Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 11/8 kur. 16-18
  • Korintho—Jiji la Bahari Mbili

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Korintho—Jiji la Bahari Mbili
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mali Yake
  • Kafilisika na Kuinuka Tena
  • Mitazamo-Nyuma Yetu
  • Mvua Ikaja!
  • Korintho “Jiji Linalomiliki Bandari Mbili”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2009
  • “Endelea Kusema na Usinyamaze”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Kupata Kuwajua Wakristo wa Kwanza
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Kitabu Cha Biblia Namba 46—1 Wakorintho
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
Amkeni!—1991
g91 11/8 kur. 16-18

Korintho—Jiji la Bahari Mbili

“WATU wa kale waliamini miungu kuwa halisi. Nyakati nyingine mimi hufikiria hivyo mwenyewe.” Kiongozi wetu akasema hivyo alipokuwa akituongoza kati ya magofu ya mahekalu yaliyowekwa wakfu nyakati za zamani kwa ibada ya Apolo, Herme, Hercules, na Poseidon. Harufu ya mvua ilikuwa hewani, na tukasikia mngurumo wa sauti ya chini ya mvua kubwa. “Zeu,” kiongozi wetu akasema kwa kutabasamu.

Mawingu meusi yalikuwa yameinuka juu ya Mlima wa Parnassus wakati wa asubuhi. Mawingu hayo yalikuwa yakitawanyika kwa haraka sana kupita ng’ambo ya Ghuba ya Korintho na kutandaa katika sehemu kubwa juu yetu. Lakini kiongozi wetu alibaki akiwa na furaha na kuendelea kutueleza hadithi za kale, tukufu za Ugiriki, na kuja kwa ukristo. Yeye kwa uchangamfu alichanganya mambo ya hakika, mambo ya kubuniwa, historia, na hekaya ili kutufanya tuwazie akilini mwetu majengo na watu wa mwili na damu wa enzi nyingine.

Sisi hatukuwa na wasiwasi juu ya mvua. Hunyesha mara chache sana katika Peloponiso. Kwani, peninsula hii ya kusini ni mojayapo sehemu zenye ukavu zaidi katika Ugiriki! Ni Athene pekee iliyo kavu kuishinda. Kwa upande mwingine, mvua ikija, siyo rasharasha tu. Huwa ni mvua kubwa kweli kweli yenye kufanyiza mitaro na kumomonyoa sehemu zilizoinuka na kufanya bara lililo chini ya uwanda wa juu wa Korintho kuwa na udongo wenye rutuba.

Kwa kushangaza! Kati ya vitu vifanyavyo Korintho iwe maarufu, hatukutarajia kimoja chao kiwe zao la shamba. Ndiyo, iwe inakuzwa kule Levant, katika California, au katika mahali pengine popote, kokote kule zabibu ndogo kavu hizo tunazoita currants zinaliwa kwa furaha, zinabeba jina la Korintho likiwa limegeuzwa kuwa “currant.”

Mali Yake

Udongo huenda ukawa moja ya sababu ya sifa ya Homer kwa “Korintho lenye mali.” Hata hivyo, Korintho lilipata wingi wa utajiri walo likiwa jiji la bandari linalotumikia bahari za Ionia na Aegea. Horace aliliita “bimarisve Corintho.” au “Korintho lenye bahari mbili.” Ingewezekanaje jiji moja liwe bandari la bahari mbili? Kwa urahisi, kwa vile lilikuwa katika sehemu ya mwisho kusini mwa bara nyembamba (Kigiriki, istho.moś) lililounganisha Peloponiso na bara la Ugiriki.

Korintho ilifaidika na bandari lenye kupata biashara ya mashariki-magharibi na kodi zilizotozwa kwa usafirishaji wa mizigo na pia meli ndogo ndogo kupitia mahali hapo pembamba kwenye shingo ya nchi iliyoitwa diól·kos na Wagiriki. Pia ilitoza kodi mizigo iliyosafirishwa katika bara ikienda kaskazini na kusini. Si ajabu kwamba Filipo wa 2, babaye Aleksanda Mkuu, aliiona Korintho kuwa muhimu katika kusitawisha kwake ufalme.

Kafilisika na Kuinuka Tena

Lakini hiyo ilikuwa karne nyingi zilizopita. Siku hizi, mfereji wa bahari unaunganisha ghuba za Korintho na Saroniki, na katika zile barabara kuu, malori hukipita kwa kasi sana kile kijiji cha Korintho kisicho na utendaji. Mabaharia, wenye malori na wanakijiji hawajali kwamba hapo zamani Korintho ilikuwa uvutio wa Mediterania. Ni wanaakiolojia na watalii tu ambao huja na vifaa vya uchunguzi, vya kuchukulia picha, na wakiwa na udadisi.

Katika 146 K.W.K. mwakilishi wa Roma Mumia aliharibu kabisa na kufanya Korintho karibu iwe ukiwa. Hata hivyo, baada ya karne moja bila utendaji, iliinuliwa na Kaisari Julio ikiwa koloni la Kirumi yenye watu wa kila namna wanaopendelea njia na mawazo ya Ugiriki.

Wakati mtume Mkristo Paulo alipofika huko karibu miaka mia moja baadaye, Korintho ilikuwa tena jiji la utendaji, lenye kusitawi. Watu wake walikuwa wakijenga, wakitengeneza sanaa, na kufanya biashara kwa kufanikiwa wakati wa mchana. Na wakati wa usiku je? Walikuwa wakila karamu na kulewa katika mahekalu ya sanamu na maduka ya mvinyo na kutembea huku na huku kwenye barabara za jiji zenye giza ili kutafuta raha ya ngono. Kwa kupendeza, ijapokuwa Korintho ilijulikana sana katika enzi hiyo ya uasherati na kila mtu alijua jinsi “msichana Mkorintho” alivyo, ukahaba wa kidini haukuwa zoea la Kigiriki. Hadithi isimuliwayo mara nyingi kwamba Korintho ilikuwa na wasichana elfu moja waliojitoa kwa Afrodito hutegemea oni lenye kutiliwa shaka la mwanajiografia Strabo wa karne ya kwanza K.W.K. Na bado, alionelea kwamba walikuwa wameishi katika wakati wa zamani wa kabla ya enzi ya Kiroma.

Mitazamo-Nyuma Yetu

Tukiwa tunatembea katika Njia ya Lechaeum, iliyokuwa njia kuu ya kale iliyounganisha bandari ya magharibi na jiji lenyewe, kiongozi wetu akaelekeza kwenye magofu ya majumba ya serikali, mahekalu, maduka, soko la nyama, na choo cha umma, zote zikiwa zimechangamana ovyo ovyo bila mpangilio wowote.a Hata hivyo, badala yake, kwa sababu ya ukosefu huo wa mpangilio mzuri wa mji, tulianza kuhisi hali maisha ya barabara yenye utendaji ambayo lazima Paulo alipata kuona— umati wenye shughuli na wapiga domo wasio na la kufanya, wenye maduka, watumwa, na wafanya biashara.

Tulipokaribia mwisho wa barabara, tulisikia gugumio la Bomba la kurusha maji juu la Pirene, lililokuwa chemchemi ya chini ya ardhi lililotoa maji baridi kwa maduka ya kuuza vitu vinavyoharibika haraka, maji ya kuoshea kwa watengeneza sanaa, na mwishowe maji ya kuvutwa kwa choo. Kama wenzi wa ndoa wakristo Akila na Prisila walikuwa na duka la kutengeneza hema katika eneo hili, hakuna ajuaye leo. (Matendo 18:1-3) Lakini kwa umbali wa meta moja hivi, katika gorofa inayokwenda hadi kwenye Baraza, wanaakiolojia walipata kizingiti cha sinagogi. Hivyo, huenda hapa palikuwa sehemu ya wayahudi, na tulifurahi kuwazia kwamba makao ya Tito Yusto huenda yalikuwa papo hapo!—Matendo 18:7.

Lile Baraza—mahali pa kuvutia kama nini! Limefanyizwa na michongo miwili yenye umbo wa mstatili katika mhimili ya mashariki-magharibi. Katikati ya mchongo wa juu, ukizungukwa na maduka pande zote mbili, kuna jukwaa lililoinuka linaloitwa bema, lililotumiwa na wasemaji katika vipindi rasmi. Kiongozi wetu alitukumbusha kwamba wakati tabibu Luka alipoandika juu ya siku ya Paulo mahakamani mbele ya Liwali Galio, neno la kigiriki lililotumiwa kwa “kiti cha hukumu” lilikuwa ni bema. (Matendo 18:12) Hivyo, matukio ya Matendo 18:12-17 huenda yalitukia mahali papo hapo! Tulikuwa tumesimama mahali ambapo yaelekea Paulo angesimama, tayari kujitetea huku amezungukwa na Wayahudi wanaomshtaki. Lakini la! Galio haisikizi kesi hiyo. Badala yake aachilia Paulo na kuruhusu umati wenye jeuri kumcharaza Sosthene.

Nyuma ya hiyo mahakama ya nje, katika sehemu ya mwisho ya kaskazini mwa mchimbo wa chini, lipo ‘chemchemi takatifu’ na mahali payo panaposemekana kuwa mungu fulani alizungumzia wanadamu. Kuna maoni tofauti jinsi mungu huyo alivyozungumza. Hata hivyo, inaonekana kwamba ikiwa mwenye kuomba alilipa pesa za kutosha, makasisi walifanya “muujiza” na kugeuza maji ya chemchemi kuwa divai. Ikidhaniwa kwamba tendo hilo lilihakikishia mwenye maombi kwamba alikuwa karibu kufunuliwa kwa nguvu zisizo za kawaida. Wanaakiolojia wasema kwamba mahali hapo pa ibada palikuwa pakitumiwa kwa muda mrefu sana, katika Korintho ya kale ya kabla ya Ukristo na katika jiji la Korintho lililojengwa Upya la siku za Paulo. Tukichunguza katika mpito wa siri, tuliona njia ya ufanyizaji wa ujanja wa divai na tukatoka tukiwa tumeridhika kwamba wadanganyaji wa kidini si wapya.

Ingawa Poseidon anafikiriwa kuwa mungu mfadhili wa Korintho, jumba linalostaajabisha kushinda zote ni hekalu la Apolo lenye mtindo wa Doric. Kati ya nguzo zake 38, nguzo 7 bado zabaki zikiwa zimesimama. Zikiwa na urefu wa kuenda juu wa karibu meta 7.2 na urefu wa kipenyo wa meta 1.8 kwenye msingi, kila kimoja cha nguzo hizo kimetengenezwa kwa chokaa yenye nakshi ya mifuo ambayo hapo awali kilipakwa chokaa ya kukandika iliyo ngumu, na nyeupe. Likiwa limeinuka juu ya jiji kwenye mwinuko wa kati —gofu jeusi kati ya magofu—hekalu hilo la kale hata hivyo huendelea kuamsha hisia za ndani. Hekalu hilo laweza kukumbusha anayeitazama kile alichoandika Goethe—ufundi huo ni “muziki ulioganda.”

Mvua Ikaja!

“Njooni. Kuna mengi zaidi ya kuona!” splash. “Bado hatujaona mahekalu yenye majiko na vyumba vya kulia vyenye uzuri.” Splat. “Ni lazima tuone sakafu ya mawe iliyowekwa msingi na Erastus.” Splatter. “Na hamtaki kukosa kuona jumba la mvinyo la Afrodito au lile la Aeskulapeamu.” Naam, matone ya mvua makubwa makubwa yalikuwa ishara ya mvua kubwa ya upepo.

Kwa ghafula, watu na majengo tuliyokuwa tukiwazia juu yao yalitoweka. Tukarudi haraka tulikotokea, huku kiongozi wetu akitaja vitu vingi ambavyo hatukuwa tumeona. Matone ya mvua sasa yakitiririka yaligeuza sakafu ya mawe kuwa rangi za unyevu zenye uangavu na kutoa vumbi kwenye marmar ya majengo ambayo hapo awali yalikuwa yakijivunia sifa. Mvua kubwa ilipoanza, tulikimbia. Bado tungeweza kusikia kiongozi wetu akiwa huko mbele akiitana: “Kujeni, kila mmoja!” Katika mvua hiyo nzito, hata majengo nusu nusu kando kando ya Njia ya Lechaeum ya Korintho yalitoweka. Hakuna kilichosalia, wala umbo la bara wala kwa mawazo. Tukiwa tumelowa maji, tuliikimbilia basi yetu huku tukitumaini kwamba dereva hakuwa ameondoka kwenda kunywa kahawa.—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

a Soko la nyama (Kigiriki, maḱel·lon): Duka lililouza nyama na samaki na pia vitu vingine vingi.—1 Wakorintho 10:25.

[Ramani katika ukurasa wa 16]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Korintho

UGIRIKI

BAHARI YA IONIA

BAHARI YA AEGEA

[Picha katika ukurasa wa 17]

Juu: Duka lililojengwa upya katika lile Baraza

Katikati: Ile “bema”

Chini: Hekalu la kale la Apolo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki