Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 11/8 kur. 20-22
  • Pikipiki—Ni Zenye Hatari Kadiri Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pikipiki—Ni Zenye Hatari Kadiri Gani?
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kinachovutia Hasa
  • ‘Je! Niendeshe Pikipiki?’
  • Akili Timamu
  • Wao Walisadikishwa Juu ya Upendo wa Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Niliishi Maisha ya Ubinafsi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Yehova Ni Mungu Anayenionyesha Fadhili-upendo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • “Ahadi ya Dunia Kuwa Paradiso Ilibadili Maisha Yangu!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 11/8 kur. 20-22

Pikipiki—Ni Zenye Hatari Kadiri Gani?

Na mleta habari za Amkeni! katika Japan

PIKIPIKI ndogo ya Susumu ilikuwa inaenda kwa utaratibu wakati alipoliona kwa ghafula gari likivuka kisehemu chake cha barabara. Kitu alichofuata kuona ni paa ya nyumba alipokuwa amerushwa juu angani. Alianguka kwa kichwa na bega lake. Mpasuko katikati ya kofia yake ya kujilinda ulionyesha namna aksidenti hiyo ilivyokuwa mbaya. Alinusurika kifo katika aksidenti hiyo, lakini mguu wake ulivunjika na kupindika ukawa na umbo la U.

Aksidenti ya Susumu haikuwa ya pekee. Gazeti The Globe and Mail la Kanada laripoti kwamba katika mwaka mmoja Waamerika 166,000 walilazwa hospitalini kufuatia aksidenti za pikipiki. “Kati ya hao, 4,700 walikufa. Wengine wengi walilemaa muda wote wa maisha.” Gazeti ilo hilo lasema kwamba katika Kanada, aksidenti za pikipiki ziliongezeka maradufu katika kipindi cha miaka kumi. Na katika Japan waendesha pikipiki 2,575 walipoteza uhai wao katika 1989. Kati ya hao, ukiondoa waendesha pikipiki-baiskeli, zaidi ya asilimia 70 walikuwa vijana kati ya umri wa miaka 16 na 24.

Hesabu hizo zinalinganaje na takwimu za aksidenti za magari? Makampuni ya bima yadai kwamba katika nchi fulani-fulani, kwa umbali ule ule wa safari, vifo vya waendesha pikipiki viko juu zaidi yapata mara tisa zaidi ya vifo vya watu wanaosafiri kwa gari. Ni nini kinachosababisha idadi hiyo kubwa zaidi ya vifo? Jarida Consumer Reports linatoa sababu tatu: (1) Ni vigumu zaidi kuona pikipiki kuliko kuona gari. (2) Pikipiki ina ulinzi kidogo au haina wowote kwa mwendeshaji wayo. (3) Kuendesha pikipiki kunahitaji ustadi zaidi—ikiteleza, mara nyingi huanguka. Si ajabu kwamba watu wengi huziona pikipiki kuwa hatari. Wengine hawakubali. Wao husema kwamba kuna manufaa katika kuendesha pikipiki. Wewe waonaje?

Ni kweli, kwa kuwa pikipiki huwa na gharama ndogo ya usafiri, huwa haina kifani. Matumizi yake kidogo ya petroli ndiyo sifa yake kubwa. Ukiwa na pikipiki yenye ukubwa wa kadiri, lasema jarida Consumer Reports, unaweza kusafiri kilomita 25 hadi 30 kwa lita moja ya petroli. Kwa kuongezea ina magurudumu mawili tu. Manufaa nyingine ni hizi zifuatazo: ni rahisi kwenda mahali popote, haina matatizo ya kuegesha, na bei yake ni rahisi zaidi ya gari. Hata hivyo, wengine ambao wana uwezo hata wa kuwa na magari ya bei ya juu bado hupendelea pikipiki. Kwa nini?

Kinachovutia Hasa

Wengi wa wale wanaopenda pikipiki wanakubali kwamba kile kinachovutia hasa kuhusiana na pikipiki ni ule msisimuko unaotokana na kuiendesha. “Huenda ukawa ni mngurumo wazo,” asema mpenda pikipiki mmoja. Ule mngurumo wa injini ya silinda mbili ya Uingereza, mvumo wa injini ya silinda mbili ya Japan, au ule mkoromo wa injini ya silinda nne—sauti hizo zote ni kama muziki masikioni mwa wapendao pikipiki.

Kwa waendesha pikipiki wengine, ni ile hali ya uhuru na hisia ya uthibiti. Mmoja asema hivi: ‘Inasisimua kuhisi pikipiki chini yako, kujua kwamba itaitikia nia yoyote yako au uelekezi, ukiendesha kwa kulalia kona na kujua kwamba itakupeleka uendako kwa kutegemeka.’ Mchanganyiko huu wa sauti, mwendo wa kasi, na hisia ya uhuru huenda ukakuvutia hata wewe pia. Lakini kuna hatari. Msisimko huo unaweza kuja kuwa uzoevu mbaya.

Vijana hasa wamo hatarini. “Unaogopa unapoona kona inayopindika sana,” asema mmoja aliyekuwa mwanagenge wa pikipiki, “lakini ule msisimko wa kupinda kona hiyo kwa mwendo wa kasi bila kuteleza husisimua sana. Nilikuwa nikitafuta kona zilizopindika zaidi na zaidi na kuzipinda kwa mwendo wa kasi zaidi.” Yoshio, ambaye hapo awali alikuwa na kichaa cha kuendesha pikipiki asema hivi: “Nilikuwa nikiendesha katika hali zozote, kwa sababu kuendesha huko kulinifurahisha sana. Kuendesha kulikuwa kama dawa ya kulevya kwangu.” Na Susumu, aliyetajwa hapo mwanzoni asema hivi: “Sikujali kama ingeniua au la—ilikuwa ni lazima niendeshe pikipiki.” Hivyo, kabla hata plasta kuondolewa katika mguu wake uliovunjika, alikuwa akiendesha pikipiki tena. Yeye akiri hivi: “Nilikuwa mzoevu sana.”

‘Je! Niendeshe Pikipiki?’

Hivyo, pima uvutano huo pamoja na usalama unapofikiria kuendesha pikipiki. Na ikiwa wewe ni Mkristo anayethamini dhamiri safi na kustahi Biblia, kuna maandiko fulani pia ambayo ungeyafikiria.

Mithali 6:16, 17, kwa mfano, imeorodhesha vitu saba ambavyo ni chukizo kwa Yehova. Kimoja cha vitu hivyo ni “mikono imwagayo damu isiyo na hatia.” Sheria iliyotolewa kwa taifa la kale la Israeli inatuonyesha zaidi maoni ya Yehova juu ya kumwaga damu isiyo na hatia. Sheria hiyo inasema hivi: ‘Ikiwa ng’ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameonyeshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mtu mume au mwanamke; huyo ng’ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa.’ (Kutoka 21:29) Kwa maneno mengine, tunatakwa tutoe hesabu kwa vile vitu tunavyomiliki.

Kwa hivyo, ikiwa unafikiria kupata pikipiki, utaiendeshaje na utachagua ya aina gani? Je! utachagua moja ya zile zenye nguvu nyingi, zilizo hatari sana ambazo hutengenezwa kwa ajili ya mwendo wa kasi na ambazo kwa kawaida huhusika katika aksidenti zilizo mbaya sana? Ikiwa ni hivyo, je, hutakuwa na hatia ya damu ukihusika katika aksidenti? Hata ikiwa huumizi wengine, vipi juu ya uhai wako mwenyewe? Je! utaonyesha staha kwa zawadi ya uhai ikiwa unaendesha kwa kasi katika kona zenye hatari kwa sababu tu ya msisimko wa kufanya hivyo?

Kanuni hiyo inatumika pia kwa utunzi mzuri wa pikipiki yako ikiwa una moja tayari au ikiwa utapata moja. Pikipiki yako inaweza kugeuka iwe kama ‘ng’ombe apigaye,’ ikiwa hutunzi vizuri breki zake. Kwa kuongezea, kila wakati kabla ya kuendesha pikipiki, yakupasa kuchunguza mnyororo na injini. Na namna gani ikiwa unaudhi majirani kwa kuendesha vibaya na kwa kelele nyingi?

Ni kweli, ikiwa wewe ni mpenda pikipiki, huenda ukapenda sauti ya pikipiki yako, lakini si kila mtu ana maoni kama hayo. Kwa kweli, sauti hiyo inawaudhi sana watu wengine hivi kwamba hao hugeuka na kuwa wajeuri. Gazeti Nara Shimbun laripoti juu ya mtu mmoja aliyekuwa na hasira kali sana hivi kwamba alitupa gogo la mti kwa mwendesha pikipiki aliyekuwa akipita. Mwendeshaji huyo mwenye umri wa miaka 16, aliyekuwa mmoja wa wanagenge wa pikipiki, alikufa. Mtu mwingine, laripoti gazeti Asahi Shimbun, alifunga kamba na kuikaza kuvuka njia waliyopenda sana kutumia wanagenge wa pikipiki. Kamba hiyo ilishika shingo ya mwendeshaji kijana na kumnyonga akafa. Na gazeti hilo lilipoalika maoni ya wasomaji kuhusu jinsi walivyohisi juu ya makelele ya pikipiki, wasomaji wengine waliwapendelea wale waliowatenda jeuri waendesha pikipiki.

Bila shaka Biblia inapinga matendo ya jeuri kama hayo. Lakini kwa upande mwingine, waendesha pikipiki hawapaswi kuchokoza wengine kwa kuendesha huku na huku katika sehemu za makazi ya watu kwa pikipiki ambazo hazina vizuia sauti, kama wafanyavyo wakati mwingine wanagenge wa pikipiki. Na hata hivyo, yatupasa tutake kuishi kulingana na sheria ambayo Yesu Kristo aliwapa wafuasi wake: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”—Mathayo 22:39.

Akili Timamu

Je! hiyo inamaanisha kwamba haikupasi kuendesha pikipiki? Sivyo, lakini akili timamu inahitajika. Watu wengi wanaweza kununua pikipiki kwa urahisi, ina mafaa, na ni njia yenye raha ya kusafiri mahali popote. Hata hivyo, katika nchi nyinginezo, mara nyingi watu hutumia pikipiki kwa tafrija. Jambo hilo laweza kufurahisha, lakini uwe mwangalifu sana. Usiziache tamaa za kuendesha kwa mwendo wa kasi na nguvu zayo zishinde uamuzi wako timamu.

Wengine ambao waliishi kwa ajili ya pikipiki zao tu wamefanya mabadiliko. Yoshio, kwa mfano, alipenda kuendesha pikipiki zenye nguvu sana. Leo yeye asema hivi: “Nilipoendesha kwa ajili ya msisimko, nilikuwa najipendeza tu mwenyewe. Sasa nina shangwe ya kutoa nikiwa mhudumu Mkristo.” Yoshio hakufanyiza upya leseni yake kwa sababu alijua kwamba hawezi kujidhibiti mara apandapo kuendesha pikipiki.

Aliyekuwa mmoja wa genge la waendesha pikipiki katika Hokkaido, Japan, akumbuka hivi: “Nilikuwa ninaendesha pikipiki ili kujionyesha. Nilikuwa nikitumia dawa za kulevya sana kwa sababu ya mashirika mabaya na wanagenge wa pikipiki.” Lakini alianza kufikiria wakati ujao. Alichunguza vikundi mbalimbali vya kidini na hatimaye akapata kweli kwa kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova.

Na vipi Susumu? Kwake, kuendesha pikipiki si jambo kuu maishani mwake tena. Susumu, pamoja na wapenda pikipiki wawili ambao wametajwa hapo juu, sasa wanatumika wakiwa wahudumu Wakristo wa wakati wote. Mmoja wao alibadilisha pikipiki yake kubwa na pikipiki-baiskeli na yeye huitumia kueneza kweli za Biblia kwa wengine.

Naam, pikipiki inaweza kuwa njia ya usafiri iliyo bora sana, lakini ni lazima itumiwe kwa uangalifu sana kila wakati na kwa kuheshimu hisia za wengine.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

MAPENDEKEZO YA USALAMA KWA WAENDESHA PIKIPIKI

◼ Endesha kwa Uangalifu Sana: Kuelekeza, kuongeza mwendo, na kushika breki huhitaji ustadi na upatanisho wa hali ya juu sana.

◼ Epuka Kuendesha Katikati ya Barabara Yoyote: Hapo ndipo takataka na mafuta kutoka kwa magari hujikusanya.

◼ Vaa Mavazi Yafaayo: Hakikisha umevaa kofia ya kujikinga. Glovu, koti la juu, na viatu vya kujikinga vitakulinda.

◼ Uwashe Taa Nyakati Zote Unapoendesha: Sheria za barabarani zikiruhusu hivyo, basi fanya hivyo hata wakati wa mchana. Utaonekana zaidi na madereva wengine.

◼ Uweke Utepe Unaoangaza Kwenye Kofia Yako ya Kujikinga: Hilo lakufanya uonekane zaidi wakati wa usiku.

◼ Endesha Ukiwa na Mwelekeo wa Kujikinga: Usitazamie kwamba madereva wa magari watakupa nafasi ya kupita hata kama ni haki yako.

◼ Usiendeshe Pikipiki Ukiwa Umelewa Pombe au Ukiwa Umetumia Dawa za Kulevya

◼ Chagua Pikipiki Unayoweza Kuendesha Bila Matatizo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki