“Mimi Ni Macho Yake Naye Hutumika Kama Miguu Yangu”
JOSÉ Luis Escobar na Artemio Duran wanatumikia wakiwa wazee katika kundi la Kikristo la Mashahidi wa Yehova katika Meksiko. José Luis ni kipofu, na Artemio hawezi kutembea.
Alipokuwa na umri wa miaka 16, José alipendelea ndondi. Siku moja alialikwa achukue mahali pa mwanandondi wa kulipwa katika pigano. Kufikia raundi ya nne, wote wawili walikuwa wamechapana vibaya sana hata ikawa lazima kusimamisha pigano. Ingawa ushindi ulipewa José Luis, mapigo aliyopata yalimpofusha.
José Luis alienda kuwaona madaktari kadhaa na pia aliwaendea wawasiliani-roho waovu. Lakini hakuna yeyote aliyeweza kumsaidia. Kwa kukata tamaa, alijaribu kujiua mara kadhaa. Baadaye alitembelewa na Mashahidi wa Yehova, akajifunza kweli za Biblia, na hatimaye akaweka wakfu maisha yake kwa Mungu. Alibatizwa Agosti 1974.
Kwa upande ule mwingine, Artemio alipatwa na aksidenti mbaya sana ya motokaa katika 1981. Jambo hilo lilitukia wakati alipokuwa akiishi na kufanya kazi isivyo halali katika United States. Wawakilishi wa dini mbalimbali walimtembelea hospitalini na kumwambia kwamba alikuwa anaadhibiwa na Mungu kwa sababu ya njia yake mbaya ya maisha. Baadaye Artemio alitembelewa pia na Mashahidi wa Yehova. Alijifunza Biblia, akafanya mabadiliko yaliyohitajiwa katika maisha yake, naye akabatizwa Mei 1984.
Sasa wanaume hao wawili ni waandamani katika kundi moja la Kikristo. Wanaandamana kwa ukawaida katika huduma ya nyumba kwa nyumba, wanafanya pamoja ziara za kurudia wenye kupendezwa, na kutembelea washiriki wa kundi ili kuwajenga kiroho. José Luis hukisukuma kiti cha mgonjwa chenye magurudumu naye Artemio humwelekeza mahali pa kwenda. Artemio huongea juu yao kuwa kitu kimoja: “Mimi ni macho yake naye hutumika kama miguu yangu.”