Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 4/8 kur. 27-29
  • Wakati Mvurugo wa Vitu Vingi Ukosapo Kudhibitiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wakati Mvurugo wa Vitu Vingi Ukosapo Kudhibitiwa
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Hawawezi Tu Kuvitupa Nje?
  • Mahali pa Kuanzia
  • Katoweka—Kawekwa Kwenye Kijumba
  • Maoni Yaliyosawazika Kuhusu Mali
  • Tumia Wakati Vizuri kwa Kuwa Huwezi Kuuhifadhi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2006
  • Wazionaje Mali?
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Nyumba Safi—Kila Mtu Ana Sehemu Yake
    Amkeni!—2005
  • Naweza Kuboreshaje Jumla ya Mavazi Yangu?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 4/8 kur. 27-29

Wakati Mvurugo wa Vitu Vingi Ukosapo Kudhibitiwa

TAZAMA huku na kule nyumbani mwako. Je! unakosa nafasi kwa sababu ya mvurugo wa vitu vingi? Je! ungeona haya kama rafiki yako angechungulia mahali pako pa kuweka nguo? Je! unapata tatizo unapotafuta kitu fulani kwa sababu kimefichika chini ya rundo la vitu vingi? Ikiwa ndivyo, si wewe peke yako.

“Mimi ni ‘mwekevu’ mno,” aungama Ralph. Leon aongezea hivi: “Ilikuwa ni kama ninafunikwa na wingi wa nguo, magazeti, na vitabu nilivyokuwa nimekusanya kwa zaidi ya miaka 15.” “Kule kufikiri tu juu ya kuviondolea mbali kwanifanya niwe mchovu kabla ya kuanza,” mwingine mwenye tatizo la mvurugo wa vitu vingi asikitika.

Watoto fulani hukua katika mazingira yenye mvurugo wa vitu vingi. Mtu mmoja aliyekua katika hali kama hiyo asema: “Kwa kadiri niwezavyo kukumbuka, nyakati zote nimewatahadharisha watu kile ambacho wanaweza kutazamia wajapo nyumbani mwetu kwa mara ya kwanza. Niliwaambia kwamba ilikuwa sawa kusogeza kitu fulani ili wawe na mahali pa kuketi.” Hata watu wazima huenda wakasita kualika yeyote asiye wa familia yao azuru kwa sababu hali ya nyumba yao haipendezi.

Mara nyingi watu hawang’amui jinsi walivyorundika vitu mpaka wanapokuwa wakihama. Ikiwa mtu hajaweka programu ya kawaida ya kudhibiti mvurugo wa vitu vingi, kuhama huchukua wakati mwingi zaidi—na hugharimu zaidi.

Lakini kwa watu wengi, kuondoa mvurugo wa vitu vingi huhusisha mengi kuliko jambo rahisi la kutupa tu vitu nje. Vikwazo kadha wa kadha lazima kwanza vishindwe.

Kwa Nini Hawawezi Tu Kuvitupa Nje?

Kwa muda fulani, mwanasaikolojia Lynda W. Warren na mfanyikazi wa kijamii wa kliniki Jonnae C. Ostrom walikuwa wamefikiri kwamba wale walio na mvurugo wa vitu vingi walikuwa wazee-wazee pekee, waliookoka ule Mshuko wa Thamani ya Fedha wa miaka ya 1930. Walifikiri kwamba, uwekevu wa vitu akiba ulikuwa “jambo la kiajabu-ajabu lisilo la kawaida na lisilodhuru.” Hata hivyo, baada ya kuchunguza jambo hilo, waliripoti hivi: “Tulishangaa kugundua kizazi kichanga cha panya wawekevu, waliozaliwa muda mrefu baada ya miaka ya 1930. . . . Sasa tunaamini kwamba tabia kama hiyo ni ya kawaida na kwamba, hasa wakati inapokuwa ya kupita kiasi, inaweza kufanyiza matatizo kwa panya wawekevu au wale walio karibu nao.”a

Hilo laweza kupita kiasi kadiri gani? “Ostrom amepata kuona ndoa zikivunjika kwa sababu ya ukosefu wa utaratibu,” gazeti Health laripoti. Watu fulani huwaendea washauri wastadi kupata msaada. Kwa kweli, gazeti Health huita ushauri unaohusu utaratibu wa kibinafsi “biashara inayokua ambayo wanabiashara wayo hutoza kiasi cha dola 1,000 [za U.S.] kwa siku moja kufanya yale ambayo mama zetu walitukemea ili tuyafanye: kuweka vyumba vyetu vikiwa nadhifu.”

Inaelekea kwamba wewe huna tatizo kubwa la mvurugo wa vitu vingi kama hilo. Walakini, huenda ukaona kuwa tatizo kukwepa vizuizi vinne vifuatavyo ambavyo huwa kama vikwazo dhidi ya kutupa vitu kwenye pipa:

◻ Uwezekano wa kukihitaji wakati ujao. (“Afadhali kukiweka kuliko kujuta baadaye.”)

◻ Kuambatanisha kitu na shauku za upendo. (“Shangazi yangu Mary alinipa hiki.”)

◻ Uelekeo wa kuwa na dhamani wakati ujao. (“Huenda kitakuwa na dhamani fulani siku moja.”)

◻ Kutokuchakaa au kutokuharibika. (“Hiki ni kizuri mno kisiweze kutupwa.”)

Matokeo? Psychology Today chasema: “Vitu hivyo huzidi kuongezeka, na ndivyo na matatizo vinayotokeza.”

Kwa hiyo wewe waweza kudhibitije vitu vingi visivyohitajiwa?

Mahali pa Kuanzia

Mwanamke mmoja alipoulizwa awazie jinsi angehisi kama kimbunga kingepiga na kuharibu karibu mali yake yote, yeye alisema: “Jinsi hasa nilivyohisi kwa wazo hilo la kupoteza kila kitu ni faraja—kuondolewa vitu vyangu vyenye vuruguvurugu bila ya mimi kuwa na hangaiko la kuchagua nitakachoweka na nitakachotupa.” Hilo latoa kielezi chema kwamba kuchagua na kutupa kwaweza kuwa jambo la ushindani.

“Wenye mvurugo wa vitu vingi wana matatizo mawili,” asema mshauri Daralee Schulman. “Vitu ambavyo tayari vimo nyumbani na vitu vinavyoletwa nyumbani.” Badala ya kujishughulisha na usafi, yeye adokeza kutumia dakika kama 15 kila siku kupanga kitaratibu sehemu moja baada ya nyingine. Hiyo ndiyo njia yenye matokeo zaidi katika kushughulika na mvurugo wa vitu vingi visivyohitajika nyumbani. Lakini namna gani kuhusu “vitu vinavyoletwa nyumbani”?

Kabla ya kununua kitu chochote cha nyumbani, jiulize: ‘Je, nakihitaji kweli kweli? Nitakiweka wapi? Je, nitakitumia?’ Daralee Schulman adai kwamba kwa kuuliza maswali kama hayo, “asilimia 75 ya vitu ambavyo ungevileta nyumbani, hutavileta.”

Kwenye makao makuu ya Watch tower Society na ofisi za tawi, wakazi wanatarajiwa waweke vyumba vyao vikiwa havina mvurugo wa vitu vingi na wapunguze hesabu ya vitu vya kurembesha vinavyowekelewa juu ya vyombo vya nyumbani au kwenye rafu kuwa vichache. Hilo hurahisisha kazi ya usafi na hupendeza kwa macho zaidi. Makaratasi, magazeti, vitabu, mifuko ya kubebea vitabu, vyombo vya kuchezea muziki, vifaa vya michezo, nguo, vyombo vya kulia, na vitu vingine havipaswi kuachwa vikiwa vimetapakaa huku na kule. Kwa kweli, hakuna kitu chochote kinachopaswa kuwa sakafuni mwa chumba isipokuwa kiwe ni chombo cha nyumba. Bila shaka hicho ni kiolezo kwa wowote ambao wangependa kuwa na mazingira yasiyo na vurugu la vitu vingi.

Katoweka—Kawekwa Kwenye Kijumba

“Ningepewa habari siku moja kimbele, ningeweza kupanga nyumba yangu kwa utaratibu,” asema Joan, “lakini vijumba vya kuwekea vitu vilikuwa katika hali mbaya sana nyakati zote.” Wengine hutumia kijumba chao kama mahali pa kuondolea mbali vitu vyao, kwa kuhamisha tu vitu visivyohitajika kwenye mahali visivyoweza kuonwa. Tatizo huendelea kuwa kubwa tu kwa vile vitu zaidi na zaidi huwekwa kwenye nafasi isiyobadilika ukubwa.

Je! inawezekana kupunguza rundo la vitu katika kijumba chako cha kuwekea vitu? Gazeti Good Housekeeping ladokeza: “Mifumo ya kuweka utaratibu-wa-vijumba huwa katika unamna-namna wa vifaa na vyombo vingine vya ziada ambavyo vyaweza kubadilishwa vitoshee nafasi yoyote. Tumia mmoja ili kushinda tatizo la uwekevu nyumbani mwako.” Hivyo usitumie kijumba chako kama mahali pa kujazia vitu. Kiweke kikiwa bila mvurugo wa vitu vingi na katika utaratibu.

Maoni Yaliyosawazika Kuhusu Mali

“Mali yangu inanionyesha jinsi nilivyo, hiyo ni sehemu ya vile mimi binafsi nilivyo,” akasema mwanamke mmoja. “Mawe yangu ya thamani hunituliza sana,” mwingine aongezea. “Mimi ninapenda sana pete zangu na mikufu yangu.” Bado mwanamke mwingine asema hivi kwa kukaidi: “Hivi vitu ndiyo mimi mwenyewe—ndiyo vile nilivyo binafsi na hutavitupa nje!”

Kwa kutofautisha, Yesu Kristo alisema: “Maisha ya mtu hayawekwi salama na kile alicho nacho, hata anapokuwa na vingi kuliko vile anavyohitaji.”—Luka 12:15, The Jerusalem Bible.

Hivyo Biblia hupendekeza kuwa na maoni yaliyosawazika kuhusu mali. Pia huunga mkono kuwa na utaratibu, hiyo ikifanya hilo liwe takwa kwa wale wanaotumikia wakiwa wazee katika kundi.—1 Timotheo 3:2.

Kwa nini usianze kutumia maishani baadhi ya madokezo yaliyo juu kwenye sehemu fulani nyumbani mwako ambayo ina vitu vingi kupita kiasi? Kwa jitihada za kila siku na maoni yaliyosawazika kuhusu mali yako, mvurugo wa vitu vingi waweza kudhibitiwa.

[Maelezo ya Chini]

a “Panya mwekevu” ni mtu akusanyaye vitu visivyo na maana. Anaitwa hivyo kutokana na aina ya panya mwenye mkia wa manyoya mengi (aitwaye pia panya wa msituni) aliye na vifuko vikubwa vya mashavuni ambavyo huweka chakula na vitu visivyo na maana. Ingawa mwenye kukusanya huchagua aina moja ya vitu au kikundi fulani cha vitu, panya mwekevu ataweka aina zote za vitu na huvitumia mara chache sana.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 28, 29]

Kuchagua na Kuondolea Mbali

Yanayofuata ni madokezo yenye msaada kuhusu vitu hususa vinavyoweza kuvuruga nyumba yako kwa urahisi ukikosa kuwa mwangalifu.

Vifaa vya kusoma: Je! unaona kuwa vigumu kuondolea mbali magazeti au nyusipepa za zamani? Kichwa fulani cha habari kinakuvutia, kikifanya uwaze kwamba: ‘Nitasoma hili karibuni’? Badala ya kuweka gazeti zima au nyusipepa, kata makala inayokupendeza na uiweke katika kiwekeo (jalada) cha “Mambo ya Kusomwa.” Ikiwa baada ya muda unaotosha bado hujaisoma—labda majuma kadhaa—itupe.

Mavazi: Je! mavazi yako huongezeka na kuwa mengi mwaka baada ya mwaka, na hali huvai nusu yayo? Wengine huwaza: “Vazi hili litaonekana vema nikilivaa—baada ya kupunguza uzito wangu.” Hii inakuwa kama leseni ya kuweka kitu fulani au vitu vyote katika mahali pa kuwekea nguo. Ili kuzuia mvurugo wa nguo kama huo, ikiwa vazi fulani halivaliwi katika mwaka mzima, liweke katika sanduku la “Visivyoamuliwa.” Halafu, ikiwa bado halivaliwi baada ya kipindi cha wakati, mpe mwingine au litupe.

Barua: Ziondolee mbali barua kila siku. Barua za kibinafsi na nyingine unazotaka kuweka zapaswa kufailiwa mahali hususa. Ungeweza kuwa na kitu cha kuwekea makaratasi ya kila mwezi na baada ya mwaka mmoja utupe yaliyomo ili kufanya nafasi kwa barua za mwezi mpya unaofuata. Kanuni yenyewe ni weka faili usiweke rundo. Ikiwa unapokea barua nyingi za utangazaji wa biashara, amua mara hiyo kama utazihitaji. Ikiwa sivyo, zitupe. Ikiwa unaona vigumu kuamua, ziweke katika sanduku la “Visivyoamuliwa” kwa muda wa juma moja. Ikiwa kufikia wakati huo bado hutakuwa umezishughulikia, zitupe.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki