Jinsi ya Kujiepusha na Deni
KATIKA nyakati hizi zenye kubadilika, kushughulikia mapato ya familia kwaweza kuwa jambo gumu. Waweza kukabilije ugumu huo kwa mafanikio?
Jibu si lazima liwe kuchuma fedha zaidi. Wataalamu wa kifedha husema kwamba jibu lahusiana na kujua mahali zinakotoka fedha na mahali zinakoenda na vilevile kuwa tayari kufanya maamuzi yafaayo. Ili kufanya hili, wahitaji bajeti.
Kushinda Ukinzani Dhidi ya Bajeti
Hata hivyo, kufikiria bajeti “hutokeza mawazo tofauti-tofauti yasiyopendeza,” asema mshauri wa kifedha, Grace Weinstein. Kwa hiyo, watu wengi hawatayarishi yoyote. Wengine pia huhusianisha kuhitaji bajeti na mapato ya chini au ukosefu wa elimu. Lakini hata wataalamu wenye mapato ya juu wana matatizo ya kifedha. Mshauri mmoja wa kifedha asema: “Mmoja wa wateja wangu wa kwanza alikuwa akipata dola 187,000 kwa mwaka . . . Deni lao la kadi ya mkopo pekee lilikuwa chini tu ya dola 95,000.”
Michael, aliyetajwa mbeleni, alisita kutafuta msaada wa kifedha kwa sababu nyingine. Yeye akiri: “Nilihofu kwamba wengine wangeniona kuwa asiyejua mambo na mpumbavu.” Lakini hofu kama hiyo haina msingi. Kushughulikia fedha huhitaji namna tofauti ya ustadi mbali na kuchuma fedha, na watu wengi hawajazoezwa kushughulikia fedha. Mfanyakazi wa kijamii ataja: “Sisi huhitimu kutoka shule ya sekondari tukiwa twajua mengi zaidi kuhusu pembetatu pacha kuliko jinsi ya kuweka fedha akiba.”
Ingawa hivyo, kutayarisha bajeti ni rahisi kujifunza. Huhusisha kutengeneza orodha ya mapato na orodha ya matumizi—na kuzuia matumizi yasipite mapato. Kwa kweli, kutayarisha bajeti kwaweza kufurahisha, na kuishi kupatana nayo kwaweza kutosheleza.
Kuanza
Acheni tuanze kwa kutengeneza orodha ya mapato. Kwa wengi wetu, hii yapasa iwe rahisi kwa sababu kwa kawaida huhusisha vitu vichache tu—mshahara, mapato ya ziada kutoka akaunti ya akiba, na kadhalika.
Lakini usifanye mipango kwa mapato yasiyo hakika, kama yale yatokanayo na malipo ya ovataimu, bakshishi, au zawadi. Washauri wa kifedha huonya kwamba kupanga kulingana na vyanzo vya mapato visivyo vya uhakika kwaweza kukuingiza katika deni. Mapato hayo yakijitokeza, huenda ukachagua kutumia fedha hizo kujifurahisha pamoja na familia, kusaidia walio na uhitaji, au kuchangia panapostahili.
Hata hivyo, kutengeneza orodha ya matumizi kwaweza kutatanisha kidogo. Robert na Rhonda, waliotajwa katika makala zilizotangulia, hawakuweza kufahamu fedha zao zilizochumwa kwa jasho zilikokuwa zikienda. Robert aeleza jinsi walivyotatua tatizo hilo: “Kwa mwezi mmoja kila mmoja wetu alibeba kipande cha karatasi na kuandika kila ndururu tuliyotumia. Hata tuliandika fedha tulizotumia kwa kikombe cha kahawa. Na mwishoni mwa kila siku, tuliingiza kiasi hicho katika kitabu cha bajeti nilichokuwa nimenunua.”
Kurekodi kwa uangalifu fedha zote unazotumia kutakusaidia ujue fedha zilitumiwa kwa vitu gani. Hata hivyo, ikiwa wajua mazoea yako ya utumizi, huenda ukaamua kuepuka kuweka orodha yenye mambo mengi ya fedha unazotumia kila siku na kuendelea kutengeneza makadirio ya fedha ya kila mwezi.
Kuorodhesha Gharama za Kila Mwezi
Huenda ukataka kutengeneza chati kama inayoonyeshwa hapo juu. Katika safu ya “Matumizi Hususa,” weka kiasi unachotumia wakati huu kwa kila kitu. Punguza idadi ya sehemu kuu, kwa kutumia vichwa kama vile “chakula,” “nyumba,” na “mavazi.” Hata hivyo, usisahau sehemu ndogo za maana. Kwa Robert na Rhonda, sehemu kubwa ya fedha zao ilikuwa ikitumiwa kula katika mikahawa, kwa hiyo kutenganisha “kula mikahawani” na “ununuzi wa vyakula” kulisaidia. Ikiwa wewe hufurahia kukaribisha wageni, hii pia yaweza kuwa sehemu ndogo chini ya “chakula.” Wazo ni kufanya chati hiyo ionyeshe utu na mapendezi yako.
Unapotengeneza chati yako, usisahau gharama za baada ya kila miezi mitatu, nusu mwaka, kila mwaka, na gharama nyinginezo za pindi kwa pindi, kama vile malipo ya bima na kodi. Ingawa hivyo, kuviongeza katika chati ya kila mwezi, itakubidi ugawanye kiasi cha fedha kwa idadi ifaayo ya miezi.
Kitu muhimu katika orodha ya gharama ni “akiba.” Ingawa huenda wengi wasione akiba kuwa gharama, utapangia kwa hekima baadhi ya mapato yako ya kila mwezi kwa ajili ya hali za dharura au makusudi ya kipekee. Grace Weinstein akazia umuhimu wa kutia ndani akiba katika orodha yako ya gharama: “Ikiwa huwezi kufaulu kuweka akiba angalau asilimia 5 ya mapato yako baada ya kodi (na hicho ni kiwango cha chini kabisa), itakulazimu kuchukua hatua kali. Achana na madeni, panga tena mtindo wako wa kuishi, na ufikirie mahitaji yako ya msingi.” Ndiyo, kumbuka kutia ndani akiba katika bajeti yako ya kila mwezi.
Ili kupunguza athari ya matatizo wakati wa ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, wakati huu hupendekezwa kwa kawaida kwamba ujaribu kuweka akiba iwezayo kupatikana kwa urahisi ya angalau mapato ya miezi sita. “Ukiongezwa mshahara,” asema mshauri wa kifedha, “weka akiba nusu yao.” Je, wahisi kwamba huwezi kuweka akiba?
Fikiria Laxmi Bai, ambaye sawa na wengi katika sehemu za mashambani za India ni maskini sana. Yeye alianza kuweka kando katika nyungu konzi moja ya mchele kutoka fungu la kila siku alilopikia familia yake. Baada ya kipindi fulani, alikuwa akiuza mchele huo na kuweka akiba fedha hizo katika benki. Hii ilikuwa hatua ya kupata mkopo wa benki ili kumsaidia mwana wake kuanzisha kibanda cha kurekebisha baiskeli. Akiba hizo ndogo-ndogo zimeleta mabadiliko yenye maana katika maisha za wengi, laripoti India Today. Hilo limefanya kujitegemea kiuchumi kuwe jambo halisi kwa watu fulani.
Hata hivyo, kusawazisha bajeti ni zaidi ya kutengeneza orodha ya mapato na gharama. Huhusisha kudhibiti gharama zisipite mapato, jambo ambalo huenda likahitaji kupunguza matumizi yako.
Je, Ni Muhimu?
Ona kichwa “Ni Muhimu?” kwenye fomu katika ukurasa 9. Safu hii ni ya maana sana kuifikiria, hasa ikiwa unapata kwamba jumla katika safu ya “Kiasi Kilichopangiwa” ni kuu kuliko mapato yako. Hata hivyo, kuamua ikiwa kitu ni muhimu na ni kiasi gani cha fedha kinachohitajiwa kwa ajili yacho kwaweza kuwa tatizo. Ndivyo ilivyo hasa katika nyakati hizi zenye kubadilika wakati ambapo tunaletewa kwa wingi na kwa mfululizo bidhaa mpya ambazo zatangazwa kuwa ni mahitaji. Kupanga kila gharama kulingana na uhitaji hususa, uhitaji uwezekanao, au anasa ambayo ni nzuri kuwa nayo kutasaidia.
Tazama kila gharama ambayo umeorodhesha, na baada ya kuchunguza kwa uangalifu, katika safu yako ya “Ni Muhimu?” weka “Ndiyo” ikiwa kitu hicho ni cha muhimu hasa; na “?” ikiwa ni uhitaji uwezekanao; na “Nzuri” ikiwa kitu hicho ni anasa nzuri ya kuwa nayo. Kumbuka, jumla iliyoorodheshwa katika safu ya “Kiasi Kilichopangiwa” haipaswi kuwa kuu kuliko mapato yako ya kila mwezi!
Vitu vilivyotiwa alama “?” na “Nzuri” bila shaka vitakuwa vya kwanza kuondoshwa. Huenda gharama hizi zisihitaji kuondoshwa kabisa-kabisa. Wazo ni kuchunguza kila kitu na kuona ikiwa gharama yastahili raha inayoletwa na hicho kitu na kuondosha ifaavyo. Robert na Rhonda waliona katika orodha yao kwamba walikuwa wakitumia dola 500 kila mwezi kula mikahawani. Lilikuwa zoea ambalo walikuwa wameangukia kwa sababu hakuna mmoja wao aliyejua kupika. Lakini Rhonda alichukua hatua za kujifunza na asema: “Sasa kupika kunafurahisha, nasi hula nyumbani mara nyingi zaidi.” Robert aongeza: “Sasa sisi hula mikahawani katika pindi za pekee, au inapokuwa lazima.”
Badiliko katika hali zako huenda likakufanya uchunguze tena hali yako kikamili kuhusu kilicho muhimu. Kama ilivyotajwa katika makala ya kwanza, mapato ya Anthony yalishuka sana. Kutoka dola 48,000 kwa mwaka hadi chini ya dola 20,000 na kubaki katika kiwango hicho kwa miaka miwili. Hili likikupata, huenda ukahitaji kuanzisha bajeti ya kusalimika, ukikata matumizi yote ya ziada.
Hivyo hasa ndivyo alivyofanya Anthony. Kwa kukata sana fedha zitumiwazo kwa vyakula, mavazi, usafiri, na tafrija, yeye alifaulu kwa jitihada nyingi kulipia nyumba yake ili asiipoteze.a “Tukiwa familia ilitulazimu kupambanua mahitaji yetu ya lazima na mambo tunayotaka,” yeye asema, “nasi tumenufaika na ono hilo. Sasa twajua jinsi ya kuridhika na machache.”
Punguza Deni
Deni lisilodhibitiwa laweza kuharibu jitihada zako za kuishi kulingana na riziki yako. Ingawa deni la muda mrefu litumiwalo kulipia mali kama vile nyumba ambazo huongezeka katika thamani laweza kuwa na faida, madeni ya kadi za mkopo ya kulipia maisha ya kila siku yaweza kuleta msiba. Kwa hiyo, jihadhari na “usijiingize katika madeni ya kadi za mkopo,” lasema Newsweek.
Wataalamu wa kifedha hutia moyo kulipa madeni ya kadi za mkopo hata ikiwa itakulazimu kutoa fedha katika akiba yako. Ni jambo lisiloeleweka kuwa na madeni yenye kiwango cha juu cha riba huku ukiwa na akiba yenye kiwango cha chini cha riba. Walipotambua hili, Michael na Reena walilipa madeni yao ya kadi za mkopo kwa kubadili kuwa fedha dhamana zao za akiba, kisha wakaazimia kutoingia tena katika hali hiyo.
Robert na Rhonda, kwa kuwa hawakuwa na rasilimali hizo, waligeukia bajeti ya kusalimika. Robert asema: “Nilitengeneza grafu kwenye ubao mweupe kuonyesha jinsi deni lingekuwa likipungua mwezi baada ya mwezi kisha nikaangika ubao huo katika chumba chetu cha kulala mahali ambapo tungeweza kuuona kila asubuhi. Hilo liliandaa kichocheo cha kila siku.” Mwishoni mwa mwaka, walifurahi kama nini kuwa huru kutokana na deni lao la kadi za mkopo la dola 6,000!
Katika nchi fulani hata amana si kitega-uchumi kizuri sana kama kilivyokuwa. Na kununua nyumba kwaweza kukugharimu fedha nyingi kwa sababu ya utozaji wa riba. Waweza kufanya nini ili kupunguza gharama ya amana? “Ama ulipe kiasi kikubwa cha malipo ya kwanza kuliko inavyohitaji benki au ununue nyumba isiyo ghali sana,” lapendekeza Newsweek. “Ikiwa tayari una nyumba, kinza tamaa ya kutaka kununua nyumba kubwa au bora zaidi.”
Waweza kupunguza gharama ya mkopo wa gari kwa kulipa kiasi kikubwa cha malipo ya kwanza. Lakini utalazimika kuyawekea akiba muda mrefu kabla ya wakati huo kwa kuyafanyia safu kwenye bajeti ya familia. Namna gani kuchagua gari zuri lililotumiwa?b Gharama yalo ya mwanzoni huenda ikawa ya chini. Huenda hata ukaweza kununua moja bila hata ya kutafuta mkopo.
Je, Utafaulu?
Kufaulu kwako katika kufanya bajeti yako ifanikiwe hutegemea kwa sehemu kubwa jinsi ilivyo ya uhalisi. “Bajeti haitafanya kazi ikiwa kiasi kilichowekwa kando kwa ajili ya mambo ya nyumbani ni kidogo sana hivi kwamba hamwezi kumaliza mwezi mkikitegemea,” wasema mume na mke ambao wameishi kwa mafanikio wakitumia bajeti.
Jambo jingine la maana sana katika kufanya bajeti ifaulu ni mawasiliano mazuri kati ya washiriki wa familia. Wale walioathirika kwa bajeti wapaswa kuwa na fursa ya kueleza maoni na hisia zao bila kudhihakiwa. Ikiwa washiriki wa familia wanaohusika wanafahamu mahitaji na kile anachotaka kila mmoja na kutambua jinsi hali ya kifedha ya familia ilivyo, yaelekea kutakuwa na ushirikiano na nafasi nzuri ya kufanikiwa kwa bajeti ya familia.
Katika nyakati hizi zilizo ngumu, huku mandhari ya ulimwengu izidipo kubadilika, msongo kwa fedha za familia huongezeka. (2 Timotheo 3:1; 1 Wakorintho 7:31) Twahitaji kudhihirisha “hekima kamili” katika kukabili magumu ya uhai wa kisasa. (Mithali 2:7) Kuweka bajeti ndiyo hatua hasa itakayokusaidia kufanya hivyo.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa madokezo juu ya kukata gharama za matumizi ya kila siku, ona Amkeni! la Aprili 8, 1986, kurasa 18-19, na la Aprili 8, 1984, ukurasa 27, la Kiingereza.
[Blabu katika ukurasa wa 11]
Chunguza kila kitu uone ikiwa gharama yastahili raha inayoletwa na hicho kitu
[Blabu katika ukurasa wa 12]
Uwe mwangalifu na utozaji wa riba ya kadi za mkopo!
[Chati katika ukurasa wa9]
CHATI YA MATUMIZI NA UCHANGANUZI WA KILA MWEZI Mwezi
GHARAMA Matumizi Hususa Ni Muhimu? Kiasi Kilichopangiwa
Chakula:
Ununuzi wa vyakula
Kula mikahawani
Ukaribishaji-wageni
Nyumba:
Amana au kodi ya nyumba
Faida
Mavazi
Usafiri
Zawadi
●
●
●
Akiba
Kodi
Bima
Mambo Mengine
JUMLA (linganisha na mapato)
MAPATO YA KILA MWEZI
Mishahara
Nyumba ya kukodisha (ikiwa unayo)
Riba za akiba
JUMLA (linganisha na matumizi)
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mawasiliano mazuri ya familia ni ya maana katika kufanya bajeti ifaulu