Ukipoteza Kazi Suluhisho Ni Nini?
“Itakuwa katili. Biashara nyingi zimedhoofika, lakini bado hazitakubali.”—Mkopesha fedha wa U.S.
WENGI tayari wameona uhalisi wa utabiri huo, uliofanywa mwishoni mwa 1990. Katika makampuni mengine, waajiriwa “waliobaki” waliwaziawazia ikiwa wao ndio watakaofuata kufutwa.
Ungefanyaje ikiwa ungepoteza kazi yako leo? Ni jambo la hekima kujitayarisha. Kama vile makala iliyotangulia imedokeza, kupoteza kazi hutokeza pigo la kiuchumi na la kihisia. Basi, mengi yanatiwa ndani zaidi ya kulipa deni tu. Inayofuata ni baadhi ya miongozo ambayo imesaidia wengine waendelee kuwa imara kiuchumi na kihisia walipokabili ukosefu wa kazi.
1. Usiwe na Hofu Kuu
Dominick alipopoteza kazi yake, ilimbidi kurudisha nyumba yake kwa benki na ahamishe familia yake waishi na mama yake. Ushauri wake ni kubaki ukiwa mtulivu, bila kujali hali ni mbaya kadiri gani. “Uwe au usiwe na kazi, hautakauka au kuisha,” anasema. “Nilijifunza kwamba sisi sote hatungekufa.” Badala ya kujaza akili na mawazo mabaya, fanyia kazi kwa utulivu suluhisho zenye matokeo.
2. Fikiria kwa Mwelekeo Mzuri
Jim na Donna wana kazi nne za nusu wakati miongoni mwao. Hata hivyo, mapato yao ni ya chini kuliko wakati Jim alikuwa anafanya kazi ya wakati wote. Licha ya hilo, wameliona kuwa fundisho kwa watoto wao watano. Donna alisema: “Bila matatizo hayo wangekuwa na hali nzuri sana ya vitu vya kimwili. Lakini wangekosa shida ambazo hufunza mtu jinsi ya kuishi.”
3. Fungulia Akili Yako Aina Mpya za Kazi
Hata wafanya kazi wa ofisini wanaweza kuchagua kubadilisha stadi na kuanza kazi mpya. “Watu huwa hawaangalii mambo mengine hadi hali iwalazimishe,” akasema Laura, ambaye aliondoshwa katika kazi ya usimamizi. “Katika miaka ya 90,” akasema, “watu wanapaswa kujifunza kuwa wenye kubadilika na hali.” Kujaribu kutafuta aina ya kazi ambayo unaifahamu—au yenye malipo sawa—kunaweza kupoteza nafasi zako za kupata kazi. Hili laweza angalau kueleza ni kwa nini huwachukua wafanyakazi wa ofisini muda mrefu kupata kazi kuliko wafanyakazi wa kazi ngumu-ngumu. Kwa hivyo fungulia akili yako uwezekano wa aina mpya za kazi. Wengi wamefanikiwa kwa kujitolea kufanya aina fulani za utumishi kwa wengine, kama vile utunzaji wa nyumba.
4. Ishi kwa Uwe wa Mapato yako Mwenyewe—Si ya Mwingine
Zana yenye nguvu sana katika matangazo ni kutokeza “uhitaji” ambao haukuwako. Mara nyingi unafanywa uhisi kwamba kila mtu (isipokuwa wewe) anajua na anashughulikia uhitaji huo. ‘Huu ndio mtindo anaovaa kila mtu [isipokuwa wewe].’ ‘Sinema inayosemwa na kila mtu [kwa nini hujaiona?].’ ‘Gari analoendesha kila mtu [utalinunua lini?].’
Vivyo hivyo sihi kama hiyo yaweza kuathiri jinsi tuonavyo na kutumia pesa zetu. Rafiki anafunga safari yenye gharama ya juu. Kwa ghafula unahitaji likizo. Rafiki mwingine ananunua gari. Kwa ghafula gari lako laonekana kuwa limechakaa, lisilofaa. Kuwa na wivu wa kila kitu kinachofanywa na wengine kwaweza kukufanya utumie pesa usizonazo, ukinunua vitu ambavyo huhitaji sana. Epuka aina hiyo ya milinganisho.
Jim, mfanyakazi aliyefutwa aliyetangulia kutajwa, alionelea: “Watu huvunjika moyo wakishindwa kufuatia mtindo wa maisha wanaofikiri wanataka. Unapaswa kuhangaikia chakula na makao tu. Mengine kwa kweli ni yasiyo ya lazima.” Kama vile Biblia ishaurivyo katika 1 Timotheo 6:8, ‘ridhika na chakula na nguo.’
5. Uwe Mwangalifu na Mkopo
Kadi ya mkopo yaweza kuwa kitu muhimu, lakini pia yaweza kuwa dhima yako kubwa. Wengine hutumia kadi ya mkopo kuwa tegemezo. Wanaitumia kuachilia kabisa swali la ‘Je! nina uwezo wa kuipata?’ Kadi hiyo inakuwa kituliza-maumivu ambacho hukufanya ununue bila kufikiri au kuhisi athari za kupoteza pesa.
Katika miaka ya karibuni kichaa cha kadi za mkopo kimekumba nchi nyingi. Matokeo ni nini? Mwuzaji kompyuta kutoka Korea ambaye alinunua gari jipya kwa kadi ya mkopo alisema kuhusu jambo hilo: “Wakati ufikapo wa kulipa mkopo, sikuzote mimi huhisi vibaya sana. Ni kama tu nilipeana pesa hizo bure.” Katika Japan karibu nusu ya wote wanaotafuta ushauri wa kiuchumi wako katika miaka yao ya 20. Kadi za mkopo milioni 140 katika nchi hiyo zinasababisha kwa kiwango cha juu deni ambazo vijana wanazo.
Kwa hivyo uwe mwangalifu na kadi za mkopo. Itumie, lakini usiiwache ikutumie wewe. Usiiwache ikupofushe usione hali yako ya kiuchumi jinsi ilivyo. Hili litaongezea tu mkazo wa akili wa kupoteza kazi.
6. Endeleza Umoja Katika Familia
Katika uchunguzi wa watu 86,000, zaidi ya theluthi moja walisema kwamba pesa zilikuwa tatizo namba moja katika ndoa zao. Uchunguzi mwingine ulionyesha kwamba pesa zilisababisha vita vingi kati ya vile vilivyopiganwa. “Mielekeo tofauti juu ya pesa inaweza kuharibu uhusiano,” akasema mshauri wa kiuchumi Grace Weinstein.
Hata wenzi walio karibu sana wanaweza kuwa na maoni tofauti sana kuhusu pesa na jinsi zinapasa kutumiwa. Mwingine anaweza kuwa mwenye akiba sana, na mwingine mwenye kutumia sana kwa pupa.
Mambo ya pesa yasipozungumzwa, yanaweza kutokeza vita vya familia. “Pasipo mashauri makusudi hubatilika,” yasema Biblia kwenye Mithali 15:22. Na mzungumzapo mambo ya kifedha, jaribu kuelewa na kutumia maoni ya mwenzi wako.
7. Endelea Kujistahi
Grace Weinstein alionelea: “Mwanamume au mwanamke ambaye hapokei mapato tena, ana tatizo la kihisia la hali za kupungukiwa na upungufu wa tegemezo, yote hayo yakileta ukosefu wa kujistahi.”
Usikate kauli mara moja kwamba ulifutwa kwa kuwa haustahili kuwa mfanyakazi. Rani mwenye umri wa miaka ishirini na tisa alifutwa tu baada ya majuma matatu ya kuongezewa mshahara wa juu sana katika daraja lake kwenye ukaguzi wa kazi yake kila mwaka. Ijapokuwa kuwa mnyofu, na mfanyakazi mwenye kuaminika kwaweza kumfanya mtu asifutwe, siku zote haiwi hivyo. Kwa hiyo mtu hapaswi kuona hastahili kufutwa kazi. Wafanyakazi wenye kuthaminiwa,na wenye kutegemeka pia huenda wakaathiriwa.
Panga Bajeti
Wengi hujikunyata kwa wazo la kupanga bajeti. Wanahisi kwamba ni kama kifungo, ambacho kitawazuia kununua wanachotaka. Sivyo ilivyo. Bajeti ni chombo cha kukusaidia ufikie miradi yako, si kizuizi. Ni njia tu ya kujidhibiti, mpango wa kukusaidia kujua pale pesa zako zinakoenda na jinsi ya kuzifanya ziende pale unapotaka.
Kwa kushangaza, wengi hawajui pale pesa zao zinatumika. Badala yake, wanakuwa wa kununua vitu tu wanapoviona na baadaye kuomboleza: “Zote zilienda wapi?” Uhitaji wa kuepuka utumizi wa aina hiyo wa pesa ni wa maana hasa wakati nyakati ni ngumu kiuchumi. Biblia yasema kwa hekima kwenye Mithali 21:5: “Panga kwa uangalifu na utakuwa na wingi; ikiwa utafanya haraka haraka, hautakuwa na utoshelezo kamwe.”— Today’s English Version.
Ili kufuata shauri hili, andika rekodi. Andika kila kitu unachotumia kwa mwezi wote mzima, ukigawanya matumizi yako. Pia, weka rekodi ya kiwango cha pesa kinachokuja. Ikiwa unaona kwamba nyingi zinatumika kuliko zinazoingia, tazama matumizi yako ujue shida inatokea wapi. Unapojua kiasi cha pesa unazotumia na unakozitumia, unaweza kudhibiti hali yako ya fedha.
Fanya bajeti yako iwe yenye kubadilikana. Katika majuma machache ya kwanza, makosa yataonekana, na baadhi ya gharama zinaweza kusahauliwa. Usahihishe na kurekebisha bajeti yako hadi itosheleze mahitaji yako. Hivyo bajeti nzuri ya matumizi itakuwa mtumishi wako, si bwana wako.a
Miongozo iliyo juu huenda ikasaidia mtu avumilie kipindi cha ukosefu wa kazi. Lakini ili iwe na matokeo, madokezo haya ni lazima yasawazishwe na kadirio linalofaa la umaana halisi wa pesa. Kwa kweli, ni la maana kadiri gani? Je! lolote lapaswa kuwa la kwanza kabla ya pesa, hata ikiwa mtu amepoteza kazi yake? Tutachunguza maswali haya katika makala inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa ajili ya msaada zaidi juu ya kupanga bajeti, ona Amkeni!, Aprili 22, 1985, kurasa 24-7. (Kiingereza).
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Kutayarisha Bajeti
1. Piga hesabu ya pesa zinazoingia.
2. Weka rekodi ya mwezi mzima ili ujue pesa zako zinatumikaje.
3. Tayarisha bajeti inayotegemea hatua hizo mbili za kwanza. Amua ni kiasi kipi kitagawanywa katika kila hali.
4. Fanya marekebisho kwa bajeti yako kama ihitajiwavyo.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wenzi wa ndoa wanapaswa kuwasiliana ili mambo ya pesa yasigeuke kuwa vita vya familia