Kuutazama Ulimwengu
Utegemezo Mchache wa Umma kwa Kanisa la Hispania
Katika Hispania serikali inaendelea kutoa tegemezo la kifedha kwa Kanisa Katoliki. Kulingana na gazeti la kila siku la Madrid El País, mwaka jana kanisa lilipokea peseta 15,000,000,000 (dola 140,000,000, za U.S.) Sehemu fulani ya fedha hizo ilitoka kwa walipa kodi, waliotia alama ya sanduku katika fomu zao za kodi wakionyesha sehemu fulani ya kodi zao kuwa mchango kwa Kanisa Katoliki. Hata hivyo, El País ilisema kwamba hesabu ya walipa kodi wanaotaka kufanya mchango kama huo inapungua. Katika 1989 asilimia 38 pekee ya watu wanaolipa kodi walisema kwamba walitaka fedha kama hizo ziliendee kanisa. Hilo ni katika taifa ambalo husemwa kwamba karibu asilimia 100 ni Wakatoliki.
Watoto Wanaotendewa Vibaya
Katika sehemu fulani za Afrika Kusini, kuna ongezeko la watoto wanotendewa vibaya kimwili. Hesabu kubwa ya watoto wanaotendewa vibaya ni wachanga sana na hawawezi kutafuta msaada. Kulingana na gazeti la Cape Town liitwalo Cape Times, uchunguzi wa hivi karibuni wa watoto 350 waliolazwa hospitalini kwa kutendewa vibaya ulifunua kwamba “asilimia 60 walitendewa vibaya kingono na asilimia 40 kimwili.” Cape Times lilisema kwamba “asilimia 90 hivi ya waliotendewa vibaya kingono walikuwa wasichana wa wastani wa umri wa miaka sita, hali asilimia 60 ya wagonjwa waliotendewa vibaya kimwili walikuwa wavulana wa wastani wa miaka mitano-u-nusu.” Katika Hospitali ya Watoto ya Msalaba Mwekundu, “robo ya wale wote (wa rangi zote) waliotendewa vibaya kimwili (si kingono) waliotibiwa katika miaka miwili iliyopita walikuwa chini ya umri wa mwaka mmoja.”
Mtindo-Maisha Unaoua
Nusu ya vifo vyote vyaweza kuzuiwa kwa kubadilisha mtindo-maisha, adai Dakt. Ivan Gyarfas, msimamizi wa kituo cha maradhi ya moyo cha Shirika la Afya Ulimwenguni. Kansa ya mapafu, msukumo wa damu, magonjwa ya ghafula ya moyo, na potezo la ghafula la fahamu ubongoni hufanyiza asilimia 70 hadi 80 ya vifo vyote katika mataifa yaliyositawi. Maradhi hayo mara nyingi huambatanishwa na tabia zisizo za kiafya za uvutaji sigareti, aina ya chakula kisichofaa mwili, na kukosa kufanya mazoezi—mtindo-maisha wa wale waitwao eti matajiri. Hata hivyo, International Herald Tribune la Paris laripoti kwamba “maradhi hayo ya mtindo-maisha” sasa husababisha kuanzia asilimia 40 hadi 50 ya vifo vyote katika mataifa yanayositawi pia. Kama kwa njia ya kujipinganisha, inaonekana kwamba mtindo wa maisha ambao kwa kawaida huonwa kuwa alama ya kuonyesha maendeleo ya kiuchumi unahusiana moja kwa moja na vile visababishi vikubwa vya vifo ulimwenguni pote.
“Chuo Kikuu cha Maisha”
John Major alitumika akiwa chansela wa Idara ya Kutunza Uchumi Uingereza kabla ya kuwa waziri mkuu katika Novemba 1990. Aliacha shule akiwa na miaka 16, na kulingana na alivyokiri yeye mwenyewe, elimu yake ilipatikana kutokana na “chuo kikuu cha maisha.” “Mimi ninajua watu wengi sana ambao wana vyeti vingi vya kielimu,” akasema, “na . . . wao hawafai kabisa, wengi wao. Hawatumii akili ile ya kawaida ya kung’amua mambo. Ni lazima kuchanganya uelewevu na akili ile ya kawaida ya kung’amua mambo ikiwa watu wataka kweli kutimiza mambo na mara nyingi akili ya kawaida huwa ndiyo ya maana zaidi.” Ingawa wengi hawakukubaliana na maoni yake, The Times la London lilimripoti aliyekuwa mwalimu mkuu John Rae akikubali: “Vyeti vya kielimu vinamaanisha tu kwamba mtu huyo amehitimu katika jambo hilo hususa, si zaidi. Baadhi ya wanachuo, hasa katika vyuo vikuu, hawajui linaloendelea katika ulimwengu halisi. . . . Mimi ninaona kwamba watu wasio na vyeti mara nyingi huwa wana uwezo zaidi.”
Hakuna Woga wa UKIMWI
Maofisa wa serikali kwenye Vituo vya Udhibiti wa Maradhi katika Atlanta, Georgia, U.S.A., wameshangaa na kugutushwa na ongezeko la utendaji wa kingono kati ya wasichana matineja katika United States kujapokuwa na ogofyo la UKIMWI. Gazeti la Kanada, The Medical Post, laripoti kwamba “kwa mfano, wale walio na umri wa miaka 15 leo, wanaelekea kuwa watendaji kingono mara tano zaidi ya vile wenzao walivyokuwa kizazi kimoja kilichopita.” Hesabu ya wanawake wachanga wa umri wa miaka 15 hadi 19 wanaokubali kwamba wamehusika katika ngono ya kabla ya ndoa karibu imekuwa maradufu. Hiyo ndiyo hali hasa kwa wasichana wa miaka 15. Kulingana na The Medical Post, “wastadi wa afya walilaumu tamaduni zinazopendwa na wengi zinazotia umaana mkubwa kwenye ngono na kushindwa kwa kampeni ya elimu ya ngono katika miaka ya 1980 kuwa ndivyo visababishi vya tarakimu hizo zenye kupanda.”
Mafahamiano ya Kutafuta Uchumba Katika India
Kuwekeana miadi kunazidi kupendwa na wengi katika India, na wengine sasa ni kama wanakukubali kuwa jambo hakika la maisha. Gazeti India Today lasema kwamba miaka kumi iliyopita, kuweza kuona wenzi wawili wakitembea pamoja huku wameshikana mikono kulikuwa “kama kuona ndege ambaye huwa vigumu kumwona hivi hivi tu. Siku hizi, wao ni jambo la kawaida kama ndege shorewanda.” Wenzi wawili-wawili wanaofanya mafahamiano ya kutafuta uchumba waweza kuonekana kwenye fuo za bahari za umma, katika bustani, katika majumba ya sinema, na kwenye mikahawa ya vyakula vyepesi. Mionyesho ya vitendo vya upenzi sana ni ya kawaida zaidi. Wengine wanaona kwamba badiliko hili katika jamii ya watu wa India limeletwa na msongo wa marika katika shule na koleji na ongezeko la sinema zenye kuonyesha ngono za waziwazi na programu za televisheni.
Wachawi Wakatoliki
Uchawi unakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Wameksiko wengi. Gazeti la kila juma, Siete Días, laripoti kwamba watu hutafuta msaada wa wachawi katika kusuluhisha unamna-namna wa matatizo, kama vile kuumwa na kichwa, mafua, na magumu ya kikazi na ya kimahaba. Majimbo ya kusini na ya sehemu ya kati ya Veracruz, Oaxaca, Morelos, na Michoacán yanajulikana sana kwa wachawi wayo. Siete Días yasema kwamba “uchawi katika Meksiko ulianzia siku za Waazteki. Wahispania walipowasili, wachawi pamoja na waganga walichanganya mapokeo ya Ulaya katika kazi yao, kama vile Ukatoliki.” Mchawi mmoja mashuhuri katika La Petaca hupokea wateja wake katika chumba “kilichojaa sanamu za Bikira wa Guadalupe na Yesu, picha za John Paul wa 2, na mishumaa iliyowashwa.”