Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w88 6/15 kur. 21-23
  • Wao Walisadikishwa Juu ya Upendo wa Yehova

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wao Walisadikishwa Juu ya Upendo wa Yehova
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ithibati ya Upendo wa Yehova
  • Twafika Kami Mwishowe
  • Pikipiki—Ni Zenye Hatari Kadiri Gani?
    Amkeni!—1992
  • Tungefanya Nini Bila Punda?
    Amkeni!—2006
  • Kuwafikia Watu Wasiofikiwa
    2016 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Yehova Abariki Udumifu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
w88 6/15 kur. 21-23

Wao Walisadikishwa Juu ya Upendo wa Yehova

MAWIMBI yaliyoinuka yanagonga-gonga meli iliyonaswa katika dhoruba kubwa sana baharini. Baada ya kupambana siku 14 na maji hayo yenye fujo nyingi, abiria na wanameli wamebaki wakiwa hoi, isipokuwa mmoja. Yeye alikuwa na uhakika kwamba Yehova angempa himaya, huku yale maneno ya kufariji, “Usiwe na hofu, Paulo” yalipovuma akilini mwake. Wakati wa saa zilizofuata za kukata maneno, meli ilishika chini, na hiyo ikaruhusu wote waweze kufika bara wakiwa salama. Kwa mara nyingine mtume Paulo alikuwa na sababu ya kusadikishwa juu ya upendo wa Yehova.​—Matendo 27:20-44.

Je! wewe unasadikishwa juu ya upendo wa Mungu kwa kadiri iliyo sawa na hiyo? Ni jambo muhimu kujifunza daima Neno la Mungu na kutumia unayojifunza ili uimarishe wengine. Hata hivyo, ili usadikishwe kweli kweli juu ya upendo wa Yehova, ni lazima wewe uishi kikweli kwa kujilisha matamko ya Yehova kwa kujionea mwenyewe akichukua hatua kwa ajili yako. Mmoja anayesadikishwa kwa uthabiti juu ya jambo hili ni mwangalizi-msafiri mmoja anayefanya kazi katika milima ya Bolivia iliyoinuka sana ambaye, kama wengine wengi, amejionea mwenyewe utunzaji wa Yehova.

“Nikiwa ninafanya kazi nje ya Oruro,” yeye anasimulia, “nilikuwa nizuru kundi moja katika Kami, mji mmoja wenye migodi ya madini kilometa 100 kutoka hapo. Ile barabara ya vilimani, yenye kupotoka-potoka, hufikia altitudo za meta 4,600 na inaweza kuwa isiyotegemeka, hasa wakati mvua inapokunya. Mara nyingi hali za joto zinashuka kufikia digrii -10 Selsio, au chini zaidi.

“Ndugu mwingine, Aníbal, alikuwa anibebe katika pikipiki yake, nasi tukaondoka saa 12 ya asubuhi, tukiwa tayari kwa kisafari chenye kuchukua muda wa saa tano. Tangu mwanzoni mvua ilikuwa inakunya, na matope yaliendelea kujazana-jazana kati ya gurudumu na kikinga-gurudumu, nayo yakatukwamisha. Ni baada tu ya kazi nyingi ya kudokoa-dokoa matope hayo kwamba tuliweza kuendelea. Nikiwa nimekalia kiti cha nyuma ya Aníbal, nilijaribu kuhami viatu na suruali yangu visichafuliwe lakini nikaacha kufanya hivyo wakati vilipolowanishwa kabisa.

Ithibati ya Upendo wa Yehova

“Muda wa saa sita ulikuwa umepita wakati enjini ilipozimika juu ya kilima chenye kuinamilia sana, nasi tukaanza kurudi-rudi nyuma. Tuliruka chini, tukajaribu kwa kila njia kushikilia mashine hiyo nzito katika matope hayo yenye utelezi. Hata hivyo, hiyo ilithibitika kuwa kazi-bure tu, na mioyo yetu ikazimia wakati pikipiki ilipoporomoka upande wa kibonde chenye kina cha meta 90! Sisi tulitazama chini kwa wasiwasi. Kwa njia isiyoaminika, mashine hiyo ikawa imekuja kukwama nusu tu ya mshuko huo. Hata hivyo, sisi hatungeweza kamwe kuiinua bila msaada.

“Saa zilizidi kuyoyoma, lakini sisi hatukuwa na tumaini kubwa kwamba mtu ye yote angepitia penye barabara hiyo ya mahali pakiwa. Ndipo mwanamume mmoja aliyekuwa pamoja na punda na mallama (maalupaka) kadhaa akatokea. Kwa kuona shida yetu, yeye alisema katika ulimi wa Kikwechua: ‘Ndiyo, mimi nina kamba fulani za kufungia wanyama.’ Akafunga kamba zile za ngozi kwenye punda na kwenye pikipiki. Halafu, sisi tukainua tukiwa chini kule huku yeye akimtia moyo punda yule avute. Hatimaye, baada ya kumchokoa-chokoa sana punda yule, tukawa tumerudi barabarani, vipaji vya uso wetu vikiwa na jasho. Tungeweza jinsi gani kumlipa kwa jambo hilo? Tulimtolea kitabu kimoja cha Hadithi za Biblia, naye akavutiwa na kitabu hicho hata akataka kurudisha hisani hiyo kwa kutupatia viazi kutoka kwenye mzigo wake!

“Enjini ikanguruma, nasi tukampigia Yehova asante kubwa sana. Kule mbele zaidi, tulifikiria kusimama, kwa kuwa enjini ilianza kuzimika-zimika. Tukaja kwenye mkahawa mdogo. ‘Ninyi mnaelekea wapi?’ mwenyeji akauliza. Sisi tukamwambia na kumweleza tatizo letu. ‘Mimi nina spakiplagi na nitawaazima vyombo fulani,’ akasema. Ilikuwa vigumu kuitikadi tuliyoyasikia—hapa palikuwa ni mahali ambapo mara nyingi marafiki hawaitibariwi, achia mbali watu wasiojulikana kabisa. Ilipokuwa na spakiplagi ile mpya, enjini ilienda vizuri.

“Sasa giza lilikuwa limeingia, nami nikawa na wasiwasi kwa kushangaa itakuwaje, kwa kuwa miguu yangu ilikuwa ikifa ganzi katika baridi ile ya kugandisha. Ndipo, tulipokuwa tukipanda mahali pamoja palipoinuka sana, enjini ikazimika tena. Ikathibitika kuwa kazi-bure kukanyaga-kanyaga stata na kuisukuma pikipiki kwa kilometa tatu. Tukiwa tumechoka kabisa, sisi tuliketi chini kando ya barabara. Angalau miguu yangu ilikuwa imeacha kufa ganzi! Lakini sisi wote wawili tuliudhika na tulishindwa tufanye nini. Tulipata pumziko fupi na ndipo tukajaribu kungurumisha tena enjini. Je! ingefanya kazi?

Kwa mshangao wetu enjini ilinguruma. Hata hivyo, sasa mvua ilianza kunya, na kwenye mwinamio ule mwingine wa barabara tukakwama tena. Kwa mara nyingine tukawa tumeketi kando ya barabara, wakati huu tukiwa katika mvua yenye kumwagika. Tulipumzika tena. Tukiwa na mashaka fulani tukajaribu kungurumisha enjini tena—nayo ikanguruma! Baada ya muda mfupi tukawa tunavuka sehemu iliyo ya juu zaidi ya safari yetu. Mimi nilihisi wasiwasi ukiwa umenitoka, nikifikiri kwamba hata kama enjini ingezimika, tungeweza takriban kuambaa-ambaa mpaka tuingie Kami. Lakini katika mteremko ulioinama sana kile kishikio cha breki kikavunjika katika mkono wa Aníbal! Niliruka chini haraka huku nikiwa nimeshikilia kile kiti cha nyuma, nikachimbiza miguu yangu chini na kuteleza nikiteremka kilimani. Kwa njia hii niliweza kufanya tusimame. Jambo hili lilitukia kwenye miinuko miwili mingine ya barabarani.

Twafika Kami Mwishowe

“Ilikuwa saa 9 ya usiku tulipofika Kami hatimaye. Tulikuwa tumekuwa barabarani kwa muda wa saa 21. Kuwapata akina ndugu kungekuwa tatizo, kwa kuwa hii ilikuwa ziara yangu ya kwanza. Tulipiga hodi milangoni lakini tukaambiwa: ‘Nendeni zenu! Sisi tunalala!’ Baada ya kupiga hodi milango mbalimbali, mimi nilihisi kwamba jambo bora zaidi lingekuwa kupumzika chini ya paa moja yenye kuning’inia juu yetu na kuwatafuta akina ndugu asubuhi. Mwili wangu ulibwagika chini kwa kuchoka, nikalala fofofo. Nilipoamka, nilijikuta nimezungukwa na watu. Nilisimama, na mwanamume mmoja mwenye mwili mkubwa akaja na kunikumbatia sana. Ndiyo, wao walikuwa ni ndugu zetu! Aníbali alikuwa amewapata. Sikuweza kunena kwa kuwa hisia-moyo zangu zilijazana-jazana ndani yangu.

“Bila kupoteza wakati, wao walichukua vitu vyetu, kutia na ile pikipiki iliyotandwa na matope, na ndugu mmoja akainyanyua kihalisi mpaka kwenye kiwanja cha nyumba yake. Walionipa mahali pa kukaa walikuwa mume na mke wanyenyekevu, yule mke akiwa amevaa vazi polera, rinda refu sana lililoungwa-ungwa visehemu-sehemu. ‘Wewe lalia kitanda chetu,’ wakasema. Mimi sikuwataka walalie sakafu, hasa kwa kuwa mke alikuwa na mimba. Lakini wao walisisitiza.

“Nilipojifahamu tena, ilikuwa ni saa 2 asubuhi. Mtu fulani alikuwa akigonga hodi mlangoni. ‘Akina ndugu wako tayari kwa ajili ya utumishi,’ nikaambiwa. Kwa kuona nyuso zao za tazamio zikiwaka uthamini, sikuwa na uchaguzi mwingine wo wote ila kukokota mwili wangu wenye kuniuma utoke kitandani na kuanza ziara. Nayo ilikuwa ziara ya kuchangamsha moyo kama nini! Nilipokuwa nikiandamana na akina ndugu katika huduma yao, wao walijaa furufuru shangwe na idili. Mimi nilitafakari juu ya jinsi ziara hizi zilivyo muhimu, yajapokuwa mambo yale yote tuliyokuwa tumepitia—kama ‘vijito vya maji katika nchi isiyo na maji.’​—Isaya 32:2,NW.

“Siku iliyofuata tulizuru kijiji kimoja ambako mchungaji mwevanjelisti alikuwa ametisha kuvunja-vunja mkutano wetu nilipofika. Baada ya hotuba, mwanamume mwenye maungo alinipa kumbatio la Kiboliviaa na akasema: ‘Ndugu, ninyi ndinyi wenye ukweli!’ Baadaye, niliuliza alikuwa nani. ‘Ndiye mchungaji,’ wao wakasema.

“Ziara ya kwenda Kami iliisha upesi mno, nasi tukawa tunaondoka. Akina ndugu walikuwa wameitengeneza pikipiki na kusafisha nguo zetu zote zenye matope. Tulipomtaja mwanamume aliyetuazima vyombo vile, wao walistaajabu, kwa kuwa yeye anajulikana kuwa mtu ambaye takriban hasaidii kamwe. Baada ya makumbatiano mengi na mitikisano ya mkono, sisi tuliondoka na upesi tukawa tumerudi tumwone yule mwenyeji mfadhili wa mkahawa mdogo. Baada ya kurudisha kila kitu, tulimwuliza hivi: ‘Tuna deni la kiasi gani?’ ‘Hakuna,’ yeye akajibu. ‘Mimi niliterema kusaidia!’

“Tulipokuwa tumerudi katika Oruro, muda wa saa tano baadaye, tulifikiria jinsi lilivyokuwa jambo la maana kutochoka na kuacha, na jinsi Yehova alivyotutunza vizuri ajabu. Aníbal alivutwa kwa kina kirefu na alilojionea hata akapaaza sauti kwa mshangao hivi: ‘Mimi ningetoa cho chote kile ili nirudi kule!’ Yeye amefanya hivyo hivyo, akipeleka waangalizi wengine wenye kusafiri wakiwa juu ya pikipiki yake kwenda Kami na mahali pengine pengi. Ndiyo, sisi tulikuwa na sababu thabiti ya kusadikishwa hata zaidi juu ya upendo wa Yehova.”​—Kama ilivyosimuliwa na mwangalizi wa mzunguko Ricardo Hernández.

[Maelezo ya Chini]

a Kumbatio la Kibolivia latia ndani mtikiso wa mkono, kila mmoja kupiga-piga mwenziye mgongo, na mtikisano mwingine wa mkono.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ile barabara ya milimani yenye kupotoka-potoka inayoongoza kwenye mji wa migodi ya madini ya Kami

Barabara ya kupitia milimani kwenda Kami

Punda wanaweza kuwa na mafaa sana katika dharura!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki