“Hivi Ndivyo Tunavyofua Nguo Zetu. . . ”
KATIKA mabara mengi maneno hayo yanajulikana sana kwa vizazi vingi vya watoto ambao wameimba kwa furaha na kucheza wimbo huu unaojulikana sana. Na ikiwa wazo la kufua nguo halikufurahishi sana, hebu fikiria: Baada ya kuoga, je! haistareheshi kujipangusa kwa kitambaa cha kujipangusia kilicho laini, na safi? Ni mtu gani hajisikii nadhifu na ustarehe anapokuwa amevaa nguo safi? Kwani, hata watoto huonekana wakifurahia kuvaa nguo ambazo ni safi na zenye kunukia—hata kama ni kwa muda mfupi tu!
Hivyo kufua nguo zetu ni jambo la maana sana kwa maisha yetu na afya yetu kushinda vile sisi hudhania. Hata hivyo, jinsi sisi hufua nguo zetu huenda ikategemea tunakoishi duniani.
Kufua Bila Mashine za Kufua
Katika mabara mengi yaliyoendelea, neno “kufua” nyakati zote limeunganishwa na neno “mashine.” Hata hivyo, katika mabara yenye ufukara, ufuaji bado mara nyingi hufanywa kwa mikono, na kwa kushangaza matokeo huwa mazuri! Chukua, kwa mfano, zile nguo nyeupe zilizo ngumu kufuliwa. Katika nchi zenye hali ya ujoto na ukavu, wanawake hutumia jua kwa manufaa yao.
Utaratibu wa kufuata ni rahisi. Beseni inajazwa maji na sabuni ya kutosha. Nguo nyeupe zinazamishwa ndani, na mikono ya wafuaji wenye bidii inatikisa maji na kusugua maji yenye povu kwenye nguo. Ikiwa hakuna dawa za dukani za kufanya nguo iwe nyeupe, wengine hutumia vitu vya kale kutia vyeupishaji, kama vile siki ya nazi. Kisha, baada ya kusuzwa haraka nguo hizo zenye maji huanikwa kwenye vichaka vinavyofaa au ua linalofaa na kutiwa weupe kabisa na jua. Sasa inarudishwa kwenye beseni na kusuzwa mara kadhaa na kukaushwa kwa mara ya pili chini ya jua kali la kitropiki. Matokeo? ni nguo nyeupe zinazong’aa kwa usafi!
Mke aishiye nyumbani karibu na mto au kijito huenda akajaribu njia tofauti kidogo. Kwanza achagua mahali pazuri, kama ukingo unaotelemka vizuri kuingia ndani ya maji. Iwapo mto ni wa kwenda kasi, basi achagua kwa uangalifu kiingilio cha maji mahali patulivu ambapo patasaidia nguo zake zisipelekwe na mkondo wa maji. Au kuna mwamba karibu? Sawasawa. Mke huyo wa nyumbani sasa atumia kibao kama mwiko kupiga nguo zenye maji kwenye mwamba. Uchafu huondoshwa kabisa kutoka nguoni.
Mashine za Kufua—Za Kikale na za Kisasa
Katika mabara yaliyoendelea mashine za kufulia nguo zimeondoa ufuaji wa kutumia mkono. Lakini mashine za kufua ni za kale kushinda unavyoweza kudhania. Wakati wa Enzi za Kati katika Ulaya, beseni ya kufulia ndiyo iliyokuwa njia ya wengi kufulia nguo hadi ilipobadilishwa pole kwa pole na mashine za kutumia mvuke. Baadaye, katika karne ya 19, kulitokea mashine ya kufua inayofanana na ya kisasa. Katika 1830 dobi moja ya Uingereza ilifua nguo kwa kutumia bomba lililorusha-rusha nguo katika maji moto yenye sabuni. Njia hii ya msingi haijabadilika hadi leo hii.
Hata hivyo, mashine ya kufua ilichukua muda kuanza kutumiwa na watu wengi. Watumiaji wa mashine ya kuzungushwa na mkono waliipata kuwa inachosha mwenye kuitumia na kuharibu nguo. Hivyo kufikia mwisho wa karne ya 19, mbao zilizo na mikunjo-kunjo za kufulia, beseni, na mashine ya kuendeshwa kwa mkono zilikuwa vifaa vya uchaguzi kwa wake wengi wa nyumbani.
Hata hivyo, mashine ya kufua ilitokea tena katika 1910 wakati mashine ya kutumia nguvu ya umeme ilipotokea. Miaka kumi na mbili baadaye, mashine ya kwanza ya kutikisa-tikisa ilitokea. Tangu wakati huo, maendeleo mengi na marekebisho mengi yamefanywa kwa mashine za kufua. Kampuni nyinginezo zimeanza hata kuuza mashine zenye kutumia kompyuta hivi kwamba kugusa tu kibonyezo ‘kunaamua kadiri ya uchafu wa nguo zako na kisha kuchagua sabuni ya kufaa zaidi na njia bora zaidi ya kuzifua.’—Popular Science, Julai 1990.
Vidokezo vya Kutumia Mashine za Otomatiki
Mashine ya kufua ya otomatiki ya kawaida hupatikana katika nyumba nyingi za Magharibi. Hata hivyo, neno “otomatiki,” halimaanishi kwamba inaweza kutumiwa tu bila kufikiri kwa uangalifu. Kwa mfano, katika mashine ya kufua nguo nyingi, uzito usiolingana wa nguo waweza kuzungusha mashine hiyo kwenye sakafu wakati izungushapo nguo na kuharibu kila kitu kilicho kwenye chumba chako cha kufulia. Mioshi hatari yaweza kutokea ukitumia dawa ya kuua vijidudu ya klorini pamoja na amonia. Hivyo fuata njia za msingi za usalama. Usiweke mikono yako ndani ya mashine mpaka utendaji wowote ule wa mashine usimame. Utoe kwanza plagi ya umeme kabla ya kujaribu kuifanyia kazi ya marekebisho. Na usiwache watoto wako waiendeshe wala waichezee mashine yako ya kufua.
Lakini wawezaje kuwa na uhakika kwamba utapata matokeo mazuri unapofua nguo? Hapa pana madokezo kadha ya msingi:
◻Toa vitu vyote mifukoni, ukigeuza mifuko nje.
◻Kunjua sijafu za mikono ya nguo, na kupiga brashi uchafu wowote uwezao kutoka.
◻Funga kamba na mishipi ili zisifungamane pamoja.
◻Vuta zipu, vifungo, vyango vya nguo, ili visishikane na vitu vingine.
◻Toa alama na mawaa kabla ya kufua.
◻Usiweke nguo kupita kiasi. Hiyo yaweza kuwa na matokeo ya ufuaji usio safi, yaweza kuongeza mikunjo ya nguo, ifumue nguo, na kuharibu nguo zako.
Ni kweli, wengi bado hufua nguo zao kwa mtindo wa kikale—kwa mkono. Lakini hata mashine yako ya kufua iwe ni beseni ya chuma, kijito chenye kwenda kwa kasi, au kompyuta ya hali ya juu, matokeo yaweza kufanya jitihada zako ziwe zafaa—nguo safi, zenye kutakata kwa ajili ya wewe na familia yako, na pia uradhi wa kazi iliyofanywa vema!
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kufua kando ya mto
Kutia weupe katika jua