maofisa wa serikali na serikali za nje zenye hangaiko zaelekeza stadi zao za kitaaluma na utegemezo wa kifedha kwa kusuluhisha matatizo kama vile ugawaji usiotosha wa mashamba au umaskini wa majijini katika maeneo yanayozunguka Amazon, zitapunguza mmiminiko wa wakulima wajao Amazon na kusaidia kuokoa msitu huo.
Ingawa hivyo, wakulima ambao tayari wanaishi Amazon waweza kufanyiwa nini? Maisha yao ya kila siku yanategemea kukuza mazao kwenye udongo ambao haufai kilimo.
Kuhifadhi Msitu ili Kutumia Miti
Kutumia na kutumia tena msitu huo. “Misitu ya kitropiki inatumiwa vibaya kupita kiasi lakini haitumiwi ifaavyo. Kusalimika kwayo kwategemea jambo hilo lenye kutatanisha,” chasema The Disappearing Forests, kichapo cha UM. Badala ya kutumia vibaya msitu huo kwa kuukata, wasema wataalamu, mwanadamu apaswa kutumia msitu huo kwa kuzidua, au kuvuna, mazao yao, kama vile matunda, kokwa, mafuta, mpira, manukato, mimea ya dawa, na mazao mengine ya asili. Inadaiwa kwamba mazao hayo, huwakilisha “thamani ya kiuchumi ya msitu huo iliyokadiriwa kuwa asilimia 90.”
Doug Daly, wa Bustani ya Kibotania ya New York, aeleza kwa nini aamini kwamba kuachana na kuharibu msitu na kuingilia uziduaji wa msitu ni jambo la kiakili: “Kufanya hivyo hutuliza serikali—hazioni sehemu kubwa za Amazon zikiondolewa kutoka ulimwengu wa biashara. . . . Kwaweza kuandaa riziki kwa watu na kuhifadhi msitu huo. Ni vigumu sana kusema jambo la kupinga hilo.”—Wildlife Conservation.
Kuhifadhi msitu huo ili kutumia miti kwa hakika huboresha hali za kuishi za wakazi wa msitu huo. Kwa mfano, watafiti katika Belém, kaskazini mwa Brazili, wamekadiria kwamba kugeuza ekari mbili na nusu kuwa mashamba ya malisho hutoa faida ya dola 25 pekee kwa mwaka. Kwa hiyo ili kupata tu mshahara wa chini wa Brazili wa kila mwezi, mtu atahitajika kuwa na ekari 120 za mashamba ya malisho na ng’ombe 16. Hata hivyo, Veja laripoti kwamba huyo mtu atarajiaye kuwa mfugaji aweza kuchuma fedha nyingi zaidi kwa kuvuna mazao ya asili ya msitu huo. Na mweneo wa mazao yangojayo kukusanywa ni mwingi sana, asema mwanabiolojia Charles Clement. “Kuna makumi ya mazao ya mboga, mamia ya mazao ya matunda, utomvu wa miti, na mafuta ambayo yaweza kukuzwa na kuvunwa,” aongeza Dakt. Clement. “Lakini tatizo ni kwamba mwanadamu lazima ajue kwamba msitu ni chanzo cha utajiri badala ya kuwa kizuizi cha kuwa tajiri.”
Fursa Nyingine kwa Bara Lililoharibiwa
Maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira vyaweza kuambatana, asema João Ferraz, mtafiti wa Brazili. “Tazama kiwango cha msitu ambacho kimeharibiwa tayari. Hakuna haja ya kukata misitu ambayo haijaguswa bado. Badala ya hivyo, twaweza kuokoa na kutumia tena maeneo yaliyokatwa miti na kuharibiwa.” Na katika eneo la Amazon, kuna mabara mengi sana yaliyoharibiwa yawezayo kuokolewa.
Kuanzia mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1960, serikali ilitoa kiasi kikubwa sana cha fedha ili kutia moyo wawekaji wa rasilimali wakuu kugeuza msitu huo kuwa mashamba ya malisho. Walifanya hivyo, lakini kama Dakt. Ferraz aelezavyo, “mashamba hayo ya malisho yaliharibiwa baada ya miaka sita. Baadaye, wakati kila mtu alipogundua kwamba lilikuwa kosa kubwa, wamiliki mashamba hao wakuu walisema: ‘Sawa, tumepata fedha za kutosha kutoka kwa serikali,’ kisha wakaondoka.” Tokeo lilikuwa nini? “Mashamba ya malisho yenye ukubwa upatao kilometa za mraba 200,000 yanaharibika.”
Hata hivyo, leo watafiti kama vile Ferraz wanapata matumizi mapya kwa ajili ya mashamba hayo yaliyoharibiwa. Kwa njia gani? Miaka kadhaa iliyopita walipanda mbegu 320,000 za mti wa kokwa ya Amazon kwenye shamba la ng’ombe lililoachwa. Leo, mbegu hizo ni miti inayotokeza matunda. Kwa kuwa miti hiyo hukua haraka na pia kuandaa mbao zenye thamani, mbegu za kokwa ya Amazon sasa zapandwa kwenye mabara yaliyokatwa miti katika sehemu kadhaa za majaruba ya Amazon. Kuvuna mazao, kufunza wakulima kupanda mazao ya misimu yote, kuanzisha njia za kupata mbao bila kuharibu misitu, na kuhuisha bara lililoharibiwa, kulingana na maoni ya wataalamu, ni vibadala vyenye ujuzi ambavyo vyaweza kufanya msitu huo uendelee kubaki.—Ona sanduku “Kufanyia Kazi Uhifadhi.”
Hata hivyo, wasema maofisa, kuokoa msitu huhitaji zaidi ya kugeuza bara lililoharibiwa. Kufanya hivyo huhitaji kugeuza hali ya binadamu.
Jinsi ya Kunyoosha Kilichopotoka
Kushughulikia ukosefu wa haki. Mwenendo usio na haki wa wanadamu unaovunja haki za wengine mara nyingi husababishwa na pupa. Na, kama mwanafalsafa wa kale Seneca alivyoonelea, “pupa haiwezi kutoshelezwa na maumbile yote ya asili”—kutia ndani msitu wa mvua wa Amazon.
Kinyume na wakulima maskini wenye kujikakamua, ambao kazi yao ya kuvunja mgongo hutokeza yahitajiwayo tu ya kulisha familia zao, wenye viwanda na wamiliki wa mashamba makubwa wanakata sana msitu huo ili kutengeneza faida nyingi. Wataalamu wataja kwamba mataifa ya Magharibi yapasa kulaumiwa pia kwa kuchangia ukataji wa miti katika Amazon. “Nchi tajiri zilizoendelea,” kikamalizia kikundi kimoja cha watafiti Wajerumani, “zimesababisha kwa sehemu kubwa madhara yaliyopo ya mazingira.” Tume ya Maendeleo na Mazingira ya Amazonia hutaarifu kwamba kuhifadhi Amazon kwa hakika huhitaji “maadili mapya ya tufeni pote, maadili ambayo yatatokeza mtindo ulioboreshwa wa maendeleo, utakaotegemea muungano na haki ya kibinadamu.”
Hata hivyo, mawingu ya moshi unaoendelea juu ya Amazon hukumbusha mtu kwamba japo jitihada za wanaume na wanawake wenye kuhangaikia mazingira ulimwenguni pote, kugeuza mawazo ya ujuzi kuwa uhakika kunathibitika kuwa jambo gumu kama kushika moshi. Kwa nini?
Mizizi ya mabaya kama vile pupa imezama kwa kina sana katika msingi wa jamii ya kibinadamu, kwa kina kirefu sana kuliko vile ambavyo mizizi ya miti ya Amazon imeingia katika udongo wa msitu huo. Ingawa twapaswa kufanya tuwezacho kibinafsi ili kuchangia uhifadhi wa msitu, si jambo halisi kutarajia kwamba wanadamu, hata wawe na moyo mweupe kadiri gani, watafaulu kuondoa visababishi vilivyo tata sana vya uharibifu wa msitu. Kile alichotaja Mfalme Solomoni wa kale, mtazamaji mwenye hekima wa asili ya binadamu, miaka ipatayo elfu tatu iliyopita bado ni cha kweli. Kwa jitihada za kibinadamu pekee, “yaliyopotoshwa hayawezi kunyoshwa.” (Mhubiri 1:15) Unaofanana na maneno hayo ni msemo wa Kireno, “O pau que nasce torto, morre torto” (Mti uliomea ukiwa kombo, hufa ukiwa kombo). Hata hivyo, misitu ya mvua ulimwenguni pote ina wakati ujao. Kwa nini?
Kuna Mnurisho Mbele
Miaka ipatayo mia moja iliyopita, mtungaji-vitabu wa Brazili Euclides da Cunha alipendezwa sana na wingi wa Amazon wa namna za viumbe hai hivi kwamba akaufafanua msitu huo kuwa “ukurasa usiochapishwa bado na wa kisasa wa Mwanzo.” Na ingawa mwanadamu amekuwa na shughuli nyingi kuchafua na kurarua “ukurasa” huo, msitu wa Amazon uliopo bado, kama ripoti ya Amazonia Without Myths isemavyo ni, “kifanano chenye kuhuzunisha cha jinsi dunia ilivyokuwa wakati wa Uumbaji.” Lakini kwa muda gani ubakio?
Fikiria hili: Msitu wa mvua wa Amazon na misitu mingineyo ya mvua ya ulimwengu hutoa uthibitisho wa, kama alivyosema Da Cunha, “akili ya kipekee.” Tangu mizizi yayo hadi majani yayo, miti ya msitu huo hutangaza kwamba hiyo ni kazi ya mikono ya msanifuujenzi mahiri. Hali ikiwa hivyo, basi, je, Msanifuujenzi huyo Mkuu ataruhusu mwanadamu mwenye pupa aharibu kabisa misitu ya mvua na kuharibu dunia? Unabii wa Biblia wajibu swali hilo kwa la yenye mkazo! Huo wasomeka hivi: “Mataifa wakawa na hasira ya kisasi, na hasira ya kisasi yako [Mungu] mwenyewe ikaja, na wakati uliowekwa rasmi kwa ajili ya . . . kuwaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.”—Ufunuo 11:18.
Hata hivyo, ona kwamba unabii huu watuambia kwamba Muumba hatafikia tu kwenye kisababishi cha tatizo hilo kwa kuondoa watu wenye pupa tu bali pia atafanya hivyo katika wakati wetu. Kwa nini twasema hivyo? Unabii huo wasema kwamba Mungu achukua hatua katika wakati ambapo mwanadamu atakuwa ‘anaiangamiza’ dunia. Maneno hayo yalipoandikwa karibu miaka elfu mbili iliyopita, wanadamu hawakuwa wengi na vilevile hawakuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Lakini hali imebadilika. “Kwa mara ya kwanza katika historia yao,” chataja kitabu Protecting the Tropical Forests—A High-Priority International Task, “wanadamu leo wako katika hali ya kuharibu misingi ya kusalimika kwao si tu katika maeneo ya watu mmoja-mmoja au sehemu fulani, lakini kwa kiwango cha tufeni pote.”
Kwa hivyo “wakati uliowekwa rasmi” ambapo Muumba atatenda dhidi ya “wale wanaoiangamiza dunia” uko karibu. Msitu wa mvua wa Amazon na mazingira mengineyo yaliyo hatarini duniani yana wakati ujao. Muumba atahakikisha kwamba hilo limetokea—na hiyo si ngano, bali ni jambo hakika.
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Kufanyia Kazi Uhifadhi
Eneo lenye ukubwa wa meta za mraba zipatazo 400,000 za miti na mimea yenye kunawiri baada ya msitu wa awali kukatwa katika jiji la Amazon ya kati la Manaus kuna ofisi kadhaa za Taasisi ya Kitaifa ya Brazili ya Utafiti katika Amazon, au INPA. Shirika hili lenye umri wa miaka 42, lenye idara tofauti-tofauti 13 zinazoshughulikia kila kitu kuanzia ikolojia hadi usimamiaji wa misitu na afya ya binadamu, ndilo shirika kubwa zaidi la utafiti katika eneo hilo. Pia lina mojawapo mikusanyo yenye viumbe wengi zaidi ulimwenguni ya mimea, samaki, wanyama-watambazi, amfibia, mamalia, ndege na wadudu wa Amazon. Kazi ya watafiti 280 wa taasisi hiyo yachangia ufahamu mzuri zaidi wa mwanadamu wa mifumikolojia tata yenye kuhusiana ya Amazon. Wageni wanaozuru taasisi hiyo huondoka hapo wakiwa na hisi ya kutumainia mazuri. Licha ya vizuizi vya kiserikali na kisiasa, wanasayansi wa Brazili na wa kutoka nchi za nje wameazimia kufanyia kazi uhifadhi wa msitu wenye kutokeza zaidi ya misitu yote ya mvua ulimwenguni—Amazon.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Barabara ya ukataji wa miti iliyochongwa kutoka kwa msitu huo
[Picha katika ukurasa wa 11]
Bidhaa kutoka msitu wa mvua: matunda, kokwa, mafuta, mpira, na mazao mengineyo mengi
[Hisani]
J. van Leeuwen, INPA-CPCA, Manaus, Brazili