Tumbo la Uzazi—Makao Yetu ya Kwanza ya Ajabu
MAKAO yako ya kwanza ni mahali pa ajabu kama nini! Penye joto na ustarehe. Pana malisho ya kutosha yanayofaa mwili. Ni salama salimini.
Uliishi miezi kadhaa hapo, ukinenepa na kukua. Hata hivyo, makao yako yalionekana yakiendelea kuwa na nafasi ndogo zaidi na zaidi, hadi kufikia siku moja ambayo hungeweza kusonga hata kidogo. Yawezekana sana kwamba kufikia wakati huo hata ulijikuta ukisimama kwa kichwa chako! Kisha, kwa ghafula tu ulihisi ukifinywa kwa nguvu zenye uweza mwingi, na ukatoka kwa nguvu kupitia mlango wa makao yako kwenye uangavu wa ulimwengu wa nje ulio baridi na wenye makelele mengi.
Wewe hukumbuki maono kama hayo? Bila shaka hukumbuki. Lakini unawiwa uhai wako na makao hayo ulimokuwa—tumbo la uzazi la mama yako. Lilitengenezwa vizuri sana kwa ajili yako, likiandaa malezi yote na ulinzi ambao kitoto kinachokua kinahitaji. Kwa nini basi usifunge safari sasa ya kurudi na kuzuru makao yako ya kwanza ya ajabu—tumbo la uzazi?
Ukaribishaji Mchangamfu Wakungojea
Uhai wako labda ulianza ulipokuwa njiani kuelekea makao hayo mazuri. Yai lililopevuka la mama yako lilisafiri polepole kupitia mrija mrefu wenye upana wa unywele. Wakati uo huo, mamilioni ya shahawa za baba yako zilikuwa njiani kwenye barabara iyo hiyo, ili zikutane moja kwa moja na lile yai. Shahawa moja ilifaulu kurutubisha lile yai, na hivyo ukaja kuwa wewe.
Kufikia wakati huu, matayarisho kwa ajili ya kuwasili kwako yalikuwa yanafanywa. Kuta za tumbo la uzazi, au mji wa mimba, zilikuwa zikijitayarisha zenyewe, na mahali hapo palikuwa pamejaa malisho. Utando wa mji wa mimba ulikuwa umejifurisha maradufu kushinda ulivyo kwa kawaida, sehemu yao ya ndani ikiwa yavuyavu na nyororo.
Baada ya siku tatu au nne, ulipitia lango la makao yako mapya. Kwako—ukiwa mdogo kama kichwa cha pini na ukiwa tu mkusanyo wa makumi machache ya chembe zinazoitwa blastosito—makao yako yangeonekana kuwa pango kubwa sana. Hata hivyo, nafasi ya mle ndani ni ndogo sana. Mji wa mimba kwa kweli ni kiungo chenye uvungu, kilicho laini na chenye rangi nyekundu-nyeupe, kikiwa na ukubwa na umbo sawa na parachichi lililogeuzwa juu chini.
Hayo yangekuwa ndiyo makao yako kwa siku karibu 270 hivi zinazofuata, na mama yako, hata kwa hasara ya mwili wake, angekuandalia malisho unayohitaji ili ukue na kuendelea hadi wakati ufikapo wa kuzaliwa. Majuma kadhaa yangepita hata kabla mama yako kung’amua kwamba unaishi, na inaweza kuchukua miezi mingine mitatu au minne kwa tumbo lake kufura kiasi cha kutambuliwa na wengine.
Baada ya kushuka ndani ya uvungu wa mji wa mimba, ulieleaelea kwa siku nyinginezo tatu. Hatimaye, katika siku ya saba baada ya kuingia katika mji wa mimba, ulijishikamanisha kwa ukuta wao. Vimeng’enya kutoka blastosito viliyeyusha chembe za juu za ukuta huo wa mji wa mimba, unaoitwa endometriamu, kisha ukaingia na kujishikamanisha salama kwenye ukuta huo ulio kama bahameli. Iwapo yai halingalirutubishwa na kupachikwa katika utando huo, basi mji wa mimba ungaliliondoa hatimaye na kuliondoa kutoka kwa mama yako likiwa hedhi (damu ya mwezi).
Kukabiliana na Mkatao
Kazi nyingi za ajabu zilikuwa zinafanywa kuhakikisha kwamba ulifurahia kukaa kwako. Jambo moja ni kwamba ulihitaji ulinzi kutoka kwa mfumo wa kinga wa mama yako mwenyewe. Wanasayansi bado wanashindwa kujua ni kwa sababu gani mwili wa mama yako haukukuona kama mvamizi wa kigeni na kukushambulia. Kwa kawadia, ule mfumo uliotatanika wa mkatao huanza vita mara tu ishara ya mvamizi yeyote inapoonekana. Na bado hatimaye wewe ungekua uwe mwili wa kigeni mkubwa mno wenye uzito wa kilo kadhaa. Mbona haukushambuliwa?
Mtafiti David Billington wa Chuo Kikuu cha Bristol alieleza hivi: ‘Hasa pana ukuta kati ya mama na kijusi. Ukuta huo husimamisha kwa kadiri kubwa mabadilishano kati ya mama na kijusi.’ Alikuwa akirejezea utando wa mnofu unaoitwa trofoblasti, ambao hukizunguka kijusi. Ukuta huo ulizuia mguso wa moja kwa moja kati yako na mama yako. Ni fumbo kujua ni kwa sababu gani kinga zake hazikushambulia ile trofoblasti ikiwa kitu cha kigeni. Jibu la swali hilo laweza kutuonyesha pia sababu ya mimba nyinginezo kuharibika.—Ona kisanduku kwenye ukurasa 29.
Ulishaji na Utunzaji Waendelea
Fikiria hamu yako kubwa ya kula, hasa katika siku hizo za mapema. Katika majuma yako ya kwanza manane ukiwa hai, ulirefuka karibu mara 240, na uzito wako ukaongezeka kuwa karibu mara milioni moja kushinda wakati ulipotungwa mimba. Hatimaye, uzito wako unapozaliwa ungekuwa mara bilioni 2.4 kushinda wakati ulipotungwa mimba, huku makao yako yakipanuka kama kibofu ili utoshee. Tumbo la uzazi wakati huo linakuwa lenye uzito mara 16 kushinda tumbo la uzazi ambalo halina mimba, kwa majuma machache baada ya kujifungua, hurudia kipimo chalo cha zamani. Katika miezi mitatu ya kwanza ya uhai umbo la mwili wako lilifanyizwa, huku viungo na mfumo wa neva zikiwa tayari kwa hatua za ukuzi ambazo zingefuata.
Mapema kabla ya hapo, mfuko wa mimba wenye maji ulifanyizwa. Mfuko huo ulikuandalia chumba cha kuchezea chenye takia na halijoto iliyopimwa ambamo ungejifingirisha na kuchezacheza katika miezi mingine mitatu yako. Ulikuwa unaiimarisha misuli ambayo ungehitaji nje ya mfuko wa mimba wenye maji usio na uzito wowote. Ulimeza maji-maji ya mimba kidogo-kidogo, ili labda upate malisho. Maji-maji hayo yaliwekwa upya kwa ajili yako kila baada ya saa mbili hadi tatu.
Kulikuwa na tishu kama takia iliyoanza kukua kwenye ukuta wa nje wa blastosito iitwayo kondo la nyuma (Placenta; neno la Kilatini linalomaanisha “keki bapa”). Hebu fikiria baadhi ya utumishi mbalimbali lililokufanyia.
Kondo la nyuma lilifanya kazi ya mapafu, likibadilishana hewa za oksijeni na kaboni dayoksaidi kati yako na mama yako. Likifanya kazi ya ini, liliyeyusha baadhi ya chembe za damu za mama yako ili litoe vitu ambavyo ungehitaji kutumia kama vile chuma. Lilifanya kazi ya figo kwa kuchuja nje mkojo kutoka kwa damu yako na kuupeleka kwa mkondo wa damu wa mama yako ili utolewe nje kupitia figo. Likiwa kama matumbo, kondo la nyuma liliyeyusha vipande vya chakula. Mambo hayo yote yalifanyika kupitia kiunga-mwana chenye urefu wa sentimeta 55.
Ilifikiriwa wakati mmoja kwamba kondo la nyuma lilikuwa mfumo wa ulinzi usiopitika kamwe, kwamba halingeruhusu chochote kiwezacho kudhuru kipite kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. Ni sikitiko kwamba sasa tunajua ya kuwa kuna maambukizo mengi ambayo yanaweza kuvunja mfumo huo wa ulinzi, na pia vitu kama vile dawa ya kutuliza yenye sifa mbaya inayoitwa thalidomidi vyaweza kuharibu ulinzi huo. Maradhi kama vile surua ya Ujerumani pia huwa hatari kubwa katika wakati fulani fulani wa mimba.
Ile kinga ya damu ya ubongo ambayo watu wazima huwa nayo haijasitawi vizuri katika ubongo unaokua wa kijusi, ikiuacha katika hali ya kuathiriwa na vivamizi kama vile moshi wa sigareti, kileo, madawa, na sumu nyinginezo za kikemikali. Utafiti waonyesha kwamba kileo huathiri sana kitoto ambacho hakijazaliwa. Je! kafeini ambayo inaweza kulipita lile kondo la nyuma, inaweza kuathiri ukuzi wa kitoto? Je! vitamini za ziada zaweza kunufaisha kitoto kinachokua kwa njia yoyote ile? Mengi zaidi yanahitaji kujulikana kuhusu maswali hayo.
Basi, mfumo wa kinga kwa kitoto chochote ni lazima uanze na utunzi wa mama mwenyewe, akijiepusha kutumia mwilini vitu ambavyo vinajulikana kuwa vinaumiza kitoto. Kwa upande mzuri, mama akitumia vyakula vinavyofaa mwili, na akikubaliwa na daktari kufanya mazoezi, yote yaweza kuendeleza sana afya ya ujumla na hali bora ya mama na mtoto.
Kuaga Makao Yako
Wakati miezi yako mitatu ya mwisho imeendelea sana, matayarisho yalianza kwa ajili ya kuondoka kwako. Misuli yenye nguvu kwenye ukuta wa mji wa mimba ilianza mazoezi ya ghafula-ghafula ya kujishikanisha na kujiachanisha, jambo ambalo wakati mwingine huitwa utungu bandia. Mji wa mimba ukaja kuwa mwororo zaidi na wenye kunyumbuka zaidi.
Badala ya kusema, “Mtoto aliteremka,” ni sahihi zaidi kusema kwamba mji wa mimba uliteremka, mtoto akiwemo ndani. Hiyo ni kwa sababu mji wa mimba hujilainisha kama silinda na kuteremka chini kidogo ili kichwa cha mtoto kitokee kwenye uvungu uliopo kati ya mifupa ya nyonga.
Hakuna mtu ajuaye ni nini kilichoamua kwamba sasa ni wakati wako wa kutoka. Labda ilikuwa ni hormoni kutoka kwa mama yako, au wewe mtoto, zilizopatia tumbo la uzazi ujumbe. Ujumbe wa: “Anza utungu!”
“Utungu” unaeleza vema zile hatua tatu zilizochukuliwa na mji wa mimba. Kwanza, kuta zenye misuli za mji wa mimba zilijishikanisha huku shingo ya mji wa mimba pamoja na uke ukipanuka kwa matayarisho ya kuteremka kwako. Huenda ule mfuko wa maji ulipasuka wakati huo.
Pili, kazi ya mama sasa ikaanza huku akisukuma kichwa cha mtoto kuelekea chini kupitia shingo ya mji wa mimba na uke. Kule kujishikanisha kukaendelea, kukija kwa nguvu zaidi na kwa haraka zaidi mpaka kichwa chako kilipopita ule mfereji wa uzazi. Sehemu ya mwili wako iliyobaki ilifuata kwa urahisi. Katika hatua ya mwisho ya utungu, mama yako alitoa lile kondo la nyuma na masalio ya kile kiunga-mwana, vinavyotoka tumboni baada ya mtoto kuzaliwa.
Sasa ukawapo—ukiwa umeshtuka, mwenye baridi na ukilia—bila shaka ukiomboleza kuondoka kwako kwa ghafula katika makao yako yenye ustarehe ambayo ulitumia kwa miezi tisa hivi. Lakini unaweza kufurahi kama nini kwamba una zawadi ya uhai na unaweza kuthamini ule utunzi wa Muumba mwenye upendo, aliyehakikisha kwamba ulikuwa na makao bora kuanzia mwanzoni kabisa!
[Sanduku katika ukurasa wa 29]
Kuharibika Mimba—Uhamisho Wenye Msiba
MSIBA unaweza kupata hata mama mwenye kujali zaidi. Sababu za kuharibika mimba hazijulikani vizuri na mijadala ya kuzizungumzia hupamba moto. Watafiti hata hawakubaliani juu ya asilimia ya mayai yanayorutubishwa na kuharibika yenyewe. Makadirio yanaanzia asilimia 10 hadi asilimia 20 au hata zaidi ya mimba za wanawake wakaaji wa United States.
Ni kwa nini tumbo la uzazi nyakati nyingine huhamisha kwa nguvu uhai walo mpya badala ya kuutunza humo ndani? Inawezekana kwamba mfumo wa kinga wa mama huitikia kwa kujikinga dhidi ya trofoblasti inayozunguka kijusi, ukiushambulia ukuta wayo wa ulinzi na kusababisha kuharibika kwa mimba. Kuharibika kwingine huenda kukasababishwa na vile viitwavyo vichukua tabia-urithi, ambavyo huharibu kabisa kile kijusi au kitoto kiasi cha kutoweza kuishi tena kamwe. Au huenda ni tukio lisilo la kawaida kwa mfumo wa uzazi—yai kuingia mapema mno kwenye mji wa mimba kabla utando kuwa tayari kulipokea au lichelewe mno hivi kwamba lipate endometriamu ikiwa tayari imeanza kutoka. Labda kasoro fulani kwenye mji wa mimba wa mama unaweza kumfanya asiweze kujifungua.
Uchunguzi uliofanyiwa wanawake karibu 200 katika Uingereza (1990) ulidokeza kwamba kutoweza kurutubika na kuharibika kwa mimba huenda kukasababishwa na matatizo ya hormoni. Kutolewa kwa LH (hormoni ya luteini), ambayo hutoka kwa tezi ya pituitari, huongezeka karibu siku ya 14 baada ya hedhi na kusababisha yai pevu kutoka kwenye vifuko vya mayai na kuanza mwendo kwa mrija wa Falopia ili ikiwezekana lirutubishwe. “Kile ambacho kikundi hicho cha Uingereza kilipata,” laripoti gazeti The New York Times, “lilikuwa ni viasi vikubwa sana vya LH kwa wakati usiofaa, siku ya nane baada ya hedhi, kabla ya yai kutoka kwenye fuko lalo.” Uchunguzi zaidi unahitajika kuthibitisha na kuona maana ya matukio hayo.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Kijusi cha miezi mitatu
Kijusi cha miezi sita
Kijusi cha miezi tisa