Vijana Wauliza . . .
Kwa Nini Hili Linaupata Mwili Wangu?
UBALEHE—huu waweza kuwa wakati wenye kusisimua katika maisha yako. Wewe unabadilika pole kwa pole kutoka kuwa mtoto hadi kuwa mtu mzima!
Ingawa hivyo, labda wazazi wako hawajazungumza nawe mapema juu ya jambo la kutarajia. Hata ikiwa wamelizungumza, uhalisi wa ubalehe huenda ukawa tatizo la kadiri usiyokuwa umetarajia. Huenda ukawa ukipatwa na mambo yafanyayo ushangae kama wewe una kasoro nzito. Lakini sivyo ilivyo hasa!
Ile Kawaida ya Hedhi (Mwezi)—Laana au Baraka?
Karibu miaka miwili baada ya ubalehe kuanza, msichana mchanga hupatwa na tukio la maana—mwanzo wa ile kawaida ya kutokea kwa hedhi. Hata hivyo, bila matayarisho ya kutosha, tukio hili lililo hatua ya umri laweza kuogopesha, kushtua.a “Mimi naogopa kweli kweli,” akaandika msichana mmoja jina lake Paula. “Karibu miezi mitatu iliyopita, nilianza kutoka damu kwa siku chache kila mwezi. Je! hii yamaanisha nina kansa? . . . Naudhika sana ninapofikiria mtoko huu wa damu hivi kwamba ninalia na kutetemeka.”
Kitabu Adolescents and Youth charipoti kwamba wasichana fulani hata huhisi aibu na hatia wakati kawaida yao ianzapo. Basi, si ajabu kwamba wasichana wengi huweka tukio hilo likiwa siri. Msichana mmoja mchanga alisema hivi: “Mimi niliona aibu kumwambia mama yangu. Yeye hakuwa ameongea nami juu ya jambo hilo nami niliogopa wee.”
Lakini kawaida ya kutokea kwa hedhi si jambo la kuonea aibu hata kidogo, bali ni uthibitisho wa kwamba nguvu zako za uzazi zinakomaa. Sasa mwili wako waweza kutungwa mimba na kuzaa mtoto. Ama kweli, miaka kadhaa itapita kabla hujawa tayari kabisa kuwa mzazi. Lakini sasa wewe ndiye huyo, ukiwa ukingoni pa uanauke. Je! hili ni jambo la kuonea aibu na haya? Hata kidogo!
Zaidi ya hilo, huu ni muono wa wanawake kila mahali ulimwenguni. Biblia huirejezea kawaida ya hedhi kuwa “mambo ya kike [jambo la kidesturi kwa wanawake, NW].” (Mwanzo 31:35) Na kinyume cha rai ya watu fulani, hiyo si laana.b Ingawa hivyo, labda baadhi ya hofu zako zitatulia ukielewa ni kwa nini na ni jinsi gani kawaida hii hutukia.
Ule “Mwujiza wa Kila Mwezi”
Neno menstruation (hedhi) latokana na neno la Kilatini ambalo humaanisha “-a kila mwezi.” Mara moja kwa mwezi mwili wako huwa na uwezo wa kutungwa mtoto. Kwanza, ongezeko la kiasi cha homoni zako huutolea ishara mji wa mimba, au tumbo la uzazi. Nao hujitayarisha kupokea na kukuza yai lililotungwa uzazi; utando wao huwa na wingi wa damu na vilishaji. Hapo karibu pana vile viungo viwili vyenye umbo kama lozi vijulikanavyo kuwa mifuko ya mayai, kila kimoja kikiwa na maelfu ya mayai madogo sana. Kila yai ni mtoto wa uwezekano, likihitaji kutungwa uzazi tu na mbegu ya kiume. Mara moja kwa mwezi, yai moja hukomaa na kupasuka kuwa huru kutoka kwenye mifuko ya mayai.
Sasa “vidole” vyenye uanana hulivuta yai hilo juu na kuliingiza ndani ya mmoja wa mirija ya Fallopio. Sasa yai hilo dogo sana huanza safari ya siku nne hadi sita kupitia humo hadi kwenye mji wa mimba. Mwanamke asipopata mimba wakati huu, lile yai dogo sana huvunjika-vunjika. Pia ule utando wa mji wa mimba ulio na damu nyingi humegeka-megeka. Mji wa mimba huanza kufinyana na kwa uanana huuondosha utando huu kupitia njia ya kuma.
Kwa muda wa kuanzia siku mbili hadi saba hivi (ikitofautiana kwa mwanamke na mwanamke) mtoko wa hedhi hutiririka. Halafu utaratibu huo hujirudisha, mwezi nenda, mwezi rudi, mpaka kikomo cha hedhi.c Kwa kufaa mwandikaji mmoja aliueleza huo kuwa “mwujiza wa kila mwezi”! Ni utaratibu ulioidhinishwa kwa sahihi hakika ya Mbuni Stadi. Ni sababu moja ya ziada ya kupaaza sauti, kama alivyofanya mtunga zaburi: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha”!—Zaburi 139:14.
Kupata Msaada
Hata hivyo, ile kawaida ya hedhi hukutolea wewe mahangaiko kadhaa yafaayo kufikiriwa. Kwa kielelezo, wasichana wengi huwa na wasiwasi kwamba, ‘Namna gani ikianza nikiwa shuleni?’ Ni kweli kwamba ingeweza kutia madoa katika nguo zako na kukuaibisha kidogo. Hata hivyo, Lynda Madaras aliye mwelimishaji wa mambo ya ngono atuhakikishia kwamba “pale mwanzoni wasichana walio wengi hawatoki damu ya kutosha kuweza kuonekana nje ya nguo zao.” Na bado, wewe utataka kujitayarisha kwa kadiri ya kutosha.
Vitabu kadhaa hutoa ushauri timamu wa kitiba. Lakini kwa nini usishiriki mahangaiko yako pamoja na mama yako pia? Bila shaka atakuwa na madokezo kadhaa yenye kutumika. “Mama yangu alikuwa kama rafiki kwangu,” asema mwanamke mmoja kijana. “Tulikuwa na mazungumzo marefu, naye akawa akijibu maswali yangu.”
Ni kweli kwamba akina mama fulani hutatizika kuongea juu ya mambo ya kindani. Lakini wewe ukimkaribia mama kwa staha na kumjulisha kwamba hili ni jambo la maana kwako kweli kweli, huenda akaweza kushinda kutotaka kwake kuongea. Hilo lisipofanikiwa, kwa nini usieleze usiri wako kwa mwanamke Mkristo aliye mkomavu ambaye wahisi ukistareheka naye?
Ingawa wanawake walio wengi huweza kuendesha kazi zao za kila siku wakati wa kipindi chao, kitabu Changing Bodies, Changing Lives chatukumbusha kwamba wanawake fulani hupatwa na “maumivu ya kichwa, maumivu ya mgongo, matatizo ya ngozi, mabadiliko ya tabia-moyo, mshuko wa moyo, mipindano ya misuli, kutaka kutapika, na kubakia kwa mkojo katika kibofu.” Mara nyingi aspirini za kawaida huondoa dalili hizi. (Daktari wako aweza kuamua kama dawa kali zaidi yahitajiwa.) Na ikiwezekana, wakati huo wewe waweza kuepuka mkazo wa bure tu kwa kupanga utendaji wako wakati wa kawaida yako ya hedhi.
Mitoko ya Usiku
Wavulana wachanga pia wana matatizo kadhaa ya kushughulika nayo wakati mfumo wao wa uzazi uwapo ukikomaa. Kwa kielelezo, viungo vyako vya ngono huenda vikaanza kufanyiza umajimaji uitwao shahawa. Huu una mamilioni ya mbegu zisizoonekana bila kutumia darubini, kila moja ikiweza kutunga uzazi katika yai la kike na kuzalisha mtoto ikiachiliwa wakati wa mwingiliano wa ngono.
Kwa kuwa wewe hujafunga ndoa, mbegu hizo hujazana tu. Pole kwa pole baadhi yazo hufyonzwa na mwili wako. Lakini mara kwa mara, baadhi yazo huachiliwa usiku wakati wewe umelala. Kwa kawaida hiyo huitwa ndoto-majimaji. Ingawa hivyo, jina zuri zaidi kwayo ni mtoko wa usiku, kwa kuwa mara nyingi mtoko huo hutukia wenyewe tu, kwa kuandamana au kwa kutoandamana na ndoto ya kimahaba.
Tukio la kwanza la mvulana kupatwa na mtoko wa usiku huenda likamfadhaisha. “Mimi nilipata ndoto-majimaji yangu ya kwanza nilipokuwa na umri wa karibu miaka kumi na miwili na nusu,” akakumbuka tineja mmoja. “Sikujua lililokuwa likitendeka. . . . Niliamka nikakuta ni kama kitanda kina majimaji. Nilifikiri nimekojolea kitanda changu au nini.” Ingawa hivyo, wewe uwe na uhakika kwamba mitoko ya jinsi hiyo ni ya kawaida. Hata Biblia huitaja. (Walawi 15:16, 17) Ni wonyesho wa kwamba mfumo wako wa uzazi unafanya kazi na kwamba tayari umeanza mwendo wa kuelekea uanaume.
Yakiriwa wazi kwamba wazo la mama yako kugundua shuka zikiwa majimaji laweza kukuogofya. Lakini haielekei sana kwamba jambo hili lingemshtua au kumshangaza yeye. Ingawa hivyo, ingeweza kusaidia ukiongea na baba yako au mtu mzima mwingine aliye mkomavu. Huenda jambo hili likakuondolea wasiwasi wowote ambao huenda ikawa unao. Huenda hata ukaweza kupanga njia fulani ya kudumisha faragha yako katika jambo hili.
Kukabiliana na Mwamko
Kwa kadiri mfumo wa uzazi uwavyo ukikomaa, wavulana na wasichana pia huwa wepesi mno kuamka kingono. Hili lipatapo mvulana, uume, au mboo, hujazana damu, ikiufanya usimame wima au kwa kujisimika. “Lakini,” chakumbusha The New Teenage Body Book, “misimamo-wima mingi hutendeka kwa sababu zisizo za kingono—na nyakati fulani yaonekana huwa hivyo bila sababu yoyote! Mitikisiko ya basi, nguo zenye kubana, kujiachilia baridi, hofu, na vichocheaji vingine vyaweza kusababisha msimamo-wima.” Vivyo hivyo huenda wasichana wachanga wakajipata wameamka bila sababu ya wazi.
Mwamko usiotakwa wa kingono waweza kuudhi, kuaibisha. Lakini ni sehemu ya ukuzi na huenda ukatukia mara nyingi. Vijana fulani huchochea-chochea au kuchezea-chezea viungo vyao ili wapate utulizo wa kingono. Hilo ni kosa na laweza, baada ya muda mrefu, kufanyiza matatizo mengine.d Ni vizuri zaidi kujistarehesha na kuondoa akili yako kwenye jambo hilo. Muda si muda mwamko huo utapita. Upatapo umri mkubwa zaidi na kiasi cha homoni zako kutulia, utapata kwamba mwamko wenye kujitokeza wenyewe utatukia mara chache zaidi.
Ubalehe haudumu milele. Labda siku moja hata utaweza kuyacheka baadhi ya mambo ambayo sasa yanakutia msononeko. Kwa wakati uliopo, uwe na faraja katika uhakika wa kwamba wewe ni mtu wa kawaida.
[Maelezo ya Chini]
a Katika uchunguzi mmoja, asilimia 20 ya akina mama waliochunguzwa maoni hawakuwa wameambia binti zao lolote juu ya hedhi. Asilimia nyingine 10 waliwapasha kiasi kidogo sana cha habari.
b Ni kweli kwamba Sheria ya Kimusa ilijulisha rasmi kwamba mwanamke mwenye hedhi alikuwa “najisi.” (Walawi 15:19-33) Lakini hiyo ilikuwa katika maana ya kisherehe tu. Kwa wazi, sheria hizi zilitumika kufundisha staha kwa utakato wa damu. (Walawi 17:10-12) Wakati ule ule, sheria hizo zilitumika kukumbusha taifa la Kiyahudi kwamba ainabinadamu imezaliwa katika hali yenye dhambi na yahitaji mfidiaji.
c Huenda ikachukua miezi au miaka kabla kawaida hii haijadumisha kigezo cha ukawaida.
d Ona zile makala kuhusu kupiga punyeto katika matoleo ya Amkeni! ya Agosti 8, 1988, Novemba 8, 1988, na Mei 8, 1989.
[Picha katika ukurasa wa 19]
Wazazi waweza kukusaidia kujirekebisha kulingana na mabadiliko ya ubalehe