Nyumba ya Dini Iliyogawanyika
Kati ya dini zote za ulimwengu, Katoliki ya Kiroma, Uislamu, na Uhindu ndizo zilizo kubwa zaidi. Wakatoliki wa Kiroma hudai kuwa na watu milioni 985, au asilimia 18.8 ya jumla ya watu wote ulimwenguni iliyo milioni elfu 5.24, hali milioni 912 (asilimia 17.4) hudai kuwa Waislamu, na milioni 686 (asilimia 13.1) ni Wahindu—mara mbili zaidi ya Wabuddha milioni 320.
Gazeti Asiaweek lilisema kwamba “Ukristo ndio dini kubwa zaidi kati ya zote.” “Lakini imegawanyika sana katika mafarakano yenye kupingana katika historia—Waprotestanti na Wakatoliki wa Ailandi Kaskazini wakiwa kielelezo kizuri zaidi kinachoendelea kuwako—kwamba ni vigumu kwa watu wengi kuufikiria wote kuwa dini moja. . . . Waislamu hawajagawanyika sana kimafarakano kama vile Wakristo, lakini Sunni na Shia ni njia mbili tofauti zenye historia ambayo haijawa na upatano nyakati zote.” Kikundi kikubwa zaidi cha Waislamu ni Wasunni.
Kwa kuongezea, idadi kubwa ya watu wote duniani hawadai kuwa wa imani yoyote ya kidini. Sehemu kubwa ya watu hao iko katika Uchina, Ulaya ya Mashariki, na Urusi. Wale ambao hawana dini hufikia milioni 896, na wale wasioamini kuwako kwa Mungu hufanyiza milioni 236 zaidi.