Shomoro—Rafiki au Adui?
MAJIRANI wapya wahamia humo sasa hivi. Wametulia na kuendelea na shughuli zao za kila siku za kulea na kulisha familia, wakiwa wametorosha wapangaji wa kwanza na kuwafukuzia mbali watazamaji wowote wenye udadisi.
Jina lao, shomoro, linatumiwa kwa ndege kadhaa walio tofauti, lakini kwa ujumla hurejezea washiriki wa familia ya wazingi. Kwa kawaida, shomoro huwa ndege wadogo wasioonekana kwa urahisi, wenye manyoya ya kijivujivu, kahawia, na meusi. Wengi wao ni waimbaji wazuri.
Hata hivyo, labda shomoro sio aina ya majirani unaoweza kuchagua. Kwani, hali wanasifiwa na watu wengine kwa ajili ya ujasiri na uwezo wao wa kufaana na hali, ndege hao wadogo hawapendwi na wengi katika sehemu nyingine.
Kwa Nini Huonwa Kuwa Mjeuri
Shomoro wa nyumbani (Passer domesticus), au shomoro wa Uingereza, alipelekwa Amerika Kaskazini kutoka Ulaya katika 1851 kwa matumaini kwamba hilo lingemaliza nyungunyungu wenye kuharibu miti. Hata hivyo, shomoro walijifunza upesi kwamba kuishi mijini kulikuwa rahisi zaidi kuliko kuishi mashambani. Kwa hiyo badala ya kula wadudu, walianza kula mabaki ya vyakula na upesi wakawa stadi wa kuvamia mapipa ya takataka. Kitabu North American Birds chasema kwamba “Kuweza kufaana na hali na uchokozi” wa shomoro wa nyumbani, “kunalandana kitabia na wahamaji wenye manyoya kama vile panya wa kahawia, panya weusi, na panya mdogo wa nyumbani.”
Shomoro hujenga nyumba zao zilizo shaghalabaghala zisizo nadhifu katika kila sehemu iwezekanayo. Manyoya, sufu, na nguo zilizotupwa ni miongoni mwa vitu wanavyopendelea kwa kujenga viota. Mara nyingi wanafukuza ndege wenyeji na kumiliki viota vyao kifidhuli, wakiondoa mayai ya wapangaji walioondoshwa. Zaidi ya hayo, shomoro huharibu aina-aina za matunda, nao hula mbegu zinazoiva na mboga nyepesi, zilizo changa.
Katika Brazili, ambapo shomoro wa nyumbani alipelekwa kimakusudi pia, hakuharibu tu mimea bali pia alifukuza ndege tico-tico mwenye kupendwa. Tico-tico, aliye wa kimo na rangi inayofanana na shomoro, ni ndege mdogo mwenye urafiki aliye wa maana, ambaye huangamiza wadudu wanaodhuru mimea.
Sura Zinazovutia
Walakani shomoro ni ndege wanaopenda mchezo ambao hulialia kwa furaha, na watu wengi hufurahia kuwatazama wanaporuka kutoka kwa kiota chao hadi chini na kurudi juu tena. Mtazama-ndege mmoja asimulia: “Tuna karibu viota saba vya shomoro katika ujirani wa nyumba yetu. . . . Kikundi cha ndege hao chaweza kuonwa kikichezacheza majini wakati ule ule, wakigongana wanapofanya hivyo. Wengine ‘husisimuka’ sana. Wao huruka na kupiga mabawa yao, na kwenda upande kwa upande, wakipanua manyoya yao mpaka karibu yalowe maji kabisa. Halafu wanaruka kwenye ua, wanapangusa midomo yao, wanajitingisha kama mbwa afanyavyo, wanayatazama maji na kupiga mbizi tena. Hilo laweza kuendelea kwa muda wa saa moja hivi, kisha wanaruka na kwenda na kurudi tena baada ya muda wa saa moja au mbili.” Mara nyingine shomoro wanaweza kuonekana wakioga mavumbini katika mchanga mkavu kando ya barabara au kwenye konde la maua.
Kwa kupendeza, shomoro hutajwa katika Biblia. Yesu alitumia ndege hawa wanaopuuzwa kutoa kielezi mara mbili, kuhusu utunzaji mwororo wa Mungu. Alipotuma mitume wake 12 kuhubiri, Yesu aliwauliza: “Je! mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja?” ndipo akaeleza: “Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.” Baadaye katika huduma yake, Yesu alirudia kielezi hicho, hivyo akikazia kwamba kwa sababu Mungu huwa hasahau shomoro hata mmoja, Yeye hatasahau wale wanaomtumikia Yeye.—Mathayo 10:29, 31; Luka 12:6, 7.
Bila shaka, Yehova Mungu huthamini uumbaji wake wote, mdogo na mkubwa pia. Na ingawa tabia za viumbe fulani huenda zisipendeze kwetu nyakati zote, aina nyingine mbalimbali za vitu vinavyoishi huangaza hekima ya Muumba wetu Mkuu.—Zaburi 104:24.